Leo nilikuwa benki nikimwekea ada ya mwanangu wa kwanza, anayesoma darasa la pili shule fulani ya kimataifa Dar. Nikiwa ninahangaika na mstari mrefu wa benki nikafikiria mambo mengi niliyokumbana nayo nikiwa primary, wakati elimu ya primary ya enzi zile ikiishiaishia ile miaka ya themaninini mwishoni (Nimemaliza primary 1992). Hatukuhitaji kusoma international schools. Tulikuwa tunasoma na watoto wa mawaziri na yule kapuku wa kwanza mtaani. Tulikuwa tunasoma umbali zaidi ya kilometa 15, na wala hatukukosa kuchelewa namba au kufika darasani.
Nakumbuka enzi zile tulipokuwa tunapewa madaftari kila yakijaa. Ulikuwa unapeleka daftari lilojaa kwa mwalimu, naye atalichana kidogo ili lisitumike tena na pia usidanganye, halafu unapewa daftari jingine jipya papo hapo. Walimu hawakuwa wezi hata kufikiria kwenda kuyauza stationery. Wengine walibahatika kupewa hata mikebe. Nakumbuka shule tulipokuwa tunakimbia mchakamchaka saa kumi na moja asubuhi halafu ukitoka hapo kuna gwaride. Walimu wetu wote walipitia JKT.
Tukawa smart kiafya na kiakili pia. Mtaingia darasani na kusoma hadithi za akina Manenge na Mandawa, Heri mimi sijasema, Wagagagigikoko, na vingine kibao. Vitabu vilikuwa vingi kiasi na kila mtu angeweza akawa na nakala mbilimbili za kitabu kimoja. Miandiko yetu ilikuwa mizuri, maana tulikuwa tunashindanishwa na pia kutandikwa viboko ukiandika kama bata. Kweli ilikuwa Someni kwa Furaha.
Ukihitimu LY shule inakuwa imejaa kichwani, ila sekondari zilikuwa chache, hivyo wengi wetu hatukupata nafasi za kuendelea kusoma japo tulikuwa wazuri. Kuna shule yoyote uliyosoma ambayo bado yakukumbusha mazuri kama sisi tuliosoma enzi zile primary?
Nilisoma shule ya msingi mpechi, wilaya ya njombe, nakumbuka kwanza marafiki zangu Vinga, Sevanu na Royda na wengineo sijui leo hii wako wapi. nakumbuka tulivyokuwa tunashindana kusoma ili ufaulu uwe wa kwanza siku mnafunga shule wazazi wakija unaona fahari matokeo ya mtihani yakisomwa mbele ya wazazi wa kwanza mpaka aliyefunga mkia.
Nakumbuka tulivyokuwa tunaenda Njosi ( njombe secondary) kuokota mavi ya ng'ombe kwa ajili ya mbolea tuliotumwa shule,
Nakumbuka somo la sanaa na sayansi Kimu tulivyokuwa tunafanya kwa vitendo, i.e kupika, kuchonga, kusuka, usafi wa mwili na jinsi tulivyokuwa tunakaguliwa mpaka chupi.
Nakumbuka mwaka ukianza mnapewa madaftari 12, rula ndefu pamoja na mkebe. nakumbuka Njombe ilivyokuwa na matunda ya aina mbalimbali na jinsi tulivyokuwa tunafaidi.
Baada ya kuhamia Wilolesi primary - Iringa mjini namkumbuka mwalimu wetu mkuu mwalimu Kajiba alivyokuwa 'smart' Gwaride kila Jumatatu au Alhamisi; Nakumbuka jinsi shule ilivyokuwa na sifa ya kuponda kokoto lakini pia wanafunzi walikuwa na sifa ya kufanya vizuri katika masomo yao; Nakumbuka pia miti miwili ya mitoo tulikuwa tunaogopa kula matunda yake tukisema kuwa kwenye hiyo miti kulikuwa na majini.
( shule ilikuwa na sifa ya kuwa na majini na kwamba kila mwaka lazima mwanafunzi afe); Pia namkumbuka mwalimu wangu wa darasa Mwalimu matola kwa kupenda kuchapa viboko vya mgongoni lakini alikuwa mwalimu mzuri asiyependa wanafunzi wavivu alikuwa anahakikisha kila mtu lazima afanye vizuri kwenye somo lake la sayansi na hesabu bila hivyo jiandae kwa mboko, pushapu na kutembelea magoti. kwa ujumla walimu wetu wa shule ya msingi enzi hizo walikuwa wachapa kazi na hodari.
Nakumbuka pia mchezo wa rede, uki, kiboleni, mdako, kuruka kamba, kombolela, kujipikilisha kibabababa na kimamamama tehe tehe....
na baadhi ya nyimbo tulizokuwa tunaziimba kwenye michezo yetu kama
kibunzi kibunzi; cha mememe; mwanambuzi kajamba kamjambia mkewe.......................
Ukuti ukuti ...............................
asiyependa shule ni mjinga kabisa; baarua ikija aitembezwa kote...............................
nilikwenda kwa dada; nikamkuta shemeji anadishi ugali; nikadishi kidogo fungulia rekodi tukacheza kidogo...........................
Halafu ikifika jumamosi saa nane kusikiliza mama na mwana na hadithi zake tamu tamu kama ua jekundu, unyoya wa kipanga azizi, binti chura, adili na nduguze, n.k wa kadhaa.