Je Rwanda na Burundi ijiunge na East Africa Community ( EAC)?
Unasemaje??
--------------------------------------------------------------------------
Ngara wapinga Rwanda, Burundi kukaribishwa EAC
Chanzo kikuu ni vita, ukabila
Wasema watavuruga amani nchini
Na Manyerere Jackton, Ngara
WANANCHI katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, wanapinga nchi za Rwanda na Burundi kupewa uanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Msimamo wa wananchi hao umefahamika kwenye mikutano iliyohutubiwa na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala, juzi.
Naibu waziri huyo yuko katika ziara ya kuitambulisha wizara, kueleza fursa zinazotokana na jumuiya hiyo; na kukusanya maoni mbalimbali ya wananchi, yakiwamo ya ama, Burundi na Rwanda ziruhusiwe kujiunga, au zisiruhusiwe.
Akiwa katika Kijiji cha Kabanga, wilayani Ngara ambako ni mpakani mwa Tanzania na Burundi, wananchi walitoa maoni yao kwa uwazi na kupinga kwa nguvu zote, Burundi na Rwanda kupewa uanachama kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aliyeanza kutoa maoni yake ni Suleiman Minani, na akasema: Kujiunga kunahitaji muda, hawa wamekuwa katika mapigano kwa muda mrefu, wametuletea uhalifu, hasa ujambazi. Hapa Ngara ujambazi umeletwa na wakimbizi hawa.
Sisi Watanzania Kiswahili ndicho kitambulisho, Warundi na Wanyarwanda sasa wakizungumza Kiswahili, wanaonekana ni Watanzania.
Kwa nini serikali inachelewa kutoa vitambulisho kwa raia wake? alihoji.
Mwananchi huyo alitoa mfano kwa kusema wakati fulani alisafiri na Wanyarwanda kwenda Mwanza. walifika kwenye kizuizi, na akastaajabu kuona wakitoa kadi za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuruhusiwa kuendelea na safari.
Mimi nilipita kwa kitambulisho cha gazeti, hatuna vitambulisho na viwango vya kuoleana ni vikubwa, kule (ngambo upande wa Burundi) tuna wajomba, mimi nashauri wasubiri kujiunga kwenye jumuiya, wakiruhusiwa sasa, usalama wetu utayumba, alisema.
Mwananchi Seleman Senduka, alisema: Kabla ya kuwakaribisha Rwanda na Burundi, kwanza tujue sisi (Kenya, Tanzania na Uganda), tumefaidika vipi na Jumuiya yetu.
Naye Jason Bahina, alisema: Sisi Watanzania hatuna matatizo ya ukabila na vita; wenzetu wanamalizana kwa kuuana. Wanahukumiana kwa kuangaliana pua.
Kabla ya kuwakaribisha, CCM ifanye kwanza kazi ya kisiasa, ijiridhishe kama kweli kujiunga kwao hakutaleta mgogoro. Kilichosambaratisha jumuiya ya kwanza ni tofauti za kisiasa, kwa hiyo kabla ya kuwakaribisha Rwanda na Burundi, lazima mataifa haya yaeleweke siasa zao.
Mwananchi mwingine, Joseph Balindie, yeye alisema wananchi wana wasiwasi mkubwa kuona Rwanda na Burundi, zinataka kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tuna wasiwasi, tabia za wenzetu-kuwashirikisha ni ngumu, wale wanauana, kuwashirikisha si rahisi, alisema.
Naye Gideon Ruvulahende (66), alisema: Kuungana ni jambo zuri, sasa kama Rwanda na Burundi nao wanataka kuungana na sisi, kwanza wapewe masharti ya kuumaliza ukabila wao.
Japhet Israel (62), alisema kwa umri wake huo, hajawahi kusikia Rwanda na Burundi kuna amani.
Alikiri kuwa wananchi katika nchi hizo ni ndugu zetu, na kwamba hata baadhi yao wanafanana na Watanzania, lakini kwa suala la kuwakaribisha kwenye jumuiya kwa sasa, haliafiki.
Tukiungana tutaharibu usalama wetu, kwanza wajirekebishe, wajue sote tu Waafrika, wajue Watutsi na Wahutu wote ni Waafrika-wajue weupe (Watutsi) na weusi (Wahutu), ni Waafrika, wakijua hivyo, sasa ndipo wakaribishwe kujiunga, alisema Israel.
Ofisa Uhamiaji Mkuu wa Kituo cha Kabanga, Harride Mwaipyana, alitumia fursa ya mkutano huo wa hadhara kutoa maoni yake.
Nipo hapa kuanzia mwaka 1999, nimesoma tabia za pande zote. Tusikurupukie kitu bila kukijua. Sisi Tanzania, Kenya na Uganda tunajuana tabia zetu.
Tabia za hawa wenzetu (Rwanda na Burundi) ni mbaya-hawana amani, wanabaguana, kuna vikao vya usiku vya kujadiliana. Wanakutana kwa mambo ya siri wakitumia viji-sherehe, wanaalikana.
Ukiwaingiza hawa, nchi itaharibika, wanapenda kutawala, wanajiona ni bora kuliko mtu yeyote duniani, tusiwakaribishe kabisa. Tuchukue muda mrefu sana.
Mheshimiwa Naibu Waziri naomba ulichukue hili kwa umuhimu wa kipekee.
Ujambazi wameleta wao, alisema Mwaipyana, akionekana dhahri kuchukizwa na Rwanda na Burundi kujadiliwa kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Maoni kama hayo yametolewa na wananchi wengi katika maeneo mengi ambayo Dk. Kamala ameyazuru.
Chanzo: Tanzania Daima