Dubai: Kutoka kijiji cha uvuvi mpaka kuwa jiji la dunia

Kikwajuni One

JF-Expert Member
Mar 18, 2013
13,142
6,947
dubai-sand-storm.jpg

Jangwa halikuwa mbali sana na milango ya Dubai. Mji mkuu huu, ambao sasa umegeuzwa kuwa kituo cha kisasa cha fedha ambacho, pamoja na wakazi wake milioni tatu ndio jiji lenye watu wengi zaidi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), umepakana na bahari, kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine kunaonekana kama zulia la mchanga lisilo na mwisho.

Kwa wakazi wa eneo hili, kwao ni hadithi ya mafanikio isiyowezekana, kile kijiji cha uvuvi kisichokuwa na maendeleo ambacho katika miaka 50 kimebadilishwa na kuwa jiji la kisasa.

Lakini licha ya uzuri na utajiri, mji huu unakabiliwa na changamoto kubwa: jangwa vamizi ambalo linatishia ardhi yenye rutuba iliyosalia katika emirate.

UAE ina ukubwa sawa na Ureno, lakini karibu 80% ya eneo lake la ardhi tayari ni jangwa.

Kutafuta suluhu ya uhakika ya changamotto hiyo imekuwa kipaumbele kikubwa kwa nchi hiyo. Lengo sio kukabiliana na jangwa, lakini kuyarejesha maeneo ya ardhi ambayo hayana tija tena.

UAE iko katika nafasi ya kipekee ikilinganishwa na nchi zingine zilizoathiriwa na jangwa, kwani ina uwezo wa kufadhili mawazo ya ubunifu. Ukweli, inawekeza katika mawazo mapya kuboresha ukijani na kusaidia teknolojia kwenye ubunifu na taasisi za elimu.

Dubai ni mfano wa kile kinachoweza kufanikiwa wakati tamaa na lengo linaungwa jambo Fulani linapoungwa mkono kifedha. Mawazo ambayo yalisaidia kujengwa mji kwenye mchanga sasa yanaunganishwa ili kupambana na uvamizi wa jangwa.

Ikiwa itafanikiwa, ufumbuzi huu uliobuniwa unaweza kuwa na athari kubwa duniani kote.

Karibu hekta milioni 12 hupotea duniani kote kila mwaka kutokana na matokeo ya moja kwa moja ya ukame na jangwa, sawa na viwanja 1,300 vya mpira wa miguu kila saa.

Ili kuiweka katika muktadha unaoeleweka vyema, kama ungeunganisha ardhi ungelazimika kuendesha gari kwa umbali wa kilometa 210 kwa saa kuuifkia upana wa jangwa.

Katika miaka 20 iliyopita kumekuwa na uharibifu mkubwa wa ardhi. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, UAE ilikuwa na hekta 75,000 za ardhi ya kilimo mwaka 2002, lakini kufikia mwaka 2018 zilishuka mpaka kufikia 42,300.

Mwaka 2012, Sheikh Mohamed bin Rashid Al Maktoum, Makamu wa Rais wa UAE na Emir wa Dubai, alitangaza mkakati wa kujenga uchumi wa kijani unaozingatia uendelevu na wenye ukuaji wa muda mrefu.

"Viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wa UAE wanaelewa kuwa kuboresha mazingira ni muhimu ili kuifanya nchi hiyo na miji kama Dubai kuendelea kuwa wa kisasa," anasema Profesa Natalie Koch, mtaalamu wa jiografia ya kisiasa katika Chuo Kikuu cha Syracuse huko New York.

Mamlaka za UAE zina wasiwasi pia juu ya namna wataweza kudumisha utajiri wao wa sasa wakati rasilimali za mafuta itakapopungua au kushuka thamani, anasema Gökçe Günel, profesa wa anthropolojia katika Chuo Kikuu cha Rice huko Texas na mwandishi wa Spaceship katika Jangwa, kitabu kinachohusu nishati, mabadiliko ya hali ya hewa na muundo wa mijini huko Abu Dhabi.

"Kwa kweli kulikuwa na msukumo wa kuvutia biashara mpya za teknolojia kwa kanda tangu mapema katika miaka ya 2000s kama sehemu ya mabadiliko ya Dubai kuelekea kwenye uchumi wa ujuzi," anasema Günel.

Tayari kuna mipango mingi inayotekelezwa kuhusu Dubai. Lakini matatizo ya mazingira katika mji huo yako mbali na ufumbuzi, hasa kuhusu jangwa.

Ukame, matumizi makubwa ya rasilimali za asili, maendeleo ya haraka ya mijini na kuongezeka kwa chumvi kwenye udongo ni hatari kwa mji huu. Kushindwa kushughulikia ipasavyo mambo haya kunatishia kila kitu ikiwemo kupoteza ardhi inayofaa kwa kilimo pamoja na kutoweka kwa viumbe vya asili ya mji huo.

Suluhisho linalofahamika kitambo la mazingira la kupanda miti mingi zaidi, kwa muda mrefu limechukuliwa kama lengo kuu kwa nchi hiyo.

Mwaka 2010, Emir Mohamed alizindua mpango wa "Miti Milioni Moja", kwa lengo la kupanda kiasi hicho cha miti ili kuongeza maeneo ya kijani katika mji na kuzuia jangwa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Hamza Nazal, mwakilishi wa Green Land, kampuni iliyoendeleza mradi huo kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Mazingira la Zayed linaloungwa mkono na serikali, "100% ya miti ilikufa na mpango huo ulifeli kabisa."

Christian Henderson, profesa wa masomo ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Leiden nchini Uholanzi, anasema "Kwa mtazamo wa kiikolojia, kushindwa kwa mradi huu ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya miti haikuzoea mazingira ya UAE," anaongeza.

BBC iliwasiliana na Dubai Holding na Manispaa ya Dubai kuhusu mpango huo lakini haikupata jibu.

Kuchagua aina sahihi ya miti, hasa ya asili, ni muhimu kwa miradi ya upandaji miti.

Licha ya mpango wa upataji mipiti kufeli, bado zoezi la upandaji wa miti linachukuliwa kuwa sehemu kuu ya mkakati wa kupambana na jangwa huko Dubai, kama ilivyo mahali pengine katika Mashariki ya Kati.

Saudi Arabia, kwa mfano, hivi karibuni ilitangaza nia yake ya kupanda miti bilioni 10 katika miongo ijayo kama sehemu ya mpango wa mazingira wa Saudi Green Initiative.

Teknolojia mpya zilizobuniwa ili kutekelezwa mpango wa kijani kama Udhibiti wa Jangwa la Norway inaleta suluhu kwa njia tofauti.

Teknolojia mojawapo inahusisha nanoparticles ya asili ya udongo wa kioevu ili kugeuza haraka mchanga wa jangwa kuwa udongo wenye rutuba.

Katika kudhibiti wa jangwa Dubai, wanatumia tope jepesi kugeuza mchanga kuwa udongo wenye rutuba

Teknolojia hiyo inahusisha kumwagilia udongo mkavu usiofaa kupata mchanganyiko wa maji na udongo na kutengeneza safu yenye unene wa sentimita 50. Topetope hili utengeneza kitu kama sponji ambayo baadae hubadili mchanga kuwa udogo wenye rutuba.

Inakadiriwa kuwa 75% ya uso wa ardhi ya sayari yetu tayari umeharibika, lakini suala hilo mara nyingi linakosa tahadhari inayostahili.

"Ni tatizo ambalo linaathiri zaidi Afrika, Asia na Amerika ya Kusini, na maeneo maskini ya nchi zilizoendelea, kama vile baadhi ya maeneo kame na yaliyotengwa ya Mediterranean," anasema Anna Tengberg, profesa kutoka Chuo Kikuu cha Lund nchini Sweden.

Kutokana na utajiri wake mkubwa, msukumo wake wa kuwa mstari wa mbele katika maendeleo, na haja ya kurejesha ardhi inayozidi kuchukuliwa na mchanga, juhudi za UAE za kupambana na kuenea kwa jangwa zinaweza kutoa mwanga na muarobaini kwa matatizo ya kimazingira ya aina hii na kuwa mfano kwa ulimwengu wote kuufuata.

Kama nchi inayoongoza kwa teknolojia katika eneo hilo, njia ya maendeleo iliyobuniwa na nchi hiyo inaweza kuleta faida kubwa kwa majirani zake na maeneo mingine yanayokabiliwa na jangwa.

BBC Swahili
 
Back
Top Bottom