SEHEMU YA 46
Kwa muonekano wake tu, alitisha, alivalia suruali ya jinsi, ilionekana kama kuchoka, ilichanikachanika huku kwa juu akiwa na fulana nyekundu iliyoandikwa maneno yaliyosemeka vizuri machoni mwake, Gucci.
Chini alivalia raba nyeusi, mkononi alikuwa na saa moja iliyoonekana kuwa na gharama kubwa.
Alisimama imara huku akimwangalia Johnson ambaye muda wote huo alikuwa akitetemeka.
Swali ambalo aliuliza, hakujibiwa, mwanaume huyo akaondoka huku akiufunga mlango, na taa hakuizima.
Hapo ndipo macho ya Johnson yalipoanza kukiangalia chumba hicho.
Kilitisha, hakikuwa chumba cha kawaida hata kidogo.
Katika maisha yake aliwahi kuona filamu nyingi za kutisha ambazo watengenezaji waliamini kabisa watu wangeogopa mara baada ya kuzitazama, ila kwa vyumba vyote, mauaji yote yaliyokuwa yakitokea ilikuwa tofauti na chumba hicho.
Kilitisha kupita kawaida. Chini kulikuwa na damu, zilitapakaa kila eneo, kulikuwa na minyororo ya nguvu, kamba, mijeredi lakini pia kulikuwa chupa zilizokuwa zimepasuliwa, kichwani mwake kukamwambia chupa zile zilipasuliwa mwilini mwa mtu. Kwa kifupi chumba kile kilitisha sana.
Hakujua sababu iliyomfanya kuwa mahali hapo, hakufikiri hata kidogo kama Bhoke inawezekana alikuwa sababu, kitu ambacho kilikuja kichwani mwake ni jina moja la mwanaume aliyeitwa Thuram.
Alikuwa na mipango yake ya dhati, alijipanga kwa ajili ya kumgeuka mwanaume huyo.
Alimwambia kuhusu pesa zilizokuwa mahali fulani ambapo hakutaka ajue lakini ili kuzipata ilikuwa ni lazima kuzungumza na mwanaume alieitwa kwa jina la Bruce ambaye alifahamu kila kitu kuhusu pesa hizo.
Alihisi kabisa mwanaume huyo aligundua kwamba alikuwa akienda kusalitiwa na ndiyo maana aliamua kuwatuma watu kwa lengo la kwenda kummaliza.
Alijuta.
Alijilaumu mno kuingia mikononi mwa mwanaume huyo. Hakuona dalili za kupona tena, alijua kabisa huo ndiyo ungekuwa mwisho wake endapo tu mwanaume huyo angeagiza mara moja auawe hukohuko nchini Tanzania.