Hadithi: Kesi ya Mzee Mnyoka

CK Allan

JF-Expert Member
Aug 14, 2013
2,729
5,923
KESI YA MZEE MNYOKA 01

Mzee Mnyoka alikua na kawaida ya kuchelewa kurudi nyumbani kwake, Mzee Mnyoka hakua mlevi au mchawi lakini tuseme tu hakua na mazoea ya kurudi nyumbani mapema.

Siku ya Alhamis Kama ilivyo kawaida yake Mzee Mnyoka alikua akirudi nyumbani kwake majira ya saa 4:45 hivi usiku. Akiwa mita kadhaa kabla ya kufika kwake kwa mbali alimuona mwenyekiti wake wa Kijiji akiwa anaburuta ng'ombe dume.

Mzee Mnyoka kwanza alijifanya hajamuona mwenyekiti, Mzee Mkude, lakini baadae Mzee Mkude alimuona Mzee Mnyoka , hivyo wakaonana macho kwa macho! Na ndipo Mzee Mkude akastuka sana na kutahayari!

“Kwanza Mzee Mkude hakuwa anafuga hata kuku nyumbani kwake! Lakini pia hakuwahi kufanya biashara ya nyama! Na hivi karibuni hajatangaza sherehe yoyote! Sasa huyu ngo'mbe usiku huu anampeleka wapi?”
Nahisi hicho ndicho kilichomstua Mzee Mkude! Mzee Mnyoka aligundua mfadhaiko wa mwenyekiti lakini hakuona Kama Kuna umuhimu wowote wa kuendelea kushangaa Mambo yasiyo mhusu! Mzee Mnyoka akajiendea zake nyumbani.

Kesho yake ijumaa habari zikaanza kusambaa kwa Kasi kuwa Mzee Pembe ameibiwa dume lake alilopewa Kama malipo ya mahari baada ya kumuoza binti yake Asha!

Msako ukaanza ili kumbaini mwizi wa lile dume, hatimaye siku ya jumamosi Mzee Mnyoka na Mzee Mkude wakakutana! Walipotazama hakuna aliyeongea kitu lakini macho yao yalizungumza!

Macho ya Mzee Mnyoka yalisema wazi wazi "najua mwizi Ni wewe" Huku macho ya Mzee Mkude yakisema "Ole wako unitaje!" Hatimaye wakasalimiana na Mzee Mnyoka akaaga na kuondoka kwa haraka, huku Mzee Mkude akipigwa na mshangao! Maskini Mzee Mnyoka alijilaumu kuona mpaka Sasa mwizi akiwa bado hajakamatwa, lakini ilimuuma Sana kuona huyo mwizi Ni mwenyekiti wake wa Kijiji,
Mzee Mnyoka alichoka!

****
Mzee Mnyoka alikuwa na kawaida ya kuchelewa kurudi nyumbani ndio, lakini siku za jumapili na mwisho wa mwezi Mzee Mnyoka alikua anawahi Sana! Na pengine siku nyingine hakutoka kabisa!
Siku hiyo jumapili baada ya siku tatu kupita tangu wizi utokee Mzee Mnyoka akiwa nyumbani kwake akisuka mkeka alipokea wageni wa kustaajibisha.

Polisi! Ndio, polisi walifika na kumueleza Mzee Mnyoka kuwa yupo chini ya ulinzi kwa tuhuma za kuiba Ng'ombe dume wa Mzee Pembe!

Mzee Mnyoka alikataa Kata Kata! Lakini polisi wakambeba msobe msobe na kwenda kumuweka lupango, huku wakimtolea maneno mazito kuwa atakoma, na huo ndio mwisho wa wezi kama yeye.

**********
Mzee Mnyoka alipiga kelele huku machozi yakimtoka "Jamani mnanionea! Mnanionea! Sijaiba Mimi! Sijaiba Mimi!" Wale polisi waliendelea kucheka na kupiga stori zao huku wakimuamuru Mzee Mnyoka kuacha makelele.
"We Mzee, hakuna mtu aliletwa hapa akakubali kosa kirahisi, wewe tuachie makelele yako hapa sio nyumbani kwako" Polisi mmoja aliongea huku wenzake wakimuunga mkono.

Nyumbani kwa Mzee mnyoka, mkewe hakupata usingizi, pamoja na tabia yake ya kuchelewa kurudi lakini Mzee Mnyoka aliishi vizuri na majirani, jioni Ile nyumbani kwa Mzee Mnyoka mtaa mzima ulihamia kwake, mkewe alikuwa amesharudia kuhadithia jinsi mumewe "alivyodakwa" na polisi, na Sasa mama Alli alikua amechukua jukumu la kusimulia kuhusu kukamatwa kwa Mzee Mnyoka.

"jamani Mzee Mnyoka sio mwizi, sote tunajua, haiwezekan wamchukue, twendeni huko polisi" Waliongea majirani. Hata hivyo mpaka saa 2 usiku bado hawakufikia muafaka na hatimaye usiku , mwenyekiti wa kitongoji ambaye ni kijana tu alifika Nyumbani kwa Mzee Mnyoka kutoa taarifa kuwa Mzee Mnyoka anaweza kupata dhamana kesho yake jumatatu na hivyo wasijisumbue kwenda usiku kule polisi na badala yake kesho waende kumuona!

Hakika Mzee Mnyoka Hakupata tabu peke yake Bali mkewe, na mtaa mzima walipata tabu. Kwanza Nani alienda kumshtaki Mzee Mnyoka? Mbona Mzee Mnyoka hajawahi kuiba hata kuku pale mtaani?

********

Mzee Mnyoka alilala mahabusu huku akiwa anaelewa kwanini Yuko pale! "Mkude mwanaharamu wewe labda nisitoke hapa !" Mzee Mnyoka alipaza sauti akiwa lupango...."Mkude , mshenzi Sana wewe, uibe Ng'ombe mwenyewe halafu unisingizie Mimi? Nikitoka hapa nakuua mshenzi wewe!" Mzee Mnyoka alikuwa anaropoka tu, na kupelekea polisi kuja kumtuliza ...

"We Mzee ukiendelea na hayo makelele yako tutashindwa kukuvumilia" alisema Afande mmoja aliyeitwa Paul. Mzee Mnyoka Hakupata usingizi kwani selo ilijaa harufu Kali ya kinyesi, na giza Totoro, huku mbu wakiwa wanapiga kelele za furaha, Mzee Mnyoka nguvu zilimuishia

*******
Mzee Mnyoka alishindwa kusimama na akajikuta anakaa chini na ndipo Sasa Mzee Mnyoka akapigwa na butwaa, Naam macho yake Sasa yalianza kuzoea giza la pale ndani baada ya kuwa alitoka kwenye mwanga mkali, Na ndipo Mzee Mnyoka akang'amua kuwa hakua peke yake pale ndani!

Ndio,
Mahabusu Tena mwishoni mwa wiki haiwezekan ikawa tupu! Kwa haraka haraka walikuwa Saba mle ndani, huku wa Nne wakiwa wamesimama na watatu wamelala! Mzee Mnyoka alijikuta akicheka!
Ndio alicheka kicheko Cha uchungu! Inawezekaje mtu apate usingizi katika chumba kile ambacho Mzee Mnyoka hakuelewa Kama anatakiwa kuziba pua au mdomo? Inawezekaje mtu apate usingizi katikati ya sherehe za mbu?

Mzee Mnyoka Sasa alitambua kuwa bila shaka wale waliolala, Ni watu wa Aina mbili, mosi,
Wameamua kusamehe na kujisamehe wao wenyewe na kusahau shida zote na kuamua kulala fofofo, ama Ni watu waliozoea Yale mazingira pale ndani! Lakini kwa namna yoyote Ile Mzee Mnyoka asingepata usingizi,
Kwanza alimkumbuka mke wake , mama Monica, pamoja na watoto wake,

Lakini pia Mzee Mnyoka aliwaza kesi iliyoko mbele yake, Kesi ambayo alikua hajui anaanzaje kujitetea. Ni kweli hakufanya, Ni kweli alimjua mhusika, lakini Nani atamuamini? Mzee Mnyoka machozi yalimtiririka.

************

Asubuh na mapema kituo Cha polisi mama Monica na majirani wengine walifika kumjulia Hali Mzee Mnyoka,
Polisi alienda kumtoa Mzee Mnyoka. Ambaye alijikaza huku akijilazimisha kutabasamu baada ya Kumuona mkewe. Alipata wasaa wa kuongea na mkewe na akapewa masharti ya dhamana, hivyo mkewe akishirikiana na majirani walienda "kuchakarika" kuhakikisha Mzee Mnyoka anapata dhamana, siku ile Ile ya jumatatu!

Baada ya mipango yote kukamilika ikiwemo kuuza mbuzi wake wawili na kuweka rehani cherehani yake , mama Monica alifanikiwa kupata dhamana ya mumewe saa 11 jioni! Na safari ya kurudi kijijini ikaanza!

Inaendelea
 
KESI YA MZEE MNYOKA 02
Mzee Mnyoka hakutaka kuongea chochote, hata katika mahojiano asubuhi Ile na Polisi ambayo yaliwekwa katika maandishi mzee Mnyoka hakusema chochote Wala kumtaja mhusika!
Zaidi alikanusha kuwa hakuhusika na wizi wa dume la ng'ombe, Mzee Mnyoka pia alienda mbali kwa kuwataka Polisi wamtaje huyo anayedai yeye aliiba Ng'ombe, lakini Polisi walikataa kumtaja kwa madai kuwa mtoa taarifa analindwa...
Mzee Mnyoka alikumbuka usiku ule pia akiwa nahabusu kuwa alimuona Mzee mmoja ambaye baada ya kusalimiana yeye nae alisema alitengenezewa kesi ya kumtorosha mwanae wa kumzaa ili akamuozeshe, wakati kwa uhalisia yeye ndio alikua anataka kuzuia mtoto wake huyo asiolewe, Ila ndugu na jamaa baada ya kuona watakosa "mahari" ndio wakaona wamtengenezee hiyo kesi na ili yeye akiwa jela wao wapige Pesa huko!
Mzee Mnyoka alikuwa akiwaza hayo yote huku akiwa kwenye piki piki pamoja na mkewe wakirudi nyumbani ...
Majirani wengine walikua wako nyuma na wengine kadhaa wakiwa mbele na kufanya Kama msafara mdogo hivi kurudi kijijini kwa Mzee Mnyoka,

*********

Sasa haikuwa Siri Tena , na taarifa zikaanza kusambaa Kama Moto kuwa mwenyekiti Mzee Mkude ndio aliyepiga simu Polisi, au tunaweza kusema ndie aliyesuka mipango yote Mzee Mnyoka kukamatwa....
Kitu pekee ambacho watu walishindwa kujua Ni kuwa Mzee Mnyoka ndie shahidi pekee aliyemuona mwenyekiti akiiba ng'ombe! Na Sasa kila mmoja akaanza kutoa mawazo yake!
Kuna waliosema Ni wivu tu baada ya Mzee Mnyoka kupata nafasi ya kuwakilisha wanakijiji kwenye mkutano wa ushirika huko wilayani, na hivyo mwenyekiti aliona wivu,
Na wengine walisema itakuwa mwenyekiti anaona Mzee Mnyoka anaweza kugombea uenyekiti na kumpiku!
Wengine wakasema pengine wanagombea mwanamke, ili mradi tu kila mmoja atoe mawazo yake!
Hata hivyo mawazo yote yalichagizwa na ukweli kuwa mwenyekiti Kama baba katika Kijiji hakuweza kumtembelea Mzee Mnyoka akiwa kituoni au hata kumtembelea nyumbani baada ya kutoka! Na hii ilidhihirisha Sasa kuwa wawili hawa Wana uadui!
Mzee Mnyoka si kwamba aliogopa kumtaja mhusika la hasha! Mzee Mnyoka alishahisi Polisi na Mkude lao moja! Hivyo asingeweza kupeleka kesi ya Nyani kwa tumbili....
Na hivyo alijipanga kupeleka vielelezo vyake kwenye mahakama za juu endapo mahakama hii ya mwanzo wangemkuta na hatia!
Hata hivyo Polisi walikua na ushahidi gani? Je walimkuta na ngozi? Au mkia? Au nyama?

Lakini hata akisema Mzee Mkude ndie mwizi, ana ushahidi? Na kwa Nini asiseme tangu mwanzo Hadi alipokamatwa?
Mzee Mnyoka Sasa alikua na maswali mengi kuliko majibu....

Siku ya kesi mahakamani

Mzee Mnyoka alifika mapema na majirani zake pamoja na mkewe, kesi ilisomwa na Mzee Mnyoka akatakiwa kujitetea,
Mzee Mnyoka alisema yeye hatajitetea kwa maelezo Bali ataomba kuuliza maswali ambapo akijibiwa Basi ataridhika na maamuzi ya mahakama,

Mzee Mnyoka alikohoa kidogo Kisha akaanza kusema,
“Mheshimiwa hakimu naomba kujua
- Huyo ng'ombe ninayetuhumiwa kumuiba, je nilimpeleka wapi? Nimemchinja, nimemuuza au nimemficha?”

Na je Kama nilimuuza nilimuuzia Nani? Mbona niliyemuuzia hatajwi kwenye kesi?

Na je huyu mmiliki wa ng'ombe aliniona wakati naiba?

Je nimekutwa na ngozi? Nimekutwa na nyama au hata manyoya yanayothibitisha kuwa nilichukua huyu ng'ombe?
Naomba kujua haya machache mheshimiwa hakimu!

Baada ya maswali hayo Hakimu aliomba ufafanuzi kwa mwendesha kesi ambaye alisema..

“Mheshimiwa kwanza polisi walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema, kuwa Mzee Mnyoka ameiba, lakini pia Mzee Mnyoka ana tabia ya kuchelewa Sana kurudi nyumbani kwake, pia tumegundua siku ya tukio Mzee Mnyoka alipita kwenye barabara hiyo ambayo inasadikika ng'ombe alipitishwa,..”

Hivyo Mzee Mnyoka achukuliwe hatua Kali za kisheria!
Hakimu Sasa aliingilia Kati,
"Ndugu mwendesha mashtaka je, mlikuta na vielelezo vyovyote huyu mshtakiwa?"
Mwendesha mashtaka: mheshimiwa hakimu, Ni Kama nilivyoeleza kuwa tulipigiwa simu!

Hakimu: Naahirisha kesi hii mpaka wiki ijayo tarehe Kama hii nawasihi Tena mwendesha mashtaka na jopo lako mlete vielelezo vya kueleweka ama sivyo kesi hii naifuta"

Koooorti"
Hakimu aliahirisha kesi na watu wote wakatoka....
***********

Uamuzi wa kesi
Hakimu aliamua kutupilia mbali kesi ya Mzee Mnyoka na kusema kuwa hakuna ushahidi wa kutosha wa kumtia Mzee Mnyoka hatiani,
Hata hivyo Hakimu alipendekeza kutafutwa kwa mwizi halisi wa dume Hilo la ng'ombe na pia mshtakiwa unayo haki kudai fidia katika kesi hii Kama utaamua kufanya hivyo!
Hakimu alihitimisha kesi ya Mzee Mnyoka na watu wengine wakaondoka wakiwa wamefurahi kabisa, Mzee Mnyoka na mkewe walikumbatiana kwa furaha, Ni wakati wakiwa wanatoka maeneo ya mahakami ndipo Mzee Mnyoka alistuka kumuona mtu wake pale!

"Shenzi kabisa kumbe huyu Mwana izaya nae alikua hapa mahakamani?"
Mzee Mnyoka aling'aka akimuonyeshea mkewe,
"Mshenzi Sana shukuru Mungu mume wangu hujakutwa na hatia, tusamehe tu Ila malipo ni hapa hapa Duniani twende zetu"
Alisema mama Monica Kisha wakaenda kwenye bodaboda iliyokua inawasubiri kuelekea Nyumbani...
Itaendelea
 
KESI YA MZEE MNYOKA 03

Walifika salama pale kijijini na wanakijiji wengine walikuja kumpongeza Mzee Mnyoka kwa kushinda kesi yake, ingawa hatuwezi kusema alishinda Bali alifutiwa kesi,
Wengine hawakuja hivi hivi Bali walikuja na zawadi ndogo ndogo,
********
BAADA YA MWEZI MMOJA

kidogo watu walishasahau kuhusu kesi ya Mzee Mnyoka ingawa Mzee Mnyoka mpaka Leo alishangaa kwanini Mzee Mkude hakukamatwa Hadi kufikia wakati ule!
Ndio, Ni yeye ndiye aliwapigia Polisi simu na kuwapa taarifa za uongo, lakini kwanini yeye asihojiwe zaidi?
Wakati Mzee Mnyoka akiwa anapigwa na butwaa ndipo Jambo la kushangaza zaidi linatokea,
Siku ya jumanne wananchi walitangaziwa kuwepo kwa wageni kutoka Wilayani, wageni ambao walifika wakiambatana na diwani na viongozi wengine wa kata!
Katika mkutano huo viongozi karibia wote walisimama na kumsifia Mzee Mkude kwa Uongozi wake uliotukuka,
Mkurugenzi mtendaji alimsifia Sana Mzee Mkude na kusema kuwa Ni mwenyekiti wa kuigwa..
" Wapo wananchi baadhi ambao wanarudisha maendeleo ya Kijiji hiki nyuma, na majina yao tayari tunayo, nasikia pia yupo Mzee mmoja hapa mwizi mwizi hivi, ndie ambaye anapingana na juhudi za mwenyekiti,

Sasa niseme hivi mwenyekiti wewe piga kazi, huyo anayejifanya kukukwamisha atakwama yeye! Na tena Kama Kuna mtu hataki kuwa katika hiki Kijiji ahame yeye, lakini hatuwezi kumtoa mwenyekiti kwasababu ya mpumbavu mmoja tu"

Alimalizia Mkurugenzi mtendaji!

Mzee Mnyoka Sasa alihisi dunia yote imemuelemea na bado kidogo imuangukie!
Ni hapo Sasa minong'ono ikaanza na macho ya wengi yakamgeukia Mzee Mnyoka!
Mzee Mnyoka Sasa alishindwa kustahimili na kujikuta anaondoka pale kwenye mkutano huku machozi yakimtoka,
"Ee Mungu nisaidie Sasa nipe uvumilivu nimekosa Nini Mimi eeh Mungu?'"
Mzee Mnyoka alijisemea ....

Ni wazi kuwa Sasa mwenyekiti alishafanya Jambo mpaka huko Wilayani, Mzee Mnyoka aliwaza,
Mzee Mnyoka alifika kwake na mkewe nae akafika baada ya muda mfupi....
Kwa muda walitazamana tu..
Baadae mkewe akaanzisha mazungumzo...


Mama Monica alianza kwa kumuangalia mumewe kwa huruma,
"Mimi nakuomba tu tuhame hiki kijiji mume wangu, angalia Sasa hivi kila mtu anakuchukia!" Mama Monica alisema kwa upole,

"Sikiliza wewe unajua wazi Mimi sio mwizi achilia mbali ng'ombe sijawahi kuiba hata kuku hapa mtaani, siwezi kuhama kijiji kwa Jambo ambalo sijafanya" Mzee Mnyoka aliongea kwa msisitizo halafu akaongeza

"Hebu nitolee lile koti langu nitoke kidogo Mimi" Mzee Mnyoka aliongea huku akisimama,
"Mzee wewe haukomi hata kidogo tayari Tena unataka urudi usiku, hivi Hili halijaisha Tena ukazue mengine hukoo" mama Monica aliongea,

Mzee Mnyoka akasimama na kuondoka!

*********

Hata hivyo maneno ya mkewe yalimuingia..
"Nitakaa hapa mpaka lini, Mzee Mkude kila siku anazidi kupata marafiki wapya, Tena Wenye nguvu zaidi , ipo siku wanaweza hata kunitengenezea kesi nzito au hata kuniua kabisa"
Mzee Mnyoka aliwaza
Hakuna aliyeamini lakini ndivyo ilivyotokea baada ya muda mfupi tangu ule mkutano,

Mzee Mkude alipata uteuzi,
Alienda kuwa Katibu tarafa ya wa tarafa ya Kinjeki ambayo ndio ilikua na kata nyingi zenye maendeleo ukilinganisha na kata aliyokuwepo! Na zaidi Sana alipanda cheo zaidi kutoka mwenyekiti wa Kijiji!
Nafasi aliyokuwepo Sasa ingemfanya Mzee Mkude kuwa na nguvu Mara Tano zaidi ya aliyokua nayo mwanzo..

----+--+++++++++------

Mwenyekiti mpya alikuja kijijini na Jambo la kwanza alilofanya Ni kumuita Mzee Mnyoka ofisini kwake,
"Sikiliza Mzee, sitaki kujua Nini Wala nini, Ila ninachokuomba Mimi sio Mzee Mkude, hivyo kaa mbali na Mimi, nasikia unataka Sana hiki cheo Ila ujue sio rahisi ndio maana mpaka Leo wewe ni mwanakijiji tu! Tena kwa taarifa yako hata huo ujumbe wa kuwakilisha sijui wanakijiji huko kwenye chama Cha ushirika SAHAU!"

Mwenyekiti mpya ambae alikua Ni kijana tu alimwambia Mzee Mnyoka,
Mzee Mnyoka alitaka kuongea kitu lakini akajikuta Kuna vitu vinakwama kooni,
Hivyo akaamua kuondoka tu pale ofisini,.
"Hii Sasa Kali, "
Mzee Mnyoka aliwaza...

Ikumbukwe kuwa Mzee Mnyoka alikua na sifa nzuri sana hapo kijijini hata uwakilishi wa chama Cha ushirika huko wilayani alipata kutokana na mwenendo wake mzuri,

Sasa leo hii Mzee Mnyoka anakumbana na masaibu haya, hakika alikua katika mtihani mzito,

Hata hivyo mzee Mnyoka asingekubali "kuchafuka peke yake" wakati mtenda Jambo mwenyewe alikuwepo,..
Tena yule aliyefanya wizi azidi kupanda chati siku Hadi siku,...
Hakika Mzee Mnyoka asingekubali,
Ni siku hiyo hiyo Mzee Mnyoka akiwa anarudi nyumbani ndipo njiani akakuta gari imepaki ...
Ilikua Ni nadra Sana kukuta gari nyakati Kama hizi kwenye Kijiji Cha Mzee Mnyoka,
Ni Mara chache tu labda siku za minada au kwenye matukio muhimu,
Ni hapo Mzee Mnyoka alijawa na wasi wasi kidogo kuhusu uwepo wa Gari lile,
Mzee Mnyoka alitembea pole pole lakini kwa tahadhari kubwa, uzoefu kidogo aliokuwa nao wakati akiwa jeshini miaka hiyo kabla hajatoroka kambini, na ukichanganya na machale yake Mzee Mnyoka alihisi lile Gari Kuna Jambo,


Ni wakati anataka kulipita Hilo Gari ndipo mlango upande wa dereva ukafunguliwa na mtu mmoja aliyejazia kidogo akashuka....
"Bila shaka wewe ni Mzee Mnyoka.."
Alisema yule mtu bila salamu...

Mzee Mnyoka hakuongea kitu lakini alishangaa Sana pengine na kuogopa pia,
Muda huo ilikua yapata saa 3 na nusu ama saa 4 kasoro hivi usiku,
Mzee Mnyoka Sasa hakuwa na namna,
"Siamini Kama natekwa kirahisi hivi"
Mzee Mnyoka aliwaza Sasa,
Yule mtu Ni Kama alikua anasoma hisia za Mzee Mnyoka na Sasa kinyume na matarajio ya Mzee Mnyoka yule jamaa akatoa tabasamu na Kisha akamsalimia Mzee Mnyoka huku akitoa mkono,...

Mzee Mnyoka Sasa akazidi kuduwaa ...
"Mzee samahani Sana, Kuna mtu anahitaji Sana kukuona usiku huu, usijali tunaenda kumuona halafu tunarudi kabla ya saa 6 naamini bado utakuwa Kwenye muda wako ule ule wa siku zote,
Tena haitazidi ule muda uliorudi juzi usiku!
Alisema yule jamaa huku akimfungulia Mzee Mnyoka mlango wa pembeni upande wa abiria kwenye Ile gari ambayo Mzee Mnyoka aliweza kuifananisha na landcruiser zile za kanisani kwao,
"Ina maana hawa watu wanajua ratiba zangu zote , mpaka muda wa kurudi nyumbani kwangu"
Mzee Mnyoka aliwaza huku akijishauri Kama aende ama afanye "namna" kujiokoa,
"Sikiliza Mzee, kwanza ondoa wasi wasi, Hili Ni Jambo lenye faida kwako,
Ingia tuwahi, ili Mama Monica asije kuwa na wasi wasi!
Yule mtu aliongea Sasa na kumfanya Mzee Mnyoka Sasa kutokua na jinsi zaidi ya kuingia kwenye Gari na yule mtu akazunguuka upande wa dereva na wakaondoka wakiwa wawili tu,
Mzee Mnyoka Sasa wasi wasi ulipungua!
Gari iligeuza Kama wanaenda mjini lakini baadae Sasa wakanyoosha kuelekea makao makuu ya kata, ambapo ilikua Ni mwendo wa dakika 10 tu,
Kwenye Gari hakuna aliyemsemesha mwenzake, zaidi ya nyimbo ambazo zilikua zikisikika kwenye redio ya Gari,
Hata hivyo nyimbo zenyewe zilizidi kumshangaza Mzee Mnyoka,
"Haiwezekani hii iwe bahati mbaya" Mzee Mnyoka aliwaza,
Mzee Mnyoka alishangaa zile nyimbo ambazo zilikua zikisikika kwani Ni nyimbo ambazo alikua anazipenda Sana! Na kila siku alikua akitembea na redio yake na kuweka nyimbo hizi, Ni Kama bahati tu leo alishindwa kupata betri mpya kwenye redio yake na hivyo akarudi nyumbani mapema kidogo,
"Katika viumbe vyote vilivyoumbwa,. Binadamu kaumbika kuliko vyoteee"
Hakika Mzee Mnyoka alijisikia burudani Sana,
Dereva alimchungulia Mzee Mnyoka na kujikuta anatabasamu tuu..
Gari ilienda na hatimaye wakafika sehemu kabla ya kufika makao makuu ya kata ambapo walikuta Gari nyingine ,
Ambapo yule dereva alisimama na kuwasha taa kwa namna flani ambayo Mzee Mnyoka aligundua kuwa Ni Kama ishara ya kuwajulisha kuwa amefika na "mtu wake"
"Mzee Mnyoka, Kuna mtu anataka muongee hapa hapa, mkishamaliza Mimi nitakurudisha, Ila tunaomba Jambo Hili liwe Siri kabisa,
Aliongea yule Dereva Kisha akashuka kwenye Gari,
Mzee Mnyoka Sasa wasi wasi ulimtoka kabisa,
Potelea pote Kama Ni kuchafuliwa nimeshachafuliwa Sana Sasa niogope Nini Tena?
Mzee Mnyoka aliwaza na
Mara mlango ukafunguliwa na mtu mmoja Mzee hivi Kama yeye umri wa miaka 56 hivi akaingia...
Itaendelea
 
KESI YA MZEE MNYOKA 04

Yule Mzee alionyesha uchangamfu Sana na zaidi ya yote aliongea Mambo mengi kuonyesha anamjua Mzee Mnyoka Kisha Sasa akaendelea
" Tuna wiki Sasa hapa tunafuatilia kwa kina Mambo mawili, kwanza kuhusu kesi yako, lakini pia kuhusu huu uteuzi wa Mzee Mkude,
Labda nikueleze ukweli mzee Mnyoka,

Sisi tunajua kuwa wewe hukuiba Ng'ombe! Tunajua pia Mzee Mkude ndie mwizi wa Ng'ombe,

Sisi sio wajinga, na nikueleze tu tunajua pia mpaka huyo ng'ombe alipoenda! Kitu pekee ambacho tumeshindwa Ni ushahidi kamili wa kuweza kumtia hatiani Mzee Mkude!

Na ndio maana tukaona tukutafute ili walau utupe mwanga,

Alisema yule mtu!
Mzee Mnyoka Sasa alijisikia vizuri, kwanza hakutegemea Kama Kuna watu ambao wanafahamu ukweli! Alisubiri muda mrefu Sana kusikia hiyo kauli kuwa "hakufanya" lile Jambo!

Na hata kule polisi zaidi ya kukataa tu hakuongea chochote Wala kumtaja mhusika!

Hivyo Leo hii alijisikia kufunguka zaidi hata hivyo alihofu kidogo...

"Vipi Kama hawa wametumwa na Mkude kuja kunipeleleza zaidi wajue Kama Nina ushahidi au la?"

Aliwaza..

Potelea mbali..

Alijishauri na Kisha akaamua liwalo na liwe....ngoja amwage mboga...

"Ni kweli siku ya Alhamis wakati narudi nyumbani nilimuona Mzee Mkude akiwa anaburuta ng'ombe, na nilishangaa Sana maana yeye Kama mwenyekiti angeweza kutuma hata watu wakamsaidie, lakini nilivyogundua ameniona niliwahi kwenda nyumbani ..

"Sikiliza Mzee sisi tunajua kuwa baada ya Kumuona Mzee Mkude na yule ng'ombe wewe hukwenda nyumbani, labda Mzee Mnyoka nikuambie kitu,.
Lengo la haya yote Ni kutaka kukusafisha wewe, hivyo kuwa mkweli tu!"
Yule mtu aliongea na Sasa Mzee Mnyoka akainamisha kichwa kwa aibu!

Ni kweli Mzee Mnyoka hakwenda nyumbani! Bali alizunguuka vichochoroni na kumfuata Mzee Mkude "bampa to bampa"

Mzee Mnyoka Sasa alishangaa mpaka Hili Jambo hawa watu wanajua!

"Kwanini nyie ni kina Nani?"

Mzee Mnyoka Sasa "povu" lilitaka kumtoka!

"Mwisho wa haya yote tutafahamiana tu Mzee " hebu tuongee Sasa mama Monica asije kuchanganyikiwa huko na nadhani pia kijana amekuambia pia hakuna mtu anatakiwa kujua Kama vile ambavyo hukusema kwa mtu kuhusu kumfuatilia Mzee Mkude Basi na haya mazungumzo yetu yabaki kuwa Siri ..


Alisema yule mtu, na Sasa Mzee Mnyoka akaona Hakuna Jambo anaweza kuwaficha Tena hawa jamaa...

"Ni kweli sikwenda nyumbani, Bali nilizunguuka vichochoroni na kumfuata Mzee Mkude kimya kimya, tulienda Kama dakika 14 hivi mpaka pale darajani ambapo niliona gari Aina ya fuso ikiwa imepaki na mbele yake kulikua na Gari dogo hivi,

Baadae walitokea vijana na mmoja wapo Ni mtoto wa jirani yangu Mzee Hassan ambae anaitwa sele kwa Sasa amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya misitu ya kata,...

Wengine sikuweza kuwatambua maana nilikua mbali kidogo,

Baada ya hapo wale vijana walimsaidia Mzee Mkude kumpandisha yule ng'ombe kwenye Gari, wakati huo Mzee Mkude alikuwa amesimama pembeni kidogo na mtu mmoja ambaye sikuweza kumjua Mara moja ingawa nilimhisi tu...

"Kuwa Ni Nani?"
Yule mtu alimuuliza Mzee Mnyoka
"Kwakweli nasema nilimhisi tu , Sina uhakika Kama alikua yeye Ni hisia zangu tu"

Mzee Mnyoka aliongea..

"Mzee Mnyoka hebu sema Basi, huyo mtu ulimhisi kuwa anaweza kuwa Nani?"

"Kwakweli kutokana na muonekano wake, nilihisi yule mtu atakua diwani,...

Kwanza umbo lake, lakini vile alivyokua anaongea kwa kurusha Mikono nikahisi atakua diwani tu,"

Mzee Mnyoka aliongea!

"Good! Very Good "
Yule mtu aliongea akiwa ana tabasamu....

"Sasa sikiliza Mzee Mnyoka, kwasasa una watoto wawili tu, na mke wako anakupenda sana,

Hebu fikiria Kama utamuacha akiwa mjane, mwanao James ndio kwanza Yuko kidato cha tano , Mary ndio huyo Yuko form one,

Hivyo Sasa tumetumwa rasmi kabisa kukupa ujumbe huu kuwa fanya Mambo mawili,

Uhame kwenye hiki Kijiji au ukae kimya kwa Jambo lolote utakaloliona kwenye hiki Kijiji linatokea..

Lakini pia uelewe hutakiwi kumueleza mtu yoyote hata mkeo, kuhusu maongezi yetu haya,

Na Jambo la mwisho...


Sisi tunakufuatilia kuliko unavyoweza kudhani,"

Alimalizia yule mtu,

Mzee Mnyoka Sasa akili ilianza kumuingia,
"haiwezekani mkwara wote huu uwe kwa sababu ya kesi ya ngo'mbe tu"

Mzee Mnyoka aliwaza,

Alikumbuka akiwa jeshini miaka hiyo ya 77 hivi wakati Tanu ikiwa imepamba Moto,
Mzee Mnyoka alimkumbuka mkufunzi wake Meja Brian,

Ambaye aliwaambia..

"Mfanye adui yako akudharau, halafu baadae mshangaze"

Adui yako anapokudharau atakosa umakini katika kukushambulia lakini pia itakusaidia wewe kumshambulia na kumshangaza!

Hivyo mzee Mnyoka kwa upole alisema..
"Sasa mkuu mbona kesi hii imeisha? Na Kama ulivyoona mahakama imefuta kesi, Sasa sioni Tena Kama Kuna mwendelezo wa Jambo Hili zaidi naona Kama mnataka kunionea tu"
Alisema Mzee Mnyoka kwa unyonge

" Sikiliza Mzee Mnyoka, kwanza sisi tunakujua kuliko unavyodhani, tatizo lako unajifanya una akili Sana, lakini suala la msingi chagua kuondoka pale kijijini vinginevyo mabalaa yatakukuta"

Naomba tuachane na fanyia kazi hayo Mambo mawili kesho jioni atakuja mtu atakuletea flash yenye nyimbo zako hizi,

Lakini atakuambia kuwa ulitaka nyimbo hamsini au sabini?

Wewe ukimjibu kuwa ngoja nizisikilize kwanza hizi, maana yake umeamua kuwa hutahama hapa kijijini na Wala hujali kuhusu Mazungumzo yetu,
Lakini ukijibu kuwa nilitaka 50 maana yake umekubali kuhama,
Ukisema sabini maana yake
Hutahama lakini utakubali masharti yetu ya kuishi hapa,
Sasa unaweza kwenda,

Alisema yule mtu na akaondoka Kisha akarudi yule dereva na kumrudisha Mzee Mnyoka mpaka pale alipomchukua,
Mzee Mnyoka Sasa kichwa chake kilianza kuuma kwa mawazo, Sasa akili yake ilishamwambia Kuna kitu zaidi ya kesi ya ngo'mbe !

Haiwezekani watu hawa waje kumtisha na kumfuatilia kwa ajili ya kesi ya ngo'mbe tu Tena kesi yenyewe iliisha!

Hata hivyo mzee Mnyoka alijaribu kuunganisha matukio,

Baada tu ya ngo'mbe kupotea,
Mzee Mkude alipanda cheo,

Lakini zaidi Sana Sele mtoto wa Mzee Hassan nae akapewa kuwa mwenyekiti wa misitu wa kata,

Zaidi ya yote kulikua na zoezi la utafiti wa urenium katika kitalu kilichokuwepo kwenye msitu huo,

Isitoshe, serikali ilikua bado haijatoa taarifa rasmi ya kupatikana au kukosekana kwa madini hayo!

Sasa ng'ombe anahusikaje?


Mzee Mnyoka aliwaza na akakosa majibu...

******
Kesho yake Kama saa 12:36 jioni
Mzee Mnyoka alikua sebuleni kwake akisubiri kipindi Cha Nyundo ya Baruan Muhuza,
Kipindi alichokua akikipenda Sana,
Ndipo mgeni wake akafika!

Ni mkewe Mama Monica alisema
"Kuna Kijana amekuletea flash ya nyimbo Ila anauliza ulitaka hamsini au sabini?"

Itaendelea
 
KESI YA MZEE MNYOKA 05

Mzee Mnyoka alitoka nje kumuona huyo Kijana,.
Kwanza Mzee Mnyoka alitaka kujua huyo Kijana Ni Nani,
Lakini pia kuweza kumpa majibu ambayo Mzee Mnyoka alishajipanga kujibu,

Hivyo hakuona Vyema Kama angeweza kumtuma mkewe Kwenye "Jambo" Kama Hili,

Mzee Mnyoka alimuona huyo kijana akiwa Kwenye piki piki,..

Mzee Mnyoka Sasa alikubali kabisa kuwa sura Ile ya yule kijana haikua ngeni kabisa machoni pake,

Ila Sasa hakukumbuka Ni wapi aliweza kumuona,

Hata hivyo kutokana na mradi wa utafiti hususani ujenzi wa kitalu pale kijijini ulipelekea utitiri wa vijana wengi kutoka sehemu mbali mbali,

Kwani kulikua na ajira nyingi ikiwemo ya kuchimba mifereji na ujenzi wa visima kadhaa kwa ajili ya zoezi lenyewe,

Hivyo Mzee Mnyoka asingeweza kukumbuka sura za vijana wote,

Au pengine akawa Ni kijana tu ametumwa,

"Mzee eti ulitaka sabini au hamsini?"

Yule kijana Sasa aliongea na Mzee Mnyoka akazinduka katika dimbwi la mawazo,.

"Ooh Sasa unajua nilitaka nyimbo nyingi hata sabini Ni chache Ila Sasa ngoja mama Monica azisikilize kwanza halafu nitakuja kuongeza Kama vipi"
Mzee Mnyoka aliongea huku akitabasamu,

Mkewe Sasa hakujua chochote ingawa haikuwa kawaida ya Mzee Mnyoka kuletewa nyimbo maana tayari Mzee Mnyoka "alishakuwa na nyimbo zake"
Ambazo pengine asingesikiliza labda angeumwa!

Yule kijana aliondoka zake na Mzee Mnyoka akarudi ndani .

"Naamini watanielewa, wasipoelewa Basi!"

Mzee Mnyoka alijisemea kimoyo moyo huku hofu ikiwa inamuingia kiasi,
Mzee Mnyoka alishapiga mahesabu yake na kuona kuwa akiwajibu vile maana yake yupo Kwenye kufikiria jibu la kuwapa,
Hata hivyo mzee Mnyoka aliamua liwalo na liwe Sasa lazima ajue kiundani kuhusu muunganiko wa kesi yake na matukio ya hivi karibuni,

Ni wazi kuwa lipo Jambo, na Mzee Mnyoka alijishangaa kwanini Hadi Leo hakuchunguza kwa undani kuhusu kesi yake,

Aliwaza, mambo mengi,

"Labda Kuna Jambo zito nyuma ya hii kesi, lakini kwanini wananilazimisha kuondoka? Je kuna kitu kingine wanapanga kufanya tofauti na ule wizi wa ng'ombe? Na je huyo ng'ombe anahusikaje?"

Mzee Mnyoka Sasa alikua akiangalia Nyundo ya Baruan Muhuza,

Lakini pengine angeulizwa kinachoendelea asingeweza hata kutaja mada ya kipindi,

Mawazo yake yalikua mbali sana,..

Baada ya kipindi alitoka nje kidogo kuzunguuka Kama ilivyo ada ,

"Hapa lazima nianze kwa Mzee Pembe kwanza"

Mzee Mnyoka aliwaza,

Mzee Pembe alikua anakaa kitongoji Cha tatu kutoka kwa Mzee Mnyoka,

Na Mzee Pembe ni mojawapo ya wanakijiji ambao walikua jirani kabisa na mradi wa utafiti uliokua unaendelea,...

Hawakua na mazoea yoyote na hata Mzee Mnyoka baada ya kusikia dume lake la ng'ombe limeibwa Mzee Mnyoka hakuweza kufika kwa Mzee Pembe,

Na zaidi Sana hata siku ya kesi Mzee Pembe mwenyewe hakuwepo,
Na Kama walivyosema polisi wao walipigiwa simu tu kuwa Mzee Mnyoka ndie mwizi,

Kwa maana hiyo hata Mzee Pembe mwenyewe hakwenda kulalamika polisi!

Yeye alipiga kelele tu asubuh baada ya kuona zizi liko tupu na ng'ombe ameyeyuka!

Hivyo mzee Mnyoka alikua na kila sababu ya kuongea nae na pengine angepata pa kuanzia,

Ni wakati anakaribia kwa Mzee Pembe ndipo simu yake ilipoita,

Namba ilikua Ni ngeni hivyo alipokea tu na sauti upande wa pili ikasikika
"Tumekuelewa, hizo nyimbo Ni za wiki moja, baada ya hapo Kijana atakuja kuchukua iyo flash"

"Haloo ,! Haloo! We Nani!?"

Mzee Mnyoka alijitahidi kuongea lakini simu ilishakatwa muda mrefu,

"Shenzi !"
Mzee Mnyoka alitukana,..
Akawa Sasa anajiuliza aingie kwa Pembe ama Arudi kwanza!!

Mzee Mnyoka aliamua kwanza afanye kilichomleta pale kwa Mzee Pembe,

"Hodi wenyewe!"
Alibisha

"Hodi Tena!"
Mzee Pembe alikazana kuita alipoona kimya ikabidi azunguuke upande wa pili ambapo kulikua na jiko na Banda la ng'ombe

Na kwa bahati Mzee Pembe alikuwepo jikoni na mkewe wakiota Moto,

Mzee Pembe kwanza hakutegemea ugeni Kama ule wa Mzee Mnyoka jioni Kama Ile,

Ilishapita miezi kadhaa tangu tukio litokee,

Na bila sababu yoyote ya kueleweka sio Mzee Mnyoka Wala Mzee Pembe walishakutana na kuongea kuhusu Jambo lenyewe,


Mzee Pembe Sasa alimkaribisha Mzee mwenzake kwenye nyumba "kubwa"

Ambapo kulikua na sebule na viti kadhaa na baada ya maongezi ya kawaida Sasa Mzee Mnyoka aliomba kujua kitu gani haswa kilitokea siku ile ya Alhamis..


"Kama ujuavyo binti yako Amina aliletewa posa hapa, na tulipewa mbuzi wawili na dume moja...

Alianza Mzee Pembe,

Baada ya kushauriana Sana na wenzangu tukaona Ni vyema yule dume atunzwe mpaka sherehe ya Idd tumchinje halafu tununue ndama wawili ili tufuge rasmi tubaki na kumbu kumbu,
Sasa siku hiyo Musa hapa na mwenzake wakawa wameenda kulisha kwenye huu msitu wetu Wenye mradi wa vitalu,

Kama ujuavyo watoto hawa hawajazoea Sana kuchunga hivyo muda mwingi walizunguuka nao tu huko na huko,

Musa anadai hivi wakati wanarudi kwenye saa moja kasoro hivi usiku Kuna Kijana mmoja aliwakimbilia kabla hawajafika nyumbani akawauliza Kama huyo ng'ombe alikunywa maji kwenye kile kisima Cha mwanzo! Sasa wakina Musa walishangaa tu maana hawakujua Kama huyo ng'ombe alikunywa au la,

Hivyo wakamuambia hawajui, lakini yeye alizidi kuwauliza tu.....

"Shikamoo Mzee Mnyoka"

Mazungumzo yalikatishwa na mtoto wa Mzee Pembe ,Musa
Ambaye kama bahati upande wa Mzee Mnyoka alimuangalia Mzee Pembe kwa jicho linalosema "hebu Mussa atusimulie"

"Ooh Tena afadhali Musa , siku ile yule kijana aliyewauliza Kama ng'ombe amekunywa maji ya kisima ilikuwaje vile?"

Mzee Pembe Sasa alimuuliza mwanae Mussa
"Yaani tulikua tunakaribia kabisa kufika nyumbani akawa anatukimbilia , baadae akawa anatuuliza Kama eti ng'ombe alikunywa maji, sisi tukawa tunacheka tuu, baadae ndio akasema eti na yeye anapenda Sana kuchunga ng'ombe akasema anatusaidia kuswaga ng'ombe Hadi hapa nyumbani na akatuleta mpaka hapa nyumbani Mimi nahisi yule ndio atakua mwizi baba"

Mussa alisema

Mzee Mnyoka Sasa aliona mwili ukisisimka! Tayari Sasa alishapata picha na baada ya kunywa chai Mzee Mnyoka aliaga na kuondoka!

Njiani Mzee Mnyoka alipiga mluzi kwa furaha,

"Nilijua tu hapa tatizo halikua ng'ombe!"


Mzee Mnyoka Sasa alifunguka kabisa alielewa picha yote ...

"Maskini Mkude pengine hajui chochote kabisa!"
Mzee Mnyoka alijiwazia..


Hata hivyo Mzee Mnyoka hakujua Sasa wapi anatakiwa kufikisha taarifa hizi!

"Je vipi Kama wote Ni wale wale? Vipi Kama naenda kujichomea zaidi?"

Mzee Mnyoka aliwaza na kuwazua baadae akapata wazo!

Ndio,

"Padri John"!

Mzee Mnyoka Sasa aliona sehemu salama kabisa ya Jambo Hili Ni kumfikishia Padri John,.

Aliamini Padri John anaweza kuwa na msaada mkubwa,

Kwanza anaweza kuwa ana mawasiliano walau na viongozi waaminifu au hata usalama wa Taifa ,

Lakini pia Suala likipitia kwa Padri litakua salama zaidi kwake Mzee Mnyoka,

Mzee Mnyoka Sasa alirejea kwake akiwa na nguvu mpya huku akiomba usiku uishe haraka akamuone Padri John,
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom