Mkandara,
Kama Watanzania hawatakuwa na nia, utashi na shauku ya kuwa na mabadiliko na kutaka uadilifu na uwajibikaji, hata ukileta na kuunda Temi na falme ndogo ndogo, bado matatizo yatakuwa pale pale.
Jukumu la kwanza kwa Mwananchi kudai haki zake na hata kuhoji pato lake kutokana na jasho lake ni kwa mwakilishi wake katika Serikali, Mbunge.
Je ni jamii, wilaya ngapi ambazo zimedai kwa nguvu kutoka kwa Wabunge wao mgao wa mapato au kuhoji ni kwa nini hawana barabara, maji safi, umeme, shule, hospitali au vyuo?
Ikiwa chaguzi zetu ni kila miaka mitano na mgombea ambaye hutwaa Ubunge hutoa ahadi, je ni lini wananchi wamemshupalia Mbunge wao kudai ahadi zitimizwe? Kuna wengine watadai kisa cha Makwetta, Mzindakaya au Kimitti kuendelea kuwa Wabunge mithili ya kuwa Wabunge wa maisha na kudumu ni kutokana na wananchi kuwa masikini na kukubali kuhongwa.
Sasa swali linakuja, katika miaka 13 ya mfumo mpya wa vyama pamoja na Utamu wa CCM, vyama vya upinzani vimefanya kazi gani kwa umoja kuvunja dhana mbovu ya wananchi kuridhika na Tisheti, Khanga na Ubwabwa na kuendelea kuchagua wawakilishi wabovu?
Narudia tena matatizo makuu yanayosababisha kukwama na kuzorota kwa maendeleo ya Tanzania si mfumo wa utendaji bali ni Udhaifu mkubwa wa Uongozi na Unyonge wa Mtanzania kudai kwa nguvu haki yake bila woga au kuonea aibu.
Kama matatizo haya mawili hayatasawazishwa, kamwe hatutakuwa na uwezo wa kuwa na Maendeleo muafaka kwa Wananchi wa Taifa letu.
La mwisho, sisi tumepata fursa kubwa sana kushiriki katika mchakato wa kulijenga Taifa letu upya. Safari hii inaambatana na kutaka Uadilifu, Uwajibikaji, Ufanisi,Juhudi, Maarifa, Mipango Bora, Haki, Utu, Unyenyekevu Umakini na Uungwana. Haya matakwa si kwa ajili ya viongozi na wanasiasa pekee, ni jukumu letu sote kama kweli tuna nia ya kujenga Taifa imara, lenye uwezo wa kujitegemea na kuushinda Umasikini, Ujinga na Maradhi.
Wengi wetu hapa tuko kwenye safari moja ingawa vipawa, uwezo, maoni na mawazo yetu yanatofautiana. Hilo ni jambo la kawaida kwa jamii.
Kinachosikitisha nami nitakuwa wa kwanza kukiri, ni kule kuwa na unazi wa kuona tusipokubaliana hoja, basi wewe hufai au si mwenzetu. Kukashifiana kuwa fulani ni Fisadi kwa kuwa kahoji mantiki ya jambo, au kuambiwa kuwa ni Kibaraka wa Kikwete au CCM , tumelewa ujamaa, out of touch, mabepari uchwara na kadhalika si sahihi.
Kuna baadhi yetu ambao tunaamini Upinzani ukijengwa vizuri na kwa makini, basi CCM watajifunza na hata kujirekebisha. Kuna wengine wetu tunaamini kuwa CCM ni mama lao na hakuna mwingine kama CCM.
Sasa tukae meza moja hapa ndani katika Jamii na tufundishane pamoja na tofauti zetu za kiitikadi na falsafa kwa kuheshimiana na nia madhubuti ya kusikilizana.
Nawapa Zitto, Mnyika na Kitila ambao wako Chadema jikoni pongezi kwa unyenyekevu wao na busara za kusikiliza kauli zetu na kuzichukua kwa moyo mkunjufu na si kubeza kuwa tunaohoji hatujui tunalolizungumza.
Nawatakia Chadema kila la heri katika safari yao. Mlango wangu wote Zitto, Mnyika na Kitila mnaujua uko wazi. Tuendelee na majadiliano kama tulivyoanza kule kwenye focus 2010 na Chadema must reform.