Hadithi Fupi

Hadithi Fupi

Six Man

JF-Expert Member
Joined
Dec 19, 2017
Posts
253
Reaction score
893
NAKUCHUKIA SHADYA
Juma Hiza
0712988278

Najua utajiuliza ni kwanini namchukia Shadya. Naam! Nafahamu hili ndilo litakuwa swali la kwanza litakalokujia katika ufahamu wako. Hata hivyo sishangai kupokea swali kama hili kutoka kwako kwani kichwa cha mkasa huu kinazungumza kuwa namchukia Shadya. Ni kweli namchukia sana Shadya wala sijui kama chuki yangu dhidi yake itakuja kutoweka. Namchukia sana tena sana tu.
Ngoja nikueleze kitu ndugu yangu, mpenzi msikilizaji wa mkasa huu. Katika mapenzi kuna mambo mengi sana huwa yanatokea. Mengi kati ya hayo huwa ni yenye kuleta furaha moyoni na mengine huweza kukusababishia maumivu makali kiasi kwamba ikatokea ukayachukia mapenzi kabisa, ukaona hukustahili kupenda au kupendwa.
Mapenzi yanaweza yakakusababisha ukajikuta unaishi katika dunia usiyoweza kuitambua, dunia ya kukosa amani muda wote karaha ndio akawa ndugu yako wa karibu. Unaweza ukawa chizi usiyeokota makopo lakini sababu kubwa ikawa ni mapenzi.
Laiti kama mapenzi yangepewa umbo la kuwa kiumbe kilicho hai, yasadiki maneno yangu kuwa leo hii ninapokusimulia haya yasingekuwa hai kama siokuwa maututi hospitalini kwa kujeruhiwa vibaya na binadamu mwenye hasira kali ambaye kila siku anayachukia mapenzi kuliko kitu chochote kile katika hii dunia yenye kila jema na baya unalo lifahamu.
Asikwambie mtu mapenzi ni kitu kingine kabisa. Sijui niyaweke katika fungu gani kwani kila ninapojaribu kuyatafakari hujikuta naishia kuumwa kichwa mwisho nalala pasipo kujijua.
Kama si mapenzi nafikiri leo hii nisingekuwepo hapa nikakusimulia mkasa huu ambao naamini utabaki kama kumbukumbu kwa vizazi hadi vizazi ili nao waweze kujifunza mambo mengi kutoka kwangu na nisingependa wayarudie makosa niliyowahi kuyafanya. Nataka simulizi hii ibaki kuwa yangu ya peke yangu.
Nisingependa baada ya mkasa huu masikio yangu yasikie eti! Kuna akina Shadya wengine ambao wanaochukiwa zaidi ya huyu aliyeniumiza mimi. Aliyenipa jeraha la moyo litakaloacha kovu la milele katika moyo wangu wa nyama. Kovu ambalo litaniumiza siku zote za uhai wa maisha yangu mpaka pale mwisho wa pumzi zangu utakapowadia.
Simulizi hii ikuache na fundisho kubwa katika maisha yako.
****
Muda:Saa 4:00 usiku.
Ally anasimulia;
Nakumbuka mambo mengi sana yaliyowahi kutokea katika maisha yangu na Shadya. Nilimpenda sana Shadya kwa kuwa niliamini ni mwanamke pekee ambaye angeweza kuishi na mimi siku zote za uhai wa maisha yangu. Alikuwa ni mwanamke ambaye alivumilia mambo mengi sana, nakumbuka ugumu wa maisha niliyokuwa nao lakini bado hakuchoka kunipenda, alizidi kunionyesha mapenzi ya dhati ambayo kiukweli sikuwahi kuwaza wala kutegemea kwamba kuna siku itafika atakuja kuniumiza maishani, nilimuamini sana. Nilijinyima sana kwasababu yake. Alinikabidhi dhamana ya kuutunza moyo wake wa mapenzi uliyokuwa kwangu japo kutokana na uzuri aliyokuwa amejaaliwa alikuwa akisumbuliwa na wanaume wengi lakini hakusita kuniambia kuwa alikuwa akinipenda mimi na ni mimi pekee ambaye alikuwa akinisubiria katika maisha yake.
Ama kweli maneno ya wahenga waliyosema “Maisha ni safari ndefu iliyokuwa na kiza mbeleni”, usemi huu uliweza kujidhihirisha katika maisha yangu, sikuwa na kazi ya maana, maisha yangu niliyaendesha kwa kuungaunga kwa vibarua vya kujishikiza ilimradi maisha yasonge mbele.
Nilikuwa nikipigika haswaa! ilimradi niweze kumridhisha Shadya mwanamke wa maisha yangu. Niliamini bila ya yeye hakukuwa mimi maishani. Mtaa niliyokuwa naishi nilikuwa ni mwanaume pekee ambaye niliyebahatika kutembea na msichana mrembo sana, marafiki zangu walikuwa wakinisifia sana huku wengine wakinigeuka na kwenda kumfuata kwa lengo la kuniharibia lakini hakuna walichoambulia, Shadya alikuwa akinipenda sana, kiukweli kwa wakati ule nilikuwa nikimuamini kupita kawaida.
Kichwa changu bado kinayakumbuka vyema maneno yake aliyokuwa akiniambia kila mara kuwa alikuwa akinipenda hivyo nizidi kuishi na imani thabiti juu yake, alikuwa hapendi kuniona nikimuhisi vibaya, alifanya kila awezalo ilimradi nimuamini na kweli alifanikiwa katika hilo.
Baada ya mwaka mmoja kupita tangu uhusiano wetu ulipoanza, Shadya alianza kuitamani ndoa, kila alipopata nafasi ya kukaa na mimi alikuwa akinisihi sana suala la ndoa.
“Baby na mimi nataka kuwa mke wa mtu,” aliniambia Shadya huku akiilegeza Sauti yake iliyobadilika na kuwa kama ya kitoto.
“Shadya mpenzi wangu, mipango bado haijakaa sawa nivumilie kidogo nitakuoa tu! mpenzi,” nilimjibu huku nilimtazama usoni ni hapa ambapo nikazidi kuuona uzuri wa msichana huyu ambaye alikuwa ameziteka hisia zangu katika gereza la mapenzi, nilikuwa kipofu kwake.
“Marafiki zangu wote wameshaolewa bado mimi tu! yani watu wananishangaa,” aliniambia Shadya huku akiubetua mdomo wake. Alionekana kuchukizwa sana na maneno yangu.
“Inakupasa uwe mvumilivu mpenzi wangu,” nilimwambia.
“Sitaki mimi nataka kuolewa.” aliniambia Shadya.
Maneno ya Shadya yalizidi kuniweka katika wakati mgumu sana. Sikuwa na kazi ambayo ilikuwa ikiyaendesha maisha yangu, sasa ingekuwaje kama ningeamua kumuoa? Hili lilikuwa ni swali ambalo lilikuwa likiniumiza sana kichwa. Niliwaza mambo mengi sana juu ya hili lakini hakuna nilichong’amua sanasana nilizidi kujiumiza tu!.
Niliamua kumueleza Mama yangu kila kitu kilichokuwa kikiendelea. Nakumbuka aliniambia nitafute maisha kwanza kwani mapenzi yapo tu! na ningeyakuta mbeleni.
“Lakini Mama nina malengo naye kumbuka,” nilimwambia Mama.
“Hata kama unamalengo naye kitu cha umuhimu ni kuandaa mazingira, tafuta kazi kwanza mwanangu, kama kweli anakupenda atakusubiri.” aliniambia Mama. Mwanamke pekee ambaye alikuwa mshauri wangu mkubwa, Kauli yake ilikuwa na uzito mkubwa sana kwangu katika kufanya maamuzi.
Nilizidi kupambana kutafuta maisha usiku na mchana huku nikiamini Shadya alikuwa akinisubiri ili niweze kumuoa. Maneno yake ya kunifariji kila siku ndiyo ambayo yalikuwa yakinipa nguvu ya kuzidi kutafuta hata pale nilipokuwa nataka kukata tama niliweza kuamka na kutafuta tena bila kuchoka.
“Nimefiwa na Shangazi yangu wa Morogoro hivyo itanibidi niende kule msibani,” aliniambia Shadya siku moja alipokuja kunipa taarifa za msiba. Zilikuwa ni taarifa mbaya sana kuzipokea na kama mwanadamu ziliweza kuniumiza sana. Nilimruhusu aende msibani ambapo aliniambia angeweza kukaa kwa muda wa mwezi mmoja, aliniambia kuwa aliwakumbuka sana ndugu zake waliokuwepo huko. Safari hiyo pia aliitumia kwa kwenda kukaa na ndugu zake.
****
Baada ya mwezi mmoja kupita niliweza kupokea taarifa zilizoniumiza sana moyo wangu, nilipata taarifa kuwa Shadya alikuwa ameolewa na mwanaume mwingine huko Morogoro. Kwakweli sikutaka kuamini kile nichokuwa nikiambiwa kwa wakati huo, waliobahatika kwenda harusini waliweza kunionyesha picha zake. Nilihisi kuchanganyikiwandugu msikilizaji.
Tangu hapo sikuweza tena kumuona Shadya machoni mwangu wala Sikuweza tena kusikia japo sauti yake ikirandaranda masikioni mwangu, ameondoka na mapenzi yangu, ameiacha na kidonda kilichoacha kovu linalozidi kuniumiza kila siku maishani mwangu.
NAMCHUKIA SANA!!” alimaliza kusimulia Ally alipokuwa akihojiwa na kipindi cha redio kilichokuwa kikipendwa na watu wengi sana. Kilikuwa ni kipindi cha Mikasa ya Kimapenzi na Maisha.
Mtangazaji wa kipindi hicho aliyejulikana kwa jina moja la Salma aliruhusu maswali na ushauri kwa wasikilizaji wa kipindi hicho pendwa. Wasikilizaji wengi walikuwa wakipiga simu huku wengine wakituma ujumbe mfupi wa kumpa pole Ally kwa mkasa huo uliyomkuta katika maisha yake.

MWISHO.
 
Nyemo Chilongani
Bupe Wowowo

Ukiniambia nimuelezee msichana huyu, cha kwanza nitaanza na macho yake. Ni msichana mrembo, asiyeisha hamu hata ukikaa na kumwangalia. Alikuwa na umbo namba nane, umbo kali, balaa ambalo kila alipopita wanafunzi wote tulikuwa tunamwangalia.
Aliitwa Bupe! Bupe alikuwa Bupe kweli! Alijua kuringa, alijua kujitingisha, alijua kututega mpaka wanaume tukachanganyikiwa. Kuna watu wengi walimpenda, labda wa kwanza nilikuwa mimi kwa sababu kila siku kabla ya kulala alikuwa mtu wa mwisho kupita akilini mwangu na wa kwanza kumkumbuka kila nilipoamka.
Unaweza kusema sikupenda masomo, hapana, niliyapenda ila hayakushinda upendo wangu juu ya Bupe. Sijui ilikuwaje! Labda alijua kama nampenda! Labda alijua kwamba silali bila yeye, au alijua kwamba kila nilipomuona moyo wangu ulitetemeka sana kwani kila alipopita, alikuwa akijitingisha mno wowowo lake.
Nilimpenda Bupe, niliogopa kumwambia ukweli, nilihisi angenikataa kwa sababu nilikulia Tandale, pale shuleni, nilijitenga kwa kujiona mtoto wa uswahilini, hata kama nilimuheshimu kila mtu lakini waliona kama nawaigizia.
Wanaume hawakutaka kuchelewa, wakaanza kumfuata Bupe na kuwaambia ukweli kuhusu mioyo yao, upendo wao wa dhati juu ya msichana huyo, kitu cha ajabu sana aliwaambia kwamba alikuwa na mpenzi, mzuri, aliyempenda na aliyejua kupenda, alipouliza ni nani, eti akawaambia Nyemo.
Nilishtuka, sikujua kama alikuwa akinitega au la. Alinichanganya! Akanipagawisha! Nikaweweseka! Sikuamini kama Bupe yuleyule ninayempenda eti naye alikuwa akinipenda.
Wengi wakaniuliza, na mimi kwa mbwembwe zangu, kwa misifa yangu nikawaambia”Ndiyo! Bupe demu wangu.” Kuwa na demu kama Bupe nilijisikia fahari sana, nikazugazuga lakini kumbuka kwamba sikuwahi kuongea naye.
Mwisho wa siku nikasema sikubali, siwezi kuwa mshika mapembe huku maziwa wanakamua wengine, sikutaka kula kwa macho na wakati nilikuwa na mikono. Nikapiga moyo konde na kumfuata. Nilipomfikia, nikamwambia “Bupe! Nakupenda, naomba uwe mpenzi wangu! Hakika nitakujali sana!” nilipomwambia hivyo, akaniangalia, akanikazia macho na kuniuliza “Are you serious Nyemo?” Nikamwambia ndiyo na ndiyo maana nilisimama mbele yake.
Akacheka sana! Akaumauma lipsi zake! Akanikonyeza kidogo, kicheko kikapungua na kuanza kucheka kicheko fulani hivi amazing.
“Nyemo! Are serious?” akaniuliza tena, na mimi nikamjibu kwamba nipo serious.
“Una hela?” lilikuwa swali lililonichanganya sana! Aliponiuliza kuhusu hela, alimaanisha nini? Ya kumnunulia chai hapo shuleni au hela gani. Nikajipa moyo kwamba inawezekana alimaanisha hela ya vitafunio. Kama nilikuwa nakula mihogo kumi kila siku, nikimpa mitano na mimi nikabaki na mitano kuna tatizo? Harakaharaka nikamjibu ndiyo! Hela ninayo, tena nyingi sana.
“Hahaha! Ila naupenda mwili wako,”aliniambia, akacheka tena kwa kicheko cha mitego kisha akaondoka zake.
Nilibaki nikiwa nimesimama, nilimwangalia, alijua kwamba wanaume nikiwemo mimi walikuwa wakimwangalia, akaongeza machejo mpaka nikahisi kama wowowo lake linataka kudondoka.
Huyu Bupe alinivuruga sana. Kila nilipokuwa nikikutana naye aliniuliza kuhusu hela, na mimi nilimwambia kwamba hela ninayo kwani nilijiamini kwamba kama siku nyingine nilikuwa nawapa ofa ya mihogo wakina Hassani, ningeshindwa nini kumpa Bupe? Nisingeshindwa, hivyo nilitakiwa kukomaa naye.
Wakati naendelea kumsumbua kwa saundi zangu za uswahilini kwa kumwambia kwamba Diamond nimecheza naye, Madee alikuwa msela wangu, kumbe upande mwingine watu wenye mikono yao yao wakawa wanakula tu, wale wenye meno wakawa wanatafuna huku mimi nikibaki kumuuzia sura.
Mwisho wa siku shule nzima wakajua kwamba Bupe alikuwa demu wangu! Wale waliokuwa wakimfaidi, walicheka sana, walinionea huruma kwa sababu, jinsi alivyokuwa Bupe na mimi, ilikuwa ni sawa na kufika Tandale kwetu na kuona sehemu wanauza Baga, kilikuwa kitu kisichowezekana hata kidogo.
Washikaji zangu wakajua tu kwamba nampenda Bupe, wakaniita na kunishauri kwamba mtoto nimpeleke nyumbani, halafu akifika huko, namaliza kazi.
“Hivi mnaijua nyumba yetu nyie?” niliwauliza, wote wakaangaliana na kuanza kucheka.
“Kwani huna mshikaji wenye kideo ukutani?’ mmoja aliniuliza.
“Ninaye!”
“Huna mwana anayepiga blingblingi akuazime nguo?”
“Ninaye!”
“Sasa tatizo lipo wapi? Ng’oa mzigo kaka!”
Walinipamba weeeee, nikakubaliana nao na kumwambia Bupe. Akaniangalia mara mbilimbili kwa lile jicho lisemalo “Mimi nije kwenu! Tandale Kwa Tumbo! Kule kwenye wezi wa simu! Bupe mimi ninayeishi Tabata! Ni kitu kisichowezekana hata kidogo.”
Nilijua tu kwamba alikuwa akiniambia hivyo kimoyomoyo! Na mimi nikamwangalia jicho la kumwambia “Mbona utakuja tu! Nina geto kali la mchizi, kideo ukutani, Dstv, choo cha kuflashi, mbona utashangaa mwenyewe. Wewe twende kwanza,” macho yangu yalisema maneno hayo.
Kwa mbali nikamuona Bupe akitabasamu, akanisogelea kidogo na kunishika mkono, mapigo ya moyo yakawa juu.
“Nyemo! Kwenu ni vichochoroni?’ aliniuliza huku akiniangalia.
“Ndiyo! Kwa nini umeuliza?”
“Sitaki kukabwa!”
“Nitakuwa pamoja nawe. Hutokabwa.”
“Basi nitakuja Jumapili. Sawa baba watoto?”
“Sawa mamii!’
Kabla ya yote nikawaandaa masela kabisa, nikawaambia mtoto anakuja, cha kwanza nahitaji geto la mwanangu Noel kwa saa mbili tu, akanikubalia, mbali na yeye nikachonga na mwanangu Rajabu, akanipa nguo. Siku hiyo wakati namsubiri, nilikuwa nashaini kinoma.
Jumapili hiyo ikaingia. Bupe ndani ya Tandale. Nilimuona anashuka kwenye ndinga kali sana, ilikuwa ikiendeshwa na mzee mwenye ndevu nyeupe, akaja nilipo, ndinga ile ikaondoka na sisi kusepa kuelekea home kwa msela.
Unajua geto umelifanyia usafi ile kinoma, kunang’aa, viatu vya mshikaji umevipanga vizuri lakini demu alipoingia ndani, niliona kabisa kabadilika.
“Hapa ndiyo kwako?” aliniuliza.
“Yeah! Unataka kinywaji gani?” nilimuuliza huku nikifungua friji. Mtu mzima nilijiandaa, humo niliweka chua za soda za 7Up mbili, ndani nilijaza maji na kukikandamiza kisoda chake. Pia kulikuwa na chupa moja ya Fanta, sikuwa na uwezo wa kununua soda mbili. Nilipotoa, nikawahi chupa ya 7Up manake angeitaka yeye ingekuwa balaa.
“Kunywa soda ya wanawake hiyo! Sisi wanaume tunakunywa 7Up!” nilimwambia kwa mbwembwe huku nikimfungulia, ili asionekane kuitaka ile 7Up niliyoweka maji, nikapiga funda moja fasta.
“Umejitahidi chumbani kwako japo bado kunaonekana local sana,” aliniambia huku akiangalia huku na kule.
Kile chumba ndicho kikali kuliko cha washikaji zangu wote, yeye anasema ni local, je, inamaanisha mageto anayoingia yeye ni hatari sana, yana AC, Tv nchi 50, kapeti unyoya na madude mengine ya hatari.
“Ndiyo tunajipanga mdogomdogo. Ila umependeza! Hiyo nguo umenunua wapi manake imekutoa chicha mno,” nilimwambia harakaharaka huku nikimtoa katika ishu ya kuzungumzia geto manake nilishaumbuka.
“Kariakoo! Nikuulize kitu?”
“Uliza tu!”
“Unanipenda?”
“Hapo umeniuliza au umeniambia?”
“Nimekuuliza!”
“Mimi naona umeniambia. Ninavyokupenda, hakuna mfano! Ninakupenda mno! Angalia macho yako, kama umekula kungu, mtoto una kitumbo fulani hivi amazing, jicho nyanya, shavu laini, lipsi nene, miguu imejaajaa sana! Bupe, kwa kifupi, kila nikikuangalia natamani uuruhusu ulimi wangu ufanye ziara mwili wako wote,” nilimwambia huku nikiachia tabasamu, eti cha ajabu na mimi ninawa narembua macho.
“Hahah! Una maneno matamuuuuuu!”
“Bila shaka ya kumtoa nyoka pangoni, maneno yaliyowafanya wakoloni watuachie nchi yetu,” nilimwambia na kumsogelea zaidi, nikaupeleka mkono mapajani mwake.
“Jamani! Unataka kufanya nini?” aliniuliza kwa sauti fulani hivi nyororoooo...yaani kwa jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea mule ndani, nikasema mtoto kushnei.
“Nataka kufanya nini?”
“Ndiyo!”
“Kuimba wimbo wa CCM Mbele kwa Mbele!”
“Hahaha! Halafu wewe bwana. Unajua mimi nakuchukulia kama kaka yangu wa kuzaliwa tumbo moja,” aliniambia. Yaani maneno yake yalinichefua, nikakunja sura kwa mbali na kumpa bonge moja la mtusi kimoyomoyo. Eti unafika magetoni unaniambia kwamba unanichukulia kama kaka yako, ulivyokuwa akiniita baba watoto shuleni ulimaanisha nini.
“Bupe,” niliita kwa sauti ya chini iliyomaanisha kwamba kuna kitu nakitaka.
“Abee kaka!”
“Daah! Kaka tena!”
“Ndiyo! Kama siyo kaka yangu, niambie una shilingi ngapi!”
“Hela tena!”
“Nyemo! Niangalie jinsi nilivyo, mimi ni msichana mrembo, kila mwanaume ananitaka, napendeza, unahisi nani ananipendezesha? Unadhani ni mama yangu muuza vitumbua ndiye ananipendezesha? Nyemo, acha mawazo ya kiswahili! Yaani unataka kutembea na mtoto mkali huku ukiwa huna hela? Nyie ndiyo wale mnaosema yule nimelala naye, hana kitu, kiuno kama gogo. Mimi si wa hivyo Nyemo, mimi si mwepesi. Ni bora unipe hela, baadaye ukisema kwamba umelala na mimi, pia nami nitasema nilikula hela yako!’
Ebwana siku hiyo Bupe alinipa makavu, alinichamba mpaka nikajuta kwa nini nilimuita. Nilibaki nikishangaa, alihitaji hela na wakati mimi nilijua kwamba ananitunuku baada ya kunipamba sana shuleni.
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wangu wa kukaa na kuongea naye. Mpaka leo hii sikuwahi kuongea naye. Namjua! Yupo, namuonaga sana. Kalio lake halipo tena, amekongoroka, niliambiwa na jamaa yangu kwamba kwa sasa anatumia dawa kwani aliambukizwa Ukimwi na pedeshee lililokuwa linamiliki shimo huko migodini Shinyanga.
Makalio yakamponza, uzuri wake hakuutumia vizuri. Wakati mwingine nikawa najifariji kwamba inawezekana alipata matatizo baada ya kuniringia, baada ya kutokuniruhusu kula tunda, labda ningekula mpaka leo hii mambo yake yangekuwa safi tu.
Ndugu yangu! Haka ni kastori fulani ka kutunga lakini naamini kuna mengi umejifunza. Wakina Bupe wapo, tena wengi, wakina Nyemo nao wapo tena wengi. Hutakiwi kubabaika kisa mwili, hutakiwi kubabaika kisa wowowo. Mwanamke! Hutakiwi kubabaika kisa pesa, pesa zinapokuja, zinabeba mambo mengi sana. Hakuna pesa inayotembea peke yake, nyuma ya pesa kuna magonjwa, nyuma ya pesa kuna kifo cha mateso.
Uamuzi ni wako! Kuamua kula kwa macho kama mtu aliyekatwa mikono au kula kiuhakika kusongesha siku ziende. AMUA SASA!
 
JOHN ANAGOMBANA NA MKEWE, ADAM ANAMPENDA MKEWE.

Na Halfani Sudy (0674 395733)

Ghafla nilistuka toka usingizini, nikiwa timamu wa akili ingawa macho nilikuwa sijayafumbua bado. Yaani nilikuwa nusu nimelala, nusu nimeamka.
Ndipo niliposikia. "Nakwambia Herieth utaondoka nyumbani kwangu, mwaka wangapi huu hujanizalia mtoto mwanamke wewe, mwanamke hujawahi hata kusikia kichefuchefu looh! Mwanamke gani wewe, hujui hata wajibu wako ndani ya ndoa, kazi yako kujaza choo tu!"
Nikiwa palepale kitandani niliisikia sauti ya John ikiwa katika jazba ya hali ya juu. Lakini kwa bahati mbaya sikusikia jibu la mkewe. Nikajilazimisha kufungua macho hadi yakafunguka. Nikalizoa shuka langu pembeni na kulivirigiza mwilini, nilitoka mbio kukimbilia kwa jirani yangu kushuhudia mwenyewe, nilikimbilia nyumbani kwa Bwana John.
Nikipofika niliukuta ummati wa watu nje ya nyumba ya bwana John. Wakishangaa vitu kadhaa vilivyokuwa vimetawanywa hovyo pale nje, bila shaka vilikuwa vitu vya Herieth, mke wa bwana John. Mimi nilikuwa nahangaika kulifunga shuka langu vizuri huku nikiwatafuta walipo wagomvi wa asubuhi ile.
Ndipo niliposikia tena. "Lakini mume wangu si nilikwambia tukapime tujue tatizo liko wapi si ulikataa???.." Ilikuwa sauti yenye mchanganyiko wa huzuni na kwikwi toka mdomoni kwa Herieth.
Niliangaza kutafuta mahali ilipotoka sauti ile ndipo nilipowaona. Bwana John na mkewe mzuri sana Herieth walikuwa wanaangaliana kwa hasira mithili ya midume ya ng'ombe inayogombea ng'ombe jike. Wote walikuwa wamefura kwa hasira. Hitaji la mtoto lilikuwa linaenda kuivunjavunja ndoa ile adhimu. Hitaji la mtoto lilikuwa linaenda kuitafunatafuna ndoa ile ya mfano. Hitaji la mtoto lilikuwa linawadhalilisha wanandoa wale matajiri kabisa.
Kwa kifupi ndoa ya bwana John na Herieth ilikuwa ni ndoa ya aina yake. Ndoa uliyovunja rekodi wakati inafungwa katika mji wa Makambako. Ndoa iliyofungwa kwa sherehe kubwa sana na iliyofana kuliko sherehe zote nilizopata kuzishuhudia maishani mwangu.
Siku ya ndoa watu walikunywa vinywaji na kusaza chakula. Hakika Ilikuwa ndoa ya kitajiri ambayo haijawahi kutokea katika historia ya mji wa Makambako. Lakini kwa bahati mbaya kabisa ndoa ya kitajiri haikuleta majibu akiyoyataka Bwana John. Ni mwaka wa tano sasa wanandoa wale matajiri walikuwa hawajapata mtoto hata wa dawa.
Nikiwa umbali kama wa mita tano hivi. Nilimwangalia Herieth, mke wa bwana John. Usingizi wote ulinitoka. Macho ya Herieth yalinitoa usingizini. Herieth alikuwa anamwangalia mumewe kwa jicho la chuki, chuki ya kudaiwa mtoto, chuki ya kudhalilishwa mbele ya majirani zake. Hakukuwa na upendo hata chembe katika macho ya Herieth.
Kimoyomoyo nikajisemea peke yangu "hapa hakuna ndoa tena".
Nikiwa nimesimama na mshangao tele mara nilihisi napapaswa begani, nikageuka kwa kasi kumwangalia aliyekuwa ananipapasa. Sikumuona mpapasaji. Ila niliona kitu.... Nilikuwa natazamana na magari sita ya kifahari yikiwa yamepangwa kwa mpangilio mzuri wa kupendeza. Mmiliki wa gari zote hizo alikuwa ni bwana John. Niliwaza huku nikiwa nayatazama yale magari. Ukweli ni kwamba bwana John hana maisha ya kubangaiza hata kidogo. Ni tajiri mkubwa sana katika mji wa Makambako. Utajiri aliorithi toka kwa baba yake mzazi, nae aliuendeleza vizuri sana. Alikuwa na nyumba za kisasa zipatazo kumi na nane katika maeneo mbalimbali ya mji wa Makambako. Alikuwa na magari ya biashara yasiyo na idadi, alikuwa anamiliki vituo vya mafuta vitatu, duka la jumla la vifaa vya ujenzi, duka la jumla la vifaa vya umeme. Frem lukuki alizozikodisha kwa wafanyabiashara mbalimbali pale Makambako sokoni. John alikuwa tajiri kwa maana sahihi ya kuitwa tajiri. Hiyo nd'o sababu ya kuoa ndoa ya kitajiri. Ndoa iliyotingisha Iringa nzima. Lakini leo ndoa ilikuwa inaenda kuvunjika, kisa mtoto...
Nikiwa nimezubaa pale mara nilistuka nimesukumwa pembeni. Bado kidogo shuka yangu inivuke. Alipita Adamu na mkewe wakiwa wameshikana mikono, hadi pale waliposimama Bwana John na mkewe. Adamu alianza kuongea bila kuulizwa.
"John ndugu yangu umebarikiwa sana, una nyumba nzuri sana, una magari mazuri na ya kifahari, una pesa nyingi sana, unapata kila kitu unachokitaka katika dunia hii kasoro kitu kimoja tu, mtoto. Ona sasa mimi na mke wangu Amina hatuna kitu chochote cha kujivunia katika maisha yetu lakini bado tunapendana, hebu igeni mfano wetu. Tuna miaka tisa katika ndoa yetu, lakini hatuna magari, hatuna nyumba, hatuna maduka na wala hatuna huyo anayewafanya mgombane ninyi…mtoto, lakini pamoja na yote hayo wala hatujakorofishana hata siku moja na mke wangu, hatujaachana, ndo kwanza tunazidi kupendana. Kumbuka mtoto ni majaaliwa toka kwa Mungu, anampa ampendae, anamnyima amtakae, lakini hatutakiwi kukufuru kwa yote hayo. Hebu kumbuka hadithi ya Ibrahim na Sarah. Walikosa mtoto katika ujana wao wote lakini hawakuwahi kugombana hata siku moja kisa mtoto. Walidumu katika upendo hadi Mungu alipoamua kuwapa. Mpende mkeo bwana John na imani ipo siku mtapata mtoto. Usimkufuru Mungu wako kisa kakunyima mtoto, Mungu ana makusudi yake katika kila jambo, Muombeeni sana Mungu na mumshukuru kwa matokeo yoyote yale, yawapendeze ama yasiwapendeze"
Baada ya maneno hayo Adam alishika imara mkono wa mkewe na kuondoka zao. Baada ya maneno hayo bwana John nae alirudi ndani na mkewe akiwa amemshika kiuno, na wambea wote kutawanyika.
Toka siku ile sijasikia tena ugomvi wa bwana John na mkewe kuhusu mtoto. Hadi hivi juzi kati nilipomuona bwana John na mkewe wakienda hospitali huku tumbo la mkewe likiwa na ujazo usio wa kawaida.

Mwisho.

Imeandikwa na Halfani Sudy
 
ND'OMANA N'KAOA 2017.
Na Halfani Sudy

Nilipiga simu kwa mara ya nyingine. Mara mbili za awali simu iliita tu bila kupokelewa, lakini mara hii ilipokelewa. Nilisikia sauti ya kiume ikisema kwa fadhaha..

" Tumsaidieni jamani, tumsaidieee" Na simu ikakatwa.
Nilibaki nikiwa nimehemewa bila kujua kitu gani kimetokeaa..

Namba niliyokuwa ninaipiga ni ya mpenzi wangu Salma. Mpenzi niliyoongea nae nusu saa iliyopita akiwa stendi Mbagala, nilimwelekeza gari la kupanda ili afike nyumbani kwangu. Nilijaribu kupiga tena ile namba, simu iliita tu bila kupokelewa. Nilichanganyikiwa sana.

Nilikaa kitandani huku mikono yangu yote ikiwa mashavuni. Sikuelewa ni kitu gani kilichompata mpenzi wangu Salma.
Saa sita mchana alitoka nyumbani kwao Kilwa ili kuja jijini Dar es salaam kwa ajili yangu. Nami nilikuwa nimetoka Singida kwa ajili ya miadi hii.
Alipokuwa njiani tulikuwa tukiwasiliana mara kwa mara hadi alipofika Mbagala. Mawasiliano yetu yalikata mara tu alipopanda gari la kutoka Mbagala kuelekea kwangu.

Sauti ya mtu ikiyosema tumsaidieni jamani, tumsaidie.. ilijirudia mara kwa mara katika akili yangu. Nilikuwa namuomba Mungu Salma kisimkute chochote kibaya.
Zilipita takribani dakika thelathini ndipo simu yangu iliita. Niliichukua kwa pupa na kuangalia namba iliyokuwa inapiga, ilikuwa ni namba ya Salma.

"Haloo Salma" Niliita harakaharaka.

"Mimi sio Salma. Salma amepatwa na matatizo njoo haraka hapa temeke hospitali" Sauti nisiyoifahamu ilisema simuni.

Nilihema kwa nguvu. Simu iliendelea kuongea lakini sikusikia chochote. Harakaharaka nilijiandaa na kwenda Temeke hospitali. Nilipofika na kujitambulisha daktari aliniita pembeni na kunipa taarifa iliyoipasua moyo wangu.

"Salma amefariki ghafla akiwa katika foleni za pale Uhasibu. Kwa mujibu ya watu waliomleta, alistuka tu na kukaa kimya. Huo ndio ulikuwa mwisho, mwisho wa Salma. Wamemfikisha hapa akiwa ameshafariki!"

Nilihemewa, nilichanganyikiwa. Sikujua nilie ama nifanye nini. Daktari akaniomba niwataarifu ndugu zangu kuhusu habari ile. Salma hakuwa ndugu yangu, alikuwa mpenzi wangu na alitoroka kwa siri kwao kuja kwangu. Nilimwambia daktari achukue simu ya Salma na tuone kama kuna namba ya kuipigia. Aliileta. Tukampigia dada yake ambaye alikuwa Kilwa, na yeye alituunganisha na dada yake aliyekuwa Dar es salaam.
Dakika hamsini baadae dada yake Salma aliwasili. Akiwa mwenye sura iliyojaa machozi. Mimi na yeye tuliingia ndani na kuuona mwili wa Salma. Salma alikuwa amelala kitandani. Sura yake ikiwa katika uzuri wake uleule. Alikuwa amevaa nguo ambazo nilikuwa nimemnunulia mimi. Chini ya kitanda kulikuwa na begi lake la nguo na bahasha yenye samaki. Nilikumbuka jinsi alivyoniuliza aninunulie Samaki alipofika Somanga. Sikuweza kuvumilia kumuona Salma katika hali ile, chozi la uchungu lilinidondoka sakafuni.

Baada ya ndugu wengine kupewa taarifa na kuja hospitali, tulikabidhiwa mwili wa Salma kwa ajili ya mazishi.

Tangu siku hiyo niliiapa sitoshiriki tena mahusiano nje ya ndoa. Maana nilikumbuka jinsi Salma alivyokuja Singida na kuishi naye mwezi mmoja, je angefariki kipindi kile? Nilikumbuka jinsi Salma alivyoniomba atoke Kilwa asubuhi ili awahi kufika Dar. Kwa maana muda ule aliofariki angekuwa ameshawasili nyumbani kwangu. Angenifia ndani. Je jamii ingenielewa? Nilikumbuka Salma alivyonisisitiza nikampokee Mbagala. Inamaana angefia pembeni yangu ndani ya gari. Je dunia ingenielewa kweli?

Ni mwaka sasa tangu tukio hilo limetokea. Kwa sasa nimeoa kama nilivyojiahidi lakini bado tukio lile la Salma halijanitoka kichwani mwangu.

HAPPY NEW YEAR...2018
 
SIMULIZI YA WIKI

NIPE CHENJI YANGU

Na Fadhy Mtanga

“KONDA naomba chenji yangu?”

“Chenji ya wapi mamdogo mbona unanizingua tu hapa?”

“Yaani nadai chenji yangu unasema nakuzingua?” Neema anafura kwa hasira. Anatamani hata kumnasa makofi konda.

“Wapi wewe? Huna chenji yako hapa ishia kule.” Konda hana muda kabisa na Neema. Konda anaanza kushuka garini ilhali Neema bado kasimama ndani ya daladala akiwa haamini kinachoendelea. Koda hakuwa amemlipa kabisa chenji yake baada ya kulipa nauli. Sasa konda anapomwambia hana anachodai ndipo anapozidi kuchanganyikiwa.

Akili inamrudisha ghafla kiasi cha saa moja iliyopita akiwa ofisini.

“Vipi Neema mbona umeingia umekasirika sana?” Belinda, mfanyakazi mwenzake na shogaake wa karibu anataka kufahamu kulikoni baada ya Neema kuingia ofisini akitweta na kuurushia mkoba wake mdogo juu ya meza.

“Mmhh!” Neema anaguna badala ya kujibu.

“Ukiguna sikuelewi mpenzi wangu? Njiuze kilichokusibu.” Sauti ya Belinda ya taratibu na yenye kubembeleza. Sauti ambayo bila shaka aliyemchagua hupata nayo raha masikioni mwake. Sauti nyororo na iliyojaa mahaba kuliko kinanda. Kila mtu humo ofisini hutamani kumsikia Belinda akiufungua mdomo wake.

Neema anamkodolea shogaake, macho pima. Belinda anajua haikosi kuna zaidi ya jambo.

“Sema basi kipenzi nini tatizo? Sam tena?”

“Bora hata angekuwa Sam. Mwenzio nimetoka kwenye ATM hapo chini mshahara bado hujaingizwa.”

“Aah, pole mpenzi! Nilisahau kukwambia. Kuna kioffice memo kimebandikwa kuwa mshahara utachelewa kwa siku mbili. Hivyo utatoka kesho kutwa asubuhi. Bosi kaomba msamaha anasema watu wa Hazina wamechelewa kutoa fungu.”

“Watu wa Hazina wananihusu nini mimi?” Ni dhahiri Neema kazidi kuchanganyikiwa.

“Pole sana Ney. Sasa utafanyaje?”

“Kuna cha kufanyaje tena hapa? Mi’ nd’o nazidi kuchanganyikiwa kabisa. Ninapokuja kazini asubuhi nilikuwa na nauli tu. Mchana nimepiga ndefu. Sina pesa ya kurudia nyumbani. Sijui jioni nitakula nini. Sam bado hajarudi safari. Mbona nitakoma mie!”

“Pole jamani. Kama shida yako ni hiyo,” Belinda akauchukua mkoba wake. Akatoa noti moja ya shilingi elfu kumi. Akamkabidhi shogaake. “chukua hii Msimbazi shogaangu wala usilie bure mrembo. Najua leo na kesho uwongo. Kesho kutwa asubuhi na mapema mshahara utakuwa tayari.”

Neema akaipokea akiwa haamini macho yake. Ingawa wamekuwa wakisaidiana mara nyingi, Neema alijua pia Belinda amechacha baada ya mshahara kuchelewa takribani juma moja ukijumlisha na hizo siku mbili zingine.

“Ahsante sana mpenzi. Hapa umenifichia aibu. Maana leo hata ningetongozwa na mpiga debe ningelazimika kukubali.”

Wote wakacheka.

Muda wa kazi ulipoisha Neema akaenda hadi kituo cha daladala cha Posta ya zamani. Akasubiri kwa zaidi ya nusu saa ndipo alipofanikiwa kupanda gari baada ya kugombania. Akiwa amechoka mwili na akili akalazimika kusimama safari nzima.

Daladala ile ilipoondoka tu, konda akaanza kudai nauli. Neema akaitoa noti yake ya elfu kumi ya mawazo aliyopewa na shogaake Belinda ili aokoe jahazi lililokuwa likizama. Kila mara alikuwa akimkumbusha konda kuhusu chenji yake. Mara zote koda alikuwa akimjibu, “nakupa.”

Wala asipewe hiyo chenji yake.

Gari likafika mwisho wa safari. Kila Neema anapozungumza na konda, anaambuliwa kupewa majibu mabovu ambayo yalizidi kumchoma mshale wa maumivu makali sana moyoni mwake. Akizingatia asipokuwa makini atalala njaa na hatimaye kukosa pesa ya nauli kesho yake kwenda ofisini, Neema akaamua kukaza buti.

Neema akamfuata konda pale chini alipokuwa akichukua nauli kwa abiria waliopandia vituo vya karibu. Konda akajifanya kutokuwa na muda naye.

“Konda tuheshimiane tafadhali. Nimekupa noti ya elfu kumi. Nipe chenji yangu.”

“Oyaaa! Usiniletee za kuleta hapa. Nani unamdai chenji wewe? Hebu tupa kule.”

“Konda ustaarabu ni kitu cha bure. Nipe chenji yangu.” Sasa Neema alikuwa akizungumza huku akiweka simu na pochi ndani ya mkoba wa begani.

“Unanizingua tu. We demu umeachika nini?” Wakati konda akizungumza hivyo, abiria wengine walikuwa wakikodoa macho umbea kutaka kufahamu hatima ya kizaazaa hicho.

“Konda nipe chenji!” Neema akaendelea kudai chenji yake kwa jazba.

“Usiniyeyushe.” Konda akamjibu kwa jeuri. Kama kawaida ya makonda wa Dar.

Bila mtu yeyote kutarajia, Neema akamvaa konda na kumkunja shati lake huku akimnasa kofi la nguvu.

“Weweeeeee!” Watu wote wakaanza kushangilia.

Wakati konda akijaribu kujinasua mikononi mwa Neema ambaye alikuwa amemdhibiti hasa, Neema akamvuta karibu yake zaidi. Neema hakuongea neno zaidi ya kuhema kwa nguvu ikiwa ni mchanganyiko wa hasira na uchovu. Konda akapoteza balansi na kuteleza. Mguu mmoja ukatumbukia mtaroni na kumfanya naye kudondoka mzima mzima.

Neema akawahi kumwachia ili naye asidondoke. Lakini kwa haraka, akaushika mkono wa konda uliokuwa umeshika pesa na kudhibiti kiasi fulani cha pesa huku vijana wa kijiweni wakigombania pesa zingine zilizomwagika. Neema akaziweka pesa zile pasipo kuzihesabu ndani ya mkoba wake.

Akatokea dereva na kuja juu. Huyku bado akiwa na hasira Neema wacha afoke. “Tena usinisisumbue na wewe. Baradhuli huyu kaona mie mwanamke akadhani maji ya mtaro. Haya maji marefu. Imekula kwenu. Kama wewe mwanaume kweli sogea tuone utanifanya nini.”

Dereva akabaki akiduwaa. Vijana wa kihuni walishagawana pesa zote zilizobakia mkononi mwa konda huku yeye akiwa chini pasi kuamini kilichomtokea.

Vijana wale wakaanza kumshangilia Neema ambaye wala hata hakuhangaika na mtu.

Akageuka zake.

Akaondoka.

Fadhy Mtanga, 2010
 
SIMULIZI YA WIKI

NIPO SONGEA

DALADALA imekolea mwendo. Kondakta wa daladala ametingwa kukusanya nauli. Pamoja na kutingwa kwake, bado hasahau kuwakumbusha abiria vituo. “Manzese Darajaniiiii!”

“Shushaaa!” Abiria mmoja wa kike anapaza sauti.

Omi, dereva wa daladala hilo lililoanza kuchoka anakanyaga breki. Konda anafungua mlango, mama huyo anashuka. Kijana mmoja wa makamo anaingia ndani ya daladala hilo. Nyuma yake anapanda binti mwingine. Anakwenda moja kwa moja kuketi kwenye siti iliyo wazi, ambayo awali ilikaliwa na mama huyo aliyeshuka.

Mtu huyo anapoketi tu, analegeza tai yake shingoni. Joto la Dar es Salaam si mchezo. Mchana huu jua linawaka kweli kweli, na kuwatoa jasho wakazi wake. Mabruki anailegeza vizuri tai yake na kuacha nafasi ya kutosha kuingiza hewa.

Kisha anachukua nakala yake ya gazeti lililosheheni habari za kisiasa na kuanza kusoma kwa utulivu. Hana habari na yeyote ndani ya gari hilo. Akili yote ipo kwenye gazeti lake.

Pembeni yake anaketi kimwana mmoja. Tangu Mabruki aingie ndani ya gari hilo, binti huyo katingwa na simu yake ya kiganjani. Anaandika na kusoma ujumbe. Soga mtandaoni kwa mtindo mmoja. Mabruki wala hana hata habari.

Mara simu yake inaita. Anatulia kidogo kuusikilizia mlio wake. Mlio pekee unamtosha kumfahamu mpigaji ni nani. Huku mapigo ya moyo yakienda kasi, anaitoa simu hiyo iliyokuwa ndani ya mfuko wa shati lake na kuipokea. Anaongea kwa sauti ya chini ili kutowabughudhi abiria wengine.

“Helo my dear.”

“Baba Zahra za leo?”

“Salama tu mama. Kwema huko?”

“Kwema kabisa. Hofu juu yako mpenzi. Habari za Songea?”

“Njema mama. Bado tunaendelea na semina. Kesho tunategemea kumaliza kama nilivyokueleza. By Friday ntakuwa njiani honey.”

“Jamani baba Zahra usisahau basi kuninunulia viazi vya Songea. Shogaangu mama Hamdani kaniambia huu ndo msimu wake. Si unajua dear vilivyo bomba sana viazi vya Wangoni?”

“Yah!” Anaitikia.

Mkewe anapata uwanja wa kumwaga sera. “Niambie basi honey, utaniletea? Halafu jamani huko ukibahatisha hata kakipande ka nyamapori dear. Si unajua sijala siku nyingi, tangu kipindi kile tulipoenda kwa mama Mngazi?”

“Tatizo upatilkanaji wake. Nitaulizia ulizia.”

“Halafu tena.”

Huyu naye! Mabruki anatamani kukata simu kabla konda hajaita kituo. Lakini mke wake anazidi kuzungumza pasi kuonesha dalili ya kukata simu haraka. Mambo ya Xtreme hayo.

“Halafu tena honey, yule fundi uliyesema atufungie dishi wala hajaja kufunga. Mpigie basi umwambie afanye fasta. Si unajua tena nakosa kuangalia ze komedi?”

“Ok! Nitampigia. Basi ngoja nimpigie, kisha nitakupigia baadaye kidogo.” Mabruki anaona hiyo ndiyo njia pekee ya kumaliza maongezi kwenye simu.

“Utampigia hata baadaye kidogo. Halafu nilitaka kusahau kukwambia.”

Huyu naye, nini tena? Kwa hasira anajikuta anauliza, “nini tena?”

“Hivi yule shogaangu wa Mwanyamala yule alikuja nyumbani majuzi jioni si unamkumbuka?”

Mambo ya shoga zake na mimi wapi na wapi? “Ndiyo namkumbuka.”

Anajibu haraka haraka kumaliza maongezi.

“Basi mwenzangu kumbe shida yake yote iliyomleta nyumbani ilikuwa ni kukopa pesa. Hakutegemea kukukuta. Alipokukuta tu, akaishiwa sera. Basi leo kaja tena.”

Sijui nimkatie simu? Mabruki akashindwa kujijibu. Akabaki kimya.

“Basi mi namshangaa sana. Anapenda sana kuchonga juu ya maisha ya wenzake, kumbe naye anategemea vya kukopa.”

“Mh!” Mabruki akaishia kuguna.

“Wala hata sijampa.”

Kabla hata hajajibu, anamsikia konda, “Shekilangooo?”

“Shushaaaa!”

Mabruki aliikata simu kama aliyewehuka ghafla. Mapigo ya moyo yakaruka mapigo. Jasho lilimtoka mithili ya mtu aliye jirani na tanuri la moto.

Simu yake ikaanza kuita tena. Binti aliyeketi pembeni akishughulika na simu yake alikuwa akitabasamu kwa mbali. Dalili zote zilionesha alifanya jitihada za makusudi kuzuia kicheko chake kisitoke nje. Mabruki hakujisumbua naye. Akaonelea amwache ahangaike yake.

Akaitazama simu yake iliyokuwa ikiita kwa macho ya hofu tele. Mke wake hata hakuonesha dalili za kuchoka. Ilipokatika ikaita tena.

“Leggooo?”

“Shusha.” Mabruki akainuka haraka haraka na kushuka garini. Binti yule naye akashuka. Aliposhuka tu, akaenda haraka katika kibanda cha simu na kuzuga ananunua muda wa hewani.

Mabruki akaitazama simu iliyokuwa ikizidi kuita kwa mashaka tele. Kama atakuwa amesikia, itakuwaje? Ndilo swali lililomtawala. Akapiga moyo konde na kuipokea.

“Mbona ulikata jamani honey?” Mkewe alianza kwa lawama moja kwa moja.

“Mh eeh! Haina chaji ikazima.”

Upande mwingine jijini Dar es Salaam, mke wa Mabruki alitamani kuangua kicheko. Akaamua kuwa mstaarabu. Muda wote akizungumza kwenye simu, alikuwa ndani ya teksi. Alikuwa na haraka ya kufika mahali.

“Basi ukishaiweka chaji usisahau kunipigia mume wangu. Si unajua ninavyokumiss acha kabisa. Nakupenda sana.”

“Ok. Nami pia. Baadaye basi.”

Simu ikakatwa.

Mabruki akaenda moja kwa moja hadi ndani ya Leggo hoteli.

Yule binti aliyezuga akinunua muda wa maongezi, akainyanyua simu yake na kuzungumza huku akicheka.

“Mbona umechelewa sweetie?” Kidawa alianza kumwambia Mabruki baada ya salamu.

“Foleni mpenzi.”

“Pole sana mpenzi wangu.”

“Ahsante. Si ushakula, twen’zetu ndani.”

“Ok. Tena nina hamu nawe. Maana umekwenda Manzese umechelewa.”

“Si wale mafundi wamenichelewesha. Ila fremu yako watu wanaisifia sana. Sipati picha utakapoanza kupanga vipodozi kwenye shelfu zake patapendezaje? Hadi nina wasiwasi vijana wa siku hizi watanipora.”

Mkono wake kiunoni kwa Kidawa. Binti yule aliyekuwa akizuga kununua muda wa maongezi, akawa kesha maliza kuzungumza kwenye simu. Akaingia pale hotelini na kuagiza soda ya Mountain Dew.

“Wala hani wangu. Akupore nani wewe mwenyewe upo juu kama ndege ya Obama.”

Wote wakaangua kicheko.

Wakati wanachukua ufunguo wao mapokezi, binti yule aliwapita akiwa na chupa yake ya soda mkononi huku akizungumza na simu.

Wakaingia. Mabruki alikuwa ametoka hotelini hapo takribani masaa mawili nyuma.

Hivyo akapitiliza maliwatoni. Akakoga.

Kisha akaungana na Kidawa, mtoto wa mjini. Wakaanza kupeana mahaba.

“Ngo! Ngo! Ngo!” Mlango uligongwa wakati wao wakiwa wamezama katika bahari ya mahabadati.

“Nani?” Mabruki aliuliza kwa hasira na uchovu.

“Front office please. A minute please.”

Mabruki akamwashiria Kidawa akafungue.

Bibie Kidawa akavuta kipande cha kanga na kujisitiri japo kidogo. Akaenda mlangoni.

Akaufungua.

Wanawake wawili walikuwa wamesimama nyuma ya wanaume wawili, ambao nao walikuwa nyuma ya mhudumu wa hoteli.

Kidawa akapigwa na mshangao. Akababaika. Mmoja wa wanawake wale alimfahamu fika. Wale wanawake wawili wakapiga jicho moja kwa moja hadi ndani ili kuona kilichomo. Wakati Kidawa akiwa angali na butaa, akasukumiwa ndani mzima mzima. Kundi la watu wanne likaingia hadi ndani huku mhudumu akibaki koridoni pasipo kufahamu cha kufanya.

“Ndiyo Songea hapa?” Hilo ndilo swali pekee mama Zahra alilomudu kuliuliza.

Mabruki akabaki akiwatumbulia tu macho wageni wale mithili ya mbwa aliyekabwa na mfupa.

Mama Zahara alipojaribu kuuinua mdomo wake kuzungumza, mdomo pekee ndio uliofunguka lakini sauti haikutoka.

Mara akaanguka chini akiwa amezidiwa na mapigo ya moyo.

Kila mtu mle ndani akachanganyikiwa.

Mabruki akavaa suruali yake kwa kasi ya ajabu. Jambo lililowashangaza wote, Mabruki ndiye aliyekuwa wa kwanza kwenda kumnyanyua mke wake. Akambeba mzimamzima mithili ya kuli na gunia la nafaka.

Alipofika chini, akaita teksi haraka na kumkimbiza hospitali.

MWISHO

Fadhy Mtanga, 2010
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom