HADITHI YA KUSISIMUWA NCHI YA WACHAWI-3-
ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Nilifumba macho na kusubiri tamko jingine kutoka kwa mzee huyo au yule mwenyeji wetu. Nilihisi hali ya kama maji yakinigusa mwilini, kuanzia shingoni kuteremka na uti wa mgongo hadi kiunoni. Yalikuwa ya baridi mfano wake hakuna, nikasema siiiii.
Sii nini kijana wangu? Wewe sasa ni mtu kama mimi, utaishi kama mimi na wala hakuna binadamu yeyote atakayekuweza, mzee Madume aliniambia lakini tukiwa palepale kwenye kitanda alichonikuta.
Ha! Nilisema na kushtuka.
SASA ENDELEA
Ha nini kijana wangu?
Si tulikuwa kwenye..!
Kwenye nini kijana wangu? Nimekukuta hapa na hata sasa tuko hapahapa, alisema, lakini safari hii akiachia tabasamu pana kidogo tofauti na mara zote, nikajua ananitania tu, lakini ukweli tulikwenda mahali.
Nahisi kama naota, kwanza umeingiaje humu ndani kwangu? Nilimuuliza.
Aa, hata wewe utaweza kijana wangu, ndiyo maana nimekwambia wewe sasa ni mtu kama mimi, utaishi kama mimi na wala hakuna binadamu yeyote atakayekuweza.
Nilitaka kumwambia kitu, lakini sikumwona mle ndani, nikashtuka zaidi na kujikuta nimekaa kitadani. Sasa jasho jembamba lilinichuruzika mwilini, hofu ilinipanda, niliamini niliingiliwa na kiumbe wa ajabu aliyejifanya binadamu ninayemfahamu. Niliangalia huku na kule lakini sikuona mtu.
Nilitoka nje, nikasimama kwa muda mlangoni kuangaza kama ningeona kiumbe cha ajabu, pengine kama mtu, lakini mwenyewe akiwa na mguu mmoja, mkono mmoja, jicho moja na kalio moja, lakini hakukuwa na dalili yoyote. Hivyo nilirudi ndani nikifunga mlango kwa uhakika na kujiami, moyoni nikisema: Simfungulii mtu yeyote akitaka kuingia.
***
Nilishtuka asubuhi ya saa kumi na mbili, nikatoka kitandani haraka sana, nilikwenda nje nikiwa na shuka tu. Nilipofika niliangaza huku na kule, nikaona mambo ni shwari, nikarudi ndani.
Nilijiandaa kwa ajili ya kwenda ziwani ambapo nilipofika mtu wa kwanza kukutana naye ni mzee Madume ambaye alinilaki kwa furaha sana huku akinisifu kwa kuwahi kuliko siku nyingine.
Kijana wangu, umewahi, hongera sana. Good.
Nilimkubalia huku nikiuonesha uso wangu kuwa, hauna amani kama siku zote. Naamini hata yeye alinijua kwani alionekana kusinyaisha sura yake.
Kikubwa ambacho alinishangaza ni kitendo cha kunisifia kuwahi wakati ilikuwa kawaida yangu. Labda mimi ndiyo ningeshangaa kwa yeye kuwahi kwani haikuwa kawaida yake, mara nyingi alikuwa akifika jua liko juu.
Basi, nilibadili nguo, kwa kuvua nilizokwenda nazo na kuvaa za kazi, yeye alikuwa ameshabadili za kwake. Wakati navua nguo ili nivae, alinisogelea na kunishika begani na kuniambia:
Uko tayari ufanye majaabu kwa kazi hii ye leo?
Nilisitisha nilichokuwa nakifanya na kumkazia macho ya mshangao:
Wewe nijibu kwanza, unashangaa nini? Wewe kijana wangu bwana.
Nilimkubalia kwa kutingisha kichwa kisha nikatulia kumsikiliza alitaka kuniambia nini. Wakati huo huo akili ikanikumbusha lile tukio la usiku na mzee huyo huyo, nikataka kumuuliza, lakini nikasema moyoni, si ndoto tu.
Kabla hatujaanza shughuli nenda kasimame pale, aliniambia akionesha kidole kwenye mashua moja chakavu saana.
Nilikuwa nimemaliza kuvua na kuvaa nguo nyingine, nikaenda mpaka pale aliponielekeza palikuwa na umbali wa kama hatua kumi za miguu ya mtu mzima.
Wakati nakwenda niligeuka kumwangalia nikiamini kuwa na yeye anakuja nyuma yangu, lakini kumbe ilikuwa ni mimi tu ndiyo nikasimame pale.
Baada ya kusimama niligeuka kumwangalia, yeye naye akawa anageuka huku na kule kuangalia wenzetu wengine kama wanakuja, kasha akaniambia:
Sasa kijana wangu, mimi nakuja huko huku kama nakimbia kidogo, na wewe fanya hivyo hivyo, njoo kama unakimbia, tukikutana tunagonganisha vifua vyetu, halafu utaona matokeo yake tukiingia ziwani.
Nilimkubalia kwa kutingisha kichwa, akaanza kuja huku kama anakimbia, na mimi nilianza kufanya kama yeye, tulikutana katikati ya umbali, tukagongeshana vifua tii.
Rudi kinyumenyume hadi pale pale kisha tunaanza upya, mara tu ndiyo kipimo chake, alisema akiwa anarudi bila kuangalia nyuma.
Wakati tunakimbia kwa mara ya tatu, kabla hatujakutana, wavuvi wawili walitokea na kutushangaa.
Ha! Nyiye, huo ni uchawi au mazoezi? Mmoja alisema, mwenzake akasisitiza kuwa, ni uchawi na kuanza kulalamika kuwa, kumbe ndiyo maana amekuwa akifanya vibaya kazini kumbe kuna watu wanaroga.
Alisema maneno machafu sana licha ya yule mzee kumwomba samahani tena akimwomba asije kusema kwa wavuvi wengine wa eneo letu, lakini yule mzee hakutaka kuelewa, aliendelea kutoa maneno ya kejeli na shutuma.
Nilimwona Mzee Madume ameanza kukasirika huku akiinama na kuchota mchanga mwingi kwenye kiganja cha mkono wa kushoto, akakifumba na mchanga wake kisha akaumwaga pale pale alipouchota.
Sijui nini kilitokea, lakini ghafla wale watu, wote wawili walikimbilia majini na kujirusha huko kimyakimya.
Licha ya kuingia wenyewe, walijitahidi kupiga mbizi ili wasinywe maji, lakini wapi! Wakazama na kutoonekana tena juu.
Niliogopa sana, nilimwogopa sana mzee Madume na kitendo kile. Ilibaki kidogo na mimi nianze kutimua mbio kurudi kwangu. Wakati huo, mke wangu na watoto wawili walikuwa kijijini kwa wazazi wangu kutokana na ugumu wa maisha niliokuwa nao kwa wakati huo.
Kijana wangu usikimbie, mimi si mbaya kwako, ila hawa walitaka kutuhadhiri, we unadhani ingekuwaje leo baada ya wavuvi wengine kufika na kuambiwa? Aliniambia mzee Madume akiwa amenitumbulia macho.
Je, nini kitatokea?
Usikose kufuatilia Kesho wakati kama huu................