Funua Kawa Mwana Halali Asimame! - Mwanamapinduzi HAMID AMEIR

Funua Kawa Mwana Halali Asimame! - Mwanamapinduzi HAMID AMEIR

Mzenji73

JF-Expert Member
Joined
Jan 10, 2009
Posts
341
Reaction score
92
Funua Kawa Mwana Halali Asimame!

Okt. 24/14

Na Salim Said Salim

Watu husema ukiyajuwa ya wenzako basi elewa wapo wanayoyajua yako kama au zaidi unavyojuwa mwenyewe.
Hali hii ya ulimwengu ndiyo iliopelekea Wahenga kusema: "Funika kombe mwanaharamu apite".

Lakini, zama hubadilika na ndio maana pakaja usemi wa "Msitu mpya na komba wapya". Katika zama za hivi sasa zinazoelezwa kuwa za ukweli na uwazi wapo wanaosema: "Funua kombe mwana wa halali asimame". Huyu anayeitwa mwana halali ni methali tu, bali kinachokusudiwa hapa ni kufungua kijaluba, sanduku, kabati, kasiki au hata lango la chuma ili ukweli ujulikane.

Kwa muda mefu katika miaka ya hivi karibuni, mmoja wa wale wanaoitwa waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Hamid Ameir, amekuwa akijinata sana ju ya mchango wake katika kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Hivi karibuni mzee huyu ameamua, bila ya shaka kwa kushawishiwa, kumuandama mmoja wa wanasiasa wakongwe wa Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo, na kusema kuwa hakushiriki na hahusiki na ukombozi wa Zanzibar, iwe katika kupigania uhuru, au katika kufanyika Mapinduzi.

Ni kweli kuheshimu wazee ni wajibu, lakini ni pale tu ambapo Mzee naye atapokuwa sio tu anaheshimu watu wengine, wadogo na wakubwa na mwenyewe kujiheshimu.

Miongoni mwa njia za ambazo hupelekea mtu kuheshimiwa ni kusema kweli; na pale anapoamua kusema uwongo au kuzua jambo, basi iwe kwa kujifurahisha mwenyewe tu na sio kuipotosha jamii na kuelezea historia isiokuwa na mshiko, kichwa wala miguu.

Kwanza, ningependa kuzungumzia hizo harakati za kupigania uhuru wa Zanzibar kuanzia katikati ya miaka ya 1950 mpaka miaka ya mwanzo ya 1960. Unapopitia kumbukumbu mbali mbali na kuangalia picha, jina la huyu Mzee Hamid Ameir halijititokezi pahala popote pale, tafauti na unavyoliona kila pahala jina la Hassan Nassor Moyo.

Kumbukumbu za simulizi na zile za maandishi zinaonyesha kuwa Mzee Moyo aliuwa mstari wa mbele tokea ujana wake katika chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) na alikuwa muanzilishi wa chama kimoja cha wafanyakazi Visiwani, "Zanzibar and Pemba Federation of Labour" (ZPFL).

Mara kwa mara, Mzee Moyo alikuwa akihutubia mikutano ya ASP, lakini hapana hata siku moja Mzee Hamid Ameir alipopanda kwenye kiriri kuhutubia mkutano wa hadhara wa ASP au chama chochote kile cha kisiasa Visiwani kabla ya Mapinduzi.

Vile vile, Hamid Ameir (kisomo chake kilikuwa na mashaka) alikuwa haandiki makala zozote zile katika gazeti kama walivyokuwa wakifanya viongozi wengine wa ASP, kama Mzee Moyo, Marehemu Jamal Ramadhani Nasibu, Marehmu Abdulla Said Natepe na Marehemu Mtoro Rehani Kingo.

Mzee Moyo alikuwemo katika ujumbe wa ASP uliokwenda Uingereza kwa mazungumzo ya kuipatia Zanzibar uhuru yaliyofanyika Jumba la Lancaster mnamo mwaka 1962 na 1963. Alikuwa mmoja wa washauri wa karibu wa kingozi wa ASP, Mzee Abeid Amani Karume.

Mzee Hamid Ameir, sio tu hakuwemo katika kundi hilo, bali pia hapana kumbukumbu zinazoonyesha kuwahi kushiriki kwake katika mkutano wowote wa ndani wa ASP wakati wa matayarisho ya mazungumzo hayo ya London ya kuipatia uhuru Zanzibar.

Lakini, hata ukipitia kumbukumbu za watu waliokuwa mstari wa mbele kuvamia kambi na vituo vya polisi, kituo cha simu cha Cable and Wireless hapo Mambo Msige (saa Hoteli ya Serena), Magereza, Kituo cha Sauti ya Unguja cha Rahaleo, Uwanja wa Ndege au katika harakati za kuteka maeneo mengine muhimu kufanikisha Mapinduzi, husikii kuwepo kwa mtu aliyeitwa Hamid Ameri.

Kwa mfano, katika watu waliosifika kwa ushujaa wa kuvamia kambi ya Polisi ya Ziwani ni pamoja na Mzee Lumumba ambaye ndiye aliyemleta kutoka Pemba, yule aliyetajika kama kiongozi wa Mainduzi, John Okello, aliyekuwa huko akifanya kazi ya kupasua mawe.

Huyu Mzee Lumumba, ambaye baadaye alikuwa mmoja wa waasisi wa chama cha CUF, alikuwa pamoja na Juma Mussa (Jimmy Ringo) aliyekuja kuuawa kikatili baada ya kufanyika Mapinduzi na mtu mmoja aliyejuulikana kwa jina la Saleh (Mavi ya Mbuzi), ambaye baadaye alikuwa Sheha wa Kikwajuni).

Watu wengi walioshiriki kwa upande mwengine kuvamia kambi kuu ya Jeshi la Polisi ya Ziwani (zamani ilijulikana kama Bomani) usiku wa manane wa kuamkia tarehe 12 Januari, ni kundi liliokuwa pia na askari polisi wastaafu (wengi waliachishwa kazi baada ya kupatikana uhuru) lilioongozwa na Said Idi Bavuai.

Katika kundi hili alikuwemo Ramadhani Haji Faki (aliyekuwa Waziri Kiongozi wakati wa utawala wa Rais wa Pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi).

Kundi jengine lilioingia Ziwani liliongozwa na Aboud Mmasai (Mngazija ambaye alifanana na watu wa jamii ya Kimasai) lakini hakupewa wadhifa wowote wa juu baada ya Mapinduzi.
Katika kundi hili pia waliokuwemo Yussuf Himidi (baba yake Mansour Yussuf Himidi, aliyewahi kuwa waziri katika serikali za Rais Amani Karume (shemeji yake) na Rais Ali Mohamed Shein); Mohammed Abdulla Kaujore, Pili Khamis na Kopa, baba wa mwimbaji taarab maaruf, Khadija Kopa.

Watu walioliongezea nguvu kundi hili liliofanya mashambulizi ya awali waliongozwa na John Okello na hatimaye kuiteka kambi. Hawa ni pamoja na Khamis Darweish, Absalom Engen (Makamu wa Okello) na Juma Abdulla Mabodi, baba yake Naibu Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dk. Abdulla Juma.

Hata tangazo la kwanza la kufanyika mapinduzi lilitolewa na Mdungi Ussi asubuhi ya tarehe 12 Januari, 1964; na katika kundi la waliokuwepo hapo kufanya ulinzi hakuwepo Hamid Ameir.

Mapigano makali yalifanyika wakati wa kutaka kukiteka kituo cha Polisi cha Malindi. Mashambulizi ya kituo hiki yaliongozwa na vijana waliokuwa wamepata mafunzo katika Jangwa la Sinai, nchini Misri na baadaye Cuba.

Lilikuwepo pia kundi liliokuwa linasimamia kuzuwia uporaji kwa kuvunja majumba na maduka katika wiki ya kwanza ya kufanyika Mapinduzi. Miongoni mwa waiokuwa wasimamizi wakuu ni Ahmed Hassan Diria, Khamis Abdulla Ameir na Mohammed Mfaume.

Ni vyema Mzee Hamid Ameir akatueleza alikuwa wapi mapinduzi yalipofanyika na alikuwa katika kundi lipi na kwa nini jina lake halimo katika simulizi zote zinazozungumzia kufanyika kwa Mapinduzi?

Ukiziangalia taarifa mbalimbali utaona kuwa Hamid Ameir ambaye leo anajinata kuwa mongoni mwa wapiganaji walikuwa mstari wa mbele kufanikisha Mapinduzi alilivamia jahazi la Mapinduzi likiwa bandarini limeshatia nanga.

Alifanikiwa kujipenyeza kwa kusaidiwa na wazee wa kwao Donge ambao walikuwa miongoni mwa wasisi wa ASP, kama vile Mzee Daudi Mahmoud, na ndiko kulikopelekea Hamid Ameir kuingizwa katika Baraza la Mapinduzi ili ajipatie ulaji kwa njia rahisi.

Labda mbali ya yote hayo, itakuwa vyema kama Mzee Hamid Ameri siku moja ataeleza aliyoyafanya wakati akiwa mjumbe wa Baraza la Mapnduzi.

Ni vizuri wazee kama hawa waliodakia Mapinduzi na kuonekana ni waasisi na sasa kulipwa fedha za walipo kodi kama wastaafu wakakaa kimya kwani wanapozulia watu uwongo basi waelewe wapo watakaowaeleza wao ukweli ni upi na kwamba wao ndio waongo.

Lakini, lilio muhimu zaidi kwa huyu Mzee kwa vile sasa ameamua kuwa msemaji mzuri wa masuala ya Mapinduzi atueleze anachokijua juu ya mauaji ya wanasiasa wengi mashuhuri wa Zanzibar. Wengi wa watu hawa wanadaiwa kuuawa kwa maelekezo ya ile iliyojulikana kama Kamati ya watu 14 ambayo yeye alikuwa ni mmoja wao.

Mbali ya watu waliouawa, wapo wengi waliosema waliteswa na kufanyiwa vitendo vya kinyama. Akitaka majina ya waliouawa na walioteswa na wanodaiwa kufanya maovu hayo (wengine wapo hai) nitampatia.

Nimesema hizi ni zama za funua kawa mwana wa halali asimame. Nilichofanya ni kufunua kidogo tu hilo kawa na kulifunika ili wakati mwana wa halali amesimama yule wa haramu apite na asionekane.

Sasa ninamuachia huyu Mzee ambaye siku zote husema yeye tu kama anahutubia mhadhara na kupotosha vijana wadogo wasiojua lolote kuhusu Mapinduzi na yaliotokea baada ya hapo atueleze zaidi.

Lakini asijaribuni kuleta ubunifu kwa kutunga hadithi za uwongo na kujipakazia sifa asizostahili na kuwapaka watu wengine , kama Mzee Moyo, matope ambayo labda yalistahili kupakwa yeye (Mzee Hamid) na wengine.

Kama haki inataka ionekane, nipo tayari kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Mzee Hamid Ameir na kumuuliza mambo ambayo yanahitaji maelezo na uafafanuzi. Hapo ndipo vijana wa leo watakapojuwa ipi ni mbichi na ipi ni mbivu na ukweli juu ya mauaji ya watu wengi, hata msikitini, yaliyofanyika baada ya mapinduzi na kuelewa ni nani walihusika.

Nina hakika televisheni inayomilikiwa na serikali ya Zanzibar ambayo humpa nafasi sana Mzee na wengine kutoa hekaya za uwongo na siasa za chuki, haiwezi kuwa na ubavu wa kunipa hata dakika 15 za kumhoji Mzee Hamid Amer.

Nipo tayari kuwa na kipindi kama hicho na Mzee huyu na wataokuwa tayari kumsaidia wakati wowote na umma utajuwa nani anasema kweli. Tuache upumbavu wa kudanganya watu kwani wapo ambao wazee na ndugu zao wamedhulumiwa roho zao bila ya sababu.

Tumeamua kusameheana na kujaribu kusahau yaliopita, lakini wanapotokea watu kupotosha yaliyopita, tunao wajibu wa kuweka mambo sawa ili tusonge mbele. Sio vizuri kuipotosha historia na kuwapaka matope watu wasiostahili kupakwa hata vumbi. Baadhi ya watu wanaofanya upumbavu huu ni hao wasomi uchwara, wengine wakiwa wamekuja Zanzibar wakiwa kwenye mbeleko.

Ninamalizia kwa kumtaka Mzee Hamid Ameir, ambaye kwa mbali anao uhusiano na mababu zangu wa kijiji cha Donge, apumzike na awache kuwalisha vijana wa leo propaganda za uwongo. Tumeshalishana uwongo wa kutosha; sasa basi tena.

Kwa wale wanaomuona Mzee Moyo amekosa uzalendo, wanayo haki ya kusema hivyo, kwa vile kwao wao kuuwa na kutesa watu ndio uzalendo. Tuuombe Mungu awahidi watu hawa.
Kumbukumbu hazina hata chembe ya ushahidi ya sio tu kwa Mzee Moyo (kama kwa Marehemu Mzee Bavai) za kuuwa mtu akiwa madarakani, bali pia hata kumtesa au kumtandika mtu bakora kama walivyofanya wengi wa hao wanaojiita wana-mapinduzi.

Baadhi yao ndio wale waliopewa majina ya Mamba, Sancho, Ba Mkwe na mengine ya watu waliosifika kwa kutisha jamii katika nchi mbali mbali. Ukweli ni kwamba, badala ya kuuwa watu, Mzee Moyo amesaidia sana kunusuru kupotea kwa maisha ya watu kwa kusaidia kuleta Maridhiano ya kisiasa yaliyoepusha umwagaji damu Zanzibar na kupelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kama Mzee Moyo ataweka hadharani mengi anayoyajuwa (tumuombe Mungu astahamili) wengi wataomba ardhi ipasuke wajifukie.

Jamani tukumbuke wasia wa wazee unaosema hivi: "Mnyonge mnyongeni; lakini, haki yake mpeni".

Hapa labda nimalize kwa kuwakumbusha jambo ambalo huwa halizungumzwi; nalo ni kuwa wakati Mzee Moyo alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, tafauti na nafasi hiyo iliposhikwa na Wazanzibari wengine, hapajatokea mauaji ya kutisha nchini.

Tukipitia kumbukumbu, tutaona jinsi viongozi wa Zanzibar waliowahi kushika Wizara ya Mambo ya Ndani walivyofanya manyago na watu kupoteza maisha, ijapokuwa unaweza kusema walikuwa mbali na matukio hayo. Lakini kama viongozi wa wizara hakuna mwengine wa kuwajibika isipokuwa wao.

Yasemwe yatakayosemwa, lakini Mzee Moyo ataingia katika kumbukumbu za historia ya nchi hii kama Mzalendo kindaki-ndaki aliyechukia ubaguzi na kupenda amani mongoni mwa watu wa Zanzibar na Tanzania.

Ipo siku, kama alivyowahi kusema sahiba wangu, Marehemu Ali Nabwa (Mungu amlaze mahali pema - Peponi), ambaye kalamu yake iliwaumiza madikteta na wanaopenda dhuluma, ipo siku itakuwa kweli; na kweli ikidhihiri uwongo utajitenga. Hiyo siku ninaamini haipo mbali.
 
Hujaeleweka mkuu, habari ndefu na haieleweki. Tafadhali summarize ndipo ulete humu jamvini.
 
Hujaeleweka mkuu, habari ndefu na haieleweki. Tafadhali summarize ndipo ulete humu jamvini.

Poor you, im very sory broo, nashindwa kujua nkueleweshe wapi, coz mim nimeelewa sana,.
vumilia pengine atatokea mtu akaweza kukuelewesha.
pili acha uvivu wa kusoma
 
Hujaeleweka mkuu, habari ndefu na haieleweki. Tafadhali summarize ndipo ulete humu jamvini.

Kwa tunaoelewa anazungumzia nini tumemfahamu, pengine hii topic si muafaka kwa wewe basi wacha tu wengine tuendelee.
 
na nyie kina yakhe kila siku mwasema kuhusu mauaj na utesaj hamsem kauliwa na na nan kaua vp nyie
 
Duh! huu mchambo si wa kitoto,huyu amemnyonyoa haswa!
 
Hili jina la Dr. Shein limetumikaje hapa au kipindi hicho alikua mpiganaji?

Huyu Mzee Hamid Ameir sisi wengine hatumjui unaweza kutuwekea picha yake?

Ahsante kwa uchambuz mzuri
 
Hili jina la Dr. Shein limetumikaje hapa au kipindi hicho alikua mpiganaji?

Huyu Mzee Hamid Ameir sisi wengine hatumjui unaweza kutuwekea picha yake?

Ahsante kwa uchambuz mzuri
huyo hapo


MZEESMALLAFARIKI.jpg
 
Back
Top Bottom