Habari wataalam,
Nataka nijenge nyumba ndogo kwa mjengo wa stail ya ghorofa moja yaani floor moja kwa juu, kutokana taratibu za nchi na vibali vya ujenzi.
Naomba kwa anaejua hatua za kufanya ili kupata vibali na gharama za kupata hivo vibali, sitaki kujenga kienyeji nataka kufuata utaratibu ili wasije kuniandama.
Note: Eneo halijapimwa, ni squater tu.
BAADHI YA MASWALI YA WADAU WENGINE
Habarini wote wadau wa JF natumai mpo poa.
Dhumuni langu ni kuomba kufahamishwa vigezo na masharti ya kupata kibali cha ujenzi Wilaya ya Kigamboni, maana mimi ni mgeni kabisa kwenye masuala haya sasa naambiwa sasa hivi hakuna kujenga kiholela mpaka fundi mwenyewe akanikatalia akasema nifuate kibali la sivyo wanakuja kuwadaka mafundi unapigwa faini ya kutosha.
Wadau wenye kujua hili anipe muongozo kidogo.
======
Salaam wana jukwaa, nina kiwanja maeneo ya Mbweni nataka nianze ujenzi mdogo mdogo nyumba ya kuishi.
Kabla sijaanza chochote nimekuja humu jukwaani kuomba ufafanuzi jinsi ya kupata KIBALI CHA UJENZI.
======
Habarini za jioni,
Hapa nilipo nimechanganyikiwa kwa kweli. Mimi ni mkazi wa Kisewe-Temeke. Nimerudi mihangaikoni nimekuta barua ya kudaiwa kibali cha ujenzi,niliponunua kiwanja nilijaribu kuuliza serikali za mitaa kama kuna utaratibu wa kua na kibali cha ujenzi kabla hujajenga wakaniambia utaratibu huo hakuna; nimejenga nimehamia mwaka huu January, leo nakuta barua niende Manispaa tena kesho bila kukosa.
Kiukweli nimevurugika kichwa ukizingatia hali zenyewe hizi zilivyo ngumu. Naomba nifahamishwe japo Mukhtasari nijiandae kukabiliana na yapi, maana sielewi elewi kwa kweli.
Sent using Jamii Forums mobile app
======
Habari wana JF,
Kuna ishu imejitokeza sasa hivi mkoa wa Njombe kuhusu vibali vya ujenzi. Wiki hii wanapita watu wa ardhi mtaa kwa mtaa wakikagua nyumba.Wakikuta nyumba haijaisha, mfano bado kuweka vioo, au bado plasta, hata kama umeweka vioo baadhi ya madirisha, na hata kama unaishi humo zaidi ya miaka mitatu, wanafunga utepe, no kuendeleza finishing yako. Na wakikuta nyumba ya tofali mbichi, wanakwambia bomoa au uza kiwanja kwa wenye uwezo wa kujenga nyumba ya kisasa.
Kwa wanaojua sheria za ujenzi, watusaidie kibali ni kwa sifa ipi ya ujenzi?
======
Huku mtaani kwa sasa kuna hii changamoto ya kuandikiwa maandishi haya kwenye kuta za nyumba nyingi zinazoendekea kujengwa.
"SIMAMISHA UJENZI, FIKA OFISI YA ARDHI NA VIBALI VYAKO".
Yasemekana ni kutokana na kujenga bila kibali cha ujenzi. Tatizo ni kwamba utaratibu wa kupata hicho kibali una konakona nyingi sana na upigaji ndani yake.
Kupata ramani tu ya architect sio chini ya 100,000/=
Hapo bado kulipia kibali chenyewe
Bado injinia anayeipitisha hajaomba chochote
Kwa kifupi masikini tunaojenga kwa kuungaunga, hizi konakona ndiyo zinatuumiza zaidi. Mnatumia mbinu mbadala ipi kukabiliana na hili kwa mnaojenga maeneo ya mjini?
======
Habarini wote wadau wa JF, natumai mpo poa.
Dhumuni langu ni kuomba kufahamishwa vigezo na masharti ya kupata kibali cha ujenzi Wilaya ya Kigamboni, maana mimi ni mgeni kabisa kwenye masuala haya sasa naambiwa sasa hivi hakuna kujenga kiholela mpaka fundi mwenyewe akanikatalia akasema nifuate kibali la sivyo wanakuja kuwadaka mafundi unapigwa faini ya kutosha.
Wadau wenye kujua hili anipe muongozo kidogo.
BAADHI YA MAJIBU YA WADAU
KIBALI (BUILDING PERMIT) KABLA YA KUANZA UJENZI
Kibali cha ujenzi (Building permit), ni moja ya kanuni muhimu sana ya upangaji wa miji nchini Tanzania. kila anaehitaji kujenga anapaswa kufuata kanuni za kibali cha ujenzi atakachopewa, mara nyingi kwa mujibu wa sheria kibali cha ujenzi hutolewa na mamlaka za serikali ambazo ni halmashauri kupitia idara ya mipango miji na mazingira.
Kulingana na sheria ya ujenzi wa majengo mijini Na 101 ya mwaka 2009 si ruhusa kwa mtu yeyote kujenga au kuanza kujenga jengo bila ya kuwa na;
- Uhalali wa umiliki wa ardhi mahali unapojenga.
- Kibali cha ujenzi kutoka mamlaka husika.
1. UMUHIMU WA KIBALI CHA UJENZI
- Kutimiza matakwa ya kanuni za ujenzi mijini.
- Kuwezesha kujenga majengo ya nyumba kama yaliyoelekezwa katika mipango miji ya sehemu husika.
- Kudhibiti ujenzi holela.
2. JINSI YA KUPATA KIBALI CHA UJENZI
- Kuwasilisha michoro ya ramani ya jengo kwa ajili ya uchunguzi.
- Kulipia malipo stahiki ya uchunguzi wa ramani hizo.
- Kulipia malipo ya kiwanja kwa mwaka husika.
3. JINSI YA KUWASILISHA MAOMBI MICHORO YA MAJENGO MAALUMU.
Michoro ya majengo maalumu(Maghorofa, kumbi, Taasisi mbalimbali, Bar, Vituo vya mafuta, Viwanda, Hospital na majengo mengine ya jinsi hiyo iwasilishwe kwa kuanza na michoro ya awali ya kisanifu(Preminary Drawings) ambayo itahusisha.
- Michoro ya sakafu(Floor plan) 1:100
- Sura ya jengo(Elevations) 1:100
- Mkato wa jengo(Section) 1:100
Baada ya uchunguzi wa michoro ya awali kukamilika itawasilishwa michoro ya michoro(Final Drawings) ambayo ni michoro ya kisanifu na ya kihandisi(Architectural and structural drawings) kwa ajili ya uchunguzi.
● Michoro inayowasilishwa izingatie kanuni na taratibu zote muhimu za kiuchoraji(Architectural and Engineering Aspects) na iwe imesainiwa na msanifu majengo/Mhandisi anayetambuliwa(Architectural and Structural Endorsement).
● Michoro hiyo iambatane na nakala ya cheti cha uchunguzi wa athari za kimazingira(Environment Impact Assessment EIA).
● Michoro iambatane na nakala za nyaraka zote halali za umiliki wa kiwanja husika pamoja na stakabadhi ya malipo ya kiwanja kwa mwaka husika.
● Michoro yote iwasilishwe ikiwa na maandishi yanayosomeka(Readable text).
● Michoro yote iwasilishwe kwenye ukubwa wa karatasi(paper size) A0,A1,A2 au A3.
4. JINSI YA KUWASILISHA MAOMBI YA MICHORO YA MAJENGO YA KAWAIDA.
Michoro ya majengo ya kawaida itawasilishwa kwa kuzingatia maelezo ya hapo juu isipokuwa haitatangiliwa na michoro ya awali(Preminary Drawing) kama ilivyo katika michoro ya majengo maalumu.
- MICHORO ILIYOANDALIWA IONYESHE NINI
●Litakavyokuwa(Plans, Sections, Elevations, Foundation, Roof plan, Site plan).
●Ramani ya kiwanja (Location plan).
●Namba na eneo la kiwanja kilipo.
●Jina la mmilikaji ardhi inayohusika.
●Jina la mchoraji, ujuzi na anuani.
●Ukubwa wa jengo kwa mita za mraba.
●Ujazo wa kiwanja(Plan ratio).
●Urefu wa jengo(Height).
●Matumizi yanayokusudiwa.
●Idadi ya maegesho yatakayokuwepo.
●Umbali kwa jengo kutoka kwenye mipaka ya kiwanja(Setbacks).
●Mfumo wa kutoa majitaka hadi kwenye mashimo.
- VIAMBATANISHO UNAVYOTAKIWA KUWA NAVYO
● Fomu moja ya maombi iliyojazwa kwa usahihi.
● Hati ya kumiliki kiwanja au barua ya toleo.
● Kumbukumbu zingine zinazohusu kiwanja hicho kama hati za mauzo makabidhiano na mengine.
● Nakala ya risiti ya kodi ya kiwanja na kodi za majengo.
● Mabadiliko ya matumizi ya ardhi.
● Ramani ya kiwanja iliyosajiliwa.
- UMUHIMU WA KIBALI CHA UJENZI
● Kutimiza matakwa ya kanuni za ujenzi mijini.
● Kuwezesha kujenga majengo na nyumba kama yaliyoelekezwa katika mipango miji ya sehemu husika.
● Kudhibiti ujenzi holela.
- MUDA WA UPATIKANAJI WA KIBALI CHA UJENZI
● Endapo mwombaji atakamilisha hatua zote muhimu kwa wakati atapata kibali cha ujenzi ndani ya majuma mawili(2) hadi manne(4).
● Hii ni pamoja na uwasilishaji wa ramani zilizoidhinishwa na wataalamu husika na hati za umiliki zilizo sahihi.
- WAJIBU WA MWANANCHI
Ni wajibu wa kila mwananchi kujenga au kukarabati nyumba yake iliyo ndani ya mji/jiji kwa kibali kutoka halmashauri.
- TAHADHARI
● Endapo mwananchi yeyote atajenga au kukarabati nyumba bila kibali cha ujenzi toka halmashauri,atapewa ilani ya kusimamisha ujenzi au ukarabati na kushauriwa kufuata taratibu za kuomba kibali cha ujenzi ndani ya siku saba(7).
● Kama mwombaji atakaidi ilani ya kusimamisha jiji au miji litampa ilani ya kubomoa jengo lake mwenyew na akishindwa jiji litabomoa jengo husika na kudai mmiliki gharama za utekelezaji wa ubomoaji.
Imeandaliwa na; UTUKUFU CLEMENT MWANJISI
(Planning Officer wa kujitegemea).
======
USIJENGE KIHOLELA, TAMBUA MAMBO HAYA MUHIMU KUHUSU 'KIBALI CHA UJENZI'
1. KIBALI CHA UJENZI
Kulingana na sheria ya ujenzi wa majengo Mijini si ruhusa kwa mtu yeyote kujenga au kuanza kujenga jengo bila ya:-
(i) Kutuma maombi kwa mamlaka ya mji
(ii) Kuwasilisha michoro ya jengo na kumbukumbu husika
(iii) Kupata kibali kwa maandishi kinachoitwa “Kibali Cha ujenzi”
2. KIBALI CHA AWALI (Planning consent)
Inashauriwa kupata kibali cha awali kabla ya kuomba kibali cha ujenzi. Hivyo muendelezaji anatakiwa aandae mchoro wa awali (Outland plan) kwa utaratibu unaotakiwa ukionyesha aina ya ujenzi atakaokusudia kufanya ili aweze kupata ridhaa ya kuendelea na hatua za kuandaa michoro ya mwisho.
Faida:
• Kuokoa muda na gharama iwapo michoro ya mwisho itaonekana kuwa na dosari za kitaalam ambazo zitahitaji kufanyiwa marekebisho.
•Kuwa na uhakika kuhusu mahitaji muhimu ya kuzingatiwa wakati michoro inaandaliwa.
3. JINSI YA KUWASILISHA MAOMBI YA KIBALI CHA UJENZI
Baada ya michoro kukamilika, iwasilishwe ikiwa kwenye majalada kwa namna ambayo inaweza kufunguliwa na kusomeka. Michoro hiyo iwasilishwe ifuatavyo:-
• Seti tatu za michoro ya jengo (Archectural drawing)
• Seti mbili za michoro ya vyuma/mihimili (structural drawings) kwa michoro ya ghorofa
4. MICHORO ILIYOANDALIWA IONYESHE NINI
Michoro itakayoandaliwa inatakiwa ionyeshe mambo yafuatayo:-
• Namna jengo litakavyokuwa (plans, sections, elevations, foundation and roof plan)
• Namba na eneo la kiwanja kilipo
• Jina la mmilikaji ardhi inayohusika
• Jina la mchoraji, ujuzi na anwani
• Ukubwa wa jengo kwa mita za mraba
• Ujazo wa kiwanja (Plot coverage)
• Uwiano (Plot ratio)
• Matumizi yanayokusudiwa
• Idadi ya maegesho yatakayokuwepo
• Umbali wa jengo kutoka kwenye mipaka ya kiwanja (setbacks)
• Mfumo wa kutoa maji taka hadi kwenye mashimo
5. VIAMBATANISHO
• Fomu za maombi zilizojazwa kwa usahihi
• Hati ya mmiliki wa kiwanja au barua ya toleo
• Kumbumbuku nyingine zinazohusu kiwanja hicho kama hati za mauzo, makabidhiano n.k
• Nakala za risiti ya kodi ya kiwanja na kodi ya majengo
• Mabadiliko ya matumizi ya ardhi
6. HATUA ZINAZOFUATWA KATIKA KUSHUGHULIKIA MAOMBI YA KIBALI
Zifuatazo ni hatua zinazofuatwa wakati wa kuchunguza michoro hiyo:-
• Uhakiki wa miliki
• Kukaguliwa usanifu wa michoro
• Kukagua kiwanja kinachokusudiwa kuendelezwa
• Uchunguzi wa matumizi ya jengo na uwiano
• Uchunguzi wa maofisa wa afya
• Uchunguzi wa mipango ya uondoaji maji taka
• Uchunguzi wa tahadhali za moto
• Uchunguzi wa uimara wa jingo
• Kuwasilishwa kwenye kikao cha Mipangomiji na Mazingira baada ya kukamilisha taratibu zote
• Hatimaye kuandika na kutoa kibali
7. TARATIBU ZA KUFUATA BAADA YA KUPATA KIBALI CHA UJENZI
Kwa mujibu wa sheria ya ujenzi mijini ujenzi wowote ambao umepata kibali unapaswa kukaguliwa kwa kila hatua ya ujenzi. Baada ya kupata kibali cha ujenzi mambo yafuatayo yanapaswa kufanyika:-
1. Kutoa notisi ya masaa 48 kabla ya kuanza ujenzi. Fomu ya notisi hii utapatiwa unapokabidhiwa kibali cha ujenzi
2. Kujaza fomu ya ukaguzi na kuwasilisha kwenye ofisi ya ujenzi ili hatua hiyo ya ujenzi unayotaka kufanya ikaguliwe
3. Utapatiwa “Certificate of Occupation” baada ya ujenzi wako kukamilika iwapo tu hatua muhimu za ujenzi zimekaguliwa
8. FAIDA ZA KUJENGA NYUMBA IKIWA NA KIBALI CHA UJENZI
1. Kuishi kwenye nyumba ambayo imethibitishwa kitaalamu kuwa ni salama
2. Kuwa na mazingira bora kwa kuwa na mji uliopangwa
3. Kuepuka hasara na usumbufu unaoweza kutokea iwapo ujenzi umefanyika bila kibali ikiwa pamoja na kushitakiwa mahakamani, kuvunjiwa na kulipa gharama za uvunjaji.
Hayo ndio Mambo muhimu ya kuyafahamu kuhusu 'Kibali cha Ujenzi' (Building Permit), Epuka usumbufu fuata sheria!.JENGA KWA RAMANI.
======
Vitu kumi na moja (11) vya kuzingatia katika michoro ya jengo ili kupata kibali cha ujenzi
Kulingana na sheria ya ujenzi wa majengo mijini si ruhusa kwa mtu yeyote kujenga au kuanza kujenga jengo bila ya kuwa na seti ya michoro ya jengo (architectural drawings), hivyo basi kuna vitu vya kuzingatia na ambavyo vinatakiwa kuwepo kwenye michoro hiyo ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza wakati ukitafuta kibali cha kujenga jengo.
Vitu hivyo ni;
1. Namna jengo litakavyokuwa (plans section, elevation, and foundation and roof plan)
Ili kupata kibali cha ujenzi lazima kuwe na michoro itakayoonesha msingi(foundation) utakavyokuwa, mchoro wa kipande/sehemu ya jengo(section plan), paa, na mionekano ya mbele, nyuma, kushoto, na kulia. Michoro yote hii ya namna jengo litakavyokuwa inatakiwa iwe na vipimo vinavyoonekana vizuri.
2. Namba na eneo la kiwanja kilipo
Hivi huonekana sehemu ya chini au kulia Katika michoro ya namna jengo litakavyokuwa.
3. Jina la mmilikaji ardhi inayohusika
Pia sehemu hii huonekana katika michoro yote ya jengo upande wa kulia au chini.
4. Jina la mchoraji na anwani
Pia hii sehemu huonekana chini au kulia katika michoro ya jengo.
5. Ukubwa wa jengo kwa mita za mraba
Hii sehemu huonekana kwenye mchoro wa jengo(floor plan) au kwenye mchoro unaoonesha mpangilio kati ya kiwanja na jengo (site plan).
6. Ujazo wa kiwanja (plot coverage)
Hii sehemu hueleza ujazo utakao chukuliwa na jengo katika kiwanja, pia huonekana kwenye mchoro unaoonesha mpangilio kati ya jengo na kiwanja(site plan).
7. Uwiano (plot ratio)
Hii sehemu hueleza uwiano kati ya jengo na kiwanja, pia huonekana katika mchoro wa site plan.
8. Matumizi yanayokusudiwa
Hii sehemu hueleza kusudio la matumizi ya jengo, pia huonekana kulia au chini katika michoro yote ya jengo.
9. Idadi ya maegesho yatakayokuepo
Hii sehemu huonesha idadi ya maegesho ya magari na vitu vingine vinavyozunguka jengo ndani ya kiwanja husika, pia huonekana katika mchoro wa site plan.
10. Umbali wa jengo kutoka kwenye mipaka ya kiwanja (setbacks)
Hii sehemu hutumika kuonesha umbali uliopo kutoka katika mipaka ya kiwanja mpaka jengo husika, pia huonekana kwenye mchoro wa site plan.
11. Mfumo wa kutoa majitaka hadi kwenye mashimo
Hii sehemu huonesha jinsi ya kutoa majitaka kutoka kwenye jengo mpaka kwenye mashimo ya kuhifadhia,pia sehemu hii huonekana kwenye site plan.
Kutokana na maelezo hapo juu, kwa mtu yeyote anayehitaji kujenga jengo inabidi ahakikishe kila kitu nilichokielezea hapo juu kinaonekana katika seti ya michoro ya jengo (architectural drawings) kabla ya kuendelea na utaratibu mwingine unaofuata.
View attachment 1356883
Mchoro wa jengo (floor plan)
View attachment 1356884
Mchoro wa sehemu ya jengo(section plan)
View attachment 1356885
Mchoro wa paa (roof plan)
View attachment 1356886
Mchoro unaoonesha mionekano ya jengo (elevation)
Chanzo: Ujenzi Elekezi Blog