SEHEMU YA 15
Hakutaka mtoto wake agundue kilichokuwa kikiendelea, alikuwa msiri huku akiendelea kufanya mambo yake kama kawaida. Siku zilikatika lakini kikafika kipindi sauti yake ikaanza kukauka na koo kuanza kuoza.
Hilo lilimuuma sana, kutokana na maumivu makali, mwisho wa siku akaanza kukonda na kwenda kulazwa hospitalini. Alitamani kuongea, kumuonya mwanaye kuhusu ugonjwa huo lakini alishindwa hata kutoa sauti yake.
Alilazwa hospitalini kwa siku mbili na kuruhusiwa. Alikuwa hoi, hakuweza tena kwenda kujiuza, hakuwa na pesa na matibabu yake yalihitaji sana pesa.
Kwa kuwa Bhoke alikuwa na rafiki yake, Johnson, akaamua kumwambia kuhusu mama yake, alikuwa akihitaji msaada mkubwa kutoka kwake.
“Johnson...mama anaumwa,” alisema Bhoke huku machozi yakimlenga.
“Anaumwa nini?”
“Ana kansa ya koo! Nanahitaji unisaidie pesa,” alisema Bhoke huku akimwangalia Johnson.
Alikuwa kijana mdogo, aliyeishi kwa wazazi wake, hakuwa na pesa, alimwambia hivyo Bhoke kitu kilichomuuma sana. Akaondoka kwa hasira na kurudi nyumbani.
Kila alipomwangalia mama yake, moyo wake ulimuuma sana na hivyo uamuzi wa mwisho ambao aliuchukua ni yeye mwenyewe kuingia mitaani, kujiuza ili apate pesa ya kumuuguza mama yake.
Huko alipokuwa akienda kujiuza, Bhoke alikuwa tishio, alikuwa mdogo, mzuri, alimpagawisha kila mwanaume aliyekuwa akimwangalia. Hakukuwa na mtu aliyeamini kama wangekutana na msichana huyo mitaani na kwenye klabu akitafuta wanaume.
Alipapatikiwa, aliwachukulia pesa nyingi ambazo hizo zilimsaidia mama yake ambaye hali yake ilizidi kuwa mbaya kila siku. Bhoke alitembea na watu mbalimbali, Wazungu, Waswahili, Wachina, Wahindi na wengine.
Alipofikisha umri wa miaka kumi na nne, hali ya mama yake ilikuwa mbaya zaidi na hatimaye kufariki dunia akiwa kitandai, Bhoke alilia sana, hakuamini kama mama yake alifariki dunia, aliumia mno lakini hakuwa na jinsi.
Kwa kusaidiwa na majirani, wakamzika na hatimaye kuanza kuishi peke yake, maisha bila mama huku akiyaendesha kwa kujiuza mitaani.