raiamwematz24
Member
- Dec 6, 2025
- 8
- 20
Katika Kata za Kimara, Makoka na Saranga, mashimo makubwa, matope na mifereji mibovu vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wakazi.
Barabara kama Kimara Suk, Golani hadi Saranga, Kimara Stop Over hadi Daraja Bovu, Kimara Mwisho hadi Bonyokwa na Kimara Temboni hadi Matosa zimeendelea kuzorota licha ya kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara.
Wananchi wanasema matengenezo hayo ni ya muda mfupi na hayazingatii viwango vinavyoweza kudumu kwa muda mrefu, hali inayosababisha kurudiwa kwa tatizo kila mvua inaponyesha.
“Kila siku ni ahadi tu lakini hakuna utekelezaji tunaouona inaishia tu kuona barabara zinaparazwa na kuchongwa juu juu kama danganya toto na baada ya mwezi tu mvua ikipita tunarudi kuteseka,” alisema dereva wa bodaboda mmoja wa kijiwe cha Mama Nyenzo Kimara Mwisho mtaa wa Vinane.
Wananchi wengi wanasema matengenezo yanayofanyika ni ya kusambaza kifusi au kufukia mashimo bila kuweka miundombinu ya kudumu kama mifereji ya maji. Baada ya mvua chache, hali hurudi kama ilivyokuwa au kuwa mbaya zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa za bajeti za Manispaa, fedha hutengwa kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara za mitaa kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Husika.
Manispaa ya Ubungo ilipitisha rasimu ya bajeti ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo kwa shilingi 143,142,599,995 kwa mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni pamoja na vipaumbele vya kuendeleza miundombinu kama barabara za mitaa. Hii ni bajeti ya jumla, na inajumuisha matumizi mbalimbali ya Maendeleo siyo kiasi kilichotengwa tu kwa barabara peke yake.
Mzee Abdallah Mussa wa Kimara Mwisho anahoji, “Fedha zinatangazwa kwenye bajeti, lakini sisi hatuoni matokeo yake. Kama miradi ipo, iwe wazi tujue nani kajenga, kwa shilingi ngapi na lini itakamilika.”
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika nyakati za kampeni, Diwani wa Kata ya Kimara, Ismaili B. Mvungi, aliahidi kuwa barabara za Kimara mwisho hadi Vinane zingewekewa mpango wa ujenzi wa kiwango cha changarawe imara na mifereji.
“Tayari tumewasilisha ombi la fedha za ziada. Ndani ya mwaka huu wa fedha, barabara hizi zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” alinukuliwa akisema mbele ya wananchi.
Upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, katika moja ya ziara zake, aliwahakikishia wakazi kuwa serikali imeongeza bajeti ya matengenezo ya barabara za mitaa na kwamba kipaumbele kitatolewa kwa maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.
“Serikali haitawaacha wananchi wa Ubungo. Tunasukuma ili barabara hizi zijengwe kwa kiwango kinachostahili,”Akizungumza wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani humo juni 6, 2025.
Aidha aliongeza kwa kusema kuwa Serikali ina lengo madhubuti la kupunguza ajali za barabarani kwakuzingatia miundombinu salama. Hata hivyo, miezi kadhaa baada ya ahadi hizo, hali ya barabara nyingi bado ni ile ile.
Juni 20, 2025 DC Msando wakati akizungumza na madiwani waliomaliza muda wao aliwataka wakandarasi wote ambao walifanya kazi ya matengenezo ya barabara mbalimbali katika wilaya ya ubungo kurudia matengenezo hayo kwani yalikuwa chini ya kiwango. Licha ya kauli hiyo lakini bado hakukuwa na marekebisho yeyote yaliyofanyika.
Afisa mmoja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Ubungo alikiri kuwepo kwa changamoto za kifedha na ongezeko la kasi la makazi mapya.
“Ubungo imekua kwa kasi sana. Bajeti iliyopo mara nyingi haitoshi kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami. Tunafanya matengenezo kulingana na fedha zilizotengwa.”
Aliongeza kuwa baadhi ya uharibifu unatokana na mvua kubwa na ukosefu wa mifereji:
“Tunapanga kuanza miradi ya kuboresha mifereji katika baadhi ya maeneo ya Kimara na Saranga, matosa na makoka ili kupunguza tatizo la maji kuharibu barabara.”
Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Afisa Mipango Bi Emelda Dotto alisema ushirikishwaji wa wananchi unafanyika kupitia mikutano ya mitaa na vikao vya maendeleo.
“Tunawahimiza wananchi kushiriki mikutano ya kupanga vipaumbele. Mapendekezo yao huwasilishwa kwenye bajeti ya halmashauri.”
Kwa sasa, kilio cha wananchi wa Ubungo ni kimoja tu wanahitaji barabara za kudumu, si ahadi za kila mwaka. Barabara ni uti wa mgongo wa uchumi wa jiji bila miundombinu imara, maendeleo yanabaki kuwa kauli mbiu tu.
Swali linalosalia ni kama mamlaka husika zitachukua hatua za dhati kuondoa aibu hii ya miundombinu, au kama Ubungo itaendelea kuwa na miundombinu mbovu inayolazimu uharibifu mkubwa kwa vyombo vya usafiri na kuongezeka kwa gharama za usafiri kipindi cha mvua.