SoC03 Elimu bila Lugha: Mtaala mpya haujatutoa kwenye mtumbwi wa Vibwengo

Stories of Change - 2023 Competition

fmulinda

New Member
Aug 27, 2022
1
3
Nilipopata habari za mpango wa serikali ya Tanzania wa kupitia upya mtaala wa elimu, nilipata faraja na matumaini. Kuna matarajio makubwa yalianza kujijenga kichwani mwangu – matarajio ya kuondokana na elimu isiyoweza kutafsirika katika uhalisia wa maisha na kazi. Lakini kama wasemavyo waswahili mtaani, hii pia haikuwa riziki…bado tutaendelea na safari katika mtumbwi wa vibwengo. Uwezekano wa kufika tuendako ni mdogo sana.

Ulimwenguni kote, elimu hutumika kama nyenzo kuu ya kuendeleza jamii. Watu wakisoma wakaelewa vizuri na kupata maarifa yanayogusa maisha yao, basi jamii inaendelea. Sehemu kubwa tunakotofautiana na mataifa mengi yaliyoendelea ni kwenye lugha ya kufundishia. Ukiusoma mtaala mpya unaopendekezwa, utagundua kwamba kuna mabadiliko makubwa sana ya kimaarifa na ujuzi. Kuna matumaini makubwa sana ya kubadilika kama Taifa na kuanza kuona matunda ya elimu. Tatizo kubwa lililofumbiwa macho ni lugha ya kufundishia. Kiingereza kinaendelea kupewa jukumu la kumpa maarifa msukuma wa Bariadi, mmakonde wa Chitohori, mpogoro wa Morogoro, pamoja na mnyambo wa Karagwe. Huu mtumbwi hauwezi kufika!

Elimu ya Tanzania (shule za Umma) inatambua Kiswahili kama lugha ya kufundishia tangu elimu ya awali hadi darasa la saba. Kuanzia kidato cha kwanza na kuendelea, Kiingereza huchukua jukumu zito la kubeba maarifa. Matarajio ni kwamba Mhandisi aliyejengewa msingi wa elimu yake kwa Kiswahili atajiimarisha kitaaluma kwa kutumia Kiingereza kisha awe na uwezo uleule alionao mhandisi mchina aliyejengwa tangu kuzaliwa kwa kichina!

Mimi nimebahatika kufundisha lugha katika ngazi mbalimbali, na wakati wote nimeishia kusikitika zaidi kuliko kufurahia somo. Kazi kubwa ya Mwalimu wa sekondari niliyoiona ni kutafsiri maarifa kutoka kiingereza kwenda Kiswahili, kisha ayafafanue. Matokeo yake ni kwamba wanafunzi wanasoma matini za kiingereza, wanajifunza kwa Kiswahili, wanajibu mtihani kwa kiingereza. Huu mvurugiko ni mkubwa sana; ulitakiwa ufe!

Sisi walimu wa lugha ya kiingereza pia ni wahanga wa mfumo huu wa lugha ya kufundishia. Miongoni mwa sababu za wanafunzi kushindwa kujua kiingereza ni walimu husika kukosa umahiri wa kutosha (ni zao la mfumo ule ule), pamoja na ulazima wa walimu wa masomo mengine kutumia kiingereza. Katika moja ya madarasa yangu ya lugha niliwahi kuwaelekeza wanafunzi namna ya kutamka neno kwa usahihi, kisha mwanafunzi mmoja akauliza, “mbona mwalimu flani amelitamka tofauti?” Nililazimika kuficha aibu ya mwalimu kwa kuonyesha kwamba pengine hawakumsikiliza vizuri. Ukweli ni kwamba mwalimu huyo hakujua namna sahihi ya kulitamka neno lile, na uwepo wa matamshi yangu sahihi na yale ya mwalimu mwingine kuliwachanganya wanafunzi. Tafiti zimeonyesha kwamba lugha ya kigeni ikifundishwa peke yake ikiwa siyo lugha ya kufundishia, inaeleweka zaidi kuliko ikitumika kama lugha ya kufundishia bila kuwa na msingi mzuri.

Kila ninapopata nafasi ya kulizungumzia hili huwa nadhaniwa kuwa nachukia kiingereza; si kweli. Lengo langu mara zote ni kuhakikisha tunatafuta namna ya kuwapa watoto wetu maarifa kwa lugha moja katika ngazi zote. Kwa mfano, kuna tatizo gani tukifundisha kwa Kiswahili tangu elimu ya awali hadi Chuo Kikuu, kisha Kiingereza (na lugha nyingine za kigeni) kikafundishwa kama somo? Au basi kuna baya gani kama tutafundisha kwa kiingereza tangu elimu ya awali hadi chuo kikuu, na Kiswahili kikawa lugha ya lazima katika hatua zote za elimu? Tukifanya lolote kati ya haya, tutajenga kizazi cha wasomi wenye maarifa, badala ya kutengeneza watu wanaoteseka kila wanapohitaji kujieleza kwa taaluma zao au kufafanua jambo kwenye taaluma zao. Tunapata faida gani kama Taifa kuwa na wasomi ambao kila wakitakiwa kusema jambo kwa uzito wa taaluma zao wanaomba fursa ya kuzieleza zaidi kwa Kiswahili wakati hawakusoma kwa lugha hiyo? Tujitafakari kama Taifa, bado mtumbwi unaweza kugeuzwa.

Wakati mtaala pendekezwa unatangazwa, nilipata hamu ya kusikia eneo la lugha limefanyiwa marekebisho gani; sikuona badiliko lolote. Shule za binafsi zinaendelea kuwa na uhuru wa kuchagua lugha ya kufundishia, wakati shule za serikali zikiendelea kutumia lugha mbili katika ngazi tofauti. Katika kipindi chote cha ualimu wangu, huwa naumia sana pale mwanafunzi anaponiomba atumie Kiswahili kuuliza swali au kufafanua jambo darasani. Siumii kwa sababu napenda kiingereza, naumia kwa sababu natambua kwamba mwanafunzi wangu ana hamu ya kujieleza lakini amenyimwa lugha, amefumbwa mdomo!

Namna pekee ya kuwasaidia watoto wetu ni kujenga mfumo wa elimu unaowasiliana na jamii zetu kikamilifu. Kama tunaona kiingereza ni muhimu sana, basi kianzie ngazi za chini kabisa. Ukiingia darasa la Chuo Kikuu chochote Tanzania, haitakuchukua muda kumgundua mwanafunzi aliyesoma shule binafsi na yule wa shule za serikali. Haya tayari ni makundi yaliyojengwa kwenye misingi miwili tofauti. Kundi moja limeonewa kwa kuchanganyiwa lugha mbili katika mfumo mmoja wa elimu, na jingine limebahatika kuwa na uwezo wa kuikimbia elimu ya serikali. Lugha ya kufundishia si jambo la mchezo au la kupuuzwa.

Natambua kwamba mtaala mpya tayari umepita hatua nyingi za awali, lakini naamini hatujachelewa sana. Mara hii tupange kufika mwisho wa safari, tuukatae mtumbwi huu wa vibwengo. Thamani ya uwekezaji katika elimu itapotea ikiwa hatutazingatia ushauri wa wadau muhimu wa elimu. Elimu bila lugha ni bure. Tanzania ni yetu sote, tuipe elimu sahihi, tuipe mfumo sahihi wa elimu, tuipe wasomi sahihi. Tushuke kwenye mtumbwi huu wa vibwengo!​
 
Back
Top Bottom