NAKUFAHAMU VIZURI
MTUNZI: KJM-0718274130
SEHEMU YA 14
Huo ndio ulikua mwisho wa Mzee Mbogo, alishafariki. Sikupenda kifo cha babu yangu huyu kipenzi nikisababishe mimi, lakini nani wa kulaumiwa kati yangu mimi na yeye? Tamaa zilimponza. Licha ya kuwa ni moja kati ya vifo vilivyonihuzunisha sana, lakini sikujutia hata kidogo. Sababu kuu ya kutokujuatia ni madhara ambayo yangenikuta endapo Mzee Mbogo angefanikisha mpango wake wa kidhalimu na wenzake dhidi yangu.
Wale kina Mzee Said walibaki kama waliopigwa shoti ya umeme, wameduwaa tu na hawajui cha kufanya. Nikautumia mwanya huu kumshika mmoja kati ya wale wazee, yeye alikua pembeni yangu kabisa, nilimshika bega, akaanguka chini na kupoteza maisha. Hapo ndipo wale kina Mzee Said na wenzake waliposhituka na kuamua kutoweka, wakiwaacha Mzee Mbogo na yule Mzee mwengine ambaye nilikuja kugundua kuwa ni babaake mdogo Lutfiya akiitwa Mahmoud Noor.
Baada ya kina Mzee Said kutokomea, niliingia katika kile chumba na kuchukua dawa ya kuifunga ile nyumba sasa. Nilifanikiwa kuifunga ile nyumba, na asingeweza kuingia mchawi au jini wa aina yeyote mle ndani pasi na idhini yangu. Kisha nikaingia chumbani kwangu kuumalizia usingizi wangu. Nililala mpaka asubuhi, nikaamka na kuingia bafuni kuoga, kisha nikavaa na kurudi pale sebuleni kuangalia zile maiti. Cha ajabu, sikuikuta maiti ya Mzee Mbogo pale nilipowaacha, alikuwepo Mzee Mahmoud peke yake. Nilipigwa na butwaa. Nilijiuliza sana atakua amechukuliwa na nani Mzee Mbogo? Kwanini maiti yake haipo? Kwanini imebaki ya yule jini pale? Sikupata jibu!!. Wakati nikiwa bado katika mshangao, mlango wa nyumba yangu uligongwa.
“Nanii??” Niliuliza wakati nikielekea kufungua mlango.
“Naitwa Mubarak Said Mansour”. Ilisema sauti iliyokuwa nyuma ya mlango huko nje.
Nilifungua, na kukutana na mzee mmoja wa kiarabu, amevalia kanzu na kofia ya kutunga na uzi. Miguuni alivalia kobadhi nyeusi, mkononi ameshika bakora ya chuma iliyonakshiwa vizuri.
“Karibu sana, naweza kukusaidia”. Nilimwambia yule mzee huku nikisindika mlango, sote tukiwa nje. Nilimnyooshea mkono kama ishara ya kusalimiana, lakini hakupokea mkono wangu.
“Sina maongezi marefu, mimi ni baba mzazi wa huyo maiti humo ndani, nimekuja kukuomba nimchukue mwanangu nikamzike”. Aliongea yule Mzee akiwa amenikazia macho. Sikutaka kubishana nae, nikamfungulia mlango na kumuonyesha ishara ya kumkaribisha ndani.
“Naomba unitolee hapa nje, siwezi kunasa katika mitego midogo kiasi hicho mimi ni mtu mzima kuliko marehemu baba yako”. Aliongea Mzee Mahmoud, na kunifanya nikakumbuka nilivyoifunga hii nyumba, nikaingia ndani na kumburuza yule marehemu nikamleta mpaka nje. Mzee Mahmoud alimbeba mgongoni na kitendo cha kupepesa macho, sikuwaona walishatokomea.
Sikurudi ndani, nikaelekea kwa Zahara muuza uji, akanikaribisha huku akiniwekea uji.
“Mbona kama nilikuona unaburuza kiroba? Ni mzigo gani mzito ulikua unauleta nje? Au sio wewe?”. Aliniuliza Zahara na kufanya nihamaki. Kumbe yule marehemu alionekana kama kiroba huku nje? Daah.. Sikuamini. Nilizama katika dimbwi la mawazo kutafakari mengi juu ya maisha ninayopitia sasa, maisha ya ulimwengu wa pili. Yakaja pia mawazo juu ya babu yangu Mzee Mbogo, sikupata majibu kamili.
“Vipi Adam? Uko sawa?”. Aliniuliza Zahara baada ya kuona niko mbali, hapo ndipo nliposhtuka kutoka katika dimbwi la mawazo na kumjibu niko sawa. Nikanywa uji wangu, nikamlipa kisha nikarudi nyumbani.
Nikiwa pale nyumbani, nilipata wazo la kwenda nyumbani kwa Mzee Mbogo, nikaangalie kinachoendelea. Niliamini huenda Mzee Mbogo amechukuliwa kutumia nguvu zake za kichawi na wameenda kumzika huko kwake.
Nilienda kituoni kupanda daladala mpaka mjini, ambapo nilipanda magari yanayoenda Mtakuja. Nilifanikiwa kupata gari mapema wala sikusubiri. Wakati tuko njiani, mvua kubwa sana ikaanza kunyesha, na kila tulivyokaribia ndivyo mvua ilivyozidi. Kwakuwa haukuwa msimu wa mvua, nilishangaa sana, nikajaribu kulihusisha tukio la mvua na safari yangu, lakini nikajipa moyo.
Tulifika, mvua bado ikiwa inanyesha, nikakaa katika moja ya baraza za nyumba pale kituoni, nikisubiri mvua ipungue. Hatimaye ilikata. Nikamuomba boda boda anipeleke kwa Mzee Mbogo.
“Bro, huko hakwendeki, mvua imeharibu njia, labda uuchape kwa mguu kaka”. Majibu ya bodaboda yalinivunja moyo. Ila niliamua kuukanyaga kwa mguu hadi nikashuhudie kinachoendelea huko Mtakuja. Nilitembea kwa masaa matatu mpaka nilipoiona nyumba ya Mzee Mbogo kwa mbali. Niliwaona watu wengi sana wamekusanyika nje ya nyumba ile. Machozi yakaanza kunitoka kwa kujua ukweli wa kuwa kifo cha Mzee Mbogo nimekisababisha mimi. Nilijutia sana, pamoja na aliyoyakusudia kuyafanya Mzee Mbogo kwangu, bado nilitamani sana isingekuwa vile, nilitamani afe kifo ambacho sitakibeba mimi kama mhusika mkuu.
Kadri nilivyosogea, ndivyo majuto yangu juu ya niliyoyatenda yalivyozidi. Sikutakiwa kuamua kumkamata mtu yeyote pale ilihali nikijua yupo babu yangu kipenzi Mzee Mbogo. Nilifika hadi nje kwa Mzee Mbogo, niliwakuta kina mama wengi zaidi kuliko wanaume. Vilio vilitawala kila kona ya uwanja wa nyumba ile ya Mzee Mbogo. Nikazama moja kwa moja pale katika kisebule kidogo cha Mzee Mbogo, nikawakuta wazee wa familia wote wapo pale, akiwemo Mzee Mbogo-Para mwenyewe. Nilinyong'onyea..
Itaendelea...
Sent using
Jamii Forums mobile app