FULL TEXT: Hotuba ya KUB, Freeman Mbowe bungeni - Mei 12, 2015

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,070
Hotuba ya KUB Freeman Mbowe bungeni leo

HOTUBA YA KIONGOZI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE.FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KATIKA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99 (9), ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013)
_________________________________

1. UTANGULIZI:
Mheshimiwa Spika,

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunitunza ili niweze kutumikia taifa langu. Napenda kuishukuru familia yangu kwa msaada mkubwa na uvumilivu hasa katika harakati na shughuli zangu za kisiasa.

Mheshimiwa Spika,Napenda kuchukua nafasi hii pia, kuwashukuru watanzania wote kwa ujumla kwa kupokea na kulea harakati za mabadiliko nchini. Shukrani hizi za pekee ziwafikie wenyeviti wenza wa vyama vinavyounda UKAWA , Mhe. Prof Ibrahim Lipumba, Mhe. James Mbatia na Mhe. Dk Emanuel Makaidi. Vilevile, kwa makatibu wakuu viongozi wa UKAWA Mhe. Maalimu Seif Shariff Hamad, Mhe. Wilbroad Slaa, Mhe. Mosena Nyambabe na Mhe. Tozi Matwange. Aidha, shukrani hizi ziende kwa timu ya wataalamu wa UKAWA, viongozi, watendaji, wanachama na wapenzi wa vyama vyetu vinavyounda UKAWA vya NLD, CUF, NCCR-Mageuzi na CHADEMA. Niwatake wanachama na wapenzi wa UKAWA kujipanga, kujituma na kujiandaa kushinda kwa kishindo na kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa Tanganyika na Zanzibar.

Aidha, shukrani za pekee ziende kwa wabunge wote wa Kambi ya Upinzani Bungeni wanaounda UKAWA kwa kazi nzuri ya kutetea na kusimamia maslahi ya wananchi. Na pia kwa watendaji wa Kambi ya Upinzani ambao wamekua msaada mkubwa kwetu na kwa kazi yao nzuri kwa taifa letu.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwashukuru kwa kipekee, wananchi wa Jimbo letu la Hai kwa ushirikiano mkubwa na imani waliyonayo kwangu kama mwakilishi wao. Niliwaahidi kuwatumikia kwa moyo wangu wangu wote na naendelea kuwaahidi kuwa imani yao kwangu haitopotea bure.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuwashukuru kwa kipekee wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Peter Kayanza Pinda, Spika wa Bunge Mhe. Anna Makinda, Naibu Spika Job Ndugai na Katibu wa Bunge Ndugu Dk. Thomas Kashilila pamoja na wafanyakazi wa Bunge kwa ushirikiano mliotupa toka kuanza kwa Bunge la 10, vilevile napenda kuwatakia heri Mhe. Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mhe. Spika Anne Makinda katika maisha mengine nje ya siasa za Bunge kwani walishatangaza kustaafu ubunge.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya shukrani hizo za kipekee napenda kunukuu maneno machache kutoka kwa Nelson Mandela aliyepata kusema; "I learned that courage was not the absence of fear, but the triumph over it. The brave man is not he who does not feel afraid, but he who conquers that fear." "Nimejifunza kwamba ujasiri si kukosekana wa uoga bali ushindi dhidi ya uoga. Mwanadamu jasiri si Yule ambaye hahisi uoga bali Yule anayeshinda uoga" Vilevile Nelson Mandela alipata kusema; "When a man is denied the right to live the life he believes in, he has no choice but to become an outlaw." "Pale Binadamu anaponyimwa kuishi maisha anayoyaamini, huwa hana njia bali kuwa mvunjaji wa Sheria"

2.
MWAKA WA TUMAINI JIPYA Mheshimiwa Spika, Huu ni mwaka ambao nchi yetu itafanya uchaguzi Mkuu wa Kihistoria ambao utakitoa chama ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50 na hivyo kujikuta kimechoka na kukosa mawazo mapya na ya kisasa ya kuendesha na kuendeleza nchi yetu. Ukweli huu mchungu ni vyema ukaanza kuwaandaa kisaikolojia wote walioko kwenye mamlaka kutambua kwamba kubadilisha chama kinachoongoza Taifa siyo jambo geni duniani. Ni fursa ya nchi kutafuta muelekeo mpya wenye kujaza tumaini jipya, fikra mbadala na SHAUKU ya kuondokana na uendeshaji wa kimazoea wa Serikali na maisha ya wananchi wake. Nipende kuwahakikishia wote, hususan walioko madarakani kuwa UKAWA umedhamiria kwa dhati kurejesha utawala bora wenye kuzingatia haki na sheria, usimamizi makini wa rasilimali na tunu za Taifa na umekusudia kujenga Tanzania mpya yenye mshikamano wa kweli, uhuru wa kweli, amani ya kweli na ustawi wa wote bila kubagua kwa misingi ya kiitikadi, dini, kabila, jinsia au rangi kama ilivyo leo.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa mwaka huu kuwa wa uchaguzi Mkuu kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu nitajikita zaidi kwenye eneo hilo. Lengo ni kuweka rekodi sahihi kuwa sisi Kambi ya Upinzani tulionya sana na kwa muda mrefu kuhusu umuhimu wa uwazi na maandalizi shirikishi ya mapema ili kulihakikishia taifa mserereko salama wa mpito, yaani "smooth transition" kutoka awamu ya nne ya Utawala wa nchi yetu kwenda awamu ya tano. Mpito salama ambao utatokana na kuwepo kwa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.

3.
DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA (BVR)

Mheshimiwa Spika,
Tume Taifa ya Uchaguzi imeanza zoezi la kuandikisha upya wapiga kura katika mfumo mpya wa kielectronic ambao unajulikana kama BVR na zoezi hili lilianzia katika mji wa Makambako mkoani Njombe Mwezi Februari 2015 na Sasa linaendelea kwenye baadhi ya Kata za Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa na Mbeya .

3.1 Hujuma za Serikali dhidi ya Tume :


Mheshimiwa Spika ,
Pamoja na kuwa tarehe ya uchaguzi mkuu ilijulikana tangu tulipomaliza uchaguzi mkuu uliopita, Serikali ama kwa makusudi ama kwa kugubikwa na misukumo ya kimaslahi, imeshindwa kukamilisha daftari la kudumu la wapiga kura kwa wakati muafaka. Pamoja na mengine, Ucheleweshaji wa kuandikisha wapiga kura umesababishwa na Tume kutopewa fedha na Serikali kwa wakati muafaka. Mwezi Februari 2013 wakati Rais Kikwete akizindua vitambulisho vya taifa alisema vitambulisho hivyo ndivyo vitakavyotumiwa katika kura ya maoni na uchaguzi mkuu. Hata hivyo Serikali haikufanya uratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Uchaguzi ili taasisi mbili zishirikiane na kukamilisha zoezi hili. NIDA haikupewa fedha za kutosha kukamilisha zoezi la kuandikisha na kutoa vitambulisho vya taifa. Tume ya Uchaguzi ikaanzisha mchakato wa kuandikisha wapiga kura bila kutengewa fedha za kutosha za kununulia vifaa, kuajiri na kuwapa mafunzo wafanyakazi husika, na kutoa elimu kuhusu kujiandikisha kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika,
Hivi sasa serikali inaonekana kuwa na matatizo makubwa ya fedha baada ya wahisani kusitisha kutoa fedha za msaada wa bajeti kwa sababu ya ufisadi wa kutisha wa Tegeta Escrow Account.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na ukweli kuwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi inahitaji Tume kuboreshaDaftari la Kudumu la Wapiga kura angalau mara mbili kati ya uchaguzi mkuu na unaofuata; Kwa makusudi Serikali iliamua kuivunja sheria ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inaona kuwa ,Kitendo hiki kina malengo na nia mbaya ya kutaka kuongezea muda wa utawala wa Rais Kikwete kwa kisingizio kuwa uchaguzi mkuu hauwezi kufanyika kwani daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika kuboreshwa.

3.2 Udhaifu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika BVR.


Mheshimiwa Spika ,
Pamoja na zoezi kuanza kwa kusuasua ni wazi kuwa Tume haina watumishi wa kufanya kazi katika zoezi hili muhimu kwa uhai wa Taifa , pamoja na ushauri wa mshauri Mwelekezi kutoka Kampuni ya IPSITI ya Nchini Marekani na ambayo ripoti iliwasilishwa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwezi Januari 2015 , Mshauri ambaye Tume ilimpa majukumu ya kuwashauri na kumlipa mamilioni ya fedha za walipa kodi na hata alipowashauri Tume kuwa wanahitaji kuwa na zaidi ya watumishi 10,000 kwa ajili ya kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaweza kufanyika kwa ufanisi na kufanikiwa kwa nchi nzima. Mshauri huyo mwelekezi alienda mbele zaidi na kuwaambia Tume kuwa Ni lazima watumishi hao wawe wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu jinsi ya kuweza kutumia mfumo huu mpya wa BVR kuandikisha wapiga kura na hata jinsi ya kutumia mashine zenyewe .

Mheshimiwa Spika,
Jambo la kusikitisha ni kwamba Watumishi wa Tume ambao wameanza kufanya kazi ya kuandikisha wapiga kura wamepatiwa mafunzo kwa muda wa siku moja au mbili tu kabla ya zoezi la kuandikisha wapiga kura kuweza kuanza , kati yao wapo watanzania ambao wamepewa kazi hiyo na hawajawahi kutumia Kompyuta kabisa katika maisha yao na hata hizi mashine ni mara ya kwanza kuonekana na kutumika Nchini mwetu, na hivyo kulifanya zoezi kuwa gumu zaidi kutokana na watumishi kutokupata mafunzo ya kutosha na hivyo kuweza kuwasaidia katika kutumia mashine za BRV na hata wanapoanza kupata uzoefu muda wa kuandikisha unakuwa umeisha ,yaani siku saba. Aidha , baadhi ya Wapiga picha wameshindwa kutimiza majukumu yao kwa wakati kwani wanashindwa kutumia Kamera ambayo wamepewa kwa ufanisi na hivyo kulifanya zoezi kwenda taratibu sana na foleni kuwa ndefu vituoni.

Mheshimiwa Spika,
Tume haisemi kweli kuhusiana na zoezi hili. Mara kadhaa, viongozi wa Tume wamekuwa wakitoa kauli kadhaa zisizotekelezeka na kisha kuzibadilisha bila maelezo yenye mantiki. Tume imeendelea kusisitiza kuwa zoezi hili litaweza kukamilika kwa muda uliopangwa bila kuweka hadharani imani hiyo inatokana na nini ilhali mazingira yote ya kisayansi yanaonyesha kinyume. Ikiwa Tume ina nia ya kuwapa fursa ya kujiandikisha Watanzania wote takribani milioni 24 wenye sifa na haki ya kupiga kura, haiwezekani ikakamilisha mchakato mzima kabla ya kuanza kwa kampeni mwezi wa Agosti 2015 labda pengine miujiza ifanyike.

Mheshimiwa Spika,
Tume haitaweza kuandikisha wapiga kura wote kwa muda wa siku saba ambazo imeweka kwa kila kituo .- Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Lubuva alipokuwa anamkaribisha Waziri Mkuu Pinda kuzindua rasmi uandikishaji wa wapiga kura katika Mji wa Makambako alisema kuwa tarehe 24 /2/2015 waliweza kuandikisha wapiga kura 3,014 katika vituo 55. Yaani kila mashine moja ilikuwa na uwezo wa kuandikisha wastani wa wapiga kura 54 kwa siku, hii maana yake ni kuwa kama tume ikiweza kupata mashine zote 7750 ilizoagiza kwa wakati na kuwa na jumla ya mashine 8000 inaweza kuandikisha wapiga kura 432,000 kwa siku na hivyo kwa siku 7 za ratiba ya tume kwa kutumia mashine zote 8000 wataweza kuandikisha wapiga kura 3,024,000 tu.

Mheshimiwa Spika ,
Ili kuandikisha wapiga Kura 24,000,000 wanaokisiwa, itahitajika wastani wa siku 56 kila mashine kuandikisha kwenye vituo nchi nzima ili kukamilisha zoezi hilo na bila mashine kuharibika. Na hivyo ni ukweli uliowazi kuwa mpaka tarehe ya mwisho ambayo haijajulikana kwani Tume haijasema itaandikisha wapiga kura mpaka lini ili kuwe na muda wa kuhakiki Daftari lenyewe , kwa mwendo huu wa kuandikisha wapiga kura 54 kwa mashine moja kwa siku, lengo la kuandikisha wapiga kura wote 24 milioni halitawezekana kwa muda huu ambao Tume imelitangazia taifa.

Mheshimiwa Spika,
Zoezi hili linaendelea kufanyika licha ya Tume kutokuwa na vifaa vya kutosha kama ambavyo iliomba ipatiwe na serikali BVR kits 10,500 lakini serikali ikawaahidi kuwapatia KITS 8000 na ambazo mpaka leo hazijafika nchini zote kwa kuwa serikali ilichelewesha fedha makusudi na hivyo Mkandarasi akasimamisha uzalishaji wa mashine hizo hadi Serikali ilipomalizia malipo hayo mwezi Machi mwaka huu na hii ni kwa mujibu wa Randama ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo wamesema , nanukuu uk.10 ‘Baada ya kupatikana fedha kidogo kwa ajili ya uendeshaji, zoezi la Uboreshaji limeanza tarehe 23 Februari,2015 katika Mkoa wa Njombe , Halmashauri ya Mji wa Makambako na baadaye mikoa mingine itafuata kulingana na kufika kwa BVR Kits 7,750 zilizobaki.'Mwisho wa kunukuu. Hii ni taarifa ya tume ya April ,2015.

Mheshimiwa Spika , Tume kwenye randama yao wameendelea kueleza kuwa , nanukuu uk.10 'Awali Tume ilipanga kutumia BVR kits zipatazo 10,500 kwa nchi nzima,lakini baadaye zilipunguzwa hadi BVR kits 8,000 baada ya majadiliano na Serikali' Hii maana yake ni kuwa Serikali iliamua makusudi kupunguza BVR kits hizo bila kujali ushauri wa kitaalamu wa Tume. Na hata baada ya kupunguza mashine hizo bado ilishindwa kuzilipia kwa wakati ili kuiwezesha tume kuandikisha wapiga kura kwa mujibu wa kalenda yao jambo ambalo sasa linatishia uhakika wa kuwepo kwa uchaguzi Mkuu hapo Mwezi Octoba.

Mheshimiwa Spika, Tume haijatoa taarifa za kutosha kwa wadau wote kuhusu teknolojia ya BVR, kampuni inayotengeneza mashine zinazotumiwa, kampuni gani iliyopewa tenda ya programu ya kompyuta (software) itakayoendesha na kusimamia daftari la kudumu, taratibu za kuhifadhi kumbukumbu, usafirishaji wa kumbukumbu kutoka vituo vya kuandikisha wapiga kura, mashine za kutambua wapiga kura siku ya uchaguzi na kadhalika.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na tume kukosa mashine hizo imeamua kupunguza siku za kuandikisha wapiga kura kutoka 14 za awali na sasa wanaandikisha kwa siku 7 tu kwa kituo jambo ambalo limeanza kuwa na madhara kwani wapiga kura wengi wanaachwa bila kuandikishwa. Mfano mzuri ni Wilayani Namtumbo ambako mkandarasi aliyepewa jukumu la kubeba vifaa alihamisha bila kujali kuwa kuna wananchi ambao walikuwa kwenye misururu ya foleni vituoni humo.

Mheshimiwa Spika, Tume pia haijatoa taarifa juu ya vituo vya kuandikishia wapiga kura na idadi ya wapiga kura inayotegemea kuandikisha kila kata. Katika zoezi la majaribio la uandikishaji wapiga kura katika Jimbo la Kawe wilaya ya Kinondoni, Tume iliandikisha wapigakura katika kata ya Bunju na Mbweni. Katika kata hizo Tume iliandikisha wapigakura 15,123 na kuvuka lengo iliyojiwekea la wapiga kura 14,312 kwa karibu asilimia 6. Hata hivyo matokeo ya Takwimu za Sensa ya watu ya mwaka 2012 yanaonesha kuwa kata ya Bunju ina wakazi wenye sifa za kuwa wapiga kura 42,227 na Mbweni wapigakura 9,650. Idadi hii haijajumlisha watu waliohamia maeneo hayo baada ya sensa. Walioandikishwa katika kata mbili za Kawe ni chini ya asilimia 30 ya wapigakura wanaostahiki kuandikishwa.

Mheshimiwa Spika,
Siku 7 hazitoshi kuandikisha wapiga kura wote kwa kila kata, na hasa ikizingatiwa kuwa Tume inaandikisha wapiga kura msimu wa masika wakati wananchi wengi wako katika shughuli za kilimo na vituo viko nje hivyo kuathiri utendaji kazi. Kwa hiyo muda wa ziada unahitajika kuwaandikisha. Matatizo yanayojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapiga kura yanaonesha wazi kuwa daftari la wapiga kura halitakamilika ili litumiwe katika zoezi la Uchaguzi Mkuu. Ni vyema Waziri Mkuu na Serikali mkakubali ukweli huu kuwa bila mkakati wa makusudi wa kuiwezesha na kuisimamia Tume ya Taifa ya Uchaguzi , hakuna uchaguzi Octoba.

Mheshimiwa Spika, Kama kuna jambo litawasha nchi hii ni mkakati wowote wa kujaribu kuongeza muda wa kuwepo madarakani Serikali ya awamu ya nne. Chaguzi kwa mujibu wa Katiba siyo jambo la kuchezea hata kidogo. Tume na Serikali zimekuwa zikitoa majibu mepesi tena wakati mwingine ya kejeli kwa maswali magumu. Ni dhahiri, tume imetumika kama "mshirika na msiri" wa Serikali. Tume inajua uchafu na ufisadi mwingi unaogubika uagizaji na uingizaji wa BVR kits lakini imeendelea kudumisha siri hii. Kuhairisha uchaguzi kwa uzembe wa aina hii haikubaliki. Ni vyema Bunge lako likajadili kwa kina ratiba ya uchaguzi mwaka huu na wote waliozembea na kulisababishia Taifa hofu ya kiwango hiki wawajibishwe haraka. Aidha, tume nzima ya uchaguzi ijitafakari kama kweli ina weledi wa kuendelea kuwepo na kusimamia uchaguzi mkuu ujao bila kusababisha machafuko makubwa nchini,

Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ,Tulisema kuwa kura ya maoni haitawezekana kufanyika tarehe 30 mwezi Aprili , lakini serikali na tume hii hii iliendelea kutubeza. Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na hata Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi waliendelea kusisitiza kuwa kura ya maoni ya Katiba pendekezwa itafanyika. Tarehe 30 Aprili kura ya maoni haikufanyika na haijulikani hatma yake. Fedha za walipa kodi zimepotea kwa mabilioni. Hakuna aliyewajibika.... huo ndiyo utawala wa Rais Kikwete. Hii ndiyo CCM.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu kutoka serikali hii ya CCM kwenye mambo yafuatayo; i. Mashine za BVR zitawasili lini nchini kwa ukamilifu wake? ii. Tume itamaliza lini (tarehe) kuwaandikisha Watanzania wote wenye sifa ya kuwa wapiga kura katika Daftari la wapiga kura? iii. Ni lini Watanzania ambao watakuwa wameandikishwa kwenye Daftari la wapiga kura watapata fursa ya kuhakiki Daftari la wapiga kura kwa mujibu wa sharia na zoezi hili litachukua muda gani? iv. Je, Tume itaweza kufanya maandalizi mengine ya kina ya uchaguzi Mkuu na ikizingatiwa kuwa muda wote itakuwa inaendelea kuandikisha wapiga kura? v. Tume itaweka lini hadharani mpango mzima na ratiba za utekelezaji kuelekea uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Octoba 2015 ambapo kwa mujibu wa sharia zimebaki siku pungufu ya 100 kwa kampeni za uchaguzi kuanza.

3.3 Mpango haramu wa Tume: Watanzania 2.9 milioni kutokuandikishwa:

Mheshimiwa Spika, Kutokana na kukosekana kwa muda na vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura wote wenye sifa kwa mfumo wa BVR , Tume imeshaamua kwa makusudi kutokuwaandikisha wapiga kura zaidi ya milioni 2.9 katika zoezi linaloendelea. Hii ni kwa mujibu wa taarifa rasmi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoko kwenye Randama yake. Nanukuu uk.10 ‘Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakadiria kuandikisha wapiga kura 21 milioni kati ya watanzania 23.9 milioni wenye sifa za kuwa wapiga kura, kulingana na Takwimu za Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2012. Makisio ya wapiga kura inazingatia wale ambao hawatajiandikisha kutokana na Voter Apathy'

Mheshimiwa Spika,
Tafsiri ya kuwaacha bila kuwaandikisha Watanzania 2.9 Milioni kama Tume inavyosema kwenye randama yake kwa hoja ya ‘Voter Apathy', maana yake ni sawa na kuacha mikoa zaidi ya sita ya Tanganyika bila kumwandikisha mwananchi hata mmoja. Mikoa hiyo (kwenye mabano ni takwimu za wenye sifa za kuandikishwa kwa mujibu wa sensa ya 2012) Lindi (0.518 milioni), Singida (0.698 milioni), Njombe (0.392 milioni), Katavi (0.271 milioni), Rukwa (0.472 milioni) na Iringa (0.524 milioni).

Mheshimiwa Spika,
Tume inataka kuhalalisha kuacha kuandikisha Watanzania wengi kiasi hicho kwa hoja dhaifu kama hiyo? Kazi ya Tume ni kuwaandikisha Watanzania wote wenye sifa na hivyo basi Tume inatakiwa kuhakikisha kuwa inatoa elimu kwa umma, hamasa na umuhimu wa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la wapiga kura kwa Watanzania na sio kukaa kimya bila kufanya matangazo ya kina ya kuwahamasisha wananchi kama wanavyofanya sasa na kuishia kujificha kwenye kichaka cha ‘Voter Apathy' hali hii haikubaliki hata kidogo.Kambi Rasmi ya Upinzani, tunataka kujua kutoka serikalini Tume imetumia kigezo gani cha kusema kuwa zaidi ya asilimia 12.1 ya Watanzania wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura hawatajiandikisha mwaka huu? Imefanya utafiti huo lini, na ripoti yake iko wapi? Au huu ni mkakati wa makusudi ambao unaoratibiwa na serikali ya CCM na Tume wa kupunguza wapiga kura baada ya Tume kutokupewa vifaa vya kutosha kwa ajili ya kuwaandikisha watu wote wenye sifa? Ama huu ndio mpango mzima wa hujuma ambao unaendana sambamba na kupunguza muda wa kuwaandikisha wapiga kura kutoka siku 14 kama ilivyokuwa imepangwa awali na kuwa siku 7 za sasa ? Aidha, tunaitaka serikali kutoa majibu ya kina imejipanga vipi katika kuwahamasisha, kuwaelimisha na hatimaye kuwaandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura Watanzania wote wenye sifa za kuandikishwa kwa muda wa siku saba ambazo tume imeweka kwa kila kituo?

3.4 Takwimu za Tume ni Utata Mtupu:


Mheshimiwa Spika,
Kwa Mujibu wa Takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kuwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 Watanzania waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 16.4 Milioni na waliojitokeza kupiga kura walikuwa 11.3 milioni, Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 walijiandikisha watanzania 20.1 Milioni na waliopiga kura walikuwa 8.3 Milioni . Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka majibu ya swali hili, Tume inaposema kuwa Mwaka 2015 itaandikisha wapiga kura 21 Milioni , maana yake ni kuwa tangu mwaka 2009 ambapo ndio ilikuwa mara ya mwisho kuandikisha wapiga kura, watanzania ambao umri wao umeongezeka na hivyo kuwa na sifa za kuandikishwa kwenye Daftari ni 0.9 Milioni tu au kuna mchezo mchafu ambao umepangwa kuchezwa na Tume ikishirikiana na Serikali ya CCM? Ama serikali na Tume inataka kusema kuwa tangu 2009 Watanzania ambao walikuwa wamejiandikisha wamefariki dunia na hivyo kufanya idadi ya watu wenye za kujiandikisha kuwa kiasi hicho?

4.
MAANDALIZI YA UCHAGUZI MKUU ,2015.

4.1 Tume haijapewa fedha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na ukweli kuwa muda haupo upande wetu lakini mpaka sasa hakuna maandalizi yoyote ambayo yamefanyika na yenye kuashiria kuwa uchaguzi mkuu unaweza kufanyika mwezi Octoba,2015 kwa mujibu wa Katiba .Ukweli huu umethibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenye randama yao walipoandika, nanukuu uk.13 ‘Kwa upande wa Maandalizi ya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu,2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa'

Mheshimiwa Spika
, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inajiuliza Kama serikali haijaipatia Tume fedha kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, wanategemea miujiza gani kuwa ifikapo Octoba uchaguzi Mkuu utafanyika? Ni lini Zabuni zitatangazwa kwa ajili ya wakandarasi mbalimbali ambao watasambaza vifaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, na tarehe ya kuwapata hao wazabuni ni lini ?

Mheshimiwa Spika,
Wakati Serikali hii ikishindwa kuipatia fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa ajili ya kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Octoba, 2015 ili uweze kufanyika katika mazingira ya amani, haki na utulivu, Serikali hii ya CCM imeamua kuwekeza na kujiandaa kupambana na wananchi wake, hii ni kutokana na ukweli kuwa ,wakati Tume inakosa fedha za kulipia vifaa kwa ajili ya kuandikisha wapiga kura na kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu , tuna taarifa kuwa Serikali imeamua kuagiza zaidi ya magari 777 kwa ajili ya Jeshi la Polisi, kuanzia yale ya Maji ya kuwasha, Doria na shughuli za Ukaguzi katika Mwaka huu wa Fedha.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ,
inajiuliza kwamba hivi ni nini kipaumbele chetu kama taifa kwa sasa? Je, ni kuandaa mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu kwa hali ya haki, amani na utulivu? Au ni kujiandaa kuuvuruga uchaguzi huo? Ndiyo maana tunashuhudia jitihada hizi za kujiandaa kupambana na wananchi wakati uchaguzi Mkuu utakaposhindikana kufanyika kwa sababu ya kukosekana kwa maandalizi thabiti na ya kina ya kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi huo? Na hizo ndio sababu za serikali hii ya CCM kukataa kufanya maandalizi ya kina kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na kuwekeza katika Mapambano?

4.2 Aibu ya Tume na Madeni :

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na Tume ya Uchaguzi kutokupewa fedha kwa ajili ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu na Serikali hii ya CCM , bado Tume wanadaiwa madeni na wakandarasi ambao walisambaza vifaa kwa tume kwenye Chaguzi mbalimbali zilizopita, madeni hayo ya Tume yanathibitishwa na maandishi ya Tume kwenye randama yao uk .13 nanukuu ‘Hata hivyo kuna Wazabuni waliotoa huduma ambao wanatudai fedha kiasi cha USD 8,377,134.56.....' Hizi ni sawa na Shilingi Bilioni 16.754 kwa viwango vya bei ya soko leo kutokana na kudorora kwa shilingi, laiti kama deni hilo lingeweza kulipwa mapema kabla ya Shilingi kudorora na kuporomoka tusingekuwa na deni kubwa kiasi hiki leo hii. Aidha kutokana na Tume kudaiwa kiasi hicho cha fedha wakandarasi wameshindwa kuiamini tume na ndio maana haikopesheki tena na hivyo kushindwa hata kuanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu Octoba 2015, kwa njia ya Mkopo,hawana pa kukopa!

Mheshimiwa Spika,
Ukiangalia Jedwali Na:4 Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mwaka 2015/16 kwenye randama ya Tume utaona kuwa fedha iliyoombwa ni kiasi cha shilingi 192.409 Bilioni, na fedha hizo zimeombwa kwa ajili ya Mishahara 2.144 bilioni, Matumizi mengineyo 2.302 bilioni na kiasi cha shilingi 187.962 bilioni kwa ajili ya uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu.Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inauliza hivi deni la zaidi ya bilioni 16 ambazo tume inadaiwa na wakandarasi hazitalipwa mwaka huu wa Fedha? Na kama zitalipwa zitatoka fungu gani hasa ikizingatiwa kuwa tayari Tume imeshatoa rai kuwa fedha zake ziwekwe kwenye Fungu 61 na sio Mfuko Mkuu wa Hazina ambao ulikuwa ukitumika kama kichaka cha kuficha ukweli katika bajeti zilizopita.

4.3 Fedha za Uendeshaji Uchaguzi Mkuu hazina Mchanganuo:

Mheshimiwa Spika,
Tume ya Taifa ya uchaguzi wameomba kupatiwa kiasi cha shilingi 187.962 Bilioni kwa ajili ya uendeshaji wa Uchaguzi ambao unapaswa kufanyika Octoba ,2015 kwa mujibu wa Katiba yetu, fedha hizi hazina maelezo wala mchanganuo wake kuwa zinaombwa kwa ajili ya kulipia kitu gani hasa , ni Mawakala ,vifaa vya uchaguzi au ni kwa ajili ya kulipia posho kwa wasimamizi wa uchaguzi huo?

Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupatiwa mchanganuo wa kasma 229914 :Uendeshaji wa Uchaguzi Mkuu kiasi cha sh.187,962,160,000 hizi ni fedha kwa ajili ya vitu gani na hasa ikizingatiwa kuwa Tume haijatangaza zabuni kwa ajili ya vifaa vya Uchaguzi Mkuu, wamekokotoa kiwango hicho kutokana na msingi upi? Au wamefanya mazoea ? wamezingatia kiwango cha kuporomoka kwa shilingi na hasa kwa vifaa ambavyo tutalazimika kuagiza kutoka nje ya Nchi ?

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa randama ya Tume imeonyesha kuwa Tume tayari imeshafanyia maboresho sheria na kanuni za uchaguzi, na hiyo ipo uk 12 wa randama , naomba kunukuu ...'imeanza pia kufanya Maboresho ya Sheria na Kanuni za Uchaguzi...' Kambi rasmi ya Upinzani inataka kujua ni lini sheria hizo zitawasilishwa Bungeni? kwani kwa mujibu wa Katiba chombo chenye mamlaka ya Kuboresha ama kubadilisha sheria ni Bunge na sio chombo kingine chochote kile , na hasa ikizingatiwa kuwa hili ni Bunge la Bajeti na la mwisho kabla ya uchaguzi Mkuu Octoba 2015. Maboresho hayo ya sheria yatafanyika wapi na kupitishwa lini ?

Mheshimiwa Spika,
Tume pia imeonyesha kwenye randama yake kuwa kuna mpango wa kupitia upya mipaka na majina ya majimbo ya Uchaguzi , nanukuu randama uk.12 .....'kupitia mipaka na majina ya Majimbo ya Uchaguzi na kuyarekebisha ....' Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu ni majimbo yapi ambayo yatahusika na mpango huu wa Tume na hasa ikizingatiwa kuwa tayari vyama vimeshaanza michakato yake ya ndani ya kutafuta na kuteua wagombea wa nafasi za Udiwani, Ubunge,Uwakilishi na Urais. Ni vyema Tume ikayatangaza mapema Majimbo hayo ili wananchi pamoja na wadau wa uchaguzi (Vyama vya siasa) wakapata muda wa kutosha wa kujiandaa na hasa kuandaa wagombea katika Majimbo hayo.Kambi rasmi ya Upinzani , inakubaliana na rai ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kama ilivyo kwenye randama yake uk.14 nanukuu ‘Fedha kwa ajili ya shughuli za Uchaguzi ziwekwe kwenye Fungu 61 badala ya kuwekwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, ili kuiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kulingana na Ratiba' Kwani ni ukweli uliowazi kuwa Mfuko Mkuu wa Hazina umekuwa kama kichaka cha kuficha mambo na hasa ikizingatiwa kuwa hata bajeti ya mwaka 2014/2015 Kambi rasmi ya Upinzani tulipohoji ziko wapi fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu tuliambiwa kuwa ziko Mfuko Mkuu wa Hazina jambo ambalo halikuwa kweli na ndio maana Tume haijapewa hata senti moja kwa ajili ya Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa octoba 2015 . Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , inaitaka serikali kufuata ushauri wa Tume ya Uchaguzi wa kuhakikisha kuwa haiongezi maeneo ya utawala tunapokaribia Uchaguzi kwani kunaifanya Tume kushindwa kupanga mipango yake katika kuandaa uchaguzi Mkuu .

5. KURA YA MAONI 5.1

Kura ya maoni haipo kwa mujibu wa sheria ;


Mheshimiwa Spika ,
Pamoja na utamaduni wa Serikali hii wa kuvunja sheria zilizotungwa na Bunge lako kuwa ni jambo la kawaida , tumeshuhudia kuvunjwa kwa sheria ya kura ya maoni kwa kiwango ambacho hakivumiliki tena .Hali hiyo imeipelekea hata Tume ya Uchaguzi kushindwa kuendela kuvumilia uvunjwaji huu wa sheria unaofanywa na serikali hii ya CCM na ndio maana sasa wameamua kuuweka ukweli hadharani na kwa sauti kuu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa randama, Tume iliandaa swali la kura ya maoni kama sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 ilivyowataka kufanya tangu Octoba, 2014. Na Tume imesema hivyo kwa mujibu wa nyaraka zake kwa Bunge, naomba kunukuu tena Randama ya Tume ya Uchaguzi uk.12 ‘Tume tayari zimekutana na kuandaa swali la Kura ya Maoni na kulichapisha kwenye gazeti la serikali la tarehe 17 Octoba,2014'..

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 , iliyotungwa na Bunge hili iliweka bayana muda maalum wa kuchapisha swali la kura ya maoni, kutoa elimu kwa umma na siku ya kufanyika kwa kura ya maoni. Kwa masikitiko ni kuwa muda wa kufanya yote hayo kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni umeshapita tayari.

Mheshimiwa Spika, Sasa ni dhahiri na ni ukweli mtupu kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni kuwa , Haiwezekani tena kwa kura ya maoni kufanyika sasa au baadaye bila kwanza sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 kuletwa hapa Bungeni kwa ajili ya kurekebishwa ili kuruhusu kura hiyo ya maoni kufanyika .

5.2 Elimu kwa Umma juu ya kura ya Maoni ni utata mtupu:

Mheshimiwa Spika,
Jukumu la kutoa elimu kwa umma kuhusu kura ya maoni ni jukumu la Tume ya Taifa ya Uchaguzi pamoja na asasi ambazo zimeidhinishwa na Tume kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, na sio jukumu la Serikali .

Mheshimiwa Spika,
Kwa kipindi kirefu sasa tumeshuhudia kwenye baadhi ya vyombo vya habari na hasa Magazeti, Redio na Television wakiendelea na vipindi vya elimu juu ya kura ya maoni na msisistizo mkubwa ni kupiga kura ya ndiyo ya Katiba Pendekezwa , na hata kwenye maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano kwaya ya vyombo vya dola ambayo ilishirikisha Jeshi, Polisi na usalama wa Taifa , na wao kwenye wimbo wao ambao waliimba mbele ya Rais Kikwete waliweka msisitizo wa kupiga kura ya ndiyo kwenye katiba pendekezwa, ilihali hivi ni vyombo vya dola na ambao havipaswi kufanya kazi hiyo ya kushawishi umma kufanya uamuzi ambao wanautaka wao na walioandaa kwaya hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Hatujashangazwa na taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoko kwenye randama yake kuwa haijawahi kupokea fedha kwa ajili ya kuendesha zoezi la kura ya maoni ,na hii ni kutokana na ukweli kuwa kura hiyo ya maoni haiwezekani kufanyika kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, na hii inathibitishwa na randama ya Tume ambao uk 12 wanasema kuwa, naomba kunukuu ‘kwa upande wa maandalizi ya kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu, 2015 Tume hatujapokea fedha hadi sasa' .

Mheshimiwa Spika,
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,inataka kufahamu ni nani anayegharimikia gharama za matangazo hayo na fedha hizo zimetoka kwenye kasma au fungu lipi la bajeti?Je? anayefanya kazi hiyo amesajiliwa na Tume kwa mujibu wa sheria ? Na kama siyo ni kwanini Tume imeendelea kukaa kimya huku sheria ya kura ya maoni ikiendelea kuvunjwa ? Ofisi ya Waziri Mkuu imeshachukua hatua gani mpaka sasa kuzuia uvunjwaji huo wa sheria ya kura ya maoni?

5.3 Sherehe za Muungano wa miaka 51 na Kura ya Maoni ya Katiba :

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, Tunajiuliza , hivi wale waliokuwa kwenye ile kwaya iliyokuwa uwanja wa Taifa na kutambulishwa kuwa ni kutoka vyombo vya dola , bado ni askari wetu na ambao tunategemea kuwa sehemu ya kusimamia haki kama hiyo kura ya maoni itafanyika ? Serikali imeweka utaratibu gani wa kuhakikisha kuwa wale wote ambao waliweka msimamo wao hadharani kuwa kura ya maoni ni lazima kila mwananchi akapige kura ya ndiyo; kama walivyoimba uwanja wa taifa; wanaondolewa kwenye utaratibu mzima wa kuwa sehemu ya wasimamizi wa kura ya maoni? Haki iko wapi kama hawa ndio vyombo vyetu vya dola, ambao wanaopaswa kutokufungamana na upande wowote wa kisiasa kwa mujibu wa sheria ?

5.4 Tume ya Uchaguzi imeweka msimamo kuwa Hakuna kura ya Maoni bila sheria kurekebishwa na Bunge :


Mheshimiwa Spika, Pamoja na madhaifu yote ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi , kuna jambo moja ambalo walau Tume wamekubaliana nasi kama Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni , wananchi, wanaharakati na viongozi wetu wa dini na hasa Shura ya Maimamu na wale wa Kikristo, nalo ni kuhusu 'kutokuwezekana kufanyika kwa kura ya maoni katika wakati huu kutokana nasababu za kuvunjwa na ama kuwa na sheria ambayo haieleweki na haitekelezeki.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa randama ya Tume uk 14, nanukuu kipengele cha 2.6 kuhusu Changamoto , wamesema kuwa ‘Sheria ya kura ya maoni ina maeneo ambayo hayawezi kutekelezeka na baadhi yake kuwa na tafsiri zaidi ya moja .Eneo ambalo linaweza kuleta utata ni Uhesabuji wa Kura ya Maoni na Utangazaji wa Matokeo'

Mheshimiwa Spika,
Tume Imependekeza kuwa ili kura ya maoni iweze kufanyika ni lazima sheria ya kura ya maoni ya mwaka 2013 irekebishwe kwanza na Bunge , kifungu cha 2.7 cha randama, suluhisho la Changamoto uk 14 kinaeleza kuwa ili kura hiyo iweze kufanyika ni lazima ‘Sheria ya Kura ya Maoni ifanyiwe Marekebisho kwenye maeneo ambayo hayatekelezeki au kuwa na tafsiri zaidi ya moja'

Mheshimiwa Spika
, Huu ni ukweli mchungu ambao Bunge hili linapaswa kuuchukua kwani Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, tumekuwa tukilalamika juu ya utaratibu wa Bunge na ambavyo tumekuwa tukitunga sheria zetu mbalimbali hapa Bungeni japo mapendekezo yetu yamekuwa yakitupwa au kutokusikilizwa kutokana na mantiki yake na madhara yake ni haya ya kutunga sheria ambazo hazitekelezeki , mbovu na ni aibu kwenu ambao mara zote mmekuwa mkipiga kura za Ndiyo bila kujali hoja yenyewe , hii ni aibu kubwa kwenu na mmelisababishia taifa aibu kubwa!

Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
, inakubaliana na ukweli huu kuwa kura ya maoni haiwezi kuwepo mwaka huu wa fedha bila kwanza sheria kurekebishwa Bungeni na ndio maana hata kwenye maombi ya fedha yaliyoletwa na Tume katika mwaka huu wa fedha 2015/2016 haikuomba kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya kura ya maoni

5.5 Msimamo wa Tume, hakuna kura ya maoni ni wa Kikatiba na uheshimiwe !

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Katiba yetu ibara ya 74 (7) imeweka wazi kuwa Tume ya Uchaguzi ni idara huru inayojitegemea ,itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa vikao vyake . Kwa mujibu wa Katiba ibara ya 74(11)imeweka wazi kuwa "katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa masharti ya katiba hii,Tume ya Uchaguzi haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya serikali , au maoni ya chama chochote cha siasa" Hivyo basi ni imani ya Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni kuwa , kwa kuwa Tume ya Uchaguzi imeshakaa kwenye Vikao vyake kwa mujibu wa Katiba na kuweka wazi vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2015/16 ambavyo vinapatikana kwenye randama yake uk 15 . Kura ya maoni siyo moja ya vipaumbele vyake kwa mwaka huu wa fedha , Hivyo basi ni imani yetu kuwa viongozi wa serikali na CCM wataheshimu maamuzi haya ya Tume na kamwe hawataiingilia Tume katika kutekeleza vipaumbele vyake kwa mujibu wa Katiba kama ilivyojiwekea katika mwaka huu wa fedha . Hatutaki kuamini kuwa Waziri Mkuu anaweza kuendelea kuwa sehemu ya kuvunja Katiba na kulazimisha kura ya maoni ambayo hata hivyo kwa upande wa Zanzibar hata sheria ya kura ya maoni haijawahi kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la wawakilishi, na hata kama ingepitishwa tunategemea kuwa wananchi wa Zanzibar wafanye kura ya maoni ili kuruhusu kura hiyo kufanyika kwa upande wa Zanzibar kwa Mujibu wa katiba yao kama ilivyorekebishwa mwaka 2010.

6.
MAPITIO YA BAJETI YA SERIKALI MWAKA 2014/15 NA UTEKELEZAJI WAKE. 6.1 FEDHA ZA MIRADI YA MAENDELEO.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa randama za wizara na idara mbalimbali za Serikali ni kuwa Fedha zilizoidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2014/15 zimetolewa chini ya kiwango cha asilimia 40 na maeneo mengine kukosa kabisa fedha kwa ajili ya miradi iliyokuwa imeidhinishiwa bajeti na Bunge hili. Eneo linaloonekana kupokea fedha yote iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya Maendeleo kwa asilimia 100 ni fungu 30 Ofisi ya Rais Ikulu eneo la 'Ukarabati Ikulu' ambapo zilidhinishwa jumla ya shilingi bilioni 10 na zote zilikuwa zimeshatolewa na Hazina na kutumika hadi mwezi Machi, 2015

Mheshimiwa Spika, Maeneo muhimu kama Vile fungu 40 Mahakama ya Tanzania iliyokuwa imeidhinishiwa na Bunge hili jumla ya shilingi bilioni 40 walikuwa hawajapewa hata senti moja na Hazina kwa ajili ya maendeleo hadi mwezi Aprili ,2015 . Maeneo mengine ambayo yaliidhinishiwa fedha na ambayo yalikuwa hayajapokea ni pamoja na fungu 16 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyoidhinishiwa bilioni 5, fungu 41 wizara ya sheria na Katiba ,Fungu 37 Ofisi ya Waziri Mkuu ,Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali iliyoidhinishiwa Bilioni 1.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
inataka kupata majibu ya Kina ni kwanini maeneo muhimu kama Mahakama hayakupatiwa fedha zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili? Hivi kipaumbele chetu ni kukarabati Ikulu kwanza au ni kuziwezesha Mahakama zetu kuwa bora na ili haki iweze kutendeka kwa wananchi wetu? Ni lini serikali itaweka utamaduni wa kuheshimu muhimili huu muhimu wa Dola? Kama bajeti ya mwaka wa fedha ulioisha haikutekelezwa, hivi kuna maana gani kwa Bunge hili kuendelea kukaa hapa kwa gharama za walipa kodi kupitisha Bajeti ambayo mwisho wa siku haitatekelezwa na serikali hii ya CCM? Waziri Mkuu unaisimamia serikali ambayo haiheshimu maamuzi ya Bunge ?

7. BAJETI YA SERIKALI 2015/16 NA HALI YA UCHUMI WA TAIFA.

Mheshimiwa Spika,
Serikali ya CCM ili kuweza kupata fedha ambazo imeweka kwenye bajeti yake imeamua kukopa katika mabenki ya Ndani karibia shilingi Trilioni 6, maana ya hatua hii ya serikali ni kuwa itapunguza mzunguko wa pesa ambazo mabenki ya kibiashara, yangekopesha sekta binafsi kwa ajili ya uzalishaji na biashara ambayo ni muhimu kwa ukuwaji wa uchumi na ajira. Badala yake hizo pesa sasa zinapelekwa serikalini zikatumilke kulipia matumizi ya kawaida yasiyo ya maendeleo. Kwa maneno mengine Serikali imeamua kuiua Sekta binafsi kwa kuweka ushindani wa moja kwa moja kwenye kugombania mikopo kutoka kwenye mabenki ya ndani.

Mheshimiwa Spika ,
Hali hii inatokana na serikali kutumia zaidi ya uwezo /kipato chake! NI hali ambayo itaenda kuongeza deni la ndani na hii inatokana na serikali kushindwa kupata au kukopa fedha toka kwa mabenki na wafadhili wa nje (Development partners) kutokana na mahusiano mabaya na hasa yaliyosababishwa na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi .

Mheshimiwa Spika,
Madhara mengine ya hatua hii ya serikali ni Riba kupanda kwa wakopaji kutoka sekta binafsi maana umepunguza fedha kwenye mabenki na hivyo kufuatia mahitaji, bei za mikopo (riba) zinaweza kupanda japo hata sasa ziko juu sana, na kumekuwa na malalamiko mengi toka sekta binafisi kwamba riba za mikopo kwa ajili ya uzalishaji na uwekezaji ziko juu. Hii itapelekea mambo kuwa magumu zaidi na zaidi kwa wakopaji wa ndani.

Mheshimiwa spika ,
Kwa miaka ya siku za karibuni, nchi yetu imekuwa na utamaduni wa kukopa kutoka mfumo wa kibenki (Benki Kuu na Benki za Biashara) kama njia ya uhakika ya kufidia nakisi ya bajeti yake . Ukopaji huu si tu unadidimiza ukuaji wa sekta za uwekezaji na uzalishaji kama ilivyoelezwa hapo juu, bali pia unaipa Benki Kuu wakati mgumu wa kusimamia ujazi wa fedha katika uchumi. Pia, kupanda kwa riba kutokana na mabenki kuwa na fedha kidogo kunaweza kusababisha sekta zisizokuwa na uwezo wa "ku-break even" kwa muda mfupi hasa sekta ya kilimo na viwanda kudidimia zaidi.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na ‘risk' na gharama ya mabenki kukopesha sekta binafsi ni wazi kuwa mabenki mengi yatapendelea kukopesha serikali kwa kuwa ‘risk' ya kupoteza ni ndogo sana. Na kwa kuwa tofauti kati ya riba zinazotolewa kwenye akiba ni kidogo kuliko zinazotolewa na serikali kwenye uwekezaji wa hati fungani, mabenki mengi kwa kuwa ‘risk averse' zitawekeza kwenye hati fungani za serikali. Haya ni mabenki, mbali na kuwa na riba za juu zimekuwa zikisita kukopesha sekta binafsi kwa kuhofia usalama, hivyo hapa zitapata mteremko wenye gurantee ya usalama.

Mheshimiwa Spika , Kutokana na Serikali kukopa kwenye mabenki binafsi katika riba ya soko (isiyo na unafuu) ili kujalipa baadae, hiyo itapelekea deni la serikali kueindelea kuwa kubwa, jambo ambalo halitakuwa tu msalaba kwa Taifa na Watanzania, bali deni hilo litawaogopesha wawekezaji na wakopeshaji wa nje kama serikali ita-default katika urejeshaji wa mikopo hiyo.

Mheshimiwa Spika, Ni kweli kuwa kwa mujibu wa takwimu, Uchumi unakua na kwa sasa ni takribani asilimia 7, lakini umasikini umebakia pale; inequality imeongezeka na ajira hasa kwa vijana zimepungua sana. Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia inaonyesha umasikini bado uko juu kwani umepungua kidogo sana toka asilimia 34 mwaka 2007 mpaka asilimia 28 mwaka 2012, na umebadilika kwani masikini wengi wa vijijini wanahamia mijini. Hizi takwimu za serikali zikifanyiwa uchambuzi huru hali ya umasikni na inequlity unaweza kuwa mbaya zaidi. Kwa ufupi, matunda yanaliwa na wachache walioko kwenye sekta zinazokua zaidi (utalii, biashara, madini, viwanda, etc.) wale walioko kwenye sekta ya kilimo cha jembe la mkono (75%) inayokua taratibu ukilinganisha na ukuaji wa jumla, wana njia ndefu ya kwenda, umaskini unakithiri!

Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inataka kupata majibu ya kina serikali imejipanga vipi kuondokana na utaratibu huu wa kuwa na bajeti kubwa kwenye makaratasi wakati kiuhalisia haina uwezo wa kuitekeleza bajeti hiyo? Aidha, kuna mkakati gani wa kuhakikisha kuwa inawanusuru wawekezaji wa ndani na riba kubwa kutokana na serikali kuamua kukopa kwenye sekta za ndani za fedha ? Ofisi ya Waziri Mkuu ina mikakati gani ya kukuza ajira na kuwezesha sekta binafsi kuweza kuzalisha?

8.
MAMLAKA YA USTAWISHAJI MAKAO MAKUU-CDA Mheshimiwa Spika, CDA ni mamlaka ambayo ilianzishwa rasmi mwaka 1972 na hivi sasa ina umri wa miaka 43 katika utendaji kazi wake wa jukumu la kwanza lilikuwa ni kuhakikisha kuwa Mji wa DODOMA ardhi yake yote imepimwa.

Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama Fungu 37 Uk. 126 inaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2014/15 mamlaka kupitia Mradi wa Uboreshaji Miji(TSCP) ilitengewa jumla ya Tshs.206,744,000/- kwa ajili ya kujenga uwezo wa Taasisi. Kambi Rasmi ya Upinzani inajiuliza Taasisi yenye miaka 43 na ambayo inakusanya kodi za nyumba na viwanja kwa muda wote huo inapokeaje fedha za kujengewa uwezo?

Mheshimiwa Spika
, CDA kama mamlaka ya kuendeleza makao makuu imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa wakazi wa Mji wa DODOMA, kwa zaidi ya miaka 42 ya uwepo wake, Mamlaka haijakamilisha jukumu lake la kwanza la kupima viwanja maeneo yote ya mji ili kufanya ujenzi ufuate utaratibu utakao wekwa.

Mheshimiwa Spika,
Kabla ya CDA kuanzishwa na baada ya kuanzishwa, wananchi wa Dodoma walikuwa wanaishi katika maeneo yao na wanaendelea kujenga na kuishi kwa sababu hakuna mipaka ya ardhi iliyowekwa na CDA. Lakini CDA wanapotaka kupima eneo Fulani ambalo tayari lina makazi ya wananchi hutoa notice na kuwataka wakaazi wa eneo husika kubomoa nyumba zao wenyewe bila ya fidia.

Mheshimiwa Spika,
Inapotokea wananchi wanaposhindwa kubomoa nyumba hizo kutokana na kukosa mahali pa kwenda ,CDA hubomoa na kuwadai wananchi hao gharama za kubomoa nyumba zao. Maeneo ambayo yamebomolewa nyumba zao na CDA ni pamoja na : Ndejengwa mwaka 2012 ambapo zilibomolewa nyumba 127, Eneo la Itega mwaka 2013, Msangalalee kata ya Makaru mwaka 2014 nyumba 35 n.k.

Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inataka kujua ni lini uonevu huu kwa wananchi wa Dodoma utasitishwa na serikali hii ya CCM? Maana wimbo wa Makao makuu kuwa Dodoma unaonekana umekosa mchezaji na mamlaka hii haionekani ikiwa tayari kufanya jukumu lake la msingi la kuanzishwa kwake .

9. IDARA YA MPIGA CHAPA MKUU WA SERIKALI

Mheshimiwa Spika
, Idara hii ni idara muhimu sana kama ingetumika vyema na kama Serikali ingekuwa na nidhamu ya kutokuingilia utendaji wa Idara ambazo ziko chini yake. Kwani gharama kubwa zinazoingiwa na taasisi na Idara za Serikali katika kuchapa nyaraka mbalimbli ni kubwa mno. Mheshimiwa Spika, Ukiangalia Randama fungu 37 uk.3 kuhusu kupungua kwa maduhuli kuwa ni kutokana uchakavu wa mitambo ya uchapaji ya Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hii ni aibu kubwa kwa Serikali kwani ofisi ambayo ni tegemeo katika kuliingizia Taifa fedha inawezekanaje kushindwa kununua vitendea kazi wakati inazalisha fedha za kutosha?

Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka wa fedha 2014/15 Idara ilitengewa fedha za ndani Tshs.1,000,000,000/- kwa ajili ya Programu ya kuimarisha Idara hii, lakini kwa kuwa Serikali ya CCM haioni umuhimu wa Idara hii hadi mwezi Machi, 2015 hakuna hata senti moja ambayo Idara imepokea kwa ajili ya program tajwa. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka huu wa fedha Idara hii imepangiwa Jumla ya Tshs.500,000,000/- tu. Hoja ni kama mwaka jana ilipangiwa kupatiwa shilingi bilioni moja na sasa thamani ya shilingi imezidi kuporomoka imepangiwa kiasi pungufu ya nusu ya mwaka jana. Mitambo inanunuliwa nje ya nchi, Je fedha hizo si zitakuwa ni kwa ajili ya kufaulishwa kwenda kwenye mipango mingine ambayo si ya kuimarisha Idara hiyo?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kuwa kama kweli ofisi hii ikiimarishwa ni dhahiri kusingekuwa na ulazima wowote kwa Serikali kuingia kwenye Kandarasi za uchapaji wa nyaraka mbalimbali za uchaguzi na nyingine nyingi. Kwani tunaamini katika ushindani wa Zabuni hizo Idara ingeshinda kwa kuwa kuna ruzuku ya Serikali katika uendeshwaji wake. Hili lingewezekana pale tu dhana nzima ya Utawala Bora itakapotekelezwa kwa vitendo na wananchi kuona kwamba utawala bora upo katika utendaji wa Serikali. Mabilioni ya fedha za Walipa kodi yangeokolewa na pia kusingekuwepo na ucheleweshaji wa kazi kwaajili ya watendaji waandamizi wa Serikali kudai kwanza 10% kabla ya kazi kutolewa, jambo linaloturudisha nyuma.

10.
MAPENDEKEZO YETU YA NYUMA NA AHADI ZA SERIKALI 10.1 RERA (Real Estate Regulatory Authority)

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yangu ya mwaka wa fedha 2011/2012 niliitaka serikali kuanzisha chombo kitakachoweka uratibu na usimamizi wa sekta ya majengo makubwa ya biashara inayokuwa kwa kasi kubwa. Mamlaka hii siyo tu itasimamia haki za wapangaji, bali hata mapato ya Serikali na ubora wa majengo haya na huduma zake. Nilipendekeza mamlaka hii ya udhibiti iitwe "Real Estate Regulatory Authority." Tunarudia tena kusisitiza ushauri wetu huu kwani Serikali inapoteza mapato bila sababu ya msingi kwa jeuri na kiburi cha kutokubali ushauri uliotoka upinzani.

10.2
Uundwaji wa Tume Huru za Kimahakama

Mheshimiwa Spika,
Kumbukumbu za taarifa rasmi za Bunge zinaonyesha kwamba katika hotuba yangu ya mwaka 2011/2012 tuliishauri Serikali kuhusu kuunda tume ya kijaji ya uchunguzi wa vifo vya raia. Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walikubali na wakaahidi kutekeleza hilo, lakini toka mwaka huo hadi sasa hakuna chochote kilichotekelezwa na Serikali hii ya CCM.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba Serikali haina dhamira yeyote ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hili ambalo wananchi wamekuwa wakililalamikia kuhusu jamaa zao kuuawa na vyombo vya dola. Ni ukweli uliowazi kwamba tangu kipindi hicho vimeripotiwa vifo kadhaa, majina ya watu waliouawa yanapatikana katika taarifa ya haki za binadamu ya mwaka 2013, uk. 22.

10.3
UNUNUZI WA SAMANI ZILIZOTENGENEZWA NCHINI

Mheshimiwa Spika,
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na msisitizo kuhusu ofisi na taasisi za serikali kununua samani zinazotengenezwa nchini. Ni dhahiri kuwa nchi zilizoendelea hazikufanikiwa kupiga hatua bila kushirikiana na wafanyabiashara wa ndani hivyo samani za ndani zikinunuliwa kwa wingi pato la taifa litaongezeka kwani lita – stimulate sekta nyingine za uchumi ikiwemo ajira. Serikali lazima sasa ieleze ni wizara, taasisi na ofisi zake ngapi zimeanza kutekeleza tamko la Serikali la kuanza kutumia samani zilizozalishwa na viwanda vya ndani ya nchi , pamoja na ahadi za Waziri Mkuu hapa Bungeni?

10.4
Gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali

Mheshimiwa Spika,
Kama Serikali ingekuwa inajali gharama basi ingekuwa inafanyia kazi mapendekezo ya Kambi ya Upinzani tangu mwaka 2011 ambapo tuliishauri kupunguza matumizi ya kawaida na kuongeza fedha katika miradi ya Maendeleo. Aidha, Serikali ingeacha kuendelea kugawa mikoa na Wilaya kwani kwa kufanya hivyo ni kuongeza gharama za uendeshaji wa Serikali. Ni jambo la ajabu kabisa kwamba kwa jinsi Serikali hii isivyojali gharama za uendeshaji wa Serikali, hata Kata ya Mbagala sasa inapendekezwa kuwa Wilaya Mpya!!! Ofisi ya Waziri Mkuu imeshindwa kumshauri Rais juu ya ugawaji wa Mikoa na Wilaya, matokeo yake kila kukicha tunajenga Makao Makuu ya Wilaya na Mikoa wakati fedha hizo tungeweza kuzielekeza kwenye miradi ya Maendeleo na huduma za jamii kama vile shule, hospital , hata Tume ya Uchaguzi imelalamikia jambo hili kuwa linawavuruga sana katika kuweza kupanga mipango yake kama kuweka mipaka ya majimbo na Kata kwa mujibu wa sheria .

10.5
Sherehe za Kitaifa

Mheshimiwa Spika,
maadhimisho hayo yote hufanyika kuanzia ngazi ya Taifa hadi ngazi ya Wilaya kwa kufanya sherehe mbalimbali zinazohusisha viongozi wa kiserikali, na hivyo ni dhahiri matumizi ya kodi za wananchi hutumika. Kambi ya Upinzani inasema kuwa matukio hayo ya kihistoria ni muhimu yaeleweke kwa vizazi vyetu vya sasa na vijavyo.

Mheshimiwa Spika, katika kufikia azma hiyo si lazima tutumie fedha nyingi za walipa kodi wakati Serikali inashindwa kutimiza wajibu wake muhimu zaidi wa kutoa huduma za msingi kwa wananchi wake, kama vile huduma ya maji safi na salama, elimu bora kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu, kupeleka nishati kwenye maeneo ya uzalishaji na kwa Watanzania waishio vijijini n.k.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali badala ya kufanya maadhimisho ya Sherehe hizo zote tuchague ni sherehe zipi zinatoa tija kwa Watanzania na zipi hazileti tija na maadhimisho yake yaweke kwenye kumbukumbu za kihistoria. Hoja yetu hiyo imeungwa mkono katika taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu pamoja na Bajeti ya Matumizi ya kawaida na Mpango wa maendeleo ya Mwaka 2013/14, 2014/15 na Makadirio ya mwaka 2015/16 ya Mkoa wa RUKWA fungu 89 uk. 15 Nanukuu "Kuongezeka kwa vikao, mikutano na makongamano yanayoitishwa na ngazi za Kitaifa kwa maagizo ya kugharamiwa na Mikoa na Halmashauri, ambayo hayapo katika bajeti za mikoa na Halmashauri, katika mazingira ambapo Mikoa na Halmashauri haina fedha za kutolea hata huduma za msingi kwa wananchi" Hiki ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya Taifa .

10.6
Pension kwa Wazee

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani wakati tunawasilisha hotuba yetu mwaka 2011/2012 tulisema yafuatayo, nanukuu:

"
Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa dhana ya hifadhi ya jamii ni pana sana, Kambi ya upinzani tunaitaka serikali kuzingatia pendekezo letu kuweka mfumo utakaowafanya wazee wote kupata pensheni (Universal pension) kila mwezi ili kuwapunguzia wazee wetu hasa waishio vijijini gharama kubwa za maisha". Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika,
Kambi ya Upinzani inasisitiza kuwa pensheni hii ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza kipato kwa wanaoishi vijijini ambako umasikini wa kipato umejikita na kupunguza umasikini kwa kiwango cha takriban asilimia 57.9 kwa wazee walio na umri zaidi ya miaka 65.

11.0 SERIKALI KUPUUZA NA KULIDANGANYA BUNGE


Mheshimiwa Spika, Taifa hili limekuwa mhanga wa mara kwa mara wa uzembe au kudanganywa na hata kupuuzwa kwa maazimio ya Bunge, ambalo kikatiba, ndilo lenye wajibu wa kuisimamia Serikali. Kupuuzwa huku kwa Bunge, kunadhalilisha uwepo wa taasisi hii nyeti ya Taifa, kunaondoa uwajibikaji wa Viongozi na watumishi wa Serikali na hatimaye kunalisababishia Taifa hasara kubwa siyo tu kiuchumi katika maeneo yanayohusu musuala ya kiuchumi, bali pia katika upatikanaji haki katika Taifa.

Mheshimiwa Spika,
Wakati Dunia inajua vilivyo kwamba Bunge lilifanya kazi yake katika kuisimamia serikali, juu ya kashfa ya Operesheni Tokomeza na mwishowe kuishia kwa mawaziri wanne kuachia madaraka kwa kuwajibika kisiasa, leo serikali inarudi kwa mlango wa nyuma na kudai eti hakukuwa na tatizo. Aidha, Serikali imeendelea kufanya mkakati wa makusudi wa kuficha uovu na uzembe kwa kusafisha viongozi katika masuala yote yanayohusu umma hususan pale viongozi wa serikali na familia zao wanapokuwa ni wahusika wakuu katika kashfa husika. Kwa mfano, Serikali imeshindwa hadi leo kuweka hadharani ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais ya majaji watatu; Jaji Hamisi Msumi (Balozi) akiwa mwenyekiti; Jaji Stephen Ernest na Jaji Vincent Kitubio ikiwa imekabidhi ripoti yake serikalini na badala yake kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue. Kwa mfano, Balozi Sefue anasema mawaziri wote wanne waliojiuzulu mwaka 2013 kwa sakata la Operesheni Tokomeza hawana hatia. Yaani serikali inataka hata kusema kwamba hata kule viongozi hao kuchukua wajibu wa kisiasa kuwajibika ni kinyume cha utawala bora. Wakati ikisema hivyo, serikali hii ya CCM inakubali kwamba kuna watu waliuawa kwa makosa, idadi ya ilikuwa inaonyesha ni watu 15 ingawa Tume inathibitisha vifo tisa; Tume inakiri kwamba kuna watu walidhalilishwa; kuna watu waliharibiwa nyuma na mali zao kama mifugo kupigwa risasi na kila aina ya uonevu. Serikali imekubali kulipa fidia kwa wote waliokumbwa na madhila haya. Katika mazingira haya uwajibikaji wa kisiasa unakuwaje kosa? Serikali inasafisha vipi waliowajibika kisiasa?

Mheshimiwa Spika,
Kwa nini hatujifunzi kwa Mzee wetu, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, alipowajibika miaka ya sabini kwa sababu ya madhila waliotendewa wananchi na askari ingawa yeye mwenyewe hakushiriki. Serikali hii kwa nini inaogopa na kukwepa uwajibikaji? Kama serikali hii inaamini katika uwajibikaji na uwazi iweke hadharani ripoiti ya Majaji watatu kuhusu kashfa ya Operesheni Tokomeza ili wananchi waisome na kujiridhisha vinginevyo serikali hii inaendeleza tabia ile ile ya kukwepa kuwajibishwa na Bunge kama ilivyokuwa kwenye maazimio ya Operesheni Tokomeza.

Mheshimiwa Spika,
Juhudi za serikali za kutaka kusafisha na kufunika kashfa zake pia kumethibitika wiki iliyopita tu baada ya Katibu Mkuu Kiongozi tena kujaribu kuwasafisha wahusika wa sakata la Tegeta Escrow. Watanzania wanajua na dunia inajua kwamba kama kuna wizi wa mchana kweupe umefanyiwa nchi hii ni kashfa ya Tegeta Escrow, watumishi wa umma wamehongwa mamilioni ya fedha, majina yametajwa; aliyekuwa Katibu Mkuu Nishati na Madini, Eliackim Maswi na Waziri wake, Profesa Sospeter Muhongo, walionyesha ni kwa jinsi gani walishindwa kuisaidia serikali na nchi isiibiwe kwenye kashfa hii, lakini pamoja na maazimio ya Bunge kuwataja kwa ushahidi jinsi walivyoshindwa kutekeleza majukumu yao, serikali imekuwa hailali eti ikitafuta njia ya kuwasafisha. Hii ni serikali pekee duniani inayokasirika Bunge likifanya kazi yake sawa sawa ya kuisimamia ndiyo maana mara nyingi imegeuka na kutafuta njia ya kufunika madudu ambayo siyo tu yameiaibisha sana, bali yamegharimu kodi nyingi za wananchi. Serikali inajua kwamba utekelezaji wa bajeti ya serikali inayomalizika ya mwaka 2014/15 umekwamishwa sana na kashfa ya Tegeta Escrow baada ya nchi wafadhili kuzuia kutoa fedha za kuchangia fungu la maendeleo kutokana na tabia ya serikali kufunika kombe mwanaharamu apite kwenye kashfa hii. Tunataka serikali iseme kwamba inapolinda na kubeba wahusika wa kashfa hizi wanataka kuwasaidia wananchi au viongozi wameamua kujiunga dhidi ya wananchi wao? Serikali inajua kuwa kashfa ya Escrow ina mizizi katika kashfa ya IPTL iliyoanza mwaka 1994 ndani ya Wizara ya Nishati na Madini Rais Jakaya Kikwete akiwa waziri, ikaidhinishwa mwaka 1995 Rais Jakaya Kikwete akiwa Waziri wa Fedha na sasa inafumuka katika sakata hili la Escrow na kuiparaganyisha serikali Rais Kikwete akiwa madarakani. Ni kwa nini mambo haya yanatokea na serikali inaendelea kuyabeba na kusafisha uoza huu? Ni kwa faida ya nani?

Mheshimiwa Spika,
Kamato Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mhe. Christopher Ole Sendeka ilitoa mapendekezo muhimu na mazuri wa namna ya kukabiliana na kutatua migogoro yo muda mrefu ya Wakulima na Wafugaji. Hadi sasa Serikali haijaeleza kinagaubaga imejipanga vipi kutekeleza maazimio haya ya Bunge, lakini tunashuhudia wakulima na wafugaji wakiendelea kupambana na kuharibiana mali na hata kuuana,

Mheshimiwa Spika,
Katika mlolongo huu wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi na vita vya kisiasa ndani ya CCM na serikali yake kwa gharama ya Taifa, taifa hili sasa linadaiwa Sh. bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris. Serikali haijataka kuliweka jambo hili wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hili kuwa la usiri mkubwa. Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu Taifa mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond. Serikali isimame sasa na ilieleze Taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na serikali katika kashfa hii?

Mheshimiwa Spika,
Mapambano ya mitandao ndani ya serikali ya CCM na minyukano ya kupigania maslahi na ulaji ndani ya mikataba mbalimbali ya miradi ya umma ikiongozwa na walio karibu na Watawala na familia zao imeota mizizi katika serikali hii.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kujua kwamba serikali hii ya CCM ambayo imefikia mwisho wake ni kwa nini inawaachia Watanzania madeni makubwa hivi? Je, kashfa hizo zote za serikali kushindwa kuwajibika, kutafuta visingizio vya kufunika madhambi yake, ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo wananchi waliahidiwa miaka 10 iliyopita? Nini kauli ya serikali juu ya tabia hii ya kuwabebesha wananchi mizigo ya madeni huku serikali hiyo hiyo ikijitahidi kwa nguvu zake zote kuwasafisha viongozi walioitumbukiza nchi kwenye madhila haya? Ni jambo la kumshukuru Mungu kuwa sasa hatimaye utawala wa CCM unakaribia ukingoni na ni rai yangu kwa Watanzania wote waonyeshe hasira yao ya kuibiwa, kudhalilishwa na hata kufanywa mafukara kwa kikinyima chama hiki cha zamani kilichogawana rasilimali za Taifa hili kwa misingi ya kifisadi kwa muda mrefu.

TUKUBALIANE KWA PAMOJA KUWA NI KWA MASLAHI YA TAIFA LETU NA VIZAZI VIJAVYO KUIONDOA CCM MADARAKANI SASA KWANI KASI YA UKWAPUAJI INAZIDI KUSHIKA KASI. Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naomba kuwasilisha.
……………………………………

Freeman Aikaeli Mbowe (MB)

KIONGOZI WA UPINZANI BUNGENI (KUB)

12 Mei, 2015
 
Hotuba ndeeefu,lakini posho mnakubali kujiongezea,so sad,mil 230 duh na upinzani unacheka tu bungeni,kafulila kaka yangu kweli pesa mwanaharamu
 
Mimi sijawahi kuona hotuba yote mtu analalamika tu sijui anamlalamikia nani sasa kwani hana ufumbuzi wa jambo hata moja wala mpango wowote hana.
 
Mimi sijawahi kuona hotuba yote mtu analalamika tu sijui anamlalamikia nani sasa kwani hana ufumbuzi wa jambo hata moja wala mpango wowote hana.
Mkuu, hakuna kazi rahisi hapa duniani zaidi ya kulalamika. Kwa division Zero ya Mbowe usitegemee akaja na cha maana. Yoote aliyoongea kuhusu tume ya uchaguzi Jaji Lubuva alijibu jana
 
Hotuba ya malalamiko.

2. MWAKA WA TUMAINI JIPYA

Mheshimiwa Spika, Huu ni mwaka ambao nchi yetu itafanya uchaguzi Mkuu wa Kihistoria ambao utakitoa chama ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50 na hivyo kujikuta kimechoka na kukosa mawazo mapya na ya kisasa ya kuendesha na kuendeleza nchi yetu. Ukweli huu mchungu ni vyema ukaanza kuwaandaa kisaikolojia wote walioko kwenye mamlaka kutambua kwamba kubadilisha chama kinachoongoza Taifa siyo jambo geni duniani.

Ni fursa ya nchi kutafuta muelekeo mpya wenye kujaza tumaini jipya, fikra mbadala na SHAUKU ya kuondokana na uendeshaji wa kimazoea wa Serikali na maisha ya wananchi wake.
Nipende kuwahakikishia wote, hususan walioko madarakani kuwa UKAWA umedhamiria kwa dhati kurejesha utawala bora wenye kuzingatia haki na sheria, usimamizi makini wa rasilimali na tunu za Taifa na umekusudia kujenga Tanzania mpya yenye mshikamano wa kweli, uhuru wa kweli, amani ya kweli na ustawi wa wote bila kubagua kwa misingi ya kiitikadi, dini, kabila, jinsia au rangi kama ilivyo leo.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa mwaka huu kuwa wa uchaguzi Mkuu kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu nitajikita zaidi kwenye eneo hilo. Lengo ni kuweka rekodi sahihi kuwa sisi Kambi ya Upinzani tulionya sana na kwa muda mrefu kuhusu umuhimu wa uwazi na maandalizi shirikishi ya mapema ili kulihakikishia taifa mserereko salama wa mpito, yaani "smooth transition" kutoka awamu ya nne ya Utawala wa nchi yetu kwenda awamu ya tano. Mpito salama ambao utatokana na kuwepo kwa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.
 
Wachoù hawa

Serikali ya wachovu hawa. Wachovu wameshindwa kuendesha kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa kama ambavyo UKAWA walionya mapema.

Serikali ya wachovu hadi sasa imeshindwa kuipatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi fedha za uchaguzi mkuu.
 
Mkuu, hakuna kazi rahisi hapa duniani zaidi ya kulalamika. Kwa division Zero ya Mbowe usitegemee akaja na cha maana. Yoote aliyoongea kuhusu tume ya uchaguzi Jaji Lubuva alijibu jana

Simple. Tuwekee majibu YOTE ya Jaji Lubuva kwa hoja za KUB Mbowe. Mnawaya waya sana.
 
2. MWAKA WA TUMAINI JIPYA

Mheshimiwa Spika, Huu ni mwaka ambao nchi yetu itafanya uchaguzi Mkuu wa Kihistoria ambao utakitoa chama ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 50 na hivyo kujikuta kimechoka na kukosa mawazo mapya na ya kisasa ya kuendesha na kuendeleza nchi yetu. Ukweli huu mchungu ni vyema ukaanza kuwaandaa kisaikolojia wote walioko kwenye mamlaka kutambua kwamba kubadilisha chama kinachoongoza Taifa siyo jambo geni duniani.

Ni fursa ya nchi kutafuta muelekeo mpya wenye kujaza tumaini jipya, fikra mbadala na SHAUKU ya kuondokana na uendeshaji wa kimazoea wa Serikali na maisha ya wananchi wake.
Nipende kuwahakikishia wote, hususan walioko madarakani kuwa UKAWA umedhamiria kwa dhati kurejesha utawala bora wenye kuzingatia haki na sheria, usimamizi makini wa rasilimali na tunu za Taifa na umekusudia kujenga Tanzania mpya yenye mshikamano wa kweli, uhuru wa kweli, amani ya kweli na ustawi wa wote bila kubagua kwa misingi ya kiitikadi, dini, kabila, jinsia au rangi kama ilivyo leo.

Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa mwaka huu kuwa wa uchaguzi Mkuu kwa mujibu wa katiba ya nchi yetu nitajikita zaidi kwenye eneo hilo. Lengo ni kuweka rekodi sahihi kuwa sisi Kambi ya Upinzani tulionya sana na kwa muda mrefu kuhusu umuhimu wa uwazi na maandalizi shirikishi ya mapema ili kulihakikishia taifa mserereko salama wa mpito, yaani "smooth transition" kutoka awamu ya nne ya Utawala wa nchi yetu kwenda awamu ya tano. Mpito salama ambao utatokana na kuwepo kwa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.
Kwani kuna chama cha siasa kinachoitwa UKAWA? Mtaishia kuweweseka tu mwaka huu. CCM imejipanga ipasavyo. Wapinzani mtaishia kununa tu
 
Mimi sijawahi kuona hotuba yote mtu analalamika tu sijui anamlalamikia nani sasa kwani hana ufumbuzi wa jambo hata moja wala mpango wowote hana.

TUKUBALIANE KWA PAMOJA KUWA NI KWA MASLAHI YA TAIFA LETU NA VIZAZI VIJAVYO KUIONDOA CCM MADARAKANI SASA KWANI KASI YA UKWAPUAJI INAZIDI KUSHIKA KASI.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni naomba kuwasilisha.
 

Attachments

  • HOTUBA YA KIONGOZI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MHE.FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) .pdf
    373.3 KB · Views: 724

Similar Discussions

Back
Top Bottom