Kimbunga,
Nashukuru sana kwa kunileta kwenye uzi huu, kwani kwa sababu fulani fulani, uzi huu ulinipita. Iwapo sijachelewa sana, ningependa kuchangia mada iliyoletwa na mwenzetu 'Tubadilike Sasa' katika maeneo machache na kwa ufupi sana.
Kwanza nakubaliana na hoja yake kimsingi kwamba CCM haikistahili tena kuitwa chama cha wakulima na wafanyakazi kwani sote tunashuhudia jinsi gani makundi yote haya mawili hivi sasa yanavyozidi kuwa on a Collision Course na chama (CCM) ambacho kiliungwa mkono na wananchi wengi wakati wa harakati za uhuru wakiamini kwamba kitawatetea na kuwalinda, na wengi ya hawa walikuwa ni wakulima, na wachache wakiwa ni wafanyakazi. Napozungumzia CCM na serikali yake kuwa on a collision course na makundi haya mawili sidhani kama inahitaji mtu kuwa a rocket scientist kubaini hilo, kwahiyo sitalijadili zaidi.
Baada ya kusema hayo, ningependa kufafanua nijadili kidogo hoja kwamba huko nyuma, TANU/CCM kilikuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Kwa mtazamo wangu, Mwalimu Nyerere alipendelea iwe hivyo, hasa baada ya kufanya ziara yake vijijini (akimwachia Kawawa uongozi wa nchi) ili kujionea na kusikia njozi, matumaini na matamanio ya wengi. Tukumbuke kwamba at independence, atleast 90% ya watanzania walikuwa vijijini. Jibu alilolipata Mwalimu baada ya ziara yake ni kwamba ili kuwalipa fadhila wananchi waliojitolea kupigania uhuru, hasa waliounga mkono harakati za TANU, ilikuwa haina budi kwa Tanganyika kufuata sera ya Ujamaa, huku ikiwaweka wakulima na wafanyakazi at the centre (sio sasa ambapo wamewekwa at the periphery).
Ni muhimu sana tukaelewa kwamba kuwa chama cha wakulima na wafanyakazi lilikuwa ni jaribio tu ambalo halikufanikiwa sana licha ya kulazimisha makundi haya kwa nguvu (sio kwa ihari) yajiunge kama wanachama. Pamoja na kulazimishwa huku (badala ya ihari), kwa mtazamo wangu, kulikuwa na faida na hasara zake, lakini faida outweighed hasara, kwa hiyo kwa mtazamo wangu, the end justified the means, ingawa huu ni mjadala mwingine tofauti kabisa. Kwa mfano, kwa mujibu wa ibara ya (8) ya Katiba ya TANU/CCM [WAKATI ULE], sehemu kubwa ya wananchi ikiwemo ile ya wafanyakazi, wakulima na wengine walitengwa kukosa haki ya kuwa wanachama. Ibara ya 8)7) ilitamka hivi:
Mtu yoyote hatakubaliwa kuwa mwanachama au kuendelea kuwa mwanachama isipokuwa awe ni mkulima au mfanyakazi na asiyejihusisha na mambo yoyote ya kibepari au kikabaila kama vile:
a) Kuwa na hisa katika kampuni;
b) Kuwa mkurugenzi katika kampuni ya kibepari;
c) Kupokea zaidi ya mshahara mmoja;
d) Kumiliki nyumba ambayo anaikodisha;
Hii ni tofauti sana kwa mfano na Chama Cha Kikomunisti cha China ambapo uanachama wa chama pekee cha kisiasa nchini humo yaani Chama Cha Kikomunisti cha China, uliwekwa wazi kwa raia wa aina nyingi, na kiliweza kujizolea wanachama wengi (wakulima na wafanyakazi) kwa ihari yao. Kwa mfano ibara ya (1) ya katiba ya chama hicho (1982) ilitamka hivi:
"Mfanyakazi yoyote wa Kichina, Mkulima, mwanajeshi, msomi au mwanamapinduzi yoyote ambae atakua amefikia umri wa miaka 18 na ambaye anakubaliana na programu za Katiba ya Chama na ambaye yuko tayari kujiunga na kufanya kazi katika moja ya jumuia za uanachama ipasavyo, anaweza kuomba uanachama wa Chama Cha Kikomunisti Cha China"
Pengine nisisitize tu kwamba dhumuni la kufananisha TANU na Chama Cha Kikomunisti Cha CHina ni kuonyesha tu kwamba sio kweli Mwalimu aliiga kila kitu kutoka China, lakini muhimu zaidi ni kwamba mazingira yetu yalitulazimu kufuta suala la IHARI juu ya kujiunga na CCM i.e. Wakulima na Wafanyakazi na badala yake kuwa suala la ULAZIMA, lakini kama nilivyokwisha tamka, faida outweighed hasara, na huu ni mjadala mwingine ambae nisingependa kuingia katika uzi huu.
Baada ya kusema hayo, nadhani sasa nitaeleweka iwapo nitasema kwamba TANU/CCM haikuwahi kumilikiwa na wakulima na wafanyakazi, bali TANU/CCM kilitumiwa na wakulima na wafanyakazi kuikomboa Tanganyika, na hivyo ndivyo TANU/CCM hatimaye ikaja kushika hatamu. Kuna misconception nyingi sana hata kwenye vijiwe vya CCM vya wakubwa kuhusu chama kushika hatamu. Maana halisi ya Hatamu ni kwamba - Hatamu za TANU zilikuwa ziko katika nguvu za wananchi jambo ambalo lilifanya serikali ya kikoloni, kabla ya uhuru kutambua na kuheshimu NGUVU YA UMMA; hii ndio ilifanya TANU iwe na mizizi mirefu kwenye jamii kwani UMMA ulikitegemea sana chama cha TANU kupigania uhurum hivyo kukiunga mkono katika harakati hizo; baada ya uhuru, juhudi za Mwalimu kukifanya TANU kumilikiwa na wakulima na wafanyakazi iliingia dosari kwani halikuwa jambo rahisi; kwa mfano, kikiwa ni chama pekee cha siasa enzi hizo, kilikuwa (hadi sasa) na vyombo vikuu vitatu: (1) MKUTANO MKUU; (2) HALMASHAURI KUU (NEC); (3) KAMATI KUU; Kati ya vyombo hivi vitatu, NEC ndio ilikuwa na nguvu kichama, kiserikali, kimahakama, YOU NAME IT...; Ni CCM-NEC ndio ilipitisha sheria ya muungano; ni CCM-NEC ndio ilipitisha Katiba ya 1977...na sijawahi kusoma katika historia sehemu yoyote wakulima na wafanyakazi kushirikishwa katika haya;
Vile vile sijawahi kusikia katika historia ya CCM kwamba NEC ilikuwa na idadi tosha ya Wakulima; navyoelewa mimi, wengi ya Wakulima walikuwa ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na kama tunavyofahamu, chombo hiki kwa kawaida huwa ni Rubber Stamp tu ya NEC; Lakini again, kwa mazingira yale, the end justified the means, na faida outweighed the costs kasoro kwenye suala moja tu kubwa - MUUNGANO, na hapa nasema wazi kwamba kati ya makosa aliyofanya Mwalimu, ni muundo wa muungano, but again huu ni mjadala tofauti.
Nikirudi kwenye hoja ya 'tubadilike sasa' kuhusu CCM kutokuwa chama cha kutetea wanyonge kimsingi nakubaliana nae, kwani hata mtu ukitizama kinyang'anyiro cha sasa cha nafasi za CCM-NEC, pia nafasi za ubunge na udiwani 2010, kipimo cha kiongozi bora ni Fedha au Ukaribu/upambe kwa wakubwa, na kuwa mkulima is synonymous na didqualification kwani kwa miaka 50 CCM imeshindwa kumwezesha mkulima kuwa na uwezo kifedha, na vilevile mkulima hana uwezo wa kuwa na ukaribu na wakubwa ili na yeye ajikusanyie 'point' ili zikijumlishwa, awe na sifa za kuwa kiongozi bora.
Ningependa kumalizia kwa kuelezea jinsi gani Chama Changu Cha CCM kimeacha kusimamia mambo ambayo chenyewe iliyaweka ndani ya Muongozo (1982), na mengi ya haya, wenzetu wa Chadema wanajaribu kuyatumia kikamilifu and it pays. Chadema ina practice mambo yetu (CCM) according to Mwongozo, kwa mfano mwongozo wetu ulipotamka katika ibara ya 53 kwamba:
"Chama Cha Kijamaa kama vile CCM ni chombo cha uongozi. Hakifanyi kazi kwa amri zisizo msingi wala kufanya kazi zao kwa nguvu au vitisho vya nguvu. Kinaongoza kwa kuelimisha, kwa kuwashirikisha watu na kuonesha njia na kwa hivyo basi msingi wa nguvu zake na kuaminika kwake unatokana na kukubalika kwake kihalali miongoni mwa umma, mchanganyiko wa wanachama wake na msingi mzuri wa kisiasa ambayo inakwenda sawa na matakwa ya umma. Ili kuweza kutimiza lengo hilo Chama kinahitaji kuwa na Nguvu ya Hoja na SIO Hoja ya Nguvu."
Ni vigumu kuelewa nini kimekisibu CCM kufikia hatua ya kuwaona Chadema wanatenda sivyo huku udhaifu wetu ukizidi kukijengea Chadema HATAMU. Rejea mjadala juu ya hatamu ambapo hili ni suala la nguvu ya UMMA, sio NGUVU YA DOLA.
NI Muhimu CCM Tujisahihishe, Vinginevyo Tugawane Chama.