Ballali aitikisa serikali
(Tanzania Daima)
(Tanzania Daima)
na Charles Mullinda na Kulwa Karedia
KUNA kila dalili kwamba, mwenendo wa mambo serikalini si mzuri baada ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Daudi Ballali, kueleza nia yake ya kutaka kurejea nyumbani kukabiliana na tuhuma zinazomkabili na kuwaweka bayana wahusika wakuu wa sakata hilo.
Nia hiyo ya Dk. Ballali ya kutaka kuwaanika wahusika wakuu wa uchotaji fedha katika akaunti ya ulipaji madeni ya nje (EPA), ndiyo inayowaumiza vichwa viongozi wa juu serikali na waliokuwa madarakani wakati wa utawala wa awamu ya tatu.
Habari za hivi karibuni zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili, zinaeleza kuwa, wafanyabiashara, baadhi ya viongozi wa juu serikalini na wale waliostaafu, kwa siku kadhaa sasa wamekuwa wakihaha kuhakikisha kuwa Dk. Ballali harejei nchini.
Kwamba, mikakati ya viongozi hao ni pamoja na kuhakikisha kuwa hata kama Dk. Ballali akirejea, hafanikiwi kivifikia vyombo vya habari au vile vya sheria kwa sababu, hatua hiyo inaweza kuibua kashfa kubwa kwa serikali.
Habari hizo zinaeleza kuwa, Dk. Ballali ambaye siku chache zilizopita alikuwa akijiandaa kurejea nyumbani, alipanga mara tu baada ya kuwasili, angekutana na waandishi wa habari kuwaeleza kile anachokijua kuhusu kashfa ya uchotaji fedha za EPA kwa kuonyesha ushahidi wa vielelezo.
Habari hizo zilieleza zaidi kwamba, Dk. Ballali ambaye kwa siku kadhaa tangu uteuzi wa wadhifa wake wa ugavana ulipotenguliwa akihusishwa na kashfa hiyo, alianza kuwasiliana na wanasheria maarufu nchini ili kupata msaada wa kisheria wa kupambana na tuhuma zinazomkabili.
Alipanga kwenda mahakamani akiwa na vielelezo hivyo vya maandishi, vinavyoonyesha jinsi waliokuwa wakubwa wake kikazi walivyokuwa wakimuagiza kulipa mabilioni ya fedha kwa kampuni zilizotajwa kuhusika na ufisadi wa BoT.
Inaelezwa kuwa, mikakati hiyo ya Dk. Ballali iliwashtua wakubwa ambao walianza kupanga ajenda za kuhahakisha kuwa harejei nchini.
Hilo linathibitishwa na taarifa zilizolifikia gazeti hili mwanzoni mwa wiki hii, zilizodai kuwa uraia wa Dk. Ballali una utata, hivyo anaweza asirejee nchini kwa sababu si raia wa Tanzania.
Taarifa hizo zilidai zaidi kwamba, Dk. Ballali aliukana uraia wa Tanzania na kuchukua uraia wa Marekani wakati akifanya kazi katika moja ya mashirika makubwa ya kimataifa nchini humo.
Kwamba, hata hatua ya Marekani kutengua visa yake, haimfanyi Dk. Ballali kuwa na ulazima wa kurejea nchini kwa sababu ana uraia wa nchi nyingine.
Gazeti hili liliwasiliana na Waziri wa Fedha kupitia simu yake ya kiganjani Jumatano wiki hii kuomba miadi ya kukutana naye kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa madai hayo.
Waziri Meghji alieleza kuwa muda wake kwa siku zilizobakia kabla ya kwenda bungeni anautumia kwa ajili ya vikao, lakini aliahidi kuwasiliana na gazeti hili siku iliyoafuata (Alhamis), ili kutoa ufafanuzi wa madai haya kutokana na unyeti wake.
Katika hali ya kushangaza, Waziri Meghji hakutekeleza ahadi yake siku hiyo na alipotafutwa siku hiyo jioni, alitoa ahadi nyingine ya kutafuta muda wa kuzungumza na gazeti hili siku ya Ijumaa, jambo ambalo hakulitekeleza pia.
Tanzania Daima liliendelea kumtafuta Waziri Meghji Ijumaa jioni, lakini simu yake ya kiganjani ilikuwa ikiita bila majibu kama ilivyokuwa Jumamosi kwa simu yake kuita bila kupokelewa pia.
Hata hivyo, Alhamisi wiki hii, gazeti hili lilimkariri Waziri Meghji alipokuwa akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari katika viwanja vya Ofisi Ndogo ya Bunge, Dar es Salaam kuwa hatazungumza tena kuhusu sakata hilo la ufisadi kwa sababu sasa limefika katika ngazi nyingine.
Baadhi ya wadadisi waliokuwa eneo hilo walieleza kuwa, Waziri Meghji amelazimishwa kukaa kimya ili kuondoa mkanganyiko wa kauli kutoka kwa viongozi wakuu serikali.
Mmoja wa watumishi wa taasisi ya fedha aliyekuwa eneo hilo alisema, sababu nyingine inayomfunga mdomo Meghji, ni kuibuka kwa tetesi kuwa makandarasi wadogo waliopewa tenda ya kujenga minara miwili ya BoT, hawakuwa na sifa stahiki.
Mambo yameingiliana, mama (Meghji) lazima akatae kuzungumza, huku kuna ufisadi huku kunaibuka ubora na uimara wa jengo, kuna makarandasi wadogo hapa ambao walipewa tenda kinyemela, hawakuwa na sifa za kujenga, hawa wakifuatiliwa, yanaweza kuibuka mapya, alisema mtumishi huyo ambaye jina lake tunalo.
Gazeti hili pia lilijaribu kumtafuta Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe kupitia simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia uraia wa Dk. Ballali na mahali alipo sasa baada ya visa yake kutenguliwa nchini Marekani bila mafanikio, simu yake ilikuwa haipatikani.
Wakati hali ikiwa hivyo serikali, kwa upande wa wanasiasa kadhaa walioongea na gazeti hili walieleza kushangazwa kwao na ukimya wa serikali kuhusu Rais wa Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa ambaye kambi ya upinzani imekuwa ikimtuhumu siku nyingi kuwa alikiuka miiko ya uongozi kwa kufanya biashara Ikulu.
Kiongozi mmoja wa kambi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa Rais Kikwete asifikiri vita ya ufisadi iliyoanzishwa na kambi ya upinzani imekwisha baada ya kumuondoa Dk. Ballali katika wadhifa wa ugavana.
Alisema, kambi ya upinzani inafahamu kuwa Dk. Ballali ametolewa kafara ili kunusuru viongozi wa juu waliopo katika safu ya ungozi wa sasa serikali na wale walio nje waliohusika katika kashfa ya uchotaji wa fedha hizo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa ambaye alizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, alisisitiza kuwa Rais Mkapa anapaswa kukamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa kosa la kutumia rasilimali za nchi vibaya.
Mimi niko wazi katika hili, Mkapa si kwamba ajitokeze, bali anapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa hilo. Ni jambo lisilovumiliwa, kuona kiongozi wa nchi anachukua asilimia 85 ya rasilimali za taifa na kulibakizia taifa asilimia 15.
Nasisitiza, Mkapa si wa kuombwa ajitokeza kusema chochote, anapaswa kukamatwa, Rais Kikwete amkamate Mkapa ni mhalifu, alikiuka maadili ya uongozi akiwa Ikulu, ni kama Chiluba tu.
Rais Kikwete anapaswa atuambie kama Mkapa alivunja sheria au hakuvunja sheria kwa kufanya biashara akiwa Ikulu, tena si Mkapa tu, bali yeye na waziri wake, walijichukulia mradi mkubwa tu wa serikali bila ya kufuata taratibu au kushinda tenda yoyote, nasisitiza jamani huu ni uhalifu, alisema Dk. Slaa kwa kusisitiza.
Mkapa amekuwa akituhumiwa kwa muda mrefu kuwa alitumia vibaya madaraka yake katika kipindi cha miaka kumi alichokaa madarakani.
Viongozi kadhaa wa upinzani wamekuwa wakidai kuwa akiwa madarakani, aliitumia kofia ya urais kujitajirisha yeye binafsi, familia na marafiki zake.
Kwa uchache, mali zinazodaiwa kuwa alichuma akiwa Ikulu ni pamoja na kuanzisha kampuni yake ya biashara, ANBEM, ambayo mkewe ni mshirika wake kibiashara.
Pia, anadaiwa kusajili kampuni binafsi, yeye na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, iitwayo Tanpower Resources Company, ambayo aliisimamia kununua asilimia 85 ya uliokuwa mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira, mkoani Mbeya.
Kwamba, aliutumia wadhifa wake wa urais kuhakikisha kampuni yake hiyo inaingia mkataba wa kuizuia Tanesco megawati 200 za umeme katika gridi ya taifa, kampuni ambayo mkewe na mtoto wake ni wakurugenzi.
Mbali na wapinzani, Mkapa pia aliwahi kutuhumiwa na mmoja wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeheshimika hapa nchini, Joseph Butiku kuwa alipageuza Ikulu kuwa mahali pa kufanyia biashara.
Katika hatua nyingie, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amesema sheria ya vyama vya siasa iliyopo sasa, ina upungufu mkubwa unaomnyima nguvu za kisheria za kubana matumizi ya fedha zenye shaka za vyama vya siasa.
Tendwa aliyasema hayo juzi, ofisini kwake alipozungumza na gazeti hili kuhusu matumizi makubwa ya fedha ya vyama vya siasa wakati wa kampeni za uchanguzi na madai ya baadhi ya vyama kumegewa fedha zilizochotwa EPA na kuzitumia katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.
Alisema, vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, vimekwishawasilisha ripoti zake za fedha, lakini hana mamlaka ya kisheria ya kuhoji ripoti hizo, isipokuwa kuzipokea na kuzitunza ofisini kwake.
Vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu mwaka 2005 vimeshawasilisha ripoti zao za fedha, ripoti hizo ninazo, lakini sheria inasema chama kinaweza kupata fedha toka kwa wafadhili wa ndani au nje na ni lazima vitoe taarifa ya fedha kwa msajili wa vyama vya siasa.
Lakini mpaka sasa sina taarifa hizo, kama walipata fedha za misaada kutoka kwa wafadhili toka chama chochote, sheria nayo iko kimya haisemi mimi kama msajili iwapo nawajibika kufanya uchunguzi wa mapato yoyote ya chama ambayo si ruzuku ya serikali.
Ndio maana nimekwishapeleka mapendekezo serikalini ili sheria hizi zifanyiwe marekebisho, kwa kweli zina kasoro, na marekebisho haya ya sheria niliyopeleka, ndio yamepitishwa katika nchi za Zambia na Msumbuji, wanalichukua toka hapa kwangu, wamerekebisha kidogo tu, mimi nimepeleka tangu mwaka 1995, lakini hayajapitishwa, alisema Tendwa.
Hata hivyo alisema, kama kuna mtu ana ushahidi wa tetesi zilizopo sasa kuhusu baadhi ya vyama kupatiwa fedha zilizoibwa kutoka EPA, ampelekee na yeye atawaita wahusika na kuwaomba taarifa zao za fedha, lakini alirejea kauli kwamba akishapatiwa taarifa hizo, hana uwezo wa kuchukua hatua yoyote wala kuchunguza.
Alisema, shaka waliyonayo wananchi wengi inatokana na utata wa maelezo yanayotolewa na viongozi wa serikali kuwa fedha zilizochotwa kutoka EPA na kupewa Kampuni ya Kagoda Agriculture zilikuwa maalumu kwa kazi za usalama wa taifa.
Kagoda Agriculture Company na masuala nyeti ya usalama wa taifa wapi na wapi? Agriculture na ulinzi na usalama vina uhusiano gani? Inatia shaka kwa kweli, jina la kampuni na sababu zilizotolewa haviendani kabisa, alisema Tendwa kwa mshangao mkubwa.
Tangu Rais Kikwete atengue uteuzi wa Dk. Ballali kama Gavana wa BoT kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa sh bilioni 133 za EPA, kumekuwa kukitolewa kauli za kumtaka achukue hatua zaidi dhidi ya walioshirikiana na Dk. Ballali katika ubadhirifu huo.
Kauli nyingi zinazotolewa sasa zimekuwa zikiwalenga baadhi ya viongozi wakuu waliokuwa madarakani wakati wa upotevu wa fedha hizo, akiwemo Rais mstaafu Mkapa ambaye kwa mara kadhaa ameshutumiwa na watu mbalimbali wakiwemo wana CCM kuwa, alitumia vibaya madaraka ya urais, hivyo kumtaka Rais Kikwete kuchukua hatua zaidi.