SEHEMU YA 25
Walikwenda mpaka Texas, walisoma ramani ya nyumba ile, walifuatilia kwa karibu na kuijua vizuri ratiba ya walinzi waliokuwa wakilinda, kwa kutumia utalaamu wa vijana wake wa kompyuta, walidukua kamera, wakazima umeme na kuingia kininja ndani ya nyumba hiyo kubwa.
Humo walikutana na chumba kilichokuwa kimefungwa kwa vault, kwa kumtumia mtu wao wa umeme, akarekebisha kwa kuukata umeme wa ndani kabisa kuachana na ule wa nje, walipoona wameshindwa kabisa, mtu wa kompyuta akaanza kufanya vitu vyake kwa kutumia alama za mikono ya Petrov ambayo aliitumia kufungulia vault hiyo na kuingia ndani.
Waliipata almasi hiyo, walinzi walifungwa katika kibanda kimoja na wao kuondoka nayo. Hiyo ndiyo ilikuwa michezo waliyokuwa wakiicheza, Thuram aliwatumia vijana hao kufanya uhalifu kila kona ambapo aliona angeweza kupata kiasi kikubwa cha pesa.
Alifanikiwa pasipo FBI wala CIA kugundua kitu chochote kile kwani kwenye kila tukio ambapo kulikuwa kukifanyika uhalifu, hakuwepo, kulikuwa na vijana wake tu ambao alikuwa akiwalisha maneno mengi na kuwaambia kwamba hawakutakiwa kutoa siri juu ya kitu chochote kile, nao wakala yamini.
Huyo ndiye ambaye Johnson aliambiwa kwamba kama angeungana naye basi angeweza kupata kiasi kikubwa cha pesa na kuwa tajiri. Alifanikiwa kuonana mara mbili na mwanaume huyo, alizungumza naye, alimwambia ni kwa jinsi gani alitamani sana kuingia kwenye kundi lake la Nyoka.
Mara ya kwanza Thuram hakumwamini, alihisi kama alikuwa ofisa wa CIA ambaye alifika hapo kwa ajili ya kumpeleleza. Alimkatalia na hata alipomwambia tena, alimkatalia pia.
Hilo lilimpa mawazo Johnson, ilikuwa ni lazima aungane na mwanaume huyo. Alipoambiwa kuhusu madili ya pesa nyingi, yalimchanganya na ukiangalia alikuwa Mchaga aliyeijua pesa, kichwa chake kilivurugika zaidi.
Hakuacha kumsumbua mwanaume huyo, alimuomba sana, kwa miezi miwili mfululizo yeye ndiye alikuwa akiongoza kumpigia simu mpaka pale ambapo mwanaume huyo aliamua kuwaita vijana wake na kuongea nao kuhusu Johnson.