Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Story kunoga ikisindikizwa na shunie Wa humu hongera kwako shunie
 
NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
SEHEMU YA 28

Bonge alikuwa baa, alikunywa sana lakini hakulewa, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, kifo cha Sultani kilimfanya kutokuwa sawa kabisa. Kwa namna kifo kile kilivyotokea ilionyesha kabisa kulikuwa na kitu, inawezekana kulikuwa na mwanamke jini alimuua ama mtu wa kawaida tu.
Kwa jinsi hali ilivyokuwa ilikuwa ni vigumu kuamini kama Sultani aliuawa kwa sababu aliamini walikuwa na ulinzi mkubwa, yaani walikuwa na nguvu fulani iliyokuwa ikiwalinda nyuma yao, hivyo kuuawa kizembe vile lilikuwa suala lisilowezekana hata kidogo.
Labda alikufa kwa presha!
Aliliwaza hilo, kuuawa kilikuwa kitu ambacho hakikuingia kichwani mwake hata mara moja, nguvu waliyokuwanayo ilikuwa kubwa kupita kawaida. Alikaa kaunta huku akiyapitia hayo yote, akiyafikiria kwa kina kabisa lakini akakosa jibu.
Alikunywa mpaka ilipofika majira ya saa nane, alipoona halewi, akaamua kutoka baa, alikuwa akitembea kwa mwendo wa kawaida kana kwamba hakuwa amekunywa pombe yoyote ile, aliliendea gari lake na kuingia ndani.
“Pombe hazileweshi tena, naona kama nakunywa juisi,” alisema, akaupiga usukani na kuanza kuondoka mahali hapo.
Aliendesha kwa mwendo wa kawaida tu alipofika maeneo ya Morocco, akamuona msichana mmoja akiwa amesimama pembeni ya barabara akimpungia mkono kumtaka kusimama.
Kwanza akataka kupitiliza, mahali hapo hapakuwa na mtu yeyote zaidi ya msichana huyo, ilikuwaje awe mahali hapo? Hakuwa anaogopa jinsi kulivyokuwa, akawaza kumpita lakini napo moyo wake ukawa mgumu kufanya hivyo.
Alihitaji msaada, alikuwa mahali hapo peke yake, endapo msichana huyo angevamiwa na kundi la watu, akaibiwa na kubakwa, hakika lingekuwa jambo baya sana, linawezekana hata kumletea laana kwa kuwa alihitaji msaada wake lakini alikataa kufanya hivyo.
Hayo yote yaliibuka kichwani mwake ndani ya sekunde chache tu na uamuzi alioufikia ulikuwa ni kusimama karibu na msichana huyo na kumtaka kuingia ndani, akaufungua mlango na kuingia.
Harufu nzuri ya manukato ya msichana huyo yakaanza kumpa burudani puani mwake, alinusa vilivyo, yalikuwa manukato yenye harufu nzuri ambayo hakuwahi kuyanusa sehemu nyingine yoyote ile.
Alimwangalia msichana huyo, alikuwa mrembo mno, hakutakiwa kuwa hapo usiku huo eti akisubiri kupewa lifti, kwa jinsi alivyokuwa, alitakiwa kuwa na mwanaume mwenye pesa ambaye angemchukua na kumpeleka popote pale alipotaka kwenda.
“Nashukuru kwa kunisaidia,” alisema msichana huyo.
Sauti yake ilikuwa kitu kingine kabisa kilichouvuruga moyo wa Bonge, hakuamini kama kulikuwa na msichana aliyekuwa na sauti nyororo, ya kumtoa nyoka pangoni kama huyo aliyeingia ndani ya gari lake.
“Mbona usiku hivyo na upo peke yako sehemu hatarishi kama hii?” aliuliza Bonge huku akimwangalia msichana huyo.
“Yaani acha tu! Nimetoka kwenye pati ya rafiki yangu,” alijibu msichana huyo.
“Oh! Lakini ulitakiwa kuwasiliana hata na bodaboda akaja kukuchukua, usiku una mambo mengi sana,” alisema Bonge.
“Yaani acha tu!”
“Kuna nini kwani?”
“Hata simu sijui nimeiwekea wapi! Nadhani nimeibiwa kwenye pati!” alijibu.
“Pole sana!”
“Nashukuru!”
Kila mmoja akakaa kimya kwanza, kichwa cha Bonge kilikuwa kikimfikiria rafiki yake tu, hakuwa kwa huyo mwanamke hata kidogo. Hakuwa mtu wa wanawake, alipenda kufikiria kuhusu biashara zake, kuhusu watu hao aliwapa kisogo kabisa.
“Unakwenda wapi?”
“Nyumbani, hapo Mwananyamala! Wewe unakwenda wapi?” alijibu msichana huyo na kuuliza.
“Nyumbani kwangu, Kawe. Acha nikufikishe huko kwako halafu mimi nitaendelea na safari, wala usijali,” alisema Bonge.
“Nitashukuru sana!” alisema msichana huyo.
Wakaendelea na safari, kazi ya msichana huyo ilikuwa ni kumuelekeza njia tu na Bonge alikuwa akizipita mpaka walipofika KWa Manjunju ambapo wakakata kona ya kushoto kama unaelekea Tandale Chama, mbele kidogo karibu na daraja akamwambia Bonge asimamishe gari.
“Nimefika! Nyumbani ni hapo mbele,” alisema msichana huyo.
“Utafika salama?”
“Yeah! Wala usijali! Asante!” alisema na kuufungua mlango, akatoka, akaufunga na kuondoka mahali hapo, Bonge akageuza gari na kuondoka zake.
Hapo kidogo akaanza kumfikiria msichana huyo aliyempa lifti, alionekana kuwa tofauti kabisa, lilikuwa suala gumu kwa msichana mrembo kama yeye aende sehemu, usiku sana, awe peke yake halafu asiwe na hofu hata kidogo.
Alihisi labda alikuwa msichana aliyekuwa akijiuza na siku hiyo biashara yake ilimuendea vibaya na ndiyo maana aliamua kurudi nyumbani haraka sana.
Hakuchukua dakika nyingi, akafika nyumbani kwake, akaliingiza gari lake na kuelekea chumbani ambapo akalala usingizi mzito.
Majira ya saa tatu asubuhi akaamka, akainuka na kueleka bafuni kuoga, alipomaliza, akarudi chumbani kwake na kutulia huku akifikiria ni kwa namna gani angeianza siku hiyo hasa kwenye mambo ya biashara yake. Akiwa anafikiria hayo, mara simu yake ikaanza kuita, akaichukua, namba ilikuwa ngeni, akaipokea na kuipeleka sikioni.
“Halo!” aliita.
“Halo Christopher!” ilisikika sauti ya mwanamke kutoka upande wa pili.
“Halo!”
“Nashukuru kwa msaada wako, nilifika salama!” alisikika.
“Ulifika salama? Wewe nani?”
“Msichana uliyempa lifti jana!”
“Msichana niliyempa lifti jana? Umenjuaje kama naitwa Christopher?” aliuliza huku akionekana kushtuka kidogo.
“Uliniambia jana!”
“Nilikwambia?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Na namba yangu umeipataje?”
“Ulinipa pia!”
“Nilikupa na namba yangu?”
“Eeh! Jamani kweli ulikuwa umelewa! Nimeamini hilo!” alisema msichana huyo na kutoa kicheko kidogo cha chini.
“Nililewa? Hapana! Sikulewa!”
“Ulilewa. Kwani wewe uliniambia ulitoka wapi?”
“Nilikwambia nilipotoka kwani?”
“Ndiyo! Ulisema umetoka baa kunywa, una mawazo ya rafiki yako kipenzi aliyekufa nyumbani kwake!” alisema msichana huyo.
“Mh!”
“Ndiyo! Sasa mimi ningeyajuaje kama usingeniambia?” aliuliza msichana huyo.
Maneno aliyoyasema yalikuwa sahihi kabisa, kwa Bonge ilikuwa ni vigumu kuamini uchawi ama jambo lolote lile, maneno hayo yalionyesha ni kwa namna gani alikuwa amelewa, yaani alimwambia msichana huyo mambo mengi ambayo hakumbuki hata kama aliwahi kuyatamka.
Alijuaje? Hapakuwa na sababu nyingine zaidi ya yeye kumwambia tu, na kama aliyajua, alikuwa na uhakika asilimia mia moja alimwambia na ndiyo maana aliyafahamu.
“Halooo!” aliita msichana huyo baada ya ukimya wa sekunde kadhaa.
“Naam! Nipo! Okay nimekuelewa. Unaitwa nani binti?” aliuliza.
“Shunie!”
“Oh! Sawa. Nashukuru sana!”
“Haina shida. Nitakuja ofisini kwako kukusalimia pia,” alimwambia.
“Ofisini kwangu?” akauliza Bonge, sasa hapa akashtuka zaidi.
“Ndiyo!”
“Napo nilikwambia ninapofanyia kazi?”
“Ndiyo! Inaelekea umesahau mengi sana. Kuwa makini jamani! Pombe sio nzuri,” alisema Shunie.
“Sawa. Nashukuru sana,” alisema na kukata simu.
Bonge akabaki akiwa ameduwaa, kwa yale aliyokuwa ameambiwa hakika yalimchanganya kupita kawaida, hakuamini kama yeye alimwambia msichana huyo maneno yote hayo.
Alikuwa na uhakika hakuwa amelewa sana lakini kitendo cha kuambiwa hayo yote kilimfanya kuwa na hofu tele kwamba kulikuwa na mambo mengi aliyomwambia. Alihisi hakuwa amelewa lakini kwa jinsi Shunie alivyomwambia hayo yote, sasa akapata jibu alilewa ila hakujua kama alilewa.
Hakutaka kujali sana, alichokifanya ni kuendelea kujiandaa na kuondoka kuelekea ofisini kwake. Njiani aliwaza mengi kuhusu Shunie, yale aliyomwambia hakika yalikichanganya kichwa chake, hakuwa akiamini kama alikuwa muwazi kwa mwanamke kama alivyokuwa kwake na wakati hakuwahi hata kuonana naye kabla.
Hakuchukua muda mrefu akafika ofisini kwake, haraka sana akaanza kufanya kazi huku akimwambia sekretari wake ampelekee mafaili ambayo alitakiwa kuyafanyia kazi. Akapelekewa mafaili hayo na kuanza kufanya kazi zake, ilipofika majira ya saa tano asubuhi akaambiwa kulikuwa na mgeni wake.
“Yupoje?”
“Ni mwanamke. Mzuri kweli!”
“Mwambie aingie!”
“Sawa.”
Ndani ya sekunde kadhaa, mgeni huyo akaingia, alikuwa Shunie, msichana aliyekuwa mrembo kupitiliza, alivalia vazi fulani laini lililoonyesha mpaka maungo yake ya ndani kwa mbali.
Uso wake ulikuwa na tabasamu pana, tabasamu ambalo baada ya Bonge kuliona tu, naye akatabasamu, wakasalimiana kwa kushikana mikono na msichana huyo kukaa kitini.
“Umependeza,” alimwambia huku akimwangalia.
“Sikushindi wewe!” naye akamwambia.
Walikaa na kuzungumza mambo mengi, muda wote Bonge alikuwa mtu wa kufurahi tu, hakuamini kama kwenye maisha yake sasa amekutana na msichana aliyekuwa mrembo kama huyo.
Baada ya dakika chache akapokea simu ya mezani kutoka kwa sekretari wake ambaye alimwambia kulikuwa na mgeni mwingine aliyetaka kumuona.
“Nani?”
“Bazoka!”
“Bazoka?” aliuliza, Shunie akashtuka.
“Ndiyo!”
“Mwambie aingie,” alisema Bonge, aliruhusu Bazoka aingie kwa lengo moja tu, alihitaji kumtambia kuwa na msichana mzuri kama yule aliyekuwa kwenye kiti, mlango ukafunguliwa na Bazoka kuingia ndani, macho yake yakagongana na ya Shunie aliyekuwa kwenye kiti.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumanne hapahapa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom