Ni vizuri kusoma maandishi pembeni na katikati ya mstari ili kupata mantiki yake vizuri. Ukisoma juujuu utaibuka na hitimisho la juujuu.
Naelewa hasira zinatokana na makala inayowakosoa Zitto na wakosoaji wake. Naelewa vilevile kwamba ambacho nilitakiwa kuandika ni kuungana na wengine kumlaani vikali Zitto kwa kutangaza kugombea urais, na sio kuwalaumu pia wale wanaomlaumu yeye. Huu ndio utamaduni unaotakiwa kwa sasa katika siasa za Tanzania, hasa hapa jamvini kwetu JF-group think!
Lakini ni muhimu tukakumbuka kwamba utamaduni wa fikra hodhi kwa kisingizio cha kutetea maslahi ya chama ndio iliyoifikisha CCM hapa na ndio mwanzo wa kumomonyoka kwa utamaduni wa kuwajibika katika nchi hii. Tumeua kabisa fikra huru kwa sababu ya kuogopa kuonekana tunaenda kinyume na watu fulani.
Mwalimu Nyerere ametufundisha katika kitabu chake cha 'Tujirekibisha' kwamba kosa ni kosa tu bila kujali nani kafanya kosa. Narudia kusema kama nilivyosema katika makala yangu kwamba 'kosa' la Zitto kutangaza urais ni la kimantiki na la kiutamaduni zaidi na wala halina uhusiano wowote na yeye kuvunja sheria au kanuni yeyote ya chama na katika nchi. Sasa sioni kusema hivi kunachangia vipi kuleta mzozo ndani ya chama.
Demokrasia ndani ya vyama na nje haijengwi kwa kuficha fikra na mawazo ndani ya uvungu wa kitanda. Demokrasia inakuzwa kwa mnyukano wa fikra, uwazi na ukweli. Msimamo wa pamoja wa viongozi unatakiwa katika mambo ya msingi ya kisera na kimkakati na sio katika kila jambo. Kutaka wote muwe na mfanano katika fikra na mitazamo kwa kila jambo ni kujaribu kuwafanya watu wawe binadamu nusu na wanasiasa nusu. Hivi tunavyoongea maelfu ya wanachadema wamekwisha kutangaza nia na haja zao za kugombea udiwani na ubunge katika uchaguzi ujao, katika majimbo na katakata mbalimbali, zenye madiwani na wabunge wetu na zile ambazo hatuna. Sasa kama kule katika majimbo na kata hakuna tatizo kwa nini iwe tatizo juu? Au ndio tunatakiwa tuendelee utamaduni wa CCM wa kuruhusu wanachama wao kufikiria kugombea nafasi yeyote lakini sio uenyekiti?
Kupachika watu majina na kuwaweka kwenye mafungu kwa sababu hajafikiri na kutenda kama wewe ni fitina, na ni jambo ambalo Mwalimu alilikemea sana katika uongozi, nami nalikemea kabisa katika wiki hii tunayeendelea kumkumbuka Mwalimu. Kwa wale ambao hawakusoma makala yangu, naiweka tena hapa.
______________________________________________________________________________________
Unafsi wa Zitto na wapinzani wake
Kitila Mkumbo
Raia Mwema, Toleo la
262
10 Oct 2012
KATIKA siku za hivi karibuni kumetokea malumbano kutokana na uamuzi wa Zitto Kabwe kutangaza kwamba atagombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao. Katika kutekeleza azima yake hiyo ametangaza pia kwamba hatogombea tena nafasi ya ubunge katika Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ikumbukwe kwamba hii si mara ya kwanza kwa Zitto Kabwe kutangaza kutogombea ubunge huko Kigoma Kaskazini.
Mwaka 2007 akiwa ziarani nje ya nchi alitangaza kwamba asingegombea ubunge katika uchaguzi wa mwaka 2010. Hata hivyo aligombea na akashinda na ni mbunge hadi leo hii. Nitaeleza baadaye katika makala haya nini maana yake kisiasa na yeye mwenyewe Zitto ni mwanasiasa wa namna gani.
Watu kadhaa ndani na nje ya CHADEMA wamehamaki baada ya Zitto kutangaza nia yake ya kugombea urais. Wengi wa wanaopinga kauli ya Zitto wanaipinga kwa minajili kwamba ametangaza mapema na kutangaza huko kutasababisha mgogoro, mgawanyiko na fujo katika chama.
Hamaki hii imekolezwa zaidi na mwasisi wa CHADEMA na mwanasiasa mkongwe hapa nchini, Mzee Edwin Mtei, ambaye amesema kwamba hatua ya Zitto kutangaza mapema kugombea urais ‘itasababisha mzozo na mpasuko' kwa kuwa wapo wanachama wengine pia wanaoutaka urais. Kuna wengine ambao wamemuona Zitto Kabwe kwamba ni mbinafsi anayejijali zaidi yeye bila kujadili mustakabali wa chama chake.
Wengine wameenda mbali zaidi na kusema kwamba Zitto Kabwe amenunuliwa na anakitumikia Chama cha Mapinduzi na kutangaza urais ni moja ya mikakati katika kufikia azima ya kuidhoofisha CHADEMA. Katika makala haya ninajadili mantiki ya hoja hizi na kuanisha kama uamuzi wa Zitto kutangaza kugombea urais ni jambo la afya kwa CHADEMA na demokrasia yetu au la.
Pamoja na kwamba nami pia siungi mkono tabia ya wanasiasa, hasa katika CHADEMA kutangaza katika muda huu kugombea urais, siwaoni wanasiasa hao kama wanakikosea chama chao kufanya hivyo. Aidha, siwaungi mkono kabisa wale wote wanaompinga Zitto Kabwe kutangaza kuutaka urais katika kipindi hiki.
Siyaungi mkono makundi haya kwa sababu nadhani kwamba yanaenda kinyume cha utamaduni wa kisiasa tunaojaribu kuujenga ndani ya CHADEMA. Kimsingi, makundi yote mawili, Zitto na wapinzani wa tabia zake, wanaendekeza unafsi, jambo ambalo CHADEMA wanajaribu kulikomesha katika siasa za Tanzania. Nitaeleza baadaye maana ya dhana hii.
Wanasiasa wa aina ya Zitto Kabwe ni waathirika wa mfumo uchwara wa uliberali ambao tumeamua kuufuata kimya kimya bila hata kuuelewa vizuri.
Aidha, hamaki na upinzani dhidi ya kutangaza kugombea urais inadhihirisha jinsi ambavyo wengi wetu hatujaielewa vizuri dhana ya uongozi katika mfumo tulio nao wa uliberali uchwara. Tunataka tutende kijamaa wakati tunaishi kiliberali. Katika mfumo wa ujamaa tuliojaribu kuujenga baada ya uhuru, suala la uongozi lilikuwa si suala la mtu binafsi.
Uongozi ulikuwa ni jukumu la wanataasisi kuamua nani anafaa katika nafasi gani. Hivi ndivyo Rashidi Kawawa alivyoweza kuacha cheo cha uwaziri mkuu kwa kumpisha Edward Moringe Sokoine na yeye kuchukua nafasi ya Waziri wa Ulinzi.
Hii ni kwa sababu enzi hizo waliokuwa wanaamua nani ashike nafasi gani ni chama na si mtu kujichagulia nafasi ya uongozi. Katika enzi za ujamaa wetu wa kitanzania, kiongozi mwenye cheo kikubwa na kidogo wote walikuwa ni viongozi wanaoheshimika na kuheshimiana; na ndio maana wote waliitwa ‘ndugu', sawa na wananchi wenzao ambao hawakuwa viongozi.
Utaratibu huu tumeuua baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi na kuamua kuufuata mfumo wa kiliberali bila kuuelewa sawa sawa misingi yake. Katika mfumo wa kiliberali uchwara inaelekea haikubaliki kwa mtu aliyewahi kuwa waziri mkuu arudi kuwa waziri wa kawaida. Katika mfumo wa kiliberali, ngazi moja ya uongozi huzalisha ngazi nyingine ya juu zaidi, na ukishaenda huko hurudi chini bali unahakikisha unaendelea kwenda juu zaidi. Kwa hiyo, ukizingatia mantinki hii ya uliberali uchwara, huwezi kumshangaa Zitto kwa kuutaka urais na kusema kwamba yeye sasa ubunge basi; anataka kwenda juu zaidi na pengine ubunge sio saizi yake!
Kwa hiyo, Zitto Kabwe ameonyesha unafsi ambao ni tabia ya kawaida katika uliberali, hususani huu uliberali uchwara tunaofuata sisi. Mfumo huu una tabia ya kuzalisha viongozi wenye matamanio na utashi binafsi. Katika mfumo huu uongozi ni biashara. Ili uwe kiongozi katika mfumo wa kiliberali lazima uonyesha matamanio na utashi, na ujiuze vya kutosha kabisa. Kwa hiyo kutangaza nia na kujimwagia sifa juu ya uwezo ulio nao katika nafasi fulani ni sehemu kabisa ya mfumo wa kutafuta uongozi katika mfumo wa kiliberali.
Uongozi katika mfumo wa kiliberali ni juu ya mtu na wala sio juu ya taasisi. Anayepata uongozi katika mfumo huu ni yule mwenye uwezo wa kutengeneza mtandao wa wafuasi ambao atahakikisha anakuwa nao kwa kipindi chote hadi uchaguzi utakapofanyika.
Mkakati mwafaka wa kutafuta uongozi katika mfumo wa kiliberali unaambiwa ni kufanya maandalizi mapema. Huu ndio utamaduni ambao CCM imeuasisi kuanzia mwaka 1995 na ambao mtu alitarajia CHADEMA wangeukwepa.
Hata hivyo, sioni kwamba kitendo cha Zitto Kabwe kutangaza kuutaka urais kama ni kosa kwa sababu CHADEMA haijaweka rasmi utaratibu wa kuukataa utamaduni huu. Kwa kuwa utamaduni huu haujakataliwa rasmi kimfumo, haiwezi ikawa kosa mtu moja moja kuchagua kuutumia. Ndio maana Mzee Mtei kawataja watu wengine kadhaa, akiwamo yeye, kwamba nao wanaoutaka urais lakini hawajatangaza nia bado kwa hoja eti muda wa kufanya hivyo bado, kama vile ndani ya CHADEMA kuna muda rasmi uliowekwa wa kutangaza nia ya kugombea.
Ni wazi basi kwamba hata wale wanaompinga na kumzomea Zitto Kabwe kuutaka urais wanaonyesha unafsi. Hawafanyi vile kwa sababu wana misingi fulani wanayoiamini juu ya namna ya kupata uongozi, la hasha. Hawa wanafanya hivyo kwa sababu ya aina ya pili ya unafsi, ambayo ni fitina.
Hawa wanajaribu kuonyesha kwamba Zitto Kabwe kafanya kosa kubwa kutangaza kugombea urais, lakini hawasemi ni kosa gani na amevunja kanuni gani ndani ya chama. Wengine wameenda mbali zaidi na kumuona Zitto kama ni msaliti ambaye amenunuliwa ili kukidhoofisha CHADEMA.
Hii ni fitina na ni aina mbaya kabisa ya unafsi na tabia inayojitokeza vile vile katika uliberali uchwara. Nina wasiwasi kwamba watu wanaompinga Zitto kwamba nao labda wana watu wanaodhani wanafaa kuwa marais na wanajaribu kumchonganisha Zitto na jamii, ili hatimaye njia yao ya kuusaka urais iwe nyeupe huko mbele.
Katika mfumo wa kidemokrasia za kiliberali kutangaza kugombea urais hakupaswi kuleta mzozo wala vurugu katika chama. Wakati mwingine kitendo cha Zitto ni jibu kwa wapinzani wa CHADEMA aina ya Samuel Sitta wanaojaribu kujenga taswira ya hovyo kwamba ndani ya CHADEMA hakuna wenye uwezo wa urais zaidi ya Dk. Slaa aliyegombea kwa mafanikio mwaka 2010.
Kwa hiyo, wakati huu ambapo CHADEMA haina mwongozo elekezi juu ya namna ya ‘kuutaka' urais, kutangaza kuutaka urais mapema ndio demokrasia yenyewe . Kwa hiyo tunapaswa kuwatia moyo wanachama wengine wenye matamanio ya urais watangaze wakati wowote na mahala popote wanapojisikia, wakati tukiweka misingi murua ya namna ya kupata mgombea mwafaka kwa wakati husika kutoka kwenye kundi la hao wanaojitangaza au wengine.
Kwa hiyo, wosia wangu wa leo ni kwamba kutangaza kugombea urais mapema hakupaswi kuleta mzozo au vurugu katika chama cha kidemokrasia kama CHADEMA. Ndiyo kusema hakuna sababu ya kupachika watu majina ya kifitina wanaotangaza kuutaka urais sasa na baadaye.
Muhimu ni kuweka mfumo utakaohakikisha kwamba CHADEMA hakizidiwi na nguvu za mfumo wa uliberali uchwara ambao umetamalaki nchini, ili hatimaye chama ndicho kiamue nani anakuwa mgombea.