Fahamu upimaji wa Virusi vya Corona Maabara

Bonge La Afya

Member
Dec 19, 2016
31
71
COVID-19.jpg

Na Festo Donald Ngadaya
Twitter, Instagram and Facebook @FestoNgadaya

Mwezi wa kwanza mwaka huu shirika la afya la dunia (WHO) lilitanganza covid-19 kama janga la kidunia (global pandemic). Toka hapo kumekuwa na miongozo tofauti tofauti ya upimaji wa virusi vya corona maabara. Covid19 ni kifupi cha Coronavirus disease of 2019 ikiwa na maana ugonjwa wa kirusi cha corona uliogunduliwa mwaka 2019. Virusi vya corona sio virusi vipya kwani vilikuwepo tangu mwanzo, aina hii mpya iligundulika mwaka 2019 huko wuhan china na kupewa jina SARS-cov 2 ikiwa na maana Severe Acute Respiratory Infection – coronavirus2

Upimaji wa corona maabara unahusisha njia mbalimbali ambazo hutumika kutambua uwepo wa kirusi katika mwili wa binadamu. Mtaalamu atahitaji kuchukua sampuli sahihi kulingana na kipimo anachotaka kutumia kisha kuichakata maabara na kutoa majibu. Vipimo vya virusi vya corona vimegawanywa katika makundi makuu mawili, moja ni upimaji wa virusi kwa kuangalia maambukizi ya sasa (viral test for current infection), pili ni upimaji kwa kuangalia kinga za mwili ambazo huashiria uwepo wa virusi kwa muda uliopita (antibody test for the past presence of the virus).

Kama nilivyosema upimaji wa virusi vya corona maabara umegawanywa katika makundi wakuu mawili:
· Kuangalia kama mtu amewahi kupata maambukizi ya corona (maambukizi ya zamani).
· Kupima maambukizi ya sasa.

1. Kuangalia maambukizi ya zamani
Kama inavyotokea kwa wadudu wengine, Kirusi cha corona kinapoingia mwilini mwili hutengeneza askari ili kupambana na mgeni huyu ambaye mwili haumtambui kwa muda ule. Askari hawa kitaalamu wanaitwa antibodies. Antibodies huwa na sifa ya kuwa maalumu (specific) kwa mdudu husika hii inatokana na kuwa mwili hutengeneza antibody kutokana na mdudu aliyeingia kipindi hicho ndio maana mtu mmoja anaweza kuwa na antibody za malaria huku upande mwingine ana antibody za virusi vya ukimwi ni mifumo ambayo haiingiliani.

Ufanyaji kazi wa kipimo hiki ni kama vipimo vingine vya haraka (serological rapid tests) vinavyofanyika, huangalia na kukamata hizi antibodies zilizotengenezwa mwilini baada ya kirusi kuingia. Kama nilivyosema mwanzo, mwili hutengeneza antibody pale tu unapogundua kirusi kimeingia mwilini, hii ina maana mwili usingetengeneza antibody hizi kama hiki kirusi kisingeingia mwilini, sasa kipimo hiki kimetengenezewa uwezo wa kuzitambua hizi antibody na kuonesha alama ya mstari (positive) kuashiria antibodies zipo.

Kinaitwa kipimo cha kuangalia maambukizi yaliyopita sababu antibody sio mdudu bali ni kinga ya mwili inayotokana na kuingiliwa na mdudu, na mwili ulivyo hata kama mdudu huyu ataondoka kinga zitaendelea kuonekana kwa siku kadhaa ili kuhakikisha hakuna mdudu kabisa kwaiyo ukipima ndani ya siku ambazo kinga bado zipo kwenye mzunguko kwa kutumia kipimo hiki bado utaonekana una ugonjwa. Mwili wa binadamu unapopata maambukizi ya virusi vya corona huchukua wiki moja mpaka tatu ili kutengeneza antibody hizi (IgM na IgG) mwilini, Hii ina maana unaweza kuwa na ugonjwa ila kabla ya hizi siku za utengenezaji wa kinga kukamilika ukipimwa kwa kipimo hiki utaonesha huna ugonjwa.

Ndio maana kinaitwa kipimo cha kuangalia maambukizi ya zamani. Inabidi mtu awe ameugua kwa muda, atengeneze kinga ndio uweze kupima kuangalia uwepo wa virusi vya corona, Hata kama mtu ameugua na kupona kwa siku kadhaa (mpaka siku 28) bado kinga hizi zitaendelea kuonekana katika mzunguko. Kipimo hiki kinatumiwa katika upimaji wa watu wengi (mass screening) na sampuli ya damu ndio hutumika. Damu inachukuliwa kisha inawekwa kwenye kipimo cha haraka (rapid test) kama inavyofanyika kwa ukimwi na malaria. Baada ya muda majibu yanatoka.

2. Kuangalia maambukizi ya sasa
Hii ni kundi la pili la upimaji wa virusi vya corona na hapa tunatumia mashine aina ya RT-PCR (Reverse Transcription – Polymerase Chain Reaction), Mashine hii ina uwezo wa kuangalia maambukizi ya sasa kwa sababu inapima uwepo wa virusi katika mwili wa binadamu. PCR imebaki kuwa kipimo cha kuaminika kitaalamu inaitwa confirmatory test ikiwa na maana licha ya mgonjwa kupima kipimo cha kwanza cha haraka (rapid test) hiki ndio kipimo kitakacho tuhakikishia kuwa ni kweli huyu mgonjwa anaumwa au haumwi.

Sifa ya kirusi ni kuwa na RNA na sio DNA, hivyo hatua ya kwanza ya PCR ni kubadilisha RNA iliyo ndani ya kirusi kuwa DNA katika utaratibu unaoitwa RT au Reverse Transcription, Baada ya kubadilisha RNA kuwa DNA mashine hii hukuza na kuzalisha nakala nyingi za hii DNA ili kumuwezesha mtaalamu kusoma kirusi hiki na kukitambua.

Kama unavyoona hakuna namna mashine hii inaweza kukosa kirusi ikiwa kweli kipo katika mwili wa binadamu kwani inahusisha vinasaba (DNA). Sampuli kama mate, maji maji katika njia ya pua na koo (nasal and throat swab) au makohozi hutumika katika upimaji wa virusi vya corona aina ya SARS-CoV-2

Hitimisho:
Tutasema mgonjwa ana ugonjwa wa corona endapo vipimo vyote viwili vitatumika (Atapiwa kipimo cha awali (Antibody test) na kuhakikiwa na kipimo cha pili - PCR). Kuna sababu kadhaa ambazo husababisha kupata majibu ambayo sio sahihi huku sababu kubwa ni sampuli kutokuwa sahihi au kutokuwa na ubora, kuwahi au kuchelewa kukusanya sampuli, usafirishaji mbovu au endapo mtu akiwa ametumia dawa kabla ya kupima. Matumizi ya sampuli sahihi ni muhimu katika ugunduzi wa ugonjwa huu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom