Pole na uchovu wa safari na kuendesha chombo kwa umahili mkubwa, hata hivyo mimi mmoja wa abiria wako nina swali moja tu, je Lori letu linaelekea wapi??
Wala hata usikasirike dereva wangu najua umechoka japo hukubali kamwe kuchoka, je tupo eneo gani na tunaelekea wapi?? maana huku nyuma hatuoni na giza limeingia mbaya zaidi kondakta wa gari kagoma kutoa ushirikiano na abiria hadi wengine wamepitiliza vituo, si ulisikia zile kelele? Abiria wenye busara wamemshauri aombe msamaha kagoma basi kaombewa msamaha japo abiria bado wamenuna!
Ndiyo nauliza tu dereva maana huko nje kelele za wapiga debe zinanichanganya sana, sijajua je ni njaa nzao ama mapenzi yao kwa dereva na lori ndo vinawasukuma ama ni chuki zao tu kwa wasiotaka tuendelee na safari na lori lako??
Dereva jitokeze sema nasi abiria na mioyo yetu ipone maana wapiga debe wanatuchanganya na kondakta maelezo yake yanatuchanganya pia kwani ni giza hatuoni, je askari usalama barabarani ni kweli wamekamata lori? Shiida ni nini, mwendo kasi maarufu kama kupigwa tochi?, mzigo umezidi?, huna leseni au tatizo nini?? Tuna haki ya kujua kama abiria wako.
Dereva wetu pamoja na hayo njaa kali sana kwani mara kadhaa umegoma kupitia hotelini ikiwa unataka tuwahi safari, lakini je hata kuchimba dawa haraka gani dereva wetu hiyo??
Ni hayo tu dereva najua kazi yako si rahisi, abiria wengi wana hasira sana jitokeze sema neno kwa upole waeleze tuko wapi na tunaelekea wapi?? wengi wanahisi lori linapoteza mwelekeo!