Buriani Suleiman ''Baku'' Ismail

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,906
30,248
BURIANI NDUGU YANGU SULEIMAN ‘’BAKU’’ ISMAIL
Siku ya Alkhamis, tarehe 9 tumemzika ndugu yetu Baku mtu maarufu kupita kiasi Mafia.

In Shaa Allah nitakuja kueleza umaarufu wa Baku baadae.

Ningeweza kuweka picha nyingine yoyote lakini hii picha ya pili niliyoweka hapo chini amejilaza kwenye sofa nyumbani kwangu nimeiweka kwa sababu maalum.

Picha hii yuko na kiongozi mwenzake Bwana Hassan Ali Dilu aliyekuwa Katibu wa Jimbo, Mafia ACT Wazalendo.

Hapo ndipo ilipokuwa Majlis yetu kila Baku anapokuja nyumbani.
Mimi na Baku tumeoa nyumba moja.

Picha hii tuko Majlis inanikumbusha miaka na siku zangu nilipofahamiana na Baku hadi kufikia kifo chake.

Picha hiyo inamuonyesha Baku akiwa amekaa mkao wa kupumzika na mimi ndiye niliyempiga.

Ilikuwa kawaida yake kila akija Dar es Salaam kwa shughuli za chama lazima tutaonana.

Baku na mimi tumeoa nyumba moja.

Siku zote nilipokuwa na Baku sikupata kumuona na wahka ambao ni kawaida kwa wanasiasa.

Baku alikuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Jimbo la Mafia akitokea CUF baada ya ''Shusha Tanga Pandisha Tanga.''

Misukosuko yote ile ya CUF ya miaka nenda miaka rudi ya uchaguzi na mengineyo Baku alikuwa kila akija Dar es Salaam tukikaa kuzungumza siasa kama zilivyokuwa Mafia na Tanzania kwa ujumla kwangu mimi ilikuwa kama mtu nitazamae filamu nzuri iliyojaa matukio yanayonogesha mchezo wa senema.

Ama iwe vurugu za Blue Pearl Hotel za mwaka wa 2016 zilizosababisha baadae wanachama wengi wa CUF kuhamia ACT Wazalendo maarufu shusha tanga pandisha tanga au kufutwa kwa wagombea wote wa upinzani katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Mkutano wa Blue Pearl Hotel ulikuwa Mkutano Mkuu Maalum wa CUF kumchagua Mwenyekiti Taifa kujaza nafasi ya Prof. Ibrahim Lipumba baada ya yeye kujiuzulu.

Yaliyotokea siku ile pale Blue Pearl yatabaki kama kumbukumbu katika historia ya vyama vya siasa vya Tanzania kwa miaka mingi.

Lakini kubwa litakalobakia katika historia ya vyama vya siasa duniani labda ni kule kwa wanachama wa chama cha siasa wote kwa mkupuo kuhama chama chao na kuhamia chama kingine.

Baku alipokuwa akinieleza yale yaliyotokea siku ile kwa hakika yalinishangaza.
Katika haya yote nilikuwa na mwalimu aliyekuwa anajua kulisomesha somo lake.

Baku alikuwa na kipaji cha kukufanya ucheke kwa yale maneno yake hata kama yalikuwa ya kuhuzinisha na kuleta fadhaa.

Baku alikuwa akikueleza kila uchaguzi ambao CUF walishiriki baada ya mahakama kumrejesha Prof. Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF baada ya vurugu za Blue Pearl Hotel utacheka ingawa kwa hakika yaliyokuwa yakitokea yalikuwa yakisikitisha.

Baku atasema katika uchaguzi mdogo mahali fulani CUF kura zake ni sawa na namba ya saizi za viatu yaani kiatu saizi namba 7 au 8 nk.

Atakuambia kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa waliochaguliwa kwa mtindo ule wa kufuta wapinzani ni kuwa hao waliochaguliwa wakiwa hawana wapinzani ni wagombea wa ‘’Viti Maalum.’’

Baku alikuwa anaijua CUF vizuri sana na wahusika wake wakuu achilia mbali viongozi bali hata wanachama wa kawaida karibu nchi nzima ambao walikuwa na sauti ndani ya chama iwe Pemba au Tandahimba.

Alikuwa anayo ''dramatis personae,'' yaani orodha ya waigizaji wa mchezo mzima ''scene'' kwa ''scene.''

Niliahidi kueleza umaarufu wa Baku nilipoanza kuandika taazia hii.
Wenyeji wa Mafia walikuwa wanasema Baku anaweza kugombea udiwani mahali popote Mafia na kushinda kwa ule umaarufu wake.
Hakuna Mafia ambae alikuwa hamjui Baku.

Katika uchaguzi Mkuu wa 2020 Baku alimsindikiza Mgombea Ubunge wa ACT Wazalendo, Bi. Riziki Shahari Mngwali kwa Mkurugenzi wa Halmashauri (Msimamizi wa Uchaguzi Wilayani) ili kuhakiki majina ya wadhamini wa mgombea.

Madhumuni ya zoezi hili ni kuwatambua wadhamini wa mgombea kama ni wapiga kura halali na sehemu wanazotoka.

Hii kazi si nyepesi ni ngumu inayohitaji kukagua makazi na vituo walivyojiandikisha wadhamini.

Baku aliwashangaza maofisa wa uchaguzi na mwisho wa zoezi walimshukuru kwani kwa msaada wake zoezi lilikuwa jepesi sana.

Kila liliposomwa jina Baku alitaja jina la kitongoji anachokaa na kituo cha kupigia kura (alichojiandikisha) mdhamini mmoja baada ya mwingine.
Mkononi Baku hana karatasi usema anasoma yote yanatoka kichwani.

Kwa hakika si tu kuwa alikuwa anawajua wadhamini wa mgombea anaemsimamia bali alikuwa anajua hadi idadi ya kura za ushindi za mgombea wake.

Hapo Baku atanihadithia vituko vyote kuanzia uandikishaji hadi kuhesabu kura.
Siasa za uchaguzi Tanzania zina raha, karaha na starehe zake.

Yanayoandikwa katika magazeti huwa hayatoshi kutoa picha kamili na hali halisi unataka mengine uyapate kwa wachezaji wenyewe, watu kama Baku.

Watu wa Mafia Allah kawajalia kitu kimoja, hukuti mjinga.
Kisha wana fasaha katika kuzungumza.

Utapenda kusikiliza mazungumzo yao.

Nakumbuka mkutano uliofanyika Blue Pearl Hotel na vurugu zilizotokea.

Mkutano ule ulikuwa unarushwa mubashara mtandaoni na vurugu zilitokea pale Prof. Lipumba alipoingizwa mkutanoni na watu ambao inasemekana ni polisi.
Lakini kulikuwa na watu wengine mfano wa Walinzi Maalum (Security Guards) waliokuwa wamevaa unifomu zilizoandikwa jina la kiongozi mmoja wa juu wa CUF.

Baku akiwa kajipumzisha katika Majlis yetu akasema, ''Usishtushwe wala kufadhaishwa na hayo kwani huo ndiyo mwisho wao."

‘’Huo ni mzigo mzito mbebaji atachoka na ndiyo utakuwa mwisho wa hayo yote.''
Kama alivyotabiri Baku mwaka wa 2016 ndivyo hali ilivyokuja kuwa.


Rafiki yangu Ridder Samson Mtaalam wa Lugha kutoa Chuo Kikuu Cha Hamburg, Ujerumani alikwenda Mafia kwa ajili ya utafiti basi nikamwomba Baku ampokee,

Ridder lau kama ni Mzungu anakisema Kiswahili vizuri sana.
Baku alimpokea na walikuwa pamoja katika kipindi chote cha utafiti wake.

Ridder alimsifia sana Baku kwa ukarimu.

Ridder akanihadithia vipi alivyokuwa akiletewa chai asubuhi na mapema kutoka nyumbani kwa Baku na mtoto wake kwenye nyumba aliyofikia.

Ridder akanieleza vipi Baku alivyomtembeza kisiwa chote cha Mafia na kote wakipokelewa kwa heshima kubwa.

Kwa heri sahib yangu na mume mwenzangu Sheikh Suleiman Ismail Suleiman.
Allah akufanyie wepesi safari yako.

1655097460439.png
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom