Steve Dii
JF-Expert Member
- Jun 25, 2007
- 6,403
- 1,241
Habari kutoka Mwananchi zinasema ukaguzi wa 'ufisadi' BoT umekamilika. Soma zaidi hapa chini:
Source link:mwananchi.co.tz
Swali: kwanini ipelekwe Uingereza kwanza?!
SteveD.
Ukaguzi wa tuhuma za ufisadi BoT wakamilika
Na Ramadhan Semtawa
WAZIRI wa Fedha, Zakia Meghji amesema ukaguzi wa tuhuma za ufisadi wa mahesabu ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliofanywa na Kampuni ya Ernst &Young, umekamilika.
Meghji alisema jana kuwa ukaguzi huo uliokuwa unadafanywa na kampuni ya ukaguzi ya Ernst & Young kufuatia tuhuma za kuwepo ubadhilifu katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA)umekamilika na kwamba ripoti ya awali imepelekwa London, uingereza kwa ajili ya kuandaa ripoti kamili ambayo itakabidhiwa serikali.
Ukaguzi huo ulioanza Septemba 9 na ulipaswa kukamilika katika kipindi cha ndani ya siku 60 ambazo ziliisha jana.
Akizungumzia ukaguzi huo, Meghji alisema ripoti ya matokeo imekwenda kuandaliwa nchini Uingereza na kwamba itakabidhiwa serikalini ndani ya wiki tatu.
Meghji alisema serikali ilitoa siku 60 na kwamba baada ya kuuliza kampuni husika ilitoa maelezo kwamba kuchelewa kukabidhi ripoti kulitokana na ukaguzi ambao ulivuka hadi nje ya nchi.
Waziri Meghji alisema ukaguzi huo ambao ulisimamiwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), uliwezesha kampuni hiyo kwenda hadi nchini Afrika Kusini.
"Ukaguzi umekamilika kwa maana ya Field (vitendo), lakini ripoti bado haijawasilishwa serikalini, lakini kila kitu kwa maana ya Field tayari," alisema Meghji na kuongeza,
"Ripoti wamekwenda kuiandaa Uingereza, wameahidi kuikabidhi ndani ya kipindi cha wiki tatu baada ya kuifanyia kazi vema," alisisitiza waziri Meghji.
Alisema matokeo ya uchunguzi huo yatatangazwa hadharani baada ya ripoti yake kuwasilishwa kutoka kwa wakaguzi na kisha serikali kuipitia kwa kina.
Tuhuma katika EPA zinahusu pia sh10 bilioni ambazo zinadaiwa na wapinzani kuchotwa na kutumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye kampani za Uchaguzi Mkuu wa wa mwaka 2005.
Kaimu Gavana wa BoT, Juma Reli aliliambia gazeti hili kwamba tuhuma hizo za kuchotwa sh 10 bilioni na CCM nazo zitafahamika baada ya uchunguzi huo.
Reli alisema hakuna kitakachofishwa na kwamba wakaguzi hao walifanya kazi zao kwa ufanisi kwa kuhoji na kupitia nyaraka mbalimbali za BoT.
Ernst &Young ilishinda zabuni hiyo baada ya kuyashinda makampuni saba, ambayo uchunguzi wake umekuwa ukiangaliwa kama kipimo kikuu cha serikali katika suala zima la kupambana na ufisadi nchini.
Uchunguzi huo unasaubiriwa kwa hamu kutokana na nchi 14 wafadhiri ambazo zilitoa msimamo wiki iliyopita kwamba matokeo ya uchunguzi huo utatoa mwelekeo wa uchangiaji wake wa fedha katika bajeti ya Tanzania kwa mwaka 2008/09.
Kampuni hiyo inapitia mahesabu katika kumbukumbu za malipo yaliyofanywa na benki hiyo katika kipindi cha mwaka 2005/6, kubaini kama kuna ukweli juu ya madai ya ubadhirifu wa fedha katika benki hiyo katika kipindi hicho.
Hata hivyo, serikali ilitoa tamko kwamba uchunguzi huo utakuwa huru na matokeo yake yatawekwa bayana na Rais Jakaya Kikwete, ameahidi kuwachukulia hatua wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu huo kama ripoti itakavyoonyesha.
Source link:mwananchi.co.tz
Swali: kwanini ipelekwe Uingereza kwanza?!
SteveD.