CHADEMA: Ipsos-Synovate Iwaombe Radhi Watanzania, Utafiti wao Upuuzwe, Utafiti wa TADIP una Kasoro

Ben Saanane

JF-Expert Member
Jan 18, 2007
14,581
18,124
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Wanahabari,

CHADEMA na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya wananchi (UKAWA) tumesikitishwa na taarifa ya utafiti wa taasisi ya Synovate iliyotolewa Septemba 24,2015 , na ile ya Taasisi ya Tanzania Development Initiative Programme(TADIP) iliyotolewa Tarehe 25 Septemba ,2015 jijini Dar es Salaam na kuripotiwa na vyombo vya habari jana na leo hii namna zinavyojichanganya,zisivyozingatia uhalisia na kupuuza misingi ya sayansi ya siasa kufanya kile ilichokiita Utafiti .


i) RIPOTI YA TADIP

Wao katika Utafiti wao wanaonyesha kwamba Mgombea Urais wa CHADEMA anayeungwa Mkono na Vyama washirika wa UKAWA kama uchaguzi ungefanyika angeshinda kwa asilimia 54 ya Kura.
Utafiti huu hatukubaliani nao kabisa kutokana na mapungufu mengi yaliyojitokeza katika utafiti huu hasa mbinu za sampuli(sampling technique) iliyotumika. Wao walitumia sampuli holela(Random Sampling) ambayo haionyeshi makundi Rika,Jinsia n.K katika kuhalalisha hitimisho kwani makundi mahsusi ni muhimu sana kwa kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu vijana wamejiandikisha kwa wingi zaidi kuliko makundi mengine na kuliko miaka mingine yote ya uchaguzi,halikadhalika Wanawake
Ingawa haikuwa lengo la utafiti wao kutafuta ushawishi wa makundi mbalimbali lakini ni muhimu sana kama hilo lingefanyika ili kupata hitimisho linaloakisi uhalisia
Ni kutokana na mapungufu kama hayo yaliyopelekea hitimisho ambalo tunaona si sahi kabisa.

Asilimia 54 alizopewa mgombea wa CHADEMA sio sahihi kwani kulingana na Tafiti tatu zilizofanyika zikihusisha taasisi mbalimbali zikiwemo za kimataifa ilionyesha Mgombea wetu angeshinda kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura.
Tunaamini kuwa mapungufu ya mbinu za kisayansi katika utafiti huu ndizo zilizopelekea TADIP kufikia hitimisho ambalo sio sahihi

ii) RIPOTI YA SYNOVATE

Kwani idadi ya asilimia walizopewa wagombea kwa ujumla wao ni 100.3 wakati ilipaswa kuwa asilimia 100 na si zaidi ya hapo na hata ile ya Mgawanyo wa makundi mbalimbali ya kijamii ukijumlisha asilimia zote itaonyesha asilimia 107

Tunashangazwa sana na kutilia mashaka umakini wa Synovate inayojipambanua kuwa ya kimataifa na yenye weledi inapofanya makosa makubwa kama haya ambayo hayahitaji kuwa msomi wa kiwango cha juu kujua kiwango cha mwisho cha asilimia katika utafiti wowote ni 100.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Synovate,Inaonyesha kwamba Kama uchaguzi ungefanyika kipindi walipofanya utafiti basi Wagombea Urais John Magufuli wa CCM angepata 62%, Edward Lowassa (CHADEMA) angepata 31%,Anna Mgwira (ACT-Wazalendo) 0.3 na 7% hawajaamua watampigia kura mgombea gani.Ukijumlisha alama zote jumla utapata asilimia 100.3.

Katika ripoti hiyo hiyo, mbali na mapungufu kadhaa haiakisi uhalisia . Mgawanyo wa makundi mbalimbali katika ripoti yao kulingana na kazi zao imeonyesha ifuatavyo


Mama wa Nyumbani-----------------8%
Walioajiriwa sekta Rasmi ------5%
Waliajiriwa sekata isiyo Rasmi ------------4%
Wastaafu/Waliopo katika Pensheni----------------2%
Wanafunzi-----------------------5%
Waliojiajiri/wamiliki wa biashara--------------27%
Wasioajiriwa lakini wanatafuta kazi----------------4%
Wasioajiriwa lakini hawatafuti kazi---2%
Vibarua---1%
Wakulima-41%
Wengineo-3%

Ukijumlisha asilimia za makundi hayo yaliyohojiwa utapata asilimia 107 badala ya 100. Hakuna weledi katika mchanganuo huu bali ni takwimu zilizopikwa tu mezani tena chini ya kiwango
Mathalani,Katika makundi hayo matatu hapo juu tu yaani Wasioajiriwa lakini wanatafuta kazi,Wasioajiriwa lakini hawatafuti kazi,Vibarua jumla yao kwenye hii ripoti ni asilimia 7 ya waliohojiwa lakini kiuhalisia kundi hili linawakilisha zaidi ya asilimia 30 kwani wanaotafuta ajira rasmi kwa mujibu wa ripoti za serikali ni asilimia 15 ya Watanzania na vibarua ni wengi zaidi jambo linalofanya kundi hili kuwa kubwa na kubeba takribani asilimia 30 ya wapiga kura ambao ni zaidi ya milioni 7.2 kati ya wapiga kura milioni 24 waliojiandikisha kwa mujibu wa ripoti ya tume ya uchaguzi na hawa ndio wanaounga mkono kwa kiasi kikubwa harakati za mabadiliko kupitia UKAWA

Vilevile katika kuchagua sampuli(sample target) utaona kwa mfano baadhi ya makundi hususani kundi la watu waliojiajiri au wamiliki wa biashara(27%) ili kukisaidia chama tawala ingawa hawajasema ni wafanyabiashara wa kada gani kwani wafanyabiashara wa kada ya kati nay a chini wanaunga mkono UKAWA kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini hata soko kuu la Kariakoo

Haya mapungufu machache tu ya kisansi katika hiki kinachoitwa utafiti yanapaswa kuiondoa ripoti hii katika viwango vya ripoti za kisayansi kwani ukifanyika utafiti kama huu mara 100 huwezi kupata matokeo kama hayo hata mara tatu.

Kwa kawaida matokeo ya utafiti uliofuata kanuni na taratibu zote, unatakiwa mwingine akiufanya mara 100, apate majibu kama yale ya utafiti wa awali mara 95. Hiyo kwa kitaalamu inaitwa confidence level, (namna ya kujiaminisha, kuwa na imani na majibu).

Tunapenda kuwakumbusha Watanzania kuwa Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, taasisi hii hii ya Synovate walitoa utafiti ulioonyesha kwamba asilimia 94 ya Watanzania wako tayari kupiga kura lakini baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilitoa takwimu zake zilizoonyesha kuwa waliopiga kura walikuwa asilimia 42 tu. Je,Taasisi hii ina hadhi na kiwango cha kuaminika(credibility) mbele ya macho ya watanzania tena?

Ni vyema Watanzania wakaelewa kwamba mapungufu haya katika ripoti hii si ya bahati mbaya,kwani Taasisi hii imekua na utamaduni wa kutoa ripoti zenye mashaka na zilizokosa kiwango cha uaminifu(Confidence level) katika ripoti zake maeneo mengi barani Afrika hasa nchi za ukanda wa Jangwa la Sahara nyakati za uchaguzi kwani imekuwa ikilalamikiwa mara kadhaa na vyama mashuhuri barani Afrika,Wasomi na wananchi mbalimbali.Nitaorodhesha mifano michache kama ifuatavyo;

i) Katika Ripoti ya Synovate ya Mwezi Oktoba 2011 nchini Ghana ilionyesha kuwa Mgombea wa chama cha Upinzani Nana Akufo-Addo wa Ghana angeshinda uchaguzi mkuu wa Ghana dhidi ya John Evans Atta Mills. Matokeo yalionyesha kinyume chake kwani Prof.Atta Mills na chama chake cha NDC kilishinda kwa kishindo baada ya Wananchi wa Ghana kutoyumbishwa na utafiti huo uliopikwa kama ulivyolalamikiwa na baadhi ya wanasiasa nchini Ghana.

ii) Katika Ripoti yake nchini Zambia mwezi August mwaka 2011 ,ilionyesha kuwa Mgombea Urais Rupiah Banda wa chama Tawala Movement for Multiparty democracy(MMD) angemshinda mgombea wa upinzani aliyekuwa akipendwa na wengi Michael Satta kutoka chama cha Patriotic Movement(PF). Mwezi mmoja baadae yani septemba 20,2011 wananchi wa Zambia walimchagua kwa kishindo Michael Satta kutoka upinzani kuingia Ikulu

iii) Katika ripoti yake nchini Kenya Mwezi Januari 2013,ilionyesha kuwa Raila Odinga angeshinda Uchaguzi wa Kenya ambao ungefanyika miezi miwili baadae dhidi ya Uhuru Kenyatta.Matokeo yake ni kuwa Wakenya walipuuza Ripoti hiyo

iv) Mapema mwezi February mwaka 2012,taasisi hii ilizua mabishano katika siasa za Kenya dhidi ya taasisi nyingine za kiutafiti pale ilipotangaza ripoti yake kuwa 60% ya Wakenya waliunga mkono uamuzi wa Mahakam ya ICC kuendelea na mashtaka dhidi ya Mwanasiasa aliyekua na kashfa nyingi za kuchochea machafuko nchini humo mwaka 2007 baada ya uchaguzi mkuu,huku ripoti ya shirika lingine maarufu la Smart Octopus ikionyesha kuwa asilimia 73 ya wakenya walikuwa hawaungi mkono uamuzi huo.
Matokeo yake Uhuru Kenyatta alitetewa na wakenya na kuaminiwa kiasi ya kupigiwa kura za kishindo na kuwa Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya watu wa Kenya

Tunasikitishwa na jinsi ambavyo taaluma zinatumika kupotosha na kuegemea katika maslahi finyu yasiyojenga demokrasia .Tunajiuliza ,Je ,Taasisi zinazofanya kazi kwa upotoshaji kama huu zinafanya kazi kwa maslahi ya nani?Je,Ni sehemu ya kamati ya watu 32 wa chama tawala ili kuongeza nguvu kupitia propaganda na vita ya kisaikolojia hasa baada ya chama tawala kuelemewa? Je, ni kwa sababu ya mfungamano wa kimaslahi baina ya taasisi na chama tawala iliyopelekea Msemaji wa Chama tawala kwa jina la kalamu(Pen Name) kuwa wa kwanza kuripoti taarifa za utafiti kabla taasisi yenyewe haijatangaza Rasmi kwenye mitandao ya kijamii na pia ripoti kuvuja kwenye vyombo vya habari kabla haijatangazwa Rasmi?

Je,Ni kwa bahati mbaya kimgongano(coincidental) kuwa Taasisi mbili mfululizo za Synovate na TWAWEZA kutoa ripoti zake zikiwa na saizi ya sampuli(sample size) inayolingana yaani 1,836 na 1,848 mtaalia(respectively) na pia matokeo kushabihiana kwa karibu .Je,Ni kwa sababu kuna mtendaji mmoja ambaye anafanya kazi katika taasisi zote mbili kama Meneja Utafiti(synovate) na pia kama Manager,Sauti ya Wananchi-TWAWEZA)?

CHADEMA na vyama washirika wa Muungano wa vyama vinavyounda UKAWA tunaitaka taasisi ya Syonovate iwaombe radhi watanzania, kwani ripoti yao inaonyesha kuwa, wananchi wa nchi hii bado ni mbumbumbu wa kupenda chama au mtu kwa sura yake na wakaendelea kuwa na imani nae hata kama wanatambua fika ameshindwa kuwapatia huduma muhimu, huku ni kuwadhalilisha Watanzania na kazi kubwa inayofanywa na vyama vya upinzani, taasisi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari juu ya kuelimisha umma.

CHADEMA na vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) tunatoa Rai kwa Watanzania kuipuuza Ripoti hiyo kama walivyofanya Wananchi wa Zambia,Ghana,Kenya,Nigeria,Senegal na kwingineko na kufanya maamuzi

Aidha,CHADEMA na vyama washirika wa UKAWA tupo tayari kujifunza kutokana na ripoti za tafiti zilizofanywa kiweledi ili kuongeza bidii katika harakati zetu za kampeni.

Kwa kumalizia,Tunaona kuwa kuna haja ya kuhakikisha Tume ya Taifa ya uchaguzi inatengeneza kanuni zitakazozibana Taasisi ili kuhakikisha viwango bora katika Utafiti vinafikiwa kipindi cha chaguzi kama hizi.Hatuoni haja ya Tume kuzuia tafiti nyingine kufanyika badala yake ingepaswa kutengenezwa kanuni au sheria zitakazoongoza tafiti kama hizi kipindi cha chaguzi

Mwisho,Tunawatahadharisha Watanzania kuwa makini katika kipindi hiki cha uchaguzi, kwani taasisi mamluki zitatumia taaluma zao kuwapotosha na kuwavunja moyo mliokuwa nao wakukataa ufisadi na dhuluma inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi dhidi ya mali asili na mapato ya nchi, ili siku ya uchaguzi Oktoba 25, wananchi msijitokeze kwa wingi kwa kudhani kuwa CCM bado inakubalika,


TUNAWASIHI WANANCHI WA TANZANIA WALIOJIANDIKISHA KUPIGA KURA, JITOKEZENI KWA WINGI SIKU YA KUPIGA KURA NA MFANYE MAAMUZI SAHIHI YA KULETA MABADILIKO



Imetolewa na :

Ben-Rabiu Saanane,
Idara ya sera na Utafiti-CHADEMA
 
...nakuunga mkono kamanda msomi ben saanane, kwa hoja hizi hata tafiti ya kkoo naiamini zaidi kuliko twaweza na synovet. Naamini mzee Bana ameona aibu kukidhalilisha udsm maana naye angetembea kwenye uongo kama huu. Sisi wapiga kura tunajiandaa na visu vyetu na hakika tutawachinja na tafiti zao wakaweke kwenye makabati yao....
 
Kama mnaamini hizo tafiti ni za uongo si mkae kimya mtulie msubiri matokeo ya uchaguzi. Mnapiga kelele na kutoa matamko kwa vitu visivyokuwa na tija. Ishu kama za wabunge kuongezewa posho wala hata hamkujisumbua kutoa matamko kisha leo hii mnajifanya mnajali sana kwa kutoa matamko kwe tafiti huru za watu. Tafiti hazipingwi kwa matamko, tafiti zinapingwa kwa tafiti.
 
Yawezekana ni makosa ya uchapaji tu tulia wapiga kura ndo wataamua mbona unaharaka sana?
 
Utafiti hupingwa kwa utafiti not otherwise.
Na pia matokeo ya utafiti does not necessarily guarantee aliyeonekana kushinda kuwa watashindwa jamani
 
Kama mnaamini hizo tafiti ni za uongo si mkae kimya mtulie msubiri matokeo ya uchaguzi. Mnapiga kelele na kutoa matamko kwa vitu visivyokuwa na tija. Ishu kama za wabunge kuongezewa posho wala hata hamkujisumbua kutoa matamko kisha leo hii mnajifanya mnajali sana kwa kutoa matamko kwe tafiti huru za watu. Tafiti hazipingwi kwa matamko, tafiti zinapingwa kwa tafiti.
Hawawezi kukaa kimya. Ni lazima waseme ukweli ujulikane. Pamoja na hayo kitu cha muhimi ni kuhakikisha kura hazichezewi siku ya kupiga kura.
 
Back
Top Bottom