Barua kwa mwanangu - Tanzania

Dr Yesaaya

Member
Jul 25, 2022
9
23
Anaandika MTANGANYIKA - Rais wa TEGETA Empire - 0752591744/0682080069.

Barua Kwa Mwanangu

MTANGANYIKA BARA,

S.L.P 1961,

Mbinguni.

12/ 09/ 2022.


MTANZANIA BARA VISIWANI,

S.L.P 1964,

DODOMA, UNGUJA

K.K

Malaika Mkuu Gabriel

Mawinguni JUU.

Kwako mwanangu nikupendae sana.

Hujambo mwanangu? Mimi mama yako nimekukumbuka sana tangu nilipofariki miaka hiyo nimeketi juu ya mawingu nikikutazama kwa ukaribu sana.

Ninayo mengi kusema nawe, hivyo nimetafuta njia kufikisha ujumbe nikaona niandike hii barua ya upendo Kisha nimtume Malaika Gabriel akuletee.

Unajua Mimi na baba yako tulipokuzaa mwaka 61 tukakupa jina Tanganyika, jina hili ulipewa kwa kuwa ulikuwa mzuri sana mwenye mwenye nguvu, macho angavu na moyo wa ushujaa.

Mwenzako, pacha wako nae alikuwa mrembo mwenye sura nyeupe ya kupendeza yeye tukampa jina zuri akaitwa Zanzibar. kwakuwa tulitamani msiachane tukawaunganisha kwa Pamoja mtembee Pamoja ikabidi tuwaunge na kuwabatiza jina jipya mwaka 1964 tukakuita Tanzania. Kiukweli ukuwaji wenu ulikuwa wa shida na tabu.

Jambo zuri ni kwamba Tulikuwa na amani, mshikamano na umoja lakini njaa, Mahangaiko na dhiki zilikumba Kijiji chetu. Magonjwa, umaskini, rushwa na hali duni zilituandama. Tukaweka vijiji vya ujamaa ili kujikwamua, tukakwama. Ghafla Akaja nduli Idi Amini Dada mwaka 1978 akutuvamia, akitutukana mimi na babako na ndugu wote, na kutishia kutupora mali zetu tulizoachiwa na mababu zetu.

Japokuwa hatukuwa na uhakika kama kweli ni zetu au babu nae alipora kwa wengine, sisi hatukukubali na tukapanga kumpiga. kiukweli alitusumbua karibu mwaka mzima tulipambana hali na mali ili kushita vita ile. Ilifikia kipindi tulikopa. Deni hilo linaumizza hadi wewe mwanangu.

Hadi leo. Mwanangu tuliumia sana, kimwili kiakili, kijamii na hata kiuchumi. Tulimpiga na kumuondosha lakini ni waz tuliumia pia. Wengi wakajeruhiwa, kupata vilema na wengine wakafa vitani. Ni wazi Hatukuwa vilevile tulidhoofu kwa njaa na huzuni tele mioyoni ila tulishinda vita.

Lakin mwanangu, Tangu kipindi hicho hadi leo bado unapita shida, tabu na misukosuko? pole sana mwanangu.

Mimi mama yako nakutazama kila siku nikiwa peponi naona maumivu yako. Jua lako mvua pia yako. Unahangaika mwanangu. Jipe moyo utashinda. Ugonjwa unaokusumbua kwa sasa unaitwa ubinafsi wanaojifanya Rafiki zako ni wanafiki, wanajifanya kama wanakupenda kumbe waongo. Wanyonyaji.

Wachumia tumbo tu hao. Wanakufirisi wanakunyonya kisha wanakuacha taabani. Pole mtoto wangu. Hawa waliojiita nduguzo wakajiita wanasiasa wengi wao si wema, wanakuja kwako kwa maneno matamu ndani yake kuna hila, husda na njama hawakutakii mema wanakumaliza taratibu mwanangu, wachunguze wote wabaya wakatae.

Tanzania Mwanangu, nakuhumia sana pia nakuombea wewe na wajukuu zangu, wampee ujumbe wajukuu zangu walioko vyuoni wanasoma kwa tabu wakati wanasiasa watunga sera, wao walisoma bure hawakudaiwa hata thumni, leo wajukuu wananyimwa hata hicho kidogo wanachokiita mikopo. Wanakunyanyasa mwanangu kodi nyingi na tozo nyingi wananunulia maprado na kujenga majumba inayobaki hujenga madaraja na shule kadhaa.

Dawa akuna hospitali. Waalimu mishahara duni. Ila wao wana Maisha mazuri na wanaishi kwenye apatimenti. Tozo kila siku na hupumui mwanangu. Mafuta bei juu. nawaona wajukuu zangu hawatembei hadi leo wanatambaa, wamekosa virutubisho na lishe bora.

Polen jamii yangu. Nilipowazaa sikutaka muishi hivyo nilitaman kabla sijafa niwe nimewaachia msingi imara wa Maisha bora ila ndio hivyo mipango ya maulana. Ukipanga lako na yeye mola anapanga lake. Naumia japo kamwe siwez kumlaumu Mungu. Yanapita Mwanangu. Yana mwisho.

Ila mwanangu Tanzania, Mbona mwanangu usawa akuna hapo nyumbani? Nyie si jamii moja, iweje kuwe na tabaka la walio nacho na wasio nacho? Ikipikwa pilau hapo nyumban wakubwa wachache wanakomba nyama zote na kachumbali, wadogo husongewa ugali wale wakilumangia na chumvi wajaze tumbo tu ilmradi wasife – mwanangu kila siku nakuangalia nikiwa mawinguni, wachache wanapendelewa wengi wanaonewa na kudhulumiwa, usawa hakuna mwanangu, marafiki wema watakukimbia wote mwanangu.

Nakuombea Malaika mwanangu akufungue macho ili uone hatari iliyopo mbele yako ewe mwanangu Tanzania. Naakusia chagua watu wote kwa usawa, iwe katika ajira, maombi ya kazi au masomo ya shule na vyuo, mahali pote wapeni wote haki sawa.

Lingine mwanangu, Watoto wako umewazaa mwenyewe, baadhi yao wanakuangusha sana, ni wajukuu zangu lakini wa hovyo sana. Nawaona toka mawinguni, baadhi yao wakiwa Kazini maofisini uwajibikaji hakuna,watasaini kuingia wakishakunywa chai au supu na chapati huondoka zao, mwisho wa mwez hukinga bakuli walipwe mishahara.

Wengine wakipewa kazi haifanyi wanakula wao kwanza kinachobaki kidogo wanakiweka kama kuzugia mtafanikiwaje mwanangu? watafute hawa wote wafukuze mara moja.

Umejenga mashule na mahospitali bila uwajibikaji ni bure mwanangu. Madaktari wazuri wanakimbia nchi sababu mishahara midogo eti mwanangu hela zote za madini unapeleka wapi, wajukuu na vitukuu vyangu wamepewa jina la wanyonge wanateseka sana hebu waoneeni huruma.

Mwanangu, enzi za uhai wetu tuliweka sheria mama yaan katiba na sheria ndogo ndogo ili ziongoze watu waishi kwa utaratibu, ustaarabu na maelewano, mbona sasa hamzifuati, mnazikanyaga kanyaga na kuzisigina? Wengine wanasema katiba iliopo haifai ibadilishwe, kwanni mnadharau mawazo yao mwanangu? Kama ni wengi wasikilize, wape haki yao ya msingi, kumbuka mwanangu Sikukufundisha ubabe bali unyenyekevu mwanangu.

Nikiwa mbinguni huku nashindwa kupumzika kwa amani nalia uiku na mchana kwa uchungu sababu ya maumivu juu ya vijukuu vyangu vinavyoteseka kwa kudhulumiwa haki zao. si mliweka sheria zutawala wa sheria zifuaten mwanangu.

Wapeni wajukuu uhuru wa kusema kamwe msiwazibe midomo, msiwauwe wanaowakosea kwa kuwavizia na mitutu au kuwapoteza. Achaneni na mambo ya “watu wasiojulikana” hayatowafikisha popote mwanangu.

Tanzania Mwanangu, nakusihi Boresheni mifumo ya elimu – wajukuu wasome elimu ya kuwasaidia sio kukariri mitahala isiyo na tija wala faida, wape elimu yenye manufaa wajukuu zangu – competence based education, watajitegemea na sio kutegemea kuajiriwa pekeake.

Mtoto wangu nakuandika ujumbe huu sababu najua wewe unategemea kilimo ndio uti wa mgongo, mbona sasa unaweka bajeti ndogo katika hilo halafu unaongezea bajeti ya kununua magari mazuri na mishahara minono kwa wabunge na wanasiasa? Magari ya kawaida ya kuanzia mil 20 hayafai mwanangu? Mnanunua magari ya mil 400 wakati wajukuu hawana vyoo mashuleni na masokoni.

Sikukufundisha hivyo mwanangu. Peleka wataalamu wakajifunze nchi z anje wenzenu wanafanikiwaje katika kilimo na katika elimu. Kisha igeni mfano wao. Usikae kama kisiwa mwanangu nenda kajifunze kwa waliofanikiwa. Kilimo cha miwa cuba wanawezaje, kajifunze. China wanawezaje katika viwanda, peleka wajukuu kule wakajichukulie ujuzi.

Mwanangu Tanzania, pole sana na kupambana na Maisha kujiletea maendeleo, unajitahidi kwa kiasi ila bado kasi yako hairidhishi, niko mawinguni nakutazama na kukuombea uongeze spidi Zaidi. Madini ya kila aina yapo, mbuga za Wanyama, maziwa, mito, bahari, udongo wenye rutuba misimu ya mvua ya kutosha. Wewe ni Tajiri mwanangu. Amka. Fanya kazi. Himiza siasa bora, afya, uwajibikaji, kata rushwa, watu wasaidiwe kuinuka kiuchumi, kijamii na kifikra.

Nakupenda sana mwanangu,

Mimi mama yako,

Mtanganyika Bara

mbinguni peponi
 
Umegusa mioyo yetu

Ingawa barua ndefu namna hii. Mwanao ambaye hana utamaduni wa kujisomea anawezaje kuhimili urefu huu?
 
Inasikitisha na kufikiri sha
IMG_0507.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom