Hadithi:Moyo usinidanganye

Hadithi:Moyo usinidanganye

mtzmweusi

JF-Expert Member
Joined
Apr 20, 2013
Posts
8,700
Reaction score
9,070
MOYO USINIDANGANYE

NO :01

Mara yangu ya kwanza kuja Dar es Salaam, rafiki yangu Obey alinizungusha kariakoo. Zanzibar pamechangamka lakini mji huu ni hatari. Kuna kila aina ya bidhaa, na nyingi hupatikana kwa bei rahisi kuliko Zanzibar, hasa za madukani. Tulipita sehemu moja, kununua nguo za ndani maarufu kama boxer, mtaa wa DDC. Niliona boxer nzuri zilizouzwa kwa bei nafuu, nikachanganyikiwa kidogo lakini Obey akanipeleka duka ambalo alidai ni mteja hapo. Nilitegemea angemchangamkia muuzaji, ama kuonesha anamfahamu, lakini ilikuwa tofauti. Walisalimiana kama watu wasiojuana kabisa, huku mimi nikiwa nimetoa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango.

Nilishindwa kujizuia kumkodolea yule dada muuzaji, kiasi cha yeye mwenyewe kujistukia, hivyo akanitazama na kutabasamu, na kunipa salamu ambayo kwa mara ya kwanza ni kama sikuisikia japo niliisikia. Mara ya pili akanistua tena kwa kuniita, “Kaka, habari yako?”. “Oh, nzuri, za kwako mrembo?”, nilijibu kwa aibu.
Obey alimuulizia mwenye duka, nikaelewa kumbe yule mrembo hakuwa mwenye duka au muuzaji wa awali.”Ametoka kidogo, ameenda kuniulizia boxer fulani kwa rafiki yake, hapa zimeisha. Lakini naweza kuwauzia chochote mnachohitaji, hakuna shida, pia kama hamniamini, jirani yake huyo anamlindia”. Alizungumza huku akionesha tabasamu mahiri. Hakujua muonekano wake usingefanya mtu yeyote kutomuamini. Kusikia hayo maelezo, moyo wangu ulisononeka kidogo, kwani maelezo yake yalionesha aidha ameolewa ama yuko kwenye mahusiano imara. Baada ya muda mfupi, alikuja muuzaji, aliyezoeana vizuri na Obey, akampa yule dada mzigo wake, kisha binti akaondoka.

Tulinunua tulichohitaji kununua, tukaondoka, akilini nikiwa na mawazo utadhani nimepoteza hela. Obey alianza kunicheka, jinsi nilivyomshangaa yule binti ambaye kwa bahati mbaya hata jina au namba ya simu yake sikufanikiwa kuuliza. Obey ananijua kuwa mimi si kijana ninayezuzuka na mabinti, na nina misimamo yangu fulani kuhusu mahusiano. Hata kwangu pia ilikuwa ni ajabu kuvutiwa na msichana kiasi kile, kwa mara ya kwanza tuu namuona. Miezi miwili iliyopita tuliachana na aliyekuwa mpenzi, bila sababu ya msingi naweza sema, kwani chanzo cha kukosana kilikuwa kidogo sana, kikapelekea kukorofishana mpaka kuachana. Nadhani ni kama nilimsukuma aliyechuchumaa, kwani kabla ya hapo viliwahi kutokea visa kadhaa kuniashiria kuwa Fatmah, mpenzi wangu huyo, hakuwa ananipenda tena. Hata hivyo si lengo langu kuelezea sana uhusiano wangu uliopita.
Nilirudi Zanzibar, wiki mbili baadaye. Nikaendelea na biashara zangu za kusambaza bidhaa za kula kwenye maduka na supamaketi mbalimbali pale Zanzibar. Huwezi amini, akili yangu ilishindwa kupuuza sura ya mrembo niliyekutana naye kariakoo, kwa muda wa miezi kadhaa. Siku ile nilipomtazama kwa kuduwaa, niliona uzuri wa ajabu kwa binti yule. Rangi yake ni ya kahawia, si nyeusi lakini si mweupe pia. Ngozi laini kama ya mtoto, yani utadhani hajawahi hata kung’atwa na mtu. Alipotabasamu meno yake meupe sana yalionekana, na kama pengo dogo upande wa kushoto wa kinywa chake pia nililiona kwa mbali nalo liliongeza mvuto. Zaidi ya hayo, mrembo huyu aliongezewa kionjo cha dimpoz katika uumbaji wake, mashalaah, Mungu fundi jamani! Macho yake meupe, makubwa kiasi, niliwaza akilini mwangu, akiwa ndio yuko mikononi mwangu ananitazama kwa mahaba itakuaje? Sitaki kuongelea umbo lake kwani sikupata fursa kulitazama kwa ufasaha, lakini kwa sekunde chache nilizomtizama akiondoka pale dukani, naweza sema ile ni namba sita ndefu, nadhani unanielewa.

Kwa jinsi alivyoiteka akili yangu, haikuwa ajabu kumuota mara kadhaa. Niliota nimekutana naye tena, na mara hii nikamuomba namba yake. Lakini mara ya pili niliota niko naye eneo zuri, kama wapenzi, huku tukifurahia kila mmoja wetu hiyo fursa. Asubuhi kuamka, Kumbe! Ni mawazo na hisia zangu hunipeleka mahala ambapo hakuna matumaini ya kufika. Kumuwaza yule mrembo mara zote kulinisaidia kumsahau kabisa Fatma, kwani mpaka wakati huo nilikuwa nikijaribu kumbembeleza kwa simu turudiane, huku nikiambulia vichambo na matusi. Basi maisha yaliendelea hivyo, kwa miezi kadhaa, nikamkatia tamaa Fatmah kabisa, nikawa mpole, nikifarijiwa na hisia zangu hewa za binti mrembo, ambaye hakuna matumaini hata tone ya kumuona tena.
Utaendelea

Sent using Jamii Forums mobile app
 
MOYO USINIDANGANYE 2
Endelea

Mwaka mzima ulipita, na wa pili, nikiwa singo kama wanavyosema vijana wa mjini. Biashara zilichanganya, kuna wakati nilipigwa, yaani niliibiwa kidogo na vijana wangu, lakini si kiasi cha kunitia hasara. Niliongeza mtandao, na marafiki katika biashara, kwani nilianza kuwa mkombozi katika upatikanaji wa nguo za ndani kwa urahisi na kwa bei nafuu pale Zanzibar. Baada ya muda nilikutana na binti mwingine, tukaanza mazoea na kuwa kama wapenzi. Nadhani nilichoshwa na upweke na kuamua kuwa kwenye mahusiano, japo sikuwa nimemaanisha sana. Mungu anisamehe, kwani mpaka leo nahisi sikumtendea haki yule mpenzi wangu mwingine baada ya Fatmah. Utanielewa baadaye.

Miezi michache tena ikapita, nikiendelea na biashara zangu na uhusiano wangu wa kupotezea muda. Nakumbuka siku moja, nikiwa Dar es Salaam, nikisubiri safari yangu kufata mzigo Uganda, siku moja kabla ya safari. Nikiwa kwa rafiki yangu Obey, tunakula chakula cha mchana kilichoandaliwa na mkewe Obey alipigiwa simu na jamaa yake fulani akimualika kwa chakula cha jioni. Ni rafiki yake, walisoma naye miaka sita ya sekondari, waliishi naye chumba kimoja, kwa wakati huo walikuwa wamepotezana kama miaka miwili huku huyo jamaa akiwa jeshini ambako hakutakiwa kuwa na mawasiliano na watu. Alipopokea simu, alipata msisimko na hakutaka kutakaa kabisa ule mualiko. Alianza kutushawishi mimi na mkewe twende naye, lakini mke wake aliyekuwa na mimba changa hakutaka kusumbuka kabisa. Nilitaka kumkatalia pia, ili nijiandae na safari kesho yake, lakini alinishawishi sana, nikashindwa. Tukamuacha mkewe, na binti wa kazi, tukaondoka.

Tulikutana hoteli moja nzuri mjini Dar es Salaam, maeneo ya Posta, inaitwa lamada. Tulifika, na kuongoza kwenye meza moja yenye watu wawili, mwanaume na mwanamke, walioonekana ni wapenzi. Lahaula! Sikutaka kuamini macho yangu kile nilichoona mbele yangu. macho yangu yaligonga moja kwa moja katika sura ninayoifahamu, ya binti aliyewahi kunivutia kuliko wanawake wote kabla. Msichana niliyemuota na kutamani kuwa naye kuliko mwanamke mwingine yeyote. Ghafla akili yangu ilihama, nikajihisi kuchanganyikiwa, nikatamani tungeipita ile meza, yani wasiwe ndio hao watu ambao tutakaa nao. Lakini nikiwa katika lindi la mawazo, nilijikuta tayari tumekaa kwenye meza hiyo hiyo, na muhudumu ameshafika kutusikiliza. Obey na rafiki yake walisalimiana kwa furaha, Obey akanitambulisha, huku nikiwa kama mtu aliyenyeshewa. Tukatambulishwa pia huyo mrembo, aliyeitwa Latiffa, ambaye jamaa alisema ni mkewe mtarajiwa. Rohoni nikajisemea,”bora ni mtarajiwa”, huku nikijipa matumaini kwa mbaali kwamba kama bado hawajaoana pengine bahati inaweza kunigeukia mimi.

INAENDELEA...

Sent using Jamii Forums mobile app
 
MOYO USINIDANGANYE

NO :03

Marafiki wawili walifurahiana, wakipiga gumzo za hapa na pale, huku kwa namna fulani wakijaribu kutufanya mimi na yule mchumba wa jamaa tusijisikie wapweke. Kiukweli akili haikuwa hapo. Kila wakati nilimtupia Latiffa jicho la wizi, huku nikitamani azungumze. Kuna wakati alizungumza kidogo, basi nikamuitikia kwa shamra mpaka nikajistukia. Tuliendeleza zogo kwa muda, lakini nilijihisi nahitaji kwenda kupata pumzi, nikainuka kwenda uani. Yaani muda wote niliokaa pale mezani nilihisi hewa hainitoshi. Nilikuwa na hisia mchanganyiko, furaha ya kumuona mrembo wangu kwa mara ya pili, ambaye sikutegemea, lakini pia sikuwa na namna ya kumuiba mrembo huyo kwa jamaa hivyo niliishia kujisikitikia. Niliinuka na kwenda uani, nikajiangalia kwenye kioo, huku nikijiambia,”Ni sawa tuu Hammy, sio wako. Inatosha kumuona kwa mara nyingine na walau kukaa naye meza moja”.
Nilirudi, na haikuchukua muda tukaondoka. Kesho yake nilisafiri, nikimuwaza Lattifa akilini, lakini walau nilifanikiwa kumuona kwa mara nyingine, kujua jina lake na zaidi kujua anafanya wapi kazi. Akilini mwangu hakuondoka kuanzia wakati huo, japo nilijilazimisha kumtoa. Sijawahi kupenda hivi, wala kuhisi kama naweza kumpenda mwanamke ghafla kiasi hiki. Latiffa aliingia akilini mwangu, aliingia moyoni mwangu, alichukua nafasi ndani yangu kiasi ambacho sikutegemea. Sauti ya maneno machache aliyoongea usiku ule ilijirudia kichwani mwangu kana kwamba yalinihusu mimi. Sura yake haikuniacha akilini hata dakika moja. Hisia hizo zilinipa raha kiasi, kwani niliiruhusu akili yangu imuwaze, iwaze uzuri wake na kila kizuri kumuhusu yeye. Lakini wakati huo huo zilinipa mawazo, na huzuni pia kwani ni kama nilijaribu kujenga ghorofa hewani. Nilifarijika kwa kumuwaza tuu, hivyo safari nzima nilimuwaza binti huyu aliyeuteka moyo wangu kwa kasi

Maisha yaliendelea kwa miezi kadhaa, nikaendelea na biashara zangu. Kila nilipowasiliana na Obey nilimuuliza kuhusu rafiki yake. Sikutaka kumwambia kuwa Lattifa ndiye binti aliyenipagawisha siku ile kariakoo kwani Obey hata hakukumbuka ile sura. Nilijaribu kuulizia habari zake za kuoa, huku nikimdodosa kujua kama anamaanisha kumuoa Latiffa, japo sikutaka kudodosa sana kwani Obey angenistukia. Haikupita muda mrefu, nilitafuta tena safari ya Dar es Salaam, kama kawaida nikaenda kwa Obey ambaye hata baada ya kuoa hakuwa ananiruhusu nifikie hotelini. Siku moja usiku, mkewe akiwa amelala nasi tuko sebuleni kuzungumza kidogo, niliuliza tena habari za jamaa na kama ana nia kweli ya kuoa. Alistuka kidogo, akaniuliza kwanini nafatilia sana habari za huyo jamaa yake. Sikumwambia, lakini nilikazana kuuliza, akaniambia, “Jamaa si muoaji. Labda kama amebadilika sasa hivi, lakini kipindi chote namfahamu huwa, kila binti anayenitambulisha ni kama atamuoa mwezi ujao, lakini ukikutana naye wakati mwingine unamkuta na msichana mwingine”. Kwangu hiyo ilikuwa habari njema sana, hakujua tuu.
Niliacha kuuliza habari hizo tena kwa muda, lakini nikaamua kufanya jitihada zangu binafsi kumtafuta Lattifa. Kipindi hicho nilikaa Dar kama mwezi mzima, kiasi cha Obey kushangaa imekuaje, lakini sikumwambia nini hasa kimenikalisha. Kwa asili, sipendi kuonesha udhaifu wangu juu ya wanawake, hivyo japo Obey ni rafiki yangu wa ndani sana, sikutaka kumuonesha kiasi gani Lattifa aliiteka akili na moyo wangu, hasa kwa kuwa bado hakukuwa na mwanga wowote wa kumpata.
Endelea kufatilia.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
MOYO USINIDANGANYE 04

Nilimfatilia alipofanya kazi, nikafanikiwa kumpata, lakini sikujionesha kwake. Niliamua kutumia mbinu fulani kumvuta karibu kwanza, kabla hajanifahamu. Nilianza kumtumia zawadi, huku nijitambulisha kama secret admirer yaani akupendaye kwa siri. Nilifanya hivyo, kwa ujanja, mara kadhaa. Nikaondoka na kurudi Zanzibar, na kuendelea kutuma zawadi kadhaa zenye hamasa ya mapenzi. Sikujua anazichukuliaje, labda sikutaka kujua kwa wakati huo. Kiasi, naogopa kukataliwa, pengine nina moyo muoga wa maumivu, hivyo nilijaribu mbinu ambayo ingenipa nafasi ya kukubalika kiurahisi. Kwenye mizigo au parcel nilizomtumia, niliambatanisha na jumbe fupi, nikimsifia, kumwambia namna nilivyohisi mara ya kwanza namuona, na mambo mengine mengi. Sikumpa anuani wala kumpa fursa ya kunijibu. Nilifanya hivyo kwa miezi mitano mfululizo, ndipo nikapanga kuonana naye.

Nilimtumia mzigo wa mwisho wenye ujumbe wa kumuomba kumuona, na namba yangu ya simu, nikimsihi sana anipigie ili tuonane. Hapa nilikuwa narusha kete zangu nikiwa na matumaini kidogo kuwa angenipigia. Hatima ya mimi na huyu mrembo kuwa pamoja ilikuwa juu yake, kama angepiga simu. Nilipata mawazo sana tangu nilipotuma ile parcel kwani hapo ndipo nilielewa nilishapenda kiasi gani. Kitendo cha kukaa siku kadhaa nikisubiri anipigie huku nikishindwa kufuatilia kama kweli atapiga au la, kilinipa mawazo kiasi cha kunipungua uzito.

Siku zilipia, tofauti na matarajio yangu ukapita karibu mwezi mzima, kiasi cha kunifanya nikate tamaa kabisa. Lakini nakumbuka siku kama ya 27 au 28 hivi tangu nitume ule mzigo, nikasikia simu inaita nikiwa bafuni. Nilitamani kutoka na povu kichwani, kwani kwa wakati huo wote sikuwa najiruhusu kukosa simu hata moja. Nilipotoka haraka sana nilishika simu yangu na kuona namba mpya. Lahaula, moyo ulistuka, nikasema ndio nshamkosa hapa. Nilishika simu kupiga huku moyo ukienda kasi kama treni ya umeme, na sijui kwanini akili yangu yote iliniambia ndiye, kwani kama mfanyabiashara haikuwa kitu cha ajabu sana kupokea simu mpya. Lakini nadhani siku hiyo moyo wangu uliamua kunielekeza kwa Lattifa. Nilijaribu kupiga lakini haikupokelewa, hapo nikakata tamaa kabisa. Lakini baada ya kama nusu saa simu iliita tena, namba ile ile, nikiwa nimejilaza kitandani kwangu na kuitizama kana kwamba nimeambiwa nisubirie. Niliipokea nadhani kabla aliyepiga hajajua kama imeanza kuita. Ikasikika saauti ya kike
Kwenye simu: Halo!
Mimi: Halo, habari?
Kwenye simu: Nzuri, naongea na Shivo? mzigo wa mwisho kumtumia uliokuwa na namba ya simu, nilijitambulisha kwa jina hilo moja
Mimi: Ndio, hujakosea, nani mwenzangu? hapo sasa nilibakiza hatua moja kuhakikisha kwamba huyu ndiye. Sikungoja tena kusikiliza sauti, ilibidi nimuulize
Kwenye simu: Naitwa Lattifa

Sikusubiri aendelee kuzungumza au kujieleza zaidi. Nilipiga kelele, bila hata mimi mwenyewe kujua imekuaje nimepiga kelele kubwa namna hiyo. Lakini nilijikuta nashangilia kwa sauti, huku nikimshukuru sana kwa kupiga nisijali kwamba amepiga kukubali wito au pengine kunionya nisiendelee kumtumia zawadi. Nilianza kumshukuru sana kwa kunipigia, nikimwambia jinsi gani nimekuwa nikisubiria simu yake. Nilitumia kama dakika mbili nzima kujieleza jinsi gani simu yake imekuwa ya maana kwangu. Baadaye nikajistukia, ikabidi nimwambie,”Hata kama umepiga kunionya au kunigombeza lakini kitendo tuu cha wewe kunipigia simu nafsi yangu imefurahi sana”. Alicheka kwa sauti kidogo, nikavuta pumzi nikiwa na matumaini kwamba kwa cheko lile basi kuna ushwari.

“Nimekuwa nikipata parcel zako, nashukuru”, alianza kwa kusema hivyo, nami nikamjibu kwa haraka,”Asante wewe mrembo, kwa kupokea”. “Kwani ulinipa nafasi ya kukataa?” alitania, “Hapana lakini kitendo cha kunishukuru sasahivi kimenipa amani kwamba ulizipokea. Sasa niambie kama naweza kukuona tafadhali. Hata kama huna cha kuniambia, au kwenye simu hii ulitaka kunitukana basi utafanya hivyo huku umenitazama sura”, nilijipendekeza na kujihami huku nikimsihi tuonane. Alicheka kidogo na kuniambia, ni sawa. Nadhani unapata picha ni furaha kiasi gani nilikuwa nayo kupata hiyo fursa. Alitaka kuanza kuuliza maswali kuwa naishi wapi na tutaonana wapi nikamkatiza na kumjibu kwa haraka,”Niambie ratiba yako tuu mrembo, lini na saa ngapi ungetaka tuonane. Wapi pa kuonana tafadhali niachie mimi, nitakuchukua ofisini kwako au popote utakapotaka nikuchukue siku hiyo tutakayo onana”. Aliguna na kukubali kwamba tungeonana siku mbili baadaye.

INAENDELEA...

Sent using Jamii Forums mobile app
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom