Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Katavi kimepiga yowe kwa mawakili na asasi za haki za binadamu nchini kujitokeza kwa wingi kutoa msaada wa kisheria kwa kijana Lubamba Geremia Lubamba (21), anayeendelea kusota mahabusu kwa shtaka la uhujumu uchumi lisilo na dhamana.
Taarifa kwa umma iliyotolewa leo Agosti 18, 2026 na Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Katavi, Deus Kamoja, imeeleza kuwa kijana huyo alikamatwa tangu Julai 5, 2026 Mlele kwa tuhuma za uchochezi, kabla ya kufikishwa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Julai 30 na kusomewa shtaka hilo zito la uhujumu uchumi (Shauri Na. 17065/2026).
Kamoja amebainisha kuwa ingawa uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Katavi chini ya Mwenyekiti Rhoda Kunchela tayari umemtafuta Wakili Kenani Chombala kutoka Tabora, uzito wa shtaka hilo unahitaji jopo pana zaidi la mawakili ili kuokoa haki ya kijana huyo.
"Lubamba anaendelea kushikiliwa katika Gereza la Mpanda kwa kuwa shtaka linalomkabili halina dhamana. Tunaendelea kuwaomba wadau wengine wa haki za binadamu kuongeza msaada wa kisheria, ikiwemo kuongeza idadi ya mawakili katika shauri hilo," amesisitiza Katibu Kamoja.
CHADEMA imetoa wito kwa wananchi na watetezi wa haki za binadamu kujitokeza kwa wingi katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda tarehe Agosti 27, 2026, wakati shauri hilo litakapotajwa tena.
#SasaLive #CHADEMA #Katavi #Mpanda #MsaadaWaKisheria HakiZaBinadamu TanzaniaNews