Hadithi ya Mapenzi: Nakufahamu vizuri

Hadithi ya Mapenzi: Nakufahamu vizuri

NAKUFAHAMU VIZURI


MTUNZI: KJM


SEHEMU YA 12


“Adam tafadhali nisamehe sana, mimi nilishawishiwa tu na wazazi, sio kuwa ni mpango wangu binafsi”. Aliendelea kumwaga machozi Lutfiya. Sikuamua kumuonea huruma. Nilikasirika sana kutokana na tamaa zao walizozionyesha juu yangu. Walinifanya nikumbuke mbali sana, enzi za uhai wa baba yangu. Baba hakutaka niteswe na kiumbe wa aina yeyote hapa duniani kama alivyokuwa yeye, lakini kutokana na kujiweka mbali na habari hizi, sikutilia maanani maagizo yake. Niliamini naweza kuishi tu bila kujishughulisha na hizi habari. Kumbe nilifanya kosa kubwa sana, maadui zangu walitaka kutumia udhaifu huu kutaka kunipiku, kutaka madaraka. Niliamua kujiingiza rasmi katika kutetea kilicho changu, nilichagua kuingia mzima mzima, kuliko kuwaachia majini washirikiane na watu waliojaa tamaa ya pesa kina Mzee Mbogo kupitia mgongo wangu.

“Siwezi kukusamehe Lutfiya, lazima nikufunze adabu”. Nilisema kwa hasira, kisha nikatoka na kuelekea chumba kidogo cha pale nyumbani, nikimuacha Lutfiya pale ndani akiendelea kulia.

Baba yangu kabla hajafariki, aliniita na kunikabidhi mkoba mdogo mweusi. Mkoba huu ulikuwa na vifaa kadhaa wa kadha ambavyo mimi sikuona kama vina maana yeyote. Mlikuwa na pembe ndogo, mkia wa ngombe, vipande vya mizizi mitano ya miti tofauti, na hirizi kadhaa pamoja na dawa mbili tatu za unga zilizofungwa katika karatasi tofauti tofauti. Maelezo aliyonipa baba ni kuwa mkoba huu ni muhimu sana kwa ajili ya kinga ya maisha yangu binafsi. Alinieleza kuwa mimi ni mmoja ya watu wachache sana wenye maadui wengi sana hapa duniani, kwahiyo mkoba huu ndo kinga yangu. Alinielekeza pia namna ya kutumia vile vitu vilivyo katika mkoba ule kimoja baada ya kingine. Lakini pia aliniambia kuwa mkoba ule ni hazina kubwa inayotafutwa na watu kadhaa hasa majini kwa ajili ya kurahisisha shughuli zao. Kwahiyo niwe makini sana, na yeye hana mtu wa kumkabidhi zaidi yangu.

“Baba lakini mimi ni msomi, siwezi kutumia mavitu haya, siwezi kujiingiza katika mambo ya aina hii, mimi nitafanya kazi zangu tu za kitaalamu”. Nilimueleza baba ukweli wangu katika kipindi hicho.

“Huu mkoba utauhitaji tu kwa namna yeyote, hata katika hizo shughuli zako, kwahiyo hakuna namna unaweza usiwe muhimu kwako”. Alinieleza Mzee wangu.

“Ikiwa sihitaji kuutumia nifanyeje?”.

Nilimuuliza swali, nilihisi kero sana, mimi msomi na vitu hivi wapi na wapi.

“Usipoutumia utunze vizuri na usikubali mtu yeyote aje akulaghai kwa namna yeyote ili auchukue mkoba huu, utakua umenisaliti”. Aliongea baba kwa msisitizo. Nilimuahidi kuutunza na sitokubali mtu yeyote auchukue. Ila pia nilimuahidi kuwa sitoutumia.

Baba aliridhika, na kunifundisha mambo mengi mno juu ya mkoba ule. Nilimuelewa, ila sikuwa na muda wa kuamini wala kufuatilia habari za ule mkoba. Alinielekeza dua maalum ambayo aliniambia nisimwambie mtu yeyote, dua iliyotumika kuuhifadhia mkoba huu. Dua ambayo aliniambia hakuna mtu wala jini anayeweza kuuona ulipohifadhiwa kwa kutumia dua hiyo.

Nilienda pale chumba kidogo maalumu ambacho ndipo nilipouhifadhi mkoba ule, nikasoma dua yangu maalumu, nikaufungua. Nikachukua dawa moja katika zile zilizofungwa katika karatasi, dawa nyeusi ambayo iliitwa 'Ndaila', nikachanganya katika mafuta ya zaituni kisha nikajipaka mikononi, usoni na kichwani. Nikarudisha dawa zote katika mkoba, nikaufunga kwa dua maalum, kisha nikatoka na kuelekea uani. Nilichuma majani matatu ya mkomamanga, nikafikicha katika mkono wangu ambao ulikuwa na mchanganyiko wa yale mafuta na dawa. Nikatoka uani na kuelekea chumbani ambako nilimuacha Lutfiya. Nilimkuta, amejiinamia akiendelea kulia kilio cha kwikwi.

“Lutfiya, njoo mpenzi wangu, nimekusamehe”. Nilimnyooshea mikono Lutfiya na kumuomba asogelee na kunikumbatia ambao ndio ungekua mwisho wake, angekufa palepale.


Itaendelea...




Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom