Chapa ya Mnyama

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,136
4,298
Chapa ya Mnyama

Mrefu tena mpole,rangiye ya kupendeza
Rangi kama ya vipele,manyoa ya kuteleza
Wale wazee wa kale,wao walipendekeza
Chapa ya huyo mnyama,yafaa wakilogewa.

Mwenye mwendo wa maringo, na mwili ulonyooka
Ndefu sana yake shingo,matawini inafika
Hawa walishwa uongo,kumbe wamelaanika
Chapa ya huyo Mnyama,ndio waliyologewa.

Hata wakidhulumiwa,watabaki wanacheka
Na kama wakiuliwa,wenyewe watajizika
Mikate wakigawiwa,yote yanasaulika
Chapa ya huyo Mnyama,ndio waliyologewa.

Bidhaa wakiuziwa,kwa bei iliyo ghali
Wataona ni maziwa,na wanalishwa asali
Hao walipuuziwa,kisa hawana akili
Chapa ya huyo Mnyama,ndio waliyologewa.

Wao ni kama samaki, wanalia baharini
Wakipewa hata laki,waona mamilioni
Wanachoamini haki,eti kwao ni amani
Chapa ya huyo Mnyama,ndio waliyologewa.


Akija mzinduaji,wamuita msaliti
Akifika msemaji, wamuona mamluki
Hawa kweli wafamaji,wao nzi siyo nyuki
Chapa ya huyo Mnyama,ndio waliyologewa.

Shida ya wadanganyika,ni sukari na vitenge
Matumbo yakizajika,wanakuwa kama kenge
Mchana watazunguka,huku wameshika mwenge
Chapa ya huyo mnyama,ndio waliyologewa.

Kumtawala mjinga,kuna hitaji akili
Kwa kiroba cha mpunga,utamfanya jahili
Akili utamfunga,umgeuze tumbili
Chapa ya huyo mnyama,ndio waliyologewa

Kuwatawala werevu,kwa hitaji sana nguvu
Tena nguvu na mabavu,hata bunduki na nyavu
Ila kweli wapumbavu,hutishiwa na siafu
Chapa ya huyo Mnyama,ndio waliyologewa.

Chapa ya mtema kuni,balaa imeongeza
Hata nembo ya shambani,ngoma yake twaicheza
Kwa wazee I moyoni,vijana wanaibeza
Chapa ya huyo mnyama,ndio waliyologewa.



Ila muda utafika,na chapa zitaondoka
Watu watakusanyika,mikononi wameshika
Midomo itafungika,mikono itapayuka
Hapo moto unawake,hakuna wakuuzima.

Idd Ninga.
Arusha,Tanzania
+255624010160
iddyallyninga@gmail.com
 
Back
Top Bottom