NAKUFAHAMU VIZURI
MTUNZI: KJM-0718274130
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
Kofi la Mzee Mbogo liliingia sawasawa sana kwenye shavu langu la kulia. Pamoja na kuniumiza, lakini Mzee Mbogo alinitia hasira sana. Nilianza kuona dhahiri kuwa alikuwa na mpango maalumu juu yangu, alikuwa na kitu anataka kufanya akishirikiana na hawa majini. Nilikaa nikiwa nimeinamia chini nikiuguza uchungu wa lile kofi, mwisho nikasimama.
“Najua mnayotaka kuyafanya, siwezi kumuoa huyo binti Mzee Mbogo, nasema siwezi abadan!!”. Nilisisitiza na kugeukia mlango wa kutokea mle kwenye kile kibanda.
“Kama mimi ndiye babu yako Mzee Mbogo, utamuoa tu Lutfiya”. Alisisitiza Mzee Mbogo.
“Nadhani unalijua vizuri balaa la baba yangu Mzee Ahmad Ngudu. Na unajua vizuri kuwa huwezi kunisumbua Mzee Mbogo. Unapata kiburi cha kunilazimisha kufanya hivi kwa sababu unajua niliachana na hizi habari kwa sababu niliamua kusoma na kujikita katika maisha yangu mengine, naona unanilazimisha nirudi katika asili yangu ambayo siku zote babaangu alikuwa akipigania nisiitelekeze hazina niliyoachiwa. Sasa mimi naondoka rasmi kwa ajili ya kwenda kuanza mapambano tuone upande gani utashinda”. Nilisema kwa hasira kumwambia Mzee Mbogo na kisha nikatoka nje. Nilikuwa na uhakika wa asilimia zaidi ya mia moja kuwa maneno haya yangemuumiza kichwa sana Mzee Mbogo. Nilisimama nje nikifikiria cha kufanya, lakini pia nikijua kuwa lazima Mzee Mbogo atakuja hapa. Naam, haikupita hata dakika moja, Mzee Mbogo alikuwa tayari yupo nje nami.
“Tafadhali Adam, usifanye hivyo tafaadhali sana, haya mambo yanazungumzika”. Alinisihi Mzee Mbogo huku akinipigia magoti. Aliniona jinsi nilivyobadilika, alijua nilimaanisha nilichokisema. Nilimnyanyua pale chini, nikamuomba asimame. Sikupenda kuona babu yangu Mzee Mbogo akinipigia magoti, japo najua alikuwa hana namna nyingine zaidi ya hiyo kwa wakati ule.
“Watoe wale wapumbavu pale ndani halafu tuongee Mzee wangu”. Nilimpa oda Mzee Mbogo ambaye hakuongeza neno zaidi ya kukimbilia ndani. Kitisho nilichompa asingeweza kubishana na mimi kwa lolote ambalo ningemwambia kutoka sasa. Alirudi baada ya mda mfupi na kunieleza kuwa wameshaondoka.
“Vizuri sana Mzee Mbogo”. Nilimpongeza.
“Unataka kufanya jambo baya sana Mzee Mbogo, kushirikiana na wapumbavu kutaka kuharibu kizazi chako mwenyewe kwa tamaa tu ya pesa?”. Nilimtupia swali ambalo hakuweza kulijibu zaidi ya kukaa kimya.
“Unapata faida gani Mzee wangu ukiona sisi tunabaki bila ulinzi? Wewe ungebaki hivyo ulivyo kama wazee wako wangefanya hivyo? Ungekula nini Mzee babu yangu Mbogo kama wazee wako wangejifanya hamnazo kama unavyofanya wewe?”. Niliendelea kumtupia maswali ya lawama Mzee Mbogo ambaye muda wote aliendelea kusisitiza kuomba msamaha. Japo nilielewa kuwa Mzee Mbogo hawezi kurudia huu ujinga, lakini niliamua kukaza, nikiamini kuwa kama ntamdekeza atafanya ujinga zaidi.
“Adam mjukuu wangu, jambo hili halitajirudia tena, wale mabwana walikuja kunishawishi kwa pesa tu baada ya kuona huingiliki kirahisi, na wakataka wautumie udhaifu wako wa kupenda wanawake ili wapate wanachokihitaji”. Mzee Mbogo alifunguka. Nilimuelewa, sikutaka aongee zaidi, nilishaijua dhamira yao. Dhamira iliyopelekea Mzee Mbogo kuniita kule kijijini kwa njia anazozijua mwenyewe.
“Endelea na majukumu yako Mzee wangu, tutaonana”. Nilimuaga Mzee Mbogo na kuondoka pale kijijini.
Nilitembea mwendo mrefu kidogo mpaka nilipokutana na bodaboda ambayo ilinifikisha pale kituoni na kupanda gari zilizonipeleka mpaka mjini, ambako nilienda moja kwa moja nyumbani kwangu na kujitupa kitandani. Macho yangu darini nikiangazia ya dunia na ulimwengu ulivyo. Mawazo tele kichwani, kila moja zuri kushinda mwenzake. Usingizi ukapita na mimi, hadi niliposhtushwa na mwanga mkali wa taa kama siku ile ya nyuma. Nilikumta Lutfiya amekaa pembeni yangu pale kitandani.
“Hongera sana Adam, sikujua kama utapambana kiasi kile, nilidhani ingekua rahisi sana kwangu”. Aliniambia Lutfiya wakati ananitazama machoni.
“Wewe unajifanya kunifahamu, lakini HUNIFAHAMU VIZURI, wewe unanifahamu jina tu na watoto wanne niliozaa nje ya ndoa”. Nilimjibu Lutfiya kwa kujiamini.
“NAKUFAHAMU VIZURI tu, na najua ulilopanga kufanya juu yangu ndio maana nimekuja hapa kukuomba msamaha”. Aliongea kwa kujishusha kidogo Lutfiya, macho yake yalionekana wazi jinsi yalivyogubikwa na uoga.
“Huwezi kunizuia kufanya ninachotaka kufanya, ni lazima nikuonyeshe kuwa watawala wa dunia hii ni sisi binadamu na sio nyinyi majini”. Nilisisitiza mbele ya Lutfiya nikikaa vizuri kitandani pale huku nikimtizama machoni. Niliona machozi yakianza kutiririka mashavuni mwake na kuanza kutoa kilio cha kwikwi.
Itaendelea..
Sent using
Jamii Forums mobile app