bampami
JF-Expert Member
- Nov 5, 2011
- 5,700
- 4,126
Picha hii ilipigwa na Fadhy Mtanga kwa simu yake ya kiganjani, baada ya mimi kumwomba afanye hivyo. Tulikuwa tumeketi mgahawani, ndani ya viunga vya uwanja wa ndege wa JKN, ndipo alipoingia mzungu huyo pichani na kuketi. Baada ya kuagiza kinywaji, alitoa kitabu na kuanza kujisomea. Nilipojaribu kupepesa ili nione kama yupo Mwafrika mwingine anayejisomea kitabu hata cha mahepe (ngoma za kichawi) - usiniulize nimezijuaje, sikumwona. Karibu kila mmoja alishughulishwa na simu yake. Amaa kweli ukitaka kumuua Mwafrika weka ujumbe kwenye vitabu. Yaani wakati wenzetu walioendelea wakijichotea hazina za maarifa na kujiongezea maendeleo, sisi tuko busy kucheza game za nyoka. Kama si ujahili tuuiteje basi?
Siku moja akiwa safarini, mzee Masiyiwa alikutana na rafiki yake wa miaka mingi, baada ya kujuzana hali, yule bwana akamuuliza: "Siku hizi unaishi wapi?"
Mzee Masiyiwa akajibu, "Nina nyumba Johannesburg, na nyingine London."
"Vitabu vyako viko wapi?" Yule bwana alisaili tena.
Mzee Masiyiwa akajibu, "Vitabu viko nyumbani kwangu Johannesburg."
"Basi hapo ndipo unapoishi, kwa sababu mtu hupendelea kuzungukwa mali zake; na vitabu ni miongoni mwa milki zenye thamani ya juu mno."
Umeona thamani ya vitabu? Mtu ametambulika anapoishi kwa sababu tu vitabu vyake viko hapo. Ingelikuwa kwetu waswahili, ukitaka kujua kama leo 'mtu wako' hatochelewa kurudi au haendi mbali, unaangalia tu kama hakuchukua charger ya simu yake.
Chukua hii: Siku moja, baada ya misa Kanisani, Mchungaji alimsogelea kijana mmoja aliyekuwa mikono mitupu na kumuuliza: "Biblia yako iko wapi?"
"Sina Biblia," Kijana alijibu, kisha akaongezea, "sina pesa ya kununua."
Mchungaji alimtazama miguuni na kumwambia: "Uza viatu vyako na ununue Biblia."
Tazama, Mchungaji ameona aheri kijana atembee peku lakini awe na kitabu (Biblia). Yaani, kwa lugha rahisi ni kwamba, aheri kubaki na vumbi miguuni (kwa kukosa viatu) kuliko kushindwa kuondoa vumbi kwenye ubongo (kwa kutokusoma vitabu). Cha ajabu, mimi na wewe tuko radhi kuuza 'Biblia' ili kununua simu yenye camera nzuri.
Kumbuka: Katika kila kona, wenye maarifa ndiyo huitawala dunia ilhali wakiwabebesha wajinga mizigo ya uchafu wao. Kwa ajili hiyo, ni jukumu lako mwenyewe kufuta vumbi kichwani ili kujiondosha haraka toka kwenye lindi la ujinga.
- Maundu Mwingizi (Mwanabalagha)