SEHEMU YA 41
Majibu aliyopewa yalimnyong’onyeza sana, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya.
Aliondoka hapo New York na kurudi hosteli, ilikuwa ni lazima ajipange, ajue ni kwa jinsi gani alitakiwa kupambana kuhakikisha anazungumza na mwanaume huyo na kumwambia kuhusu mahali pesa zilipo.
Kwa sababu hakuwa mwepesi kusema kuhusu jambo hilo, kitu kilichokuja kichwani mwake ni yeye mwenyewe kwenda huko gerezani, afungwe hata kwa miezi sita, wakati akiwa huko afanye kila liwezekanalo kuhakikisha anaonana na mwanaume huyo na kujenga urafiki.
“Mh! Ila hii nayo hatari sana,” alijisemea.
Dola bilioni tano kilikuwa kiasi kikubwa cha pesa, hazikuwa pesa ndogo za kuzipotezea tu, ilikuwa ni lazima apambane kuhakikisha anazipata kwa kujua mahali zilipokuwa.
Kwenda gerezani hakukuwa na tatizo ila alitakiwa kuwa na uhakika wa kuzipata pesa hizo. Kwenye hilo aliendelea kufikiria kwamba kama angekwenda huko, ni kwa jinsi gani angemlaghai mwanaume huyo kumwambia mahali pesa hizo zilipokuwa?
“Inabidi nimtumie mwanamke,” alijisemea.
Hapo, mwanamke ambaye alikuja kichwani mwake kwa haraka alikuwa Bhoke.
Alihisi kwamba alihitaji msichana ambaye alikuwa mrembo lakini ingekuwa vigumu kufanya kazi na mwanamke wa Kimarekani kwa kuwa angeweza kudhulumiwa endapo tu angegundua kwamba kulikuwa na pesa nyingi nyuma ya kila kitu kilichokuwa kikiendelea.
Kuonana na Bhoke ilikuwa ni lazima arudi nchini Tanzania.
Kama yeye angefungwa jela na kumwambia msichana huyo ajifanye kuwa ndugu yake ambaye mara kwa mara angekuwa akimtembelea hapo, je, angekuwa radhi kufanya mapenzi na Bruce ambaye angemuunganisha kwake na kumfanya kuwa demu wake?
Hapo hakupata jibu, ila cha kwanza ilikuwa ni lazima akae na kuzungumza na msichana huyo.
|
|
|
Je, nini kitaendelea?