Barua kwa mpenzi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Barua kwa mpenzi

Discussion in 'JF Chit-Chat' started by Quinty, Apr 30, 2011.

 1. Quinty

  Quinty JF-Expert Member

  #1
  Apr 30, 2011
  Joined: Mar 25, 2010
  Messages: 463
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 35
  Mpenzi Frank,

  HABARI za Pasaka mwenzangu? Wengine wanasema eti walisaka Pasaka hadi wakawakawaka sijui na wewe uliiona? Ingawa wanaowakawaka kawaida kesho yake huwa wanatamani kufa tena badala ya kufufuka kazini.

  Lakini lazima nikuambie ukweli mpenzi wangu. Nilikumiss kama kidonda vile maana kula sikukuu bila mpenzi wako ni sawa na kula pilao ukiwa na mafua mazito. Waweka pilao mdomoni, watafuna hadi kumeza lakini ladha ndiyo hivyo tena. Sifuri.

  Hata hivyo, kwa kuwa bosi kaamua kupeleka familia huko ufukweni, na mimi nilipata wasaa wa kumtembelea mama mdogo huko Tandika. Nakuambia. Nadhani wasichana wengine huko wanavaa vimini kwa sababu ya kutolowanisha nguo tu wakati wa mchezo wa kuruka madimbwi kama si maziwa kabisa. Nashangaa kweli.

  Kila mwaka mvua inanyesha kubwa, lakini hadi sasa bado hatujaweza kutengeneza barabara ambazo hazigeuki bahari baada ya mvua ya nusu saa. Au ndizo hizo hela zinazoliwa?!

  Lakini tuache hayo maana Hidaya wako hataki kuona matatizo tu, matatizo tu kila siku. Hebu nikupashe kituko nilichopata kabla ya Pasaka. Bosi alikuwa amezamia na lishangingi lake na Mama Bosi akaenda kwenye vikao vyake vya harusi. Hivyo aliniomba niende kwa dada yake kuchukua vitambaa vipya alivyoagiza kutoka Nigeria. Tamba na vitambaa nakuambia! Basi ilibidi nipande daladala.

  Sasa wakati wa kurudi niliona vituko. Kama kawaida, pamoja na abiria watarajia wengine, walikuwapo na wanafunzi. Na kama kawaida walinyimwa kuingia hadi wazee wote walipokuwa wamepata nafasi.

  Kila wakijaribu kupita mpiga debe kawazuia (na alikuwa mtaalamu kweli kwa hilo, licha ya kuvaa nguo chafu kama nini). Kinyume cha wapiga debe wengine alikuwa anajaribu kuwaelezea wanafunzi kwa nini hawezi kuwachukua wengi lakini mbele ya shida nani atasikiliza

  ‘Acha siasa wewe! Na sisi tuna haki kama wengine. Hata kama hawa ni watu wazima, sisi si nusu watu!’

  Lakini jamaa akawazuia huku anaendelea kueleza. Mwisho aliwaambia anawaruhusu wanafunzi sita tu kuingia. Wacha wapiganie kuingia, huku wengine wakimlaumu mpiga debe kwa nini anawanyanyasa, lakini yeye hakusema neno, hadi wanafunzi sita waliweza kuingia mbinguni huku wengine wabaki nje na kusaga meno.

  Ghafla abiria mmoja akapayuka.

  ‘We kijana ukoje? Kwa nini huwaruhusu wengine kupanda?’

  Mpiga debe akajaribu kujieleza kwamba ni sera ya bosi wake.

  ‘Sikiliza Bwana, sisi lazima tupeleke hela fulani kwa bosi kila siku. Tusipopeleka, na kupata ziada juu, hatuli, hatulali. Ndiyo maana siwezi kuwachukua wengine.’

  ‘Hakuna. Wewe mshenzi sana. Kama hawapandi wengine basi twende polisi.’

  Mpiga debe hakumjibu. Akaendelea kuwazuia wanafunzi wengine wanaopanda huku akifunga mlango wa daladala.

  ‘Nimesema twende polisi. Kwa nini uwazuie? Wivu tu unakusumbua kwa sababu wewe hujasoma.’

  Lo mpenzi, hapo ndipo matamu yakaanza. Mpiga debe akageuka na kumwagia abiria bonge la ung’eng’e hadi abiria walioelewa wakakauka kucheka. Ikabidi nimwulize jirani yangu kunitafsiria maana ushambenga ulikuwa unaniwasha. Kumbe mpiga debe akamwambia abiria kwamba amesoma vizuri sana hadi Kidato cha Nne.

  ‘Unafikiri sisi wapiga debe wote ni mateja? Kwamba tupo hapa kwa sababu ya uhuni? Basi kwa taarifa yako niliacha kazi baada ya bosi kudai nusu ya mshahara wangu kila mwezi, eti yeye alinisaidia kuajiriwa.’

  Kwa mujibu wa jirani yangu, Kiingereza cha yule jamaa kilikuwa kizuri kabisa hadi hata wanafunzi waliokuwapo ndani ya daladala wakaanza kumshangalia na kumshangilia. Kijana akaendelea kumwaga ung’eng’e kama radhi.

  ‘Haya Bwana Msomi, na wewe una madigrii mangapi?’

  Kimya.

  ‘Bila shaka wewe ni Profesa wa Chuo Kikuu.’

  Kimya.

  ‘Bwana Msomi, niambie basi natakiwa kufanya nini.’

  Kimya. Watu wote tulikuwa tunamwangalia abiria tukitegemea atajibu mapigo alionekana kanywea kabisa. Basi yule mpiga debe akatoa shilingi elfu kumi.

  ‘Wewe unanikashifu mimi sijasoma, mbona hutaki kunijibu? Nijibu tu maneno matano katika Kiingereza chako cha kisomi nakupa hizi kama zawadi ya Pasaka.’

  Bado kimya. Ingawa wanafunzi na abiria wengine walikuwa wameanza kumshabikia kweli mpiga debe ambaye sasa alimwendea na kumwonyesha noti.

  ‘Hizi elfu kumi. Sema maneno matano tu, Bwana msomi, tuonyeshe usome wako sote tupate kukuabudu, na upate hizo kama sadaka.’

  Hatimaye abiria alijitahidi kujikakamua.

  ‘Toka hapa na Kiingereza chako cha kuombea maji.’

  ‘Cha kuombea maji? Bora mimi kuliko mtu aliye debe tupu. Kutika tu, kutika tu. Hamna lolote.’

  Basi zima likaangua kicheko. Mpiga debe akageuka na kurudisha elfu kumi zake mfukoni na kuendelea na kazi. Unafikiri yule abiria alikuwa na neno tena? Kainama tu na ingawa ninao uhakika alikuwa anaenda mjini, alishuka kituo kilichofuata. Aibu jamani! Kamsuta mpiga debe, kumbe asota mwenyewe. Wakati anateremka wanafunzi wakaanza kuimba.

  ‘Sema neno moja tu, roho zetu zipone.’

  Baada ya kuteremka yule, mpiga debe akatugeuka sisi tena.

  ‘Nyinyi mnatulaumu bure. Hamjui tunavyofanya kazi. Hamjui jinsi ilivyo ngumu kumpelekea bosi pesa zake za siku, sembuse kupata ziada kwa ajili yetu. Kama serikali inawapenda wanafunzi kiasi hicho, kwa nini wasitoe ruzuku kwa ajili yao? Kwa nini wenye mabasi walazimike kutoa ruzuku wakati wanafanya biashara yao?

  Mwenye mchicha anaambiwa auze mchicha bei nafuu kwa mwanafunzi? Hata mwenye kalamu, au daftari, au kitabu cha shule anaambiwa ili mradi mtu kavaa sare ya shule apewe bei ya chee? Hamna lolote.’

  Kimya kikatanda. Baada ya aibu ya yule jamaa hakuna aliyetaka kuanzisha ubishi na mpiga debe yule.

  ‘Lazima mjue adui wenu ni nani. Si sisi ambao tunahangaikia maisha. Ni hao wanaofanya mipango mibovu inayotulazimisha kugombana. Unafikiri ninapenda kuwazuia wanafunzi? Hata kidogo! Mimi mwenyewe nilicharazwa viboko na baba kila siku kwa kuchelewa kurudi nyumbani. Baba aliyegombania kiti wanafunzi wasipate!’

  Mmoja akajikakamua.

  ‘Vaa basi vizuri tukuheshimu!’

  ‘Katika mapambano hayo? Unataka nichanike shati kila siku?’

  Akageuka na kuendelea na kazi yake ya kuruhusu abiria na kuwazuia wanafunzi. Hatimaye watu waliweza kufungua midomo na wao. Wako waliokiri kwamba wanafanya makosa kuwahukumu watu kutokana na kazi zao, au hata vaa yao, lakini wabongo wengine kama kawaida! Lazima watafute sababu nyingine.

  ‘Wewe unafikiri yule ni mpiga debe kweli. Inzi yule. Kazi yake kudaka maneno yetu.’

  ‘Kweli bwana maana maneno ya daladala laana tupu. Lazima serikali ijue sisi tunasema nini.’

  ‘Ah wapi! Yule Mkenya Bwana. Tangu lini Mbongo amwage Kiingereza kivile! Hatuwezi sisi.’

  ‘Acha kutudharau sisi Wabongo …’

  ‘Basi kwa nini yule aliyemkashifu alishindwa kutoa hata maneno mawili … hata kwa dau ya elfu kumi.’

  Nakuambia mpenzi, abiria waliendelea kubishanabishana kisa mpiga debe kaona mwezi wa Kiingereza. Mimi nilikuwa nacheka tu. Katika dunia hii ya kazi kwa wazee, na sifuri kwa vijana, tunashangaashangaa nini kuona aliyesoma akishika kazi ya daladala. Kuna nini zaidi? Kwa nini kazi zote za chini zinadharauliwa kiasi kwamba anayeweza anafikirikiwa vingine. Eti shushushu. Nilicheka sana.

  Lakini zaidi ya yote, nilivutiwa sana na maneno yake kuhusu wanafunzi. Kweli ni kazi ya wenye mabasi kuwakirimu wanafunzi. Tena kwa amri bila maelewano. Kwa nini wao tu wale hasara, serikali ione takatifu wakati imesababisha hayo. Nilishangaa mama mdogo aliponiambia kwamba mwanaye, licha ya kukaa Tandika, amepangiwa sekondari ya kata ya Tegeta! Tandika iko kata ya Tegeta? Sikutaka kulalamika tena lakini serikali kweli inafanya miujiza.

  Akupendaye daima mpenzi. Kwa kuiga mfano wa mpiga debe,

  I love you my switi.

  Hidaya.
   
 2. X-PASTER

  X-PASTER Moderator

  #2
  Apr 30, 2011
  Joined: Feb 12, 2007
  Messages: 11,651
  Likes Received: 106
  Trophy Points: 160
 3. Nazjaz

  Nazjaz JF-Expert Member

  #3
  Apr 30, 2011
  Joined: Jan 20, 2011
  Messages: 5,348
  Likes Received: 1,143
  Trophy Points: 280
  x paster soma bandiko lote.
  Nimependa jinsi mwandishi alivyo present mawazo yake kwa namna ya kiendawazimu
   
 4. Avatar

  Avatar JF Gold Member

  #4
  May 1, 2011
  Joined: Jan 24, 2011
  Messages: 676
  Likes Received: 29
  Trophy Points: 35
  Aisee!...
   
 5. Futota

  Futota JF-Expert Member

  #5
  May 1, 2011
  Joined: Dec 11, 2010
  Messages: 524
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  aisee mkuu, a shorter version of this story has already been posted here in JF....
  ila no sweat, pengine wewe na yeye wote mlikuwa kwenye hilo basi! LO
  L
   
 6. W

  WAMURUBHERE JF-Expert Member

  #6
  May 1, 2011
  Joined: Apr 21, 2010
  Messages: 337
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 35
  ishabandikwa hapa ww umetohoa kidogo,fuata hiyo link utaona mwenyewe
   
 7. M

  Masuke JF-Expert Member

  #7
  May 1, 2011
  Joined: Feb 28, 2008
  Messages: 4,606
  Likes Received: 108
  Trophy Points: 160
  Haya ni maandiko ya mwandishi wa vitabu kimojawapo ni Mabala the farmer,anaitwa Richard Mabala ni Mzungu alishaadopt kabila la kinyamwezi anacolumn yake raia mwema, uandishi wake unafurahisha na kufundisha sana.
   
Loading...