Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
SEHEMU YA 26

“Kwani ulikuwa unahitaji nini?” alisikika Sultan akiuliza swali huku simu ikiwa sikioni mwake.
“Kukutana na wewe, nahitaji kuzungumza kuhusu biashara!” alisema mwanaume aliyekuwa upande wa pili.
“Biashara gani?”
“Kama uifanyayo! Kutoa nafaka mikoani na kuleta mjini. Nina ekari zaidi ya mia moja za mahindi, tunaweza kuzungumza kidogo?” aliuliza jamaa wa upande wa pili.
“Haina shida. Upo wapi?”
“Huku Tukuyu, Mbeya.”
“Aisee! Kwa hiyo tunafanyaje?”
“Sisi tuongee tu halafu nitamtuma mtu wangu aje kuzungumza nawe kiundani pamoja na kuweka mikataba, biashara kubwa hii ni lazima tufanye kiutu uzima,” alisema mwanaume wa upande wa pili.
Hakuna mtu aliyekuwa akipenda kufanya biashara kama Sultan, kwenye maisha yake alikuwa tayari kukosa kitu chochote kile lakini si michongo kuhusu biashara.
Alikuwa tajiri, utajiri wa kishirikina lakini hiyo haikumfanya kuachana kujituma na kutafuta pesa. Kwenye akaunti yake kulikuwa na zaidi ya bilioni themanini lakini hilo halimfanya kukaa tu nyumbani na kutumia.
Ndoto yake ilikuwa ni kuwa na pesa kuliko watu wote Tanzania, kila alipokuwa akipelekewa dili la biashara, hakutaka kulaza damu, haraka sana aliwasiliana na mtu huyo na kufanya biashara hiyo na kuingiza kiasi kikubwa cha pesa.
Leo alipokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakuwa akimfahamu kabisa, alimwambia alikuwa na shamba lake kubwa la ekari zaidi ya mia moja na alipanda mahindi ana alitaka kuvuna, hivyo walitakiwa kuzungumza.
Sultan hakuwa na hofu kwa sababu hiyo haikuwa simu ya kwanza kuipokea kuhusu mchongo wa biashara, mara nyingi alikuwa akipigiwa simu na watu asiowafahamu na kuzungumza nao, alipewa ishu ya biashara na kuifanya kwa mafanikio makubwa.
Alizungumza na mtu huyo kisha kukata simu, akashusha pumzi ndefu, kama kweli mtu huyo alikuwa na ekari mia moja za mahindi, kwake ilikuwa ni biashara nzuri sana, alitaka kufanya kila liwezekanalo anaondoka na faida kubwa.
Akachukua kalkuleta yake na kuanza kufanya mahesabu, alipomaliza akaangalia vizuri kiasi cha pesa ambacho angeingiza, akatoa tabasamu pana, alifurahi na kuona alikuwa akienda kutajirika kupita kawaida.
Alipozungumza na mtu yule, walikubaliana kwa kila kitu na alichomwambia angepigiwa simu na msimamizi wake aliyekuwa Dar es Salaam ambapo wangepanga kuonana na kulizungumzia zaidi.
Kwake halikuwa na tatizo, akasubiri na baada ya saa moja, simu yake ikaanza kuita, haraka sana akaichukua na kuipokea, sauti ya msichana ikaanza kusikika kutoka upande wa pili.
“Nipo Posta ofisini,” alisema baada ya kuulizwa alikuwa wapi waonane.
“Basi nakuja. Naomba tuonane Pizza Hut,” alimwambia.
“Haina shida.”
Kwa jinsi sauti ile alivyoisikia kupitia simu yake, moyo wake ulimwambia tu alikuwa akizungumza na msichana aliyekuwa mrembo mno, ambaye urembo wake inawezekana haukuweza kuonekana kwa mwanamke yeyote katika dunia hii zaidi ya Malkia Cleopatra ambaye anaendelea kusifika kuwa mwanamke mwenye sura nzuri kuliko wote.
Hakutaka kupoteza muda, haraka sana akatoka ofisini kwake, akachukua usafiri wake na safari kuelekea Pizza Hut kuanza, ilikuwa mkabala na jengo la Uhuru Height, karibu kabisa na Serena Hotel
Alipofika hapo, akatulia na kuanza kuangalia huku na kule. Moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kumuona msichana huyo, kulikuwa na wanawake wengi waliosikika kuwa na sauti nzuri kwenye simu lakini baada ya kumuona alikuwa wa kawaida sana, labda mbaya.
Lakini kila alipoisikiliza sauti ya msichana aliyezungumza naye, alikuwa na uhakika alikuwa mzuri mno, inawezekana kabisa aliendana na sauti yake, hivyo alikuwa na hamu ya kumuona.
“Huyu atakuwa demu mkali sana! Kama ni mkali kweli, simuachi,” alisema huku akijiweka kwenye kiti na pizza ndogo ikiwa mezani.
Alitulia kwa dakika kadhaa, mara macho yake yakatua katika gari ndogo tu, Vitz iliyokwenda mpaka sehemu ya maegesho na kutulia hapo, mlango ukafunguliwa na kuteremka msichana mmoja.
Moyo wa Sultan ukapiga paa! Hakuamini kile alichokuwa akikiona mbele yake. Akaanza kujiuliza kama yule aliyekuwa akimuona ndiye ambaye alitakiwa kuzungumza naye ama la.
Huku akiwa anajiuliza, akamuona msichana yule akipiga hatua kuelekea ndani ya mgahawa ule, si yeye tu aliyekuwa akimwangalia kwa uzuri wake, hata watu wengine waliokuwa humo wote walikuwa wakimtolea macho.
“Ndiye yeye ama?” alijiuliza, ghafla akagonganisha macho na msichana yule, akatolewa tabasamu na kumsogelea.
“Bila shaka ni Sultan!” alisema msichana yule huku akimwangalia, Sultan akabaki akitetemeka, hakuamini kama msichana yule alimsogelea na kumuuliza swali ambalo jibu lake lingekuwa jepesi sana, ‘Ndiye mimi, karibu sana’.
“Ndiye mimi!” alimwambia huku akimwangalia, hakuishia hivyo tu, akasimama na kumpa mkono, akamkaribisha.
Msichana huyo alikuwa Shunie.
Shunie akakaa kitini na kumwangalia mwanaume aliyekuwa naye hapo mezani, kwa jinsi alivyokuwa mzuri aliamini tu Sultan ni lazima angemtamani kwani hapakuwa na mwanaume aliyeweza kuhimili uzuri wake mkubwa na kuacha kumtongoza.
Alimwangalia Sultan, kwa jinsi alivyoonekana tu ilikuwa ni rahisi kugundua kwamba tayari alikwishampenda na kitu pekee alichokuwa akisubiri mahali hapo ni mwanaume huyo kutupa ndoano na kumnasa.
“Kwa hiyo vipi kuhusu usafirishaji?” alimuuliza Shunie.
“Hiyo ni juu yako!”
“Ila ninapochuaga mizigo kutoka mashambani, huwa wanaoniuzia wanniunganishia na watu wa usafiri na kulipia, nilihitaji kujua kuhusu nyie,” alimwambia.
“Bosi alisemaje?”
“Kwamba utanijibu maswali nitakayokuuliza!”
“Hata hili pia?”
“Yaap!”
Si kwamba hakuwa akijua kitu chochote kile, alikuwa akifahamu kila kitu ila alifanya hivyo kwa kuwa alihitaji kupata muda wa kuzungumza na msichana huyo mrembo.
Alihitaji kumzoea, kuzungumza naye mengi lakini mwisho wa siku amwambie kile alichokuwa akihitaji. Kwa mwanaume yeyote duniani kumuacha mwanamke kama Shunie ilikuwa ni ujinga sana, na hata kama ungepata nafasi na kuwaambia wenzako kuwa ulimwacha msichana mrembo kama huyo akiondoka huku ukiwa hujaonyesha jitihada zozote, hakika hukutakiwa kuishi, ilibidi upelekwe Uarabuni, atokee mtu ajitoe mhanga karibu na sehemu ulipokuwa ufe.
“Ila tukiachana na biashara sasa,” alimwambia huku akimwangalia.
“Eeh! Kuna jingine?”
“Labda ni swali tu!”
“Lipi?”
“Huu uzuri umeuchukulia wapi?” alimuuliza huku akijitahidi kuonyesha tabasamu pana.
“Mh! Jamani! Sasa nani mzuri?”
“Wewe hapo!”
“Hapana! Ni kawaida sana!”
“Basi acha nibadilishe swali. Huu ukawaida umeuchukulia wapi?” alimuuliza.
Shunie akaanza kucheka, alitoa kicheko cha chinichini kuonyesha alifurahi sana kusifiwa kama alivyotaka. Hilo ndilo lilikuwa lengo lake, hakuwa mwanamke wa kawaida, alikuwa jini ambaye alifika mahali hapo kwa lengo la kumuua huyo Sultan.
Mwanaume huyo hakuyajua hilo, tamaa kubwa ilimuingia na jambo pekee alilokuwa akilifikiria ni kufanya mapenzi na Shunie tu. Kila alipomwangalia, aliisikia kabisa roho yake ikimwambia alitakiwa kulala naye.
Ndiyo! Alale na Shunie.
Alikuwa mwanamke mzuri.
Mwenye figa matata.
Lipsi nene kidogo.
Alijua kucheka na kuongea.
Sasa kama asingetubutu kulala na huyo akalale na nani?
“Natamani sana niendelee kuongea nawe mpaka usiku,” alimwambia Shunie.
“Mpaka usiku?”
“Ndiyo!”
“Na mkeo?”
“Hahaha! Sina mke, demu wa mchumba,” alimjibu.
“Mh! Nyie wanaume waongoooo!”
“Kweli tena! Bosi wako hakukwambia kama unakuja kuonana na mwanaume aliyekuwa singo maisha yake yote?” alimuuliza.
“Nitaamini vipi sasa?”
“Hata tukienda nyumbani! Nikae na wewe wiki nzima, uchukue simu yangu, ukae nayo kipindi chote kile, hakuna mtu atakayepiga simu na kukuulizia mimi ama kukwambia kama yeye ni mke wangu,” alisema Sultan.
“Mh! Wanaume nyie!”
“Unaitwa nani kwanza?”
“Shunie!”
“Aliyekupa jina alijua ni kwa namna gani utakuwa mzuri kiasi hiki. Jina lako na uzuri wako ni vitu viwili vinavyotembea pamoja, kama kidevu na ndevu,” alimwambia, wote wakaanza kucheka.
“Kwa hiyo?”
“Alimuuliza!”
“Mi’ namuogopa mkeo bwana!”
“Sina mke! Si nimekwambia lakini! Haki ya Mungu sina mke!”
“Nitaamini vipi? Nisije kutolewa ngeu!”
“Twende kwangu! Utaamini tu!” alimwambia.
“Sawa!”
Alivyoambiwa neno sawa tu, akajiangalia kwenye suruali yake, sehemu ya zipu na kuona kama imetuna fulani hivi. Mwili wake ulikumbwa na pepo la ngono, hakuthubutu kumuacha msichana kama Shunie.
Alikuwa mrembo mno, mpaka wanaondoka pale na kuingia ndani ya gari, watu waliokuwa mahali hapo walikuwa wakiwaangalia tu. Shunie hakuingia ndani ya gari lake, aliliacha mahali hapo na kuondoka zake kwa kutumia gari la Sultan ambaye alikuwa akiliendesha kuelekea huko nyumbani kwake.
Njiani walikuwa wakizungumza mambo mengi, ni kama walikuwa watu waliofahamiana kipindi kirefu kilichopita. Sultan alijitahidi sana kuwa mchangamfu kwani aliamini ili kumuondolea hofu zaidi Shunie ni kuwa mchangamfu tu.
Huku akiendesha gari, macho yake yalikuwa yakiibia kuangalia mapaja ya msichana huyo, aliyatamani na muda wote alikuwa akifikiria ni kwa namna gani angeweza kulala na msichana huyo mrembo.
“Leo huyu simuachi! Halafu ule mkongo wangu si ninao! Yaani leo ukisikia vita ya tatu ya dunia ndiyo hii,” alisema huku akionekana kupania mechi.
Hawakuchukua muda mrefu, wakafika nyumbani kwake, mlinzi akafungua geti na kuliingiza gari lake ndani. Akateremka na kwenda upande wa pili, akamfungulia mlango Shunie na kuteremka.
Mlinzi alichanganyikiwa, alimwangalia Shunie huku akiwa haamini kama bosi wake alimpeleka mwanamke mzuri nyumbani hapo kama huyo Shunie. Mlinzi huyo alikuwa na rafiki yake, wote walipigwa na butwaa na kumwangalia Shunie tu.
“Aisee! Shemeji karibu sana,” alisema mlinzi huku akionekana kuchanganyikiwa mno.
“Ahsante sana!”
“Kaka shikamoo!” alimwambia, haikuwa salamu kama salamu, alimwambia hivyo kama kukubali kile alichokuwa akikiona.
“Nimekuletea mama yako! Umuheshimu sasa, ndiye mama wa nyumba hii kuanzia leo,” alisema Sultan huku akimwangalia mlinzi, na sura yake ilikuwa na tabasamu pana.
“Hakuna shida Baba! Karibu sana mama!” alisema mlinzi.
“Nashukuru sana!” alisema Shunie, hao wakaingia zao ndani.
“Kaka tutafute pesa! Tutafute pesa kaka! Tusikae kama wajinga tu! Tutafute pesa kaka la sivyo kila demu mkali kama huyu utaishi kumuita kaka, mama tu kama ulivyofanya," alisema rafiki yake mlinzi aliyeitwa Iddi, yaani wote hapo walichanganyikiwa kwa uzuri wa Shunie, hawakujua kama Sultan aliingiza jini ndani ya nyumba hiyo.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa hapahapa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom