Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kuwataarifu Watanzania na jamii ya kimataifa juu ya matukio matatu makubwa yenye athari kwa demokrasia na haki za binadamu nchini Tanzania:
1. Wito Kuhudhuria Kesi ya Mh. Tundu Lissu Kesho, Jumanne 06 Mei 2025 saa 2:00 asubuhi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itasikilizwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mh. Tundu Antiphas Lissu. Kesi hii si ya kawaida. Ni sehemu ya mkakati mpana wa kutumia sheria kwa njia ya kisiasa kukandamiza sauti huru na kuwatisha wapinzani wa kweli.
*Tunatoa wito kwa wanachama, wafuasi, wapenda haki na Watanzania wote kufika kwa wingi kuonesha mshikamano na kusimama na ujasiri wa kisiasa dhidi ya uonevu na vitisho.
2. Bunge la Ulaya Kujadili Hali ya Demokrasia Tanzania
Tarehe 07 Mei 2025, Bunge la Ulaya litafanya mjadala maalum kuhusu hali ya demokrasia na haki za binadamu nchini Tanzania, huku kesi ya Mh. Lissu ikiwa miongoni mwa mambo makuu yatakayoangaziwa.
Tarehe 08 Mei 2025, bunge hilo litapiga kura ya maazimio rasmi kuhusu hali ya kisiasa Tanzania.
CHADEMA inawahimiza Watanzania na marafiki wa demokrasia kufuatilia mjadala huo kupitia vyanzo rasmi. Viongozi wa chama, wanachama na wafuasi wanashauriwa kuandaa maeneo maalum ya pamoja kufuatilia mjadala huo kama sehemu ya kujenga hamasa ya kitaifa.
3. Taarifa ya Udukuzi wa Akaunti Rasmi
Kwa masikitiko makubwa, tunaarifu kuwa akaunti zetu za X (zamani Twitter) - ChademaTZ na YouTube - Chadema Media zimeingiliwa na wadukuzi.
Tunaendelea kuchukua hatua za kiusalama na kisheria kurejesha udhibiti. Kwa sasa, taarifa rasmi za CHADEMA zinapatikana kupitia akaunti ya muda ya X: @ChademaTZ2. Tunaomba wafuasi wawe makini na kupuuza taarifa zinazochapishwa kwenye akaunti zilizodukuliwa hadi tutakapotoa taarifa rasmi ya kurejesha udhibiti.
Kwa pamoja, matukio haya yanaonesha namna haki na demokrasia nchini ziko mashakani. CHADEMA itaendelea kusimama imara na wananchi kwa ajili ya Tanzania yenye uhuru wa kweli, haki kwa wote, na siasa safi isiyozalisha hofu wala ukimya.
Imetolewa leo Jumatatu 05 Mei 2025:
Brenda Rupia
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi
Pia soma Pre GE2025 - John Heche: John Mrema amekimbia na Akaunti za YouTube na X za Chama, tuligundua kila wiki analipwa Tsh. Milioni 3