SoC04 DIRA 2050: Umuhimu wa kuboresha mfumo wa uchaguzi na uteuzi wa viongozi wetu ni hitaji la lazima

Tanzania Tuitakayo competition threads

Mjukuu wa Hassan-Juma

Senior Member
Dec 3, 2022
112
96
Dira ya taifa kuelekea mwaka 2050 ni hatua muhimu sana itakayotoa taswira na muelekeo wa taifa kwa miaka takriban 25 ijayo. Umuhimu wa kuwa na malengo ya muda mrefu ya kitaifa ni nafasi nzuri ya kuiandaa kesho ya taifa kwenye nyanja tofauti ikiwemo kiuchumi, kielimu na hata kimaadili na kadhalika. Lakini pamoja na yote hayo, haipingiki kwamba utekelezaji wa mipango yote ya serikali itakayopatikana ndani ya dira hii utaegemea sana kwenye ufanisi wa mfumo wa utawala na uongozi bora ili tuweze kupata matunda yaliyotarajiwa. Kwasababu hiyo, lengo la makala hii ni kuonesha changamoto ya utendaji kazi ya mfumo wa kiutawala wa sasa na kuhamasisha umuhimu wa kuwa na mfumo imara zaidi wa upatikanaji wa viongozi na watumishi wa umma.
png-transparent-flag-of-tanzania-graphy-others-flag-national-flag-tanzania.png

Bendera ya Tanzania (Picha mtandao)

Mfumo wa utawala huwa unafanya kazi kama mwili mmoja ambapo ukamilifu wa utekelezaji wa majukumu huwa unategemea ufanisi wa kila kiungo katika mwili husika. Maumivu au kukosekana kwa kiungo fulani lazima kutaathiri utendaji kazi wa mwili mzima! Labda tujiulize maswali haya kwa pamoja, ni mara ngapi zaidi tutaendelea kusikia wizi na ubadhirifu wa pesa za umma bila wahusika kuchukuliwa hatua?! Au ni mara ngapi watendaji wa chini wa serikali wamewahi kukwamisha malengo ya viongozi wao wa juu kwa kutotekeleza kisawasawa maagizo waliyopewa aidha kwa uzembe au kukusudia?! Ni mara ngapi mawazo bunifu ya viongozi wetu yamekuwa yakikosolewa kwa kukosa tija na maono?! Halafu tujaribu kuwaza kwa pamoja shida yetu kama taifa inaweza kuwa ni nini...

Majibu yafuatayo hayawezi kuwa mbali na ukweli wa tatizo letu linapoanzia! Kwanza hatuzalishi viongozi bora kama taifa, yaani mfumo wa upatikanaji wa viongozi wetu ni huru mno kiasi kwamba yeyote kutokea kokote anaweza kuwa kiongozi akijisikia au bahati ikimdondokea. Pili, hatuna viongozi wenye haiba (Character) ya uongozi, na namna yetu ya kupata viongozi haichongi dhamira ya pamoja ya viongozi kama wataalamu wa kada zingine wanavyoandaliwa. Tatu, hatujihusishi kabisa na uwezo wa kiakili wa mtu ili awe kiongozi wetu, sisi hilo hatuna muda nalo kabisa, ilimradi anaweza kuhema na kunena tukafurahi na tayari ana historia fulani kisiasa basi tayari kwetu inatosha kabisa yeye kuwa kiongozi wetu!
pngtree-tanzania-flag-transparent-watercolor-painted-brush-png-image_2156586.jpg

Picha mtandao

Sasa je, madhara yake ni nini?! Madhara ni mengi sana ambayo kimsingi yanazalishwa na kuzembea kwetu kuweka umuhimu kwenye hatua za awali kabisa za kuandaa viongozi. Miongoni mwa "majanga" hayo ni pamoja na yafuatayo; Mfumo wa utawala unajengwa na watumishi wengi wenye dhamira tofafuti ndani ya mfumo huo. Baadhi wana dhamira ya kweli ya kuongoza kwa dhati, wengine wamo ndani ya uongozi kwa ajili ya kutafuta heshima na umaarufu kwenye jamii, na wengine wapo humo ndani kuchuma mali za wote kuwa za kwao na bahati mbaya sana hawa ndio wengi! Lakini pia kwasababu viongozi wengi hatuwaandai, wengi wao hawana haiba ya uongozi! Hawafikirii kama inavyopaswa, hawaguswi na uchungu wa kuharibika kwa jambo la kitaifa, na wala hawabuni mawazo mbadala ili kuboresha hali za wananchi.

Bado matatizo hayaishii hapo, muundo wetu huu unakwenda mpaka kuathiri mifumo ya uwajibishaji kwa viongozi waliokiuka maadili ya utumishi wa umma! Utamfanya nini mtumishi asiye muadilifu wakati unajua kabisa kuwa karibia asilimia 80 mfumo wetu unafanya kazi kwa muundo huo?! Salama yako kama muwajibishaji iko wapi?! Na hapo sasa ndio utasikia huyu kaiba milioni 150 kasimamishwa kazi! Mara yule amejikopesha bilioni kadhaa na hajarudisha. Na huyu ameiba mashine ya X-ray ameuza, yaani hata utu hakuna tena! Umegundua chochote nikushangaze?! Bado haohao waliogundulika kuwa na makosa kwenye utumishi kesho wanaweza kuteuliwa tena kuwa viongozi kwenye nafasi nyingine au kubaki kwenye utumishi wa umma na wataendelea na maisha yao. Unaweza kushawishika kuamini kwamba, ni rahisi mno kuwa kiongozi Tanzania kuliko kukodi fremu Kariakoo!!
pngtree-tanzania-flag-waving-3d-illustration-png-image_6109295.png

Picha mtandao

Mtu anayejua kwamba amepata nafasi ya uongozi kirahisi, na hata akiondolewa bado anaweza kurudishwa tena uongozini wakati wowote bila kujali historia yake ya mwanzo, kwanini asile rushwa?! Kwanini kati ya milioni 300 ya ujenzi wa zahanati yeye asichukue milioni 50. Hata tuandae mawazo "matamu" kiasi gani kwenye dira ya taifa, bado kilichotukwamisha kwenye mawazo tuliyonayo leo sio udhaifu wa mawazo yenyewe tu, bali wingi wa viongozi na watumishi wa umma wasio na dhamira nzuri ya kujenga nchi. Hapa ndipo jahazi yetu iliponasia! Tufikirie kwanza tunafanya kazi na nani kabla ya kufikiria tunaanza na jambo gani.

Ni muhimu kueleza kwamba viongozi wanaotajwa hapa sio viongozi wa kisiasa peke yao, kwamba ni wabunge na mawaziri au madiwani peke yao, hapana! Bali ni viongozi ndani ya mfumo mzima wa utendaji kazi wa dola ni lazima waangaliwe upya namna wanavyopatikana! Angalia wanajeshi wanavyopatikana, madakatari wanavyopatikana na kada zingine, huko kote utaona kuna mchakato muhimu wa kuupitia kabla hujatunukiwa heshima utakayoipata, je viongozi wetu wanapitia mchakato gani?! Kama uongozi ni heshima na mamlaka itakayotiiwa basi ni lazima iwekewe muundo wa kuipata hiyo heshima husika ili wenye nayo waitumikie huku wakijua kabisa wakiipoteza sio rahisi kuipata tena.

Kama taifa tunahitajika kurudi tena kwenye ubao wa mkakati (drawing board) ili kutafuta namna ya kujinusuru kwenye tatizo hili. Tuandae muundo imara wa kuteua na wa upatikanaji wa viongozi. Muundo utakaozingatia uwezo wa asili na akili bunifu ya mtu husika, uzoefu wa mtu kwenye uongozi ili kudhibiti balehe ya uongozi. Lakini pia kuboresha viwango vya kielimu kwa wagombea nafasi za kisiasa ili kuendana na mahitaji halisi ya nafasi husika. Tuondokane na huu utaratibu wa sasa wa kwamba yeyote anaweza kuamka asubuhi na ameteuliwa kuwa waziri, au tayari ni mkurugenzi shirika fulani. Au yeyote anaweza kuwa diwani kwa kuangalia tu ushawishi wake kwa wananchi au wateuzi na kupuuza kabisa tathmini ya uwezo wake wa kuongoza!
pngtree-tanzania-flag-with-pole-png-image_4749881.png

Picha mtandao

Kwanini mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi kirahisi?! Mtu anaweza kununua ushawishi wa wapiga kura akapigiwa kura akashinda. Anaweza kuishi mpaka miaka 55 akiwa mfanyabiashara, ghafla tu anawaza kuwa kiongozi na anakuwa. Ni utaratibu huu mnadhani tunaweza kwenda nao kwenye dira ya taifa 2050?!

Tunahitaji kuandaa mfumo mmoja, utakaofanya kazi kama mwili mmoja, kwa kutumia watumishi waliondaliwa wenye dhamira moja ili kuhuisha ufanisi na kasi ya maendeleo.
 
Mfumo wa utawala huwa unafanya kazi kama mwili mmoja ambapo ukamilifu wa utekelezaji wa majukumu huwa unategemea ufanisi wa kila kiungo katika mwili husika. Maumivu au kukosekana kwa kiungo fulani lazima kutaathiri utendaji kazi wa mwili mzima
Hui ndiyo ukweli, na ndio maana tunapokuja kuzungumzia viongozi kutotimiza wajibu au kuharibu kitu xyz lazima pia kwa nguvu ileile mwananchi atimize wajibu zake katika abc. Ndipo mwili ukamilike na kukuwa na AFYA.

Tatu, hatujihusishi kabisa na uwezo wa kiakili wa mtu ili awe kiongozi wetu, sisi hilo hatuna muda nalo kabisa, ilimradi anaweza kuhema na kunena tukafurahi
Daaah ni masikitiko tena wengine hata kuhema vizuri hawajui, anaongea hadi pumzi inakata.😆.


Tuandae muundo imara wa kuteua na wa upatikanaji wa viongozi. Muundo utakaozingatia uwezo wa asili na akili bunifu ya mtu husika, uzoefu wa mtu kwenye uongozi ili kudhibiti balehe ya uongozi. Lakini pia kuboresha viwango vya kielimu kwa wagombea nafasi za kisiasa ili kuendana na mahitaji halisi ya nafasi husika
Hakika bro, hakika kila wakati apatikane mtu bora zaidi kwa nafasi husika.

Tunahitaji kuandaa mfumo mmoja, utakaofanya kazi kama mwili mmoja, kwa kutumia watumishi waliondaliwa wenye dhamira moja ili kuhuisha ufanisi na kasi ya maendeleo.
✔👏👏
 
Hui ndiyo ukweli, na ndio maana tunapokuja kuzungumzia viongozi kutotimiza wajibu au kuharibu kitu xyz lazima pia kwa nguvu ileile mwananchi atimize wajibu zake katika abc. Ndipo mwili ukamilike na kukuwa na AFYA.


Daaah ni masikitiko tena wengine hata kuhema vizuri hawajui, anaongea hadi pumzi inakata.😆.



Hakika bro, hakika kila wakati apatikane mtu bora zaidi kwa nafasi husika.


✔👏👏
Shukran sana bro! Mawazo yetu ndio nguvu yetu.
 
Back
Top Bottom