Hadithi ya kusisimua- Mimba ya Jini

Hadithi ya kusisimua- Mimba ya Jini

HADITHI YA KUSISIMUWA MIMBA YA JINI-52-

ILIPOISHIA:
Mwezi mmoja kabla ya kujifungua Shehna alimweleza Mustafa kuwa muda ule anatakiwa kuwa sehemu maalum ambayo hatakiwi mtu yeyote kuingiza zaidi mzazi wake na mkunga tu. Pia alimweleza kuonana naye itakuwa baada ya miaka mitatu. Mustafa alikubaliana hakuwa na kipingamizi.

SASA ENDELEA...

Muda ulipofika Shehna alijifungua watoto mapacha watatu wa kike wawili na wa kiume mmoja. Ilikuwa ni furaha ilioje kufanikiwa kupata watoto toka kwa mwanadamu. Wakati wa kujifungua mawasiliano kati ya Mustafa na Shehna yalipotea, siku zote Mustafa alikuwa na hamu ya kuonana na Shehna lakini masharti yalimzuia.
Shehna baada ya matukio yote ya kuhatarisha maisha yake alikatazwa na wazazi wake asionekane mchana katika umbile la kibinadamu kwa muda wa miaka mitano nyongeza ya miaka miwili.
“Shehna kama mtoto umepata, sasa tulia kama ukiwa na shida na baba wa watoto wako tutamleta hukuhuku akiwa ndotoni baada ya miaka mitatu. Lakini kuonana naye akiwa na akili timamu ni baada ya miaka mitano.”
“Kwa hiyo nitarudi lini kama zamani?”
“Baada ya miaka kumi na tano ruksa kurudi tena katika umbile lako la kawaida na kutembea mchana kila mtu atakuwa amesahau yote yaliyopita hata watoto kumtembelea baba yao.”
“Sawa.”
Kuanzia siku ile Shehna aliendelea kulea wanaye kwa muda wote huo hakuweza kuwasiliana na Mustafa japokuwa alijua mzazi mwenzie alikuwa katika mawazo mazito ya kumtafuta mpenzi wake. Lakini aliheshimu maelekezo ya wazazi wake kwa kuhofia kwenda kinyume na kukutwa na matatizo.
Wakati Shehna akipewa maelezo na mama yake upande wa pili nyumba ya Mustafa ilikuwa inawaka moto baada ya wazazi wa Mustafa kumjia juu mtoto wao kutokana na siku kukatika bila kupatikana mtoto. Pamoja na kuwasihi wawe wavumilivu kwa vile mtoto ni siri ya Mungu hawakukubaliana naye.
Walitaka aachane na Husna kwa vile walikuwa wakitaka mjukuu, aliwaeleza mwaka ule ukiisha bila mkewe kushika ujauzito ruksa kuivunja ndoa yao. Wazazi wake walimkubalia na kumweleza mwaka ukikatika bila mtoto watampelekea mke nyumbani kwake.
Mustafa aliondoka kwao kichwa kikimuuma na kujiuliza zawadi aliyotaka kupewa na Shehna ya mkewe kushika ujauzito atapewa lini. Upande mwingine alimlaumu mkewe kwa kitendo chake kukiuka masharti ya Shehna muda ule wangekuwa na mtoto. Kibaya zaidi muda ule alikuwa amepoteza mawasiliano.
Alirudi nyumbani akiwa mnyonge sana, hakujua hatima ya ndoa yake kwa kuona mwaka unaweza kukatika kabla mkewe hajashika ujauzito na kufanya wazazi wake kumletea mke mwingine.
Usiku wa siku ile alichukuliwa na kupelekwa chini ya bahari, aliposhtuka alijiona yupo pembeni ya Shehna ambaye wakati huo hakuwa na tumbo kubwa. Ile ilimjulisha moja kwa moja tayari Shehna amejifungua.
“Pole mpenzi wangu.”
“Sijapoa kwa vile ndoa yangu inavunjika wakati wowote.”
“Najua ndiyo maana nimekuleta huku kabla muda wake, ilikuwa kazi nzito kuwashawishi wazazi wangu uje huku wakati ni juzi tu nimejifungua. Kwanza napenda kukupa hongera ya kuwa baba wa watoto wangu.
“Mungu kajalia nimejifungua mapacha watatu wawili wa kike mmoja wa kiume, wa kike ni wazuri kuliko mama yao na wa kiume ni mzuri kama baba yake. Kwa vile muda wangu wa kutoka huku bado. Niliwaomba wazazi wangu uje tujadiliane ili kuiokoa ndoa yako.”
“Nitashukuru.”
“Sasa kuna kitu nataka tukifanye iwe siri yetu, kwa sasa itakuwa vigumu kwa mkeo kushika ujauzito mpaka watoto wangu wafikishe mwaka. Kwa muda uliozungumza na wazazi wako lazima utapita na wazazi wako watavunja ndoa, najua na wewe unampenda sana mkeo.”
“Ni kweli.”
“Ni hivi nitampatia mkeo mimba tupu ambayo itakuwa ya muda mfupi kuliko mimba zote. Muda ukifika atakwenda kujifungua, kitakachotoka tumboni mwake kitakuwa upepo ambao utafanya wakunga wapitiwe na usingizi mfupi pamoja na mkeo. Sauti ya mtoto ndiyo itakayo washtua wakiamka watakuta mtoto pembeni ya mama yake.”
“Umesema atakuwa na mimba hewa na tumboni kutatoka hewa mtoto huyo atatoka wapi?”
“Mustafa nipo kwa ajili yakuokoa ndoa yako, kati ya wanangu nitamtoa mmoja ambaye wakati wamelala ataletwa na kuachwa hapo ili wakishtuka wajue amejifungua.
Nina imani baada ya hapo kesi itakuwa imeisha kwa wazazi wako kuamini mkeo siyo mgumba.”
“Kwa hiyo utamuachia huyo mtoto?”
“Hapana nitampa kwa miezi mitatu, kisha nitamchukua. Nahofia akianza kukua atakuwa na tabia za ajabu ambazo zitawachanganya hasa mkeo na majirani. Kwako atakuwa mwoga kwa vile ni baba yake lakini kwa mtu mwingine itakuwa vigumu kumsikiliza.”
“Utamchukua vipi?”
“Atapotea katika mazingira ya kutatanisha, usishtuke nitakuwa nimemchukua mwenyewe.”
“Sisi utatuachaje?”
“Najua mkeo ataumia kupotelewa na mwanaye, mbembeleze kwa vile baada ya muda mfupi atashika mimba ya kweli na kuzaa mtoto wa kwenu asiye na masharti.”
“Mmh! Sawa.”
“Mustafa usihuzunike kwa vile sina jinsi lazima nifanye hivyo ili kuokoa ndoa yako, nitakupa dawa utampa kwenye maji akinywa atakuwa na dalili zote za ujauzito. Najua atashtuka mwambie anywe maji glasi moja kuituliza.
Ujauzito huo utakuwa wa miezi mitano safari hii nendeni hospitali ili wazazi wako wajue ujauzito kumbe ni wa muda mrefu, baada ya miezi miwili atajifungua.”
“Sawa.”
Mustafa aliposhtuka akijikuta amelala kitandani kwake akiwa na dawa mkononi. Aliamka na kutulia kitandani kwa muda akikumbuka yote aliyoelezwa na Shehna, hakuwa na jinsi zaidi ya kukubali ili kuiokoa ndoa yake.
Asubuhi kabla ya kwenda kazini alimpa mkewe dawa aliyopewa usingizini na Shehna, baada ya mkewe kunywa alimuaga na kwenda kazini. Alipofika kazini kabla ya kuanza kazi mkewe alimpigia simu hali yake ni mbaya kama mtu mwenye ujauzito wa muda mrefu.


Itaendelea ijumaa usiku.....
 
Asante sana MziziMkavu kwa simulizi hii ya kusisimua..mie nimeshaimaliza ila wamemaliza vibaya kweli..tunasubiri na nyinginezo..
 
HADITHI YA KUSISIMUWA MIMBA YA JINI-53-

ILIPOISHIA:

Asubuhi kabla ya kwenda kazini alimpa mkewe dawa aliyopewa usingizini na Shehna, baada ya mkewe kunywa alimuaga na kwenda kazini. Alipofika kazini kabla ya kuanza kazi mkewe alimpigia simu kumuambia hali yake ni mbaya kama mtu mwenye ujauzito wa muda mrefu.

SASA ENDELEA...

Alimwambia anywe glasi moja ya maji, mkewe alifanya hivyo, baada ya kunywa hali ilitulia lakini alikuwa amechoka sana, alipanda kitandani kulala. Alipoamka alijishangaa kukuta tumbo limekuwa kama ujauzito wa muda mrefu.Ile hali ilimshtua na kumpigia simu mumewe kumweleza kilichotokea.
“Usiogope hiyo ni hali ya kawaida huenda ujauzito huo uliingia muda mrefu, dawa niliyokupa imeufukua hivyo usiwe na wasiwasi. Kama vipi nenda hospitali ukapime hali yako.”
“Mume wangu hunipendi, tuliambiwa nini na Shehna?”
“Amesema sasa tunaweza kwenda.”
“Hapana tafuta ufumbuzi mwingine, sirudii kosa kidogo nife,” Husna aliogopa kurudia kosa.
“Usiwe na wasi mke wangu, Shehna ameruhusu, basi subiri nije nikupeleke mwenyewe.”
“Kama hivyo sawa.”
Mustafa aliacha kazi zake na kurudi nyumbani kumfuata mkewe na kumpeleka hospitali, alipofika nyumbani alishtuka kuona tumbo la mkewe limekuwa kubwa la ujauzito wa muda mrefu.
Lakini alificha mshtuko wake kwa kuhofia kumshtua mkewe na kuona kitu cha ajabu kimemtokea. Alimchukua na kumpeleka hospitali ambako katika kufanyiwa vipimo ilionesha ujauzito upo sawa.
Daktari alishangaa kukaa nao zaidi ya miezi mitano bila kufika hospitali, alimuonya asifanye vile tena kukaa na ujauzito kwa muda mrefu vile.
Baada ya maelekezo waliruhusiwa kurudi nyumbani akiwa amechoka kama ujauzito wote ulipitia hatua zote kufikia hatua ya kumchosha vile.
Walikubali na mumewe kukaa na siri ya chanzo cha ujauzito ule, ilikuwa tofauti na ujauzito anaoufahamu. Miezi miwili baadaye ujauzito ulipofikisha miezi saba kwa vipimo vya hospitali na maelezo ya Shehna, Husna alishikwa na uchungu mkali na kukimbizwa hospitali.
Kutokana na muda wa ujauzito ule, wengi waliamini ni maumivu ya tumbo tu, lakini kulionekana dalili zote za kujifungua.
Baada ya kufikishwa Husna aliendelea kuugungulia huku mkono mmoja umeshika kiuno na mwingine kichwa kutokana na maumivu makali ya uchungu.
Wauguzi walimkimbiza wodini wakiwa hawana uhakika kama siku ile ndiyo ilikuwa ya kujifungua. Baada ya kumfikisha walimpandisha kitandani huku Husna akiendelea kulalamika katika dalili zote za kujifungua. Ilibidi wampe huduma ya kujifungua, Husna alianza kusukuma mtoto, ghafla ulitoka moshi uliowafanya wote walewe na kusinzia.
Muda huo Shehna alimtuma jini wa kike kumpeleka mtoto wake wa kiume aliyekuwa akifanana na baba yake na kumweka pembeni ya Husna. Baada ya muda wote walishtushwa na kilio cha mtoto. Mtoto alikuwa amesha katwa kitovu kabisa na kusafishwa.
Hakuna aliyejua nani kafanya vile, kila mmoja aliamini mwenzake ndiye kafanya. Walimpa hongera mzazi kwa kupata mtoto wa kiume mwenye afya nzuri, hali ya mzazi nayo ilikuwa njema. Alipelekwa wodini kwa huduma zaidi. Baada ya taratibu zote, Husna aliruhusiwa kutoka hospitali na kurudi nyumbani na mwanaye ambaye kila aliyemuona alisema anafanana na baba yake.
Mustafa alijua kila kitu na kubaki na siri nzito moyoni huku amani akirudi nyumbani kwake kwa familia kufurahi na kusema mpaka wamtishe ndipo atafute mtoto. Japokuwa yule mtoto alikuwa wa kwake lakini hakuwa wa mkewe bali wa jini Shehna.
Siku nazo zilikatika muda nao ulisogea mtoto wa Shehna kurudi kwa mama yake.
Miezi mitatu ilipotimu, alitumwa jini kumfuata mtoto, akiwa katika umbile la kibinadamu mwanamke aliyevaa kiheshima. Jini Shaunani alitembea taratibu na kubisha hodi kwenye nyumba ya Mustafa.
Wakati huo mke wa Mustafa alimkuta amemaliza kumnyonyesha mtoto, alikwenda kufungua mlango na kumuona mwanamke mzuri aliyekuwa akinukia manukato kama anayotumia mumewe.
“Karibu.”
“Asante,” mgeni alijibu huku akiingia ndani.
Alipofika aliketi na kusema:
“Habari za hapa.”
“Sultani hajambo?” lilikuwa jina la mtoto ambalo Mustafa aliambiwa ampe mtoto na ndilo lilikuwa jina lake la ujijini.
“Hajambo.”
“Hebu nimuone.”
Husna bila wasi alimkabidhi mtoto jini Shaunani ambaye alikuwa mcheshi sana. Kutokana na ucheshi wake, alimzoea haraka Husna, hakuwa na wasiwasi alimuomba samahani.
“Samahani mgeni natoa vyombo vya mtoto.”
“Hakuna tatizo.”
Husna alirudisha vyombo vya mtoto jikoni na kurudi kumsikiliza mgeni, baada ya kukaa alimkaribisha tena.
“Karibu mgeni.”
“Asante,” kabla Husna hajaongeza neno simu iliita na kumshangaza kuitia chumbani wakati alikuwa nayo muda mfupi na hakurudi chumbani.
“Jamani hii ajabu simu nilikuwa nayo hata sijui niliondoka nayo muda gani kwenda nayo chumbani.”
“Labda umesahau haiwezi kujibeba yenyewe, kasikilize huenda ni shemeji,” jini Shaunani alisema.
Husna alinyanyuka na kwenda kupokea simu, kitendo cha kuingia chumbani tu. Jini Shaunani alitoweka na mtoto. Husna alipofika chumbani alishangaa kukuta simu haina ‘missed calls’. Alishangaa wakati alisikia simu ikiita kabisa hata mgeni alisikia.
Alitoka sebuleni alishangaa kukuta sebule tupu, hakuna mgeni wala mtoto wake.
“Mgeni...mgeni,” aliita kwa sauti.
Hakukuwa na jibu alitoka nje labda ametoka vilevile hakukuwa na jibu lolote, alijiuliza atakuwa amekwenda wapi.
Alitoka hadi nyumba ya pili labda wamemuona mtu akiwa na mtoto nao walisema hawajamuona. Alimpigia simu mumewe kumueleza kupotea ghafla kwa mwanaye.
Taarifa ile haikuwa ngeni kwa Mustafa, alijua mtoto keshachukuliwa na mama yake. Alirudi nyumbani haraka ili kumtuliza mkewe ambaye muda ule alikuwa amepagawa.
Alipofika alimkuta amepagawa akilia ovyo mikono kichwani. Husna alipomuona mumewe alimkimbilia na kumkumbatia na kuendeleza kilio.
“Mume wangu mwanangu ameibiwa!”

Itaendelea Jumapili usiku.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom