SoC03 Bayogesi Itumike katika Taasisi za Umma, kupunguza hewa ya ukaa

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
242
615
ConstantineJ. Samali Mauki

Utangulizi
Bayogesi ni nini?

Kwa mujibu wa Lucía Fernández wa Statistica (Feb 8, 2023), Bayogesi ni mchanganyiko wa gesi ya methane na hewa ya ukaa (kabonidayoksaidi) inayozalishwa na viasilia mbalimbali kama mabaki ya mimea na ya Chakula katika mazingira ya ukosefu wa oksijeni.

Chanzo kikubwa cha bayogesi ni kinyesi cha Wanyama, masalia ya mimea na kinyesi cha binadamu. Gesi hii inaweza kutumika kupikia, kuwashia taa, kupasi, kuendesha mitambo mbalimbali kama jenereta ya kuzalisha umeme na magari. Bayogesi ni ya gharama nafuu ukilinganisha na nishati ya kuni, mkaa, umeme, na hata gesi asilia ambayo inachimbwa chini ardhini.

Kielelezo Na. 1: Mtambo Mkubwa wa Kuchakata Bayogesi
Mtambo Mkubwa wa Kuchakata Bayogesi.png

Chanzo: Blog ya Muungwana (Oktoba 02, 2018)

Vyanzo vikubwa vya nishati kwa Watanzania walio wengi ni kuni, mkaa, mafuta ya taa, na umeme unaosambazwa na Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (“Tanesco”). Watu wengi waliounganishwa na umeme wa Tanesco, wanautumia zaidi kuwashia taa, kwa ajili ya redio, runinga, majokofu, kuchaji simu, kupasi na kadhalika; lakini wanatumia kuni na/au mkaa kupikia kila siku.

Kielelezo Na. 2: Mtambo Mdogo wa Kuzalisha Bayogesi kwa Matumizi ya Nyumbani
Mtambo Mdogo wa Bayogesi.png

Chanzo: Google: “Biogas from Small Tanks”

Taasisi za Umma ni Zipi?

Hizi ni zile taasisi za serikali na za binafsi zinazotoa huduma kwa makundi ya watu wengi kwa muda mrefu. Taasisi hizi ni pamoja na shule za msingi na za sekondari, vyuo mbalimbali vya kati na vyuo vikuu; mahospitali, magereza, makambi ya jeshi, na nyingine kama hizo. Uwepo wa watu wengi katika taasisi hizi, inamaanisha upatikanaji wa kinyesi kwa wingi, ambacho ndio malighafi muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa Bayogesi.

Faida za Bayogesi
Kwa mujibu wa Blog ya HomeBiogas, kuna faida tano za bayogesi, kama ifuatavyo:

1. Bayogesi ni Rafiki wa Mazingira
Hii ni gesi safi inayozalishwa kutokana na umeng’enyaji wa viasilia mbalimbali ambayo haichafui hewa, na hakuna mlipuko wowote katika mchakato mzima wa uzalishaji; kwa hiyo, matumizi ya gesi hii ni njia bora kwa kudhibiti ongezeko la joto duniani.

2. Bayogesi Inapunguza Uchafuzi wa Udongo na Maji
Katika mchakato wa kuzalisha gesi kwa kumeng’enya viasilia katika mazingira yasiyokuwa na oksijeni, vijidudu vya magonjwa hufa, na hivyo kupunguza magonjwa yanayotokana na maji.

3. Uchakataji wa Bayogesi Huzalisha Mbolea ya Asili
Viasilia vilivyotumika kuzalisha bayogesi, vinakuwa mbolea nzuri ya asili ambayo ni mbadala wa mbolea za viwandani ambazo zina kemikali. Mbolea hii huharakisha ukuaji wa mimea na kuiwezesha kuhimili magonjwa mbalimbali.

4. Ni Teknolojia Rahisi na ya Gharama Nafuu
Teknolojia inayotumika kuzalisha bayogesi ni rahisi, kiasi cha kuweza kuwa na mitambo midogo ya nyumbani kwa ajili ya kupikia, kuzalisha umeme, na kupata mbolea asili ambayo ni nzuri kwa mazao ya shambani na bustanini.

5. Ni Mbadala wa Kupikia Katika Maeneo Yanayoendelea
Bayogesi inawapunguzia wanawake na watoto mzigo wa kwenda kutafuta kuni. Hivyo wanapata muda wa kutosha wa kupika na kufanya usafi. Matumizi ya bayogesi yanaepusha moshi jikoni, tofauti na matumizi ya kuni au mkaa, hali ambayo inapunguza uwezekano wa kupata maradhi katika mfumo wa kupumua. Ni jambo la kusikitisha kwamba watu milioni 4.3 wanakufa mapema kila mwaka kutokana magonjwa yanayochangiwa na uchafunzi wa hewa majumbani.

Matumizi ya Bayogesi Duniani
Pamoja na matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati, kama madini ya urani, mafuta ya petroli, gesi asilia, na vingine, nchi zilizoendelea zinazalisha na kutumia bayogesi kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa jarida la Stastica (2023), Mwaka 2014, China iliongoza kwa uzalishaji wa bayogesi (mita za ujazo bilioni 15); ikifuatiwa na Marekani (mita za ujazo bilioni 8.48); Thailand (mita za ujazo bilioni 1.3); India (mita za ujazo bilioni 0.81) na Canada (mita za ujazo bilioni 0.79).

Kielelezo Na. 3: Takwimu za Uzalishaji wa Bayogesi Duniani (Nchi), Mwaka 2014
Nchi zinazoongo uzalisha bayogesi.png

Chanzo: Statistica (2023)

Kikanda, kwa mwaka 2019, Ulaya iliongoza kwa uzalishaji wa bayogesi (mita za ujazo bilioni 18); Asia (mita za ujazo bilioni 13.1); Amerika (mita za ujazo bilioni 5); Oceania (mita za ujazo bilioni 0.5); na Afrika (mita za ujazo 0).

Inasikitisha kuona bara la Afrika ambalo Tanzania ni mojawapo wa nchi zake, likionyesha sifuri (0) katika uzalishaji wa bayogesi. Serikali zimekuwa zinatumia fedha nyingi, tena za mkopo kutoka mataifa yaliyoendelea kuwekeza katika nishati za gharama kubwa, huku zikifumbia macho nishati hii ya gharama nafuu na Rafiki wa mazingira.

Ni wakati muafaka kwa serikali kuweka nguvu katika teknologia hii ya Bayogesi, kwa lengo la kumpunguzia mwananchi wa kawaida gharama za Maisha.

Kielelezo Na. 4: Takwimu za Uzalishaji wa Bayogesi Duniani (Kanda), Mwaka 2019
Takwimu za matumizi ya Biogesi Kikanda 2019 Statistica.png

Chanzo: Statistica (2023)

Mitambo ya Kuzalisha Bayogesi Ifungwe katika Taasisi za Umma

Kwa kuwa taasisii za umma (kama nilivyozitaja hapo juu) zimesambaa karibu kila kijiji hapa nchini, na wataalamu, malighafi na teknolojia ya nishati hii vinapatikana nchini, napendekeza serikali ikishirikiane na wadau mbalimbali iweke sera na mipango ya kimkakati itakayowezesha taasisi hizi kufungiwa mitambo hii ya kuchakata bayogesi.

Huu utakuwa mwanzo mzuri, ambapo jamii na mtu mmoja mmoja watajifunza teknolojia hii kupitia taasisi hizi, na hatimaye kwenda kutekeleza katika kaya zao, jambo ambalo mbali na kuboresha mazingira, litapunguza gharama kubwa ya kununua nishati nyingine kama kuni, mkaa na gesi za viwandani.

Hitimisho
Bayogesi ni mkombozi wa mwananchi kiafya na kiuchumi. Ni teknolojia rahisi ambayo haihitaji uwekezaji na/au msaada kutoka nje ya nchi.

Marejeo
Blog ya Muungwana (Oktoba 02, 2018), Fahamu Bayogesi Ni Nini

Energy Global (Machi 10, 2023), “Global Biogas Market Forecast 2022 – 2027”

Global biogas market forecast 2022 to 2027

Advantages and Disadvantages of Biogas | Homebiogas

Lucía Fernández, Statistica (Feb 8, 2023), “Global Biogas Production by Major Country 2014”
 
Niliwahi kufanya kazi katika shirika moja la maendeleo, moja ya kazi tulioifanya ni kuwezesha wanufaika kujenga mitambo ya bayogesi. Hapo ndipo niligundua kuwa ni nishati nzuri sana, ya bei nafuu na rafiki mkubwa wa mazingira.
 
Back
Top Bottom