Lady Jay,
Pole kwa kutooombwa samahani, lakini sio wanaume wote wenye tabia ya kutoomba msamaha wanapokosea. Kuomba msamaha ni utamaduni ambao mtu anaujenga polepole kutokana na malezi au mazingira aliyopitia kama nyumbani, mitaani, shuleni, kazini na makundi aliyokulia. Kama alizaliwa na kukulia katika mazingira ambao aliona baba yake au wanaume hawaombi msamaha wake zao, au wanawake kwa ujumla, itakuwa vigumu kwake kuomba msamaha. Au kama baba yake alimuaminisha kwamba, wewe ni mwanaume usijilegeze kwa mwanamke ikiwemo kuomba msamaha, itakuwa ngumu kwake leo kuomba msamaha.
Lakini pia, kwanini kwako wewe kuombwa msamaha ni muhimu sana kwako, ili hali wanawake wengine hawana shida hata wakikosewa bila kuombwa msamaha?. Yawezekana ulishajenga utamaduni kwamba anayekosea ni wajibu wake kuomba msamaha, haijalishi ni mwanaumeau mwanamke. Yawezekana hili wewe umeliona wakati wa malezi na makuzi yako kwamba mfano ulimuona baba alimuomba mama yako (Ni mfano tu), nawe ukaona kwamba ndio mtindo wa maisha. Jifunze kuwa 'open minded' kwamba sio kila kinachofanywa na mwanaume wako sasa basi chaweza kufanywa na wanaume wote wengine. La hasha.