Hadithi: siku za mwisho za uhai wangu

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,445
4f402527e5c48bb105b52c88c8a121cb.jpg

MIKE MARTIN 1958-1996 (1)

ILIKUWA ni alfajiri yenye mawingu mazito angani. Kila mtu alijua mvua ingenyesha siku hiyo kwani dalili zote za mvua zilikuwepo angani. Waliokuwa wamelala walizidi kujifunika mablanketi vitandani mwao na waliokuwa wameamka walivaa masweta na kuendelea na shughuli zao za kila siku. Ndege wa kila aina walisikika wakilia mitini, jambo lililoashiria kuwa siku mpya ilikuwa imeanza.

Wakati huo Mike Martin alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Nsumba. Alikuwa kijana mkimya, mtaratibu na asiye na makuu katika mambo yake. Akiwa katika umri wa miaka kumi na minane, Mike alikuwa kijana mwenye uwezo mkubwa sana darasani. Alijali na kutilia maanani sana masomo yake.

Zaidi ya hayo, Mike alikuwa na uwezo mkubwa wa kuongea na kuandika kwa lugha ya Kiingereza, jambo lililofanya awe kivutio kikubwa sana miongoni mwa wanafunzi wenzake. Walimu wake walijivunia kuwa na mwanafunzi kama yeye.

Sifa za Mike hazikuishia hapo, alikuwa na sifa nyingine tena ya ziada ambayo ni kucheza muziki. Sio siri, Mike alijua namna ya kuucheza muziki, hasa wa Pop, kiasi kwamba wanafunzi wenzake walimbandika jina la “Double M” au Michael Jackson wa Tanzania!

Sifa za Mike zilitapakaa sana katika shule zote za sekondari mjini Mwanza, hasa katika shule ya Ngaza ambako alikuwa gumzo kwa kila msichana. Kutokana na sifa hizo wasichana wengi walitamani sana kumwona Mike ana kwa ana.

Mara kwa mara alipokea barua, kadi na maua kutoka kwa wasichana mbalimbali asiowafahamu wa shule ya Nganza. Sifa nyingine kubwa aliyokuwa nayo ambayo iliwashangaza hata wanafunzi wenzake ni uhusiano wake na wasichana. Mike hakuwahi kutembelewa na mwanafunzi wa kike kutoka shule nyingine ambaye wanafunzi wenzake wangeweza kuhisi alikuwa mpenzi wake!

Pamoja na kufikisha umri wa miaka kumi na minane alikuwa bado hajakutana na mwanamke kimapenzi. Si kwamba alikuwa na kasoro, ila hakuona umuhimu wa kufanya mawasiliano na wasichana kwa wakati huo. Jambo hilo liliwatesa wasichana wengi waliotamani kuwa na uhusiano naye kimapenzi.

Kijiografia shule za sekondari za Nsumba na Nganza zilikuwa jirani zikiwa zimetenganishwa na kilima kidogo tu katikati. Kwa muda mrefu wanafunzi wa shule hizo walikuwa na uhusiano mzuri wa ujirani mwema.

Wanafunzi wa shule ya Nsumba walipokuwa na sherehe, waliwakaribisha wanafunzi wa shule ya Nganza ambayo ilikuwa ni ya wasichana watupu.

Vilevile, wanafunzi wa Nganza walipokuwa na sherehe waliwaalika wanafunzi wa shule ya Nsumba iliyokuwa ya wavulana watupu, kwenda kucheza nao muziki. Huo ndio uliokuwa uhusiano wa shule hizo mbili.

***
Mara ya kwanza Mike kufika shuleni Nganza ilikuwa Mei 23, 1975. Siku hiyo wanafunzi wa Nsumba walikuwa wamealikwa kwenye malumbano ya hoja ambayo kwa kimombo huitwa “debate.” Yalikuwa ni juu ya Yapi Yalikuwa Maisha Bora kati ya Maisha ya Mjini na ya Vijijini. Malumbano hayo yalifanyika katika ukumbi wa sherehe wa shule ya Nganza.

Mike alipoondoka Nganza, nyuma yake aliacha gumzo kwa jinsi alivyojichukulia pointi nyingi baada ya kuongea Kiingereza kama mtu aliyezaliwa Uingereza! Aliwavuta wasichana wengi sana.
Miongoni mwa wasichana waliochanganyikiwa juu yake, alikuwa ni Beatrice Rugakingira. Huyu alikuwa ni msichana mrembo kutoka mkoa wa Kagera, aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo.

Beatrice alipomwona Mike akiongea, alijihisi kuchanganyikiwa! Ni wazi nyota ya Mike iliishinda ya Beatrice na kuiburuza vibaya mno. Beatrice alitamani sana kuongea na Mike lakini alishindwa aanze vipi kwa kuwa wasichana wengi walimfuata baada ya malumbano hayo na kumwomba anwani yake na vitu vingine.

Hivyo Beatrice hakubahatika kabisa kuongea naye kitu chochote mpaka anaondoka, jambo hilo lilimuuma sana moyoni mwake lakini yote alimwachia Mungu. Aliamua kuwa mvumilivu akikumbuka methali isemayo milima haikutani lakini binadamu hukutana. Aliamini siku moja angekutana na Mike na kumweleza kilichokuwa kikiendelea moyoni mwake.

Tabia za wasichana katika shule ya Nganza ziligawanyika katika makundi matatu. Walikuwepo waliokuwa na uhusiano wa kimapenzi na wavulana kutoka shule mbalimbali za sekondari mjini Mwanza kama vile Bwiru na Nsumba.

Kundi jingine lilikuwa ni la waliokuwa na uhusiano na wafanyabiashara maarufu mjini humo na kundi la tatu na la mwisho, lilikuwa ni la wasichana walioliwazana wenyewe kwa wenyewe. Hawa waliitwa wasagaji au lusibo.

Tofauti sana na wasichana wengi, Beatrice alikuwa msichana mpole ambaye katika umri wake wa miaka kumi na mitano, kama ilivyokuwa kwa Mike, hakujihusisha na kundi lolote kati ya hayo matatu. Kifupi alikuwa hajawahi kukutana kimwili na mwanamume yeyote, jambo ambalo halikuwa rahisi kwa wasichana wa shule ya Nganza wa wakati ule.

Je nini kitaendelea?
Huu ni mwanzo wa hadithi hii nzuri yenye kufundisha na kuburudisha.
 
SEHEMU YA 02

Mvulana aliyekuwa na uwezo mkubwa darasani ambaye alikuwa akisoma katika Shule ya Wavulana ya Nsumba ya jijini Mwanza, Mike Martin anajikuta akiwavutia wasichana wengi hasa wa Shule ya Wasichana ya Ngaza.
Anajikuta akipokea barua nyingi kutoka kwa wasichana hao lakini kitu cha ajabu, hakutaka kuwa na msichana yeyote yule. Mbali na uwezo wake mkubwa darasani, Mike alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza muziki kitu kilichowafanya wanafunzi kumuita jina la Double Mhuku wakimfananisha na mwanamuziki Michael Jackson.
Upande wa pili, msichana mpole na mtaratibu ambaye naye hakuwahi kukutana na mwanaume kimwili, ambaye alikuwa akisoma katika SHule ya Wasichana ya Ngaza anajikuta kuvutiwa na MIke, moyo wake unaweweseka, mapnzi mazito yanaugubika moyo wake.
Anaogopa kwa kuwa hajawahi kuzungumzia mapenzi na mvulana yeyote yule. Anapoona ameshindwa kabisa kuongea na Mike, anajukuta akijifariji kwa kusema kwamba milima haikutani ila binadamu hukutana, ipo siku atakutana tena na Mike.
SONGA NAYO...
Ilikuwa ni Januari 27, 1976 siku ambayo wanafunzi mia moja wa shule ya Nganza walialikwa kwenda kucheza disko na wanafunzi wa shule ya wavulana ya Nsumba katika sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo iliyojulikana kwa jina la “Welcome Form One!” Kiranja mkuu wa shule ya Nganza, Neema Lucas, alipopewa barua hiyo na mwalimu wa zamu alifanya hima kuwatangazia wanafunzi wenzake na kuwaomba waliopenda kwenda Nsumba wajiandikishe mapema.
Beatrice aliiona nafasi ile kama bahati ya mtende na alikuwa mtu wa sita kujiandikisha. Lengo lake halikuwa kucheza muziki bali kuonana na Mike Martin, mwanaume aliyetokea kuunyanyasa moyo wake kwa nguvu zote.
Kitendo cha Beatrice kujiorodhesha kati ya wasichana waliotaka kwenda Nsumba kilizusha mjadala mkali kati ya wasichana wa Nganza. Beatrice, ambaye siku zote alionekana mlokole, aliwafanya wengi kujiuliza imekuwaje hata akaamua kwenda Nsumba kucheza disko siku hiyo? Wengi walihofu huenda Beatrice naye alikuwa ameanza kuangukia dhambini.
“Hata wewe Beatrice? Ya leo kali!” mwanafunzi mmoja alimuuliza Beatrice baada ya kulisoma jina lake ubaoni.
“Ni lazima niende, siendi kucheza bali nawapelekea watu habari njema! Bila kuwafuata kwenye kumbi zao za starehe wataupataje wokovu? Mbona Kristo alikula na watoza ushuru?” Beatrice hakuwa na njia yoyote ya kujitetea zaidi ya kutumia Biblia hiyohiyo ingawa lengo lake lilikuwa ni kumfuata Mike.
***
Wakati wasichana kutoka Ngaza wakiwasili katika viwanja vya Nsumba, Mike alikuwa bwenini akimalizia kufanya mazoezi ya kucheza shoo ya muziki wa “Thriller” wa Michael Jackson uliokuwa umepangwa kutumika katika onyesho siku hiyo. Pamoja na kuwepo bwenini katika mazoezi makali na ya mwisho alifanikiwa kuliona lori lililokuwa limewachukua wanafunzi wa Nganza likiingia shuleni kwao.
Kitu cha kwanza ambacho wasichana hao walifanya baada ya kuteremka kutoka kwenye lori lililowaleta ni kuuliza mahali alipokuwepo Mike. Jambo hilo lilimkera sana Beatrice, alihisi nafasi yake ya kukutana na Mike ilikuwa finyu.
Muda wa kuanza kwa sherehe hiyo ulipotimu, wanafunzi wa vidato vyote walifurika katika ukumbi wa starehe wa shule ya Nsumba na sherehe ikaanza mara moja.
Macho ya wanafunzi wa Nganza yalizunguka huku na kule ukumbini yakimsaka Mike bila mafanikio. Mike alikuwa bado yuko bwenini akivaa nguo zake za kung’ara zilizomfanya afanane kabisa na Michael Jackson.
Majira ya saa sita usiku, wakati sherehe ikiwa imepamba moto, mshereheshaji au MC kwa Kiingereza, Zablon Julius, aliyekuwa kiranja mkuu wa shule ya Nsumba, aliomba muziki usimamishwe na kuwataka wanafunzi wote wakae vitini na kuacha ukumbi wazi. Muziki uliposimamishwa hakupoteza muda, aliongea kwa sauti ya juu.
“Jamani naomba mkae kwenye viti vyenu mtulie. Hivi sasa ni kipindi cha onyesho maalumu, Show time na tunamkaribisha, The Tanzanian Michael Jackson au Double M aje kutuonyesha show ya wimbo wa “Thriller” ulioimbwa na Michael Jackson.”
Alipomaliza tu kusema hayo ukumbi wote ulipiga mayowe kushangilia na taa zikawashwa ili Mike aonekane vizuri.
Beatrice aliyekuwa amekaa nyuma kabisa ya ukumbi akiwa hajacheza hata muziki mmoja tangu disko lianze, alisogea mbele ili apate kumwona vyema mtu aliyekuwa akiusumbua moyo wake kwa kipindi kirefu.
Baada ya kukaribishwa, Mike hakupoteza muda. Aliingia ukumbini, kitu cha kwanza kukifanya kilikuwa ni kuinua mikono yake juu na kutamka kwa sauti ya juu, “Hi everybody?”
Kauli hiyo iliamsha shamrashamra ya aina yake na waliokuwepo ukumbini walizidi kupiga kelele na kushangilia “Cool Mameeeeeen!” kila mtu aliitika.
DJ alianza kuachia wimbo wa “Thriller” taratibu na Mike akaanza kufanya vitu vyake. Hakuna aliyeamini kama kweli Mike angeweza kufanya vitu vikubwa namna ile. Hata wanafunzi wa Nsumba wenyewe siku hiyo walishikwa na butwaa kwa jinsi Mike alivyojinyonganyonga kama hana mifupa mwilini! Wengi wa wanafunzi walisikika wakidai kwamba siku hiyo alicheza makusudi ili kuwazingua wasichana wa Nganza.
Beatrice alishindwa kujizuia. Alitamani sana kuongea na Mike ingawa hakujua kama Mike angeweza kupoteza muda wake kumsikiliza mtu kama yeye. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake alihisi kutumbukia katika dimbwi kubwa la mapenzi ambalo lilionekana dhahiri kuutesa na kuugubika moyo wake.
Alijikuta akitafuta njia ambayo angeweza kuitumia kuwasiliana na Mike lakini bado hakuigundua kwa sababu karibu kila msichana alitaka kuongea naye.
Muziki ulipokaribia kwisha, ghafla Beatrice alipata wazo aliloona linafaa kuufikisha ujumbe. Aliingiza mkono kwenye mfuko wake wa sketi na kutoa kitabu kidogo, akachana kikaratasi na kuchukua kalamu, kisha akaanza kuandika. Alipomaliza alikichukua kile kikaratasi na kukiweka ndani ya noti na kuikunja!
Hakupoteza muda akaondoka moja kwa moja na kwenda katikati ya ukumbi alikokuwa Mike na kumtunza noti ile. Akiwa katikati ya muziki, huku watu wakimshangilia na wasichana wakimzunguka na kumpiga mabusu usoni, Mike aliipokea noti ile na kuiweka mfukoni mwake.
Baada ya onyesho aliondoka moja kwa moja hadi bwenini ambako alibadilisha nguo na kuvaa suti nzuri aliyonunuliwa kama zawadi na baba yake alipofanya vizuri katika mtihani wake na kuingia kidato cha pili!
Kabla hajaondoka bwenini kurudi ukumbini aliikumbuka ile noti aliyotunzwa na msichana wa Nganza. Ilikuwa ni pesa peke yake aliyotunzwa, akainyanyua suruali yake na kuitoa noti hiyo na kuikunjua. La haula! Ndani ya noti ile kulikuwa na kipande cha karatasi! Alikikunjua na kuanza kukisoma. Kilikuwa kimeandikwa kwa mwandiko mzuri sana:
Mike,
Naitwa Beatrice Rugakingira. Nilivutiwa na wewe kwa mara ya kwanza ulipokuja shuleni kwetu kwenye malumbano! Nahisi kukupenda Mike. Ninajua si kitu cha kawaida kwa msichana kuandika barua na kumtaka mvulana kimapenzi, lakini mimi nimeshindwa kuvumilia Mike na imebidi niseme!
Naapa kwamba siyo malaya na sijawahi kukutana na mvulana kimwili maishani mwangu, kitu ambacho unaweza usikiamini.
Naomba tuonane, tuongee kabla sijarudi Nganza. Tafadhali, usinielewe vibaya. Ni moyo wangu ndio unaonisumbua.
Ni mimi
Beatrice.
Barua ile haikumshtua sana Mike, kwani jambo lile lilikuwa la kawaida katika maisha yake. Alipomaliza kuisoma, aliiweka mfukoni na kuondoka tena kuelekea ukumbini. Aliingia ukumbini kwa siri kubwa na kujikita kwenye kiti cha nyuma kabisa.
Aliketi na kuanza kuwaangalia watu walivyokuwa wakicheza muziki. Ghafla, mawazo ya ile barua aliyoisoma yalimjia tena kichwani mwake! Alijaribu kuikumbuka sura ya msichana aliyempa barua ile bila mafanikio yoyote na kujikuta akijiinamia kwa mawazo.
Baada ya Beatrice kuzunguka ukumbini kwa muda mrefu, akimtafuta Mike bila mafanikio yoyote hatimaye alifanikiwa kumfuma akiwa amejificha kwenye giza. Alijongea taratibu mpaka sehemu ile na kusimama nyuma yake kwa takribani dakika tatu, bila kumwita wala kumgusa huku moyo ukimwenda mbio.
Baadaye Mike alihisi moyo ukimwenda mbio, alihisi mtu akimgusa begani! Alipogeuka sura yake iligongana na ya msichana mrembo, mweusi, mwenye ngozi nyororo na sura ya Kinyarwanda. Akamkumbuka kuwa ndiye aliyemtunza noti.
“Hallow habari yako?” Beatrice alimsabahi huku akitabasamu.
“Ni nzuri tu,” Mike aliitika.
“Karibu dada hakuna tatizo,” Mike alijibu.
Beatrice aliona huo ulikuwa wakati mwafaka kwake kuulizia ujumbe wake.
“Naitwa Beatrice Rugakingira, nafikiri ujumbe wangu umeupata?”
“Ah! Ndiyo! Nimeuona. Kumbe ni wewe!” Mike aliijibu kwa upole.
Baada ya mazungumzo ya muda mfupi walitoka ukumbini na kuelekea bustanini. Wakiwa huko Beatrice alimweleza Mike kila kitu kuhusu alivyojisikia mpaka wakati huo. Mike alishindwa kutoa jibu sahihi, kama alimridhia au la.
“Tafadhali Mike nipe ukweli, unanitesa mwenzio!” Beatrice alilalama huku machozi yakimtoka.
Mike alishindwa kumjibu na badala yake alibaki kimya, ameduwaa.
Waliendelea kuwa pamoja, ilipotimu saa tisa na nusu ya usiku Mike na Beatrice walikuwa bado wapo bustanini. Muda wa kuondoka ulipofika wanafunzi wa Nganza walianza kukusanywa kwa safari ya kurudi shuleni kwao. Wanafunzi wote walikuwepo kwenye gari isipokuwa Beatrice. Mwalimu aliyeongozana na wanafunzi kwenda Nsumba aliamuru Beatrice atafutwe haraka iwezekanavyo kabla hawajaondoka.
Baada ya msoko wa hapa na pale wanafunzi wa Nganza walifanikiwa kuwafuma Beatrice na Mike wakiwa wamekumbatiana bustanini. Wanafunzi hao walishangaa kumwona mlokole Beatrice katika hali ile.
Hata hivyo, walichofanya ni kumvuta tu Beatrice na kuondoka naye. Alipofika mbele hatua kama tano Beatrice aligeuka nyuma na kumwangalia Mike.
“Nenda tu, nitakuandikia barua,” Mike alisema wakati akiondoka. Beatrice alimpungia mkono Mike, huo ndio ukawa mwanzo wa Beatrice na Mike kukutana na kupendana.
Wiki moja baadaye Mike alipokea zawadi ya kanda kutoka kwa Beatrice. Kanda ile ilikuwa imerekodiwa sauti ya Beatrice akilia huku akimwomba Mike amhurumie na kukubali kuwa mpenzi wake.
Ilimaliza kwa ujumbe kutoka katika wimbo wa taarab usemao Jamani Mapenzi Yananitatiza ulioimbwa na JKT Taarab.
Kanda hiyo ilimchanganya sana Mike na kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alihisi kumpenda msichana kwa dhati. Siku iliyofuata alimwandikia barua kulikubali rasmi ombi lake lakini kwa masharti kwamba penzi hilo liwe la kawaida, siyo linaloshirikisha tendo la ndoa.
Je nini kitaendelea?
Je Mike atakubali kuwa na msichana Beatrice.
Na kama wakiwa pamoja, ahadi ya kutofanya mapenzi itatiizwa?
 
SEHEMU YA 03

Mvulana aliyekuwa na uwezo mkubwa darasani ambaye alikuwa akisoma katika Shule ya Wavulana ya Nsumba ya jijini Mwanza, Mike Martin anajikuta akiwavutia wasichana wengi hasa wa Shule ya Wasichana ya Ngaza.
Anajikuta akipokea barua nyingi kutoka kwa wasichana hao lakini kitu cha ajabu, hakutaka kuwa na msichana yeyote yule. Mbali na uwezo wake mkubwa darasani, Mike alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza muziki kitu kilichowafanya wanafunzi kumuita jina la Double Mhuku wakimfananisha na mwanamuziki Michael Jackson.
Upande wa pili, msichana mpole na mtaratibu ambaye naye hakuwahi kukutana na mwanaume kimwili, ambaye alikuwa akisoma katika SHule ya Wasichana ya Ngaza anajikuta kuvutiwa na MIke, moyo wake unaweweseka, mapnzi mazito yanaugubika moyo wake.
Anaogopa kwa kuwa hajawahi kuzungumzia mapenzi na mvulana yeyote yule. Anapoona ameshindwa kabisa kuongea na Mike, anajukuta akijifariji kwa kusema kwamba milima haikutani ila binadamu hukutana, ipo siku atakutana tena na Mike.
SONGA NAYO...
Urafiki wao uliendelea mpaka Mike akamaliza kidato cha nne na kujiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari ya Nyakato iliyoko Bukoba ambako alisoma hadi kumaliza kidato cha sita.
Baada ya kumaliza kidato cha nne Beatrice hakuendelea na kidato cha tano bali alijiunga na Chuo cha Uuguzi cha Rubya ambacho pia kipo mkoani Kagera, kwa kozi ya miaka minne ya Uuguzi na Ukunga.
Baada ya kumaliza kidato cha sita, Mike alibahatika kupata nafasi ya kwenda kusomea Shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Oxford, nchini Uingereza. Kabla hajaondoka, walikuwa tayari wamepanga kuoana baada ya kumaliza masomo yao. Mike alimsihi Beatrice awe mvumilivu na mwaminifu katika kipindi chote ambacho angekaa Uingereza ili atakaporudi wafunge ndoa yao!
***
Mike alisafiri hadi Dar es Salaam ambako alipokewa na baba yake mdogo, mzee Joshua, ambaye alimfanyia taratibu zote za usafiri.
Kabla ya safari yake ya Uingereza yeye na mtoto wa mzee Joshua, Consolatha, walikwenda Zanzibar ambapo Mike alinunua nguo na vitu mbalimbali vya safari.
Wakiwa njiani kutoka Zanzibar waliongea mambo mengi kuhusu maisha. Mike alimuuliza Consolatha alichotaka kufanya katika maisha yake. Consolatha alimjibu kuwa kama angefanikiwa kumaliza na kufanya vizuri kidato cha sita wazazi wake walikuwa wamepanga aende Marekani kwa mama yake mdogo ambako angesomea Udaktari wa Mifupa.
Alidai hiyo ilikuwa ndiyo kazi pekee ambayo angependa kuifanya maishani mwake. Siku mbili baadaye, Mike alipanda ndege ya Shirika la Ndege la Uingereza, British Airways, kuelekea Uingereza kupitia Copenhagen. Alikuwa ni mtu mwenye furaha kupita kiasi, aliona ndoto zake zikitimia! Katika maisha yake alitaka kuwa mtu mkubwa na mwenye madaraka katika nchi na kwa kwenda kusoma Uingereza aliamini hilo lilikuwa limetimia.
***
Alikuwa wa kwanza kukaa kwenye kiti cha watu wawili alichokuwa amepangiwa. Baadaye alikuja msichana mmoja wa Kisomali na kukaa jirani yake. Msichana huyo ama kwa maringo au kwa kujiona mzuri, hakumsalimu Mike na alionekana mwenye dharau nyingi! Jambo hilo lilimkera sana Mike naye akaamua kukaa kimya pia.
Baada ya kukaa kitini msichana yule alichukua gazeti la Ebony la mwezi huo akijifanya kutogundua kuwa kuliwa na mtu pembeni yake.
Mike naye hakutaka kujirahisi. Alichukua gazeti lake la Uwazi na kuanza kusoma taratibu. Hakuna aliyemjali mwenzake. Muda mfupi baadaye ndege iliruka na dakika arobaini na tano baadaye ilitua katika Uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi, nchini Kenya bila Mike wala msichana yule kusemeshana.
Lakini kabla ndege haijaruka kutoka Nairobi kuendelea na safari, msichana yule alizinduka rasmi na kuanza maongezi.
“Hi, I am Laila, and you?” (Hujambo, mimi naitwa Laila, wewe ni nani?).
“My name is Mike. Hi Leila!” (Ninaitwa Mike. Hujambo Laila!).
“Fine thank you. What’s your destination sir?”
(Sijambo! Safari yako inaishia wapi, bwana?).
“My destination is UK, what about you?”
(Safari yangu inaishia Uingereza, wewe je?).
“I’m tavelling to Capenhagen. I’m a student at the University of Copenhagen taking Medicine and Public Health. What are you doing in the UK?” (Mimi nakwenda Copenhagen ambako nasoma Udaktari na Afya ya Jamii. Je, wewe unafanya nini Uingereza?).
“I’m going to join the Univesity of Oxford for my Bachelor Degree in Economics and Extra Education in Computer Science” (Ninakwenda Chuo Kikuu cha Oxford kusomea Shahada ya Kwanza ya Uchumi na Elimu ya Kompyuta).
“Oxford?” Laila aliuliza kwa mshangao.
“Yes?” (Ndiyo).
“It’s the most expensive university in the United Kingdom! Only very bright or rich students do join there! How did you get the chance? You must either be very bright or rich! (Ni chuo cha gharama kubwa sana Uingereza na wanafunzi wenye akili nyingi ndio hujiunga, wewe ulipataje nafasi hiyo? Wewe ni tajiri au una akili nyigi mno!).
“I’m neither rich nor bright, it was just a game of luck”. (Mimi sio tajiri na wala sina akili nyingi mno lakini ilikuwa ni bahati tu).
Mazungumzo hayo mafupi yaliwaunganisha Mike na Laila katika hali ya urafiki. Tangu dakika hiyo maongezi yalipamba moto wakawa kama watu waliofahamiana miaka kumi kabla!
Saa tano baadaye, wakiwa bado angani lakini wakiwa wamekaribia kabisa kutua katika Uwanja wa ndege wa Copenhagen uliokuwa mwisho wa safari ya Laila, bahati mbaya ilimkumba Mike.
Alianza kujisikia kichefuchefu na tumbo likaanza kumkata na mtu wa karibu kwake kwa wakati ule hakuwa mwingine bali Laila. Alimweleza tatizo lake akitaka amsaidie. Laila alitoa chupa ya dawa ya maji iliyoandikiwa Mucaine Suspension na kumpa Mike akanywa lakini bado haikumsaidia.
Hali ilizidi kuwa mbaya kadri dakika zilivyozidi kwenda. Mike akaanza kutapika, ikabidi Laila awataarifu wahudumu ndani ya ndege juu ya tatizo hilo ambapo walimfanyia huduma ya kwanza bila mafanikio.
Ndege ilipotua Copenhagen ilibidi safari ya Mike ikatishwe na akimbizwe haraka sana hospitali ambako iligundulika kwamba alikuwa na tatizo la kujisokota kwa utumbo. Ugonjwa huo ulitamkwa na madaktari kama Intestinal Obstruction.
Hali ya Mike ilikuwa mbaya mno na ili kuokoa maisha yake ilibidi mipango ifanyike haraka iwezekanavyo ili afanyiwe upasuaji kurekebisha hali ya kujisokota kwa utumbo. Hata hivyo, kabla ya kufanyiwa operesheni hiyo zilihitajika chupa tatu za damu.
Laila, ambaye wakati wote alikuwepo kumsaidia Mike ambaye hakuwa na mtu aliyemfahamu zaidi yake nchini Dernmark, ilibidi aende chuoni kwake ambako aliwataarifu wanafunzi kumi wa Kitanzania waliokuwa wakisoma katika Chuo cha Kikuu cha Copenhagen. Aliwataka waongozane naye hadi hospitali kujitolea damu ili kuyaokoa maisha ya Mtanzania mwenzao.
Kuna makundi manne ya damu ambayo binadamu anaweza kuwa nayo, ambayo ni ama kundi A, B, AB na O. Kinachofanya makundi ya damu yatofautiane ni Protini ziitwazo Agglutinogen. Mtu mwenye kundi “A” damu yake huwa na protini Agglutionogen na mtu mwenye kundi “B” damu yake huwa na Agglutionogen.
Mwenye kundi “O” huwa hana aina yoyote ya Agglutionogen. Hata hivyo, ndani ya damu ya mwanadamu kuna maaskari au “antibody” kwa Kiingereza ambao hupambana na hizi Agglutionogens, maaskari hawa huitwa Agglutins.
Mtu mwenye kundi “A” la damu huwa na maaskari waitwao Agglutinions Anti B na mwenye kundi “B” huwa na Agglutinis Anti A na mwenye kundi “AB” huwa hana aina yoyote ya maaskari hao. Kwa sababu hii mtu mwenye kundi “AB” anaweza kupokea damu kutoka kwa kundi lolote la damu!
Kwa sababu mtu mwenye kundi “O” la damu ana maaskari wote wa “A” na “B” hupokea damu kutoka kwa mtu mwenye kundi “O” peke yake. Hivyo, Mike alihitaji damu kutoka kwa mtu mwenye kundi “O” peke yake.
Wanafunzi wote kumi walipopimwa damu zao hazikushabihiana na damu ya Mike, wengi walikuwa kundi “A” na “B”. Alipoona hivyo, Laila aliomba ajaribu kupimwa yeye. Kwa bahati nzuri alipopimwa damu yake ilikuwa “O” na kushabihiana na damu ya Mike. Palepale Laila alitolewa damu chupa tatu ili kuokoa maisha ya mtu waliyekutana naye kwenye ndege! Wanafunzi wa Tanzania walimshukuru sana Laila kwa moyo wa ukarimu aliouonyesha.
Wiki moja baada ya kufanyiwa operesheni, Mike alikuwa mzima kabisa. Alitoa shukurani za pekee kwa Laila na wanafunzi wengine wa Kitanzania waliomsaidia katika matatizo yake. Akaendelea na safari yake moja kwa moja hadi Uingereza ambako aliendelea na masomo kama kawaida.
Je nini kitaendelea?
Je Mike huu ndiyo mwisho wa Mike na msichana Laila?
 
SEHEMU YA 04

Mvulana mwenye akili na pia mcheza muziki, Mike Martin amekutana na msichana mzuri, mwenye mvuto na upole wa hali ya juu, Beatrice Rugakingira.
Wawili hao, huku wakiwa hawajawahi hata kukutana kimwili katika maisha yao, wanajikuta wakiangukia katika penzi zito na mahusiano kuanza rasmi huku ahadi ya kutokufanya mapenzi mpaka kuoana ikiwekwa.
Wanakubaliana, baada ya kipindi fulani, Mike anapata nafasi ya kwenda kusomea Shahada ya Uchumi katika Chuo cha Oxford nchini Uingereza. Akiwa njiani, anapata tatizo la kuumwa tumbo ambalo linamfanya kuhitaji kuongezewa damu.
Ndege inashushwa katika Jiji la Copenhagen nchini Denmark. Anapelekwa hospitali, wanapokuja wanafunzi kutoka nchini Tanzania kumuongezea damu, hakuna mwenye kundi kama lake zaidi ya msichana aliyesafiri naye, Laila.
Kinachofanyika, msichana Laila, kwa upendo wake wa dhati, anamuongezea damu Mike na kisa safari kuendelea.
SONGA NAYO...
Miaka miwili baada ya Mike kufika nchini Uingereza, kulitokea ugonjwa wa ajabu uliopunguza kinga ya mwili kupambana na magonjwa ambao Marekani na nchi nyingi za Ulaya uliitwa Acquired Immuno Deficiency Syndrome au AIDS na Tanzania uliitwa Upungufu wa Kinga Mwilini au UKIMWI. Ugonjwa huo ulitangazwa kuwa ni ugonjwa hatari duniani kote baada ya kugundulika kuwepo wagonjwa kadhaa nchini Marekani na Uganda, Afrika Mashariki.
Njia za kuambukiza ugonjwa huo zilipotajwa zilikuwa ni pamoja na ile ya kuongezewa damu. Mike aliposikia hivyo, alishtuka lakini alijipa moyo na kuamini Laila asingekuwa nao kwa jinsi afya yake ilivyokuwa nzuri.
“Hakuonekana kuwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huu,” alisema baada ya kuzisoma dalili zake.
Miaka sita baadaye Mike alimaliza masomo yake. Yalikuwa ni masomo ya miaka mitano lakini aliongeza mwaka mmoja ambao aliutumia kusomea Uongozi wa Elimu ya Kompyuta, lengo lake likiwa kupata kazi nzuri baada ya kurudi Tanzania.
Akiwa njiani kurudi Tanzania, Mike aliamua kupita Copenhagen kumshukuru Laila, mtu aliyeokoa maisha yake! Alimnunulia zawadi nzuri ya friji kama ishara ya shukurani zake. Alipofika Copenhagen alishangazwa na taarifa alizosikia kuwa Laila hakuwepo chuoni, alirudishwa Mogadishu baada ya kuugua kifua kikuu kwa muda mrefu na hali yake kudhoofika.
Mike alitamani sana kumwona Laila lakini hakuwa na uwezo wa kusafiri hadi Mogadishu. Badala yake alipanda ndege moja kwa moja hadi Nairobi na kuunganisha kwa ndege nyingine hadi Dar es Salaam.
Uwanjani Dar es Salaam alipokewa na mzee Joshua, mkewe na Lydia, mdogo wake Consolatha. Hakushangaa kwa nini Consolatha hakuwa pale. Alijua ni lazima kwa wakati huo alikuwa amefanya vizuri katika masomo yake ya kutimiza ndoto yake ya kwenda Marekani kusomea Udaktari wa Mifupa.
Wakiwa ndani ya gari kuelekea nyumbani kwa mzee Joshua, Mike alishindwa kuvumilia. Akajikuta akiuliza kama Consolatha alifanikiwa kutimiza ndoto yake. Cha kushangaza ni kwamba hakuna mtu aliyelijibu swali lake ingawa alikuwa na uhakika kabisa kuwa watu wote walimsikia.
Walipofika nyumbani alikaribishwa ndani na yakafanyika maombi maalum kumshukuru Mungu kwa kumrudisha Mike salama nyumbani Tanzania.
Baada ya maombi hayo kabla ya chakula cha jioni Mike alianza kuwasimulia yote yaliyojitokeza akiwa Uingereza, likiwemo tatizo lake la kuugua njiani na kufanyiwa upasuaji nchini Denmark.
“Namshukuru sana yule dada wa Kisomali vinginevyo nisingekuwa hai maa…” Mike alishtuka ghafla, dakika mbili baadaye alianza kulia.
“Mike mbona unalia tena?” Mzee Joshua alimuuliza.
“Yaani kumbe Consolatha alishafariki na hamjanieleza?” Mike alisema huku ameikodolea macho picha kubwa iliyokuwa imetundikwa ukutani ikiwa imezungukwa na maandishi, 'Tulikupenda mwanetu lakini Mungu alikupenda zaidi, Mungu ailaze roho yako mahali pema peponi.'
“Tulikuwa tunasubiri upumzike ili tukueleze maana tulishindwa kukutaarifu ukiwa Uingereza tukiamini tungekuvurugia masomo yako maana ulimpenda sana marehemu dada yako,” alisema mzee Joshua.
“Haya nielezeni basi,” Mike alisema huku akijifuta machozi.
“Dada yako alimaliza shule na kufanya vizuri sababu alipata daraja la kwanza kidato cha sita alipata pointi nne. Mama yake mdogo aliyekuwa Marekani, kama zawadi kwa alivyofanya vizuri katika wanafunzi wote Tanzania, alimwita akasomee Udaktari wa Mifupa, kazi ambayo marehemu aliipenda.
Kama ulivyofanya wewe, Consolatha naye aliamua kwenda Zanzibar kununua nguo za kusafiri nazo, akiwa njiani kutoka Zanzibar boti aliyokuwa akisafiri nayo ilizama, watu wote waliokuwa ndani ya boti hiyo hawakuonekana na hata boti yenyewe mpaka leo hii bado iko majini! Hivyo, Consolatha alifariki na hatukufanikiwa hata kuupata mwili wake.”
“Eee Mungu wangu ilaze roho ya Consolatha mahali pema peponi,” Mike alisema huku machozi yakimtoka na kunyanyuka kwenda kuibusu picha ya Consolatha.
***
Wakati wote Mike akiwa nje ya nchi, Beatrice alijitahidi kuwa msichana mwaminifu. Hakutaka kabisa kuvunja ahadi waliyowekeana na hakutaka kuharibu ubikira wake. Aliamini kwamba hiyo ndiyo zawadi pekee ya kumtunzia Mike mpaka siku ya ndoa yao.
Alipomaliza masomo yake ya Uuguzi na Ukunga, Beatrice aliajiriwa na Hospitali ya Mkoa wa Kagera kama Muuguzi Mkunga, na mawasiliano yake na Mike yalikuwa mazuri. Mike alimpigia simu moja kwa moja kutoka Uingereza karibu kila mwezi na kumtumia zawadi nyingi mara kwa mara.
Beatrice alisumbuliwa na wanaume wengi wakitaka kumwoa! Aliwakataa wachumba wasiopungua watatu akiwemo Meneja wa Kiwanda cha Sukari cha Bukoba kwa sababu ya Mike.
Tarehe 12 Septemba, 1986, saa 10 jioni, ikiwa ni miaka sita baada ya Mike kuondoka nchini, Beatrice akiwa amejipumzisha chumbani mwake, simu iliita ghafla naye aliipokea. Ilikuwa ni simu ya Mike.
“Hi! Darling habari za Uingereza?”
“Sio Uingereza mama, hapa nipo Bongo.”
“Dar? Mbona ghafla hivyo na hujaniambia?”
“Nilitaka kukufanyia surprise! (kukushtukiza) kwa hiyo, kesho naingia Mwanza, nakuomba uje Mwanza tukutane sawa?”
“Nitakuwepo,” Beatrice alijibu na kuongeza: “Jamani Mike miaka mingi sijakuona mpenzi wangu, nafikiri umezidi kuwa mzuri eh!” Beatrice alimwaga sifa.
“Darling utaniona kesho kutwa, lakini nafikiri nimekuwa mbaya zaidi” Mike alitania.
“Kama umekuwa mbaya basi mimi sikutaki tena,” Beatrice aliongeza utani.
“Acha utani wewe, tafadhali njoo tuongee mipango yetu ya ndoa wakati umefika sasa.”
***
Kwa kawaida, meli kutoka Bukoba huwasili Mwanza saa 12:30 asubuhi lakini Septemba 14, 1986 saa 11:00 alfajiri Mike alikuwa tayari amekwishaamka. Alikuwa na hamu kubwa ya kumwona Beatrice baada ya miaka karibu saba bila kumtia machoni.
Baada ya kufanya mazoezi na kuoga aliamua kupumzika na kungoja muda utimie ili aende bandarini kumpokea mchumba wake Beatrice, mwanamke aliyempenda kuliko wanawake wote chini ya jua. Mwanamke ambaye ndiye angekuwa wa kwanza kuvunja naye amri ya sita.
Saa 12:00 asubuhi Mike alikuwa ndani ya teksi aliyoikodi toka nyumbani kwao, Nyakato-Mecco, akielekea bandarini kumpokea kipenzi chake, Beatrice.
Dakika 15 baadaye teksi aliyokodi Mike iliegesha nje ya lango la bandari ya Mwanza na kwa mbali Mike aliweza kuiona meli ya MV Viktoria ikiwasili.
Meli ilipotia nanga moyo wake ulianza kudunda, utafikiri moyo wa mtu aliyekuwa akisubiri kuingia kwenye usaili wa kazi. Alikuwa na hamu kubwa ya kumwona Beatrice na moyoni alihisi furaha ya ajabu.
Alishindwa kuelewa ingekuwa furaha ya aina gani pindi angemtia Beatrice kwenye mboni ya macho yake. Abiria walianza kuteremka mmoja baada ya mwingine. Hata hivyo, Beatrice hakuonekana!
‘Labda aliahirisha safari nini?’ Mike alijikuta akijisemea kwa mshangao.
Akiwa karibu akate tamaa, ghafla alimwona Beatrice akiteremka ngazi taratibu ambapo bila kupoteza muda na bila aibu, alikimbia mbio kuelekea kwenye ngazi akikatiza katikati ya watu mpaka akamfikia. Beatrice alipomwona alimrukia na kumkumbatia.
“Ooh darling! Is it you?” (Mpenzi ni wewe kweli?) Beatrice aliuliza.
“It’s me Beatrice.” (Ni mimi) Mike alijibu kwa sauti ya juu.
“I can’t believe my eyes.” (Siyaamini macho yangu) Beatrice alisema huku machozi ya furaha yakimtoka.
Waliangushana chini huku wakiwa wamekumbatiana na watu wote waliokuwa pale walishangaa. Dakika tano baadaye wote walikuwa wima wakiwa wamekumbatiana, wakilia kwa furaha! Kila mmoja alimwona mwenzake kuwa amezidi uzuri.
“Hawa kweli wanapendana!” akinamama waliokuwa jirani walisikika wakisema.
Baadaye Mike alichukua begi la Beatrice na wote wakaingia ndani ya gari na kuondoka.
“Dereva, moja kwa moja hadi Natta Hotel, sawa?” Mike aliamuru.
“Hakuna taabu!” dereva alijibu na kuliondoa gari kuelekea alikoelekezwa.
Baada ya kusema hayo, Mike alimgeukia Beatrice ambaye alikuwa bado akilia kwa furaha.
“Za siku mpenzi?”
“Niache kwanza nipumzike Mike, nina mengi ya kuongea na wewe kwa sasa kifua kimenibana, nikitulia nitakusimulia mengi lakini nashukuru Mungu amekurudisha salama mpenzi wangu.”
Dakika tano baadaye gari liliegeshwa nje ya Hoteli ya Natta, Mike akamlipa dereva pesa zake, akachukua begi na kumshika Beatrice mkono. Walikaa hotelini ambako Mike alipanga chumba. Baada ya kuweka mizigo vizuri walijitupa kitandani.
“Nafikiri sasa umetulia hebu nieleze,” Mike aliyaanzisha maongezi.
“Ni mengi lakini kifupi nilikukumbuka sana, vilevile bado ninakupenda, sitaacha kukupenda milele Mike.”
Majira ya saa kumi jioni, Mike alirudi nyumbani kwao kuongea na wazazi wake. Akawaomba wamruhusu aende mjini kwa shida zake na kuwafahamisha kwamba asingerudi mpaka asubuhi siku iliyofuata.
Alidanganya kuwa kulikuwa na sherehe iliyoandaliwa na rafiki zake kumpongeza. Alilazimika kusema hivyo kwa sababu wazazi wake walikuwa bado hawajamfahamu Beatrice.
Alichukua begi lililokuwa na zawadi alizomnunulia Beatrice na kuondoka nalo.
Alipofika hotelini alimkuta Beatrice akiwa bafuni anaoga, hakupoteza muda, naye akavua nguo zake, akachukua taulo na kuingia bafuni ambako walioga pamoja.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kuoga pamoja tangu wafahamiane. Wakati wakioga ghafla Beatrice alianza kujisikia msisimko wa ajabu mwilini, ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumwona mwanaume akiwa kama alivyozaliwa.
“Mike!”
“Naam, darling.”
“NImevumilia kwa muda mrefu sana, mwenzio nimeshindwa, tafadhali naomba…naomba tu…tu..” baada ya kusema hayo alimkumbatia Mike kwa nguvu.
“Beatriceeeee!” Mike alisema kwa ukali.
“Be…e! Mike!” Beatrice aliitikia.
“Kumbuka ahadi yetu na utulie mpenzi,” Mike alisisitiza.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Beatrice kumsikia Mike akiongea kwa sauti ya ukali kiasi kile. Alitambua kuwa alikuwa amemkasirisha, hakupoteza muda, aliamua kumwomba msamaha na Mike alimsamehe.
Je nini kitaendelea?
Je Mike ataendelea kuwa mvumilivu mpaka ndoa?
Je wawili hawa wataoana?
 
SEHEMU YA 05


Mvulana mwenye akili na pia mcheza muziki, Mike Martin amekutana na msichana mzuri, mwenye mvuto na upole wa hali ya juu, Beatrice Rugakingira.
Wawili hao, huku wakiwa hawajawahi hata kukutana kimwili katika maisha yao, wanajikuta wakiangukia katika penzi zito na mahusiano kuanza rasmi huku ahadi ya kutokufanya mapenzi mpaka kuoana ikiwekwa.
Wanakubaliana, baada ya kipindi fulani, Mike anapata nafasi ya kwenda kusomea Shahada ya Uchumi katika Chuo cha Oxford nchini Uingereza. Akiwa njiani, anapata tatizo la kuumwa tumbo ambalo linamfanya kuhitaji kuongezewa damu.
Ndege inashushwa katika Jiji la Copenhagen nchini Denmark. Anapelekwa hospitali, wanapokuja wanafunzi kutoka nchini Tanzania kumuongezea damu, hakuna mwenye kundi kama lake zaidi ya msichana aliyesafiri naye, Laila.
Kinachofanyika, msichana Laila, kwa upendo wake wa dhati, anamuongezea damu Mike na kisa safari kuendelea.
Baada ya kurudi Tanzania na zawadi nyingi, mahusiano yake na mpenzi wake yanazidi kupamba moto, kuna siku Beatrice anatamani kufanya mapenzi na Mike, ila mpenzi wake huyo anakataa kwa kumkumbusha kuhusu ahadi yao kwamba wasingeweza kufanya mapenzi mpaka wafunge ndoa, Beatrice anakuwa mpole.
SONGA NAYO...
Baada ya kuoga walivaa na kutoka kwenda Hoteli ya Continental iliyokuwa maarufu mjini humo kwa kupika chakula kizuri.
Mike alivaa suti nyeusi na Beatrice alivaa suruali ya jeans iliyombana vizuri na tisheti nyeupe iliyoandikwa kifuani “My virginitiy is just for you only” (Bikira yangu ni kwa ajili yako wewe tu).
“Beatrice, ulinunua wapi nguo hii?” Mike alimuuliza.
“Dukani, huko Kampala.”
“Kwa nini ulinunua?”
“Nilitaka kukuonyesha nipo kwa ajili yako Mike.”
Mike alimkumbatia Beatrice na kumbusu kwenye paji la uso.
“Nakupenda Beatrice, nitakupenda milele na leo nakutamkia kuwa nitakuoa ili uwe mke wangu wa milele na milele.”
Beatrice akaanza kulia kwa furaha, hakuyaamini masikio yake kama yalisikia sawa maneno yale.
“Asante Mike, hata mimi nimevumilia vya kutosha nafikiri sasa ni vizuri tukaishi pamoja.”
Baada ya chakula wakarudi tena hotelini na usiku huo walikesha wakiongea kuhusu mipango yao ya ndoa na kila mtu alionekana kuwa na hamu ya harusi kumzidi mwenzake.
Siku iliyofuata baada ya kuweka mambo sawa Beatrice alirudi Bukoba huku tayari wakiwa wamepanga kwamba Mike angekwenda Bukoba kwa wazazi wake kujitambulisha.
***
Mwezi uliofuata Mike aliajiriwa na Kiwanda cha Nguo cha Mwatex kama Meneja Utawala. Kabla ya kuanza kazi alikwenda Dar es Salaam kukomboa bandarini mali zake zote alizozinunua Uingereza. Kulikuwa na malori matano na matela yake, magari madogo mawili, moja la kwake la kutembelea aina ya BMW na jingine la baba yake aina ya Mitsubishi Canter tani tatu na nusu.
Pia alinunua mashine ya kusaga, kuchana mbao, mashine za kuchapisha nakala, kompyuta ishirini na vyombo vya ndani.
Kutokana na mali alizokuwa nazo pamoja na kazi yake ya umeneja akiwa katika umri mdogo, jina lake lilivuma kupita kiasi mjini Mwanza.
Alifahamika karibu na kila mtu hadi watoto wadogo. Alipopita mitaani watoto walimshangilia Mike! Mike! Mike! Kwa muda mfupi tu alikuwa ameshakuwa maarufu kuliko hata Meya wa mji huo.
Gari lake la BMW lilizidisha umaarufu wake maradufu kwani hapakuwa na mtu mwingine mwenye gari kama hilo mjini Mwanza.
Miezi michache baada ya Mike kuanza kazi, alipewa nyumba ya kuishi katika nyumba za wafanyakazi wa Mwatex zilizokuwa mlimani Bugando.
Maisha ya kuishi pekee hakuyaweza, aliamua kusafiri hadi Bukoba kwa Beatrice ili ampeleke kwa wazazi wake kujitambulisha. Alifika Bukoba siku ya Jumamosi na jioni ya siku iliyofuata Beatrice alimpeleka Mike kijijini kwao Kanyigo kuonana na wazazi wake.
***
"Msigazi murungi nabasa kumshwela muhala waitu Beatrice." (Ni kijana mzuri anafaa kuwa mume wa binti yetu Beatrice) mama yake Beatrice alisema.
"Nanye nimbona asaine chonka munyamahanga, Msukuma.” (Na mimi naona anafaa lakini si mtu wa kabila letu, ni Msukuma).
Mzee Rugakingira, baba mzazi wa Beatrice aliitikia.
"Okuba Msukuma ti nshonga boona bashaija." (Kuwa Msukuma si tatizo, wote ni wanaume tu kama wengine), mama alimalizia.
Mzee Rugakingira na mkewe walikaa pembeni kumjadili Mike baada ya kutambulishwa kwao na Beatrice.
Baada ya chakula cha usiku wazazi wa Beatrice walimkubali Mike na kutoa baraka zao zote, ilikuwa furaha kubwa kwa Beatrice.
Mike hakuamini kama ingekuwa rahisi kiasi hicho kwani alishaambiwa kuwa watu wa mkoa wa Kagera walipendelea sana kuoana wao kwa wao, yaani watu wa kabila moja! Hakutegemea kama wangeweza kumkubali yeye Msukuma mara moja.
Pamoja na kukubali kwao kirahisi, wazazi wa Beatrice waliwasisitizia umuhimu wa kupimwa UKIMWI, kabla ya ndoa. Walidai kuwa wakati huo UKIMWI ulikuwa tishio kubwa sana kwa mkoa wa Kagera na Tanzania nzima.
Si Beatrice wala Mike aliyetiwa hofu na suala hilo la kupima UKIMWI, hiyo ilitokana na ukweli kwamba hadi umri waliokuwa nao hakuwepo mmoja kati yao aliyewahi kukutana kimwili na mtu mwingine.
Walikuwa wakisubiri siku ya ndoa yao kwa hamu ili wapate kukionja kitendo hicho.
Kabla ya kuondoka Bukoba, Mike alifanya mipango yote ya kumhamishia Beatrice mjini Mwanza kikazi ili apate kuwa karibu naye wakati wakikamilisha mipango yao ya ndoa.
Baada ya ya kufika Mwanza, Mike aliwataarifu wazazi wake ambao kwa muda mrefu aliwaficha mipango yake ya kumwoa Beatrice. Wazazi wake walifurahi sana na moja kwa moja wakatoa baraka zao zote. Mzee Martin akaahidi kusafiri yeye na wazee wengine maarufu mjini Mwanza kwenda Bukoba kufahamiana na wazazi wa upande wa pili na pia kutoa mahari.
***
Taarifa za harusi ya Mike zilipoanza kutapakaa mjini Mwanza watu wengi hawakuamini. Kwa muda mrefu watu wengi waliamini Mike alikuwa na kasoro ya kimaumbile, kwani tabia ya Mike kutojihusisha na wanawake ndiyo iliyosababisha watu kuamini hivyo.
Mzee Martin aliporudi kutoka Bukoba vikao vya harusi vilianza na kadi za michango zilisambazwa kwa kila mtu aliyekuwa karibu na Mike na familia yake. Watu wakawa na hamu kubwa ya kuishuhudia ndoa ya Mike na Beatrice.
Huko Bukoba pia taarifa zilisambaa kila kona na kwa ndugu wote na marafiki wa familia ya Rugakingira.
Hata wafanyakazi wenzake katika hospitali ya Mkoa wa Kagera walitaarifiwa. Michango ilianza kutolewa. Kwa jinsi pesa zilivyochangishwa, watu walishindwa kuelewa ukubwa wa harusi hiyo ungekuwa vipi.
***
Miezi miwili baadaye Beatrice alihamia mjini Mwanza. Alifikia Capri Point, kwa dada yake mkubwa, Margareth, mke wa Samson, mfanyabiashara maarufu mjini Mwanza. Baada ya kufika Mwanza, Mike alimtafutia kazi hospitali ya Bugando ambako alifanya kazi kama Muuguzi Mkunga kama ilivyokuwa Bukoba.
Kwa sababu ya ukaribu, mawasiliano kati yao yakawa makubwa. Walionana karibu kila siku, ambapo Mike alipotoka kazini alikuwa na kawaida ya kupitia hospitali kumchukua Beatrice na kumrudisha nyumbani kwa dada yake.
Kila mtu aliyewaona Mike na Beatrice alikiri kweli walipendana na walikuwa mfano wa kuigwa. Siku za mwishoni mwa wiki kila walikokwenda walikuwa wawili, tena mkono kwa mkono! Kila mtu mjini Mwanza alitamani kuiona ndoa yao.
***
Wakati homa ya harusi ya Beatrice na Mike ikiwa imepanda kupitia kiasi mjini Mwanza, mzee Rugakingira alipiga simu kutoka Bukoba na kuwakumbusha Mike na Beatrice juu ya kupima UKIMWI.
Ili kuonyesha kuwa hawakulidharau ombi la wazazi, siku iliyofuata asubuhi na mapema wote wawili wakaenda hospitali ya Bugando kushughulikia suala hilo.
"Sijui baba hatuamini!" Beatrice alihoji kwa utani wakiwa njiani kuelekea Bugando.
"Si unajua tena wazee wetu, si ajabu wananitilia mashaka mimi au naonekana mhuni sana nini?" Mike alitania.
Walinyoosha moja kwa moja hadi hospitali ya Bugando, baada ya kuegesha gari walipitiliza moja kwa moja hadi maabara ambako waliandikisha majina yoa na kupanga foleni, wakisubiri kuitwa.
Muda mfupi baadaye mwanamke mmoja mfupi alichungulia kutoka mlango wa maabara.
"Mike Martin na Beatrice Rugakingira, tafadhali ingieni!" Ilikuwa ni sauti ya muuguzi akiwataka waingie maabara.
Wote wawili walinyanyuka na kuingia maabara ambako walichukuliwa vipimo. Baada ya shughuli hiyo, Mike alimrudisha Beatrice nyumbani, kwa dada yake.
Siku hiyo Beatrice alitaka kuingia zamu ya mchana, hivyo alipomfikisha kwao aliondoka kwenda kazini kwake eneo la viwanda vya Nyakato, barabara ya kuelekea Musoma.
Maisha yaliendelea kama kawaida huku watu wakiendelea kuchanga maelfu ya shilingi kwa ajili ya harusi hiyo ya aina yake. Harusi iliyotegemewa kufungiwa angani ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Precision wakati maelfu ya watu wakishuhudia na kushangilia kwa chini.
***
"Siamini!" Mike alisema huku machozi yakimtoka.
"Nimeutoa wapi mimi?" Aliendelea kujiuliza maswali bila kupata majibu.
"Huu ni uongo mkubwa," alisema kwa sauti ya juu mpaka baadhi ya watu waliokuwa karibu naye wakasikia, palepale alinyanyuka na kumkaba shati daktari aliyekuwa akimpa unasihi.
"Kwa nini mnanipakazia, hamtaki nimuoe Beatrice siyo?"
"Mike wewe ni kijana unayeheshimika sana hapa mjini, tafadhali usifanye jambo hilo." Mmoja wa wauguzi waliokuwa maabara alisihi katika kujaribu kuituliza hali hiyo kabla watu hawajakusanyika kusikiliza.
"Haiwezekani, kwa nini mnisingizie kitu kama hiki mimi wakati sijawahi kukutana na mwanamke yeyote maishani mwangu? Iweje leo mniambie habari kama hii?"
"Sio hivyo kaka, tuliza moyo kwanza!" Muuguzi aliyekuwa pale aliendelea kusihi.
Mike alivikunjua tena vile vyeti vya majibu na kuanza kuvisoma kwa mara ya pili. Alikuwa haamini kabisa kama majibu yake yalionyesha alikuwa “Elisa Test Positive,” yaani alikuwa na virusi vya UKIMWI na majibu ya Beatrice yalionyesha “Elisa Test Negative,” yakiwa na maana hakuwa na virusi vinavyoambukiza UKIMWI.
"Nimeutoa wapi mimi?" Mike aliendelea kuuliza kwa sauti.
Kwa kasi ya ajabu Mike alitoka maabara na kukimbia hadi nje ya geti, akaingia ndani ya gari lake na kuliondoa kwa mwendo wa kasi kuelekea eneo la Isamilo. Alinyoosha moja kwa moja hadi kwenye majengo ya kitengo cha uchunguzi cha kitabibu cha Medical Research.
Aliyemfuata huko hakuwa mwingine bali ni Dkt. Mazira, mmoja wa marafiki zake wa karibu waliyesoma wote Shule ya Sekondari ya Nsumba.
"Ee bwana mbona macho mekundu, umefiwa?" Dkt. Mazira aliuliza mara tu baada ya kumwona Mike.
Mike alianza kulia tena.
"Bwana, mimi nimetoka Bugando, hapa nilipo nimechanganyikiwa kiasi cha kutosha."
"Kuna nini cha kukuchanganya Mike?"
"Majibu!"
"Majibu ya nini?"
"Ya UKIMWI, eti yameonyesha mimi Positive na Beatrice ni Negative hizi si njama za kukwamisha ndoa yetu, kweli? Siamini hata kidogo, nimekuja kwako ili turudie kupima?”
"Hebu njoo huku ndani."
Waliingia ndani ambako kwa haraka Dkt. Mazira alimtoa Mike damu na kuanza kuifanyia uchunguzi.
"Nisubiri hapo hapo!" Dkt. Mazira alisema.
Dakika arobaini baadaye Mike alishangazwa na jinsi macho ya Dkt. Mazira yalivyokuwa yametoka, alionyesha wasiwasi mkubwa.
"Nini daktari?"
"Hapana Mike ni kitu cha kawaida tu."
"Please tell me, is it positive or negative? That's what I want to know!" (Niambie, daktari, nina virusi au sina, hicho ndicho ninachotaka kujua).
"Ah! Ah! Ah!..." daktari alishikwa na kigugumizi.
"Niniiii?"
"Kwa kweli, Mike ni suala gumu kidogo kukueleza, nafikiri tunahitaji kurudia tena baada ya wiki tatu, kuna wakati hivi vipimo vyetu huwa vinatoa majibu yasiyo kweli?”
“Hivyo ina maana kwa leo imeonyesha mimi ni positive?” Mike aliuliza.
"Hivyo ndivyo rafiki yangu, siwezi kukuficha kitu lakini ninategemea utasimama imara katika kipindi chote tukisubiri kurudia vipimo!"
Mike aliinama na kuanza kulia tena, Dkt. Mazira alijaribu kumbembeleza lakini haikuwezekana Mike akaondoka bila kuaga na kuingia ndani ya gari lake na safari ya kuelekea nyumbani kwake ikawa imeanza.
Mike hakumwambia Beatrice habari za majibu hayo ingawa Beatrice aliingiwa na hofu kwa jinsi alivyoona mabadiliklo ya tabia ya mpenzi wake. Mike alikuwa ni mwenye huzuni kubwa na mara nyingi alikuwa akitokwa na machozi.
"Mike una tatizo gani?” Kila siku Beatrice aliuliza.
"Mimi? Sina matatizo yoyote, nina mafua tu!" Mike alitumia jibu hilo kila alipoulizwa kuhusu afya yake.
Wiki tatu baadaye Mike alikuwa tena Medical Reseach ambako Dkt. Mazira alichukua tena damu yake kwa ajili ya kupima. Majibu yalipotoka yalionyesha Mike alikuwa Positive vilevile!
Mike alilia machozi kwa uchungu na alishindwa kuelewa jibu la Positive lilitoka wapi, wakati maishani mwake hakuwahi kufanya ufuska wowote wala kutembea na mwanamke yeyote! Kitu kingine kilichomchanganya zaidi akili ni lugha gani angeitumia kuwafahamisha watu ambao tayari walishachanga pesa zao kwa ajili ya harusi yake. Je, angewaambia hataoa tena kwa sababu ana virusi vya UKIMWI? Alishindwa kupata jibu la moja kwa moja angetumia njia ngani kumwelewesha Beatrice kuwa ndoa isingewezekana tena kwa kuwa yeye alikuwa anaishi na virusi.
Kila alipoufikiria muda ambao Beatrice aliupoteza kumsubiri, alijihisi vibaya, aliulaani UKIMWI na kwa nini ulikuja duniani. Alikumbuka kuwa Beatrice alikwishakataa wachumba watatu wakati Mike akiwa Uingereza. Alishindwa kuelewa Beatrice angejisikia vipi wakati tayari alikwishawaeleza marafiki zake wote kuhusu ndoa yake na wengine tayari walishaanza kushona sare za harusi.
Mike alibaki ameduwaa bila kujua la kufanya, hakuwa tayari kuua kiumbe kisicho na hatia. Hakutaka kumuua Beatrice kwa sababu alimpenda mno! Alimshukuru Mungu kwa sababu yeye na Beatrice walikuwa hawajawahi kujamiiana tangu wafahamiane, vinginevyo hata Beatrice angekuwa Positive.
Alipofikiria ni wapi alikoupata ugonjwa huo bado hakupata jibu. Jibu lililomjia kichwani kwa haraka ni hisia juu ya damu ya Laila! Damu ile aliitilia shaka sana.
"Nitakwenda hadi Mogadishu nikamtafute Laila ili nihakikishe kama ni kweli yeye ndiye aliyeniambukiza,” alijisemea Mike. Alikumbuka kuwa Laila aliwahi kumweleza kuwa baba yake mzee Mohamed alikuwa mtu maarufu sana mjini Mogadishu.
"Hivyo ni rahisi sana kumpata na nikikuta ni kweli sijui nitampa adhabu gani...! Hakuna sababu ya kumwadhibu Laila nia yake ilikuwa njema alitaka kuokoa maisha yangu.”
Wakati Mike akiwaza yote hayo, tayari alikwishaondoka Medical Research. Gari lake aliligesha kando ya barabara ya kwenda uwanja wa ndege. Kutokana na kuelemewa na mawazo alijikuta usingizi umempitia humohumo ndani ya gari. Aligutuka saa kumi jioni baada ya kupigiwa honi na gari la wafanyakazi wa kiwandani kwake, walishangaa kumkuta bosi wao mahali pale.
Alikuwa amelala ndani ya gari hilo kwa saa tano! Alipokumbuka kilichomfanya awe pale na katika hali ile, alianza kulia tena. Baadaye kwa taabu aliliondoa gari lake kwa kasi ya ajabu kuelekea nyumbani kwake, Bugando.
Mike alianza kuamini ukweli kuwa UKIMWI ulikuwa na tabia ya kuwaua vijana mara tu wanapopata mafanikio katika maisha yao!
Alipata mafanikio makubwa katika maisha yake na sasa alitakiwa kufa na kuviacha vyote alivyokuwa navyo. Mbele yake aliona giza nene, tena aliziona siku zake za kuiaga dunia hazikuwa mbali naye, machozi yakamtoka.
Aliamini hapakuwa na mtu aliyeuogopa UKIMWI duniani kama yeye lakini sasa alikuwa nao na hakujua angewaeleza nini watu ili waamini kuwa katika maisha yake hakuwahi kutembea na mwanamke.
Aliamini kila mtu angemwona malaya kwa sababu ndivyo jamii ilivyouchukulia ugonjwa huo. Mike alitamani kujiua kwa kuogopa aibu hiyo. Alipofika nyumbani kwake aliingia ndani na moja kwa moja alikwenda mezani ambako alichukua kalamu na karatasi na kuanza kumwandikia barua Beatrice.
Mpenzi Beatrice,
Naandika barua hii nikiwa katika majonzi makubwa na machozi yakinitoka, Beatrice, jambo ninalotaka kukueleza si rahisi wewe kuliamini hata kidogo lakini ndivyo ilivyo. Najua litakuumiza zaidi lakini inabidi niseme ili angalau nipate faraja kutoka kwako! Nitakuficha hadi lini wakati hiki ni kifo?
Naikumbuka siku ya kwanza tulivyokutana shuleni Nsumba miaka mingi iliyopita, tangu siku hiyo hadi leo ni kama miaka kumi au zaidi.
Tangu wakati huo umenisubiri ili tuoane, tuzae watoto na kujenga familia yetu. Hilo limekuwa kweli, na wazazi wetu wametupa baraka zao na lilikuwa tegemeo letu kuwa siku chache zijazo tungefunga ndoa.
Beatrice, inaniuma kukueleza kuwa HATUTAOANA TENA!! Si kwamba nakuchukia, la, ila sitaki kuua kiumbe kisicho na hatia!
Beatrice, uamuzi huu unatokana na yale majibu ya damu tulivyokwenda kupimwa. Hayo ndiyo yaliyosababisha yote haya. Amini, usiamini, Beatrice, sijawahi kukutana na mwanamke kimapenzi katika maisha yangu na ndiyo maana siku zote huwa nasema ninaweza kuitwa “bikira wa kiume.”
Lakini cha ajabu na cha kushangaza majibu yameonyesha mimi nina virusi vya UKIMWI wewe huna! Nilipoyaona majibu haya sikuamini, ikabidi niende Medical Research kurudia vipimo, lakini nako majibu yakawa ni hayohayo. Leo tumepima kwa mara ya tatu bado mimi nimeonekana nina virusi, hivyo nimelazimika kuuchukua huo kama ukweli wenyewe.
Beatrice, ninakupenda na namshukuru Mungu katika maisha yetu ya kufahamiana hatukuwahi kuingia majaribuni na kufanya mapenzi. Je, unaikumbuka siku ile pale bafuni Natta Hotel? Kama tungemruhusu shetani na kufanya tendo la ndoa, wewe pia ungekuwa positive.
Sasa basi, kwa vile bado hujaambukizwa mimi sioni sababu ya kukuua Beatrice! Ni heri tuachane ili uolewe na mtu mwingine yeyote na uwe na familia yako. Naomba uniache mimi nife peke yangu. Nafikiri hivyo ndivyo Mungu alivyopanga.
Samahani Beatrice kwa kukupotezea muda wako mwingi lakini nitakulipa fidia kidogo. Nitakupa shilingi milioni kumi na gari moja lenye tela, hizo zitakuwa mali zako mwenyewe na zitakusaidia maishani.
Sina mengi ya kusema bali nakutakia maisha marefu popote. Wewe ni msichana mzuri, nina imani utapata mtu mwingine wa kukuoa na uzae watoto wazuri. Naomba ukizaa mtoto wa kiume umwite Mike kwa kumbukumbu yangu.
Asante.
Ni mimi katika majonzi,
Mike.
Je nini kitaendelea?
Tuonane siku ya Jumamosi mahali hapa.
 
SEHEMU YA 06


Mvulana mwenye akili na pia mcheza muziki, Mike Martin amekutana na msichana mzuri, mwenye mvuto na upole wa hali ya juu, Beatrice Rugakingira.
Wawili hao, huku wakiwa hawajawahi hata kukutana kimwili katika maisha yao, wanajikuta wakiangukia katika penzi zito na mahusiano kuanza rasmi huku ahadi ya kutokufanya mapenzi mpaka kuoana ikiwekwa.
Wanakubaliana, baada ya kipindi fulani, Mike anapata nafasi ya kwenda kusomea Shahada ya Uchumi katika Chuo cha Oxford nchini Uingereza. Akiwa njiani, anapata tatizo la kuumwa tumbo ambalo linamfanya kuhitaji kuongezewa damu.
Ndege inashushwa katika Jiji la Copenhagen nchini Denmark. Anapelekwa hospitali, wanapokuja wanafunzi kutoka nchini Tanzania kumuongezea damu, hakuna mwenye kundi kama lake zaidi ya msichana aliyesafiri naye, Laila.
Kinachofanyika, msichana Laila, kwa upendo wake wa dhati, anamuongezea damu Mike na kisa safari kuendelea.
SONGA NAYO...
Baada ya kuandika barua ile, huku machozi yakimtoka, Mike alianza kuisoma, hata yeye mwenyewe alisikia uchungu mwingi moyoni mwake lakini hakuwa na la kufanya. Mpaka wakati ule Mike alikuwa hajaamini kabisa kama yaliyokuwa yakitokea katika maisha yake yalikuwa kweli au ilikuwa ni ndoto na muda si mrefu angezinduka kutoka usingizini.
Kwa upande mwingine, Mike alijichukia mwenyewe na hakuona sababu ya kuendelea kuishi lakini vilevile hakuona sababu ya kujiua. Hivyo akaamua kumwachia Mungu afanye kazi yake, atakavyo mwenyewe.
Kilichomsumbua akilini mwake baada ya kuiandika barua ile ni kwa njia gani angemkabidhi Beatrice! Kwa jinsi alivyomfahamu Beatrice alijua barua ile ingemchanganya sana na si ajabu asingeyaamini majibu.
Kama msichana ni lazima angehisi ile ilikuwa njama ya kuachwa kijanja. Ili kumhakikishia kuwa aliyoaandika yalikuwa na ukweli, Mike aliamua kuzichukua karatasi za majibu ya Bugando na Medical Research na kuziambatanisha pamoja na barua ile na kuandika.
Tanbihi: Nyuma ya hii barua nimeambatisha karatasi zote za majibu ili upate kuamini.
Baada ya kuisoma barua ile Mike alijitupa kitandani bila kuvaa nguo, hakupata hata lepe la usingizi. Kulipokucha alinyanyuka kitandani kizembe na kuingia bafuni kuoga, baada ya kuoga alichukua nguo safi na kuvaa.
Akiwa tayari kwenda kazini kwake, kwa muda alijisikia kusahau kidogo habari ya majibu lakini ghafla taswira ilimrejea tena na pale pale akaishiwa nguvu za miguu na kukaa kitini. Hakujisikia tena kufanya kazi
Alichokifanya baada ya hapo ni kunyanyua simu na kupiga kiwandani Mwatex.
"Hallow nani anaongea?" Aliuliza simu ilipopokewa.
"Monica!" Katibu Muhtasi wake akajibu.
"Tafadhali waeleze kuwa hali yangu si nzuri sitafika kazini, sawa?"
"Unaumwa nini bosi?" Aliuliza Monica, ambaye naye siku zote juhudi zake za kumwinda Mike hazikukoma.
"Nimekwambia sijisikii vizuri inatosha, unataka kujua nini zaidi?” Aliuliza Mike kwa sauti ya ukali.
"Samahani bosi," alitamka Monica kwa upole.
Baada ya kukata simu aliyopiga ofisini, palepale Mike alizungusha namba ya Beatrice.
"Beatrice!"
"Naam darling," aliitika
"Nina maongezi na wewe na ningependa maongezi hayo tuyafanye sehemu ya faragha kidogo sijui unapendelea sehemu gani?"
"Ni kuhusu mipango yetu ya harusi?"
"Hapana mpenzi wangu."
"Ni juu ya nini tena Mike mbona unanirusha roho?"
"Ah! Ni mambo ya kawaida tu kati yangu mimi na wewe."
"Sawa tukutane Salma Cone basi!"
Salma Cone ni sehemu maarufu sana ya kuuza vinywaji na barafu mjini Mwanza.
"Hapana Beatrice, sehemu hiyo si nzuri sana kwa jambo linalotaka kuliongea, labda nikupitie hapo halafu twende sehemu nyingine."
"Wapi sasa?"
"Twende kisiwa cha Saa Nane!"
Kilikuwa ni kisiwa kilichokuwa kilometa moja kutoka mjini Mwanza, na ili ufike huko ilikuwa ni lazima upande boti. Wakazi wa Mwanza walipendelea kutembea huko siku za mwisho wa wiki.
"Sawa basi nipitie Salma Cone nitakuwa nakusubiri hapo, sijui ni saa ngapi?'
"Saa kumi jioni!"
Mpaka wakati huo Mike alikuwa akifikiria hali ingekuwaje mara tu Beatrice atakapoisoma ile barua, alijua angeumia mno kwa muda alioupoteza na aibu ambayo angeipata. Ni wazi angekosa mahali pa kuficha uso wake.
Mike aliligundua suala hilo lakini hakuwa na la kufanya, ilikuwa ni lazima aseme ukweli. Ndiyo alimpenda sana Beatrice lakini asingeweza kumwoa na kumwambukiza UKIMWI afe! Bado Mike alimshukuru Mungu kwa kuepusha tendo la ndoa kati yao.
***
Saa kumi kasoro dakika kumi Mike aliliegesha gari lake mbele ya jengo la Salma Cone mtaa wa Bantu. Aliamua kuwahi mapema ili walau awe anakunywa juisi wakati akimsubiri Beatrice.
Aliteremka haraka na kuingia ndani ya mgahawa wa Salma Cone. Alishangaa kumkuta Beatrice amekwishafika na tabasamu likiwa limemjaa usoni.
"Karibu Mike," Beatrice alinyanyuka kitini na kumkumbatia Mike akampiga mabusu matatu usoni! Watu wote waliokuwa ndani ya mgahawa walishangaa.
"Asante darling, nilifikiri nimewahi kumbe nimechelewa."
"Hapana, hujachelewa kwani hata mimi nimefika kama dakika kumi tu zilizopita. Nimewahi kwa sababu nina hamu kubwa ya kukijua hicho unachotaka kunieleza."
Mike alinyanyua uso wake na kumwangalia Beatrice.
"Mike mbona macho yako mekundu, unaumwa au?" Beatrice alihoji.
Palepale Mike alianza kulia tena.
"Ni mambo makubwa sana Beatrice na sijui kama utanielewa."
"Mambo gani hayo?"
"Twende Beatrice!" Mike alinyanyuka kitini huku akijifuta machozi!
Baada ya wote kuketi katika viti vyao Mike aliliondoa gari hadi karibu na Hoteli ya Tilapia kulikokuwa na kivuko cha kwenda kisiwa cha Saa Nane. Aliliegesha gari na wote wakateremka bila kuchelewa. Walikata tiketi na kupanda boti ndogo iliyowapeleka moja kwa moja hadi kisiwani. Kwa kuwa siku hiyo haikuwa mwisho wa wiki, walijikuta wakiwa wawili tu kisiwa kizima.
Mike na Beatrice walitembea mkono kwa mkono huku wakipita wanyama kama simba na chui katika seng'enge zao bila kuwajali. Lengo lao siku hiyo halikuwa kuwaangalia wanyama.
Walipandisha moja kwa moja hadi kilimani kwenye mapango yaliyo juu. Mtu akiwa huko maji ya Ziwa Viktoria huonekana kwa chini kabisa kama uko kwenye nyumba ya ghorofa tano. Beatrice aliangalia chini akasikia kizunguzungu.
"Mike hapa mtu akidondoka si anakufa kabisa?"
"Inawezekana maana maji yapo mbali sana."
"Lakini Mike, hebu tuyaache hayo bwana, nieleze kitu ulichoniitia."
Mike alinyamaza kwa muda na baadaye, huku akitetemeka alimkabidhi Beatrice barua! Beatrice aliipokea barua ambayo juu ya bahasha iliandikwa jina lake. Kabla hajaifungua alimwangalia Mike na kucheka.
"Na wewe huwa unapenda sana kunifanyia surprise."
Beatrice aliifungua barua ile na kuanza kuisoma, na kadri alivyozidi kuisoma ndivyo jasho jingi lilivyozidi kumtoka mpaka nguo alizovaa zikalowa kabisa. Alipomaliza kuisoma upande mmoja akageuza upande wa pili na kuanza kuzingalia zile karatasi zenye majibu.
"Mike, yaani umekaa chini ukaona huu ndio ujanja wa kuniacha, siyo? Mike! Mike! Mike! Mike! Mwogope Mungu Mike! Kumbuka muda ulionipotezea Mike, nimeacha wachumba wangapi kwa sababu yako? Mike leo uniache kinyama kiasi hiki? Eti kwa sababu tu umekutana na wasichana wazuri zaidi yangu! Haiwezekani.
Lakini kwa nini unanifanyia ukatili huu? Mike nimekukosea nini Mike? Ni heri nife kuliko kuiona aibu hii."
Alipomaliza tu kusema maneno hayo palepale Beatrice alijirusha kutoka juu kwenye pango walikokuwa wamekaa na kuanza kuporomoka kuelekea majini!
"Beatriceeee what have you done?" (Beatrice umefanya nini?) Mike alipiga kelele alipomwona Beatrice akielekea majini.
Eneo ambalo Beatrice alitumbukia ni eneo lililokuwa na kibao kilichoonya watu wasiogelee katika eneo hilo kwa kuwa kulikuwa na mamba wala watu.
Mike alipokiona kibao kile alichanganyikiwa akajua lazima Beatrice ataliwa na mamba. Alianza kuteremka mlima akikimbia kuelekea majini. Aliogopa sana mamba lakini alikuwa ameamua kuutoa uhai wake kwa ajili ya Beatrice kwani hata kama asingejikatisha hakuwa na maisha tena mbele!
Kabla hajaingia ndani ya maji aliona damu nyingi imetapakaa juu ya maji, akashtuka na kuamini kwamba Beatrice alikuwa tayari amekwishaliwa na mamba! Aliamini hivyo kwa kuwa kila alipotupa macho hakuweza kumwona Beatrice.
Je nini kitaendelea?
Je Beatrice amekufa?
 
SEHEMU YA 07

Wakati Mike anateremka kuelekea majini, Beatrice alikuwa akivuja damu nyingi usoni kutokana na jeraha kubwa alilolipata baada ya kujigonga kwenye mwamba. Aliogelea taratibu na kukaa juu ya jiwe nyuma ya kilima na kuendelea kulia.
Aliujutia muda alioupoteza kumsubiri Mike ambaye tayari alikuwa amemtelekeza na kwa kitendo kile aliwaona wanaume wote duniani ni wanyama.
Wakati Mike akiwa amekata tamaa kabisa, alitupa macho kwa chini na kumwona Beatrice amekaa juu ya jiwe, huku akitokwa na machozi. Alimfuata na kumbeba mgongoni na kupanda naye hadi nchi kavu ambako hakuna mamba wala mdudu yeyote aliyewagusa!
"Beatrice, imekuwaje mpenzi?"
"Ni heri nife Mike! Nimepoteza muda na vitu vingi sana kwa ajili yako, huwezi kunifanyia unyama huu na ukategemea niendelee kuishi, huu ni ukatili Mike. Mike huna hata huruma? Huwezi kunifikiria?"
"Beatrice amini nakupenda, na I am doing all these to protect you (na ninafanya hayo yote kukulinda wewe) kwa sababu sitaki kuua kiumbe asiye na hatia.”
"Mike ujanja unaoutumia ni wa kizamani sana, ni heri ungeniambia tu ukweli na ninakuambia Mike usiponioa najiua, sihitaji kuishi tena. Hebu fikiria watu wote hivi sasa wanajiandaa kwa ajili ya harusi yetu, nitawaeleza nini mimi? Sura yangu nitaificha wapi Mike!" Beatrice alisema huku akilia.
Damu kwenye jeraha usoni mwake ilizidi kumwangika!
"Beatrice twende nikupeleke hospitali!" Mike alisema.
"Sitaki kwenda hospitali, niache nife kwani hata nikifa itakuuma nini wewe?" Beatrice alimaka kwa hasira.
Mike alivua shati lake na kumfunga Beatrice usoni ili kuzuia damu isiendelee kutoka na alizidi kumbembeleza akubali kupelekwa hospitali na mwishowe alikubali.
Walipanda boti na kurudi Mwanza mjini. Mike akiwa kifua wazi! Ilikuwa aibu kwa mtu mwenye madaraka kama yake lakini hakujali.
Ng'ambo walipanda gari na kuelekea hospitali ambapo Mike alipita eneo la Makoroboi kwenye maduka ya Wachaga na kununua shati jipya akavaa.
Alimpeleka Beatrice hadi hospitali ya Sekou Toure ambako alishonwa nyuzi kumi na mbili usoni na kuruhusiwa kurudi nyumbani kwa sababu alikuwa hakuumia kiungo kingine cha mwili. Bahati nzuri kina cha maji mahali alipoangukia kilikuwa kirefu.
Njiani wakati wakirudi nyumbani Beatrice aliendelea kulia na Mike alizidi kumbembeleza akimweleza umuhimu wa mambo aliyoyaandika katika barua lakini bado Beatrice hakutaka kuelewa.
Alizidi kusisitiza waoane kwani aliyaona majibu yale ni ya bandia ili aachwe kijanja!
Walipofika Capri Point dada yake Beatrice alishangazwa na bendeji alizokuwa nazo mdogo wake usoni, wakati huohuo akilia.
"Mike vipi tena, leo mmepigana?" Maggie aliuliza.
"Hapana, Maggie, ila ni habari ndefu sana!" Mike alijibu.
"Yaani Mike umeamua kunifanyia hivyo, sawa tu!" Beatrice alisema.
"Mike vipi, mbona siwaelewi?" Alizidi kuhoji Maggie.
Wakati wakiendelea na hali hiyo mara shemeji yake Beatrice, mume wa Maggie, aliegesha gari nyumbani.
"Ndugu zangu vipi mbona bendeji kichwani, mnanitisha, kuna nini tena Maggie?" alimuuliza mke wake.
"Hata mimi ndio nauliza, sababu ndio kwanza wamefika, halafu naona kama wote walikuwa wanalia vile."
"Mike wewe ni mwanamume, hebu njoo ndani utueleze kilichotokea," Samson alisema.
"Ni habari ndefu jamani ambayo hata ninyi nikiwasimulia itakuwa ngumu sana kuiamini lakini ndivyo ilivyo," Mike alisema na baadaye akawasimulia.
"Beatrice aliponipeleka Bukoba kwa wazazi wake walinikubalia nimwoe lakini walishauri kwanza tupime UKIMWI kabla ya ndoa yetu. Tuliporudi Mwanza vikao vya harusi vilianza kufanyika, hatukupimwa mara tu baada ya kufika hapa kutoka Bukoba kwa sababu tulijiamini mno...!" Mike alisema wote wakiwa kimya. Kwikwi za kilio cha Beatrice ndizo zilizosikika.
Baadaye Mike aliendelea: "Tulijiamini mno kwa sababu mpaka wakati huu mimi binafsi sijawahi kukutana na mwanamke kimwili, mnaweza kuamini au msiamini lakini huo ndio ukweli.
Hilo hata Beatrice mwenyewe analijua na mimi naamini yeye pia hajawahi kufanya hivyo na wote tulikuwa tukisubiri siku ya ndoa yetu ili tufanye kitendo hicho. Siku chache zilizopita mzee Rugakingira alinipigia simu na kunikumbusha juu ya suala la kupimwa UKIMWI.
Ili kumridhisha tuliamua kwenda kupimwa na majibu ya kwanza yalipotoka yalionyesha mimi ni Positive na Beatrice ni Negative! Sikuyaamini majibu hayo, nilijua wananidanganya au wamekosea kupima. Ikabidi nirudie tena kupimwa huko Medical Research kwa mtu ninayemwamini zaidi. Majibu yalipotoka yalikuwa vilevile, nilikuwa HIV Positive.
Nilichanganyikiwa mno! Sikuwa na la kufanya ilibidi nilazimike kuyaamini majibu hayo, majibu yenyewe ni haya hapa!" Mike akaingiza mkono mfukoni na kutoa ile barua na majibu, akamkabidhi Maggie ambaye naye machozi yalikuwa yakimlengalenga.
"Baada ya kupata majibu hayo nilijaribu kumfikiria Beatrice, kwa bahati nzuri mimi na yeye hatujawahi kukutana kimwili hata siku moja kwa sababu ninampenda na sitegemei kama penzi la kweli linaweza kuua, nimeamua kutofunga ndoa hii!"
Mike aliingiza mkono mfukoni akatoa kitambaa na kuanza kujifuta machozi yaliyokuwa yakimlengalenga, halafu aliendelea, "Nayafanya yote haya kwa sababu nampenda Beatrice, sitaki kuua kiumbe kisicho na hatia. Beatrice ni msichana mzuri sana, ni bora nimpe nafasi ya kuolewa na mtu mwingine, kwangu mimi hili naona ndio penzi la kweli!
Nilishindwa nimweleze vipi Beatrice juu ya jambo hili, ndiyo maana nikaamua nimwandikie barua hiyo lakini alipoisoma alianza kunilalamikia kuwa nataka kumwacha kijanja na kabla sijakaa sawa alijirusha kutoka pangoni kule kisiwa cha Saa Nane. Akapasuka juu ya jicho na hivi sasa kashonwa nyuzi kumi na mbili!!” Mike alisema akijifuta machozi.
"Jamani nisaidieni, nachanganyikiwa, nifanye nini, najaribu kumwokoa Beatrice lakini hataki kuokolewa!" Mike alimaliza na kwikwi ya kulia ikamkaba, akalia kwa sauti. Samson alimsogelea na kumwekea mkono begani.
"Pole Mike!" alimliwaza.
"Beatrice!" Maggie aliita.
"Bee!"
"Unamsikia mwenzio?"
"Ndiyo, lakini ni mwongo dada, ameamua kuniacha sababu amepata umaarufu sana siku hizi lakini ukumbuke mimi na yeye tulikoanzia! Amewahonga madaktari ili aonekane ana virusi!"
"Beatrice usiwe mpumbavu, hawezi kufanya hivyo, wewe huoni ni mihuri ya Bugando na Medical Research?""Dada mimi sitaki naomba uniachie maisha yangu mwenyewe, ninachotaka ni kuolewa!"
"Beatrice una akili wewe? Utakufa!"
"Acha nife Maggie, hata wewe pia utakufa, ni lazima ujue mwisho wa maisha ya binadamu ni kifo na kumbukeni msipokufa kwa UKIMWI mtakufa na malaria, kama si malaria, kifua kikuu, kama si kifua kikuu ni homa ya matumbo lakini mwisho wa kila mwanadamu ni kifo. Vitabu vitakatatifu vinasema kila nafsi ni lazima ionje mauti!" Beatrice alimaliza na kuanza kulia tena.
Walijaribu huku na kule kumbeleleza lakini hakukubali, msimamo wake ulibaki palepale kuwa ni lazima Mike amwoe.
Msimamo huo uliwashangaza wote na ikabidi Maggie amshauri Mike ashikilie msimamo wake ili kuyaokoa maisha ya mdogo wake.
"Dada wewe ndiye unamshauri Mike hivyo, siyo? Sasa mimi natoa saa 72! Hivi sasa ni saa tatu, ikifika Jumapili saa tatu usiku ni lazima Mike awe amebadilisha msimamo wake, vinginevyo najinyonga. Kama hamuamini basi subirini!"
Baada ya kusema maneno hayo Beatrice alinyanyuka na kukimbilia chumbani kwake na kujifungia kwa ndani.
"Mike sikiliza sisi hapa tumeshajua hakuna harusi tena, wewe usiyafuate maneno ya huyu chizi. Umejaribu kumsaidia vya kutosha lakini hataki kuelewa. Binafsi nakushukuru sana kwa moyo wako wa upendo," Maggie alisema.
"Sasa umekwisha jaribu kuchunguza ni wapi tatizo hilo ulilipata?" Samson aliuliza.
"Kwa kweli sijui ila nina wasiwasi sana na damu niliyoongezewa Copenhagen wakati ule nilipofanyiwa upasuaji. Unajua wakati huo utaratibu wa kupima damu kama ina virusi kabla mtu hajaongezewa haukuwepo. Hilo ndilo linanitia wasiwasi na nina hakika ni wakati huo ndipo niliambukizwa, amini usiamini Samson, sijawahi kukutana na mwanamke kimwili."
Saa nne usiku Mike alisindikizwa hadi nje ambako alichukua gari lake na kurejea nyumbani kwake Bugando.
***
Siku iliyofuata Mike alikwenda kazini kama kawaida lakini kazi zilimshinda, ikamlazimu aondoke kazini majira ya saa tano kurejea nyumbani. Aliamua apitie nyumbani kwa wazazi wake kuwasalimia na pia kuwaeleza juu ya tatizo lake.
Alipofika nyumbani alikuta shamsharamsha za maandalizi ya harusi. Ilionekana kabisa kuwa maandalizi yalikuwa yakifanyika harakaharaka. Pembeni ya nyumba yao kulikuwa na ng'ombe kumi na mmoja walioandaliwa kwa ajili ya harusi yake.
Hali aliyoikuta nyumbani kwao ilimpa huzuni kubwa. Alishindwa kuelewa angewaeleza nini watu wote waliokuwa wamejiandaa kwa harusi yake.
Mike alisikia uchungu sana moyoni kwa jinsi alivyowaona akinamama wakichambua mchele na wengine wakiimba nyimbo mbalimbali kwa furaha. Walikuwa hawajui yaliyokuwa yakimsibu moyoni mwake.
Baadaye mama yake aliyekuwa jikoni alitokea sebuleni ambako Mike alikuwa amekaa.
"Mwanangu Mike kwa nini huwezi kuchangamka wakati hii ni harusi yako? Kwa nini una huzuni kiasi hicho? Unanikwaza mimi mama yako!" Alisema mama yake.
Machozi yalitaka kumtoka Mike lakini alijizuia kwa furaha aliyoionyesha mama yake, alishindwa kusema kilichokuwa kikimsumbua moyoni mwake, ikabidi akichimbie moyoni.
"Mike mwanangu unaumwa baba?" Mama yake aliuliza.
"Ndiyo mama!" Alijibu.
"Unaumwa nini mwanangu?" Mama aliuliza kwa wasiwasi.
"Mafua mama!" Alijibu harakaharaka.
"Sasa ni kwa nini usinywe vidonge vya Contac au Piriton mwanangu, unaendekeza ugonjwa wakati siku zenyewe zimebaki chache?" mama yake alionekana kutofahamu kitu.
Hapo Mike alishindwa kujizuia ikabidi machozi yamtoke, akachukua kitambaa na kujifuta kabla mama yake hajagundua.
"Nimepanga kununua Contac nikifika mjini mama."
Alipotoka nyumbani kwao alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwake na kujitupa kitandani. Hakuchukua muda mrefu akapitiwa na usingizi. Kitendo cha kutolala kwa siku mbili mfululizo kilisababisha alale usingizi mzito. Hakuzinduka hadi saa tano usiku. Baada ya hapo hakulala tena mpaka asubuhi. Siku hiyo pia hakwenda kazini, aliamua kushinda nyumbani, akiwaza na kuwazua matatizo yaliyokuwa yakimsibu. Jioni alimpigia simu Beatrice na kuongea naye, aliendelea kusisitiza msimamo wake.
"Mike kumbuka zikipita saa 72 tu nisilaumiwe, si wewe unajifanya kumsikiliza Maggie kuliko mimi?" Alipomaliza kusema hayo akakata simu.
Mike alizidi kuchanganyikiwa, hakujua la kufanya, tatizo la Beatrice tayari kwake lilikwishakuwa kubwa kuliko hata tatizo alilokuwa nalo yeye. Alijaribu kufikiria nini afanye ili kumwelewesha juu ya nia nzuri aliyokuwa nayo.
Mike alikosa njia kwa kuwa tayari Beatrice alikwishajenga hoja akilini mwake kuwa Mike alifanya hivyo ili amtelekeze. Kila alipofikiria walikotoka na Beatrice tangu enzi za Nsumba, alichanganyikiwa, alishindwa kuelewa ni nini kilikuwa kikitokea katika maisha yake.
Pamoja na hayo yote hakutaka kabisa kumwoa Beatrice kwa sababu kwa kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na kumchinja au kumtilia sumu kwenye chakula.
Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 08

Jumapili asubuhi Mike aliamua kwenda kusali, lengo lake likiwa kutubu dhambi zake zote kwa vile alijua hakuwa tena na maisha marefu mbele yake. Hakujua dhambi alizokuwa nazo lakini aliamua kwenda kutubu tu.
Kanisani Mike alikaa kiti cha nyuma kabisa.
Kama dakika kumi baada ya yeye kuingia akiwa katikati ya sala alisikia sauti ya viatu vikigonga sakafuni kwa nguvu. Alipogeuga nyuma macho yake yaligongana na ya Beatrice ambaye alikuwa akiingia kanisani.
Beatrice alionekana kakonda mno na mwenye huzuni kubwa, alipita moja kwa moja hadi kwenye kiti kilichokuwepo mbele ya Mike na baada ya misa waumini wote walitoka nje ambako Beatrice na Mike walikutana.
"Mike sikiliza hivi umechoka kuniona duniani au?"
"Hapana Beatrice, nakupenda mno na nisingependa kukupoteza, ndiyo maana sitaki kukuambukiza virusi! Kwa nini hutaki kunielewa Bite?"
"Mike kumbuka mwisho ni saa 72 ni leo saa tatu usiku, kama muda huo utafika bila kunitaarifu kuwa umebadili msimamo wako utanikuta naning'inia mtini unasikia?”
Baada ya kusema hayo Beatrice alianza kutoa machozi na kuondoka bila kuaga!
Mike alibaki kimya, kwa upande mmoja maneno ya Maggie kuwa Beatrice asingejiua yaliendelea kumtia nguvu lakini alipojaribu kufikiria upande mwingine, hasa kutokana na hali aliyokuwa nayo Beatrice pale kanisani, Mike alianza kuhisi kuwa yawezekana kabisa Beatrice angefanya kweli.
Alipofika nyumbani Mike akiwa mwenye mawazo mengi, alijitupa kitandani na kulala. Aligutuka usingizini saa tatu kasoro dakika kumi! Alikuwa amelala kwa karibu saa kumi mfululizo tangu atoke kanisani.
Ghafla alikumbuka kitu akilini mwake, kengele ya hatari iligonga kichwani mwake, zilikuwa zimebaki dakika kumi tu Beatrice ajinyonge kama kweli nia yake ilikuwa hiyo.
***
Mike aliinua simu na kupiga nyumbani kwa Samson, kuulizia kama kweli Beatrice alikuwepo.
"Ngoja nimwangalie chumbani mwake," Maggie aliongea bila wasiwasi wowote.
"Beatrice hayupo ndani lakini usiwe na wasiwasi wowote Mike!" Maggie alimpoza.
Maneno yale ya Maggie yalimtia Mike wasiwasi, alitoka nje na kuingia ndani ya gari kuelekea Capri Point, dakika saba tu zilikuwa zimebaki kabla ya kwisha kwa muda aliotoa Beatrice.
Mike aliendesha gari huku akimwomba Mungu njiani kusiwe na msongamano wa magari ambao ungemkwamisha kufika Capri Point kabla ya saa tatu kamili.
Alipokuwa akiingia barabara ya Nyerere, askari mmoja wa usalama barabarani alimsimamisha lakini Mike alipuuzia na kuendelea na safari yake.
"Tutajua kesho," Mike alijisemea baada ya kumpita askari huyo.
Alipofika eneo la kituo cha mafuta cha Jamhuri, karibu na jengo la Benki ya Taifa ya Biashara alikutana na msusuru mrefu wa magari uliosababishwa na ajali mbaya iliyotokea eneo hilo!
Alipoangalia saa yake ilionyesha kuwa zilikuwa zimebaki dakika tano tu, akaamua kuliweka gari pembeni akatoka na kukimbia hadi mtaa wa pili, alikochukua teksi na kumwamuru dereva aendeshe kwa mwendo wa kasi kuelekea Capri Point.
***
Walipofika maeneno ya bustani ya CCM, makao makuu dereva aliona kitu na kumgutua Mike.
"Ona yule dada anapanda kwenye mti usiku huu sijui anatafuta nini?”
"Yuko wapi?"
"Pale kwenye mti mkubwa!" Dereva alimwonyesha tena huku akipunguza mwendo.
"Achana naye, wewe ongeza mwendo kuna kitu cha muhimu sana tunawahi!" Dereva akabadilisha gia na kuweka namba nne, kisha kukanyaga mafuta ya kutosha.
Alipoangalia saa yake ilimwonyesha saa 2:58 na ghafla wazo lilimjia.
"Mungu wangu yule dada anaweza kuwa Beatrice sijui nirudi nikamwangalie au sijui niende tu?" Mike alijiuliza na kujikuta yuko njia panda.
"Geuza gariii!" Mike alimwamuru dereva wa teksi na bila ubishi, dereva alipiga “norinda” gari likatimua vumbi na kukata kona.
Walirudi mahali pale walipomwona yule msichana, dereva wa teksi alifanya yote hayo bila kujua linaloendelea, alifanya hivyo kutii amri ya tajiri wake.
Walipoukaribia ule mti ilikuwa inatimia saa 2:59:58! Zilikuwa zimebaki sekunde mbili tu kufika saa tatu. Mike alikwishakata tamaa ya kuyaokoa maisha ya Beatrice tena.
Alipofika pale chini ya mti yule msichana alijiachia na kamba ikamkaba shingoni! Alipoviangalia vizuri viatu alivyovaa msichana yule ALIVIFAHAMU! Vilikuwa ni viatu ambavyo alimnunulia Beatrice kama zawadi kutoka Uingereza.
Baada ya kugundua kuwa aliyekuwa akijinyonga ni Beatrice, Mike alipiga kelele kama mwendawazimu Beatrice don't kill yourself! (Beatrice usijiue).
Aliushukuru uamuzi wake wa kuamua kugeuza gari.
Tayari Beatrice alikuwa akining'inia mtini! Bila kuchelewa Mike aliikamata miguu ya Beatrice na kuisukuma juu ili Beatrice asizidi kukabwa zaidi. Wakati akifanya hivyo alimwita dereva aje amsaidie.
"Una kisu hapo karibu?" Alimuuliza dereva alipomkaribia.
"Ndiyo lakini kipo ndani ya gari."
"Kilete upesi, nisaidie kuikata kamba shingoni mwake."
Dereva alikimbia haraka kwenda kwenye gari na kuchukua kisu. Aliporudi alipanda harakaharaka mtini na kuikata ile kamba! Beatrice akaanguka chini kama mzigo.
Mike alipomchunguza Beatrice kwa harakaharaka kifuani aligundua alikuwa hapumui na alipomgusa upande wa moyo alihisi kutopiga.
"Dereva hebu mshike na wewe kifuani, nashindwa kugundua vizuri kama moyo wake unapiga au umesimama."
Dereva aliushika moyo wa Beatrice.
"Hata mimi siusikii ukipiga." Mike alizidi kuchanganyikiwa.
"Sasa wewe mpigepige kifuani upande wa moyo na mimi nimpulizie pumzi mdomoni labda ataamka," Mike alisema kwa hofu kubwa.
"Kwani huyu msichana ni nani yako?" yule dereva aliuliza.
"Okoa maisha kwanza tutaongea baadaye!"
Mike alianza kumpulizia Beatrice pumzi ya uhai mdomoni na dereva akawa anaupigapiga moyo wa Beatrice ili kuushtua lakini pamoja na juhudi zote hizo Beatrice hakuamka. Alionekana kama mtu aliyekwishapoteza uhai wake.
Jambo hilo lilimuuma sana Mike, alipofikiria kifo cha Beatrice alisikia uchungu sana moyoni mwake na machozi yakaanza kumdondoka.
"Ni heri ningekubali kumwoa," Mike aliwaza huku akiendelea kulia, ndani ya nafsi ya alijilaumu sana kwa kusababisha kifo cha mwanamke aliyempenda.
"Dereva sogeza gari tujaribu kumpeleka hospitali."
"Hospitali gani?"
"Sekou Toure!"
Dereva alilisogeza gari na wote wakampakia na kuondoka kuelekea Isamilo, mahali ilipo hospitali ya Sekou Toure.
Walipofika hospitali wote waliteremka garini na kumbeba Beatrice hadi mapokezi.
"Huyu dada si alikuwa hapa juzi tu?" Muuguzi mmoja pale mapokezi aliuliza baada ya kuziona bendeji alizokuwa nazo Beatrice usoni.
"Ndiye."
"Imekuwaje?"
Mike alipata kigugumizi kulijibu swali hilo lakini alipogundua kuwa ilikuwa ni lazima kusema ukweli ili aokoe maisha ya mpenzi wake ilibidi atoe jibu.
"Alikuwa akijaribu kujinyonga."
"Unasemaje?" Aliuliza yule nesi kwa mshangao na Mike akarudia tena kutoa jibu.
"Kwa sababu gani?"
Swali hilo lilifuatiwa na kimya kikubwa.
Bila kuchelewa, Beatrice alikimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi ambako alilazwa na kutundikiwa chupa ya maji ya Normal Saline ambayo yalikwenda kwa kasi ili kunyanyua mapigo yake yaliyokuwa chini sana.
Pia, daktari aliagiza awekewe mashine ya hewa ya oksijeni ili kumsaidia kupumua. Alidai kama kusingefanyika juhudi za haraka, maisha ya Beatrice yangepotea kwa kuwa mapafu na moyo wake yalikuwa hayafanyi kazi vizuri.
Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 09

Baada ya huduma zote hizo Mike alimlipa dereva kiasi cha shilingi elfu tisa kwa kazi yake aliyoifanya.
"Pole sana bwana, tuombe Mungu amnusuru mgonjwa wetu!"
"Asante sana umenisaidia sana, bila wewe sijui kama ningeweza!"
"Usijali!"
Kabla dereva hajaondoka Mike alikumbuka kitu.
"Nimeacha gari langu mtaa wa Nyerere, karibu kabisa na mnara wa saa, hebu naomba uchukue hizi funguo ukaliondoe hapo lilipo ulipeleke nyumbani kwangu!"
"Ni gari la aina gani bwana?" Aliuliza yule dereva wa teksi.
"BMW!" Alijibu.
"Unaishi wapi rafiki?"
Mike alimwelekeza yule dereva nyumbani kwake na baada ya kuelewa dereva aliondoka kuelekea mjini.
Mike alibaki amekaa kwenye benchi nje ya chumba cha wagonjwa mahututi hakutaka kuondoka, alitaka auone mwisho wa maisha ya mpenzi wake. Akiwa katikati ya mawazo, ghafla mlango ulifunguliwa na nesi mmoja akatoka.
"Kaka huyu dada namfahamu, nafikiri anafanya kazi Bugando, au siyo?" Aliuliza.
"Hapana nafikiri umemfananisha," Mike alificha.
"Si anafunga ndoa hivi karibuni, maana kuna rafiki yangu wanafanya naye kazi Bugando aliniletea kitambaa cha sare kwa ajili ya harusi ya dada huyu na tayari nimeshashona, siyo huyu kweli?" Aliendelea kuuliza.
"Nafikiri umemfananisha," Mike alijibu harakaharaka.
Maswali ya dada yule yalimuumiza sana Mike na hakutaka kabisa yaendelee. Alijua ni lazima yangefika mahali pa kuulizwa sababu ya Beatrice kuamua kufanya hivyo, kitu ambacho Mike hakuwa tayari kukiongelea.
"Samahani dada kwani huko ndani kunaendelea nini?" Mike aliuliza kwa sauti iliyojaa wasiwasi.
"Anaendelea vizuri ila mapigo yake yapo chini mno, tumejaribu kuyainua kidogo lakini bado!"
"Je, anapumua?"
"Anatumia mashine ya oksijeni!"
"Lakini atapona kweli sista?"
"Usiwe na wasiwasi, tuendelee kumwomba Mungu."
Kauli hiyo ya nesi ilimtia Mike hofu zaidi, nesi alipoondoka Mike alianza kusali sala ya “Baba Yetu Uliye Mbinguni!” Alisali sala hiyo mara nyingi mno akimwomba Mungu ayanusuru maisha ya Beatrice.
Mwisho wa sala yake alisema: “Ee Mungu unaijua nia yangu, mimi nina virusi lakini Beatrice hana, nimejaribu kila niwezalo kuokoa maisha yake lakini Beatrice hanielewi, Ee Mungu wangu, kosa langu mimi ni lipi? Baba nipe njia iliyo njema ya kuepuka tatizo hili!"
Mike aliendelea kusali huku machozi yakimtoka.
Akiwa katikati ya mawazo, mara mlango wa chumba cha wagonjwa mahututi ulifunguliwa tena.
Mike alisimama wakati huo machozi yakimtoka.
"Sista vipi? Kuna nini? Tafadhali niambie ukweli!" Mike aliuliza maswali mengi kabla hajajibiwa swali moja.
"Hakuna tatizo ila naomba uingie ndani maana hapo nje kuna mbu wengi sana, njoo tu huku ndani ukae karibu na mgonjwa wako!"
"Asante sana sista,” alisema Mike na kabla hajaingia alikumbuka kitu:
"Sista kuna sehemu naweza kupiga simu hapa?'
"Unataka kupiga simu wapi?"
"Nyumbani kwao Beatrice kwani hawana habari juu ya haya yanayotokea."
"Hawana habari?"
"Ndiyo!"
"Basi ingia humu ndani nitakupatia simu."
Mike aliingia ndani na kwenda moja kwa moja hadi ofisini kwa nesi na kupewa simu. Alipiga simu ya nyumbani kwa Samson ambapo simu iliita kwa muda mrefu sana bila kupokewa. Hakuwa na haraka kwa kuwa alijua kabisa kuwa kwa wakati ule lazima walikuwa wamelala. Baada ya kungoja kwa muda wa dakika tatu simu ilipokewa.
"Hallow! Hallow nani anaongea?" Ilikuwa ni sauti ya Samson.
"Ni mimi Mike."
"Vipi mbona usiku hivi simu?"
"Nipo Hospitali ya Sekou Toure, Beatrice amelazwa"
"Amelazwa anaumwa nini?"
"Ah! Alitaka kutimiza alichokiahidi na sijui kama atapona. Kwa kweli inaniuma sana na ninahitaji msaada wenu."
"Kweli?"
"Ndiyo."
"La, tumejaribu sana kumtafuta na hata tukapiga simu nyumbani kwako lakini ilikuwa haipokewi!”
"Nafikiri ni wakati huo ndio nilikuwa nahangaika hospitali, nilikuwa nimechanganyikiwa mno!”
"Ok! Tunakuja sasa hivi."
Dakika kumi baadaye Samson na Maggie walisimamisha gari getini mbele ya Hospitali ya Sekou Toure.
"Mzee, samahani unaweza kutueleza ni wapi ilipo wodi ya wagonjwa mahututi?" Walimuuliza mlinzi waliyemkuta getini.
"Zungukeni upande wa pili kuna chumba kimeandikwa ICU," aliwafahamisha.
Walizunguka kama walivyoelezwa, haikuwa kazi kubwa kukiona chumba hicho. Walibonyeza kengele iliyokuwa mlangoni na mlango ukafunguliwa.
"Karibuni!" Ilikuwa ni sauti ya nesi wa zamu.
"Asante sana! Mimi naitwa Samson na huyu ni mke wangu anaitwa Maggie, tunaomba utusaidie kumwona ndugu yetu amelazwa hapa wodini."
"Hivi sasa siruhusiwi kabisa kuingiza mtu wodini, hata hivyo nitawasaidia , ndugu yenu ni Beatrice?"
"Ndiyo, anaendeleaje?" Aliuliza Maggie.
"Hali yake siyo mbaya ingawa haongei, haya ingieni mmuone!"
Samson na Maggie waliingia chumbani na moja kwa moja walikwenda hadi kitandani ambako walimkuta Mike alipowaona tu alianza kulia tena.
"Mike wewe ni mwanamume, jikaze," Samson alimsihi.
"Nashindwa Samson, Beatrice amefanya kitu kibaya sana kama akifa mimi nitajisikia vibaya mno maisha yangu yote. I will feel guilty for the rest of my life” (Nitajisikia mwenye hatia maisha yangu yote).
"Nyamaza shemeji, Beatrice hawezi kufa," Maggie alimpoza Mike.
Maggie aliinama na kumwangalia Beatrice pale kitandani, alipomwona Beatrice anatupa shingo yake huku na kule naye pia alishindwa kuvumilia akaanza kulia huku akisema maneno ya Kihaya: "Omwisiki ogu mufela nayenda kushasa emitima yaitu busha." (Msichana huyu ni mjinga sana anataka kututia huzuni ya bure).
Wote walisimama wakiwa wamekizunguka kitanda bila kujua la kufanya. Chupa za maji ziliendelea kuingia katika mishipa ya Beatrice. Mdomoni alikuwa amefungwa mashine ya kusaidia kupumua.
"Samson kweli Beatrice atapona?" Mike aliendelea kuuliza.
"Usiwe na wasiwasi atapona tu," Samson alimliwaza.
"Heri ningemuoa."
Saa tisa usiku Samson na Maggie walipitiwa na usingizi lakini Mike alibaki amesimama pembeni mwa kitanda akimwangalia Beatrice. Hakuwa hata na lepe la usingizi. Yote hayo yalitokana na kutaka kufahamu maendeleo yote ya mpenzi wake.
Ilipotimia saa kumi na moja alfajiri wakati muadhini anaadhini, kwa mbali Mike alimwona Beatrice akifumbua macho. Aliwaangalia Samson na Maggie wakiwa wamelala huku wameegemea meza, akawatingisha.
"Amkeni, Beatrice kafumbua macho! Kafumbua macho! Kafumbua macho!” Mike alisema kwa sauti kama mtu aliyepagawa, alikuwa na furaha mno moyoni mwake.
Samson na Maggie waliinuka na kukimbilia kitandani ambako walimkuta Beatrice kweli kafumbua macho na kuyapepesa akiangalia darini.
"Lihimidiwe jina la Mungu!" Samson alisema na wote wakapiga magoti kumshukuru Mungu. Walipomaliza walisimama na kuendelea kuangalia maendeleo yake.
Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 10

Ilipotimu saa 12 kamili, Beatrice alimudu kunyanyuka kutoka kitandani.
"Hapa nipo wapi?" Ndilo lililokuwa swali lake la kwanza.
"Hospitali!" Mike alijibu.
"Nani kanileta hapa?"
"Kwa nini hukuniacha nife Mike?" Beatrice alimaka na baada ya kusema hayo alizichomoa sindano zote za dripu zilizokuwa kwenye mishipa yake na maji yakaanza kumwagika chini. Alikuwa amechanganyikiw
a. Hakuna aliyeamini kuwa Beatrice alikuwa na akili timamu!
"Sista!" Mike alimwita nesi.
"Bee!"
"Tafadhali njoo, mgonjwa analeta fujo."
Baada ya sekunde chache nesi alikuwa pale.
"Vipi?" aliuliza kwa mshangao
"Anazichomoa dripu."
"Niachieni nife na ni lazima nife tu, unajidai kuniokoa siyo? Kama usiponioa ni lazima nitajiua Mike, nimeamua hivyo na hivyo ndivyo itakavyokuwa," Beatrice alipiga kelele.
Nesi alipigwa butwaa kusikia habari hiyo akawa amekwishagundua kuwa Mike alimdanganya lakini akajifanya hakusikia. Akarudi ofisini na kumpigia simu daktari wa zamu.
Daktari alipokuja alimwandikia Beatrice dozi kubwa ya Valium ili alale usingizi.
Baada ya kufanya hayo nesi alimwita Mike ofisini kwake na kuanza kuongea naye.
"Enhe! Kaka kwa nini ulinidanganya? Kumbe ni Beatrice yuleyule na wewe ndiye mwanamume wake! Kwa nini hutaki kumwoa? Lakini ninyi wanaume ni wanyama sana!" Nesi alijikuta akipayuka hovyo akikiuka maadili ya kazi yake na kuongea kwa jazba.
"Ni habari ndefu sista, na nisingependa kuiongelea sasa hivi, samahani kwa kukudanganya, ilibidi iwe hivyo lakini nakuahidi ipo siku utanielewa hata kama ni baada ya miaka ishirini. Ninachotaka kukuhakikishia ni kwamba bado nampenda Beatrice. Naomba unisamehe sana sista," Mike alimaliza.
Asubuhi Mike aliitwa na daktari na kumwagiwa kapu la maswali, hakuona sababu ya kumficha daktari ukweli kuhusu jambo lililokuwa likiendelea, ilibidi aseme kila kitu kuhusu majibu ya VVU na harusi yao.
"Uamuzi wako ni wa busara sana lakini nakuomba usikate mawasiliano ghafla, kata taratibu kwa sababu ukifanya haraka huyu msichana atajiua! Nimegundua hatanii hata kidogo, " daktari alisema.
Saa sita mchana Beatrice alizinduka usingizini na kukikuta kitanda chake bado kimezungukwa na watu. Aliwaangalia mmoja baada ya mwingine. Alimtambua Maggie.
"Wewe ndiye unayechangia sana kukwamsiha ndoa yetu, hivi nikifa utafaidika na nini?"
"Beatrice mdogo wangu nimekukosea nini, kumbuka tunafanya haya kwa faida yako!"
Baada ya kusema hayo Beatrice alizungusha kichwa chake upande wa pili, akamtambua Mike.
"Mike mpenzi wangu nimekukosea nini mimi? Hivi nikifa utafurahi kweli? Mike ni lazima ukumbuke Nsumba na Nganza."
"Sitaki kukuua Beatrice!" Mike alimjibu huku machozi yakimtoka.
"Sasa Mike, chagua moja, unioe ili tuishi angalau miaka michache pamoja kabla hatujaugua UKIMWI kama kweli unao au uache kunioa nife leo au kesho. Kipi bora kwako?" Beatrice aliuliza kwa uchungu.
Maneno hayo yalikuwa kama msumari wa moto, yalijipenyeza na kuuchoma moyo wa Mike akajikuta akiyaweka katika mizani ndani ya akili yake.
Beatrice aliruhusiwa kutoka hospitalini jioni ya siku hiyohiyo. Suala la kutaka kujiua liliendelea kufanywa siri ili asishitakiwe. Nyumbani aliwekewa ulinzi mkali sana na Maggie ili asije akafanya tena kitendo alichotaka kukifanya. Maggie alikwishaamini kabisa kuwa Beatrice alikuwa hatanii.
Akiwa nyumbani kwake usiku huo Mike aliendelea kuyawaza yaliyokuwa yakiendelea katika maisha yake. Aliyafikiria sana maisha ya Beatrice, uamuzi wake wowote ulimanaanisha kifo cha Beatrice!
Kama angeacha kumwoa angekufa, tena haraka zaidi na kama angeamua kumwoa pia angekufa lakini angalau wangeishi pamoja kwa miaka kadhaa.
Mike alijikuta njia panda, mahali ambapo alitakiwa aamue kitu kigumu sana maishani mwake.
Ghafla alijikuta akibadili uamuzi wake wa awali na kusema, "Sasa nafunga ndoa na Beatrice lolote na liwe!"
***
Siku hiyo ya Jumanne kulipopambazuka Mike hakujisikia kwenda kazini, baada ya kupiga mswaki aliwasha gari lake na kuondoka moja kwa moja hadi Capri Point ambako alibahatika kumkuta Samson akiwa bado hajaondoka kwenda kazini kwake. Aliwaita Samson na Maggie na kukaa nao kikao.
"Jamani nimekuja ili tuongee vizuri kuhusu suala zima la mimi na Beatrice, usiku wa kuamkia leo nimewaza sana na kugundua kuwa uamuzi wowote nitakaochukua utamaanisha kifo cha Beatrice," alisita kidogo na kuwaangalia akina Maggie.
“Nimegundua Beatrice hatanii, amedhamiria kutimiza lengo lake, hivyo natamka hapa mbele yenu kuwa nitamuoa Beatrice na mipango ya ndoa iendelee."
Maggie na Samson walishangaa.
"Ninachowaomba ndugu zangu ni kwamba tuifanye hii kuwa siri ya watu wanne tu yaani mimi, Beatrice, Maggie na Samson, au mnaonaje?" Alimaliza na kuwatupia macho, akingoja wangesema nini.
"Sawa, tutafanya nini wakati Beatrice mwenyewe ameamua?" Maggie aliitikia.
Kikao kiliishia hapo na Mike aliomba kumwona Beatrice chumbani mwake, akaruhusiwa.
"Hallow darling!" Mike aliita akiwa na tabasamu mdomoni, lakini Beatrice alionyesha kutomchangamkia.
"Beatrice, nina habari njema mpenzi!"
"Habari gani?" Beatrice aliuliza kwa ukali.
"Nimekubali kukuoa tena."
Beatrice aliruka kitandani na kumkumbatia Mike kwa furaha.
"Asante sana mpenzi, sasa umeyaokoa maisha yangu," Beatrice alitamka kwa furaha kubwa.
Mike alitulia kidogo na baadaye aliendelea kumweleza. "Beatrice nimekubali lakini kwa masharti yafuatayo: Tutaishi pamoja kama mke na mume lakini siku zote katika tendo la ndoa tutatumia kondomu, sharti la pili ni kwamba sitakuwa tayari kuzaa kwani kwa kufanya hivyo kutasababisha kuua kiumbe kisicho na hatia, nafikiri unanielewa Beatrice?”
"Hilo tusiliongelee sasa hivi Mike, cha muhimu ni ndoa mengine tutayongea mbele ya safari lakini..." Beatrice alikatisha maongezi yake.
Walikumbatiana na kupigana mabusu na kisha wote wakatoka nje Maggie alishangaa kuuona uso wa Beatrice ukiwa na furaha asubuhi ile. Beatrice alimfuata dada yake na kumkumbatia, halafu akamkumbatia shemeji yake Samson akisema: "Nisameheni sana."
"Basi jiandae uende kazini siku zako za mapumziko zimekwisha jana."
"Kwa sababu furaha yangu imerejea tena nitakwenda kazini," alisema Beatrice akitabasamu.
Beatrice alijiandaa na alipomaliza Mike alimchukua kwa gari lake hadi hospitali ya Bugando.
Historia ya virusi vya Mike ilibaki ni siri ya watu wanne tu. Sio mzee Rugakingira, mkewe wala mzee Martin, mkewe wala ndugu, jamaa na marafiki waliolifahamu jambo hilo. Vikao vya harusi Bukoba na Mwanza mjini viliendelea kama kawaida.
Ilikuwa ni ndani ya Kipepeo Grill ukumbi uliopo katika Hoteli ya New Mwanza ambako kikao cha tatu na cha mwisho cha harusi ya Mike kilikuwa kikiendelea.
Kepha Masaga, rafiki mkubwa wa Mike kutoka Dar es Salaam alikuwa ni miongoni mwa watu waliohudhuria kikao hicho, alikuwa mfanyabiashara maarufu.
"Tumsikilize Masaga, anatoa nini kutoka Dar es Salaam," Mwenyekiti wa kikao hicho, Emmanuel Chacha, mwandishi maarufu wa vitabu mjini Mwanza alisema.
Baada ya Mwenyekiti kusema hivyo, Masaga alinyanyuka kitini na kuanza kupandisha suruali yake kwa mbwembe na kusema: "Kwa kweli mimi na bwana Mike ni marafiki wa muda mrefu sana na tulikuwa wote masomoni Uingereza. Kwa sababu hiyo gharama zote za usafiri, fungate lao katika Hoteli ya Sheraton jijini Dar es Salaam, vinywaji vyote siku ya harusi vitakuwa juu yangu, " alimaliza Masaga na kupigiwa makofi.
Mchango wa Masaga ulikuwa changamoto kubwa sana kwa wafanyabiashara wa Mwanza.
Msungu, mvuvi maarufu katika Ziwa Viktoria, naye alinyanyuka kwa mbwembe nyingi.
“Mimi nataka hii iwe harusi ya aina yake katika historia ya mji wa Mwanza na Tanzania nzima kwa ujumla. Hivyo, nataka harusi hii kwa gharama zangu ifungwe angani na nitakodi ndege ya kampuni ya Precision ambayo itawachukua mchungaji, bwana na bibi harusi, wapambe wao, wanakwaya, wazazi na marafiki na kuruka angani ambako harusi itafungwa. Watu wengine wote watakuwa chini wakisubiri harusi ifungwe angani. Wakishuka kutoka angani ndio magari ya bwana Masaga yatawatachukua watu, au sio jamani?"
"Sawa kabisa!" watu wote waliitikia huku wakipiga makofi, hawakuwa na habari yoyote juu ya VVU alivyokuwa navyo Mike!
Ilipofika zamu ya Samson, alisimama lakini alimwangalia Mike, alijisikia kushtakiwa sana ndani ya nafsi yake, aliona kutoa kwake mchango ilikuwa ni sawa na kuchangia kifo cha shemejiye Beatrice. Alijikuta yupo njia panda, upande mmoja wa akili yake ulimwambia, "Usichange." Alishindwa afanye nini.
"Bwana Samson tunakusikiliza bwana, nyie ndio wazee wa mji huu," Mwenyekiti wa kikao alichombeza.
Mike alijua kilichokuwa kikiendelea akilini mwa Samson, hofu kubwa ikamwingia kuwa huenda siri yake ingefichuka! Machozi yakaanza kumtoka, Mwenyekiti alipigwa na butwaa, akaamua aulize.
"Mike vipi tena mbona unalia?"
"Machozi yanatoka yenyewe tu Mwenyekiti, sijui nataka kuugua mafua nini?" Alijibu.
Baada ya ukimya wa kama dakika mbili, Samson alijikuta akisema:
"Mimi nitagharimia usafiri, chakula na malazi ya wageni kipindi chote cha harusi."
Hivyo ndivyo hali ya michango ilivyoendelea mjini Mwanza na huko Bukoba maelfu ya pesa yalikusanywa kwa ajili ya harusi ya Beatrice, hali iliyowafanya watu washindwe kuelewa ukubwa wa harusi hiyo ungekuwaje.
Pamoja na michango yote iliyochangwa bado Mike hakuwa na furaha moyoni mwake, hali iliyosababishwa na mazingira yenyewe ya ndoa yalivyokuwa. Kwa Mike ndoa ile ilikuwa ni kama kesi ya mauaji.
Mawazo kama hayo pia yalikuwa kichwani mwa Maggie na Samson, watu hawa wawili walijihisi kushirikishwa katika mauaji bila wao kutaka. Tofauti na wenzake, Beatrice alikuwa na furaha isiyo kifani. Alifurahia kufunga ndoa baada ya kusubiri kwa miaka kumi na mitano!
Mpaka wakati huo, bado Beatrice aliendelea kuamini kuwa yaliyotaka kufanyika yalikuwa njama ya kuzuia ndoa yake. Hakuwa tayari kuamini kuwa ni kweli Mike aligundulika kuwa na virusi vya UKIMWI, aligawa kadi karibu kwa kila rafiki yake katika hospitali ya Bugando ambako habari za Beatrice kutaka kujinyonga zilikuwa hazijafika na ziliendelea kufanywa siri. Watu wachache waliosikia na kumuuliza aliwatakalia na ili kuthibitisha kuwa ule wote ulikuwa uvumi, aliwapa kadi.
Karibu kila mtu mjini Mwanza alikaa mkao wa kula, akiisubiri ndoa ya Beatrice na Mike, kutokana na ukweli kwamba ndoa hiyo ilikuwa ni ya mtu maarufu sana, na habari zake zilisambaa karibu kila kona. Kutokana na mapenzi yao kwa Mike, wafanyakazi wa kiwanda cha Mwatex walikubali kwa hiari yao kukatwa shilingi 20,000 kila mmoja katika mishahara yao kuchangia harusi hiyo.
Hilo lilikuwa tukio la kwanza katika historia ya kiwanda hicho.
Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 11

Wiki tatu kabla ya harusi, shilingi milioni tano na laki sita zilikuwa zimekwishachangwa huko Bukoba kufanikisha ndoa ya Beatrice. Wazazi wa Kihaya hawakutaka kabisa kushindwa kitu na wazazi wa Kisukuma. Yalikuwa ni kama mashindano ya makabila mawili maarufu.
Ili kuifanikisha ndoa hiyo, Mzee Rugakingira aliamua sherehe ya kumuaga binti yake ifanyike mjini Mwanza eneo la Capri Point, kwa binti yake mkubwa, Maggie. Hivyo ndugu wote kutoka Bukoba walitakiwa kuwa Mwanza wiki moja kabla ya harusi.
Wakati mipango hiyo ikiendelea, Mike na Beatrice waliendelea na kazi zao kama kawaida. Pamoja na kuwa harusi ilikaribia, watu wengi waliomwona Mike walishangaa kwa kuwa hakuonekana kama ni mtu aliyekuwa na harusi karibuni. Alikuwa na huzuni mno na muda mwingi akiwa ofisini aliinamisha kichwa mezani kwake na kulala, jambo ambalo lilimshtua pia sekretari wake.
“Samahani bosi, naomba leo nikuulize,” Monica alisema.
“Uliza tu, nakusikiliza,” alimjibu.
“Nakuona siku hizi huna furaha kuliko hata kabla ya mipango yako ya kupata jiko, vipi bosi wangu unaumwa?”
“Hapana, siumwi kitu ila mipango ya harusi inanipeleka puta kidogo.”
“Puta vipi bosi, wakati watu tumejitolea kukatwa hata mishahara yetu?” Monica alitania.
“Basi tu, lakini ndio hivyo,” Mike alificha lakini ukweli wa mambo ulibaki palepale. Suala la ‘mauaji’ ya Beatrice bado liliendelea kumsumbua kichwani.
“Alijua kabisa yeye na Beatrice wasingeweza kutumia kondomu siku zote. Ungefika wakati fulani wangeshindwa kuendelea na hatimaye, Beatrice naye angeambukizwa, kitu ambacho hakutaka kitokee.
“Beatrice mpenzi, kweli nimeamua tuoane lakini kuna kitu kimoja hajanijibu vizuri. Unakumbuka siku ile niliongea na wewe juu ya matumizi ya kondomu, lakini hukunijibu, naomba leo nikuulize tena swali hilo bibie.”
“Hilo lisikutie wasiwasi, tutaangalia tu mume wangu,” Beatrice alijibu.
“Tutaangalia vipi tena Beatrice? Hilo ni lazima nilifahamu, vinginevyo nitabadili mawazo kama kujiua ujiue!”
“Ah! Ah! Ah! Yamefikia vipi huko tena? Basi tutatumia kondomu Mike, usiwe na wasiwasi.”
“Hapo sawa basi usiku mwema mpenzi.”
***
Wiki moja kabla ya harusi, hoteli zote maarufu mjini Mwanza zilijaa wageni waliokuja kuhudhuria harusi ya kifahari katika historia ya mji wa Mwanza na Tanzania nzima. Hata hivyo, Mike aliwaona wageni hao kama watu waliokuja kuhalalisha mauaji.
Miongoni mwa wageni waliofika mjini Mwanza alikuwa ni Edmund Edgar, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Oxford alichosoma Mike huko Uingereza.
Wakati Mike akisoma, Chancellor Edmund alitokea kumpenda sana kutokana na uwezo wake darasani uliowashinda Wazungu kiasi cha kubandikwa jina la “Machine.” Wakati Mike anaondoka Uingereza, alimjulisha Edmund tarehe ya kufunga ndoa yake.
Mzungu huyo alikuwa mjini Mwanza kama mmoja wa mashahidi. Mchango pekee wa Chancellor kwa Mike ulikuwa ni suti nzuri ya kumeremeta ya bwana harusi na shela ya bibi harusi alivyovinunua Uingereza.
Ilikuwa ni suti nzuri sana. Kila aliyeiona hakusita kusema ukweli wake kuwa ilishonwa kistadi. Shela ya bibi harusi mtarajiwa Beatrice pia ilikuwa nzuri mno kwani ilikuwa ni ya rangi nyeupe na nyuma ilikuwa na vitu kama manyoya marefu ya tausi. Kutokana na urefu wake, ilihitaji watu kuinyanyua kwa nyuma siku ya harusi wakati bibi harusi anatembea.
“I wanted you to look attractive on your wedding day! (NIlitaka uvutie sana siku ya harusi yako).
“Thank you, Chancellor.” (Asante Mkuu).
“Mike you know what?” (Unajua, Mike…?)
“No! (Hapana, sijui).
“A day before my wedding I looked very happy and smiled all the time! But it is different with you. You look so sad and shrunk. What’s the matter, son? Something troubling you?” (Siku moja kabla ya ndoa yangu nilikuwa mwenye furaha, nikitabasamu muda wote lakini wewe unaonekana ni mwenye huzuni, kuna tatizo lolote mwanangu?”) Aliuliza Chancellor baada ya kuhisi kitu.
Haikuwa rahisi kuificha huzuni aliyokuwa nayo Mike. Alijitahidi sana lakini haikuwezekana.
“No, I’m just fine, Chancellor.” (Hapana sina tatizo kabisa Mkuu).
Chancellor Edmund alikutana na wazazi na ndugu wengine wa Mike lakini hakubahatika kukutana na Beatrice wala wazazi wake.
“How is she? I guess she is beautiful, isn’t she?” (Nafikiri msichana wako ni mzuri ,au siyo?)
“Probably, you will see her on the wedding day.” (Bila shaka, utamwona siku ya harusi).
“I’m anxiously waiting! (Nasubiri kwa hamu kumwona).
***
Siku zilijivuta taratibu na hatimaye siku ya Alhamisi, Septemba 20, iliwadia. Mamia ya watu walikusanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Mwanza ili kumshuhudia Beatrice akiagwa na wazazi na ndugu zake. Ilikuwa ni sherehe ambayo wengi huiita “Send Off Party” au karamu ya kumwaga mwali.
Siku hiyo Beatrice alionekana mwenye furaha kupita kiasi. Kitu cha kushangaza siku hiyo hata Mike alionekana mwenye furaha kubwa kupita kiasi. Watu walikula, wakanywa na kusaza.
Kabla Mzee Rugakingira hajanyanyuka kitini kutoa nasaha zake za mwisho kwa binti yake, watu mbalimbali walitoa hotuba zao kumuasa Beatrice juu ya maisha ya ndoa.
“Sasa tumkaribishe mzee Rugakingira awape machache vijana wetu hawa, unajua tena wazee wetu waliotutangulia kuliona jua!” Mshereheshaji wa siku hiyo, Henjewele, kutoka Dar es Salaam, ambaye ni maarufu nchini Tanzania,” alisema.
Mzee Rugakingira alijikongoja na kukikamata kipaza sauti. “Binafsi sina mengi sana ya kusema kwani mengi yamekwishasemwa na walionitangulia. Ila ninalotaka kumwambia mkwe wangu ni kuwa nimempa mke, tena ni mke kwelikweli!
“Beatrice mwanangu, kwa ulinzi niliokuwa nao na maadili mema niliyomjaza, nina hakika hakumjua mwanamume. Hivyo, ninategemea hata baba naye atakuwa mtulivu katika ndoa maana siku hizi kuna huu ugonjwa mnaouita sijui nini vile?”
Watu wote wakitikia: “UKIMWI!”
“Na si mkwe peke yake, hata binti yangu naye atulie asimletee baba gonjwa hilo hatari.”
Mzee Rugakingira alilitamka neno UKIMWI bila kujua pale hakupakuwa mahali pake, kwani likayeyusha furaha yote aliyokuwanayo Mike na kumrudisha kinyumenyume mpaka akaukumbuka uuaji aliokuwa akilazimishwa kuufanya. Palepale alijiinamia, machozi yakaanza kumtiririka usoni mwake.
Magie na Samson nao waliposikia neno hilo UKIMWI likitajwa, liliwafanya wajisikie vibaya na wote walitoka ukumbini na kuzunguka nyuma ya jengo ambako Maggie aliendelea kulia na Samson akimbembeleza.
“Yaani mdogo wangu anakufa hivihivi naona mie?” Maggie alisema.
“Sasa utafanya nini mke wangu? Kuna mambo huwezi kuyazuia, ili mradi yeye mwenyewe kaamua na tulitaka kumsaidia akataka kujinyonga basi, hakuna la kufanya,” Samson alisema.
Ndani ya ukumbi sauti ya mzee Rugakingira iliendelea kusikika.
“Bahati nzuri sana watoto wangu hawa wamepima na kukutwa wapo swafii kabisa! Hivyo nawaomba vijana wengi ambao hamjaoa muige mfano wa wenzenu hawa maana hili gonjwa siku hizi ni hatari mno, “ mzee Rugakingira alimalizia bila kujua kilichokuwa kikiendelea mioyoni mwa Maggie, Samson, Beatrice na Mike.
***
Siku ya siku ilifika, mamia ya watu walifurika katika ukumbi wa Gandhi Hall mjini Mwanza ambako ndiko msafara wa magari kuelekea uwanja wa ndege ulipangwa kuanzia. Huko ndiko ambako harusi ilipangwa kufungwa angani.
Kila mtu uwanjani pale alipewa maputo na kitambaa kidogo cheupe kilichoandikwa Mike to Beatrice. Maputo hayo yalitakiwa kuachiwa ili yapasuke huku vitambaa vikipeperushwa angani kama ishara ya kuitakia mema harusi ya Mike na Beatrice.
Kamati ya harusi ilifanya mambo kama yalivyopangwa. Ndege ya Precision Air iliyokodiwa rasmi kwa ajili ya harusi hiyo ilikuwa uwanjani ikiwasubiri watarajiwa wawasili. Padri na wanakwaya kumi na watano wa kanisa la Roman Catholic la Bugando, nao walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakisubiri msafara uanze.
***
Saa 3.15 asubuhi gari aina ya Benz likiwa limepambwa vizuri, liliegeshwa upande wa kulia wa jengo la Gandhi Hall. Mtu mmoja alionekana kuteremka kutoka mlango wa mbele na kufungua mlango wa nyuma. Mike aliteremka akiwa amevaa suti aliyoletewa na Chancellor Edmund. Kila mtu alionyesha kushangazwa na mng’aro wa suti ile.
Baada ya mlango wa Mike kufunguliwa, mfungua mlango alizunguka upande wa pili wa gari akafungua tena mlango wa nyuma. Kiatu cheusi kilichong’arishwa vizuri kilikanyaga ardhi. Watu wengi walibaki kuangalia ni nani angeshuka, na muda mfupi baadaye, Chancellor Edmund alichomoza kutoka garini.
“Ee bwana eehe! Mpambe wa mshikaji ni Mzungu, hii ni kali!” Kijana aliyekuwapo katikati ya kundi la watu alisema.
Baada ya kupokwa waliingizwa katika chumba maalumu kwa ajili ya kusubiri kuanza kwa msafara. Dakika chache baadaye gari jingine la aina ya Benz liliegeshwa upande wa pili wa jengo.
Mtu aliyewekwa tayari kufungua milango alifanya kazi yake. Kiatu cheupe kikakanyaga chini na baadaye Beatrice alitokeza. Watu wote walijikuta wakishangilia kwa jinsi Beatrice na shela yake alivyopendeza!
Upande wa pili aliteremka msichana mwingine ambaye alionekana kuwa mgeni machoni mwa watu wengi. Alikuwa ni msichana mzuri mwenye urefu sawa kabisa na Beatrice. Kwa hakika walifanana sana. Huyo ndiye aliyetegemewa kuwa mpambe wa Beatrice.
Baada ya kupokewa nao waliingizwa katika chumba maalumu. Tofauti na Mike, hawa hawakutakiwa kukaa pamoja mpaka ndani ya ndege.
Saa nne kamili ulianza msafara kuelekea uwanja wa ndege. Beatrice na mpambe wake walitumia gari walilokuja nalo na Mike na Chancellor Edmund lao. Mabasi yote ya Mwatex yaliyowachukua wafanyakazi yalikuwa miongoni mwa msafara huo. Magari ya Mike, marafiki zake na mabasi ya kukodi yalizidi kuupamba msafara huo. Kwa pamoja magari yalikadiriwa kufikia 150.
Watu waliimba na kuishangilia ndoa ya Beatrice na Mike. Wazazi wa pande zote mbili, ndugu na marafiki walishangilia kupita kiasi bila kujua kilichokuwa akilini mwa Mike, Beatrice, Maggie na Samson.
Mike hakuwa na raha hata kidogo na mara nyingi kila alipokumbuka alichokuwa akilazimishwa kufanya, machozi yalimtoka. Mpambe wake Chancellor Edmund alizidi kuhisi kuwepo tatizo.
“Mike, are you forced into this marriage? (Mike umelazimishwa kuoa?).
“No, Chancellor.” (Hapana Mkuu).
“Why are you crying then?” (Sasa kwa nini unalia?).
“It’s a long story, I will tell you when the time is right.” (Ni habari ndefu sana, nitakuambia muda utakapofika).
“Tell me now!” (Niambie sasa hivi).
Wakati Chancellor anamalizia kusema maneno hayo, gari lao lilikuwa likiegeshwa mbele ya Uwanja wa ndege wa Mwanza. Magari mengi ilibidi yazuiwe kuingia uwanjani kwani hapakuwa na nafasi ya kutosha kuegesha magari yote hayo.
Padri Nicodemus na wanakwaya waliongozwa hadi kwenye ndege. Padri aliomba apewe kama dakika tano ili aingie ndani ya ndege yeye na watumishi ili aitakase ndege hiyo ifae kufungisha ndoa.
Muda huo Mike na Chancellor Edmund walikuwa katika chumba cha kusubiri ambapo Beatrice, mpambe wake na ndugu wengine walikuwa ndani ya gari lao wakisubiri kuitwa.
Edmund alikuwa hajasahau wasiwasi wake.
“Please Mike can I know what is making you sad? (Tafadhali Mike naweza kujua kinachokusikitisha?).
Kabla Mike hajajibu swali hilo saa ya ukutani iligonga saa 4:30 asubuhi na msichana mmoja mrembo aliingia chumbani humo.
“Naomba Mike na Chancellor wanifuate kuelekea kwenye ndege tafadhali,” msichana huyo alisema.
Je nini kitaendelea?
Je harusi itafungwa?
 
SEHEMU YA 12


Mzee Simba ambaye alikuwa mtaalamu wa maabara alikuwa katika mjadala mkubwa na Dkt. Mgonelwa, mtaalamu wa wadudu au ‘pathologist’ ndani ya chumba cha maabara.
“Jambo hili linanisumbua sana akili yangu, kwa kweli nashindwa kuvumilia, namwonea huruma sana msichana huyu kwani inavyoonekana hajui kuwa bwana anayemuoa ana virusi!
Inawezekana baada ya kumpa majibu Mike hakumwonyesha na leo hii ameamua kumwoa ili amuambukize UKIMWI kwa makusudi. Haiwezekani ni lazima nimuokoe yule msichana!” alijikuta akimpigia kelele Dkt. Mgonelwa.
“Sasa utafanyaje?” Dkt. Mgonela alimuuliza.
“Nasikia ndoa inafungwa uwanja wa ndege leo! Nitawahi kuizuia, wacha nikimbie hukohuko uwanjani, litakalokuwa na liwe lakini lazima niseme siri hii, huyu binti hawezi kufa hivihivi huku naona!”
Baada ya kusema hayo mzee Simba alifungua faili, akachukua nakala za majibu ya Mike na Beatrice akamuaga Dkt. Mgonela na kuanza kutembea kwenda nje ya ofisi.
“Vyeti hivi ndivyo vitaonyesha ukweli, yule kijana ni muuaji kabisa haiwezekani,” mzee Simba aliwaza akiingia ndani ya gari lake na kuanza kuliendesha kwa kasi kuelekea uwanja wa ndege.
Alikuwa amepania kumwokoa Beatrice kutoka mikononi mwa kifo. Hivyo ndivyo alivyoamini.
***
Laila alikuwa katika hali mbaya ya kufa kutokana na kuugua kifua kikuu na majipu kwa muda mrefu. Ndugu zake wote waliamini alikuwa na UKIMWI na walikwishakata tamaa juu ya maisha yake, walichokuwa wakisubiri wakati ule ni kifo chake tu.
Laila alikuwa amekonda mno na nywele zake kichwani zilikuwa zimekwisha kabisa. Alikuwa na vidonda karibu sehemu zote za mwili wake, na pamoja na kuwa mgonjwa taabani, alisikitishwa na kitu kimoja tu, nacho ni Mike! Alijua kwa vyovyote damu aliyomwongezea kule Copenhagen ilikuwa na virusi vya UKIMWI.
Alijilaumu lakini moyoni alitambua kwamba hakufanya makusudi. Kosa lililojitokeza ni kutokuwepo kwa utaratibu wa kupima damu kabla ya mtu kuongezewa. Aliamini kama utaratibu huo ungekuwepo, asingemwongezea.
Aliyawaza hayo yote akiwa nyuma ya kompyuta yake akisoma habari kwenye mtandao wa intaneti. Ghafla alishangaa kusoma habari juu ya harusi ya aina yake iliyokuwa mbioni kufungwa mjini Mwanza, Kaskazini mwa Tanzania, Afrika ya Mashariki.
“An incredible wedding in the history of Africa is to be held in Mwanza, one of the Northern towns in Tanzania, East Africa,” ilisema habari hiyo ikimaanisha ndoa ya kuvutia ilikuwa inafungwa nchini Tanzania katika mji wa Mwanza ulioko Kaskazini mwa nchi hiyo.
Alipofuatilia zaidi habari hiyo iliendelea kusema: “The bride will be Beatrice Rugakingira and the bridegroom will be Mike Martin.” (Bibi harusi atakuwa Beatrice Rugakingira na bwana harusi atakuwa Mike Martin).
Laila alishtuka ghafla alipoliona jina la Mike, aligundua ndiye aliyemwongezea damu kule Copenhagen.
“Mike anaoaje huku akijua ana virusi vya UKIMWIau hajui kama mimi ni mgonjwa taabani? Mike anaua kiumbe kisicho na hatia, ni lazima nisaidie. Si ajabu hajui kuwa damu niliyomuongezea ilikuwa na matatizo!” Alijisemea Laila.
Pamoja na hali yake mbaya, Laila alifikia uamuzi wa kusafiri hadi Mwanza akiwa na lengo moja tu; kumjulisha Mike ukweli wa mambo na kumsihi avunje harusi.
“Masikini sijui watakuwa wamekwishakutana kimwili na binti yule!
Sina uhakika lakini ni lazima niende tu Tanzania, nikifika Mwanza nikimuulizia ni lazima nitampata tu!” Laila alijipa moyo.
Alijua wazazi wake wasingemruhusu kwa sababu ya hali aliyokuwa nayo lakini siku iliyofuata alitoroka na kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kuwasili Dar es Salaam majira ya jioni akiwa hoi bin taabani, mwili wote ulikuwa ukiuma.
Kwa kuwa hakukuwa na usafiri wa ndege kwenda Mwanza jioni hiyo alilala Dar es Salaam, na siku iliyofuata alipanda ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania kwenda Mwanza.
Ndege hiyo ilitazamiwa itue Mwanza saa tatu asubuhi. Hivyo Laila alijua angeweza kuwahi kabla ndoa ya Mike iliyotegemewa kufungwa saa 4:30 asubuhi.
Mwaka wa hasara ni hasara tu. Ndege ya ATC aliyopanda Laila ilipata hitilafu ikiwa angani na kuanza kuvujisha mafuta. Tatizo hilo lililazimisha ndege hiyo kutua kwa dharura katika Uwanja wa ndege wa Kilimanjaro ambako ilifanyiwa matengenezo yaliyochukua saa nzima. Baadaye iliruka na kutua Mwanza saa nne na dakika ishirini zikiwa zimesalia dakika kumi tu kabla ya kufungwa ndoa.
Alipotua tu uwanjani hapo Laila alijikongoja taratibu hadi nje ya uwanja. Alishangaa kuona watu wengi na magari uwanjani hapo, mengi ya magari yakiwa yameandikwa “Mike to Beatrice!” Laila akahisi kitu.
Alimsogelea mtu mmoja na kumuuliza kama alimfahamu Mike Martin. Mtu yule alimjibu kuwa Mike aliyekuwa akimtafuta ndiye alikuwa akifunga ndoa uwanjani pale.
“How can I see him? I have something urgent to tell him.” (Nitamwonaje? Nina kitu cha haraka cha kumweleza).
“Labda uingie ndani ya uwanja uombe wakupeleke kwenye ndege uongee naye,” alisema kijana huyo huku akimwangalia Laila kwa mshangao, afya yake ilikuwa mbaya mno.
Wakati wakiendelea kuongea, ghafla alifika mtu mwingine akikimbia. Hakuchelewa, alijitambulisha.
“Jamani mimi naitwa mzee Simba kutoka maabara ya Bugando, nataka kumwona ama Beatrice au baba yake, sijui mtanisaidiaje?” Aliuliza.
“Hata huyu dada anataka kuonana na Mike hebu njooni huku ndani niwapeleke.”
Wote kwa pamoja walimfuata yule kijana hadi ndani kabisa ya uwanja.
“Kimbieni ndege inataka kuruka,” aliwaambia.
Wote walijitahidi kukimbia ingawa Laila alishindwa kufanya hivyo kutokana na udhaifu wa afya yake. Kabla hawajaifikia ndege walishuhudia mlango ukifungwa na ndege taratibu iliacha ardhi kwenda angani ambako ndoa ingefungwa. Walikuwa wamechelewa, Laila alimwaga machozi.
“Mimi nawasubiri wakishuka tu nataka niongee na baba yake,” mzee Simba alisema huku akimgeukia yule mwanadada. “Vipi mbona unalia?” mzee Simba alimuuliza Laila kwa Kiingereza. Laila hakusita, alimsimulia mzee Simba kila kitu juu ya ugonjwa wake na jinsi alivyomwongezea Mike damu ambayo aliamini kabisa kwamba ilimsababishia Mike aambukizwe virusi vya UKIMWI.
“Mama yangu! Sasa kwa nini Mike anaoa wakati anajua kabisa yeye ni mgonjwa?” Aliuliza mzee Simba.
“Ndiyo maana nimesafiri kutoka Mogadishu mpaka hapa katika kujaribu kuizuia ndoa hii isifungwe!”
“Hata mimi niko hapa kwa lengo hilohilo, sababu ni mimi niliyempima Mike damu na kugundua ana virusi vya UKIMWI!”
“Kwa hiyo Mike anafahamu hali halisi?” Laila aliuliza.
“Ndiyo.”
“Sasa kwa nini anataka kuua?”
“Nafikiri msichana anayemwoa hajui, vinginevyo asingekubali,” mzee Simba alidakia.
“Nimekuja hapa na karatasi zote za majibu ili nimwonyeshe msichana anayeolewa au hata mzazi wake, ni heri nipewe lawama kuliko kushirki katika mauaji.”
“Sasa tutafanya nini?” Laila aliuliza.
“Hata mimi sielewi inaonekana kama tumechelewa.”
“Masikini Mike, anamuua mtoto wa watu bure!” Laila alisema katika hali ya kulaumu na kusikitika.
***
Si Beatrice, Mike, Maggie, Samson, Padri wala wanakwaya waliokuwepo ndani ya ndege waliojua kilichokuwa kikiendelea chini. Padri aliendelea kufungisha ndoa kama ilivyopangwa.
“Unakubali kumwoa Beatrice Rugakingira?”
Mike alikuwa kimya tu, ikabidi Padri arudie kwa mara ya pili na ya tatu lakini bado hakupewa jibu.
“Mike….,” Beatrice aliingilia kati.
“Mmmmmmh!” Mike aliguna, akawa kama mtu aliyezinduka usingizini.
“Unaulizwa swali. Umekuwaje?”
“Swali gani?”
Padri aliuliza tena.
“Ndiyo nakubali kumwo… kumwo…Beatr….” Mike alisema huku akilengwalengwa machozi.
Zamu ya Beatrice ilipowadia mambo yalikuwa safi, kila alichoulizwa kikawa “ndiyo nakubali!”, “ndiyo nakubali!” na ndoa ikafungwa angani.
Wazazi, ndugu, marafiki na mawaziri watano wa wizara mbalimbali walikuwa ndani ya ndege kushuhudia tukio lile la kihistoria. Hata hivyo, kwa Maggie na Samson mambo yalikuwa huzuni kubwa sana kushuhudia ndoa ile. Bado walijisikia kushtakiwa ndani ya nafsi zao. Wakati wote ndoa ikifungwa walishindwa hata kugonganisha macho kabisa.
***
Dakika 30 baadaye, ndege ilipokuwa ikishuka, huko ardhini watu walikuwa wamechanganyikiwa kwa furaha ya kushuhudia harusi ya aina yake, mikono ilikuwa angani ikipeperusha vitambaa vyeupe vilivyoandikwa “Mike to Beatrice!” Laila na mzee Simba walikuwa wakisubiri kwa hamu ndege itue ili wakamilishe kazi yao.
“Can we go and sit somewhere? Coz I fee dizzy!” (Je, tunaweza kwenda kukaa sehemu? Najisikia kizunguzungu) Laila alimwambia Mzee Simba.
“Wait, the plane will land in no minute.” (Subiri ndege itatua muda si mrefu).
Dakika tatu baadaye ndege ilitua ardhini na milango ikafunguliwa. Padri ndiye alikuwa wa kwanza kuikanyaga ardhi akifuatiwa na wanakwaya. Baadaye walifuata watu wengine, halafu kukawa na ukimya kwa muda.
“Bwana na bibi harusi pamoja na wapambe wao ndio wanajiandaa kutoka ndani ya ndege jamani! Nawaomba sana muwe watulivu na gari lao la kuvutwa na farasi naomba lisogezwe hapa karibu kabisa ya ndege ili wasije wakachafua viatu vyao vya thamani kwa kutembea umbali mrefu kwenda kwenye gari. Pia nawaomba watakapoteremka kila mtu ashangilie, au sio jamani?” Ilikuwa ni sauti ya MC Henjewele.
Gari zuri lenye rangi nyeupe likivutwa na farasi weupe wenye manyoya marefu, lilisogezwa karibu kabisa na mlango wa ndege.
“I can’t go on standing like this, I fee like fainting,” (Siwezi kuendelea kusimama, najisikia kuzimia) Laila alimwambia mzee Simba.
“Be strong, let’s move forward!” (Kuwa imara, haya twende) mzee Simba akiwa na vyeti mkononi alisema huku akimvuta Laila mkono kuelekea kwenye mlango wa ndege ambako tayari Mike na Beatrice walikuwa wakiteremka ngazi.
Huku miguu yake ikiishiwa nguvu, Laila alijikongoja mpaka karibu kabisa na gari la kuvutwa na farasi. Yeye na mzee Simba walisimama pale kumsubiri Mike! Pamoja na kujua kuwa ndoa ilikwishafungwa bado waliona wanayo nafasi ya kuokoa maisha ya Beatrice kama yeye na Mike walikuwa hawajakutana kimwili.
Saa sita mchana ilipotimu Mike na Beatrice walitembea wakiwa wameshikana mikono kuelekea kwenye gari lao. Nyuma yao aliyekuwepo Chancellor Edmund na mpambe wa Beatrice, ambaye watu wengi uwanjani pale hawakumfahamu.
Kila mtu alikuwa na furaha. Wasukuma waliimba Kisukuma: “Kubyala ng’wana nkima kwilolela banhu kaganda kaganda!....” Wahaya nao walisikika wakiimba: “Akanana, akanana kahile kona, kahile nikeogola….” Kwa kweli ilikuwa ni siku ya furaha mno, watu wakiimba na kushangilia bila kujua walikuwa wakishangilia mauti. Laiti wangekijua walichokuwa wakikishangilia, machozi yangewatoka maana walikuwa wakipigia vigelegele kifo.
Baada ya kupanda tu kwenye gari, na farasi kuanza kuondoka taratibu, Mike alisikia sauti ikiita nyuma yake.
“Miiiiiiikeeeeee!”
Kila mtu aliisikia sauti ile. Mike alipogeuka kuangalia ni nani alikuwa akimwita, alikutanisha macho na sura isiyo ngeni kabisa machoni pake. Alikuwa ni msichana aliyekonda sana na alionekana waziwazi kuwa ni mgonjwa! Mike alijaribu kuvuta kumbukumbu zake kutaka kujua msichana huyo alikuwa nani lakini kumbukumbu zake zilimtupa mkono, ilikuwa si rahisi kufahamu.
“Kuna msichana ameniita jina, sura yake si ngeni machoni pangu, sijui nilimwona wapi,” Mike alimweleza Beatrice.
“Kumbuka vizuri labda jina litakujia baadaye,” Beatrice alimjibu.
Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 13


Japokuwa Mike hakutaka kumuoa Beatrice kwa kuwa alikuwa na Ugonjwa wa UKIMWI, msichana huyo hakutaka kukubali, aliona ni bora kufa lakini si kuona Mike akiacha kumuoa.
Harusi inafungwa, moyo wa Beatrice unafarijika kwa kuona kwamba naye kwa sasa anaitwa mke wa Mike. Lakini kabla ya harusi hiyo kufungwa, msichana ambaye alimuongezea damu Mike anafika nchini TAnzania huku lengo lak likiwa ni kuhakikisha harusi hiyo haifungwi kwa kuwa alijua kwamba Mike alikuwa ameathirika kwa Ugonjwa wa UKIMWI.
Anachelewa, anakuta harusi imekwishafungwa, Mike na Beatrice wamekuwa mke na mume.
SONGA NAYO...
Mzee Simba alichanganyikiwa kiasi cha kutosha. Laila alikuwa amelala miguuni kwake kwani baada tu ya kuliita jina la Mike, alianguka chini na kupoteza fahamu. Watu walimzunguka mzee Simba na kuanza kumuuliza nini kilimpata nduguye maana kila mtu aliamini kuwa mzee Simba alikuja pale akiwa ameongozana na Laila.
Mzee Simba alipoinama kuusikiliza moyo wa Laila aligundua ulikuwa bado ukipiga. Akaomba msaada wa watu wamsaidie kumbeba Laila hadi kwenye gari lake ili amwahishe hospitali kuyaokoa maisha yake.
Baada ya kumpakia ndani ya gari, mzee Simba aliondoka kwa kasi ya ajabu kuelekea hospitali ya Bugando. Kutoka uwanja wa ndege hadi Bugando ni umbali wa kilometa sita. Alipomaliza kilometa moja mzee Simba alimwangalia Laila na kugundua kwamba moyo wake ulikuwa bado ukidunda kwa mbali, isipokuwa macho yake yalikuwa yamegeukia juu kama mtu mwenye kifafa.
“Nataka huyu msichana kutoka Somalia aliyemwongezea Mike damu apone ili maneno nitakayosema dhidi ya Mike yasionekane uongo,” Mzee Simba alijisemea huku akiendelea kuongeza kasi ya mwendo wa gari lake.
***
Wakiwa maeneo ya Pasiansi mawazo juu ya msichana aliyemwona uwanja wa ndege yalimreja tena Mike.
“Nasindwa kukumbuka vizuri, lakini namfahamu yule msichana!” Alisema kwa sauti.
“Yaani bado hujamkumbuka tu?”
“ Kwa kweli bado!”
Mike na Beatrice waliendele kuongea huku wakiwapungia mikono watu waliosimama pembeni mwa barabara kuishuhudia harusi hiyo.
***
Mzee Simba aliliamini gari lake kwa sababu ilikuwa haijapita hata wiki moja tu tangu alitoe gereji kulifanyia marekebisho madogomadogo. Hivyo, aliliendesha kwa kasi ya ajabu ili amwahishe Laila hospitali.
Gari lilipofika kwenye barabara ya Posta na Nyerere, bila kutegemea, basi moja la abiria lililokuwa likitokea Geita liliingia barabarani na sababu ya kasi aliyokuwanayo, mzee Simba hakuweza kufanikiwa kulikwepa na kujikuta gari lake likigongana uso kwa uso na basi lile.
Kwa bahati mbaya, mzee Simba hakufunga mkanda wa gari. Hivyo alirushwa nje kupitia kioo cha mbele. Kichwa chake kilijipigiza kwenye bodi la basi ambalo ubavuni liliandikwa maneno
“Lushange Bus Services!” Akadondoka chini na kufa palepale! Laila naye alipitia palepale na kutupwa kama mita ishirini kutoka eneo la ajali.
“Majeshi wabulaga! “ (Majeshi umeua!) konda alisikika akimwambia dereva wake kwa lugha ya Kisukuma. Dereva aliruka na kuanza kukimbia.
Watu walijaa eneo hilo na kuanza kutoa msaada. Dakika chache baadaye lilipita gari la kampuni la maji ya RIDEP, wakalisimamisha na kuwapakia mzee Simba na Laila na kwa haraka wakakimbizwa hospitali ya Bugando.
Walipokewa mapokezi na daktari alipowapima aligundua tayari wote walishafariki dunia! Walikufa na siri zao moyoni.
Vibaka waliokuwa eneo la tukio walifanya kazi zao sawasawa, walifanikiwa kumpekua mzee Simba na kuchomoa pesa na karatasi alizokuwa nazo, zikiwemo zenye majibu ya Mike. Vibaka haohao walishindwa kumpekua Laila kwa jinsi alivyoonekana kukonda, waliamini hakuwa na kitu!
Baadaye alipopekuliwa alikutwa na kijitabu kidogo kilichoandikwa anwani na namba za simu za watu mbalimbali, pamoja na pasipoti yake ya kusafiria. Ni pasipoti yake iliyomtambulisha kuwa hakuwa raia wa Tanzania.
Viza ilikuwa imepigwa muhuri kama siku mbili kabla ya kifo chake na kuonyesha kuwa alitokea Mogadishu, Somalia. Kwa uamuzi wa haraka ilifahamika kuwa Laila hakuwa na ndugu kabisa mjini Mwanza.
Watu walishindwa kuelewa Laila alikuja Tanzania kufanya nini. Ndani ya Ukumbi wa Kipepeo katika Hoteli ya New Mwanza, watu walikuwa wengi mno wakila na kunywa.
Kreti za bia zilizokuwepo zilitaka kuzidi idadi ya watu.
Nyama za kuku, mbuzi, ng’ombe zilikuwa nyingi mno na watu waliruhusiwa kuchukua chochote baada ya sherehe hiyo. Ilikuwa ni harusi ya kwanza ya aina hiyo kufanyika mjini Mwanza. Hata wakazi wa Mwanza wenyewe walikiri hivyo.
Saa tano na nusu ya usiku Mike na Beatrice waliondoka ukumbini kuelekea Hoteli ya Continental ambako walipanga chumba kwa ajili ya kulala siku hiyo, ili siku ya pili wapande ndege kwenda Dar es Salaam kula fungate lao katika Hoteli ya Sheraton kwa muda wa mwezi mmoja, gharama zote zikilipwa na Kepha Masaga, rafiki yake Mike.
***
Asubuhi na mapema, Mike alizinduliwa na kipindi cha “Majira” cha Redio Tanzania Dar es Salaam - RTD, kilichokuwa hewani.
“Harusi yaiingia doa. Harusi ya aina yake iliyofungwa jana mjini Mwanza iliingia dosari pale mmoja wa wageni waalikwa kutoka Mogadishu, Somalia, aliyejulikana kwa jina la Laila Mahate Mohamed na mzee Simba, mfanyakazi wa maabara ya hospitali ya Bugando, walipofariki katika ajali mbaya ya gari baada ya gari walilokuwemo kugongana uso kwa uso na basi lilikokuwa likiingia mjini Mwanza kutoka Geita!”
Mike alisikia tangazo hilo kwa mbali akashtuka kutoka usingizini!
Baadaye mtangazaji aliendelea: “Ajali hiyo ilitokea katika makutano ya barabara za Posta na Nyerere na inadaiwa mzee Simba ambaye pia alikuwa mwalikwa katika harusi hiyo, alikuwa akimkimbiza Laila hospitalini baada ya kuzimia akiwa uwanja wa ndege.
Mwili wa Laila ulipopekuliwa ulikuwa na pasipoti iliyoonyesha kwamba Laila ni raia wa Somalia. Marehemu Simba alipopekuliwa alikutwa na karatasi mbili za majibu ya hospitali ambazo bado zinafanyiwa uchunguzi.”
Taarifa hizo zilimshtua sana Mike akaanza kumwamsha Beatrice aliyekuwa amelala pembeni yake.
“Beatrice!”
“Naam, mume wangu!”
“Nimesikia taarifa mbaya sana redioni.”
“Taarifa gani tena!?”
“Nimemkumbuka yule dada niliyemwona uwanjani.”
“Ni nani?”
“Anaitwa Laila Mahate ndiye aliyeniongezea damu kule Copenhagen!”
“Sasa yuko wapi?”
“Yeye na mzee Simba wa maabara ya Bugando wamepata ajali na wamefariki dunia!”
“Ni nini?”
“Hivyo ndivyo ninavyokuambia.”
“Na yule msichana alikuja lini Mwanza?”
“Kwa kweli hata mimi sijui.”
Baaadaye Mike alishikwa na huzuni, akaanza kulia na Beatrice akawa anambembeleza.
Saa moja asubuhi gari lilikuja hotelini kuwachukua maharusi na kuwapeleka uwanja wa ndege ambako walipanda ndege kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya fungate lao.
Pamoja na kuwa ni Laila aliyemwambukiza virusi, bado Mike alitamani kuahirisha safari ili ajue mwisho wa msichana huyo lakini ilishindikana kufanya hivyo kwa sababu ratiba tayari ilikwishapangwa.
***
Marehemu mzee Simba alizikwa siku hiyohiyo lakini mwili wa Laila ulikaa chumba cha maiti kwa siku tatu zaidi wakisubiri ndugu zake toka Somalia. Ndugu hao walipelekewa taarifa kwa njia ya simu kupitia namba zilizokutwa ndani ya kitabu alichokuwa nacho kabla ya kukutana na kifo chake.
Siku ya nne ilibidi maiti yake izikwe na Halmashauri ya Mji wa Mwanza kwa sababu ilikuwa imekwishaharibika mno na isingewezekana kusubiri zaidi. Mike aliyasoma mambo yote hayo katika magazeti akiwa Dar es Salaam na yalimsikitisha sana.
***
Mwezi mmoja baadaye fungate lilikwisha. Mike na Beatrice wakarejea Mwanza kuendelea na maisha yao kama mke na mume. Kwa Beatrice ilikuwa furaha kubwa lakini ndani ya kichwa cha Mike suala hilo liliendelea kumsumbua hasa alipoanza kusikia uvumi miongoni mwa watu juu ya karatasi za majibu alizokutwa nazo mzee Simba mfukoni.
Mike alimkumbuka Laila kila siku. Alishindwa kuamini kama kweli Laila aliyemjua kama msichana mrembo wa Kisomali ndiye ailyemwona Mwanza akiwa amekondeana na kubadilika sura kiasi cha kutokumtambua kirahisi.
Aliingiwa na hofu kubwa kuhusu mwisho wa maisha yake. Alianza kuuogopa UKIMWI. Alijua wazi kifo chake kingekuwa cha mateso makubwa. Kilichomuumiza zaidi ni kwamba alijua hakuwa na maisha marefu sana mbele yake!
Kila alipoufikiria mwisho wa maisha yake alijikuta akikosa raha na kulia.
Hata hivyo, yeye na Beatrice waliendelea na maisha kama walivyokubaliana kabla ya ndoa yao kwamba: Bila kondomu hakuna mapenzi. Jambo hili ndilo lililokuwa faraja kwa Mike maana alijua kwa kufanya hivyo asingemwambukiza Beatrice UKIMWI kabisa na angekufa peke yake bila dhambi ya kumuua mtu mwingine.
Mawazo yalipomzidi sana Mike aliamua kujiunga na kikundi cha watu waishio na virusi vya UKIMWI mjini. Wengi walikiita kikundi hicho kuwa ni cha Watu Waishio kwa Matumaini na Ukimwi (WAMAU).
Huko alipata faraja kubwa baada ya kukutana na watu wengine waliokuwa na tatizo kama lake. Alijifunza mengi sana kuhusu UKIMWI na kidogokidogo akajikuta ameizoea hali aliyokuwa nayo na kuwa mwenye furaha tena.
Alipofikia hatua hiyo, hakuona tena sababu ya kulificha jambo hilo wala hakulifanya siri. Aliacha wanaotaka kujua wajue.
Je nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 14


Mwaka mmoja baadaye Mike aliamua kuacha kazi na kujiingiza katiba biashara moja kwa moja. Wengi walimshangaa kwa uamuzi huo lakini kumbe Mungu alijua huko ndiko yalikokuwa mafanikio yake kwani mwaka mmoja tu baadaye biashara zake zilikuwa mara tatu zaidi.
Akafungua kiwanda cha mbao alichokiita Martin Timbers na kiwanda cha kusaga chakula cha kuku alichokiita Martin Millers.
Pia, alianza biashara ya kusafirisha mifugo kwenda Rwanda na Burundi. Biashara hiyo ilimpa pesa nyingi sana akaanzisha kampuni ya usafirishaji iliyoitwa Martin Transpoters Limited ambayo ilimiki malori karibu kumi na matela yake. Kazi ya malori hayo ilikuwa ni kusafirisha mizigo kwenda sehemu mbalimbali za Tanzania na hata nchi za nje.
Hayo yote yalitokea ndani ya miaka minne tu tangu aache kazi! Yalikuwa ni mafanikio makubwa mno kwa kijana mwenye umri kama wake na watu wengi walishangaa na kumwona kuwa na bahati ya aina yake kwa sababu kila alichokifanya kilifanikiwa.
Kazi zilipomzidi ilibidi amwachishe mkewe kazi. Akamwajiri katika kampuni yake kama Afisa Utawala wa Fedha na kwa ushirikiano huo walizidi kufanikiwa zaidi. Beatrice akawa anaendesha gari aina ya Benz, na mumewe akawa anaendesha BMW! Si hayo tu, walijenga nyumbani nyingi Mwanza na Dar es Salaam.
Hakuna mtu ambaye hakumjua Mike mkoani Mwanza. Watu wengi waliamini huenda ndiye aliyekuwa kijana tajiri kuliko wote Kanda ya Ziwa.
***
Miaka mitano ilikuwa imekwishapita na hakuna mmoja wao aliyeonyesha dalili yoyote ya UKIMWI. Ndipo siku moja walipokuwa kitandani Beatrice aliona kuna haja ya kujaribu kufanya mapenzi bila kutumia mpira.
"Mume wangu leo hii ni mwaka wa tano tupo katika ndoa na kila siku tunatumia mpira, hivi ni halali kweli? Au wewe unaona ni sawa tu?" Beatrice alimuuliza mumewe wakiwa wamelala chumbani.
Mike alishangaa sana kwani tangu mwanzo jambo hilo aliliweka wazi.
"Beatrice umeanza tena mambo hayo lakini si unajua mimi nina matatizo? Kwa nini usitulie mke wangu?"
"UKIMWI gani huo usioonyesha dalili? Leo mwaka wa tano. Huwezi kuelewa Mike kuwa si ajabu zile zilikuwa ni njama za watu ambao hawakutaka mimi na wewe tuoane? Kama tungefuata maneno yao si ajabu mimi tayari ningekwishakufa," Beatrice alisema kwa kusisitiza.
Mike alipagawa na ombi lile la ghafla la mkewe. Pamoja na kwamba hakuliafiki siku hiyo lakini Beatrice hakuacha, kila siku alirudia tena na tena, alitaka mchezo wa pekupeku.
Sijui kama alikuwa ni shetani au kitu gani, maneno yale yalimwingia Mike akajikuta ghafla akibadili msimamo wake!
"Lakini kweli mke wangu inawezekana marehemu mzee Simba alitumiwa na watu ili kuikwamisha ndoa yetu lakini mbona nilipopima tena Medical Research majibu yakawa hivyohivyo?" Mike alishikwa na kigugumizi.
"Achana na Medical Research Mike, sogea nikukumbatie."
Mike alisogea na tangu hapo waliweka mpira pembeni, wakaendelea hivyohivyo, kitu pekee walichofanya ni kufuata njia ya uzazi wa mpango ili wasipate mtoto.
Ulipotimu mwaka wa saba wa ndoa yao, Mike alianza kuhisi dalili za uchovu, kila asubuhi na akawa mvivu wa kwenda safari. Mwanzoni hali hiyo aliichukulia kama kitu cha kawaida lakini ilipoingiliwa na kikohozi kikavu na kutoka jasho usiku, kupoteza hamu ya chakula na homa kali zisizokoma, ndipo alipogundua kuwa kuna jambo ambalo halikuwa la kawaida mwilini mwake. Akaamua kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi.
Vipimo vilionyesha kuwa alikuwa na homa ya matumbo. Alipatiwa dawa aina ya Chlorophenical atumie nyumbani kwa muda wa siku kumi na nne lakini dawa hizo hazikumsaidia chochote.
Homa zilizidi kupanda kila siku, alipopimwa tena majibu yalionyesha bado alikuwa na homa kali ya matumbo. Akapewa dawa nyingine kali zaidi iitwayo Ciproflaxin aitumie kwa muda wa siku tano.
Dawa ile ilimpa nafuu kidogo lakini alipungua sana uzito na kikohozi kilikuwa bado kikiendelea kumsumbua. Ilimbidi apimwe tena na aligundulika kuwa na kifua kikuu.
Akaandikiwa sindano sitini za dawa ya Streptomycine. Mike akalazwa katika hospitali ya Sekou Toure ambapo alianza kuchomwa sindano sitini na alipewa vidonge vingine vya aina ya Thiazina avitumie.
Alitakiwa avitumie mwaka mzima.
Baada ya kukaa wodini kwa miezi miwili, Mike alimaliza sindano zote sitini na akaruhusiwa kurudi nyumbani ambako aliendelea na vidonge vya Thiazina. Hali yake ilikwishabadilika kabisa, ngozi ilikwishapauka na kitambi kiliporomoka, ikionyesha wazi alikuwa bado mgonjwa.
***
Kutokana na Mike kuwa kipenzi cha watu, habari za kuugua kwake zilitapakaa kila mahali mjini Mwanza. Watu walisikitishwa mno na habari hizo na wengine hawakuamini, kiasi kwamba kila Mike alipopita mtaani kila mtu alitaka kumwona. Wengine walimfuata kwa nyuma wakitaka kujua mtu mwenye UKIMWI alifanana vipi.
Watu walimwonea huruma sana, akina mama wengi walilia walipomwona Mike kutokana na hali aliyokuwa nayo.
"Pole mwanangu, Mungu atakusaidia," ndiyo maneno aliyokuwa akiambiwa kila siku alipokutana na akina mama.
Na kila mara Mike aliwajibu: "Asanteni sana, ninaendelea kupambana nao ila nanyi inabidi mjitahidi sana msiupate! Ugonjwa huu unatesa sana."
Mike akawa mtu wa kushinda ndani huku Beatrice akiendesha biashara zote.
***
"Beatrice unaona sasa yaliyotokea, nilikueleza mdogo wangu hukutaka kunisikia!" Maggie alimwambia Beatrice siku alipomtembelea ofisini kwake.
"Maggiiie huu si wakati wa kulaumiana, ni vizuri tukapeana moyo na kutiana nguvu, kumbuka Mike aliupata kwa mtu na mtu aliupata kwa mtu vilevile! Maggie siujuti hata kidogo uamuzi wangu wa kuolewa na Mike," Beatrice alisema huku akitabasamu.
Maggie alishangazwa sana na msimamo wa mdogo wake!
Siku zote Mike hakuacha kumlaumu mkewe kwa kitendo chake cha kumfanya muuaji.
"Unaona sasa mke wangu Beatrice, nilikuambia tusioane ukalazimisha. Matokeo yake na wewe utakufa! Najisikia vibaya sana kukuua Beatrice wakati kulikuwa na uwezekano wa wewe kuishi maisha marefu zaidi."
"Mike, unayakumbuka maneno niliyomwambia Maggie miaka saba iliyopita?" Beatrice alimkumbusha.
"Maneno gani mke wangu?"
"Kila roho itaonja mauti. Mimi sijutii uamuzi wangu wa kuolewa na wewe, ninakupenda, nitakuwa na wewe siku zote mpaka mwisho wa maisha yetu."
***
Wakati Mike akiwa katika hali ile ya kuugua Beatrice alisikia habari za dawa ya Kemron iliyogundulika huko Kenya iliyodaiwa kuwa na uwezo wa kuutibu ugonjwa huo wa UKIMWI, yeye na mume wake walisafiri hadi Nairobi kwa basi la Tawfiq na safari hiyo iliwachukua saa kumi na mbili, alifika salama ingawa alikuwa amechoka kupita kiasi.
***
Ilikuwa safari ndefu mno kwa Mike, ukizingatia afya yake ilivyokuwa imedhoofika. Akiwa njiani, Mike alikuwa akikohoa sana kiasi cha kuwafanya abiria wengine ndani ya basi hilo kuanza kumtilia shaka kuwa alikuwa na kifua kikuu na kuomba madirisha yote ya basi yafunguliwe ili kuepuka kuambukizwa! Kitendo hicho kilimuumiza moyo.
Walifika Nairobi saa kumi na mbili asubuhi na kwenda moja kwa moja kwenye kituo cha utafiti wa afya cha Kenya, Kenya Medical Research Insitute, walikokuwa wagunduzi wa dawa hiyo ya Kemron!
Kwa mwezi mzima, Mike alilazwa katika kituo hicho akitumia Kemron, dawa iliyoaminika kuwa na uwezo wa kutibu UKIMWI ingawa ilikuwa bado haijathibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kemron ilikuwa ni dawa yenye nguvu sana, ilimpa taabu sana Mike kuitumia na badala ya kumsaidia ilizidi kumdhoofisha afya yake. Ilidaiwa kwamba sambamba na kutibu UKIMWI, dawa hiyo ilikuwa pia na tabia ya kuua chembechembe nyeupe za damu, jambo lililosababisha hali ya wagonjwa wengi walioijaribu kuwa mbaya kuliko awali.
Hivyo, Mike pia akadhoofika na kupoteza nguvu nyingi, akawa anashinda amelala tu! Pamoja na kuzidi kupungua kwa kinga ya mwili kulikosababishwa na Kemron, Mike alipatwa na ugonjwa wa kuharisha.
Kuharisha huko ndiko kulimdhoofisha zaidi. Alipewa dawa mbalimbali za kufunga kuharisha lakini bado aliendelea kuharisha! Mara nyingi alipungukiwa maji ya mwili na kulazimu atundikiwe dripu za maji kila siku.
Hali hiyo ilimtia Beatrice wasiwasi mkubwa na kumfanya apoteze matumaini ya mume wake kupona.
***
"Beatrice mke wangu, kifo ni kitu cha kawaida kama ulivyowahi kumwambia dada yako Maggie kwamba, kila nafsi ni lazima itaonja mauti. Hata hivyo, kifo cha UKIMWI mke wangu kinatesa na kinaumiza zaidi hasa pale kinapomchukua kijana kama mimi ambaye ndio kwanza naanza kupata mafanikio katika maisha yangu kabla sijafaidi chochote!
“Nimesoma miaka yooote, leo hii ndoto zangu zinakatika ghafla. Kwa kweli, hili linaniuma sana," Mike alimwambia mkewe huku machozi yakimtoka.
"Siyo hivyo mume wangu, tutamwomba Mungu muujiza wa uponyaji utendeke."
"Inawezakana nikapona kweli Beatrice! Mbona ugonjwa huu hauna tiba? Nashauri kama imeshindikana mke wangu, kuliko niendelee kukusumbua, ni bora unirudishe nikafie nyumbani mikononi mwako na wazazi wangu," Mike alisema kwa sauti ya chini huku akilia.
"Hapana mume wangu, hatuhitaji kukata tamaa, ni lazima tutafute msaada mwingine haraka iwezekanavyo, nyumbani tutakwenda kufanya nini?"
"Lakini mke wangu, ni lazima ufahamu kuwa ni damu ya Laila inayoniua. Simlaumu Laila kwa sababu hakuwa na nia ya kuniua bali alifanya hivyo kwa lengo la kuyaokoa maisha yangu. Ninaamini hii yote ilikuwa mipango ya Mungu lakini ninaomba uamini sikuwahi kutembea na mwanamke mwingine maishani mwangu.
Wewe ni mwanamke wangu wa kwanza na wa mwisho; sitamjua mwanamke mwingine tena!" Mike alilalama.
"Ninakuamini mume wangu!" Beatrice alimjibu huku machozi yakimlengalenga. Maneno ya mume wake yalimuumiza sana.
"THE BIG NOVEMBER CRUSADE, NAIROBI INAWATELEA MKUTANO MKUBWA WA INJILI KATIKA VIWANJA VYA UHURU! WALETENI WAGONJWA WENYE MAGONJWA YALIYOSHINDIKANA WATAOMBEWA NA MTUMISHI WA MUNGU, ARON MAGABILO, KUTOKA TANZANIA. PIA WENYE SHIDA MBALIMBALI WATAOMBEWA" ilikuwa ni sauti ya kipaza sauti nje ya wodi ya Kenya Medical Research Insitute, ilimfikia Mike moja kwa moja, kitandani alipokuwa amelala.
"Mke wangu ni lazima unipeleke nikaombewe kwa sababu hizi dawa naona hazinisaidii lolote na inaonekana kupona kwa nguvu ya mwanadamu imeshindikana ni bora nirudishe matumaini yangu kwa Mungu."
"Nimefurahi sana kusikia jambo hilo na nitahakikisiha tunakwenda kwenye mkutano leo jioni. Lakini kabla hatujakwenda huko inatubidi kuwataarifu madaktari kuwa tunahama kutokana na Kemron yao kushindwa kukusaidia."
"Pia, mke wangu lazima ukumbuke kuwa mimi ninahitaji kutubu dhambi zangu kabla sijalala kaburini na hii ndio nafasi yangu pengine ya mwisho. Leo ninajisikia kuwa karibu na Mungu, Beatrice."
Je nini kitaendelea?
Je Mike aliweza kupona ugonjwa huo?
 
SEHEMU YA 15


Maelfu kwa maelfu ya watu walikusanyika katika viwanja vya Uhuru Park, kumsikiliza mtumishi wa Mungu, Aron Magabilo, mamia ya watu wenye shida na wagonjwa mbalimbali walikuwepo na walikaa mbele ili waombewe. Miongoni mwa watu hao walikuwepo Mike na mke wake Beatrice.
"Ninajisikia amani sana moyoni mwangu siku ya leo mke wangu."
"Hata mimi na ninategemea leo tutatoka hapa tukiwa wapya kabisa."
"Praise the Looooooord! (Bwana asifiiiiiiwe) sauti ya mtumishi wa Mungu, Magabilo, ilisikika hewani na watu wote wakaitikia.
"Ameeeni!"
"God is powerful and there is nothing impossible before him, if you believe in his loving son Jesus Christ, tonight you are going to be delivered from all the sickness and agonies you have been suffering from! Because Jesus is the true Healer, Ameeen!" (Mungu ana uwezo mkubwa, kwake hakuna kisichowezekana! Jioni ya leo kama ukiamini katika mtoto wake mpendwa, Yesu Kristo, utafunguliwa kutoka katika magonjwa na maumivu yote ambayo yamekuwa yakikupata kwa sababu Yesu ndiye mponyaji wa kweli! Ameeni).
Watu wote wakaitikia Ameeeni.
"Now if there is anyone among you with any disease please come foward and witness the miracles of Jesus (Kama kuna mtu kati yenu mwenye ugonjwa ulioshindikana, tafadhali naomba apite mbele ili ashuhudie miujiza ya Yesu Kristo). Mchungaji Aron Magabilo aliendelea kusema.
Baada ya ukimya mrefu bila mtu kujitokeza mchungaji Aron alikumbushia tena.
"Mume wangu twende!" Beatrice alimwambia Mike.
"Beatrice nitapona kweli?" Mike aliuliza akiwa katika kusitasita na baadaye alinyanyuka kwenda mbele.
Aliponyanyuka tu watu wote waligeuza macho kwake, Mike aliona aibu lakini hakuwa na la kufanya, yeye alichotaka ni kupona, awe mzima tena, hakutaka kufa kabisa.
***
"Tatizo lako ni nini ndugu yangu?"
Kabla Mike hajajibu kitu Beatrice aliingilia kati.
"Mchungaji mume wangu yupo katika mateso makubwa sana kwa muda mrefu sasa akisumbuliwa na UKIMWI, sisi ni Watanzania tulikuja hapa Nairobi kujaribu dawa ya Kemron lakini imeonekana kutomsaidia mgonjwa wangu, ndio maana leo tumekuja kwa Yesu ili tupate uponyaji wa kweli."
Maneno hayo yote yalisikika kwenye kipaza sauti na watu wote walikuwa kimya.
Mchungaji alimgeukia Mike: "Pole sana Mtanzania mwenzangu, lakini jioni ya leo utashuhudia muujiza wa Yesu Kristo na nguvu za shetani zitashindwa katika jina la Yesu! Je, unayo imani kuwa Yesu atakuponya jioni ya leo?""Nd...o!" Mike aliitikia kwa sauti ya huzuni huku machozi yakimtoka.
"Basi nyanyua mikono yako juu!" Mike akafanya hivyo na mchungaji akamwongoza katika sala ya toba, baada ya hapo mchungaji aliwaita wachungaji wengine waliokuwa nyuma yake wafanye maombi pamoja.
***
"Ninalifungua pepo la UKIMWIkatika jina la Yesu Kristo, shetani ashindwe ukamweke huru kijana Mike ambaye ameteseka kwa muda mrefu, baba ninakuomba ukatende miujiza TIKARABOSHONDOBORO! BO! BO! BO! TIKA! TIKA! SHANDOROBOBO!" Mchungaji Aron Magabilo alianza kunena kwa lugha palepale Mike akaanguka chini na kuanza kutoa povu mdomoni.
"Haleluuuuuya! Namshukuru Mungu pepo la UKIMWI limemwachia kijana Mike, kijana unajisikiaje sasa?"
"Na...fu..u..ki...dogo lakini ba...do," Mike alijibu kwa sauti iliyokatikatika, alionekana kuwa na imani kidogo sana na kilichokuwa kinafanyika.
“Basi nenda nyumbani uendelee kumtumaini Mungu na muujiza utaendelea kutendeka siku hadi siku," alisema mchungaji.
Pamoja na kuombewa, wiki mbili baadaye hali ya Mike ilikuwa bado mbaya na walikuwa bado wako hotelini. Mzee Martin na mkewe waliwasili Nairobi kumwona mtoto wao. Hali waliyomkuta nayo ilimfanya mama yake atokwe na machozi.
"Usilie mama, nitapona tu!" Mike alimfariji mama yake.
"Mimi nimesikia huko Zaire kuna dawa inayoitwa, MMI inadaiwa kuponyesha kabisa, hivyo ninaona twende huko tukajaribu. Hatuwezi kuendelea kukaa tu wakati kuna msaada sehemu fulani," alisema mzee Martin.
Wote waliafikiana kwenda Zaire kujaribu dawa ya MMI. Hali ya Mike ilikuwa dhaifu mno kwa wakati huo na kilichomdhoofisha zaidi kilikuwa ni kuharisha, Mike aliharisha mno! Katika muda wa saa moja alibadilishwa nguo si chini ya mara mbili.
Mipango ya usafiri ilipokamilika Mike alisafirishwa hadi Lubumbashi, Zaire, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia. Kabla hajapandishwa katika ndege alitundikiwa kabisa dripu ya maji ambayo ingemsaidia njiani.
"Mama na baba endapo Mungu akiniweka hai tutaonana tena lakini tusipoonana basi tutaonana mbinguni; nisalimieni dada yangu, Violeth," alisema Mike.
"Hakuna tatizo, tutakuombea mwanetu na Mungu atakusaidia," mama yake Mike alisema kwa sauti ya huzuni.
Kwa mzee Martin na mkewe ile ilikuwa ni kama mara ya mwisho kumwona mtoto wao akiwa hai. Mama yake Mike aliinama na kumbusu mtoto wake usoni.
"Mungu akusimamie mwanangu, nakupenda na nitaendelea kukupenda siku zote za uhai wangu uwe hai au umekufa?" Mama Mike alisema akilia.
Mzee Martin na mkewe walikuwepo uwanjani hadi ndege iliporuka kutoka uwanja wa ndege wa Nairobi. Walirudi stendi ya basi na kupanda basi la Takrim kurudi Mwanza. Ilikuwa ni siku ya huzuni kubwa mno maishani mwao kushuhudia mtoto wao akiondoka kwenda ugenini akiwa katika hali mbaya kabisa kiafya.
Mzee Martin alipenda sana asafiri na mtoto wake lakini ilishindikana kwa vile alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa BP uliomfanya anyimwe kibali cha kusafiri kwa ndege.
Maandalizi ya kutosha yalikuwa yamefanywa na hospitali ya majaribio, Patrice Lumumba Research Center. Ndege ilipowasili tu Mike aliteremshwa na kupelekwa ndani ya gari la wagonjwa na kukimbizwa hospitali. Bila kupoteza muda Mike alianzishiwa dawa ya MMI ambapo ilibidi aongewezwe chupa nyingine ya maji.
Pia alipewa dawa za kuzuia kuharisha na za vitamini ili kuupa mwili wake nguvu. Madaktari waliamini kuwa kutokana na hali aliyokuwa nayo Mike kama angepewa dawa hiyo ingeweza kumuua.
Wiki mbili baadaye Mike alikuwa bado akiharisha ingawa mwili wake ulikuwa umepata nguvu kidogo! Mwezi mmoja baadaye Mike alifunga kuharisha na mwili wake ukapata nguvu, akaanzishiwa dawa ya MMI. Aliitumia kwa miezi miwili lakini hakupata nafuu yoyote zaidi ya kufunga kuharisha.
Mdomoni alikuwa na madonda mengi yaliyomfanya ashindwe kula chakula vizuri. Mwili wake ulipungua mno na kichwani alinyonyoka nywele.
"Mke wangu hivi ni dhambi gani niliyoifanya hapa duniani kustahili adhabu kama hii?" Mike alimwambia mkewe baada ya kuona mateso yanazidi.
Huko Zaire nako, pamoja na kutumia dawa, hali ya Mike iliendelea kuwa mbaya siku hadi siku. Hata mama yake mzazi alipokwenda Zaire kumwona aliamuru Mike arudishwe Mwanza haraka iwezekanavyo.
"Mama inaonekana hakuna jinsi ya kumsaidia kijana huyu, hivyo ndivyo ilivyopangwa, nakusihi umrudishe nyumbani," mama yake Mike alimweleza Beatrice.
"Sawa mama," Beatrice hakuwa na pingamizi.
Alikwishahuzunika, ikatosha, alikwishalia machozi yakakauka, mwisho akamwachia Mungu aamue hatima ya mumewe!
Mike alikuwa kipenzi cha watu, habari za kuingia kwake mjini Mwanza kutoka Lubumbashi zilitapakaa mji mzima, watu waliomwona uwanja wa ndege walisikitishwa kwa jinsi hali yake ilivyokuwa. Wengine walitokwa na machozi na wengine walilia hadharani.
Mike alipelekwa moja kwa moja hadi Nyakato kwa wazazi wake, mama yake alitaka Mike akae karibu naye asaidie kumuuguza wakati Beatrice akiwa anaangalia biashara zao zilizosimama kwa muda mrefu.
Jonas, rafiki mkubwa wa Mike, ambaye huko nyuma naye aliwahi kuvumishiwa kuwa na UKIMWI, alikwenda kumtembelea Mike aliposikia amerejea kutoka Lubumbashi.
"Mimi niliwahi kuugua watu wakasema nina UKIMWI, haukuwa uongo, ugonjwa huu kweli ninao! Hata hivyo, kuna njia ambayo ninaitumia kurefusha maisha yangu," Jonas alisema.
Waliongea mengi sana Jonas akiwaeleza siri ya yeye kuendelea kuishi.
Wiki mbili baadaye Jonas, Mike na Beatrice walikuwa ndani ya ndege ya British Airways wakielekea Marekani ambako ndiko ilipokuwa siri ya afya ya Jonas.
Walikaa Marekani mwezi mmoja, waliporudi Mike alikuwa na nafuu kubwa, watu wengi walishindwa kuelewa nini kilichofanyika Marekani.
Mike alikuwa na nguvu tena na kuendelea na kazi zake, hata baba na mama yake walishangazwa na mabadiliko hayo. Ilibidi Mike na mke wake warudi nyumbani kwao Isamilo kuendelea na maisha. Walimchukua Violeth ili aishi nao.
Mike alinenepa na kunawiri kuzidi hata alivyokuwa mwanzo kiasi kwamba baadhi ya watu walianza kuvumisha kuwa Mike hakuwa na UKIMWI ila alirogwa na wafanyabiashara kutoka Zaire aliowadhulumu pesa zao.
Biashara za Mike zilizokuwa zimesimama ziliendelea vizuri na kila alikokuwa akifanya alimshirikisha Beatrice na dada yake, Violeth. Alifanya hivyo kwa sababu alijua hana muda mrefu wa kuishi duniani, alitaka baada ya kufa Beatrice aendeleze biashara na kama Beatrice angekufa Violeth aendeleze biashara zao.
Kila baada ya miezi mitatu hali ya Mike ilipobadilika, alisafiri kwenda Marekani na aliporudi kutoka huko afya yake ilikuwa njema. Watu walishindwa kuelewa huko Marekani Mike alifanyiwa kitu gani.
***
Baada ya kumaliza sindano sitini za kifua kikuu Mike alipewa dawa aina ya Thiazina kutumia nyumbani kwa muda wa mwaka mzima lakini katika mizunguko yote ya Nairobi na baadaye Zaire, Mike hakumeza tena vidonge hivyo, hali iliyosababisha kifua kikuu kumrudia tena.
Ghafla hali yake ikawa mbaya kwa kikohozi na vichomi kifuani, ikabidi alazwe katika hospitali ya Bugando na kuanzishiwa matibabu ya kifua kikuu tena.
Alipopigwa picha ya “X-ray” ilionyesha mapafu yake yalionekana yameharibika kabisa na yalijaa maji, pamoja na matibabu ya kifua kuu aliyopewa, hali ya Mike ilizidi kuwa mbaya. Kitambi alichokuwa amekipata tena kiliporomoka na kumrudisha katika hali yake ya mwanzo kabisa.
Alipotaka kusafiri tena kwenda Marekani alinyimwa viza kwa sababu afya yake ilikuwa mbaya mno, hivyo ilibidi aendelee na matibabu katika hospitali ya Bugando mpaka aliporuhusiwa mwezi mmoja baadaye na kurudi kwake, huku hali yake ikiwa mbaya kupita kiasi.
Karibu kila mtu mjini Mwanza alishalielewa tatizo la Mike na wanachama wenzake wa WAMAU walimtembelea mara kwa mara kumpa moyo na kumfariji.
Je nini kitaendelea?
Mara ya kwanza kuandika hadithi hii, moyo uliniuma sana, nilihuzunika sana japokuwa niliandika kitu kutoka moyoni mwangu, nilihuzunika kila nilipokumbuka idadi ya watu wengi wanaougua ugonjwa huu. Mungu awatie nguvu.
Tukutane siku ya Jumanne mahali hapa.
 
Back
Top Bottom