SEHEMU YA 96
Njiani, hakukuwa na mtu aliyezungumza lolote lile, kila mmoja alikuwa kimya. Kumkamata Bilionea Matiku ilikuwa ni amri kutoka ngazi ya juu hivyo walitakiwa kumkamata kwa gharama yoyote ile.
Alipofikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, akapelekwa katika chumba maalum cha mahojiano na kuanza kuhojiwa, kwa kuwa lengo lao lilikuwa ni kumlaza kituoni hapo, wakamlaza.
Matiku alijua kwamba kulikuwa na mtu nyuma aliyekuwa akifanya mambo hayo yote, aligundua kwamba sababu ya mambo hayo ni kwa sababu tu alimsaidia mwanamke mjane wa Mapoto ambaye alikuwa akichukiwa na serikali iliyokuwa madarakani kipindi hicho.
Kukamatwa kwake ikawa ni stori kubwa, kila mtu akaanza kulizungumzia jambo hilo, wengi waliona kabisa kwamba polisi walitumwa kwani kwa sababu iliyowekwa wazi kwamba ndiyo iliyosababisha bilionea huyo kukamatwa haikuonekana kuwa na mashiko hata kidogo.
“Huu ni uonevu ujue,” alisema jamaa mmoja.
“Kwani geni lipi? Au umetusahau Waafrika?” aliuliza jamaa mwingine.
Wakati Bilionea Matiku akisota sero ndicho kipindi ambacho Rosemary alikuwa nje na watoto wake, hakujua ni sehemu gani alitakiwa kwenda. Moyo wake ulikuwa kwenye majonzi mazito, hakuamini kile kilichotokea, aliwapenda watoto wake, alitamani sana wapate elimu bora lakini kila kitu kilionekana kubadilika.
Akasimama pale alipokuwa, aliwaangalia watoto wake, Irene na Godwin, moyo ulimuuma mno lakini hakuwa na la kufanya. Akawashika mikono na kuondoka nao mahali hapo huku akiwa na kadi yake ya benki ambayo ilikuwa na kiasi cha shilingi milioni tano tu.
“Mama! Tunakwenda wapi?” aliuliza Godwin huku akimwangalia mama yake ambaye mashavu yake yalilowanishwa na machozi.
“Tunakwenda sehemu nyingine,” alijibu.
“Na hapa nyumbani vipi?”
“Twendeni! Nitawaambia kila kitu!”
Hawakuwa na jinsi, mama yao ndiye alikuwa kila kitu, wakaondoka mpaka walipofika Msasani ambapo Rosemary akaingia katika kibanda cha ATM na kutoa kiasi cha shilingi laki tano na kuondoka mahali hapo.