SoC02 Changamoto za mitaala, shule na elimu

Stories of Change - 2022 Competition

Botolani

Member
Jul 23, 2022
6
8
Utangulizi
Habari za wakati huu mwana JF. Karibu kwenye makala haya ya kimtazamo yanayoangazia changamoto za mitaala ya shule pamoja na elimu kwa ujumla.

Katika hali ya kawaida Msingi wa elimu huanzia shuleni ambapo mwanafunzi huanza akiwa hajui kusoma wala kuandika mpaka kufikia hatua ya juu kabisa. Na kinachoongoza na kuelekeza yanayotakiwa kufundishwa shuleni ni mitaala. Kunapokuwa na dosari hasa kwenye sehemu ya mtaala au shule, ni lazima athari zake ziathiri sehemu ya mwisho ya matokeo ambayo ndio elimu. Yani mtaala unapokuwa na shida, tutapata matokeo yasiyoridhisha shuleni na hiyo itaakisi mwishoni kwenye elimu anayotokanayo mwanafunzi.

Katika andiko hili naomba nijikite sana kwenye elimu ya shuleni(darasani). Ukitazama na kulinganisha idadi ya vijana wanaomaliza masomo na kasi ya maendeleo yatokanayo na hilo utagundua kuna ombwe kubwa sana! Utagundua kuwa pamoja na kuwa na elimu lakini bado vijana wamekuwa si mchango toshelevu kwenye ustawi wa taifa kutokana na elimu zao. Na kwakuwa elimu ni matokeo ya mitaala na shule,basi shida hii inaanzia huko. Tuangazie mapungufu hayo moja baada ya jingine kabla ya kufikiria nini cha kifanya;

Mapungufu ya mtaala
1. Moja kati ya mapungufu makubwa sana ya mitaala yetu ya elimu ni kwamba tunahamasisha ukumbukaji (remembering) na sio ufikiriaji (thinking). Mpaka leo hii kwenye mitaala yetu asilimia kubwa ya mambo yanayoelekezwa yafundishwe shuleni ni kuhusu kukumbuka historia, majina, michakato, kanuni, hatua na kadhalika. Ndiomaana ukitaka kufaulu, unaambiwa unatakiwa ufanye maswali mengi ya mitihani iliyopita ili ujaze kumbukumbu za kutosha za majibu kichwani.

Tatizo la kujaza kumbukumbu ni kwamba unapokutana na kitu kipya huwezi kukishughulikia hatakama ni kipo ndani ya eneo lako ulilosomea. Na matokeo yake ndio haya ambayo tunaona leo, tuna taifa la wachapakazi lakini hatuna ugunduzi/uvumbuzi wowote ule, tunaagiza kutoka nje mpaka vijiti vya kuchokonolea meno! Tuna matatizo mengi nchini lakini malalamiko ni mengi kuliko fikra na mbinu za kutatua. Mfumo huu unatufanya tuwe tegemezi wa kutatuliwa matatizo yetu na watu wengine.

2. Uzingatiwaji mdogo wa vipawa(genius) vya tofauti na lugha na mahesabu. Mitaala yetu ya elimu inazifanya shule ziegemee zaidi kwenye wanafunzi wenye aina mbili tu za vipawa ambazo ni kipa wa cha lugha na kipawa cha mahesabu au namba (logic), hao ndio mfumo wa shule unawapatia tija na kuwaacha wengine wenye vipawa kamavile muziki,uhusianojamii, picha, michezo ya mwili na ubunifu wa kimazingira.

Hawa wote mfumo wa elimu yetu ya kawaida hauwatambui na huwaacha njiani wakiwa hawana muelekeo kabisa. Wachache wenye bahati ndio hufanikiwa kutoka kupitia mifumo isiyo rasmi na kuonyesha uwezo wao lakini bado wanachukuliwa kuwa ni watu walioamua kufanya wanachofanya baada ya kufeli shule. Lakini ukweli ni kwamba hawakufeli shule ila shule ndio iliwafeli wao kwakuwa walikuwa tofauti na shule ilivyozoea. Pia mara nyingi wanakuwa hawana sifa za kiushindani duniani kwakuwa wanakuwa sio rasmi kwa kukosa kupita darasani.

Ndio maana miaka nenda-rudi hatuna wanamichezo wakubwa wa kitanzania huko duniani, hatuna wabunifu wakubwa wa kitanzania huko duniani,hatuna wachezafilamu au waongoza filamu wakubwa huko duniani, hatuna wapiga picha wakubwa huko duniani,hatuna wachoraji wakubwa huko duniani. Na hizi shughuli zote ni miongoni mwa shughuli zinazowaingizia watu pesa nyingi sana huko duniani. Na sio kwamba nchi hii haina hao watu wenye uwezo wa kufanya mambo hayo,wapo lakini wametupwa huko mtaani baada ya kuonekana wameshindwa shule.

3. Kutumia muda mrefu kufundisha vitu vichache/kidogo kidogo. Hili nalo kwa upande wangu ni tatizo jingine, sioni sababu ya kuwa na miaka saba shule ya msingi inayofuatiwa na miaka mingine minne ya sekondari kisha miwili ya sekondari ya juu halafu miaka mitatu mpaka minne ya chuo.

Ukipiga mahesabu hapo ni jumla ya miaka 17 mtu yupo shule tu, ikiwa alianza shule akiwa na miaka saba maanayake atamalizana na mambo ya shule akiwa na miaka si chini ya 27 hadi 28, miaka saba tu imebaki ili atoke kwenye kundi la vijana! Hapo ungeweza kutegemea kwa miaka yote hii basi mtu akitoka hapo awe na uwezo mkubwa sana wa kiakili kutatua changamoto tulizonazo. Lakini kinyume chake,baada ya miaka 17 anaingia mtaani na kuanza kulalamikia hakuna ajira, au hata akiwa na sifa za kuajiriwa au kujiajiri,atatumika kwa muda mchache tu kwakuwa umri umeenda.

4. Lugha ya kufundishia. Moja kati ya mijadala ambayo ina mivutano ni kuhusu lugha inayotumika kufundishia hapa nchini. Kwa sasa kinatumika kiswahili kwa shule za msingi, baada ya hapo ni kiingereza kwenye ngazi zote za elimu.

Hii inawapa changamoto wanafunzi wanapoingia ngazi ya sekondari kwakuwa wanakutana na kiingereza kwenye kila kitu ambacho awali walijifunza kwa kiswahili, licha ya kuwa mada nyingi zinakuwa ni marudio au mwendelezo lakini lugha inafanya mambo kuonekana kuwa mageni kabisa kwao na hata yale masomo waliyokuwa wakifaulu wanajikuta wakianza kufeli na wengine huanza kuchukia shule kabisa.

Unakuta mwanafunzi alitoka akiwa yupo vizuri sana shule ya msingi lakini kufika sekondari anaanza kuharibikiwa. Wengine miaka yote ya sekondari wanapambana kujifunza kiingereza mpaka wakianza kujua kidogo tayari mtihani umekaribia na hatimaye anafeli. Na wakatimwingine wanalazimika kukariri bila ya kuelewa ilimradi tu afanye mtihani, huyu anaweza kufaulu lakini akifika kwenye mazingira ambapo sasa anatakiwa kufanyiakazi alichokisoma inakuwa ngumu kwake.

Mapungufu ngazi ya shule
1. Vitendeakazi. Changamoto kubwa kwenye shule zetu ni vitendeakazi vya kuwezesha hiyo mitaala kufuatwa na kufanyiwakazi. Wakati mwingine mtaala uneweza kuwa umeelekeza jambo zuri na namna ya kufanyika kwake lakini kwa kukosekana vitendeakazi wanafunzi wanajikuta hawapati kile hasa wanachostahili kupewa shuleni. Mfano; mitaala ya shule za sekondari inaelekeza mwanafunzi ajifunze na afanye mtihani wa vitendo kupitia maabara ya shule lakini shule nyingi unakuta hazina maabara au zina maabara lakini hazina vifaa husika.

2. Kufundisha sana nadharia kuliko vitendo. Elimu ya vitendo kwa sasa imekuwa mfu kwenye shule zetu, wanafunzi wanapewa maelezo tu bila kushiriki au kuonyeshwa kitu halisia. Na hii mojawapo pia ya matokeo ya kukosekana kwa vitendeakazi vya kufundishia. Mfano somo la TEHAMA limekuwa likihamasishwa sana sikuhizi tangu kwenye shule za msingi lakini wanafunzi wanafundishwa kompyuta kwa kutumia maneno na michoro ya ubaoni tu. Sehemu ambayo angalau wanafunzi wanapata kujifunza kwa vitendo ni ngazi ya chuo.

Lakini tatizo linakuwa ni kwamba wanakimbizana na muda,kunakuwa na mambo mengi ya kufanya ndani ya muda mfupi. Hili linasababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendana na hiyo kasi na kuishia kufeli na wengine wanahitimu wakiwa hawajui kwa hakika namna ya kutenda vitu walivyojifunza darasani. Nimewahi kukutana na wahitimu wengi wa vyuo ambao baada ya kumaliza chuo wanaenda kutafuta kozi za muda mfupi ili ndo wakajifunze utendaji wa kitu kilekile walichokisomea.

Nini kifanyike
Kutokana na mapungufu haya, tunahitaji kufanyakazi ya kurekebisha na kuweka mambo sawa ili mfumo wetu wa elimu uwe na tija. Baadhi ya mambo muhimu tunayotakiwa kurekebisha ni;

1. Kufanya mitaala yetu ichochee na kuleta hamasa zaidi kwenye eneo la kufikiri kuliko kukumbuka. Watu wengi hudhani akili ni kumbukumbu ya mambo,lakini ukweli ni kwamba akili ni uwezo wa kufikiri na kuchanganua mambo. Haitotusaidia sana kujua kutaja sehemu za mti au jani,bali itatufaa kama tukianza kufikiri tunawezaje kutengeneza kidonge cha kutibu homa kwa kutumia mti au jani hilo.

2. Mitaala itoe kipaumbele pia kwenye vipawa vingine vya tofauti na lugha na hesabu tangu mwanzo kabisa mtu anapoanza shule. Tunaweza kuwa na shule za muziki,sanaa za ubunifu,michezo ya mwili na kadhalika ambapo mwanafunzi atajifunza tangu awali kabisa mpaka kufikia ngazi za juu. Shule hizi zinaweza kutengwa na kuwa shule zinazojitegemea zenyewe kama shule zingine au vikateuliwa vyumba kadhaa vya madarasa kutoka kwenye shule zilizopo ambapo humo wanafunzi watafundishwa kusoma na kuandika kama wengine lakini watatofautiana masomo mengine kulingana na vipawa vyao. Mfano; kama tuna darasa la kwanza mpaka la saba la kawaida,basi tuwe na darasa la kwanza mpaka la saba la muziki,sanaa,michezo na kadhalika.

3. Kupunguza idadi ya miaka kwenye mfumo wa elimu na kufundisha yale mambo muhimu yenye tija tu kwaajili ya kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuitumia elimu yake kutatua matatizo. Hili linaweza kufanywa kwa njia mbili, aidha kupunguza idadi ya madarasa; yaani badala ya kuwa na darasa la kwanza mpaka la saba, kuwe na darasa la kwanza mpaka la tano. Au kuweka madarasa zaidi ya moja ndani ya mwaka mmoja; kwa mfano kuweka madarasa mawili mawili kila mwakan. Hii itasaidia kuwapata wasomi watakaokuwa na muda mwingi wa kulitumikia taifa ipasavyo na itawahisha maendeleo binafsi na taifa. Pia itasaidia kupunguza mzigo mzito kwa wanafunzi kwa kusoma mambo mengi ambayo pengine sio ya kipaumbele sana.

4. Lugha ya kufundishia iwe moja tu kuanzia msingi mpaka ngazi ya chuo kikuu. Japo mjadala huu ni mrefu, hapa sipendekezi lugha gani itumike ila napendekeza tu kuwa iamuliwe lugha moja itakayoonekana inafaa kwa kuzingatia vigezo vyote ndio itumike kufundishia. Hii itasaidia kuokoa kundi kubwa la watu wanaoachwa njiani na mfumo wa elimu kwa sababu za kubadilika kwa lugha.

5. Kwenye bajeti ya Wizara ya elimu, suala la vitendeakazi na nyenzo za kufundishia liongezewe nguvu na umakini mkubwa. Kwasasa kuna shule nyingi za sekondari za kata karibu katika kila wilaya. Serikali ianze japo kwa kuteuwa shule moja yenye vigezo kutoka kila kata na kujenga maabara ambayo itakuwa ikitumika kwa kushea na shule zote za wilaya husika kwaajili ya kutoa nafasi kwa wanafunzi ilimradi tu wapate kujifunzia kwa vitendo. Wakati huohuo juhudi ziendelee kufanyika kuhakikisha kila shule inajitosheleza kwakuwa na vitendeakazi vyake yenyewe.

6. Pia suala la kuwa na mtazamo kwamba watu kusomea ualimu ni chaguo la mwisho baada ya kushindwa kupata nafasi ya kufanya vitu vingine liondolewe. Uwalimu isiwe kama kimbilio la watu walioshindwa,bali iwe ni sekta nyeti inayochukua watu ambao wana uwezo mkubwa na waliofanya vizuri kwenye masomo yao. Tuwe na watu ambao wanapata daraja la kwanza na kuchagua kuwa walimu bila shuruti. Na bilashaka hili litatokana na kuwepo kwa mazingira na maslahi shawishi kwa walimu. Natamani katika nchi hii miongoni mwa wafanyakazi wanaolipwa mishahara mizuri na mikataba minono wawe ni walimu.

Mwisho,Kuboresha mazingira ya elimu ni jambo lisiloepukika kwenye nchi yoyote inayotaka kupiga hatua kupitia wananchi wake. Kama taifa hili linayo nia ya dhati ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii,ni lazima tuwe na mfumo wa elimu hapa nchini ambao utapelekea kupata wataalamu na wabobezi wa kutosha wa kutatua matatizo yetu wenyewe. Sijisikii vizuri sana kuona kwamba wale watu wachache tulionao ambao wanafanya mambo makubwa yenye tija kupitia elimu zao ni watu ambao walisoma nje ya nchi. Je watanzania wangapi wanauwezo wa kusoma nje ya nchi?
 
Utangulizi
Habari za wakati huu mwana JF. Karibu kwenye makala haya ya kimtazamo yanayoangazia changamoto za mitaala ya shule pamoja na elimu kwa ujumla...
Hongera sana kwa kufanya uchechemezi huh ambao unafungua fikra zetu na kutufanya tuingie kwenye tafakuri ya kina kuhusu mitaala yetu.

Nakumbuka kabla ya mlipuko wa UVIKO 19 kulikuwa na mijadala mingi kuhusu Mabadiliko na maboresho ya mtaala wetu wa Elimu.

Wizara ilikusanya maoni mengi na yaliundwa makundi ya WhatsApp watu wakatoa hoja zenye mashiko huko. Mpaka sasa mchakato huo hatuelewi umefikia wapi maana hakuna aliyeleta mshindo nyuma wa mijadala ile.

Tuendelee kupaza sauti tutaleta Mabadiliko yenye tija katika maendeleo endelevu.
 
4 Reactions
Reply
Back
Top Bottom