CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) kimesisitiza kuwa, mgomo wake uliopangwa kuanza leo upo palepale.
Hatua hiyo ya CWT imekuja siku moja baada ya Serikali kutangaza kuwa mgomo huo ni batili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Rais wa CWT, Gratian Mukoba ameitaka Serikali kuacha vitisho dhidi ya walimu.
Alisema kuwa Serikali imekuwa ikiwalazimisha walimu kujaza fomu zinazowataka kuorodhesha majina yao na shule wanazofundisha na kueleza kama wanaunga mkono mgomo huo au la.CWT imesema walimu wanatakiwa kushiriki mgomo huo kwa kuwa ni halali na umeitishwa na chama hicho kwa kufuata taratibu zinazotakiwa.
Mukoba alisema, Baraza la CWT lilitoa notisi ya saa 48 kuanzia jana (juzi) saa 8 mchana, ambayo inamalizika leo saa 8 mchana, kisha kutangaza rasmi kuwa utekelezaji wa azma yao ya kugoma unaanza kesho.
Walimu wataanza mgomo rasmi Jumatatu (kesho), kwa kubaki nyumbani bila ya kwenda kazini hadi watakapotaarifiwa vinginevyo na Rais wa CWT, alisema Mukoba.
Alisema kuwa, wanachama waliopiga kura kuamua kuwepo kwa mgomo walikuwa 183,000 ambapo kati yao 153,000 waliunga mkono azimio hilo wakiwa sawa na asilimia 95.7 ya wanachama, hivyo kuhalalisha mgomo huo.
Hata hivyo, Mkoba alisema kuwa mgomo huo hautahusiana na zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 26, mwaka huu ambapo aliwataka walimu kushiriki kikamilifu.
Walimu wanahakikishiwa kuwa mgomo hautaathiri utumishi wao kwa kuwa umezingatia sheria, ingawa tunategemea kuwapo kwa vitisho na propaganda nyingi kutoka kwa waajiri wetu, alisema Mukoba.Mukoba alieleza kuwa mgogoro uliotangazwa na walimu kupitia CWT ulishindikana kusuluhishwa na msuluhishi aliyeteuliwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
"Nawataka walimu wote nchini kuungana na kuhakikisha kuwa mnashiriki zoezi hili lenye lengo la kumshinikiza mwajiri wetu (Serikali) kusikiliza madai yetu," alisema.
Alhamisi wiki hii CWT ilitangaza mgomo wa walimu nchi nzima kupinga Serikali kushindwa kuwatimizia madai yao ya siku nyingi ikiwamo ongezeko la mishahara.
Madai ya walimu
Madai ambayo walimu wamekuwa wakiitaka Serikali kuyatafutia ufumbuzi ni pamoja na ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho ya kufundishia kwa walimu wa Sayansi asilimia 55, asilimia 50 kwa walimu wa masomo ya sanaa na posho kwa walimu wanaoishi katika mazingira magumu.Mgogoro kati ya CWT na Serikali umedumu kwa zaidi ya miaka mitano sasa, ambapo licha ya ahadi ya kulipwa madai hayo, fedha zimekuwa hazikidhi ukubwa wa tatizo na kusababisha madeni kurundikana.