CCM Kujivua Gamba; Tafsiri Yangu ( Makala, Raia Mwema, Leo Jumatano)

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Na Maggid Mjengwa,


INAZUNGUMZWA sana mitaani , dhana hii ya CCM kujivua gamba. Najiuliza, je, huku ni ‘ Kuzaliwa kwa Chama ‘kipya’ au kuzaliwa ‘upya’ kwa chama kikongwe? Unaweza kukiona ninachokiona kadri unavyofuatilia mtiririko wa fikra zangu.


Nionavyo, wengi tumebaki tukijadili kilicho juu ya gamba. Hatuzami kuangalia kilichomo ndani ya gamba. Ndio maana, kama kawaida yetu, tumejikita kwenye kujadili zaidi majina ya watu.


Na tujiulize; ni nini hasa maana ya CCM kujivua gamba? Ni bahati mbaya, kuwa neno kujivua gamba linatoa tafsiri nyingi hasi na chanya. Na wakati mwingine, limewahamisha watu kutoka kwenye hoja za msingi juu ya nini kinachotokea . Mimi nitaelezea kujivua gamba kwa kutoa mfano wa nyumba .


Ndio, CCM ni chama kikongwe. Ni kama nyumba kongwe. CCM wanataka kuikarabati upya nyumba yao. Ipate mwonekano mpya. Kuikarabati upya nyumba kongwe huweza pia kupelekea kuibomoa nyumba yenyewe. Kutakuwa na fito na vipande vya matofali vya kurudishia. Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndio, fito na matofali mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima yatupwe, basi. Na hapo utakuwa umeikarabati upya nyumba yako.


Na nyumba kongwe ya CCM kwa sasa imechakaa, haina mvuto. Wengi hawaipendi, na hususan vijana. Hawa ndio hao walio wengi kwenye kupiga kura. Kwa CCM kurudisha imani ya wapiga kura hawa inahitaji kufanya ukarabati mkubwa wa nyumba yake kongwe. Katika Afrika hii kuna kisa cha Chama tawala kilichochukiwa mno na wapiga kura kiasi kikaamua kubadilisha jina na rangi ya bendera yake ya chama!


Turudi kwenye gamba. Hivyo basi, katika kujivua gamba huku, CCM, kama nyumba kongwe inayofanyiwa ukarabati, yumkini inaweza kubomoka. Hayo yatakuwa ni matokeo ya kawaida kabisa. Ndio, kuna watakaondoka na fito na matofali yao, watakwenda kujenga mahali pengine. Na katika mchakato huu wa kujivua gamba kuna mawili nayaona yatatokea; Mosi, CCM Kuzaliwa Upya au pili, Kuzaliwa kwa Chama kipya. Na mawili hayo yakitokea yatadhihirisha ukweli wa alichoandika Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chake; ’ Uongozi Wetu Na Hatima Ya Tanzania’. Hapa kuna mawili, ama kuna Wana- CCM waliosoma kitabu hicho cha Mwalimu bila kukielewa au hawakukisoma kabisa.


Na nini maana ya Kuzaliwa kwa Chama Kipya? Naikumbuka vema Jumamosi ya Februari 5, 1977. Siku hiyo nilibaki na mwezi na wiki moja kabla sijatimiza miaka 11. Ni siku ile Chama Cha Mapinduzi kilipozaliwa. Nikiwa na watoto wanzangu tulikwenda pale ofisi za TANU Ilala Boma kushuhudia tukio lile la kihistoria. Nilichoshuhudia pale Ilala Boma ni ’Kuzaliwa Kwa Chama Kipya’. Niliziona nyuso nyingi za watu wazima zilizojaa matumaini ya siku zijazo, nasi kama watoto, ujio wa Chama kipya ulitujengea matumaini ya baadae.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini.


Na imani ya wananchi kwa viongozi wao ni shina la matumaini yao. Inakuwaje basi mwananchi anapokosa imani kwa kiongozi? Jibu; hukosa matumaini. Atakimbilia popote pale anapoona kuna matumaini. Wahenga walinena; mtoto akikosa titi la mama, atanyonya hata la mbwa. Chama Cha Mapinduzi kihistoria kimekuwa ni kimbilio la wanyonge, lakini sivyo ilivyo kwa sasa.


Na tuamini, kuwa Jakaya Kikwete ameingia katika kazi ya kuongoza Mabadiliko Makubwa ndani Ya CCM. Mwingine atauliza; Je, mabadiliko hayo yatakuwa makubwa kwa kiasi gani? Jibu; ni suala la kusubiri na kuona. Na hapo ndipo tutaweza kutoa hukumu stahili.


Ieleweke, kuwa CCM ni Chama tawala. Kinachotokea ndani ya CCM chaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa taifa letu. Na ndio maana, kwa kutanguliza maslahi ya nchi, tuna wajibu wa kumuunga mkono Rais wa nchi na Mwenyekiti wa CCM katika kazi yake hii.


Nimepata kuandika, kuwa ya CCM yanatuhusu sote, wanachama na tusio wanachama. Kwa sasa, CCM inapitia moja ya vipindi vigumu sana tangu kuanzishwa kwake, hivyo basi, nchi yetu nayo inapitia moja ya vipindi vigumu sana tangu tupate uhuru. Hiki ni Kipindi Cha Mpito kuekelea kwenye mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.


Na hakuna atakayeweza kuyauzuia mabadiliko haya makubwa, maana wakati umebadilika. Chama Cha Mapinduzi kina jukumu la kuyaongoza mabadiliko haya. Na nimepata kuandika, kuwa CCM ina mawili ya kuchagua; kuendanda na mawimbi ya mabadiliko haya, au kukubali kusombwa na kutupiliwa kando.


Yumkini Jakaya Kikwete amezisoma alama za nyakati. Na hakika, sikupata kufikiri, kuwa katika mwaka wa kwanza tu wa awamu yake ya mwisho ya uongozi, Jakaya Kikwete angekifikisha chama chake katika hatua ya kujivua gamba kama tunavyoshuhudia.


Tunaona, CCM imeanza kujivua gamba, lakini hiyo haitoshi. Taifa letu nalo linahitaji kujivua gamba. Na sisi , kama taifa, hatutakuwa wa kwanza, imetokea katika nchi za wenzetu. Kuna mifano hai.


Utawala wa Kikomunisti wa Urusi ya zamani ulianguka mara ile Mikhael Gorbachev alipoanzisha mageuzi makubwa ya kimfumo kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi. Mabadiliko haya makubwa ya kimfumo yalipata majina mawili; Perestroika na Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya na Glasnot ni uwazi .


Kabla ya mageuzi hayo makubwa, Urusi ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana kwa uwazi. Jamii ilijawa hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha. Kulikuwa na usiri mkubwa. Lakini, ndani ya kufichwa huko, kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa. Gorbachev, daima atakumbukwa kwa ’ Kuvunja Ukimya’ na kuifanya Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana sasa.


CCM ina cha kujifunza kutokana na yaliyotokea Urusi na yanayoendelea sasa katika nchi za Kiarabu na kwingineko. Ni ukweli, kuwa ndani ya CCM na hata Serikalini, kuna watendaji wenye kufanya kazi kama vile tuko kati kati ya miaka ya sabini. Halafu bado ndani ya CCM kuna wanaoshangaa kuona vijana wa leo wakikipa mgongo chama hicho.


Maana , imefika mahali, kuwa moja ya sifa ya kushiriki siasa ndani ya CCM
ni kuwa na uwezo wa ’ kuendekeza fitna na kusema uwongo!’ Na kwa wengine, uongozi ndani ya CCM unapatikana kama vile mtu anayekwenda kununua ng’ombe mnadani.


Na kuna kauli za Wana-CCM zenye kuthibitisha ukweli huu. Mojawapo ilipata kutolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Phillip Mangula aliyepata kutamka; ” Isifike mahala CCM ikatangaza tenda za uongozi!”.
Naam. CCM wanajivua gamba. Kila la kheir Chama Cha Mapinduzi.

MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
0788 111 765
 
Tuwape dole CCM kwa kujitambua na kuanza hatua za marekebisho ndani ya chama! Kwa kweli CCM kama chama kimerudisha imani kwa wanachama na watz kwa ujumla
 
CCM hawaja tambua tatizo, kama wametambua basi hawataki kulitatua. Swala sio magamba(mafisadi) bali ni mfumo unao zaa ufisadi. Sijawasikia wakielekeza uchambuzi wao kwenye azimio la Zanziba ambalo ndilo liliuweka rasmi mfumo wa ufisadi. Kwanini wana tumia nguvu nyingi kutibu dalili za ugonjwa badala ya ugonjwa wenyewe? Falsafa ya magamba waliyoanzisha haina manufaa, zaidi itazidisha uhasama na chuki kati yao. Warudi,wakae na kuchambua ukweli wa tatizo, la sihivyo wakubali kwamba wanacheza mziki mnene wa CHADEMA bila kufuata step.
 
Wanachofanya CCM ni usanii mtupu hadi sasa, walipaswa kuchukua hatua kali zaidi ya hii ya kutajana majina na kutishiana. Sera za CCM zinazungunza kwa uwazi juu ya maadili ya viongozi, lakini tatizo kubwa ni kukosekana na usimamizi wa sera na maadili hayo. Mfumo waliouweka wa kupeana uongozi wenyewe una walakini. M-kiti mwenyewe aliingizwa kwenye uongozi wa juu na hawa wanaotajwa kuwa mafisadi. Atahitaji kufanya maamuzi ya kiuendawazimu kuwatosa waliokuwa wapambe wake wanaomfahamu kwa undani.

Nani aliye safi kusimamia sera nzuri za CCM, Nape! Mkama! Nani? Uadilifu imekuwa sifa adimu sana kwenye CCM. Ni lazima awepo mwenye macho safi kusafisha nyumba hii. asiyekuwa na boriti wala kibanzi. Ni nani?
 
Wanachofanya CCM ni usanii mtupu hadi sasa, walipaswa kuchukua hatua kali zaidi ya hii ya kutajana majina na kutishiana. Sera za CCM zinazungunza kwa uwazi juu ya maadili ya viongozi, lakini tatizo kubwa ni kukosekana na usimamizi wa sera na maadili hayo. Mfumo waliouweka wa kupeana uongozi wenyewe una walakini. M-kiti mwenyewe aliingizwa kwenye uongozi wa juu na hawa wanaotajwa kuwa mafisadi. Atahitaji kufanya maamuzi ya kiuendawazimu kuwatosa waliokuwa wapambe wake wanaomfahamu kwa undani.

Nani aliye safi kusimamia sera nzuri za CCM, Nape! Mkama! Nani? Uadilifu imekuwa sifa adimu sana kwenye CCM. Ni lazima awepo mwenye macho safi kusafisha nyumba hii. asiyekuwa na boriti wala kibanzi. Ni nani?

Wanachofanya CCM ni costmetic, wanajaribu kuvuta muda yasiwakute yaliyomkuta Mubarak na timu yake (kushitakiwa kwa mchango wao wa ubadhilifu liliotendewa taifa hili na makada wake walioko serikalini na kwenye Chama)... haingii akilini kumwambia mwizi aondoke na ukamuacha aondoke bila kumchukulia hatua zozote za kisheria ikiwa kuna utawala wa sheria... nikisikia wameshitakiwa wale wote waliofanya ubadhilifu kupitia Meremeta, Kagoda, Richmond/Dowans, IPTL, RITES, ATCL, Uuzwaji wa mali za umma, n.k. ndipo nitajua wako serious...

LAKINI hata hivyo tatizo kubwa lililopo ni kuwa wanaotakiwa kuwawajibisha wenzao siyo wasafi na wakathubutu kuwawajibisha wao pia watawajibishwa!
 
Nimewahi uliza hivi ni wabunge wangapi kupitia CCM hawakutoa rushwa kupita ktk kura ya maoni na wkt wa uchaguzi mkuu 2010? Ni wajumbe wangapi wa NEC hawakutoa rushwa ktk uchaguzi wao 2007? Nashangaa sana ndugu yangu Mjengwa unatoa wapi matumaini kwamba chama ya aina hiyo inaweza fanya mageuzi,kama siyo usanii. Kama bado unayo matumaini ya mageuzi ndani ya chama hicho kikongwe,subiri vituko na rushwa zitakazotembea mwakani ktk uchaguzi wao wa ndani kuanzia kata mpaka taifa.
 
Kazi njema Maggid, ila hapa hakuna mtu wakumletea hizo habari za kusadikika. hivi nyoka anapojivuwa gamba huwa anageuka kuwa chura? Watanzania hawana shida na uongozi wa chama cha ccm hata waongoze ukoo wa Kikwete tupu, Watanzania wanahitaji maisha bora na zile ahadi 68 alizoahidi Kikwete kwenye kampeni zitekelezwe. labda nikukumbushe baadhi ya ahadi hizo kwa picha ni hizi hapa chini.

pic06.jpg


MELI.jpg
 
Hakuna ulichoandika hapo.
Unaonekana umewaandikia ccm, na kama hivyo ndivyo peleka kwenye gazeti la uhuru na mzalendo.
Wakati unawapigia kampeni ulikuwa hujayaona hayo magamba....?
 
Kwa sisi tunaoelewa mambo ni kwamba MAGAMBA si hao watatu mnaowataja tu..ni wengi mno, karibia NEC nzima, pamoja na mzee wao!
Hata mleta mada anaelewa hilo, kwamba ni uonevu mkubwa sana kuwakamia watu 3 tu kuwa ndio magamba, wakati nyumba nzima ni ya wezi!
Inajulikana kabisa taratibu za kugombea kuwa mjumbe wa NEC zilivyo na kila aina ya rushwa na ufisadi, na kuwa masikini hawagusi wadhifa huo...je ni ukarabati wa aina gani wa hiyo nyumba utakaoipendezesha kama si kuvunja nyumba nzima>?
Mleta mada acha kutumika. Labda kama una kitu fulani kichwani hakijakazwa vizuri ndiyo utajaribu kupindisha ukweli, kitu ambacho kwa karne za leo ujue utaishia na aibu!
Fanya kazi uliyotumwa kwa namna ingine , si kwa suala hili la MAGAMBA!...I beg you broda!
 
majidi ndugu yangu sisiti kusema akili au mawazo yako yamechakachuliwa, huyu nyoka aliyejivua gamba kwa sasa ndio anazidisha sumu yake kama kutugonga ndio anatugonga kwa ari zaidi,nguvu zaidi na kasi zaidi. kuhusu hao mafisadi wawataje hadharani tujue pumba ni zipi na mchele ni upi.
Kikwete anajaribu kucheza na akili za wtz ili na yeye aonekane mmoja wa wapiganaji wa ufisadi, pesa ambazo hao mapacha watatu wamekwiba wamepeleka wapi kama si kufadhili uchaguzi wake? Kama ni kumfukuza mtu uanachama aanze kujifukuza yeye mwenyewe kwanza.
 
CCM KUJIVUA GAMBA; TAFSIRI YANGU SASA.....
Moja kwa moja kwenye tafsiri kwa namna niionavyo,sina muda wa kupoteza kwa makala ndefu!
Ni kama mwanamke aliyesaliti ndoa, akajiingiza kwenye ukahaba. Kisha akakutwa na maradhi yaliyopelekea afya yake kuporomoka, na hivyo kupoteza mvuto wake wa awali. Anatamani kuolewa tena,.........na anaamua kutumia MKOROGO kurejesha mvuto.
 
CCM KUJIVUA GAMBA; TAFSIRI YANGU SASA.....
Moja kwa moja kwenye tafsiri kwa namna niionavyo,sina muda wa kupoteza kwa makala ndefu!
Ni kama mwanamke aliyesaliti ndoa, akajiingiza kwenye ukahaba. Kisha akakutwa na maradhi yaliyopelekea afya yake kuporomoka, na hivyo kupoteza mvuto wake wa awali. Anatamani kuolewa tena,.........na anaamua kutumia MKOROGO kurejesha mvuto.

kweli wee mshindo......
asante kwa tafsiri hii
 
Wewe Majjid acha kwanza kuwa mouth speaker ya CCM na pia acha kupotosha umma. Hivi CCM walipotumia msemo wa KUJIVUA GAMBA unafikiri walikuwa hawafahamu kwamba wangeweza kusema KUKARABATI NYUMBA KONGWE kama wewe unavyotaka tuamini. Usiwawekee maneno kwenye midomo yao NEC ya CCM ambayo hawakuyasema na hawakusudi kuyafanya.

Nina uhakika wewe Majidd huwezi kuwazidi wana CCM wote kiswahili eti walimaanisha KUKARABATI NYUMBA upya. CCM kweli wana maana ya kuvua gamba na kwa kutumia hiyo pretext wanataka wawafanye scapegoat EL, RA na AC. Lakini SUMU (read mfumo mbaya) wa kupata uongozi unaozalisha mafisadi utaendelea na bila kuuondoa huo mfumo(read SUMU) ya nyoka CCM itaendelea kutufisadi.

JK anacheza tu na hisia za watu na akithubutu tu kumvua unachamana EL kwanza CCM itakuwa imekwisha umasaini maana huko EL ni sawa na Chief. Pili EL hatamuacha tu, hata akimumezea kipindi hiki ambacho JK ni Rais lakini akimaliza muda wake lazima ataaniko uozo wake kumbukaalikuwa architecture wa JK kuingia Ikulu.

JK anatupotezea muda tusahau kujadili mambo ya KATIBA tuendelea kujadaili magamba ambayo finally hayatachukuliwa hatua yoyote.

Watanzania tuwe macho!
 
Back
Top Bottom