Hekima za Baba Askofu Bagonza
MAADUI WAKIISHA, MARAFIKI WATAGEUKA MAADUI.
Ajabu ya Wajaluo: Ukizoea kumsingizia adui kwa kila tatizo lako, siku ukimmaliza huyo adui, utawageuza marafiki zako wawe maadui ili upate wa kusingizia kila tatizo lako.
Nimesikia viongozi wetu wakidai wanaliunganisha taifa. Wengine wamesema taifa ni tulivu. Na wengine wameajiri mawakala wa kutafuta maridhiano. Sasa najiuliza:
1. Mawaziri wako London, New York, Addis Ababa na Brussels kueleza jinsi nchi ilivyotulia, LAKINI huku nyuma polisi wanakataa kwamba ndani ya Chadema hakuna wanawake na chama chote ni wanaume! Tulisitisha maadhimisho ya Uhuru; tunazuia hata siku ya wanawake wa dunia? Je, Tuna mashaka kama hao ni wanawake sawasawa?!
2. Mikutano ya hadhara inaonyesha kuna kero nyingi kuliko watatuaji, LAKINI kuna watu mitandaoni wanapongeza jinsi nchi ilivyo tulivu na maendeleo yanapaa! Tunaficha uchi, tutazaaje?
3. Janga la utekaji linaendelea na mamia wako mafichoni, LAKINI viongozi wetu hata kwenye mikutano ya hadhara hilo halizungumzwi! Kama serikali haihusiki na utekaji basi inahujumiwa na watekaji. Kauli ya serikali ilitakiwa toka juzi ileee.
4. Tunakodisha watu kwenda kuteka na kudhuru nje ya nchi BADALA ya kukodisha wapatanishi na mabalozi wa kurejesha nyumbani wakosoaji. Tunasubiri tukalishwe meza moja na Rachel Dangwa mbele ya Katibu Mkuu wa UN?
5. Polisi wanavuruga uwezekano wa maridhiano na kuizika serikali ikiwa hai. Tukumbuke: Polisi walioipigia saluti UNION JACK ndiyo walioipigia bendera ya Tanganyika huru. Serikali inawadanganya polisi na polisi inawadanganya serikali. Mchezo wa kitoto huu.
6. CCM haiko kimya. Ina historia ya kuibuka na kukataa dhuluma. Kuteka, kutesa na kuua si sera yake. Kuiba kura yaweza kuwa sera ya muda lakini si wote wanaipenda. Ukimya wa CCM ni kuchimba kaburi kwa meno yake. Itaamka, na kwa sasa adui wake si CHADEMA ambayo ni “marehemu”. Adui wa CCM anajijua na CCM inamjua. Mkumbukeni John Komba na “Jogoo limewika Dodoma”. Amkeni muokoe nchi na chama.
7. Tumekodisha mawakala wa maridhiano wakati tunavuruga maridhiano. Sasa watatuambia nini wakati hila tunaziona wenyewe? Mnawavunjia heshima hata kama wamejivunjia kwa kudokoa wali kabla haujawiva.
8. Mgonjwa wa kusahau hawezi kukumbuka tatizo lilianza lini. Serikali isiyokosolewa ni ile isiyokuwapo. Serikali isiyokosea na ile isiyofanya chochote. Serikali ipo; haina chanjo ya kutokosea. Inatakiwa kukiri makosa na kuwajibika ili tusonge mbele. Inapoteza muda na fedha kupiga propoganda. Ndevu waweza kuzificha kwa kunyoa; matiti je?
Vituko vyetu vimezidi mpaka Mjaluo amecheka na kutuonyesha mapengo anayoyaita mwanya.
Kwaresima Njema
Ramadhani Kareem