Wadau Salaam.
Leo asubuhi nilipata wasaa wa kuangalia udondozi wa magazeti kwenye luninga.Taarifa tatu kati ya nyingine nyingi zimenisukuma kuweka haya machache.Matarajio yangu ni kuwa yatasaidia kuibua fikra pana na mjadala chanya juu ya mustakabali wa nchi yetu baada ya kufikishwa hapa tulipo na chama tawala hasa hiki cha miongo miwili iliyopita.
Taarifa ya kwanza ni kuhusu tamko la Mh.Spika Anna Makinda kuhusu haja ya kuwaongezea wabunge mishahara kwa vile wabunge wa zamani wana hali mbaya mithili ya ombaomba.Kwamba Anna Makinda anahusisha kushindwa maisha kwa waheshimiwa hawa na viwango vya jumla vya mishahara ya wabunge sio dhamira ya uzi huu.
La pili ilikuwa taarifa ya hali mbaya ya shule ya sekondari mbagala ya hapa hapa Dar es salaam ambapo taarifa zinasema wanafunzi hawana madawati,wanaketi chini au kwenye ndoo,madarasa hayana sakafu na huduma ya maji na hali ya majengo ya shule hiyo ni duni sana.
La tatu ni taarifa kuwa serikali hii ya CCM imefanikiwa kuwakopa wakulima mazao yao yanayofikia kiasi cha Tshs 1.7 BILIONI!
Nikiwa njiani kuelekea kibaruani nikawa natafakari!
Hivi inakuwaje nchi moja hii hii,ikawa na pengo kubwa la uhalisia wa maisha kiasi hiki?kwamba wakati waheshimiwa wakiwakilishwa na mheshimiwa mkubwa wao (Spika)anaona vimshahara vya milioni saba na ushee,jumlisha na posho ya vikao ya Tshs 330,000/=kwa SIKU,na vijipesa vya Mafuta,Mfuko wa jimbo,ujumbe wa kamati na bodi mbalimbali na posho zake,msamaha wa kodi kwa wateule hawa bado ni kidogo sana kiasi kwamba wanashindwa kumudu ukali wa maisha na wanahitaji kuongezewa!Wakati huo huo,siku hiyo hiyo,nchi hiyo hiyo Tanzania kuna wanafunzi ambao wanakosa madawati ya kukalia!hawana hata maji ya KUNYWA!wanakalia ndoo kwenye madarasa yasiyo na sementi!
Halafu tena,Katika nchi hiyo hiyo,inayo ongozwa na serikali hiyo hiyo ya CCM,Kuna wakulima baada ya kuvuja jasho na damu kwa kilimo cha kujikimu kisicho na tija na kuvuna walichovuna serikali hiyo hiyo imeenda kuchukua mazao yao kwa MKOPO!Tena si kidogo.....BILIONI 1.7!
Nikatafakari zaidi kuwa hali hii iko kila mahali.....Kwenye huduma za afya ambapo watawala wanaenda kufanya check up Africa ya kusini,Amerika na India wakati wakina mama wajawazito wanalala wawili katika kitanda kimoja au chini sakafuni,Kwenye Elimu ambapo watoto wa watawala wanasoma English medium na Cambridge syllubus huku watawaliwa wakisoma kayumba et al,Kwenye uongozi na ajira,kwenye fursa na ushawishi....kila mahali!
Nikatafakari zaidi kuwa haya ni matokeo ya mfumo rasmi ambapo Taifa moja.....la watawala na wapambe wao,wanao nufaika na kuneemeka na utawala huu....na taifa jingine......la watawaliwa.....ambao wao kazi yao ni kuwachumia hawa watawala,kuwa neemesha kwa jasho lao na nguvu zao!wanaishi katika nchi moja!
Angalia bodi ya mikopo ya elimu ya juu,wanao pigana vikumbo kule si watoto wa watawala, ni watoto wa taifa hili la watawaliwa ambao wanakatwa kodi wasiyo itumia...watawala hawakatwi kodi....kuanzia kinara wa utawala mwenyewe!Na kwa vile sisi ni mataifa mawili tofauti katika nchi moja watawala hawawajibiki kwa watawaliwa!ila watawaliwa wanawajibika kwa watawala.
Ndiyo maana watawala wamejipa hali ya kuwa miungu watu,ambapo wanaona kila kitu ni stahili yao.Dhamira zao haziwasuti tena kuona wao wanakula na kusaza wakati jirani zao wanalala na njaa!Hawasumbuki tena na umaskini uliokithiri wa watu wetu kwa vile hauwahusu!Wanashughulika zaidi na matumbo yao kuliko kelele zetu.
Nikatafakari zaidi kuwa hawawezi kusikia kilio chetu kwa vile maumivu yetu hayawahusu,Tukiongeza kelele wao wanasikia "Uchochezi",Tukihoji wao wanaona "Chuki binafsi za wasionacho dhidi ya wenye nacho",Tukijitutumua kujitambua wao wanaona "Uhaini"!
Nilipo endelea kutafakari,Nikakumbuka maneno ya mwandishi Benjamin Disraeli katika kitabu chake Sybil. "Two nations between whom there is no intercourse and no sympathy; who are ignorant of each other's habits, thoughts and feelings, as if they were dwellers in different zones or inhabitants of different planets; who are formed by different breeding, are fed by different food, are ordered by different manners, and are not governed by the same laws ... THE RICH AND THE POOR."
Vinginevyo,Utauelezeaje ulafi huu unao endelezwa na CCM?