Boniphace Kichonge
JF-Expert Member
- Jul 31, 2017
- 1,605
- 1,957
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema Tanzana inahitaji vyama vya siasa vitakavyozingatia uzalendo na kuwaunganisha wananchi wote.
Dk Ally ameyasema hayo katika ukumbi wa Shule ya Fidel Castro Pemba alipozungumza na viongozi wa CCM wa mikoa ya kisiwani Pemba.
Amesema vyama vinatakiwa kuweka mbele maslahi ya Taifa na si matakwa ya viongozi. Alisema misingi ya uzalendo ni muhimu kwani itawaunganisha wananchi na kurudisha dhana ya uzalendo kupenda nchi na wananchi wake.
“Tanzania inahitaji vyama vya siasa ambavyo vitaweka mbele uzalendo wa nchi kuunganisha wananchi na kuleta maendeleo,” amesema.
Kwa mfano, amesema uzalendo uliooneshwa na viongozi waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume unatakiwa kuigwa ukiwa ni urithi wa taifa letu.
“Wana CCM mnatakiwa kuiga mfano wa waasisi ambao waliweka mbele maslahi ya taifa kwa kujenga Tanzania ambayo leo imekuwa kimbilio la wengi ikiwemo wageni,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Dk Abdalla Juma Mabodi amesema, kazi kubwa ya CCM Zanzibar sasa ni kuimarisha chama kwa kuingiza wanachama wengi ikiwemo vijana.
“Kazi kubwa tunayoifanya ni kuimarisha Chama Cha Mapinduzi kupitia Jumuiya zake na kuingiza wanachama wengi zaidi,” amesema.
Dk Bashiru yupo Pemba ikiwa ziara yake ya kwanza Zanzibar tangu alipoteuliwa kukiongoza chama hicho.