JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 3,177
- 7,472
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ilitoa taarifa ya kulichukua soko hilo na kuanza kulisimamia rasmi, ambapo ilieleza wazi kuwa baada ya kulichukua marekebisho yangefanyika. Baada ya kuanza kulisimamia, tuliona baadhi ya marekebisho yakianza kufanyika, ikiwemo kujenga mitaro na kurekebisha baadhi ya maboma ya wafanyabiashara waliopo ndani ya soko hilo. Hatua hiyo ilileta matumaini, na tuliamini kuwa baada ya muda hali ya soko ingekuwa nzuri.
Pia soma ~ Manispaa ya Ubungo ilituahidi baada kuanza kulisimamia Soko la Mabibo miundombinu itakuwa shwari, lakini bado hali ni tete
Hata hivyo, hadi sasa ukarabati huo uliishia katikati. Eneo kubwa la soko limejaa matope, hali ambayo inawalazimisha wateja pamoja na wafanyabiashara kuvaa buti maalumu ili kukabiliana na matope yaliyopo.
Hali ya soko si rafiki kabisa. Hata mitaro iliyojengwa haisafishwi kwa wakati, na katika maeneo mengi kumejaa taka ambazo zinaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, hasa ikizingatiwa kuwa uchafu mwingi unatokana na mabaki ya matunda.
Niungane na wenzangu Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ichukue hatua za uwajibikaji. Pia mamlaka za juu, hususan TAMISEMI, ziangalie kwa karibu kubaini nini kinachokwamisha kuendelea kwa ukarabati wa soko hilo, ilhali wafanyabiashara na wananchi wanaendelea kutozwa ushuru.
Ikumbukwe kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ilitoa taarifa takribani miaka miwili iliyopita kuwa ilikusanya zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa mwaka kutoka katika soko hilo kupitia mapato mbalimbali, ikiwemo ushuru ikiwa ni baada ya kuanza kulisimamia.