Hadithi: Malaika Mweusi

Hadithi: Malaika Mweusi

SEHEMU: 17
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Ndani ya ndege kulikuwa na watu zaidi ya hamsini kila mmoja alikuwa kimya.
Tulisafiri kwa muda wa siku mbili. Siku ya pili ndege ilitua ilikuwa ni usiku wa manane, tuliteremka sikujua ule ni mji gani hata nilipo wauliza wenzangu nao walisema hawajui lakini ni moja ya nchi za Ulaya.
SASA ENDELEA...
Hata nilipo muuliza mkuu wa msafara alinijibu eti nilichofuata ni mafunzo sio kujua ule ni mji gani au nchi gani.
Kesho yake asubuhi tuliamshwa na kukumbiza mchakamchaka, maisha yale hayakuwa mageni kwangu kwani hayana tofauti na yale niliyoishi na mzee Utakufalini ni ukomandoo tosha.
Tofauti yake mafunzo yalikuwa ya kisasa yenye kukufanya mwanadamu uwe na moyo wa chuma roho ya kinyama ya kumuua mwanadamu mwenzio kama unaua nzi. Nilijifunza vitu vingi kutumia silaha za kila aina, vifaa vyote vya electr onic kutumia vyombo vyote vya kisasa.
Niliweza kuongea lugha zaidi ya tano kiswahili kiingereza, kifaransa, kiarabu na kitaliano. Vilevile nilikuwa na uwezo wa kuigiza sauti tofauti zaidi ya ishirini.
Nilifuzu mbinu za mapigano ya silaha na mikono baada ya kuhitimu mafunzo nilirudi Tanzania kwa mtindo uleule nilioondokea wa kufungwa kitambaa usoni.
Baada ya kufika nyumbani Tanzania nilipewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kujulishwa ni kazi gani iliyo mbele yangu iliyoonekana nzito. Lakini kulikuwa na tofauti kati ya mwanzo na muda ule.
Mwanzo nilipokuwa nikiifikiria hiyo kazi nisiyoijua moyo uliingia hofu na woga mwingi ulinitawala. Lakini baada ya kurudi kutoka kwenye mafunzo ya hatari sikuwa tena na woga hata chembe, nilikuwa tayari kwa kazi yoyote iliyo mbele yangu.
Baada ya mapumziko niliitwa Kibaha tayari kukabidhiwa hiyo kazi, kama kawaida nilikutana na Dk Ray:
"Ooh karibu mrembo."
“Asante.”
“Nina imani upo tayari kwa kazi?”
“Ndio maana yake”
“Sawa, subiri wakubwa watafika muda si mrefu ili kukueleza cha kufanya
“Hakuna tabu.”
Nilikaribishwa sebuleni na kupewa kinywaji nikiwa nawasubiri hao wakubwa.
Niliendelea kupata kinywaji laini na kusoma magazeti ya siku ile.
Mara kundi la watu wasiopungua kumi na mbili walinipita kuelekea chumba cha mikutano hakuna aliyenisalimia zaidi ya kupita kimyakimya. Nami sikuwasalimia nilitulia tuli nikisoma magazeti, mara alikuja Dk Ray na kunieleza:
“Thereza jiandae wazee wameisha kuja.”
“Nijiandae kwa kipi?” nilimuuliza.
“Ili kukabiliana na maswali yao.”
“Wana swali gani jipya ambalo halijawahi kuulizwa duniani?”
“Unaonekana unajiamini sana?” Dk Ray.
“Lazima nijiamini, ndio maana nipo hapa tayari kwa lolote.”
“Nilikuwa nakutaarifu tu.”
“Shaka ondoa nipo tayari kukabiliana na mtu yeyote kama niliweza kukabiliana na kifo, mwanadamu ni nini kwangu?”
“Mmh, sikuwezi.”
Dk Ray aliondoka na kuniacha nikisoma gazeti lakini mawazo yakiwa juu ya kikao hicho. Nilijikuta najiuliza swali la awali inaweza kuwa ni kazi gani. Hao wakubwa sio siri ni wakubwa kweli wengine wapo serikalini tena wana vyeo vya juu. wengie wapo taasisi za dini walio mbele katika kutoa misaada kwa jamii lakini wengine walikuwa wageni machoni mwangu.
Kikao kilifanyika kwa zaidi ya saa mbili na mimi niliendelea kusubiri mpaka nilipo fuatwa na Dk Ray.
“Vipi upo tayari?”
“Tayari kivipi?” nilimuuliza.
“Kuonana na wazee.”
“Nilikuwa tayari tangu nilipotoka nyumbani kwangu.”
“Basi tuongozane kwenye kikao ambacho nakiona ni kizito tofauti na vikao vyote.”
Niliongozana na Dk Ray hadi kwenye ukumbi wa mikutano uliokuwa mzuri uliojengwa kisasa.
Nilipoingia nilionyeshwa kiti kwa ishara ya mkono, kilikuwa kiti cha kati yaani kinachotazamana na mwenyekiti wa kikao. Baada ya kuketi Ray alitoka nje ya chumba cha mikutano ikimaanisha kicheo ni mtu mdogo sana.
Baada ya kuketi alikuja msichana aliyevaa mavazi yaliyouacha uchi mwili wake kwa asilimia themanini. Kile kilinishtua yaani mhudumu ni tofauti kubwa na picha iliyokuwa ndani kwenye kikao cha watu wasio pungua kumi na mbili wenye heshima zao.
Walikuwepo viongozi wa dini mbili viongozi wa serikali na viongozi wa mashirika ya dini ya nje na taasisi zisizo za kiserikali (NGO!S) za kitaifa na kimataifa. Nilijiuliza iweje msichana alijiweka sehemu kubwa ya mwili wake uchi ndiye awe mhudumu wao?
Hapo kengele ya tahadhari ililia kichwani mwangu, niliachana na hilo kwa vile sicho nilichokifuata. Muhimu kwa muda ule kujua ni kazi gani ninayotaka kupewa.
Mhudumu aliyekuwa amesimama pembeni yangu aliniuliza:
“Dada unatumia kinywaji gani?”
Wakati huo kila mmoja aliyekuwa mule ndani alikuwa akitumia pombe kali.
“Nipatie soda ya aina yeyote.”
“Ooh! Samahami dada yangu hakuna soda ya aina yeyote zaidi ya pombe kali na pombe zingine.”
“Maji yapo?”
“Ndio yapo.”
“Niletee.”
Mhudumu aliondoka baada ya muda alirudi na chupa kubwa ya maji pamoja na glasi. Baada ya kunijazia maji kwenye glasi aliondoka, wakati wote huo kikao kilikuwa kimya wakipitia nyaraka muhimu kila mmoja alikuwa ameinama akisoma. Wakiwa wanaendelea kupeuzi na mimi muda ule niliutumia kuwasoma sura zao.
Kati ya watu kumi na mbili sura sita nilizifahamu hazikuwa ngeni machoni mwangu ila sita kila nilivyojitahidi kuzikumbuka jibu lilikuwa mbali. Nilitulia tuli huku nikiendelea kuisoma mandhari ya mule ndani.
Nilishtuliwa na mlio wa meza iliyogongwa ikimaanisha tuwe tayari kumsikiliza mwenyekiti wa kikao ambaye hakuwa mwingine ila Father Gin mkuu wa kanisa la Watu waliojitolea kwa ajili ya Bwana.
Alikuwa ni mtu ninayemuheshimu sana ambaye ndiye kinara wa kutoa misaada si kwa wananchi tu hata serikali nayo iliuthamini mchango wake kwa maendeleo ya nchi.
“Karibu Thereza ilikuwa sauti yake nzito Father Gin.”
“Asante.”
“Kabla ya yote sister Caroline mwapishane ili awe tayari kwa kikao chetu.”
Mmoja wa wajumbe wa mkutano alinyanyuka na kuja karibu yangu. Niliapishwa kiapo tofauti na viapo nilivyokwisha wahi kuona mtu akiapa. Kilikuwa kiapo cha kulinda na kuhifadhi siri ya kundi na kuwa tayari kufa kuliko kutoa siri ya kikundi. Vilevile kuwa tayari kuuawa pale nitapobainika nimetoa siri.
Baada ya kiapo ndipo nilipotambulishwa kwa wajumbe wa kikao kile, wageni kulikuwa na raia wa Pakistan, Columbia, Afrika magharibi , Uturuki, Marekani ya kusini.
Baada ya kutambushwa kwao Father Gin alinigeukia mimi:
“Ndugu wajumbe wa mkutano wa PT au Pigo Takatifu huyu ndiye tuliyemwandaa kwa ajili ya Operesheni Pigo Takatifu. Leo hii kama tulivyoongea kwenye kikao chetu jukumu lote tunamkabidhi binti ambaye nina imani ataifanya kazi vizuri na kuweza kufanikisha opereshemi yetu, Thereza,” aliiniita:
“Abee.”
“Nina imani lazima utashangaa na kujiuliza ni kazi gani hiyo yenye malipo mazito lazima utakuwa na wasiwasi. Kweli kazi ni nzito inabidi mafunzo ya kina ndio maana tulikuandaa kwa ajili ya kukabiliana na kazi nzito. Malipo tuliyotoa ni kulingana na kazi nzito ambayo maisha ya muhusika huwa hatarini kwa asilimia tisini, ndio maana tumetoa malipo manono pindi mtu wetu akifariki kazini kwa ajili ya watu wanaomtegemea.
"Leo hii utakabidhiwa pesa zako taslimu bilioni 60 na umalizapo kazi yetu tutakupatia bilioni 40 zilizobaki kama utaifanikisha lazima tutakupa zawadi, mimi kama mimi ninakuahidi bilioni 30 sijui wenzangu,” aliwageukia wenzake.
“Sisi hatuahidi ila ataona baada ya kazi,” walijibu wajumbe wa mkutano.
“Kwanza kabla ya kukueleza ni kazi gani lazima uelewe sababu za kukupa hiyo kazi. Hili unaloliona ni kundi la watu kumi na sita hapa tupo watu kumi na mbili na wanne waliojitoa.
"Kundi hili lina shughuli nyingi ambazo ni siri zisizojulikana na mtu yoyote zaidi yetu sisi kumi na sita. Kwanza kabisa mimi ndiye muasisi wa kundi hili nchini na kuanza kukusanya watu walio tayari kufanya kazi nami nashukuru niliwapata na wakanielewa.
"Kundi hili lina sura mbili, kwa nje lina sifa nzuri kwani lipo mbele kutoa msaada kwa jamii ambao hudhani wanakula kumbe wanaliwa. Msaada tunaoutoa kama
kujenga makanisa makubwa bila msaada wa sadaka, huduma vijijini kama maji,umeme hospitali na huduma nyingine kwa jamii.
“Kitu kinachofanya watu wajenge imani juu yetu. mradi wa makanisa au kujenga vituo vya msaada ili kuwavuta karibu na kufanikisha azma yangu. Mradi tulioanza nao ni wa kuuza damu, nina imani kazi hiyo hata wewe uliifanya bila kujua. Ulipompata mteja na kumuacha hotelini vijana wetu aliingia na kumnyonya damu na kumchuna ngozi yake.
"Biashara hii inatuingizia pesa nyingi sana hasa baada ya wakubwa wengi kuathirika na ugonjwa wa ukimwi. Katika watu walioliingizia faida kubwa ulikuwa wewe hivyo tulikuandaalia asante lakini ajabu ulipotea kiajabu.
"Mradi wetu wa uuzaji wa damu nchi za nje uliingia dosari baada ya kugundua damu nyingi za watu wazima zimeathirika hivyo ndivyo tulivyobuni njia nyingine ya kupata damu iliyo safi kwa kuanzisha mradi wa kukusanya vijana kwa njia ya kuwapeleka nje kusoma au kufanya kazi.
"Kutokana na jinsi tulivyojijenga wazazi wao hawakuwa na pingamizi njia ile ilitusaidia kupata damu iliyo safi na biashara ya ngozi za watu. Ndani ya miaka mitano tulitengeneza pesa nyingi sana. Hakukuwa na biashara hiyo tu vilevile tulitumia kivuli cha kanisa kuingizia dawa za kulevya pamoja na kusafirisha madini na nyara za serikali nje.
"Ukweli kivuli cha dini kilituingizia pesa nyingi mpaka leo hii ni nani atayeamini kuwa sisi tunahusika na kazi hii hata mheshimiwa Rais sijui kitu zaidi ya kutupa ushirikiano na yeyote aliyetaka kufuatilia nyendo zetu tulimpoteza.
"Muungano wetu uliingia ufa miaka miwili iliyopita ufa baada ya wenzetu wanne kujitoa ambao waliweka mpasuko mkubwa. Mpasuko huo ulisababisha hata biashara yetu ya damu na ngozi za watu zikose soko na kusababisha tupate hasara ya trion 20.
“Vilevile kupotea mkataba wa trilioni 150 ambazo ni malipo yetu ya uuzwaji wa damu, ngozi, pembe na madini tuliyo wapelikea mawakala wetu.
"Hizo zilikuwa njama za wenzetu manne waliojitoa hasa Marry White ambaye ni mpenzi wa bosi wa shirika tuliokuwa tunawapelekea vitu vyetu. Cha kushangaza disc iliyokuwa na mkataba wa malipo ilipotea katika mazingira ya kutatanisha hata kumbukumbu nazo zilikuwa zimefutwa kwenye Computa.
"Tuliogopa kuwajulisha tumepoteza disc hata kumbukumbu, Mary White na wenzake wana mpango wa kuchukua zile hela ambazo ni nyingi sana. Kama watazichukua litakuwa pigo kubwa kwetu.
"Cha kufanya ni kuhakikisha watu hawa wanauwawa vilevile utumie ujuzi wako uweze kupata mkataba huu ambao upo katika ofisi za mawakala wetu. Utafanyaje? Sisi hatujui ndio maana tumekupa mafunzo mazito tofauti. Watu hawa ni hatari mafunzo yao na wewe hayatofautiani sana ila yako yamezidi.
"Ila wao ni wazoefu na kazi za mauaji ni watu makini sana hawana mchezo hasa Marry White ni mwanamke hatari sana hasa akigundua wewe ni adui yake anaweza kukufuata huku huku na kukumaliza..
"Mwanzo tuliwatumia vijana wetu wenye uwezo mdogo walikufa kama nzige, wengine walikufa hapahapa siku tuliyopanga waondoke ndio siku waliouawa kinyama.
Kitu kilichotutisha na kujua vita hii ni nzito ambayo inahitaji kujipanga vizuri.
Uamuzi tuliouchukua ndio wa kukuandaa wewe ili ukabiliane na tatizo lililo mbele yetu tuna imani kubwa na wewe kuwa utaiweza.”
Muda wote aliokuwa akiongea Father Gin macho yake yalikuwa hayachezi mbali na paji la uso wangu, nami vilevile sikuchezesha macho yangu zaidi ya kumwangalia na kumsikiliza kwa makini habari ambazo zilinisisimua.
Sio siri habari zile zilifanya nimkumbuke mzee wangu mtu niliye muona ana umuhimu wa pekee mzee Utakufalini. Maelezo yao yalikuwa sawasawa na aliyonieleza juu ya kugundua unyonyaji wa damu na uchunaji wa ngozi za binadamu. Hapo ndipo nilipogundua muuaji harisi wa familia ya mzee Utakufalini ni Father Gin.
Akili yangu uligundua kitu kingine na kuona kumbe duniani wapo watu wanaotumia vivuli vya ukarimu ili kuficha maovu yao, tena wanatumia vivuli vya udini au taasisi ili kuifumba macho serikali na wananchi wake.
"Thereza," nilishtushwa na sauti nzito ya Father Gin.
"A..bee," nilikuwa kama natoka ndotoni.
"Naona upo mbali vipi umenielewa?”
"Ni kweli"...maana kazi iliyopo mbele ni sawa na kuchezea ndani ya kinywa cha mauti."
“Usemayo ni kweli ndio maana tumekupa mafunzo ya kutosha ili kukabiliana nayo vilevile tumetoa malipo manono kwa kuzingatia uzito wa kazi.”
“Sasa ni hivi.." Father Gin alinyamaza kidogo na kupiga funda mbili za Whisky kisha aliendelea kusema:
"Thereza, nilikuwa sijamaliza maelezo yangu."
"Endelea tu Father."
"Mpasuko uliotokea kwenye kikundi chetu umesababisha shughuli zetu zote zisimame hata uvunaji wa vijana nao ulisimama ilibidi tutafute sehemu tuwahifadhi hao vijana ili kusubiri hali ikitulia tuweze kuvuna damu na ngozi na hakuna njia nyingine ni kuwaua hawa watu wanne Marry White na wenzake ambao wote wapo Italy na England.
“Ukifanikiwa kuwaua hawa utakuwa na kazi nyingine ya kwenda Ujerumani ambapo ndipo makuu ya wakala wetu mnunuzi mkuu wa vitu vyote tunavyo vivuna hapa nchini na nchi zingine za Afrika.
“Matawi yetu yapo Kenya, Uganda, Sudan, Afrika ya kusini, Nigeria na Senegal. Sehemu zote hizi tuna wakala wetu wanaokusanya watoto wa kivuli cha kituo cha kulelea watoto wenye maisha magumu. Ukweli mradi huu umetuingizia pesa nyingi sana, mradi wenye siri kubwa iliyojificha nyuma ya pazia. Na sio kwamba hakuna mawakala wengine ila tunaogopa tukibadili wakala hapo lazima tutapoteza pesa zetu trilion 150.
Sijui una swali lolote juu ya yote niliyokuileza?" Father Gin aliniuliza.
Kabla ya kuuliza swali nilikohoa kidogo kisha niliuliza.
"Samahani Father Gin."
"Bila samahani."
"Unataka kunieleza kuwa kuna baadhi ya watu waliouawa ndani na nje ya nchi pale wanapotaka kufuatilia jambo hili kati ya hao kuna mtu aliyepata mwanga wowote?"
"Hakuna."
"Hao ulio watuma wana ujuzi gani?"
"Ujuzi wao si mkubwa sana ila ni wazoefu.”
"Huoni kama uliwauza?" nilimuuliza swali.
"Kuwauza kivipi?”
"Utampelikaje mtu akapambane na mtu aliyemzidi uwezo?”
‘”Tulifanya kama shambulizi la kushtukiza.”
“Kama shambulizi la kushtukiza iweje wafe kirahisi namna ile?”
“Kwa kweli hata sisi ilitushitua.”
"Usinichekeshe Father Gin iliwashtua kivipi ikiwa bado mliendelea kuwatumia vijana wasio na ujuzi, mbaya zaidi unasema waliuawa hapahapa nyumbani kabla hawajaondoka huoni vita ipo hapahapa wala sio huko mnapotutuma?”
“Maneno yako ni mazito uliyosema sio kwamba tulikuwa na nia mbaya na wote walio uawa, ukweli tulichanganyikiwa tusijue nini cha kufanya," Father Gin alijitetea baada ya kumbana.
"Si kweli siwezi kukubaliana na usemacho yaani watu wanne wawazidi akili watu kumi na mbili tena inafikia hatua watu wanaingia mpaka ndani, nauliza adui yupo wapi ili nikianza kumtafuta nijue na mtafutia wapi?"
"Swali lako ni gumu."
“Kama unaelewa au huna habari ndani ya kikao hiki kuna watu wanatoa siri za kikao hivyo hakuna kitu kitachofanyika. Hata nikikubali nitakuwa nimesaini kifo, nitawezaje
kupigana na mtu nisiyemjua, naye ananijua vizuri mbaya yeye
yupo gizani mimi nipo peupe naonekana. Hamuoni hapo nakichezea kifo, ni wazi adui yenu anawaeleweni vizuri, kuliko ninyi mnavyo muelewa yeye.
“Nikinukuu kauli yako kuwa Marry White anatisha yupo tayari kumfuata
adui yakepopote alipo pale atapojua unamtafuta ni wazi anajua kuwa
mimi nimeandaliwa kwa ajili yao lazima watanizima kabla sijaianza
kazi yenyewe.
“Kwa nini hakunieleza mapema wala nisingekubali kupoteza muda wangu kwenye
mafunzo, nitawezaje kushindana na mtu anaye nifahamu. Inasikitisha mtandao mzito kama huu siri zenu zivuje. Lazima mchunguzane wenyewe kwa hali hii sipo tayari kuifanya kazi hii vilevile nipo tayari kuwalipeni gharama zenu zote."
"Usifike huko Thereza wewe ndiye tegemeo pekee la kundi letu tutakulinda."
"Usinichekeshe, mmeshindwa vipi hao mniweze mimi kwa taarifa yenu sitasaini mkataba vilevile nawahakikishieni siri hii itabakia moyoni mwangu mpaka naingia kaburini ila onyo mtu yoyote asinifuatilie nyendo zangu tutaonana wabaya," mtoto wa kike nilitoa mkwara mzito.
"Thereza usifanye hivyo basi sema unataka kiasi gani zaidi ya Bilioni 100 sema tupo tayari kukupa."
“Father Gin nielewe, ukitaka tuongelee habari ya kazi uondoe unafiki ndani ya kundi lako hapo tutakuwa tayari kuifanya kazi yako."
"S...sa....asa..."
"Hakuna cha sasa fanyia kazi niliyo kueleza kwa heri."
Nilinyanyuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Wote walibakia midomo wazi, nilitoka hadi ofisini kwa Dk Ray.

Itaendelea
 
SEHEMU: 18
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500
ILIPOISHIA:
"Thereza usifanye hivyo basi sema unataka kiasi gani zaidi ya Bilioni 100 sema tupo tayari kukupa."
“Father Gin nielewe, ukitaka tuongelee habari ya kazi uondoe unafiki ndani ya kundi lako hapo tutakuwa tayari kuifanya kazi yako."
"S...sa....asa..."
"Hakuna cha sasa fanyia kazi niliyo kueleza kwaheri."
Nilinyanyuka na kuondoka bila kugeuka nyuma. Wote walibakia midomo wazi, nilitoka hadi ofisini kwa Dk Ray.
SASA ENDELEA...

"Vipi mmemalizana?"
"Sifanyi kazi ya kitoto."
"Mbona sikuelewi?"
''Unajua hao sijui mabosi wako wanathamini masirahi yao kuliko uhai wa mtu ambaye ndio muhimu kuliko kitu chochote.”
"Teddy mbona unazidi kunichanganya."
“Sikuchanganyi bali ninyi ndio mnataka kunichanganya.”
"Kivipi?"
"Kinachotokea kwenye kundi kama sio kugeukana ni nini iweje mtu auawe kabla ya kazi ni nani aliye toa siri kama sio ninyi kwa ninyi, mnataka mnimtoe sadaka?”
"Wacha woga nina imani mafunzo yaliyokutoa woga."
"Sio kwa mtindo huu."
"Kwa hiyo?"
"Kazi siifanyi na gharama zenu zote nijulisheni ni kiasi gani ili niwalipe," nilisema kwa jeuri.
"Thereza ni kweli usemayo lakini ni mapema sana fikiria mara mbili"
"Kwanza Ray wale vijana mliowaandaa kwa ajili ya kuvuna damu na ngozi wapo wapi?"
"Wapo kijiji cha Farijika."
"Mnawavuna toka vijijini?"
"Kapana."
''Mnawatoa wapi?"
“Sasa hivi tuna muundo mpya wa kupita vituo vyote vya kulelea watoto wa mitaani na kukusanya wale wakubwa kwa kisingizio kuna chuo tumeanzisha kwa ajili ya stadi za kazi. Tukiwachukua baada ya muda huvuna damu na ngozi."
"Ooh vizuri wacha niende."
“Sasa vipi kuhusu hiyo kazi?"
"Tafuteni mtu mwingine."
"Thereza usicheze na Father Gin utakufa kifo kibaya."
"Hiyo itakuwa kesi nyingine.''
Nilimuacha Dk Ray macho yamemtoka pima, niliingia kwenye gari langu na safari ya mjini ilianza. Nikiwa njiani nilikuwa na mawazo mengi juu ya miradi haramu ya Father Gin na kikundi chake mtu niliyekuwa namheshimu kutokana na tabia yake ya upole ukarimu anayejali watu kumbe ni subiani mkubwa mnyonya damu za watu.
Roho iliuma kuona kumbe vijana wadogo wanakusanywa wakidhani wanapewa misaada kumbe ni mavuno yao ya damu na ngozi. Suala la kuwakusanya vijana ili kutengeneza vuno la damu na ngozi toka kwenye vituo vya kuletea watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu liliniumiza kichwa.
Lilifanya mwili usisike na kuona hata katika vituo vyangu vya kulelea watoto wa mtaani wameisha nyofoa baadhi ya vijana wangu kwa kisingizio cha kuwapa stadi za kazi. Mwili ulinisisimka nikaona kuna umuhimu kuwaita wakuu wote wa vituo vyote vilio chini yangu niwaulize ni watoto wangapi wamechukuliwa.
Najua utajiuliza nini hatima yangu ya kukataa kuifanya ile kazi na kulikataa donge nono la bilioni 100. Wasiwasi wangu ulikuwa ni uamuzi wa Father Gin juu yangu. Kukataa kule nilikuwa na maana yangu tulia utaijua sasa hivi.
Mafunzo ya mwaka mzima yalinijenga kimwili na akili, niliamua kurudi nyumbani
kwangu kupumzisha akili. Nilipofika nyumbani nilioga kula na kulala ili kujipumzisha akili. Simu ya getini alilia nilinyanyuka na kuipokea.
"Unasemaje Joe?" nilimuuliza mlinzi wangu mtiifu.
"Kuna wageni."
"Waulize ni kina nani," nilimsikia akiwauliza:
"Madamu ni Father Gin na Doctor Ray."
Kusikia vile nilishtuka kidogo, baada ya kushusha pumzi nilimjibu:
"Waruhusu,” nilijinyanyua kitandani na kuelekea bafuni kuondoa uchovu kisha nilirudi chumbani na kujifunga koti langu jepesi la kulalia na kuteremka chini kuonana na wageni wangu. Niliwakuta sebuleni, nilipo waona niliwakaribisha kwa tabasamu pana.
"Karibuni sana."
"Asante sana." walijibu kwa pamoja.
"Sijui wageni wangu mnatumia vinywaji gani?" niliwauliza.
"Mimi hapana," alijibu Father Gin.
"Hata mimi nashukuru."
"Haya kama hamtaki leteni habari najua mna mengi nyuso
zenu zinajionyesha,” niliwauliza swali kwa vile nilijua lazima kile kitu kitatokea.
"Ni kweli, uamuzi wako sikuutegemea umenichanganya sana," alisema father Gin.
"Wa kuchanganyikiwa ni wewe au mimi ambaye ndiye unaye ninadi uhai wangu kwa bei nafuu."
“Sema chochote utakavyo ili tu kazi yangu ifanyike."
"Sio kwamba kazi sitaifanya.”
"Ila?"
"Pale nimeikataa makusudi lazima uelewe wenzio wanakuzunguruka we hujiulizi kwa nini siri inavuja?" nilimpa siri ya kukataa mbele ya wenzake.
“Kwa hiyo unataka kusemaje?"
"Kazi ipo palepale, ilibidi nilikatae ili kama kuna msaliti ajue sitaifanya japo najua bado nitafuatiliwa ili nitolewe uhai."
"Kazi nitaifanya ila nataka maelezo kamili ya adui zangu picha zao na wanaishi wapi ili kazi ianze mara moja."
"Ooh! Siamini maneno yako kweli wewe umetuzidi akili kwa kulijua tusilo lijua, vipi kuhusu mkataba?" aniuliza Father Gin.
"Kesho kama kawaida nitapofuata maelezo ya kazi kama ulivyo nieleza mambo yote anayo Dk Ray."
"Hamna taabu, siku njema."
"Nanyi pia," niliagana nao nami nilirudi ndani kujipumzisha.
Asubuhi siku ya pili niliamka na kwenda kibaha. Nilipofika bila kuchelewa nilipewa maelezo ya adui zangu picha zao na ramani ya miji wanayokaa. Niliingia mkataba wa shilingi bilioni 100 pale nililipwa bilioni 60 taslimu. Nilipotaka kuondoka Dk Ray alinieleza mengine mapya.
"Thereza kutokana na mapenzi mazito juu yako imebidi niuweke rehani uhai wangu."
“Una maana gani?"
"Kuna siri moja ambayo kila nikikuangalia moyo unaniuma hivyo nipo tayari kufa kwa ajili hivyo, nipo tayari kufa kwa ajili yako....najua nitahatarisha maisha yangu sina budi
kukupa siri hii."
Kauli na Dk Ray ilinishtua na kujiuliza ni siri gani itayo hatarisha maisha yake.
''Dk Ray ni siri gani hiyo mbona unanitisha?”
"Thereza hapo si sehemu yake nitakuja kwako usiku ili nikupe siri ambayo nina imani
inaweza kuchukuwa uhai wangu."
“Hakuna taabu nitakusubiri kwa hamu.”
Niliagana na Dk Ray na kurudi Dar. Nilipita vituo vyote kuchukua taarifa ya watoto walioingia na waliotoka. Baada ya kufika nyumbani nilipitia taarifa zote za vituo vilivyo chini yangu. Moyo ulinipasuka kukuta watoto zaidi ya watoto tisini wamechukuliwa na Father Gin kwa ajili ya kuvuna damu na ngozi.
Nilijiapiza kuwa si watoto wangu tu hata hao wa vituo vingine nitahakikisha
hawanyonywi damu na kuchunwa ngozi. Nilijua mimi ndiye mwenye dhamana ya
kuokoa uhai wao. Nilipanga kabla ya kuondoka nitamdanganya Father Gin
tuwatembelee watoto ili niwaone vilevile kujua mandhari yake iko vipi ili nijue
jinsi ya kuwakomboa.
Siku ile saa nne na nusu usiku Dk Ray alifika nyumbani kwangu. Nilimkaribisha sebuleni, nilimkaribisha kinywaji kikali ambacho nilikiandaa kwa ajili yake.
"Karibu sana Dk Ray.”
"Asante sana mrembo."
Tukiwa tunapata vinywaji yeye vinywaji vikali mimi nilikuwa na malta guiness.
"Dk Ray nina imani una siri nzito moyoni mwako ambayo unaonyesha wazi imekunyima raha toka ulipotamka suala la siri bado uso wako unaonyesha hofu fulani moyoni mwako."
''Ni kweli Thereza."
"Ni siri gani hiyo?"
"Thereza,"aliniita jina langu kwa sauti ya chini huku akifuta mdomo yake kwa mkono.
"Abee."
Baada ya kushusha pumzi na kunywa nusu glasi ya whisky kwa mpigo alisema.
"Thereza kwanza elewa nakupenda zaidi ya kupenda nataka kwanza uelewe hilo."
"Nashukuru kwa kunipenda," nilimjubu kwa sauti ya upole.
"Thereza wala si utani ni mapenzi yangu ya chini ya moyo wangu."
“Nashukuru nami nakupenda pia.”
"Sasa Thereza upo tayari kuwa na mimi?"
“Si tatizo ni suala la maamuzi tu hilo usihofu."
"Thereza japo nina imani penzi langu kwako sitalifaidi."
"Kwa nini?”
"Kifo kipo mbele yangu."
"Una maana gani kusema hivyo?"
Wakati huo Mr Ray alikuwa akibugia whisky kwa pupa hata sauti yake ilionyesha ameanza kulewa.
"Si unakumbuka vizuri kiapo ulicho kula kwenye mkutano?"
''Ndiyo."
"Walisema hawatasita kumuua mtu yoyote atayetoa siri ya kikundi?"
"Sasa mimi si mwanachama wa kikundi siri itakuwa ndani ya kikundi."
"Thereza hiki kikundi nakijua mimi vizuri, zipo siri zinazojulikana na zipo siri sirini
ambazo tunazijua sisi tu."
"Mmh, siri sirini?"
"Ndiyo Thereza, kama nikikueleza na wakijua lazima wataniua.”
"Basi haina haja ya kunieleza siri itayohatarisha maisha yako."
"Kama nitakaa kimya itahatarisha maisha yako."
''Maisha yangu! Kivipi?”"
"Eeh, ndiyo."
"Mungu wangu ni siri gani hiyo unayofanya mwili wangu kusisimka na kujawa na hofu kubwa?"
"Thereza bila mapenzi yangu ya dhati juu yako nisingekueleza siri hii vilevile wewe unanihusu mimi sana kuliko mtu yoyote. Pia nina imani ukivuka salama nami nikavuka mtihani ulio mbele yangu tutafunga ndoa, “ alimimina mdomoni whisky iliyokuwa imebakia kwenye glasi na kuniita jina langu kwa sauti ya kilevi:
"Thereza."
"Abee."
''Najua undi hili unalielewa juujuu siku zote jasusi hana rafiki, siku zote anajali masilahi yake..anachojali kazi yake unapoimaliza lazima apoteze ushahidi."
"Kupoteza ushahidi una maana gani?"
"Swali zuri Thereza, siku zote jasusi huwa hajiingizi kwenye kazi zenye ushahidi, humtumia mtu. Ili kufanyiwa kazi hutangaza malipo mazuri yatayomshawishi
mtu aifanye kazi lakini mwisho wa kazi unapowajulisha kazi imekwisha hapo ndipo hukuua ili kupoteza shahidi."
"Eti kufanya nini?" nilishtuka.
"Kukuua ili kupoteza ushahidi ikiwa pamoja na kuchukua pesa zao zote walizokupa kupitia watumishi wa benki ambao ni mawakala wao ambao huwalipa asilimia fulani ya pesa zile."
Habari zile zilinishtua sana zilikuwa mpya kabisa maishani mwangu ambazo sikutarajia kuzisikia. Nakubaliana na usemi wa Dr Ray Jasusi hana rafiki pia jasusi hafanyi biashara ya hasara. Macho na masikio yalifunguka.
"Dr Ray una ushahidi na unayosema?" Nilimuuliza nikiwa nimemkazia macho.
"Ndiyo, wengi wameuawa baada ya kufanya kazi na kudhulumiwa malipo yao. Japo
wamekupeleka mafunzoni nia yao ni kufanikisha kazi yao ukiimaliza ujue na we ndio mwisho wa maisha yako."
"Hivi wale watu mnaowachuna ngozi na kuwanyonya damu mnawazika wapi?" nilibadili mada kwa faida yangu.
"Kuna tanuru kwa ajili ya kuchoma miili yao na ikisha kuwa jivu tunaitupa baharini.
"Dr Ray unaweza kunisaidia vipi maana hata sijui nifanye nini hata najuta kuingia
mkataba, ningeyajua haya mapema nisingekubali, bora ningeendeleza msimamo wangu," niliingiwa wasiwasi na taarifa ile.
"Bora umekubali wangekuua."
"Na kuhusu pesa nitazilindaje?"

Itaendelea
 
SEHEMU: 19
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
"Kuna tanuru kwa ajili ya kuchoma miili yao na ikisha kuwa jivu tunaitupa baharini.
"Dr Ray unaweza kunisaidia vipi maana hata sijui nifanye nini hata najuta kuingia
mkataba, ningeyajua haya mapema nisingekubali, bora ningeendeleza msimamo wangu," niliingiwa wasiwasi na taarifa ile.
"Bora umekubali wangekuua."
"Na kuhusu pesa nitazilindaje?"
SASA ENDELEA...

"Ni rahisi zibadili kwenye akaunti ubadili na jina ukiwezakana weka mafungu hata kumi benki tofauti hapo utakuwa umewaweza tena kwa majina tofauti."
"Nini kingine cha muhimu hiki ni muhimu 'pass word' zitakusaidia sana hasa hii ya
Father Gin yule si Father bali Jasusi Gin anayepaka matope dini za watu yule ni shetani sijui kwa Mungu atajibu nini juu ya roho za watu alizozipoteza”
Dr Ray alinipa pass word zaidi ya tano za shirika lile la ujasusi ambalo halikuwa la dini kama linavyojulikana. Ndiyo maana hata Bwana Yesu kabla ya kuondoka alitutaadharisha na watu wataojinadi kwa jina lake hao tusiwaamini na ndio wanaochafua watu wa kweli walio wasafi mbele ya bwana.
Nilikumbuka kile kikao watu wanaonekana wasafi mbele ya dini zao kumbe wanyonya damu ukiwakuta mbele ya waumini wao wanavyo mtukuza Mungu kumbe mashetani.
Lakini kwa Mungu kila kitu kitalipwa kulingana na matendo yao, Mungu si mwongo wala si mtani wa mtu, ipo siku kweli itadhihiri hata ufanye gizani.
"Dr Ray ulijuana vipi na Father Gin?"
"Of course yule Father Gin alinichukua kutoka chuo cha ujasusi kazi yangu kubwa
ilikuwa kuwatibu watu wote walio chini yake, hasa kuzingatia kazi ya ujasusi ni ya
hatari yenye majeraha na makovu mengi.
"Ili kupoteza lengo tulijenga hospitali kubwa Kibaha na kuwahudumia watu wote lakini ni kituo cha ujasusi,” Dr Ray akionekana pombe zimemkolea aliongea kwa sauti ya huzuni.
"Thereza."
"Unasemaje?"
"Naomba uniahidi kama utakuwa tayari kufa kwa ajili yangu kwani na mimi nimejitoa kwa ajili yako."
"Dr Ray makuahidi."
"Basi kama nitakufa atayeniua si mwingine ila Father Gin na kuomba umuue kwa mkono wako."
"Nakuahidi nitafanya hivyo."
“Thereza naomba penzi lako kwa usiku huu japo sina uhakika kama nitauona usiku
wa kesho,” Dk Ray alizungumza kwa sauti iliyokata tamaa.
"Usihofu mpenzi leo mwili wangu utakuwa mali yako na tukivuka mtihani uliopo mbele yangu na yako ruksa kunivisha pete."
"Mpaka hapo hata kama nitakufa basi nitakufa moyo wangu ukiwa shwali nina imani
penzi lako lina thamani kwangu kuliko uhai wangu."
Nilimshika mkono na kupanda naye juu, baada ya kuongea tulioga pamoja na kujilaza
Kilichofuata nilimpa alichokitaka. Asubuhi baada ya supu zito na kuzimua na whisky Dk Ray aliniaga akiwa na furaha moyoni nina imani unajua nini kilichomfurahisha.
Baada ya kuondoka nami nilioga na kujiandaa kukabiliana na kilicho mbele yangu nilijiona nimo ndani ya kinywa cha mauti na uwezekano wa kutoka ni mdogo sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano kwani vifo vilikuwa nyuma na mbele sidhani kama vyote nitaweza kuvikwepa.
Penzi langu kwa Mr Ray si penzi la moyoni, kwangu kama shukurani ya kunifungua
macho. Yeye alikuwa na mapenzi ya kweli moyoni mwake na kuwa tayari kufa juu yangu.
Sikuwa na budi kuonyesha mapenzi ya dhati juu yake japo siyo moyoni bali ya kuunda kwa kipindi kile yeye alikuwa mtu muhimu sana ambaye alinisaidia kuyajua
mengi . Lakini mwanzo alinisaidia kwa ajili ya kuwafanyia kazi zao.
Japo Mungu kanijalia uzuri wa shani unaowazuzua wanaume wengi, nilishangaa
kwa kauli yake kuwa anipenda mtu aliyezichezea sehemu zangu za siri mara nyingi sikujua nini kilichomvutia kwangu.
Niliingia chumba changu nilicho kiteua kwa kazi zangu za kijasusi, chumba ambacho
nilikifunga mitambo ya mawasiliano. Nilizichukua zile picha tano za watu wanaotakiwa kuuawa.
Niliwaangalia kati ya hao watano walikuwa wazungu mmoja ndiye alikuwa mweusi kama mimi. Wote walionekana watu wa makamo kasoro msichana Marry White alikuwa umri kama wangu kama kunizidi ni miaka miwili. Baada ya kuzihifadhi picha zote kichwani nilianza kuangalia ramani na mitaa.
Walikuwa wanaoishi maelezo yaliyonionyesha nitateremka katika uwanja wa ndege wa London na kufikia hotel ya Browns Hotel London. Ofisi za wabaya zangu zilikuwa jirani mtaa wa Regent.
Na Italy nishukie uwanje wa ndege wa Rome na kupanga kwenye Hotel iliyo jirani na
uwanja huo wa ARZEMIDE. Na Ujerumani ilionyesha nishukie uwanja wa ndege wa
Pusseldorf ulio katika mji wa Dusseldorf. Na kupanga hotel ya karibu ya RADISSON SAS HOTEL DUSSELDORF. Iliyopo kwenye mtaa wa Kaiserwerther.
Baada ya kuihifadhi ile ramani kwenye kumbukumbu za ubongo wangu. Nilipata
kifungua kinywa nikiwa napata kifungua kinywa wazo moja lilinijia ni muhimu kujua
mazingira watoto wale waliotunzwa kwa ajili ya kuvunwa damuna ngozi hapo baadaye. Niliona haina haja ya kumshirikisha tena Father Gin juu ya safari yangu
kuwatembelea wale watoto.
Nilimuona Dk Ray anafaa sana ni muhimu anaweza kunisaidia zaidi, nilimpigia
simu.
"Vipi honey mzima?"
"Wa afya sijui wewe ua la moyo wangu."
"Mimi mzima ni hivi upo kazini?”
"Ndiyo"
"Nakuja sasa hivi nina shida na wewe."
"Nipo nimejaa tele kama pishi la mchele," kidogo nicheke Mzungu ana maneno kama
Mswahili.
Basi nakuja mpenzi."
"Ila usije moja kwa moja ofisini teremkia mbali na uje kwa kupitia mlango wa nyuma."
"Sawa," nilikata simu.
Sikuwa na muda wa kupoteza nilikodi gari, sikuwa na haja ya kwenda na gari
langu nilijiona kama nimeishaianza kazi, nilianza kwenda mwendo wa machale, kama nilivyo elekezwa na Dk Ray.
Niliwasiri Kibaha baada ya nusu saa niliteremkia mbali na kutembea kwa miguu hadi pale hospitali tena nilipitia kwa nyuma. Nilipofika ofisini nilikutana na pigo la mwaka mwili wa Dk Ray ulikuwa umelazwa juu ya meza ukiwa umetenganishwa na kichwa matumbo yakiwa nje.
Kengele ya hatari ililia kichwani kuonesha shughuli imeshaanza, nikiwa bado nimepigwa na bumbuwazi mara nilisikia sauti za watu wakiongea nje ya chumba.
"Hivi huyu malaya wake atakuja saa ngapi? Unajua sister tumemuahidi kazi itakuwa ya saa moja." mmoja alimuuliza mwenzake.
"Atakuwa amepitia wapi au tumfuate kwake?" Mwingine alichangia.
"Tunaweza kuchengana naye tumsubiri namba yake ya simu si unayo tumpigie tukijifanya Doctor Ray we nakuamini kwa kuigiza sauti za watu."
Kusikia vile moyo ulinipasuka nilijua nitajulikana, niliitoa simu haraka
na kuizima nilijua kwa mtindo huo wamenikosa. Nilimsikia mmoja akisema:
"Unajua Marc sio siri inavyoonekana huyu msichana ni mtu hatari sana, kwani hata
sister Marry White alionyesha jinsi anavyomuhofia.”
"Inawezekana machale yamemcheza hata simu yake haipatikani."
"Ingia ndani ukaangalie namba kwenye simu ya Doctor Ray kama zinalingana."
"Nilijua shughuli rasmi imeanza nilijibanza nyuma ya mlango, sauti za nyayo za viatu nilizisikia zikisogelea mlango wa ofisi, mara mlango ulifunguliwa aliingia kijana aliyeonyesha mwili wa mazoezi alikwenda kwenye meza ili achukue simu iliyokuwepo juu ya meza pembeni na mwili wa Dr Ray.
Niliurudisha mlango kwa mguu, nilimsogelea kidogo nikijua sehemu ile teke la
kuzunguka litampata vizuri. Nilikohoa ili ageuke na kuweka vizuri kisogo chake.
Alipogeuka kabla hajashangaa niligeuka na teke mzunguko lililompata kwenye kisogo. Hakuwahi kupiga hata kelele alikuwa mgeni wa kuzimu. Nilimlaza pembeni na kumsubiri wa pili niliyemsikia akimwita mwenzake:
"Marc vipi mwaka mzima?"
"Tunapoteza muda kama vipi tumfuate kwake."
Alipoona kimya aliingia mwenyewe alionyesha hakujiandaa, aliingia kizembe
ilionyesha alijiamini sana. Alipoingia alishangaa kutomuona mwenzake
alimwita.
"Marc," ilimwita kwa sauti ya juu kidogo.
"Unasemaje?" niliitikia, alipogeuka nusra azirai kwa mshtuko alikuwa kama ananifananisha.
"Wewe ni Thereza?"
"Ndiyo mimi."
"Marc yupo wapi?"
"Wanaongea lugha moja na Doctor Ray."
"Yaa..ani umemuua?" Aliniuliza macho yamemtoka pima.
"Sijui muulize mwenyewe,"nilimjibu kwa dharau.
"Sikubalii," alichomoa kisu.
"Aaah... Aibu mwanaume mzima uliyekamilika unanibebea kisu mtoto wa kike."
Kauli yangu ilimfanya aone aibu na kukitupa kisu pembeni alivua fulana
iliyo kuwa imembana na kuuonyesha mwili wake uliojengeka kimazoezi.
Nilijua lazima atapigana kwa pupa alinifuata kama mbogo na kutupa ngumi nzito iliyotoa mlio wa kukata upepo iliponikosa. Niliinama na kumpiga kiwiko cha kuzunguka kwenye mbavu changa alizozinyoosha wakati wa kupiga ngumi. Nilimsikia akiguna kwa maumivu.
Alipopiga ngumi nyingine niliiongezea na teke kwenye maungio aliongeza kilio
Kingine. Mkono ulipoteremka ulikuwa umelegea nilijua nimeshauvunja.
Nilimalizia na teke la kuzunguka la chini lililomrusha juu na kuanguka chini kama mzigo. Nilimfuata na kumuongeza ngumi mfurulizo zilizomlegeza. Nilimfuata na kumuuliza:
"Marry White yupo wapi?" nilimuuliza kwa sauti ya ukali kidogo, lakini hakujibu alionesha kiburi.
"Aaah unajifanya nunda siyo?"
Wakati huo hasira zilikuwa zimenipanda nilitamani kunywa damu ya mtu, mauaji ya Dk Ray yaliniongezea hasira.
"Utanijibu hunijibu?"
Aliendelea kuwa kimya, niligeuka kufuata kisu, akili yangu ilicheza na yeye siku zote
jasusi yoyote hakubali kufa kikondoo. Nilipogeuza uso nilikuta ndio anapeleka mkono wa kulia mdomoni kwa vile wa kushoto nilikwisha uvunja, Niliruka kama mkizi na kufanikiwa kuupiga pembeni alichotaka kukimeza ili ajiue. Nilimshikia kile kisu na kumuuliza.
"Nakuuliza kwa mara ya mwisho Marry White yupo wapi?"
"We niue tu mi sijui," alionesha kiburi cha hali ya juu.
"Aah unafanya utani siyo?"
Niliingiza kisu katika jereha lake la jichoni, maumivu yalipozidi alipiga kelele:
"Utaniua bure, we niue kabisa kuliko kunitesa hivi mi’ sijui lolote."
"Nitalitoa jicho kama utaleta kitu kujua," wakati huo nilikuwa nakandamiza kisu kwenye jeraha. Yule mtu alipiga kelele za maumivu makali.
"Ooh!Niache nitakueleza."
Nilikichomoa kile kisu kilichokuwa kimeingia robo tatu, wakati huo damu zilikuwa zikizidi kutoka kwenye jeraha.
"Haya ongea."
"Nimeamini kweli wewe mtu hatari sifa na hofu alizoonyesha sister Marry White nilifikiria ni uongo kweli dada unatisha,"alisema yule jamaa huku anauma meno kwa maumivu makali.
"Sikuja kusifiwa hapa nieleze Marry White yupo wapi?”
"Yupo Nairobi."
"Nairobi anafanya nini?"
"Sijui ila alisema mpaka jioni atakuwa Arusha."
“Yupo sehemu gani pale Nairobi?"
"Huwezi kumuwahi ila jioni ya leo wana kikao kingine Arusha."
"Vikao vyao vinahusu nini?"
"Ukweli mimi sijui, sisi kazi yetu kubwa ni kutumwa kufanya mauaji."
"Ooh, vizuri, mmeshaua watu wangapi?"
"Sisi kama tungekuua wewe ungekuwa wa sita."
"Ina maana wapo wengine?"
"Tupo wengi."
"Kwa nini mlitumwa kuniua mimi?"
"Ujuzi tunatofautiana hivyo sisi ndio tulioonekana tupo juu kutumia silaha hata mapigano ya mikono."
"Mbona unaonekana cha mtoto hata hujui kupigana?" Nilimdhihaki.
"Wewe unatisha ningejua uwezo wako uko hivi wala nisingedhubutu kuja kunadi uhai wangu kwa bei ya bure."
"Nieleze hapa mjini mpo wangapi?"
"Tupo sita."
"Wengine wapo wapi?"
"Wanafuatilia biashara za bosi."
"Biashara gani hiyo?"
"Ya kukusanya vijana" kusikia vile nilishtuka.
"Hao vijana mnawakusanya ili iweje?"
"Kwa kweli hapo mimi sijui."
"Acha kuniudhi nieleze ukweli."
"Ukweli sijui ila baada ya kuwakusanya huwapeleka nje kidogo ya mji wa Arusha sehemu hiyo nilishafika mara moja kupeleka watoto. Lakini zaidi ya hapo sielewe mara nyingi tulishawakusanya huwapeleka na tukiwafikisha sisi tunarudi."
"Umesema biashara una maana gani?"
"Mara nyingi hutumia pesa kupewa vijana waliopo kwenye vituo vya kulelea vijana."
"Hii biashara mmeianza lini?"
"Ni mwezi wa sita sasa."
"Mungu wangu!"
"Dada mbona umeshtuka kwani hii biashara ina nini?" Yule mkora aliniuliza.
"Aaah, wacha tu," nilificha ninachokijua.
"Umenieleza wenzio wapo hoteli gani?"
“Wote tupo New African Hoteli."
"Pale mmetumia majina gani?"
"Pale nilipanga chumba kimoja na Marc"
"Wewe unaitwa nani?"
"Zone."
"Ehe na wengine?"
"Yupo Cathy ambaye yupo chumba kimoja na Puchu na Kallo yupo na John."
"Ok, vizuri, umenieleza Arusha sehemu gani?"
"Nje ya Arusha mimi si mwenyeji sana."
"We raia wa wapi?"
"Kenya"
"Umesema mkishakusanya vijana mnarudi lini Arusha?"
"Leo usiku."
"Asante kwa msaada wako."
"Naomba na mimi unikimbize hospitali."
Sikumjibu nilikuwa kama nataka kuondoka niligeuka na teke kali iliyomvunja shingo na kumuwahisha kuzimu. Nilipitia mlango wa nyuma na kutokomea zangu, nilimkuta dereva wangu usingizi umempitia.
"Kaka vipi? Niwahishe Dar."
"Ooh, dada umeisharudi, umesema?" Dereva alikurupuka katika usingizi wa mang'amung'amu.
Dereva aling'oa gari kwa mwendo wa kasi kurudi Dar, njiani nlikuwa na mawazo mengi juu ya vita iliyo mbele yangu nilijua kazi imeisha anza. Kwa maana moja au nyingine niliona kazi yangu huenda ikawa nyepesi hatua za awali baada ya kujua kumbe kundi la Marry White lipo hapahapa Tanzania na shughuli zake anazifanya Arusha.

Itaendelea
 
SEHEMU: 20
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500
...ILIPOISHIA:
Dereva aling'oa gari kwa mwendo wa kasi kurudi Dar, njiani nlikuwa na mwazo mengi juu ya vita iliyo mbele yangu nilijua kazi imeisha anza. Kwa namana moja au nyingine niliona kazi yangu huenda ikawa nyepesi hatua za awali kundi la Marry White lipo hapahapa Tanzania na shughuli zake anazifanya Arusha.
SASA ENDELEA...

Nilipofika nyumbani nilibadili mavazi na kuvaa kama sister na msalaba mkubwa nilipotoka hata dereva alinishangaa.
“Vipi sister unataka usafiri?’
“Acha kujichanganya nipeleke New Africa Hotel.”
“Aah kumbe ni sister.”
“Nani alikuambia mimi ni brother?"
“Sina maana hiyo yaani mtumishi wa kanisa.”
“Utayajua yote we niwahishe.”
Alisimamisha gari kwenye maegesho ya Hotel, niliteremka na kuingia ndani, nilikwenda moja kwa moja hadi mapokezi nilimkuta muhudumu wa kike.
“Habari yako dada,” nilimsalimia.
“Nzuri tu sister.”
“Kuna wageni wangu nimeelezwa wapo hapa.”
“Wapo chumba namba gani?”
“Sikumbuki ila tarehe waliyoingia naikumbukai ilikuwa tarehe...” nilimtajia alipekua kitabu cha wageni.
“Sister majina yanaanzia hapa angalia jina la mgeni wako,” niliinama na kuanza kuangalia majina ya wale wakora niliyaona na kuangalia namba za vyumba vyao. wakati narudisha kitabu nilimsikia yule muhudumu:
“Sister tena unabahati wageni wako hao.” nilipogeuka nilikutana na kijana mmoja aliyejengeka mwili kimazoezi alikuwa amevaa fulana nyeusi ya kubana na msichana mwembamba. Walipotukaribia yule msichana muhudumu alitaka kuwaita, Nilimzuia na kumtaka akae kimya.
“Waache wapite, pale yupo nani na nani?”
“Ina maana huwajui wageni wako?” mhudumu wa mapokezi alinishangaa.
“Ukweli hawa siwajui ila ninao wafahamu ni Marc na Puchu.”
“Wacha wapumzike ili nikawaulize Marc na Zone wapo wapi,” nilitengeneza uongo.
Nilitulia kwenye makochi mapokezi kama dakika tano, nilipoona ule ni muda muafaka nilikwenda moja kwa moja hadi chumba walicho ingia. Sikugonga nilikizusha kitasa ambacho kilikubali na kuusukuma taratibu lakini yenye kasi.
Ajabu chumbani hapakuwepo na mtu zaidi ya nguo kuzikuta ovyo kitandani. Niliurudisha mlango na kukaa tayari kwa lolote. Mara walitoka bafuni kuoga wakiwa amekumbatiana waliponiona walishtuka kidogo yule msichana alisema:
“Sister Marry White umekuja si ulituambia muda huu utakuwa Nairobi?”
Lakini mwanaume alishtuka na kusema:
“Hapana si Sister Marry White, huyu humuoni maji ya kunde?”
“Mimi si Sister Marry White naitwa Thereza yule mliyetumwa na sister Marry White mje mniue,” mo;owajibu huku nikiondoa kilemba kichwani.
Kusikia vile walitaharuki kama ukuta ungekuwa una upenyo wangejipenyeza ili kukimbilia.
“Mungu wangu!” walisema kwa pamoja.
“Msishangae, kwanza hebu nielezeni kabla ya maswali yangu. Mpaka sasa mmeshakusanya watu wangapi ambao mnawapeleka Arusha kwa ajili ya kuwanyonya damu na kuwachuna ngozi?”
Swali langu lilizidi kuwachanganya macho yalinitoka pima. Mara nilisikia mlango ukigongwa nilimwonyesha yule msichana kwa ishara afungue. Msichana aliyekuwa amejifunga taulo lililoziba matiti na chini kuishia chini ya makalio alisogea hadi mlangoni.
Wakati huo nilikuwa nimeshikilia bastola mkononi huku nikifunga kibambo cha kuzuia sauti. Alikuja akitetemeka nilimwambia kwa ishara kwa ukali kidogo afungue.
Aliufungua mlango aliingia msichana mmoja mwenye umbile la kati kama langu alipoingia tu alimrukia shoga yake huku akisema mambo yote tumekamilisha hesabu imetimia jioni safari.
Wakati huo shoga yake taulo lilikuwa limemdondoka kwa woga na kumwacha mtupu kitu kilicho mshtua yule msichana aliyeingia ambaye nilikuwa na uhakika ndiye Kallo
Kallo alipotizama pembeni alishtuka nusra atimue mbio kurudi nje kwa woga. Niliwahi kuusukuma mlango kwa mguu alijibamiza nao na kuanguka chini damu zikimtoka puani na mdomoni.
Aliponyanyuka aliangalia damu mikononi mwake inavyotoka puani na mdomoni nilimwita karibu yangu na kumueleza akae chini.
“Kallo ukweli ndio yataowaokoeni na adhabu ya kifo ila ukifanya kiburi utasafiri kwenda ahera.”
''Kwanza umejuaje jina langu?''
"Kaniambia Sister Marry White."
"Ati?" alishtuka.
'Huu si muda wa kushangaa, kwanza John yupo wapi?" swali lile lilizidi kumchanganya na kujiuliza nimewajuaje.
"Sijui," alijibu kwa mkato.
“Hujui wakati ndiye mwanaume wako mlie kuwa nae kwenye upumbavu wenu.. hivi na ninyi mkinyonywa damu na kuchunwa ngozi mngefurahi au mngekubali?" swali lingine lilizidi kuwachanganya zaidi.
"Au umtoe mdogo wako au mwanao akachunwe ngozi na kunyonywa damu mngekubali?"
“ Eti kaka Puchu?” mtoto wa kiume mdomo ulikuwa mzito nilimgeukia Kallo aliye kuwa karibu yangu.
'En’he, Kallo naomba jibu zuri John yupo wapi?"
"Nimesha kujibu sijui," alijbu kwa kiburi cha kike.
"Hujui eeh, hebu simama."
Alisimama nilijifanya kama nampa mgongo huku nikiongea kwa sauti ya chini"
"Nimeisha...” kabla hajamalizia sentesi niligeuka na kelbu iliyompata sawasawa kwenye shavu la kulia na kumpeleka chini na kuzidi kumtoa damu kwa wingi mdomoni na puani
Ile kelbu ilimfanya alegee, nilimfuata pale chini na kumkwida na kumuuliza kwa hasira zilizokuwa zimeshapanda vibaya, Nilimtikisa huku nikimuuliza kwa ukali.
"John yupo wapi?"
"Yupo n.. n.. nje."
Nilishtushwa na teke zito la Puchu lililonipeleka chini kabla sijasimama aliniongeza mateke ya mfululizo kama manne lakini lililoniingia lilikuwa moja. Niliufyatua mguu wake mmoja na kwenda chini. Hapo chini tulishikana mwenzangu alikuwa na ubavu alininyanyua na kunitupa upande wa pili na kuidondosha bastola niliyo kuwa nimeichomeka kiunoni
Puchu alinirukia na kunipelekea mashambulizi mazito. Siyo siri mwanamume yule alikuwa na mshipa japo ngumi zake nyingi nilizipangua lakini mikono iliwaka moto.
Sikubahatika kujibu mashambulizi zaidi ya kurudi nyuma. Nilipofika ukutani Puchu alidhamilia animalize pale pale.
Ngumi za mbavu za mfululizo zilinilegeza nilimwona akivuta ngumi nzito usawa wa shavu, kwenye masumbwi wanaita krosi ili animalize. Ngumi ile niliiona na kuinama mkono wake ulipiga ukutani nilimsikia akiguna. Nilimpiga teke la nyuma lililomfanya ajigonge uso ukutani, kabla hajageuka nilipitisha teke kwa chini na kumpiga sehemu za siri kwenye hashua.
Alipiga kelele za maumivu na kupiga magoti nilimfuata na kumshika nywele zake na kugeuza shingo yake alionekana amelegea nilimuongeza ngumi kama kumi za mfululizo zilizomtepetesha kabisa, wakati nageuka nilikuta ndio kwanza cathy alikuwa bado yupo uchi wa mnyama akiwa ameshilia bastola yangu akitaka kunipiga risasi.
Nilijirusha pembeni risasi zaidi ya nne zilimpata Puchu na kummaliza wakati najirusha kwa kujiviringisha hewani sikumpa nafasi Cathy ya kunipiga risasi nyingine nilichomoa kisu na kumrushia Cathy kilichompata sehemu ya moyo na kumuua pale pale.
Ndani kulikuwa na maiti mbili ya Puchu na Cathy, nilijinyanyua mwili ukiwa unaniuma na damu zilikuwa zikinitoka puani na mdomoni. Niliokota bastola yangu na kisu changu.
Nilichukua shuka kitandani na kujifutia damu na kumfuata kallo aliyekuwa bado amejilaza chini. Nilimshika na kumketisha ili ajibu maswali yangu, Mara nilisikia mlango ukifunguliwa nilinyanyuka haraka na kujibanza nyuma ya mlango.
Kiliingia kipisi cha mtu kilichonyoa upara na mwili mkubwa uliojengeka vyema kimazoezi uliofichwa na fulani nyeusi ya mikono mirefu iliyo mbana na kuonyesha umbile lake vizuri.
Nilijua ni John tu, aliponiona alishtuka nusra akimbie lakini niliwahi kufunga mlango kwa mguu kitu kilichozidi kumchanganya. Nilimweleza kwa ishara asogee mbele mbali kidogo na mimi. Lakini bila kutarajia teke lake la nyuma liliipiga bastola yangu pembeni.
Kabla sijatulia nipange mashambulizi alikuwa ameshanifikia, mikono liliwaka moto nusu saa nzima hakuna aliyempata mwenzake, kila mtu alikuwa akishambulia na kuzui. John alibadili staili na kunivamia mzima mzima na kunikaba shingoni japo ngumi zangu zilimpata puani na mdomoni na kumtoa damu hakuniachia alinisukumia ukutani.
Alinibana ukutani japo nilijitahidi kujitoa mikononi mwake alinizidi nguvu alinipigiza ukutani mara tatu mpaka nikaanza kuona kizunguzungu. Alininyanyua juu akiwa amenishikilia shingoni huku akiendelea kuniminya shingo huku akisema:
“Mrembo utakufa kifo cha raha wewe hufai kuuliwa kwa risasi au kisu bali utakufa kwa busu."
Alikuwa akininyonya damu zangu zilizokuwa zikitoka mdomoni, huku akizidi kuiminya shingo, nilijua shingo si muda mrefu itavunjika. Nilikumbuka mafunzo ya kupambana na mtu mwenye nguvu pale anapokuwa amekubana. Nilipepesa mikono yangu kama mfamaji na kufanikiwa kushika sehemu za macho hapo niliingiza vidole vyangu na kucha zangu ndefu zilimuingia barabara.
Alipiga kelele za maumivu na kuniachia, nilianguka chini. Alishika macho yake niliyoyatia makucha, nilitumia nafasi ile kupeleka mashambulizi mfululizo sehemu za siri. Alipiga kelele huku akipiga magoti nilimaliza kazi kwa teke la kuzunguka lililompata chini ya kisogo na kuvunja sehemu ya nyuma, alianguka kama mzigo na kukata roho.
Nilikaa chini kuvuta pumzi mwili wote haukuwa na nguvu kama angetokea adui mwingine angeniua bila taabu. Nilijunyanyua hadi mlangoni nikipepesuka na kufunga mlango kwa ndani ili asiingie mtu mwingine. Kallo alikuwa bado amekaa ilionekana Kallo hakuwa mzoefu wa shughuli zile kelbu moja tu ndio imemfanya vile, nilimnyanyua hadi bafuni na kumwagia maji. Hapo alipata nafuu aliweza hata kutembea peke yake. Nilimkalisha kwenye kitanda mikono nimemfunga na kamba na kuanza kumuhoji:
“Nina imani umeona malipo ya kiburi cha wenzako nadhani hutapenda nawe kuwafuata nataka uniambie ukweli Dar mmekuja wangapi?”
"Sita."
"Nitajie majina?"
"Mimi,Cathy, John, Puchu, Marc na Zone.”
“Marc na Zone wapo wapi?"
"Walitumwa waje kukuue wewe."
"Wapi?"
"Kwako au Kibaha."
"Kibaha wangenipataje nami si makazi yangu?"
"Ilikuwa kubahatisha kwani Doctor Ray inaaminika ndiye anayejua habari zako zote inasemekana ndiye aliyekutafuta.”
"Vizuri, Mary Wahite alijuaje habari zangu?”
"Hapo sijui."
''Mmevuna damu na ngozi kwa muda gani?”
"Ni mwezi wa sita sasa."
"Hadi sasa mmeshauza damu kiasi gani?"
"Bado ndio tupo kwenye makusanyo vile vile mitambo ya kunyonya damu na kuisafisha inamaliziwa kufungwa, wiki hii hivyo kazi inaanza wiki ijayo.”
“Hadi saa mmeisha kusanya vijana wangapi?"
"Elfu sita."
"Elfu sita! Wote hao? Mmewahifadhi kambi moja?"
"Hapana wengi tumewaacha kwenye vituo vyao kwa udogo wa kambi yetu."
"Kambini wapo wangapi?''
''Elfu mbili na mia tatu na leo tumekusanya mia mbili hivyo watakuwa elfu
mbili na mia tano, ila mtambo ukianza ndani ya wiki mbili tutakuwa tumewamaliza wote kwani damu inatakiwa haraka."
Habari zile zilizidi kuusisimua mwili wangu mpaka nywele zilinisisimka. Nilijikuta nikipata matumaini ya kuokoa damu za watu wasio na hatia japo sikujua nzito ulikuwepo mbele yangu.
Lakini kwa uwezo wa Mungu niliamini nitashinda japo nilikuwa kwenye
kundi la uovu la Father Gin. Niliamini uwezo wa Mungu kwani yeye ndiye mwenye aliyefanya majabu kuniingiza kundini niokoe walio taabuni katika mateso mazito.
Niliamini kwa nguvu za Bwana ningeshinda uovu na kulisafisha jina la Kristo kwa
wale wanaotumia kuvuli chake kuichafua dini yake na na manufaa yao kwa kuwatendea watu uovu.
"En’he umeniambia leo umekusanya watu mia mbili?” nilimuuliza swali.
"Eeh ndiyo."
"Wako wapi?"
"Wako vituoni mwao tutawapitia jioni."
"Kambi yenu ipo wapi?"
"Nje ya mji wa Arusha ukivuka Kijenge unakata kushoto kuna barabara ya vumbi ukiifuata utafika kambini kwetu."
"We raia wa wapi?"
"Tanzania."
"Mtanzania halafu unatenda unyama kama huu?"
''Dada yangu mimi nilikuwa mhudumu wa kambi moja hapa Dar ya watoto wanaishi kwenye mazingira magumu tulichukuliwa sita kutoka vituo tofauti. Tukiwa tunawahudumia wale watoto hapo ndipo tulipopewa semina ya madhumuni ya kile kituo kuwa si kulea watoto bali kuvuna damu na ngozi na tulielezwa kuwa atayetoa siri ile atauawa
“Kwa kweli dada yangu tuliishi katika mazingira magumu sana, mmoja wa wenzetu alitoroka kwenda polisi kutoa taarifa juu ya kile kituo. Huwezi kuamini kumbe Marry White anashirikiana na polisi. Mkuu wa polisi alimpigia simu mkuu wa kituo mR Cosmas alipokwenda ndipo alipomkuta mwenzetu pale polisi na kuelezwa alichokipeleka pale.
"Tukiwa hatuna hili na lile kilipigwa king'ora tukakusanywa tulipokusanyika tulikuta Mr Cosmas akiwa amemshika mwenzetu mtupu kama alivyozaliwa na kuelezwa alichokifanya na adhabu yake alichunwa ngozi adharani akiwa hai na mwili wake kutupiwa mamba, Ooh! Maskini Devota alikufa kifo kibaya," sauti ya Kallo ilibadilika na kuwa ya kilio chenye majonzi, habari ile hata mimi ilionyesha napambana na watu wa aina gani.
Kallo aliendelea kuongea kwa sauti ya majonzi na kilio kuonyesha jinsi gani kifo cha shoga yake Devota kilivyomuuma.
“Huwezi kuamini dada kuna watu wana roho mbaya sijui nifananishe na nini nina imani wamemzidi shetani. Devota alichunwa ngozi mbele ya macho yetu kilio alicholia nilisikia maumivu moyoni. Moyo uliniuma kama vile mtu kaupasua kwa kisu butu bila ganzi vipande mbili.
“Yaani kuna watu pale kambini wameandaliwa kwa kazi mbili yupo anayejiita Zimwi shetani yeye kazi yake kuchuna ngozi za watu wote wanaopewe adhabu. Pia yupo mtu mwingine mwenye mwili mkubwa hana tofauti na mzee Ole wa gazeti la Sani yeye huyu anajiita Roho ya chuma kazi yake kuua watu kwa kuwapasua na shoka katikati ya utosi au kukucharanga shoka kama vile wauza bucha. Kuna gogo maalum lililoandaliwa kwa kazi hiyo.
“Umeshashuhudia mauaji mangapi zaidi ya Devota?”
“Mmh, ni mengi...we acha tu dada yangu yanatisha si ya kusimulia.”
“Unataka kuniambia wengine wote kosa lao ni hilohilo la kutokuwa waaminifu wa kikundi?”
“ Hapana ..wapo waliokula njama ya kuua vitendea kazi, wengine kuuza silaha na mwingine aliyeuawa wiki iliyopita alitaka kumbaka mhuduma wa kambi.”
“Vizuri unataka kunieleza mauaji ya Doctor Ray mmeyafanya kwa sababu gani?”
“Ni hivi dada hili kundi tulielezwa ni watu waliojitenga kutoka kwenye kundi moja kubwa linaloongozwa na mzungu mmoja anayefahamika kwa jina la Father Gin, lakini si Father hasa bali ni mkuu wa majasusi.”

ITAENDELEA
 
SEHEMU: 21
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“ Hapana ..wapo waliokula njama ya kuua vitendea kazi, wengine kuuza silaha na mwingine aliyeuawa wiki iliyopita alitaka kumbaka mhuduma wa kambi.”
“Vizuri unataka kunieleza mauaji ya Doctor Ray mmeyafanya kwa sababu gani?”
“Ni hivi dada hili kundi tulielezwa ni watu waliojitenga kutoka kwenye kundi moja kubwa linaloongozwa na mzungu mmoja anayefahamika kwa jina la Father Gin, lakini si Father hasa bali ni mkuu wa majasusi.
SASA ENDELEA...

“Walijitenga, walijiondoa baada ya kuona kazi wanayoifanya ni kubwa na ya kuhatarisha maisha yao, lakini malipo yao ni madogo wanamnufaisha mtu mmoja Father Gin. Hapo ndipo baadhi walipoamua kujitenga na kkutangaza wamechana na kikundi kile na kuanzisha mtandao wao wa kuuza damu na madawa ya kulevya.
“Lakini soko upande wao lilikuwa zito hivyo waliamua kutumia hila pale damu iliyopelekwa ya troni 50 kuzunguka na kuchukua pesa kupitia mkuu wa ujasusi wa ujerumani ambaye ndiye hawara yake Marry White.
“Mpango wake ulifanikiwa na likawa pigo kwa Father Gin pale alipoletewa taarifa kuwa damu yote aliyopeleka ni chafu kwa hiyo imemwagwa.Pesa zile ndizo zilizokiimarisha kikundi cha Marry White ndipo alipojenga kituo kikubwa cha kulelea watoto na vingine anajenga mikoani na kununua mitambo ya kisasa ya kunyonyea damu, matanuri ya kuchomea miili ya watu, matawi mengine yako nchini Kenya, Rwanda,Kongo na Afrika kusini.
Pia kanunua eneo ambalo ukienda vibaya utajua ni makaburi kumbe sio, ni maghala ya kuhifadhia madawa ya kulevya ipo maeneo yaleyale ya kambini Arusha. Pesa zile ndizo zilizompa jeuri kubwa Marry White ilifikia hatua ya kupenyeza mamluki kwenye kikundi cha Father Gin ambao walimpa siri zote zinazoendelea juu ya mpango wa kumsaka Marry White na wenzie watatu walio jiengua kwenye kikundi.
Taarifa zile ndizo zilizo mfanya Marry White aunde kikosi cha kukabiliana na Father Gin hapo wote tuliokuwepo tuliingia mafunzoni kwa ajili ya kukabiliana na Father Gin tuliokuwepo tuliingia mafunzoni kwa ajili ya kukabiliana na adui mazoezi yetu yalikuwa ya miezi sita.”
“Umesema mpango wenu wa kukusanya watoto kwa ajili ya vuno la damu na ngozi una miezi sita sasa mlifanyaje kazi mbili kwa wakati mmoja?”
“Sikukueleza mwanzoni, ni hivi tulipokusanywa baada ya semina ndipo zilipofika taarifa za kusakwa Marry White hapo ndipo mafunzo yalipoanza mara moja. Kwa miezi sita, baada ya kukamilika mafunzo wakati huo kambini tulikuwa na watoto mia moja na majengo zaidi yalikuwa yakiendelea kujengwa.
“Ndipo tulipoanza kazi rasmi ya kukusanya watoto japo ilikuwa kazi kwani vituo vingi Father Gin alikuwa amevihodhi. Baada ya hila za Marry White kumuharibia biashara zake ambazo zilisimama hapo ndipo alipopata nguvu ya kukusanya watoto kwa kasi vituo vingine walipokataa tuliwapa pesa ndipo siku moja Marry White alituita na kutueleza kumeandaliwa watu wamsake. Kumbuka ni siri iliyovuja toka kwenye kundi la Father Gin tulielewa jinsi tutavyokabiliana hivyo kazi ya kuwaua haikuwa nzito tuliwaua kiurahisi sana.
“Wewe umeisha ua wangapi?”
“ Watatu.”
“Unaweza kutumia silaha gani?”
“Bunduki na bastola ya aina yoyote.”
“Wote uliwaua kwa risasi au nini?”
“Mmoja kwa kisu , wengine kwa sumu na risasi.”
“Katika watu wa Father Gin umeua wangapi?”
“Wote watatu.”
“Uliwaulia wapi?”
“Hapohapo ni hawa wa mwisho mwisho ambao niliwaingilia ndani mwao siku wanayo jiandaa na safari.”
“Mmh, vizuri endelea.”
“Basi tulijua kazi imekwisha tukawa tunaendelea na kazi zetu. Siku moja Marry White hakuwa kwenye hali ya kawaida tulijua kuna jambo, siku hiyo alionekana mtu mwenye mashaka mengi. Ndipo alipotueleza habari zako kuwa umerudi kutoka mafunzoni kwenye chuo cha ujasusi ambacho ndicho alichosoma Marry White yeye alisoma kwa miezi minane wewe mwaka mzima na kutuambia jinsi gani ulivyo hatari.
“Hapo ndipo tulipopewa jukumu la kukuua ila jukumu hilo walipewa kina Zone, Marry White anawaamini wameshafanya vizuri kazi zote za nyuma walizotumwa, na jana tuliingia jioni kwa ajili ya kutekeleza kazi hii leo.”
“Sawa mlinifuata mimi na Doctor Ray kwa sababu ndiye aliyekutafuta vilevile hata wewe ukifa atawatafuta wengine na ndiye waliyemtumia ili upatikane kutokana na ukaribu wenu.”
“Umeniambia umepitia mafunzo ya mapigano kwa miezi sita iweje kofi moja likuzidi nguvu na kulegeza hivyo?”
“Tangu niingie kazi hii sijawahi kupigwa na mtu vilevile nilihisi nimepigwa na ubao ulionifanya nisikie kizunguzungu.”
“Ooh, pole sana sasa ni hivi wewe ndiye utayenisaidia kuwakomboa hawa watoto na kukomesha biashara hii.”
“Mmh, Dada itakuwa ngumu lazima Marry White atajua hivyo nitakabiliwa na kifo cha kutisha.”
“Wewe ndiye atayenisaidia kuwaangamiza Marry White na wenzie,” nilimpa moyo.
“Kukusaidia kivipi?”
“Kunipa taarifa kutoka kwenye kikundi chenu ambazo zitanisaidia kuifanya kazi yangu kwa wepesi elewa Kallo mimi sina ugomvi na nyingi bali Marry White na washirika wake pamoja na Father Gin.”
“Father Gin si ndio bosi wako?”
“Elewa kazi yangu si kutoa roho za viumbe bali kuokoa roho za viumbe wasio na hatia nina imani kwa uwezo wa Mungu nitawashinda Father Gin na Marry White.”
Kauli yangu ile yenye msisitizo ilimfanya Kallo ajae ujasiri na kuniahidi:
“Da Thereza na kuahidi nitashirikiana nawe hadi tone la mwisho la damu yangu.”
Tulikumbatiana na kupigana migongoni kupeana mioyo ya utendaji, mara simu ya Lallo iliita aliiangalia na kuseama kwa hofu.
“Nani?”
“Marry White.”
“Mungu vile ni ghafla hujapanga maneno mweleze ndio unarudi kutoka kukusanya watoto,” nilimwelekeza cha kusema.
“Haloo Sister Marry White.”
“Ee’he Kallo shughuli imefikia wapi halafu mbona simu za Marc na Zome zinaita tu hazipokelewi? Sijui wamefikia wapi katika kumuua Thereza unajua Kallo moyo wangu umeingia hofu?”
“Kwa nini Sister?”
Hata sielewi nimejikuta namuogopa Thereza japo sijaona uwezo wake huenda kishanitia hasara.”
“Hasara! Una maana gani?”
“Yaani kawaua Marc na Zone.”
“Mmh ! Sidhani.”
“We umeshawasiliana nao?”
“Ni kama nusu saa walinijulisha wameshamuua Doctor Ray na wanamsubiri Thereza ambaye walijulishwa yupo njiani kuelekea Kibaha na walinihakikishia kazi yao itakuwa nyepesi tofauti na walivyo fikiria.”
“Kwa sasa umeshawasiliana nao?”
“Hata mimi simu zao zinaita hazipokelewe sijui kuna nini?”
“Lazima kutakuwa na tatizo mtume John na Puchu wawafuatilie.”
“Sawa mimi ndio naelekea hotelini.”
“Fanya hivyo haraka unijulishe moyo wangu umeingiwa hofu lazima kuna hatari.”
“Sawa bosi.”
“Vipi nawe kazi yako imefikia wapi?”
Kwangu imekwenda vizuri sana na jioni tunarudi.”
“Hesabu imetimia?”
“Imetimia nimepata wote mia mbili.”
“Vizuri sana kazi yako nzuri Kallo, imenifurahisha lazima nikuongezee mshahara mkubwa.”
"Sawa bosi nitashukuru.”
"Kazi njema natarajia tutaonana Arusha usiku tuna kikao kingine..Kallo,” alimwita. “Unasemaje sister Marry White.”
“Huwezi amini ile 'Issue imejibu imewahi tofauti na tulivyotarajia.”
“Eehe..lete raha.”
“Saini ya Father Gin tumeipata na yale makaratasi yalikuwa yanatuumiza kichwa huwezi amini kikao cha leo kilikuwa kuzuri kuliko tulivyotarajia mengine tukionana jioni tutaongea mengi...kazi njema ila wasisitize Puchu na John wafuatilie mara moja.”
“ Sawa bosi.”
“ Kazi njema.”
“Nawe pia,” simu ilikatwa alinigeukia na kuniuliza:
“ Sasa da’ Thereza nitamweleza nini tena?”
“Usiwe na wasi nitakufundisha cha kumueleza la muhimu tuondoke humu ndani ili twende sehemu yenye usalama, chukua vitu vyote muhimu.”
Kallo alichukua vitu vyake vyote tukaondoka eneo la tukio mara moja, nilikwenda naye hadi moja ya ofisi yangu na kuingia naye ndani. Niligundua Kallo bado hakuwa na imani nami alijua nimempeleka ili nimuue.
“Kallo nina imani hii ni sehemu iliyo salama hivyo tunaweza kuongea vizuri zaidi vile vile jisikie upo huru we urafiki yangu hebu nieleze ni mpango gani unaohusiana na saini Father Gin?” nilimuuliza kwa upole.
“Kama nilivyokueleza mwanzo kuhusu kundi la Marry White baada ya kujitenga hawakujitenga bali dhamira yao kubwa ni kumtia adabu Father Gin kwa kuhakikisha wanaziba njia zote za kumuingizia na kuchukua zile pesa za mauzo kwa kuiba disc yenye mikataba ya malipo na kufuta kumbukumbu zote kwenye computer.
Baada ya kufanikiwa kuziiba zile disc walikuwa wakitafuta saini na profoma invoice za Father Gin ili kumpiga pigo takatifu.”
Nilishtuka kusikia pigo takatifu na kuona mpango huo unafanana kabisa na operesheni ya Father Gin.
“Eeeh, nina imani pigo hilo litamchanganya trion 150 si mchezo.”
“Umesema kuna mamruki kwenye kikundi cha Father Gin walio chini ya Marry White ni wangapi?”
“Huwezi kuamini ni wote kumi na tano unaowaona ndio wanaomla kisogo na kujifanya wapo pamoja naye, kama ungebahatika kukiona kikao cha leo Arusha ungechanganyikiwa yaani aliyepungua ni Father Gin tu.
“Mmh, hizi habari nzito, ina maana maisha yangu yapo mikononi mwao?”
“Ni kweli lakini nilioyaona leo nimeshawahi kuyaona kwenye sinema na kujua ni uongo kumbe yapo kweli, dada unatisha wacha Marry White akuhofie.”
Mara simu alilia, ilikuwa ya Marry White, kabla ya kupokea aliniuliza amjibu nini. Nilimwewleza amjibu kuwa amekuta mayaji ya kutisha hotelini ya wenzake wote ila yeye amefanikiwa kutoroka. Kallo alimweleza kama nilivyo mwambia aseme.
Nilisikia Marry White akipiga meza upande wa pili kwa hasira:
"Unanisikia Kallo.”
"Ndiyo sister."
“Ni hivi mambo yamesha haribika hivyo basi simamisha kazi zote za kukusa watoto njoo haraka Arusha ili tujipange upya hili ni pigo takatifu. Jitahidi utoke salana maana sina imani tena na Thereza anaweza nawe kukumalizia mbali jitahidi utoke salama kwani sasa hivi upo wapi?”
“Nipo sehemu nina imani ni salama japo siamini sana.”
“Vipi ulipoingia hotelini ulibahatika kuchukua vitu muhimu?”
“Huwezi amini sikukuta kitu chochote.”
“Ooh, Mungu wangu.” Marry White aliongea sauti ya kukata tamaa.
“Sasa ndio itakuwaje?” Kallo aliuliza.
“Kwa sasa hivi siwezi kuongea lolote nimechanganyikiwa mengi tutaongea ukifika ila ninaapa nitamshikisha adabu mshenzi huyu nitamtafuna mbichi,” Marry White alisema kwa hasira.
“Kwa hiyo unaniambia niende kwenye vituo nikawataarifu?”
“We wee..we..acha kabisa unaweza kukutana naye nasema acha kazi zote rudi mara moja.”
Ilionyesha ni jinsi gani Marry White anavyoniogopa lakini hicho hakikuwa kigezo cha kunifanya nitembee kifua mbele la muhimu lilikuwa kuwatokomeza wazandiki wale washenzi mamumiani wenye maumbile ya kibinadamu lakini mioyo yao zaidi ya ukatili wa mnyama.
Vilevile nilimshukuru Mungu ningeweza kuokoa watoto mia mbili bila jasho kwani kusitisha kuwachukkua watoto mia mbili kulinifanya niokoe watoto elfu mbili na mia tatu.
Nimemtupia macho Kallo ambaye alionyesha ni jinsi gani nilivyo mtu wa ajabu. Alinitazama macho ya mtu kuniuliza swali, hilo nililigundua.
“Sema tu Kallo usiniogope wewe sasa hivi si rafiki tena ni ndugu ambaye nakuona tumetoka tumbo moja najua unaswali uliza.”
“Sasa da’ Thereza utaniruhusu niende Arusha?”
“Hiyo ndiyo dhamira yangu kuu, ya wewe kwenda Arusha ili nipate habari za kule ambazo zitanipa urahisi wa kurahishisha shughuli yangu.
“Tutawasiliana vipi wakati huo tunaweza kuwa na Marry White?” Kallo aliniuliza swali muhimu.
“Ina maana hata kulala mnalala wote?”
“Hapana.”
“Basi muda utaokuwa peke yako ndio wakati muafaka wa kuwasiliana vilevile kuna chombo nitakiweka kwenye simu yako kitasaidia kukamata maongezi yote ya simu zinazotoka na zinazoingia. Nina imani utanisadia , lakini Kallo ukinigeuka sisemi ila shuguli yangu unaijua, sijui utajificha wapi labda nife lakini kama ningali hai nitakutia mikononi. Huyo bosi wako ninakupa wiki nitamtia mikonini si yeye hata Father Gin,” nilitoa mkwara mzito nikiwa sitanii.
“Mmh, dada umepania.”
“Unajua Kallo, Mungu namwita wa ajabu kwa sababu haya mafunzo niliyopata japo wamenipa wao lakini ndiyo silaha ya kuuangamiza udhalimu wao unaoendelea labda nife leo lakini Mungu atanilinda na kuushinda udhalimu wao.”
"Da’ Thereza maneno yako yamenipa ushupavu na ushujaa moyoni nami nitakuwa nawe bega kwa bega sitakwenda kinyume na yote tuliyoahidiana.”
“Nimekuamini usiniangushe.”
“Sitakuangusha.”
“Nina imani tutashinda.”
Tulipeana mikono na kushikana kwa nguvu kuonyesha jinsi gani tulivyoungana mioyo yetu kuutokomeza udhalimu. Nilichukua simu yake na kuweka chombo maalum cha kukamata mawasiliano.
Kallo unavyokuwa upo na Marry White mkiongea utabonyeza kwenye kidude hiki utaona neno hili baada ya kujiandika simu itarudia katika hali ya kawaida hapo utakuwa umeungana na mimi kwenye mazungumzo yenu.”
“Sawa usihofu mambo yataenda kama yalivyo pangwa.”
“Basi wewe wahi Arusha una hela?”
“Ninazo.”
Nilimsindikiza Kallo hadi sehemu walikopaki gari lililowaleta, kwa vile John ndiye aliyekuwa dereva ilibidi aendeshe mwenyewe. Kabla ya kuondoka aliniuliza swali.
“Sasa da Therza suala la watoto litakuwaje?”
“Hiyo kazi niachie nitakujulisha ulinieleza pale kambini ulinzi ukoje?”
“Ulinzi pale si mkubwa sana.”
“Una maana gani kusema si mkubwa sana?”
“Walinzi hawazidi watano, unajua wanajiamini kwa vile hakuna kitu cha kuchukuliwa zaidi ya watoto tena mwanzo kambi ilikuwa na walinzi wawili tu, watatu wameongezwa baada ya kufungwa ile mitambo ya kunyonyea damu na matanuru ya kuchomea watu.”
“ Asante kuna wahudumu wangapi?”
“Wako kumi.”
“En’he na mkutano umesema unaanza saa ngapi?”
“ Saa nne usiku.”
“Wana sehemu nyingine au ni ileile?”
“Ni ile ile, vipi utakuja?”
“Mmh..sidhani,lazima nijipange kwa leo waache wafanye mkutano wao ili kitakachofuata au ajenda ya mkutano utanijulisha ili nijipange vizuri.”
“Lakini dada si unajua jumatatu ndio inaanza kazi ya unyonyaji wa damu na uchunaji wa ngozi, ukichelewa utakuta tayari wameshateketezwa kama nilivyo kueleza damu inatakiwa haraka na leo pamoja na mkutano kuna wageni wanaokuja kuingia mkataba wa ngozi za binaadamu ambazo huzitumia kuvushia dawa za kulevya.
“Nitajitahidi lakini ondoka ukiwa na tumaini kuwa hawatadhuriwa na mtu yeyote.”
“Sawa dada wacha niwahi.”
Nilimuacha Kallo aondoke najua moyo wake wake ulitawaliwa na wasiwasi juu ya mpango tuliopanga wa kuwakomboa watoto. Pamoja na kumuamini lakini haikuwa lazima kila nilichokifikiria kukifanya basi lazima nimweleze. Huwezi kumuamini mtu kwa asilimia mia hata awe ndugu yako wa damu.

Itaendelea
 
SEHEMU: 22
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Nilimuacha Kallo aondoke najua moyo wake wake ulitawaliwa na wasiwasi juu ya mpango tuliopanga wa kuwakomboa watoto. Pamoja na kumuamini lakini haikuwa lazima kila nilichokifikiria kukifanya basi lazima nimueleze. Huwezi kumuamini mtu kwa asilimia mia hata awe ndugu yako wa damu.
SASA ENDELEA...
****
Niliamua kujipanga vilivyo ili majira ya saa moja usiku niivamie kambi ya Marry
White kuwaokoa watoto kisha niwahi mkutano wao wa Arusha mjini majira ya saa nne usiku. Najua kwa akili ya kibinadamu haiwezekani lakini tuwe pamoja.
Baada ya kujipanga nilichukua mlinzi mmojammoja mwenye uwezo wa kutumia chombo cha moto katika kila kitega uchumi changu. Pale nilikuwa nimeajili askari mgambo na askari waliofukuzwa kazi mdiyo walikuwa walinzi wa miradi yangu.
Baada ya kuwakusanya na kuwapa semina ya robo saa ambayo haikuhitaji swali zaidi ya kutekelezwa. Niliwaeleza wao kazi yao kubwa ni kuwalinda watoto kama nitafanikiwa kuwatorosha kwenye kambi.
Hakukuwa na mjadala zaidi ya kuingia ndani ya Nissan Patrol, walikuwa tisa na mimi wa kumi. Kila mmoja nilimpa silaha nzito kwa ajili ya kujihami panapo tokea tatizo. Japo nilikkuwa na uhakika shughuli itakuwa nyepesi isiyo na madhara.
Tuliingia wote na safari ilianza ilikuwa ni majira ya saa nane alasiri. Nilikimbiza gari kiasi kama ajali ingetokea au tairi la mbele kupasuka hakuna ambaye angepona.
Tuliwasili maeneo ya njia panda ya kuingia kambini ilikuwa vigumu mtu kuitilia mashaka gari letu.
Tuliteremka wote na kumuacha mtu mmoja alinde gari tuliingia porini tuliizunguka ile kambi kilichonifurahisha askari wangu walikuwa makini sana tofauti na nilivyo wafikiria. Tulikwenda kwa mtindo wa kuvamia kambi ilionyesha ni jinsi gani walivyo iva kijeshi.
Tulitembea porini mwendo wa nusu saa, wakati huo giza lilikuwa linazidi kutanda Nilipoangalia saa yangu ilionyesha ni saa mbili kasoro, taa za majengo zilitujulisha tumebakiza hatua chache.
Tulipobakiza kama hatua mia mbili niliwaomba wanisubiri na wakae tayari kutoa msaada japo sikujua uwezo wao. Nilitembea kwa mwendo wa paka kwenye mawindo hadi nyuma ya jengo. Eneo la nyuma lilikuwa linawaka taa kali iliofanya eneo ilionekana vizuri.
Nilikuwa sina ujanja niliokota jiwe na kulirusha ambalo liliipiga ile taa na kuizima eneo lote la nyuma likawa giza. Nilisikia mtu akiongea kumbe hakuwa mbali na mimi, nilimuona akinipita huku akivuta sigara.
“ Hii taa sijui imefanya nini tena?” alijisemeza.
Nilitumia uzembe wa yule mlinzi kwa kumnyatia na kumtia kabali mithili ya kicheche na kuku na kumvutia kichakani nilikowaacha wanajeshi wangu, nilipofika nilimuachia baada ya kumsachi na kumkuta ana simu, sigara bhangi, kondom na magazini iliyokuwa imejaa risasi na bastola pia iliyojaa risasi.
Nilipomwachia alianza kukohoa, maana kabali ilikua si mchezo. Japo mtoto wa kike nilikuwa nimeshupaa, nilimuuliza swali:
''Unamjua Thereza?”
"Thereza yupi?”
"Yule mliyepewa habari zake na Marry White?”
“ Sijawahi kumuona ‘live’ ila nimemuona kwenye picha.”
Niliwasha taa ya tochi na kujimulika usoni na kumweleza:
"Ndio mimi.”
"Ooh! Mungu wangu nimekwisha.”
“Wala hujaisha, ukiwa mkweli utapona ila ukileta uongo wowote utakuwa mgeni wa kuzimu.”
“Sawa dada, uliza swali lolote nitakujibu,” aliingia woga.
“Hapa kambini mpo wangapi?”
“Sisi askari au wote kwa ujumla?”
“Askari.”
“Tuko watano.”
"Wenzako wako wapi?”
“Hapa kambini tupo watatu.”
“Wengine wako wapi?”
“Wamekwenda mjini kwa wanawake zao.”
“Na wenzako wawili wako wapi?”
“Wapo ofisini wanacheza game."
“Mbona mmekuwa wazembe kiasi hicho?”
“Dada yangu tunalinda nini?”
“ Tutaongozana na wewe hadi kwa wenzako na ukileta utani au ujanjaujanja mwili wako nitatengeneza chujio la nazi kwa risasi,” nilimpa mkwara mzito.
Tuliongozana hadi kwenye ofisi moja ndani tulisikia sauti ya mlio wa game kwenye komputa na watu wakicheka kuonesha kuna mtu kamfunga mwenzake.
Nilimsukumia ndani, ile hali iliwashtua walipotaka kuwahi silaha zao nilimuwahi mmoja na kitako cha bunduki kwenye taya lililomfanya apige kelele za maumivu.
Mmoja alijifanya mjanja kuchupa kupitia dirishani, mlio wa risasi wa mmoja wa askari wangu zilizompata mgongoni na kumtoa roho.
Tulitoka na yule askari aliyebaki hadi kwenye vyumba vya wahudumu ambao nao tuliwaweka chini ya ulinzi. Tuliwaamsha vijana wote waliokuwa wamelala na kuwakusanya sehemu moja kisha tuliwahesabu walikusanya wote sehemu moja kisha tuliwahesabu walikuwa ni walewale elfu mbili na mia tatu idadi niliopewa na Kallo.
Baada ya kuwakusanya nilizungukia mitambo ya kunyonyea damu na matanuru ya kuchomea miili ya watu ilikuwa ni mitambo ya kisasa inayoonyesha kugharimu mamilioni ya dola.
Nilitega kila kona mabomu kambi nzima wakati huo msafara ulielekea msituni askari wangu waliwazunguka wale watoto na wahudumu. Nikiwa namalizia kutega mabomu mara nilikuta nimetokea kwenye ofisi iliyo kuwa na mitambo na komputa ilionyesha ndiyo ofisi ya Marry White kwa juu ya meza kulikuwa na picha yake ndogo.
Nikiwa natafakari ninzie wapi mara nilisikia breki za gari nje ya jengo na sauti ya miguu ilielekea kule kwenye ofisi mara nilisikia mlango ukifunguliwa nilijificha chooni. Taa za ofisi ziliwashwa nilisikia watu wakiongea:
"We tafuta disk mimi naangalia kwenye kompyuta.”
Nilifungua mlango taratibu wa choo na kuchungulia niliwashuhudia mwanamume wa shoka wanne wenye mavazi ya kijeshi wakifungua komputa na kusoma vitu, mwingine alifungua droo na kutoa disk nyingi na kusoma moja moja alisema:
"Hii hapa nimeipata."
"Achana nayo hata mimi nishaipata kwenye faili wacha nimtumie moja kwa moja kwenye e-mail yake sister Marry White.”
Saa yangu ilionyesha bado dakika tano mabomu yalipuke na kuiteketeza kambi yote lakini sikuwa na ujanja. Ili kuokoa maisha yangu ilikuwa lazima nijitoe muhanga la sivyo ningekufa kifo kibaya na dhamira yangu kupotea. Niliamua kusubiri dakia mbili labda watatoka.
Nilipoangalia saa ilinionyesha bado dakika mbili mabomu yalipuke, muda ulivyozidi kukatika nikajua sina ujanja maana watu walio ofisini si watu wa mchezo walionekana ni watu kazi kama ningeingia kichwa kichwa ningeishia mikononi mwao. Mbaya zaidi nilimuona mtu mmoja macho yake yametazama mlango wa choo kama vile ameona kitu au amehisi kitu.
Kitu kilichoniweka katika kipindi kigumu cha kuweza kujitoa mule chooni muda nao ulizidi kukatika. Niliwasikia wakiongea mmoja alisema.
"Oooh, afadhali imekwenda.”alisema mmoja.
“Ina maana hii CD haina umuhimu tena?”
"Haina ila mwanangu mambo yakijipa tutaukata.”
"Yajipe mara ngapi wiki ijayo Sister Marry White ana kwenda kuchukua mavumba (pesa) Italia.”
“Unakumbuka alituahidi kila mtu bilioni ishirini?”
“Si utani mwanangu lazima wanijue mi nani," mmoja alijigamba.
"Ulisema billion 150?”
"Unacheza! Trillion 150."
Taarifa ile ilinipata picha nyingine akilini mwangu juu ya mpango wa Sister Marry White ya kwenda Italia kuchukua trillion 150. Pesa ambayo ilikuwa ikimchanganya akili Father Gin.
Pamoja na kunifungua akili lakini maneno yao hayakuwa na umuhimu kwangu zaidi ya uhai wangu na maongezi yao yalizidi kula muda. Sasa ilionyesha bado sekunde sabini yaani dakika moja na sekunde kumi mabomu niliyoyatega yalipuke. Nilijikuta mwili wote unalowa jasho kwa hofu ya kufa kwa mabomu. Niliamua liwalo na liwe kama kula bora waniue wao kuliko kufa kikondoo namna ile.
Vilevile bado hofu ilinitawala huenda pakatokea mapigano yatayochukua muda utaofanya mabomu yalipuke wakati bado tunapigana. Lakini niliona uoga wangu ndio utakaosababisha nife kifo cha kikondoo na haikuwa sifa yetu.
Niliamua liwalo na liwe wazo lililoniijia ni kuipiga risasi taa na kukurupuka kuelekea mlangoni kama nitakosea mlango. Mungu ndiye anayejua na ndiye niliyemkabidhi uhai wangu.
Kabla sijatoka juu ya choo kulikuwa na ki-uwazi kidogo kilichoonyesha siku za nyuma kulikuwa na kiyoyozi (Air Condition). Japo tundu lilikuwa dogo kwa mafunzo yangu nilikuwa na imani nitapita tu.
Kwa haraka bila kuchelea niliuparamia ukuta kama paka hadi kwenye lile tundu lilikuwa dogo kwa mafunzo yangu nilikuwa na imani nitapita tu. Nilijipenya mithili ya paka na kujikuta ninafanikiwa kupita na kutoka nje ya jengo.
Wakati huo mwili wote ulikuwa unanivuja jasho kama mtu niliyenyeshewa mvua usiombe jasho la uoga, huwa linatoka mfululizo na kufanya nguo zote zitote. Asikwambie mtu maisha matamu hasa pale unapoona uhai unataka kutoka huku unaona. Nilipotua chini nilikuta zimebakia sekunde arobaini mabomu yalipuke.
Nilitimua mbio kuelekea msituni huku nikiangalia saa yangu, zilipobakia sekunde tano nilijirusha na kujilaza chini. Baada ya muda mfupi kitu kilikubali, mabomu yalilipuka kwa mpigo na kulitetemesha eneo lote linaloizunguka kambi ya Marry White.
Wale vijana wa Marry White nao wote waliteketea pamoja na mitambo yake ya kunyonyea damu, nilijua lazima litakuwa pigo lingine la mwaka "PT yaani pigo takatifu.
Baada ya milipuko kutulia nilinyanyuka kuelekea kwa wanajeshi wangu na kundi la watoto na wahudumu. Niliwakuta bado wote wamelala chini. Nilipofika niliwaamuru wote wanyanyuke.
Tuliendelia na safari kuitafuta barabara kuu tulipokaribia barabarani, niliwaamuru askari wangu wawalinde wale watoto na wahudumu mpaka pale magari yatapofika kuwachukua.
Niliwapigia simu kwa ajili ya kuleta magari zaidi ya ishirini ya kuwasomba watoto wote kuwarudisha Dar es salaam. Niliwaachia jukumu kuwa magari yakifika tu basi wawapakie wote na kurudi nao Dar es salaam. Vile vile niliwapa maelekezo ya kuwasambaza vipi watoto kwenye vituo vyangu ili wapate mapumziko mazuri.
Baada ya kukabidhi majukumu nilikimbilia kwenye gari muda ulionyesha saa tatu za usiku hivyo usiku hivyo ilikuwa imebakiza saa moja ili kuwahi mkutano wa Marry White na watu wake pamoja na hao wakala kulikuwa na ugeni wa kuingia mkataba wa kununua ngozi za binadamu.
Nilipofika kwenye gari, nilimkuta mlinzi amelala mpaka anakoroma, nilishangaa ulinzi wa kizembe namna ile. Kwa hali ile lazima adui anajitawala atakavyo mbaya zaidi anakoroma ile kumrahisishia kujua amelala kwani ameshajulishwa kwa mkoromo wa usingizi “kuwa njoo mimi mwenzio sijitambui.”
Nilimshtua nusra akurupuke nilimtuliza.
"Vipi mbona unalala kama uko msibani?”
“Aaah! Aaah..samahani sister."
"Mimi.”
“Samahani, adui utamwambia samahani itakusaidia nini? Kuwa makini bwana tupo shughulini," nilimtaadhalisha.
''Sawa sister nitakuwa makini."
Alijibu huku akipiga miayo na kujinyoosha na mkono mmoja ukifikicha macho.
"Sasa ni hivi wewe utaungana na wenzako kuwalinda wale watoto kisha nijulishe, una simu?”
"Ndiyo sister."
"Piga namba hizi ifikapo saa tano kamili, atayepokea mwambie kambi yote imeteketea kwa moto hakuna kilicho baki, sawa?”
"Sawa sister."
"Usiniangushe na kutegemia wewe."
"Sasa hivi niko makini sana."
"Ok, tutaonana wacha niwahi, magari yakifika wapandisheni watoto tutaonana Dar."
Niliingia kwenye gari na safari ya Arusha mjini ilianza mara moja. Niliwasili Arusha mjini baada ya robo saa. Nilitafuta eneo nililo elekezwa nilikuwa na imani Kallo alikuwa upande wangu.
Eneo lilikuwa lilelile kwenye maeneo ya mtaa wa sokoine, lilikuwa jengo la kisasa la ghorofa nne, mzigo ulikuwa palepale nilipomuagiza Kallo auweke, nilimweleza kama sitakwenda baada ya muda fulani auchukue.
Ilikuwa ni sare wanayovaa wahudumu wa mkutano ule niliuchukua ule mzigo na kuufungua ndani. Nilikuta sare na kijikaratasi kilichoandikwa.
Sare hiyo ni kwa ajili ya vinywaji vya wageni hivyo ukivaa ingia chumba namba 103 hapo utamkuta mkuu wa ugawaji ataye kupa utaratibu
Niliingia hadi hotelini na kuingia hadi hotelini na kuingia chooni nilibadili nguo na kuvaa sare ya muhudumu wa vinywaji. Nilitembea taratibu kuelekea ukumbi wa mkutano uliokuwa ghorofa la pili.
Jamaa mmoja mwenye suti nzito iliyomkaa vizuri mwilini alinishua:
''We vipi una fanya nini huku? Wahi ukumbi wa mikutano wageni wako njiani.”
Nilichepua mwendo kupanda ngazi hadi ghorofa la pili niliinga chumba namba 103, Nilimkuta mzee mmoja aliponiona aliniuza:
"We nimekupaga wapi?”
"Bado.''
"Basi we utakuwa upande wa kuwapa maji wageni kwa hivyo chukua chupa za maji weka kila kitu sawa pamoja na glasi fanya haraka wageni wako njiani."
Nilielekea ukumbini nilipoingia nilikuta kikao kinaendelea, meza ya kati alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa mweupe kidogo kama albino mboni za macho yake zilikuwa bluu alikuwa mwanamke mzuri.
Nilijua huyu ndiye Marry White alikuwa amezungukwa na watu waliovaa suti nzito nyeusi walikuwa kumi na wanne, kwa hiyo walikuwa kumi na tano. Niliangalia sura zao. Mmh! Nilizidi kuamini maneno ya Kallo wote waliokuwemo ni walewale washirika wa Father Gin tofauti ni watu wanne yaani Marry White na washirika wake watatu ambao wote picha zao nilikuwazo.
Kwa vile walikuwa mbali kidogo nami sikuweza kusikia walichokiongea, nilichomoa simu yangu ndogo kama kalamu yenye kamera na uwezo wa kuchukua picha za video.
Nilianza kusambaza chupa za maji, macho yangu yaliangalia kwenye meza ya mkutano wa Marry White na washirika wake niligundua baadhi ya chupa zilikuwa zimeishiwa na kinywaji japo haikuwa idara yangu.
Nilikwenda hadi kwenye meza yao na kuanza kukusanya chupa wakati huo kamera ilizidi kupiga picha na kuchukua matukio. Niliwasogelea karibu wao waliendelea na mkutano wao bila kunigundua. Nilipokuwa na uhakika picha yangu nilipokuwa na uhakika picha yangu nimeichukua vizuri niliondoka pale mezani na kurudisha chupa.
"We vipi hiyo si kazi yako, glasi umeishasambaza?” mkuu wa vinywaji aliniuliza.
"Bado."
"Ona sasa kazi yako hujaimaliza unaingilia kazi nyingine isiyokuhusu, haya sambaza glasi haraka."
Nilizibeba glasi na kuzisambaza, mara nilishangaa kuwaona wote wakinyanyuka na kutoka nje kwa pamoja baada ya dakika tano walirudi wakiwa wameongozana na msafara wa watu saba walikuwa ni waarabu saba wenye kanzu nyeupe na vilemba vyeupe.

Itaendelea
 
SEHEMU: 23
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Nilizibeba glasi na kuzisambaza, mara nilishangaa kuwaona wote wakinyanyuka na kutoka nje kwa pamoja baada ya dakika tano walirudi wakiwa wameongozana na msafara wa watu saba walikuwa ni waarabu saba wenye kanzu nyeupe na vilemba vyeupe.
SASA ENDELEA...

Kila mmoja alichukua sehemu yake muda ule walihama kwenye ile meza yao kuu ya mkutano na kuhamia meza nyingine wote walikaa pamoja. Baada ya wageni kukaa, Marry White alisimama na kuwakaribisha wageni. Wakati huo wahudumu wote tulitolewa ukumbini.
Kwa vile nilikuwa nimeshaweka kinasa sauti chini ya meza niliweza kuyasikia yote waliyozungumza. Wakati huo nilikuwa nikielekea nje ya jengo niliteremka ngazi hadi chini. Nilikwenda hadi choo nilichobadili nguo nilivaa nguo zangu na kuziacha zile za uhudumu mulemule chooni.
Niliyasikiliza maongezi yao, nilimsikia Marry White akisema:
"Karibuni sana, tena mmekuja wakati mwafaka, jumapili tutakuwa tumeshakusanya ngozi za binaadamu elfu tatu ambazo nina imani mtaondoka nazo."
"Kwa hiyo bei ni ileile?”
"Hapana kutokana na gharama za mitambo ya kisasa kila ngozi mtaongeza dola 5000."
“Sawa hamna tatizo wacha tulipie ngozi zote 3000 na zingine tutazipata lini kwani tuna uhaba wa ngozi?"
"Sawa," mara nilisikia sauti ya makaratasi baada ya kama dakika ishirini nilisikia sauti ya Marry White ikisema:
"Hela, ipo sawa jiandaeni tu, vipi mnaondoka au mnasubiri mwondoke nazo?"
"Tunasubiri kwani sasa hivi tuna safari ya kutembelea mbuga za Tanzania za sehemu zote za kitalii maana wengi wamesifia uzuri wa mbuga na maziwa na kisiwa cha Zanzibar.”
“Ooh! Itakuwa vizuri nitakupeni mtu wa kukutembezeni nitatoa ofa kama wageni wangu."
"Tutashukuru sana.”
Mara nilisikia simu ikiita nilipoangalia saa yangu ilionyesha ni saa tano na dakika tano,
Nilijua lazima atakuwa yule mlinzi niliyemwachia maagizo. Nilisikia Marry White akiita:
"Hallo unasemaje? Acha utani... Usiniambie, ooh Mungu wangu," nilijua kimenuka.
"Vipi kuna nini bosi?" walimuuliza.
"Ee.. eeti lambi ya watoto yote imelipuliwa.”
"Haiwezekani.. haiwezekani... Si rahisi huo ni utani tu bosi," mtu mmoja alipinga.
"Hapana lazima twende eneo la tukio."
Walinyanyuka niliwaona wakiingia kwenye magari yao na safari ya kuelekea eneo la tukio ilianza na kusababisha kikao kuvunjwa.
Muda kidogo walitoka wale Waarabu saba na kuingia kwenye 'Hiace' na kuondoka.
Nilikimbilia ndani nilikutana na Kallo akiwa amepigwa na butwaa.
"Ha! sister Thereza ndo unafika?”
"Eeeh... kwani vipi?”
"Nasikia kuna tukio limetokea kambi ya watoto imelipuliwa nasikia hakuna kilichobakia ina maana hata watoto walinzi na wahudumu wote wamefariki,” Kallo aliongea huku akilia.
Nilitaka kucheka lakini nikabana kicheko changu.
"Kallo zile hela wamewahi kuondoka nazo?"
"Hela zipi da Thereza?"
"Za manunuzi ya ngozi."
"Sijui lolote."
"Hebu twende kwenye meza ya mkutano."
Niliongozana na Kallo hadi kwenye ile meza tulikula fuko la pesa lipo pale pale chini ya meza. Niliingiza mkono na kutoa bando la pesa zilikuwa dola tupu.
"Ha!" Kalo alishangaa.
"Usishangae mdogo wangu hili ndilo jasho letu sasa zibebe unifuate."
Niliweka lile fuko kwenye gari langu, mara simu ya Kallo ililia alipokea:
"Haloo Kallo huwezi kuamini kambi yote imelipuliwa sijui ni mshenzi gani huyu lazima atakuwa Thereza akishirikiana na Father Gin.. Kallo..Kalo unanisikia nitawafundisha adabu labda sio mimi Marry White naapa watajuta kuzaliwa hawawezi kunitia hasara kiasi hiki subiri nirudi Italia watanijua mimi nami nitawatafuta mimi mwenyewe na kuwaua kwa mkono wangu.”
Ilikuwa sauti ya kilio ya Marry White baada ya kushuhudia jinsi nilivyo isambaratisha kambi yake vilevile alijua na watoto wote wameuawa.
"Sasa ndio itakuwaje?" Kallo aliuliza.
''Tunakuja sasa hivi tutajua la kufanya,” Marry White alikata simu.
"Umenieleza wageni wale, Waarabu wamefikia wapi?"
"Ngurudoto."
"Ok , wacha niwahi Dar tutawasiliana usiwe na wasi kila kitu kipo sawa na hii hela tutagawana sawa japo sijui ni kiasi gani.”
Niliagana na Kallo nilielekea hoteli ya Ngurudoto kuwafuatilia wale Waarabu, sikutaka ajue chochote juu ya mipango yangu. Niliwasili maeneo ya hoteli ya Ngurudoto na kuliegesha gari langu kwenye maegesho. Niliteremka na kuelekea mapokezi.
Nilimuuliza mhudumu wa mapokezi ambaye aliyeonekana kusinzia, saa yangu ilinionyesha ni saa sita kasoro. Nilimuuliza sehemu walipo wageni wale Waarabu alinijulisha wapo chumba namba 099 na 100. Niliagana naye nilimuacha akiendelea akiendeleza usingizi wake, baada ya kuondoka nilimuona akilalia kaunta kabisa. Nilikwenda hadi chumba namba 099 na kugonga wakati huo nilikuwa nimeshikilia bastolaaliyefungua nilimwekea kifuani na kumsukumia ndani.
Niliwakuta wakicheza karata usiku ule huku wakinywa kahawa iliyokuwa kwenye chupa kubwa ya chai.
Aliyenifungulia mlango nilimuamuru arudi nyuma kwa wenzake, mmoja alitaka kuchukua bastola nilimkemea kwa sauti kali kwa kumwambia akifanya ujanja wowote basi atakuwa mgeni wa kuzimu niliwaomba wanijibu maswali yangu.
“Ninyi ni akina nani mmekuja kufanya nini?”
"Sisi ni watalii tumekuja kutalii."
" Mkutano mliofanya nusu saa, mliingia mkataba wa nini na jasusi Marry White na kundi lake?”
Swali langu liliwashtua wote niliwaona wanatazamana.
"Mbona hamnijibu, mnajifanya watalii kumbe mna mchezo mchafu? Basi leo ndipo mwanzo na mwisho wenu," nilisema kwa sauti kali.
Niliifuata ile chupa ya chai yenye kahawa na kuimiminia unga wa sumu na kuwalazimisha wote wanywe. Wa kwanza alikuwa mbishi alitaka kupimana ubavu na mimi. Ngumi aliyorusha niliona nilimpiga mapigo manne ya mfululizo yaliyomvunja taya na damu kumtoka kwa wingi.
Waliobaki walikunywa kikombe kimoja kimoja na yule niliyemjeruhi naye alikunywa. Ndani ya dakika tano wote walikuwa wageni wa kuzimu, nilijisemea moyoni:
"Washenzi kama ninyi hukumu yenu ni hii.”
“Nilifanya upekuzi wa vyumba vyote walivyopanga na kukuta pesa nyingi mchanganyiko yeni, dola na pesa za Kitanzania niliziweka kwenye mfuko mmoja na kutokomea zangu.
****
Niliwasili Dar saa kumi usiku sikulala nilikwenda moja kwa moja kwenye vituo vyangu vya kulelea watoto na kukuta wote wamefika salama. Niliwapa asante wote nilioshiriki nao kwenye operesheni ile dola 1,000 kila mmoja.Nilirudi nyumbani na kupumzika kabla ya kulala nilimshukkuru Mungu kuweza kunifanikishia operesheni Pigo Takatifu PT, Baada ya kuoga nilijilaza.
Mlio wa simu ulinishtua saa ya mezani ilinionyesha tayari kumekucha ilikuwa ni saa mbili kasoro asubuhi. Nilipoangalia namba ilikuwa inatoka kwa Kallo.
"Eehe Kallo leta habari."
"Da’ Thereza kazi yako nimeisikia.”
"Ipi hiyo?"
"Ya Ngurudoto, umezidi kumchanganya Marry White, nusu aingie wazimu."
"Hiyo ndogo,” ilibidi nimweleze na ukweli wa kazi ya kambi ya Marry White.
"Aisee usiniambie kumbe wapo hai, sasa da’ Thereza ni hivi Marry White anaondoka jioni ya leo kufuata zile pesa Italia.”
"Unasema kweli?"
"Ndio mapigo uliyo mpiga yamemchanganya hivyo anafuata pesa alipe kisasi."
“Sasa sijui itakuwaje?"
"Nitaifanyia kazi."
Taarifa ya Kallo ilinivunja nguvu kwani kutokana na shuguli ya siku tatu isiyo na mapunziko nilihitaji muda wa kupumzika ili nipate muda wa kujipanga vizuri.
Lakini nilikuwa sina jinsi sababu maji niliisha yavulia nguo sikuwa na budi kuyaoga. Ilibidi niamke ili nijue nitawezaje kumawahi Marry White asichukue zile hela.
Niliamka na kuoga harakaharaka na kumpigia simu Father Gin ili aniandalie safari ya Ujerumani jioni ya siku ile.
"Vipi umeshaaanza kazi au vipi?"
"Nimeona nifanye uchunguzi kwanza kule kwenye donge nono ambalo nina imani ndio roho yako,” nilimdanganya Father Gin sikupenda ajue kinachoendelea.
"Ni kweli kabisa Thereza ukiweza kunifanikishia kuzipata hizo hela zangu zawadi nitayokupa ni ya ajabu ambayo hujaitegemea katika maisha yako yote."
Baada ya kauyli ile nilichekea moyoni na kujisemea:
“ Zawadi ya ajabu ndio hiyo ya kifo, nilimuona mtu anayejiona amevaa kumbe anatembea uchi siri zake zote zilikuwa mkononi mwangu. Vilevile nilimuonea huruma kutokana mpango kabambe wa kumteketeza na kummaliza ulioandaliwa na wenzake wanao mla mgongo bila kujijua.
"Sasa Father uhakika wa safari nitaupata saa ngapi?"
"Muda si mrefu ila we jiandae na safari vilevile kama kuna msaada wowote unaoutaka kwangu usisite njoo uchukue. Thereza wewe ndiye ninayekutegemea baada ya kifo cha Dakta Ray.”
"Hamna tatizo, halafu Father nilikuwa naomba leo kabla sijaondoka unipeleke kwenye kambi ya wale vijana, ili nikirudi niianze kazi mara moja, " nilitaka kuua ndege wawili kwa jiwe moja.
"Hamna tatizo, basi acha nishughulikie suala lako la usafiri kisha tuongozane."
"Sawa Father.”
Baada ya kukata simu nilikumbuka kuna mzigo wa pesa niliokuja nao, nilichukua mfuko na kuzihesabu zile hela nilizotoa Arusha kwenye mfuko wa mauzo wa ngozi za binadamu. Kulikuwa na dola laki nne na nusu na zile nilizochukua kule hotelini zilikuwa dola laki saba na ishirini na nne elfu.Nilitenga na kuchukua dola laki mbili na nusu ni kamwekea Kallo.
Nilichukua ramani yangu ya mji wa Dusseldorf Ujerumani, niliangalia jinsi eneo analoishi yule mkuu wa uwakala wa kununua ngozi na damu na dawa za kulevya, Ilionyesha anakaa mtaa wa Ost-strabe
Hoteli iliyopo karibu na mtaa ule ni HOLIDAN INN DUSSELDOF CITY ENTR-KONIGSA, iliyo barabara ya Harold Strabe.
Mazingira yalinionyesha kama hakutakuwa na tatizo lolote nitaweza kuingia katika chumba cha huyo mkuu bila tatizo. Nikiwa bado napanga kete zangu ili nishinde mchezo japo nilijua ni wa hatari kwani kosa langu lolote litagharimu maisha yangu, Mara simu yangu iliita, niliiangalia namba ilikuwa ya Father Gin.
"Haloo Father lete habari.”
"Mambo yamekwenda vizuri safari ipo, kama sasa hivi upo tayari njoo mara moja nikupeleke kwenye ile kambi ili upate muda wa kujiandaa na safari yako ya Ujerumani."
"Sawa nakuja."
Kwa vile nilikuwa nimeshajiandaa nilitoka kama kawaida yangu kwa kuruka ukuta na kutokea mtaa wa nyuma na kukodi gari hadi kanisani. Nilipokewa mapokezi na wasichana waliovaa mavazi ya utawa. Mabinti walipendeza kwa mtu yoyote angewaona angejua ni watumishi wa bwana kumbe ni miongoni mwa kundi la mashetani wanyonya damu.

Itaendelea
 
SEHEMU: 24
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Kwa vile nilikuwa nimeshajiandaa nilitoka kama kawaida yangu kwa kuruka ukuta na kutokea mtaa wa nyuma na kukodi gari hadi kanisani. Nilipokewa mapokezi na wasichana waliovaa mavazi ya utawa. Mabinti walipendeza kwa mtu yoyote angewaona angejua ni watumishi wa bwana kumbe ni miongoni mwa kundi la mashetani wanyonya damu.
SASA ENDELEA...

Waliponiona walinikaribisha kwa heshima na upole:
"Bwana asifiwe."
"Ameni.”'
"Karibu sana mtumishi."
"Asante."
"We ndio Thereza?"
"Ndio mimi."
"Ooh vizuri, Father amesema ukifika upite moja kwa moja.”
"Asante nashukuru."
Niliingia moja kwa moja hadi kwenye sebule bahati ndio wakati huo Father Gin alikuwa anatoka ofisini kwake.
"Ooh! Thereza karibu sana.”
“Asante Father.”
"Pata kinywaji ili tuondoke."
"Hapana Father nipo tayari."
''Ok, tunaweza kwenda.”
Niliongozana na Father Gin hadi kwenye gari Toyota Land Cruser V8 ya rangi nyeusi yenye vioo vilivyowekewa kivuli (tinted) nyeusi.
Niliongozana na Father Gin kwenye gari tulikuwa wawili, tulielekea barabara ya Kilwa baada ya ukimya mfupi Father Gin aliuvunja.
"Thereza ukifanikisha operesheni kuna mpango ambao nina imani utaniingizia pesa nyingi.”
"Upi huo?" nilimdodosa bila kujua.
"Nataka kupandikiza ugonjwa na dawa nitauza mimi."
"Utafanya vipi?”
"Unajua Thereza siku zote mtu akipanga kitu si kukurupuka hili nimelipanga muda mrefu na kama si upuuzi wa Marry White na wenzake ungekuwa umeanza ni hivi nimetengeneza virusi ambavyo nimevirutubisha kwenye mwili wa binaadamu ambao utaleta ugonjwa wa ajabu ambao dawa yake haitapatikana popote ila kwetu.
"Na tutauza kwa bei nafuu kwani wengi watanunua kwa ajili ya kinga hapo tutakusanya mamilioni ya pesa si Tanzania tu hata majirani lazima watanunua kwa ajili ya kinga.''
"Mmh! Sawa sasa unatarajia kuufanya lini huo mpango?”
"Baada ya operesheni hii."
Wakati huo tulikuwa tumefika Chamazi tuliacha barabara kubwa na kuingia kushoto, tulikwenda mwendo wa robo saa ndipo tulipofika kambi ya Father Gin. Ilikuwa imejengwa vizuri tofauti na ya Marry White. Ukifika utasema ni chuo cha dini jinsi wahudumu wake walivyovaa sare zao za utawa. Asilimia kubwa ya sehemu za Father Gin wafanyakazi wake wengi ni wanawake.
Nilipokelewa kwa heshima kama vile ni watumishi wa Bwana wa kweli lakini kumbe nyoyo zao zimeshabadilishwa na shetani anayejiita Father. Lakini Mungu hamfichi mnafiki nilijua ipo siku siri yake itakuwa hadharani kama si mimi basi yupo mwingine atayetokea kwa uwezo wa Mungu.
Alinitembeza kambi yote ambayo ilikuwa kubwa, iliyokuwa na vijana elfu nne. Pia alinitembeza kwenye kambi yote kwenye mitambo ya kunyonyea damu matanuru ya kuchomea watu.
Mitambo ya Father Gin ilikuwa mingi ila iliyoanza kuchakaa tofauti na ya Marry White. Niliiangalia mandhari ya mule ndani na eneo lote. Vilevile ulinzi ulikuwa dhaifu ilitokana kuvuli chao cha utumishi wa dini. Udhaifu huo nilijua ndio utaonisaidia kuwakomboa vijana ambao walionekana wana afya njema wanaoyafurahia maisha kumbe ni zao la damu na ngozi.
"Thereza umeona mali ilivyopendeza? Wewe tu, watoto wanazidi kunipa hasara wanakula tu kama mchwa kila siku napoteza si chini ya laki tano."
Sio siri moyo uliuma kusikia eti mtu anawaita wanaadamu wenzake mali. Nilijikuta nahama kimawazo niliijiwa na picha ya ajabu pale nilipojiona kama nitakufa basi watoto wote walio kwenye vituo vya kulelea watoto wa mitaani, yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ndio watakuwa vuno la kuwaingizia pesa madhalimu hawa. Hata Father Gin aliponiita nilikuwa mbali:
“Vipi Thereza una mawazo gani? Inavyoonekana hatuko pamoja.”
"Ni kweli Father."
"Unawaza nini?”
"Kuhusu safari yangu, nilimdanganya.
”Utashinda nakuamini."
Tulirudi mjini na kuagana na Father Gin baada ya kuniongezea vitendea kazi vya hali ya juu. Nilipita sehemu niliyomweka Kalekwa alelewe. Hali yake ilikuwa inaendelea vizuri, nilirudi hadi nyumbani na kujiandaa na safari ya Ujerumani.
****
Majira ya saa moja na nusu nilikuwa ndani ya shirika la ndege la Swiss Airways majira ya saa mbili kasoro ndege iliondoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere. Nilikuwa na mengi kuhusu safari yangu nilijiuliza uwezo wa watu ninaokwenda kupambana nao. Wasiwasi wangu ulikuwa juu ya uwezo wa jasusi mkuu kuwa ni mkubwa.
Niliwasili mji wa Dusseldort. Ujerumani majira ya saa tatu usiku siku ya pili. Uwanja wa ndege ulikuwa na pilikapilia polisi walikuwa wengi na msako ulikuwa mkubwa kutokana na tishio la kigaidi.
Ilibidi wageni tuchelewe kwa saa mbili, upekuzi wao tuliruhusiwa kutoka uwanja wa ndege wa Rhein Ruhr Flughfeh Dusseldort. Flughfeh Dusseldort.
Nilikodi gari hadi hoteli ya Holiday in Dusseldof City CNTR-Kowegsa iliyopo barabara ya HoroldsstraBe. Nilipofika nilichukua chumba na kuweka vitu vyangu nilijikoki vitu muhimu na kutoka. Mji wa Dusseldof ulikuwa na pilika pilika kila mtu alikuwa na shughuli zake hakuna aliyekuwa na habari na mwenzake.
Nilitembea kwa miguu kutoka mtaa wa Horold straBe kwa mwendo wa kuharakisha kidogo, usiku ule hali ya hewa ilikuwa ya baridi.
Nilitembea hadi njia panda ya Horold straBe na Ost-straBe nilikata kushoto na kuanza kuitafuta nyumba anayoishi Mr Michael, jasusi wakala mkuu vile nilipata historia yake ni trionea anayetikisa kwa utajiri.
Nyumba niliiona niliipita na kwenda kwa mbele kwenye mtaa wa mbele kwenye mtaa wa Stein-str nilikata kushoto hadi kwenye mtaa kipande ambao unarudi hadi mtaa wa Harold. Niliufuata ule mtaa wa tahadhari kubwa na kuangalia labda kuna mtu ananifuatilia lakini hakuwepo.
Nilivuka kama nyumba sita na kuingia kwenye uchochoto mmoja kama ramani ilivyonionyesha. Nilikwenda hadi nyuma ya jengo alilopanga Mr Michael.
Niliangalia kulia na kushoto lakini hapakuwa na kitu cha kunitilia hapakua na kitu cha kunitilia wasiwasi.
Nilitoa glovu zenye makucha na viatu vyake maalum kwa kupandia ukuta na miamba na kuvaa mikononi na miguuni, nikaanza kuukwea ukuta hadi ghorofa la tatu. Sehemu nilijiingiza hadi ndani ya bafu. Hakukuwa na mtu mlango pia ulikuwa haukufungwa.
Nilisikia watu wakizungumza, nilichungulia taratibu, na kuwaona watu wawili mzee mmoja wa makamo mwenye tumbo kubwa na kichwani vinywele kidogo lakini sehemu kubwa ya kichwa ni upara.
Alikuwa na mwanamke ambaye si mwingine ila Marry White walikuwa kwenye Computer. Mara waliacha walichokuwa wakikifanya kwenye Computer na kuanza kupapasana kimahaba mara niliona wakishikana mkono na kuondoka pale. Kutokana na hali niliyowaona nayo nilijua wamekwenda chumbani kurusha roho.
Nilisubiri kwa muda kisha nilinyata kuwafuatilia, nilipofika nilikiona chumba na mihemo ya watu walio kwenye dimbwi la mahaba ilisikika. Nilirudi hadi kwenye Computer nilikuta ndio zile pesa zinataka kuhamishiwa kwenye akaunti ya Marry White, lakini bado hazijatumwa. alikuwa ndio anaingiza namba za akaunti ya Marry White. Mara simu ya Marry White iliyokuwa juu ya meza ililia nilijikuta napagawa kwani nilikuwa nimefuta namba za akaunti ya Marry White ili niingize zangu. Nilijikuta nimetaharuki nilijiuliza nirudi chooni au nijifiche chini ya meza ile.
Ndani nilimsikia Marry White akimuomba samahani Mr Michael ili atoke kusikiliza simu. Niliamua kujificha chini ya meza, Marry White mara alitoka chumbani akiwa hana kitu mwilini, yaani mtupu, si unajua alikuwa kwenye rusha roho.
Alitoka akiwa hana wasiwasi alijiamini kwa kiasi kikubwa akijua sitaweza kuwepo eneo lilie. Niliamini kama ningemuibukia mbele ya uso wake lazima angekufa kwa mshtuko. Alitoka hadi kwenye meza ile ya Computer na kuchukkua simu yake iliyokuwa bado inaita:
"Haloo Jimmy kuna habari gani?”
"Vipi umefika salama?"
"Aah hilo si la kuuliza, nimefika salama ni sekunde chache nakamilisha mambo yote nikirudi ni chereko chereko."
“Ndicho tunachokisubiri sio siri sister, huyu malaya katutia hasara lazima nimchune ngozi kwa mikono yangu siku tutapomtia mikononi.”
“Hana ujanja ngoma yake ya kitoto haikeshi, nikirudi ajue amekwisha na huyo hawara yake shetani Gin."
"Jimmy vipi kuna jipya maana simu inaonyesha si ya kawaida?"
"Ni kweli sister."
"Ee’he, kuna nini tena?"
"Habari za mtandao zinasema Thereza ameonekana jioni ya jana anasafiri kwa shirika la ndege la Swiss Airways hatujui amekwenda wapi."
"Mmh! Mna uhakika na mnachosema?"
"Ndio maana tukakutaarifu isije kuwa anakufuatilia."
"Mmh! Sidhani, lakini nitafanyia kazi hata hivyo kishachelewa pesa yote nimeshaidhibiti hilo lisikutie wasi.”
"Hapana dada yule msichana ni hatari kwani maisha yako vilevile ni muhimu."
"Nashukuru kwa taarifa yako nitakuwa makini kuanzia sasa."
"Sawa sister ni hayo, kama kuna mengine nitakujulisha, sijui unarudi lini?"
"Kazi imemalizika, nisubiri nini narudi usiku huu huu.”
"Ok sister kazi njema.”
"Asante,” Marry White alikata simu wakati huo Mr michael alikuwa akiunguruma ndani kwa uchu kama fisi aliyenyang'anywa mfupa.
"Sweet fanya haraka bwana simu gani mwaka mzima?”
"Nakuja darling si unajua napata habari za Tanzania, nipo kwa ajili yako ushindwe wewe tu."
Marry White aliirudisha ile simu juu ya meza na kurudi chumbani kuendeleza kurusha roho na Mr Michael. Kwa upande wangu kila kilichokuwa kikifanyika nilijua ni uwezo wa Mungu. Marry White hakushtuka chochote wala hakuwa na wazo lolote la mabadiliko kwenye Computer japo alikuwa anatazamana nayo.
Aliporudi chumbani kuendeleza 'uchafu' wao nami nilichukua nafasi ile kufanya kilichonileta. Niliingiza namba za akaunti yangu na kuzituma zile pesa trion 150 bila pingamizi ziliingia kwenye akaunti yangu.
Nilichokifanya ni kuiunguza program ya Computa kufuta ushahidi niliweka kinasa sauti chini ya meza ya Computer ili kunasa mazungumzo yao wataporudi kutoka kwenye uchafu wao.
Nilitoka kwa kupitia njia niliyoingilia ni kuwaacha wapo juu ya kilele cha mahaba kila mtu akimwagia sifa mwenziwe. Nilipitia dirisha la bafuni na kutoka nje niliteremka ukuta ule mpaka chini. Wakati nafika chini nilishtukia mwanga mkali wa tochi, alikuwa mmoja wa askari wa doria.
"Haloo unatoka wapi?”
"Najisaidia afande."
"Usinichezee yaani unajisaidia juu ya nyumba za watu?"
“Watu?" nilijifamnya kushangaa.
Wakati huo alikuwa ameshanifikia karibu na kuanza kunipekua mikono ikiwa juu.
Nilijua ishakuwa noma, nilitulia nikipanga jinsi ya kujitoa mikononi mwa yule mnoko.
Vitu nilivyokuwa navyo sikuwa na tofauti na gaidi lazima ingehusishwa moja kwa moja na ugaidi.

Itaendelea
 
SEHEMU: 25
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500
.ILIPOISHIA:
Wakati huo alikuwa ameshanifikia karibu na kuanza kunipekua mikono ikiwa juu.
Nilijua ishakuwa noma, nilitulia nikipanga jinsi ya kujitoa mikononi mwa yule mnoko.
Vitu nilivyokuwa navyo sikuwa na tofauti na gaidi lazima ingehusishwa moja kwa moja na ugaidi.
SASA ENDELEA...

Aliponieleza nigeuke ili aendelee kunipekua nilitumia nafasi ile kusogea mbele kidogo na kugeuka na teke jepesi lililompata shingoni na kumpotezea fahamu. Nilimvuta pembeni na kumlaza pale uchochoroni. Harakaharaka nilirudi hotelini kupitia ule mtaa mfupi hadi mtaa wa Horold streBc.
Nilichepua mwendo hadi hotelini ambapo nilichukua mzigo wangu na kuondoka usiku ule ule. Bahati nzuri nilipata nafasi ya ndege iliyokuwa ikiishia Oman. Niliingia kwenye ndege moyo ukiwa bado si wangu.
Nilijiuliza nitatoka salama kweli? Nikiwa nimo kwenye ndege ya Gull Air nimetulia kwenye kiti changu head phone zikiwa maskioni niliwasikia Marry White na Mr Michael:
"Haloo sweet hii computer imefanya nini mbona imezima?"
“Nikuulize wewe.”
"Nitajuaje wakati tulikuwa wote?"
"Ooh..aisee huwezi amini computer imeungua.”
"Acha utani Mr Michael!”
"Ni kweli si unaona vipimo?”
"Haiwezekani! Basi washa nyingine.”
“Kumbukumbu zote zilikuwa humu, haijawahi kutokea lazima umenichezea akili Marry White.”
"Sikuelewi Mr Michael."
"Marry White nieleze ukweli nani amefanya hivi?”
"Usinichanganye Mr Michael unataka kunitapeli?"
"Hebu ngoja."
Baada ya kama dakika saba nilimsikia Mr Michael akisema:
"Marry White unanifanya mimi ni mtoto?"
"Kivipi?”
"Unaona hii.. pesa zote trion 150 zimehamishwa! kibaya zaidi mmeniulia na computer yangu muhimu kama roho yangu ni vitu vingapi vimepotea?"
"Usinichanganye, usiniletee ujanja pesa yangu utaitoa tena safari hii si kwa kuihamisha bali unanipa mkononi.” Nilisikia sauti ya Marry White.
"Unacheza binti yaani ujanja uliomfanyia Father Gin ndio umenigeuzia mimi? Hapa utachemsha kwanza toka humu ndani, ushanitia hasara kubwa.”
"Humu ndani sitoki mpaka umenipa hela yangu la sivyo nitakuua kama nilivyo muua mkeo."
"Binti mtu mzima atishiwi nyau kabla hujaniua utakufa wewe."
Dakika tatu baadae nilisikia sauti za mapigano na vilio vya maumivu, vilivyodumu zaidi ya dakika kumi..mara nilisikia sauti ya muhemo ya Marry White:
"We firauni huu ni mtambo mzito hao vijana wako sita hawatoshi labda ungekuja na jeshi zima..sasa nasema hivi nataka hela yangu au nakufumua ubongo," nilimsikia akihesabu:
Moja mbili tatu..tatu tatu shiti," nilisikia mlio wa bastola ikimaanisha Marry White kamuua Mr Michael.
"Huwezi kuniletea utapeli nikuache," sauti ya Marry White ilitamba.
Palitokea utulivu wa muda wakati huo ndege ilikuwa hewani mara nilimsikia akisema:
"Oooh..afadhali wacha niondoke na hizi hundi za Mr Michael zitapunguza maumivu, si siri mbona mwaka huu wangu sijui ni nani aliyefanya nchezo huu mchafu au Thereza? ..Inawezekana ni njama Mr Michael kunihadaa kimapenzi ili anidhulumu lakini kwa nini sikufanya nilicho kifuata na kujiingiza kwenye mapenzi na kuvuruga kila kitu? Acha niondoke niwahi ndege sehemu hii sasa hivi haifai."
Mara nilisikia sauti ya mlango kufungwa kuanzia hapo sikusikia kitu chochote nilijua Marry White ameshaondoka.
Nilimshukuru kazi yangu ilikwenda vizuri bila kumwaga damu, vilevile kupunguzana wao kwa wao nina imani mzizi mkuu Mr Michael ulisha ng'oka matawi Marry White na Father Gin watakuwa wepesi.
Nilipofika Oman niliunganisha ndege hadi nyumbani Tanzania, nilipofika nilikwenda kwangu moja kwa moja nilikuwa nimechoka kupita kiasi. Nilipofika nyumbani nilioga na kujilaza hata bila kula. Usingizi ulichukua masaa manane bila kugeuka. Nilijipa mapumziko ya wiki nzima bila kujishughulisha na chochote zaidi ya kumchukua mdogo wangu Kalekwa kuwa naye muda wote wa mapumziko na afya yake iliendelea vizuri.
Baada ya wiki, nikiwa nimetulia mara nilipata simu toka kwa Kallo:
"Vipi Kallo?"
"Da Teddy ni hivi, sasa hivi huku watu wamepagawa baada ya kuzikosa trioni 150 japo wameambulia trion 10 kutokana na hundi alizozichukua Marry kwa Mr Michael na una taarifa kama wakala mkuu Mr Michael aliuawa na Marry White?"
"Hata sijui..kwani nini?" nilijifanya sijui kitu.
"Anasema eti amemzidi akili lakini maelezo yao yanakulenga huenda ni wewe hivyo mkakati uliopangwa utafikiri Marekani walivyo mkamata Saadam Husein da’ Teddy kuwa makini ni watu waliotumwa si watu wa mchezo.”
"Usiwe na wasi mdogo wangu na kwa taarifa yako trioni zote 150 nimezichukua."
"Acha utani da Teddy!”
"Mi na wewe hatuna utani ni hivi sasa ndio naingia kazini rasmi, japo wananitafuta moto utawawakia, usihofu ndugu yangu asante kwa taarifa yako muhimu."
"Kweli we kiboko!”
"Tumeombe Mungu turuke salama ili uje uishi maisha ya peponi."
''Na dua zetu Mungu atazipokea.”
"Ameni,” nilikata simu.
Wazo lilinijia niende kwa msaidizi wa Father Gin yeye mwenyewe anapokuwa yupo nje. Alikuwa mama wa makamo mwenye sura ya upole, uso wake ulijengeka huruma sikuwahi kumkuta akiwa na furaha. Sikujua kwa sababu gani, mwanzoni nilijua huenda dini imemuingia hata kauli zake ni za kukujaza moyo ili usiwe mnyonge.
Lakini kumbe alikuwa na sura ya shilingi yenye pande mbili upande mmoja mtu mpole mwema na mkarimu lakini upange wa pili alikuwa msaidizi mkuu wa jasusi Father Gin. Sikuelewa yule mama alikuwepo sehemu inayomchukiza mwenyezi Mungu kwa kupenda kwake, njaa au ni vitisho kama alivyopata Kallo na wenzake ndio vimefanya awepo pale.
Nilijua ningepitia kwa mama huyo aliyefahamika kama mama Monika mwenye miaka 58-60 ningepata maelezo mengi kuhusu Father Gin ambayo yangenisaidia kumteketeza kirahisi lakini pia kujua mradi wake na maabara yake aliyorutubisha virusi vya ugonjwa ili niharibu mpango wake. Niliamini dawa ni kumvamia mama Monika nyumbani kwake.
Niligundua kwamba nyumba yake ilikuwa mulemule ndani ya kambi ya Kimanzichana. Niliamini kwanza uvamizi wangu isingemshtua mtu yeyote kwani wengi wangejua mimi ni mtu wao. Nilipanga siku ile majira ya saa kumi na mbili nimfuate nyumbani kwake muda huo huwa amepumzika kwa ajili ya kazi ya kutwa nzima.
Majira ya saa kumi na mbili jioni niliruka ukuta kama kawaida yangu na kutokea upande wa pili. Kutokana na msongamano wa magari na utundu wa dereva tulifika Mbagala rangi tatu saa kumi na mbili na nusu. Tulipovuka Vikindu nilishangaa kuona gari letu limezingirwa na magari zaidi ya matano.
Tulitulia bila kuteremka garini lakini nilikaa mkao wa shari kwani nilijua nipo msambweni. Mara aliteremka mwanaume mmoja mwenye mwili mkubwa wa mazoezi na kuja kwenye gari letu.
Alifungua mlango na kumtoa dereva kwa kumtupa nje, alinifuata na kunishika kunivuta nje. Alinibeba juujuu hadi kwenye uwazi na kunitupa chini, nilibakia nikishangaa nikijua nimepatikana ni yale niliyoelezwa na Kallo. Nikiwa bado nipo chini nilipotupwa mara liliingia Benzi moja jeusi.
Lilisimama katikati ya magari yaliyokuwapo pale, mtu mmoja mwenye mwili mkubwa uliojengeka kimazoezi aliyevalia fulana iliyombana barabara mwilini alikwenda kufungua mlango.
Aliteremka Marry White alisimama nje ya Benzi na kuliegemea kisha alinifuata pale chini nilipokuwa. Alinishika uso wangu na kuunyanyua kisha alisema:
"Hongera sana."
"Asante," nilijibu kwa jeuri.
"Umejitahidi, lakini nilijua ngoma yako ya kitoto haikeshi na kweli haikukesha sasa ndio utanijua mimi ni nani..huyo hawara yako shetani Gin ananijua mimi nani?” sikumjibu kitu nilimwangalia tu.
"Yaani bosi aliyekuwa anatusumbua hivi ni huyu?” aliuliza yule baunsa aliyenitoa kwenye gari.
"Ni huyu.”
"Hata mimi nashangaa basi ndio ameshaingia kwenye moto wa gesi, atabakia majivu.” Kallo alikuwa miongoni mwa watu waliokuwepo pale alimuona aliniangalia kwa uso wa huruma kwa kuamini ule ulikuwa mwisho wangu.
"Jamani shughuli yote uwanja wa damu au sio?” alisema Marry White.
"Ndiyooo,” waliitikia wote.
"Lakini hawezi kuondoka hivi hivi kama mwari yeye si mjuzi wa kupigana, George vipi upo tayari?”
"Ndiyo bosi, nampasua kifua.”
"Haya kazi kwako,” George alijianda kunishikisha adabu.
Nikajua pale maisha yangu yako hatarini kupona ni vigumu, nilitumia nafasi ile kuondoka na watu watakaojipendekeza. Nilipomuona yule mwenye mwili mkubwa anakuja nilinyanyuka.
Kama kawaida alipotaka kunipiga teke nilimpisha kidogo na kupiga teke la mchongoko kwenye sehemu zake na siri, alipiga kelele za maumivu. Nilijua pigo lile lilimtosha, alikuwa akilia huku akigaagaa chini kwa maumivu. Wa pili yeye nilimmaliza kwa teke la kuzunguka yeye alipiga la juu mimi nikausomba mguu wake chini na kummalizia na kifuti kilichomvunja shingo yake.
Kuona hivyo ndipo walipokuja wengi hapo kwa kweli nilipigana kufa ama kupona. Katika watu kumi na tano nilifanikiwa kuwaua saba lakini nilipigika sana. Ndipo Marry White alipowaamuru waniache akavua nguo zake na kubakia na 'skin tight' iliyombana vyema na kuanza upya mpambano.
Mwanzo tulipigana vilivyo kila mtu alionyesha uwezo wake, lakini kwa vile nilikuwa nimepigana kwa kipindi kirefu nilikuwa nimechoka sana. Hali ile ilimpa nafasi Marry White kunipa kipigo mpaka nikapoteza fahamu.
 
SEHEMU: 26
MTUNZI: Ally Mbetu ‘DrAmbe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Marry White alipowaamuru waniache akavua nguo zake na kubakia na 'skin tight' iliyombana vyema na kuanza upya mpambano.
Mwanzo tulipigana vilivyo kila mtu alionyesha uwezo wake, lakini kwa vile nilikuwa nimepigana kwa kipindi kirefu nilikuwa nimechoka sana. Hali ile ilimpa nafasi Marry White kunipa kipigo mpaka nikapoteza fahamu.
SASA ENDELEA...

Nilipozinduka nikijikuta nimefungwa kwenye nguzo yenye umbile la msalaba nikiwa mtupu kama nilivyozaliwa. Mazingira yaliyokuwepo kuokoka kwangu kulitegemea miujiza ya Mungu tu na si kitu kingine.
Kwani sikuwa na mtu aliyekuwa ananifuatilia au kunilinda nilikuwa peke yangu mahali pale. Nilikuwa nimefungwa kwa kamba madhubuti hata kama ingekuwa meli isingeyumba.
Nilikuwa nasikia baridi kali na muda wote huo mvua ilikuwa inaendelea kunyesha, ilionesha ubaridi wa kukaribia alfajiri, eneo lile hapakuwepo na mtu zaidi yangu.
Nilijiuliza ina maana pale ndio uwanja wa damu aliposema Marry White, sehemu niliyoelezwa na Kallo kuwa hutumika kutoa adhabu za kuchuna ngozi na kucharangwa mashoka kama buchani.
Moyo wangu ulishtuka baada ya kuliona gogo kubwa linalo fanana na yale yanayotumika katika mabucha, lilikuwa na michirizi ya damu. Kwa vile macho yangu yalikwisha kuzoea hali ya hewa niliweza kuona mafuvu na vipande vya mifupa ya binadamu.
Kufikia hapo moyo ulikufa ganzi na kujua nimekwisha sikuwa na ujanja, nilijua lazima ningekufa kifo cha kukatwa shingo na shoka au kuchunwa ngozi na kisha mwili kuliwa na mamba.
Kwa kweli kilichobakia ilikuwa ni kuomba Mungu ashushe miujiza yake kama alivyowashushia mitume wake kutoka enzi za akina Ibrahim baba wa imani, Musa, Yakubu, Daniel, Mkombozi wetu Yesu Kristo na Mtume Muhammad.
Japo ilikuwa ni vigumu sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano, lakini nilijipa moyo kwamba yote kwa Bwana yawezekana. Baridi ilikuwa kali hadi mwili niliusikia umekufa ganzi na kiu kilikuwa kikali na njaa niliisikia kama tumboni kulikuwa na msasa.
Suala la njaa sikuitilia maanani zaidi ya uhai wangu ambao sikuwa na uhakika nao. Katika kitu kilichouumiza moyo wangu kushindwa kutimiza dhamira yangu ya kutokomeza udhalimu na kuwakomboa watoto waliokuwa katika hatari ya kutokomezwa kwa kuchunwa ngozi na kunyonywa damu.
Ningejisikia fahari kubwa kufa baada ya kutimia dhamira yangu lakini ndivyo hivyo,
nilikuwa nimekata tamaa kwani nilijua siku zote mwanadamu hupanga yake na Mungu hupanga yake. Lakini niliamini kitu kimoja kwamba, Mungu kwa uwezo wake baada ya kifo changu atamwinua mwingine kama alivyo niinua mimi ili amalizie kazi niliyoianzisha.
Nikiwa katikati ya mawazo mazito, mara nilisikia mingurumo ya gari nilipo nyanyua macho yangu niliyaona magari zaidi ya manne yakielekea sehemu niliyokuwepo. Matatu yalikuwa ya wazi yaliyojaa askari wenye silaha nzito na moja lilikuwa kawaida Toyota Land Cruiser.
Waliteremka watu zaidi ya 12 waliokuwa na silaha wote walizielekeza kwangu, watatu walipanda juu na kunifungua kamba na kisha waliniteremsha chini.
Nilikuwa kama gaidi au siku Osama atakapokamatwa na Marekani, jinsi nilivyokuwa chini ya ulinzi mkali. Nilivishwa koti refu nzito, na kulivaa mwili ulikuwa hauna nguvu hata kutembea nilitembea kwa shida.
Niliingizwa garini na safari ilianza kutoka kwenye uwanja ule wa damu, nikiwa ndani ya gari nilifunguliwa pingu na kupewa onyo kali:
"Sikiliza we malaya ukileta ujanja mwili wako tutageuza ubao wa shabaha."
Ilionyesha ni jinsi gani walivyoniogopa kwani nilikuwa chini ya ulinzi mkali huku mitutu zaidi ya sita ilikuwa imenielekea mimi. Gari liliendeshwa kwa kasi kwa mwendo wa nusu saa tulifika eneo moja ambalo lilikuwa na jengo lililoonyesha bado halijamalizika vizuri vilevile kulikuwa na milio ya jenereta ikionyesha jengo lile halikuwa na umeme.
Niliingizwa ndani ya lile jengo na kupelekwa moja kwa moja kwenye jengo la mikutano. Ndani ya ule ukumbi nilimkuta Marry White na washirika wenzake wote.
Niliingizwa hadi kwenye meza kubwa tukawa tunatizamana na wale mumiani, nikiwa mtupu kama nilivyozaliwa, niliamriwa niketi nami nilitee amri.
Marry White uso wake uliokuwa umekunjamana kwa hasira aliniuliza swali lilelile la awali:
"Nafikiri sasa tutaelewana haya jibu swali langu kwa nini umenitia hasara?"
"Una swali jingine au hilohilo?" nami nilimjibu kwa swali.
"Ninayo mengi lakini jibu kwanza hili."
"Uliza jingine hili nilishalijibu awali."
Jibu langu lilimzidisha hasira Marry White alinyanyuka na kunifuata pale nilipo kuwa na kunishika sehemu za mdomoni na kuanza kunibana kwa nguvu:
"Thereza nitakuumiza jibu swali langu," maumivu yalipozidi nilimuomba aniachie.
"Haya nijibu."
"Ukinieleza kwa nini ulitaka kuniua na mimi nitakuwa na jibu kwa sasa sina jibu hata ukinikata kichwa.”
"Sikiliza binti utaongea katika mazingira magumu kitu ambacho sipendi kikutokee," alinichimba mkwara.
"Nasema sina jibu zaidi ya nililokuuliza jibu unalo wewe mwenyewe."
"John naona huyu binti analeta utani hebu mwite Zimwi Shetani na Roho ya Chuma."
Yule jamaa mwenye mwili mkubwa alitoka kuelekwa nje ya jengo, mara aliporudi alikuwa ameongozana na watu wawili wenye miili ya kutisha mmoja mfupi alikuwa hana tofauti na mzee Ole wa kwenye gazeti la Sani ungemuona ungejua ni yeye au pacha wake.
Walipofika walisimama mbele ya Marry White na washirika wake waliinama kuonyesha wameitikia wito. Walikuwa na miili ya kutisha iliyogawanyika walikikuwa vifua wazi chini walivalia chupi za ngozi ya chui.
"Zimwi Shetani," Marry White aliita.
"Naam Malkia."
"Nataka umuonyeshe huyu binti kuwa sisi si watu wa mchezo."
''Sawa Malkia."
Kusikia vile niliingiwa na woga na mwili ulianza kutetemeka ile hali Marry White aliiona na kuniambia:
"Unaogopa nini we si unajifanya umemaliza? Basi leo ndio utaijua sababu iliyomfanya kuku asikojoe."
Zimwi Shetani alikuwa ameweka shoka yake begani, shoka ya mpini wa chuma ilionekana ina makali ya kutisha.
"Mleteni mtu wa mfano aone kama atakataa kujibu jinsi tutakavyo mfanya huyo wa mfano."
Aliondoka kijana mmoja na kurudi na mtu aliyekuwa amefungwa kitambaa usoni alipofikishwa mbele na alifunguliwa kitambaa. Alionekana mtu aliyejikatia tamaa machozi yalimtoka muda wote tangu alipofikishwa pale mbele. Sio siri nilimuonea huruma na kuyasahau yalio mbele yangu.
Zimwi shetani alitoka nje na kurudi na gogo kubwa la kubebwa na watu zaidi ya wanne tena walioshiba. Lakini mwanaume wa shoka alilibeba peke yake , duniani wapo viumbe wanaotisha mmojawapo ni yule mbaba.
Lile gogo liliwekwa mbele kisha yule mtu alilazwa juu ya lile gogo, kabla ya kulazwa alivuliwa nguo zote na kubakia mtupu. Zimwi Shetani alipaka unga mweupe mikononi ilionyesha kama poda kisha alichukua lile shoka lililokuwa pembeni na kulipunga hewani.
Ulikuwa kama mchezo vile wakati Zimwi Shetani alipoliteremsha shoka lake kwenye mwili wa yule mtu aliyelazwa juu ya gogo. Mwanzo niliona kama utani lakini aliporudia pigo la pili nilipiga kelele na kufumba macho sikuangalia kilichooendelea zaidi ya kusikia kishindo cha shoka.
Shoka lilipotulia nilifumbua macho, mmh..kama kuna binadamu wenye roho mbaya basi yule mbaba ni namba moja. Juu ya gogo kulikuwa na vipande vya nyama ya mtu na pale pote palikuwa pametapakaa damu iliyomchafua yule zimwi shetani sehemu za tumbo kifua na usoni.
Nilijikuta naingiwa na woga wa ajabu lakini nilijikaza kikie ili kuficha woga wangu. Marry White alinigeukia na kunieleza:
"Nafikiri mfano hai umeuona sasa chaguo moja ucharangwe kama nyama au ujibu maswali yangu kwa ufasaha," alisema yale huku watumishi wake wakikusanya nyama za yule mtu aliyeuawa kikatili na kuziweka kwenye mfuko wa plastic.
Swali nilisikia lakini moyoni niliapa kuwa sitamjibu vizuri maswali yake kwa kujua kama nitamjibu lazima atapata faida na kisha kuniua. Niliona bora nife kuliko kumpa faida mshenzi mumiani mkubwa. Alipoona simjibu alinifuata tena na kunishika sehemu za mdomo na kuniuliza:
"Utanijibu hunijubu?"
Sikumjibu kitu, nilikaa kimya hali iliyompandisha hasira na kuanza kunipiga ngumi za usoni zilizozidisha hasira zilizonitoa damu puani na mdomoni nilisikia sehemu za pembeni ya mdomo zimechanika. Lakini vilevile sikujibu nilikaa kimya.
Alipotaka kuniuliza tena nilimtemea mate usoni yaliyochanganyikana na damu, Marry White alinipiga teke lililonirusha kwa nyuma na kuniacha uchi nilimsikia akisema:
"Zimwi shetani hebu fanya kazi yako naona analeta utani."
ITAENDELEA WHATSAPP
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom